1 Petro- Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA KWANZA WA MTUME PETRO.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.

UTANGULIZI.

Mtume Petro aliandika waraka huu kwenda kwa waamini waliokuwa katikati na kaskazini mwa Asia ndogo (leo ni Nchi ya Uturuki) yeye akiwa huko Rumi ambako anakupa jina Babeli.[1]

MTUME PETRO.

Mtume Petro ni mmoja wa mitume kumi na wawili Bwana Yesu kristo aliowachagua (Luka 6:13-16) na pia ni mmoja wa wanafunzi watatu wa karibu sana na Yesu. Wanafunzi hawa ni miongoni mwa wanafunzi wa awali kabisa wa Yesu (Luka 5:4-11), wanafunzi walioona matukio adimu ya Yesu ambayo wanafunzi wengine hawakuyaona. Matukio haya ni kama kubadilika kwa Yesu kule mlimani (Luke 9:28-36) na maombi yake katika bustani ya Gethsemane (Mathayo 26:36-46). Mtume Petro jina lake la asili ni Simon lakini alibadilishwa jina na Yesu na kuitwa Cepha (kwa Lugha ya kiaramu) ambalo ni Petros (kiyunani), ambalo ndilo Petro kwa Kiswahili.

Wapokeaji wa Awali wa Waraka.

Wapokeaji wa waraka huu ni waamini wa makanisa mbalimbali yaliyokuwa ya wamataifa ambao walikuwa wanaishi katika eneo la Katikati na kaskazini mwa Asia ndogo (Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia).

KUSUDI LA WARAKA.

Mtume Petro aliandika waraka huu kuwatia moyo waamini waliokuwa wanapata mateso kwa sababu ya imani yao (1:6-7: 2:18-20; 3:13-17, 4:1-4, 12-19; 5:8-9). Anawatia moyo kwa kuwaonyesha kwamba mateso haya ni ya kitambo kidogo (1:6), si jambo geni (4:12) na yana lengo la kuijaribu imani yao (1:7). Zaidi ya hayo mateso hayo ni heri/Baraka kwao (3:14, 4:14). Hivyo anawataka kustahimili mateso hayo kama Yesu alivyostahimili (2:18-21), si kwa kuhuzunika bali kwa kufurahi wakijua wao ni washiriki wa mateso pamoja na kristo. Na kwa kuwa wanashiriki mateso ya Kristo sasa basi watakuwa washirika wa utukufu wa kristo atakapofunuliwa/ajapo (4:12-16 na 1:6-7). Kwa kuwa Yesu mfano wao bora hakurudishia wala kuogopa mateso, wao pia wasilipe baya kwa baya wala kuongopa (2:23). Angalizo analowapa ni kwamba wasipate mateso kwa sababu wanatenda mabaya (2:20; 3:17 na 4:15).

Mateso haya yalikuwa ni ya namna gani?

Jibu la moja kwa moja ni mateso ya aina mbalimbali (1:6). Mfano wa mateso waliyokuwa wanayapata ni: mateso anayopata Mtumwa kutoka kwa Bwana wake (2:18-25), mateso kwa sababu ya kuishi maisha ya haki (3:14-15, 16-17), mateso kwa sababu ya kuondoka kwenye mwenendo wa kwanza wa dhambi (4:1-4) na mateso kwa sababu ya kuwa mkristo (4:12-16).

Pamoja na mateso Petro anawaandikia waraka huu waamini kuwataka waamini waishi maisha ya kutengwa na dhambi kama Mungu alivyotengwa na dhambi (1:13-16). Hii ni kwa sababu wao walikombolewa watoke kwenye mwenendo wao wa kwanza wa dhambi kwa njia ya damu ya thamani ya Yesu kristo (1:18-20). Lakini pia wanatakiwa kuishi kwa kufanania tabia hii ya Kiungu kwa sababu wao ni wasafiri na wapitaji katika dunia hii (2:11). Mwisho wanatakiwa kuishi kwa kufanania tabia hiyo ya Kiungu ili watu wasioamini wawatazamapo wamtukuze Mungu (2:12), pia wazibe vinywa vya watu wapumbavu (2:15) na wengine waamini bila kuhubiriwa kwa maneno (3:1-2).

