1 Timotheo – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA KWANZA WA MTUME PAULO KWA TIMOTHEO.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.

UTANGULIZI.

Waraka huu uliandikwa na mtume Paulo kwenda kwa Timotheo, mwanae katika Imani aliyekuwapo huko Efeso wakati waraka huu unaandikwa. Paulo aliandika waraka huu katika kipindi cha katikati, yaani baada ya kutoka kwenye kifungo chake kule Rumi ambako aliandika nyaraka kama vile Waefeso, Filemoni, Wakolosai na Wafilipi na kabla ya kufungwa tena ambapo aliandika waraka wa pili kwa Timotheo (2 Timotheo 1:8,16; 2:9). Baada ya waraka wa pili kwa Timotheo Mtume Paulo alikuwa anataraji kufa (2 Timotheo 4:6-8). Paulo aliandika waraka huu akitarajia kumfuata Timotheo huko Efeso (I Timotheo 3:14; 4:13).

TIMOTHEO.

Timotheo alikuwa ni mtoto wa Baba myunani na Mama myahudi aliyeamini aitwaye Eunike. Timotheo inawezekana aliamini wakati mtume Paulo alivyokwenda kuhubiri kule Listra katika safari yake ya kwanza ya kimishenari (Matendo 14). Paulo anamuita Timotheo Mwanae katika Imani (1 Timotheo 1:2), mtenda kazi pamoja naye (Warumi 16:21), mtumishi wa Mungu katika injili ya kristo (1 Wathesalonike 3:2) mwenye nia moja na yeye ya kujali waamini (wafilipi 2:19-23) na hivyo ndivyo alivyokuwa.

Paulo na Timotheo walionana mara ya kwanza huko Listra (Matendo 16:1-2) ambapo Timotheo alikuwa na sifa njema katikati ya waamini. Kwa sababu ya sifa zake Paulo akamchukua ili kufanya naye kazi ya injili. Kwa kuwa Timotheo alikuwa na Baba myunani Paulo aliamua kumtahiri ili kutokutahiriwa kwake kusiwe kikwazo katika kazi ya injili. Timotheo alifanya kazi na Paulo tangu wakati huo mpaka Paulo alipofungwa gerezani mara mwisho kabla kifo chake. Hii ndio maana Timotheo anatajwa katika nyaraka zote za mtume Paulo isipokuwa waraka kwa wagalatia, waefeso na Tito. Hii inaonyesha Paulo na Timotheo walikuwa ni Baba na mwana kweli kweli na watumishi wenza kweli kweli. Kwa ujumla Timotheo alikuwa na Sifa zifuatazo;

1. Alikuwa na mizizi ya Imani kutoka katika familia yake na hivyo katika ujana wake alikuwa na ujuzi wa maandiko ambayo alifundishwa tangu utotoni. Timotheo pia alikuwa na sifa njema katikati ya waamini. (2 Timotheo 1:5, 3:14-17 na Matendo 16:1-2).

2. Alikuwa ni mtumishi mwaminifu aliyefanya kazi na Paulo na Paulo alikuwa na uhakika kwamba Timotheo anaweza kumuwakilisha vema na kufanya kazi ya Mungu kwa uaminifu. (Wafilipi 2:19-23, 1 Wathesalonike 3:2 na 1 Wakorintho 4:17)

3.  Alikuwa na haiba ya woga na wasiwasi hivyo alihitaji kupewa maneno ya kutiwa ujasiri ( 1 Wakorintho 16:10-11). Msisitizo wa Paulo pia kwenye nyaraka hizi mbili unaonyesha Timotheo alikuwa na woga (1 Timotheo 4:12, 2 Timotheo 1:7-8). Uwoga huu labda ulisababishwa na uhalisi kwamba yeye alikuwa ni kijana mdogo katika umri na Paulo alimpa majukumu makubwa.

KANISA LA EFESO.

Kanisa la Efeso lilianzishwa na Mtume Paulo katika safari yake ya pili ya kitume (Matendo 18:19). Katika safari hii alikaa muda mfupi hapa Efeso huku akiwaaacha Priscila na Akila kwa ajili ya kuendeleza kazi ya kuhubiri na yeye akiahidi kurudi tena. Baada ya muda Apollo aliungana na Priscila na Akila huko Efeso. Paulo alirudi rasmi Efeso kwenye safari yake ya Tatu ya kimishenari na safari hii alikaa hapo Efeso kwa muda wa miaka mitatu (Matendo 19:8-10; 20:17-38 hasa 31) akihubiri na kufundisha. Hata baada ya miaka hiyo mitatu Paulo alikuwa na ukaribu na viongozi wa kanisa la Efeso. Kutokana na ukaribu huo kuna wakati aliwaita na kuwaonya viongozi wa kanisa kuhusu kulilinda kanisa huku akitabiri kwamba katikati yao kutatokea na viongozi watakaofundisha mapotovu (Matendo 20:17-38).  Utabiri huu wa Paulo ulikuwa umeshatimia wakati wa kuandika waraka huu kwa Timotheo.