MPANGILIO.

NambaMaandikoMaelezo
11:1-2Utangulizi
21:3-12Shukrani kwa Mungu kwa ajili ya wokovu.
31:13-2:10Iweni watakatifu kama Mungu alivyo.
 A1:13-17Utakatifu kama Mungu alivyo
B1:18-25Utakatifu kwa sababu Mlikombolewa
C2:1-10Mwenendo mpya kwa kuwa mmekuwa Taifa la Mungu
42:11-4:11Mwenendo mwema katikati ya Mataifa na kanisa
 A2:11-17Mwenendo mpya katikati ya mataifa 
B2:18-25Watumwa 
C3:1-7Wake kwa waume 
D3:8-12Ninyi kwa ninyi 
E3:13-4:6Mwenendo mpya kwa wale wanaowatesa 
F4:7-11Ninyi kwa ninyi 
54:12-5:11Shirikini Mateso ya Kristo
 A4:12-19Mstahimili Mateso
B5:1-4Mwenendo wa Wazee/viongozi wa kanisa
C5:5-7Mwenendo wa Vijana
D5:8-11Kesheni
65:12-14Salamu za mwisho

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.

Waraka huu una mpangilio kama ilivyokuwa kawaida ya nyaraka za wakati huo, yaani kuna utangulizi (1:2), ujumbe mkuu (1:3-5:11) na mwisho wa waraka (5:12-14). Utangulizi una utambulisho/anuani ya mwandishi (1:1a), anuani/utambulisho wa wapokeaji wa waraka (1:1b-2a) na salamu (1:2b).

Baada ya utangulizi huo Petro anamshukuru Mungu kwa kuwazaa mara ya pili yeye na wapokeaji wa waraka wake, ambapo kuzaliwa huku kwa mara ya pili kumewafanya waingie kwenye tumaini (tarajio) la Ufufuo. Tarajio hili la ufufuo ni la uhakika kwa kuwa tayari Yesu alikwisha kufufuka. Lakini pia kuzaliwa huku mara ya pili kumewapa tarajio la kupata urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yao.[2] Na hivyo Mungu anawalinda ili wapate hayo yote yatakapofunuliwa wakati wa mwisho/wakati wa kurudi Bwana Yesu mara ya Pili (1:3-5). Petro anasema habari hizo zinawafanya wafurahi japokuwa kwa sasa wanahuzunishwa na majaribu/mateso mbalimbali yanayopima imani yao. Imani yao ikishapitia hayo majaribu/mateso watapokea sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo (1:6-7). Huyo Yesu atakayefunuliwa, Petro anasema wapokeaji wa waraka wake wanampenda japo hawakumuona (Kama yeye alivyomuona) na hata sasa hawamuoni ila wanamwamini (1:8-9). Petro anamalizia sehemu hii kwa kuwajulisha wapokeaji wa waraka wake kwamba wokovu huo (1:3, 5, 9) manabii walichunguza chunguza na kujiuliza utakuaje na utakuwa wakati gani, lakini Roho wa kristo aliwajulisha kwamba haukuwa kwa ajili yao. Lakini pia Roho wa Kristo aliwaonyesha mateso ya Kristo na utukufu baada ya hayo. Mambo hayo yote Petro anasema ndiyo wapokeaji wa waraka huu walihubiriwa na watu walio na Roho mtakatifu kutoka mbinguni. Mambo hayo Malaika wanatamani kuyachungulia (1:10-12). Sehemu hii ya 1:3-12 ni sentensi moja ndefu katika kiyunani na hivyo inataja mambo ambayo mwandishi atayazungumzia katika barua yake yote. Hii inafanya sehemu hii kuwa utangulizi wa ujumbe mkuu.

Sehemu ya Kwanza ya ujumbe mkuu (1:13-2:10) Petro anawataka waamini hawa kuishi maisha ya kutengwa na dhambi kama Mungu alivyotengwa na dhambi (1:13-17)[3]. Hii ni kwa sababu ya yale Mungu aliyofanya kwa ajili yao (1:3-12) na pia kwa sababu kristo aliwakomboa kwa damu ya thamani watoke katika mwenendo wao wa zamani (1:18-22). Lakini pia anaongezea kwamba wanatakiwa kuishi hivyo kwa kuwa wamezaliwa mara ya pili kwa Neno la Mungu lidumulo hata milele ambalo ndilo walihubiriwa (1:23-25). Kuonyesha kwamba kweli neno la Mungu linadumu milele Petro ananukuu Isaya 40:6-8.[4] Kwa kuwa wamezaliwa mara ya pili na Mungu hivyo wanatakiwa kuyatamani maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ili waukulie wokovu (2:1-2). Mwisho mwandishi anawaonyesha kwamba kwa kuwa wao wamemwamini Bwana yeye aliye jiwe lililo hai lililokataliwa na wanadamu lakini limekubaliwa na Mungu wamepata heshima. Heshima hizo ni:

a. Wamekuwa mawe yaliyo hai, wamejengwa wawe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu ili watoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.

b. Wamekuwa mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu ili kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita watoke gizani waingie katika nuru yake ya ajabu. (2:5-10). [5] Heshima hizi Petro anazozitaja ni heshima ambazo Mungu aliwapa Taifa la Israeli lakini sasa wanapewa waamini.

Sehemu ya pili ya Ujumbe mkuu (2:11-4:11) Petro anawataka waamini hawa kuwa na mwenendo mzuri kwa kuwa wao ni wapitaji na wasafiri. Petro anawataka kwanza waamini wote wawe na mwenendo wa utii kwa watawala (2:11-17). Pili, anawataka watumwa (Watumishi) wawe na mwenendo wa utii kwa mabwana zao, si wale tu walio wema bali na wale walio wakali. Petro anawataka watumwa kuvumilia mateso pale watakapoteswa isivyo haki. Wanachotakiwa kufanya ni kumkumbuka Mungu wao na sio kulipiza ubaya, kama Yesu alivyofanya. Petro anawapa Yesu kuwa ndiye kielelezo cha namna ya kuvumilia mateso yasiyo ya haki (2:18-25).[6] Petro pia anawataka wanawake wawe na mwenendo wa utii kwa wanaume wao ili hata wale ambao hawajaamini waamini kupitia mwenendo wao mwema bila kuhubiriwa (3:1-6). Mwanaume pia Petro anataka waishi na wake zao kwa akili na kwa kuwaheshimu (3:7). Petro anarudi kusema na waamini wote kwa ujumla sasa. Anawaambia waamini waishi vizuri kati yao wenyewe, wasiwe wa kulipa baya kwa baya wala wasiwe wa kulipa lawama kwa lawama, bali wawe watu wa kubariki. Petro anasisitiza umuhimu wa mwenendo huo kwa kunukuu Zaburi 34:12-16[7] (3:8-12). Petro pia anawaambia waamini wawe tayari kupata mateso kwa sababu ya kutenda mema na wala wasiogope kutisha kwa wanaowatesa[8] lakini anawasisitiza wamtazame Kristo aliye mfano wa kustahimili mateso (3:13-22). Katika kumalizia sehemu hii ya pili Petro anawaambia waamini hawa muda wao wa kuishi kwenye maisha ya dhambi ulitosha, muda waliobaki nao sasa wa kuishi duniani wasiishi tena katika tamaa za wanadamu bali waishi katika mapenzi ya Mungu (4:1-6). Na kwa sababu wanaishi wakati wa mwisho waishi kwa Upendo[9] na kwa kutumikiana, kila mtu awatumikie wengine sawa sawa na karama Mungu aliyompa (4:7-11).