KUSUDI LA WARAKA.

Paulo aliandika waraka huu kwa Timotheo kwanza kumsisitiza awakataze wengine wasifundishe elimu nyingine (1:3, 18; 6:20-21). Kwa ufupi alikuwa anamsisitiza Timotheo kuwapinga wanaofundisha mafundisho ya uongo/potofu. Na hili amelieleza kwa urefu katika sura ya 4 na ya 6. Mafundisho haya potofu yalikuwa ni mafundisho yenye hadithi, nasaba (mfululizo wa majina ya watu katika ukoo fulani), matumizi yasiyo halali ya Sheria ya Musa na yalikuwa hayapatani na utauwa. Mafundisho haya yalijaa maswali na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo huzaliwa husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya. Hivyo mafundisho haya hayakuwapeleka watu katika Imani isiyo na unafiki, upendo utokao katika moyo safi na katika dhamiri njema. Kuelewa vizuri mafundisho haya potofu soma kwa taratibu na kurudi rudi sehemu hizi, 1:3-7; 4:1-7 na 6:3-10.

Hivyo Paulo anamtaka Timotheo asimame na kweli, aenende katika kweli, afundishe kweli na kupinga upotofu unaofundishwa na waalimu wa uongo (4:1-16 na 6:3-21).

Pili Paulo aliandika waraka huu kutoa maelekezo kwa Timotheo ya namna gani waamini wanatakiwa kuenenda katikati ya Kanisa. Na maelekezo ya namna ya mwenendo yanakamilika katika sura ya 3:14-16. Hivyo tangu 2:1 mpaka 3:15 Paulo anamuelekeza Timotheo namna waamini wanavyotakiwa kuenenda katika kanisa. Hili ni kusudi la Pili la kuandika waraka huu ambalo haliachani kabisa na kusudi la kwanza.

Katika picha ya kuwepo kwa waalimu wa uongo Paulo anamuelekeza Timotheo namna ya kushughulika na makundi tofauti tofauti katika Kanisa (5:1-6:3). Moja wapo ya kundi lililokuwa limeathiriwa na waalimu hawa wa uongo ni kundi la wajane vijana (5:11-15 hasa 13 na 15).

MPANGILIO.

NambaMaandikoMaelezo
11:1-2Utangulizi wa Waraka.
21:3-20Kusudi la waraka. Wakataze waalimu wa Uongo.
 A1:3-11Kumbukizi ya kusudi la Kubaki Efeso, ambalo ndio kusudi la Waraka.
B1:12-17Kumbukizi ya Neema ya Mungu kwa Paulo.
C1:18-20Muendelezo wa Kusudi la Waraka .Mfano wa Waalimu wa uongo
32:1-6:10Maelekezo kwa ajili ya Kanisa.
 A2:1-3:16Mwenendo ndani ya Kanisa
B4:1-16Shindania Imani kwa kufundisha kweli
C5:1-6:10Namna ya kushughulika na Makundi katika Kanisa.
46:11-6:21aMaelekezo ya Mwisho kwa Timotheo
 A6:11-16Fuata Utauwa
B6:17-19Maneno kwa matajiri
C6:20-21aLinda amana uliyowekewa
56:21bSalamu za Mwisho

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.

Waraka huu una muundo kama waraka ulivyotakiwa kuwa, yaani una Utangulizi (1:1-2), Ujumbe mkuu (1:3-6:21a) na Salamu za Mwisho (6:21b). Utanguzili una sehemu Tatu kama ilivyokuwa kawaida ya waraka yaani kuna Anwani ya mtuma waraka (1:1), anwani ya mpokeaji (1:2a) na salamu (1:2b).

Ujumbe mkuu (1:3-6:21a) unaweza kugawanywa katika sehemu kuu tatu na kila sehemu kugawanyika katika vipengele kadhaa. Sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu inaeleza kusudi la kuandikwa waraka huu (1:3-20). Sehemu ya Pili ni maelekezo ya mtume Paulo kwa Timotheo kuhusiana na kanisa. (2:1-6:10). Paulo anatoa maelekezo hayo kutokana na hali kanisa lilikuwa linapitia, hali hiyo ni kuwepo kwa watu wanaofundisha elimu nyingine. Sehemu ya Tatu ni maelekezo ya mwisho ya mtume Paulo kwa Timotheo (6:11-21a). Maelekezo hayo pia yanahusiana na hali ya kanisa.

Sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu (1:3-20) Paulo anamkumbusha Timotheo lengo la kumuacha Efeso, ambalo lilikuwa ni kuwakataza watu wasifundishe elimu nyingine (1:3). Elimu hiyo nyingine haiwapeleki waamini katika upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema, na imani isiyo na unafiki. Walimu hawa wa uongo walikuwa wanafundisha sheria bila kujua matumizi sahihi ya sheria (1:4-7), Hivyo Paulo anamuonyesha Timotheo matumizi sahihi ya Sheria (1:8-11). Kabla ya kuendelea kuelezea kusudi la barua hii, Paulo anamkumbusha Timotheo wito wake (wito wa Paulo) ambao ameupata kwa Kristo aliyemwokoa kwa rehema zake mwenyewe (1:12-17). Baada ya kumbukizi hiyo anamalizia kuelezea kusudi la kumwandikia Timotheo waraka huu (1:18-20). Na kumtajia majina ya moja wapo ya watu waliokuwa wanafundisha elimu nyingine ambao Paulo anasema amempa shetani watu hao. Kumpa shetani watu hao maana yake kuwatoa katika ushirika wa waamini.

Sehemu ya Pili ya ujumbe mkuu (2:1-6:10) inagawanyika katika sehemu tatu tofauti kama ifuatavyo

A. Maelekezo juu ya mwenendo ndani ya Kanisa (2:1-3:16)

B. Paulo anamtaka Timotheo kuishindania Imani kwa kuishi na kufundisha kweli (4:1-16)

C. Paulo anamuelekeza Timotheo namna ya kushughulika na makundi tofauti tofauti ndani ya Kanisa (5:1-6:10).

Sasa fuatilia taratibu.

A. Maelekezo juu ya mwenendo ndani ya kanisa (2:1-3:16).

Katika kutoa maelekezo kuhusu mwenendo ndani ya kanisa Paulo anatoa maelekezo katika sehemu mbili, moja ni kuhusu kanisa lienende vipi wanapokutana pamoja (2:1-15), na pili ni kuhusu sifa za Viongozi wa kanisa (3:1-13). Paulo anataka kanisa likikutana maombi yafanyike kwa ajili ya watu wote lakini hasa viongozi wenye mamlaka ya kiutawala/serikali (2:1-7). Katika muktadha huo huo Paulo anatoa maelekezo kuhusu mwenendo wa wanaume (2:8) na mwenendo wa wanawake (2:9-15) wanapokutana pamoja. Kuhusu viongozi Paulo anataja sifa za mwangalizi/askofu (3:1-7) na sifa za mashemasi (3:8-13). Anahitimisha maelekezo kuhusu mwenendo ndani ya kanisa kwa kuweka wazi kwamba anatarajia kwenda Efeso hivi karibuni (3:14-15).

Ukiri wa Imani (3:16).

B. Paulo anamtaka Timotheo kuishindania Imani kwa kuishi na kufundisha kweli (4:1-16).

Katika kumuelekeza Timotheo kuilinda Imani kwa kuishi na kufundisha kweli Paulo anamuonyesha Timotheo kwamba ni dhahiri watu watajitenga na imani na kufuata mafundisho ya mashetani (4:1-5). Kutokana na ukweli huo Paulo anampa Timotheo maelekezo kadhaa ya kufanya ili kuishi katika utauwa na kufundisha kweli ili kujiokoa yeye mwenyewe na wale wasikiao (4:6-16).

C. Paulo anamuelekeza Timotheo namna ya kushughulika na makundi tofauti tofauti ndani ya Kanisa (5:1-6:10).

Paulo anamuelekeza Timotheo namna ya kushughulika na makundi tofauti tofauti katika kanisa, makundi hayo ni kama ifuatavyo

1. Wanaume (5:1)

2. Wanawake (5:2)

3. Wajane (5:3-16)

4. Wazee wa kanisa/Viongozi wa kanisa (5:17-25)

5. Watumwa (6:1-2).

6. Waalimu wa Uongo (6:3-10)

Sehemu ya Tatu ya mjumbe mkuu (6:11-21a), Paulo anamalizia na maelekezo ya mwisho kwa Timotheo hasa ikisisitiza kufuata utauwa kinyume na sifa za waalimu wa uongo alizozitaja hapo juu mstari wa 3-10 (6:11-16). Pia anamuagiza awaagize matajiri wasijivunie mali walizonazo (6:17-19) na anamsisitiza yeye kulinda amana aliyokabidhiwa (6:20-21a). Amana aliyokabidhiwa ni ujumbe wa injili ya kweli aliokabidhiwa.

Mwisho anafunga waraka wake kama ilivyokuwa kawaida ya nyaraka za karne ya kwanza (6:21b).

UFAFANUZI WA WARAKA WA KWANZA WA MTUME PAULO KWA TIMOTHEO..

Unakuja hivi karibuni…….