Sehemu ya tatu ya Ujumbe mkuu (4:12-5:11) Petro anasema na waamini wote (4:12-19), wazee-viongozi wa kanisa (5:1-4) , vijana (5:5-7) na waamini wote tena (5:8-11). Waamini wote Petro anawaambia wasione kuwa ni ajabu kupatwa na mateso, bali wafurahi kwa kuwa wanashiriki mateso pamoja na kristo ili katika kufunuliwa kwake wafurahi pamoja naye katika utukufu. Petro anawaambia waamini wakubali kupata mateso ikiwa ni kwa sababu ya jina la Yesu au kwa wao kuwa wakristo ila inatoa angalizo kwamba wasipate mateso kwa sababu wanatenda mabaya /wasipate mateso kwa kuwa wanastahili kuteswa (4:12-16). Petro anawaambia mateso hayo wanayopata Mungu ameruhusu kwa kuwa ni sehemu ya hukumu yake. Sasa Neno hukumu mara nyingi limetumika kumaanisha adhabu baada ya kukosea lakini Petro anachosema sio adhabu baada ya kukosea, kwa kuwa tangu mwanzo anasisitiza kwamba mateso wanayotakiwa kupata/wanayopata hayatokani na kutenda mabaya. Hivyo Hukumu kwa muktadha huu ina maanisha ni hatua zinazochukuliwa kujaribu uhalisi wa kitu. Kwa waamini  mateso yanaruhusiwa na Mungu kuijaribu imani yao (4:12 na 1:7). Ikiwa waamini wanapata mateso wakati wao wa kusubiria wokovu ulio tayari kufunuliwa (1:5, 9) itakuaje kwa wale wasioamini Injili ya Mungu? Hili ni swali ambalo halihitaji jibu kwa kuwa lina jibu tayari. Hali ya wasioamini Injili itakuwa ya mateso makali kuliko haya wanayopata waamini.  Kwa kusisitiza pointi yake mwandishi ananukuu Mithali 11:31(4:17-19)[10].

Kwa wazee/viongozi wa kanisa Petro anawataka kulichunga kundi la Mungu si kwa kulazimishwa, si kwa kutaka fedha ya aibu na si kwa kujifanya mabwana kama watu wa mataifa (5:1-5). Vijana Petro anawataka wawe watii na wanyenyekevu. Na kusisitiza hilo Petro ana nukuu Mithali 3:34 kuonyesha kwamba “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema” (5:6-7). Petro anamalizia kwa kuwaambia waamini wote wawe waangalifu kwa kuwa mshitaki wao ibilisi yuko kazini. Pia anawajulisha kuwa mateso wanayoyapata na waamini wenzao duniani kote wanapata mateso hayo hayo, ambayo ni ya muda mfupi. Baada ya muda huo mfupi Mungu mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu (5:8-11).

Mwisho Petro anafunga waraka wake (5:12-14) kwa kusisitiza kwamba hicho alichoandika “ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo”.



FOOTNOTES


[1] Petro anapaita Rumi Babeli kwa kuwa Babeli ilikuwa ni picha ya taifa linalopingana na watu wa Mungu-Israeli na hivyo kwa sasa Rumi ndiyo ilikuwa inapingana na watu wa Mungu kanisa. Kwa wakati wa Agano jipya taifa linalopingana na Mungu kuliita Taifa hilo Babeli ilikuwa ni kitu cha kawaida (Ufunuo 16:19; 17:5, 9 ; 18:2)

[2] Urithi waamini wanaoutarajia wenye sifa hizo ni Mbingu mpya na Nchi mpya. Petro anazungumza jambo hili katika waraka wake wa Pili pia, 2 Petro 3:7-13

[3] Mstari wa 16 ni nukuu kutoka Mambo wa walawi 11:44, 45; 19:2 ; 20:7

[4] Mistari ya 24 na 25 ni nukuu kutoka Isaya 40:6-8

[5] Mstari wa 6 una nukuu kutoka Isaya 28:16. Mstari wa 7 una nukuu kutoka Zaburi 118:22 na mstari wa 8 una nukuu kutoka Isaya 8:14. Nukuu hizo zote zilikuwa ni unabii kuhusu Jiwe kuu la Pembeni ambaye ni Masihi, ambaye wengine watamkubali na wengine watamkataa.

[6] Mstari wa 22 ni nukuu kutoka Isaya 53:9

[7] Mistari ya 10,11 na 12 ni nukuu kutoka Zaburi 34:12-16

[8] Mstari wa 14 “Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike” ni nukuu kutoka Isaya 8:12

[9] Mstari wa 8 “upendano husitiri wingi wa dhambi” ni nukuu kutoka Mithali 10:12.

[10] Mstari wa 18 ni nukuu kutoka Mithali 11:31.


UFAFANUZI WA WARAKA WA KWANZA WA PETRO.

Unakuja hivi karibuni…….