MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA KWANZA WA MTUME PAULO KWA WAKORINTHO.
MAELEKEZO
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI
Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho ni waraka wa muhimu sana katika kanisa. Hii ni kwa sababu ya mafundisho yake ya moja kwa moja kuhusu namna ya kuishi katika imani yetu. Waraka huu, pamoja na kuitwa wa kwanza katika Biblia zetu, kwa dhahiri sio wa kwanza; ni wa pili au wa tatu. Hii ni kwa sababu, katika waraka huu, Paulo anatoa ufafanuzi wa maneno aliyoyaandika katika waraka wake uliopita. Anasema “Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi. Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang’anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia. Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.” 1 Wakorintho 5:9-11.
Kwa kusema hivyo, inaonyesha wazi kwamba Mtume Paulo aliandika barua kwa Wakorintho zaidi ya zile mbili tulizonazo katika Biblia zetu. Kwa kusoma nyaraka hizi mbili, ni rahisi kupata picha kwamba Mtume aliandika barua angalau nne kwa kanisa la Korintho. Hivyo, kanisa la Korintho ndilo kanisa ambalo liliandikiwa na kupokea barua nyingi zaidi kutoka kwa Mtume Paulo. Idadi kubwa ya nyaraka inaonyesha ukaribu wa Mtume Paulo na Wakorintho, lakini pia inaonyesha jinsi ambavyo kanisa la Korintho lilivyokuwa na changamoto nyingi kama kanisa la sasa lilivyo. Hivyo, barua hii inatuhusu sana na ina manufaa makubwa kwa kanisa la karne ya ishirini na moja.
KANISA LA KORINTHO
Kanisa la Korintho lilizaliwa katika safari ya pili ya kimishenari ya Mtume Paulo. Katika safari hii, Paulo alifika Korintho kutoka Athene akiwa peke yake. Alipofika aliungana na Akila na Prisila waliokuwa wametoka Rumi baada ya wayahudi wote kufukuzwa. Wote wakakaa pamoja na wakafanya kazi pamoja huku Paulo akihubiri injili katika sinagogi kila Jumamosi. Baadaye Timotheo na Sila walifika Korintho wakitokea Makedonia wakaungana na Paulo katika kazi ya kuhubiri injili (2 Wakorintho 1:19). Baada ya Wayahudi kukataa injili, Paulo akaacha kwenda kwenye sinagogi akaamua kuhubiria kwenye nyumba ya Tito Yusto, mmataifa aliyekuwa na imani ya Kiyahudi. Nyumba ya Tito ilikuwa karibu kabisa na sinagogi ambalo Injili ya Paulo ilikataliwa (Matendo 18:1-7). Baada ya mkuu wa sinagogu aitwaye Krispo na nyumba yake yote kuamini, Wakoritho wengi wakaamini na kubatizwa (Matendo 18:8 na 1 Wakorintho 1:14-16). Pamoja na upinzani mkubwa, Paulo na timu ya kimisheni (akiwemo Timotheo, Sila, Akila na Prisila) walikaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu katika kupanda na kulielea kanisa. Uamuzi huu ulifikiwa baada ya Paulo kuambiwa na Bwana aendelee kukaa huko kwa kuwa yeye Bwana ana watu wengi katika mji huo.
Kuhusu aina ya watu waliokuwa sehemu ya kanisa, kwa sehemu kubwa Kanisa la Korintho lilikuwa na waamini wa daraja la chini katika hadhi ya kijamii. Asilimia kubwa walikuwa si watu wenye elimu, nguvu, vyeo wala utajiri wa fedha (1 Wakorintho 1:26-28; 11:22). Waamini wenye fedha na wenye vyeo katika serikali (kama vile Erasto, Warumi 16:23) walikuwa wachache. Kwa upande mwingine kanisa hili lilikuwa na watu wa makundi yote mawili, yaani mataifa na wayahudi pia (Matendo 18:1-18).
Kuhusu hali yao ya kiimani, kwa sehemu kubwa Wakorintho walikuwa ni watoto wachanga kiimani pamoja na kuwa na wingi wa karama na huduma za kiroho (1 Wakorintho 3:1-3).
MJI WA KORINTHO
Korintho ulikuwa ni mji wa kusini mwa Ugiriki katika karne ya kwanza. Mji huu kwa wakati huu uliokuwa chini ya utawala wa dola ya Rumi. Mji huu ulikuwa kwenye shingo ya nchi ya Korintho, inayounganisha rasi ya Peloponesi na sehemu kubwa ya Ugiriki bara. Korintho ulikuwa mji mkubwa wa kibiashara kwa kuwa ulikuwa na bandari mbili—moja upande wa mashariki na nyingine upande wa magharibi. Kutokana na shughuli kubwa za kibiashara, mji huu ulikuwa na mchanganyiko mkubwa wa watu. Mji ulikuwa na watu kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo watu kutoka Israeli, Misri, na Asia Ndogo. Pamoja na sifa hizi zote mji huu ulikuwa ni mji mpya uliojengwa miaka machache tu kabla ya Yesu. Ulijengwa na Warumi baada ya mji wa Korintho wa kigiriki (Korintho iliyokuwa chini ya utawala wa wagiriki) kubolewa.[1]
Kidini, mji wa Korintho ulikuwa na watu wengi wenye dini wanaoabudu miungu. Kwa sababu hiyo, mji ulikuwa na mahekalu ya miungu tofauti tofauti. Mahekalu ya miungu hiyo ni kama vile hekalu la Aphrodite (mungu mke wa uzuri na mapenzi), Apollo (mungu wa uponyaji na unabii) na Asklepios (mungu wa uponyaji, mwana wa Apollo). Na kwa sababu ya uwepo wa wayahudi kulikuwa na sinagogi pia kama anavyoeleza Luka katika Matendo 18.
Katika mahekalu mengi yaliyokuwa Korintho wanyama walitolewa kafara kama sehemu ya ibada, na sherehe za kula nyama hizo zilifanyika huku zikialika watu mbalimbali. Mahekalu haya kwa kuwa yalijengwa na vyumba mbalimbali kwa ajili ya sherehe hizo, basi hata waamini walialikwa huko. Hii ndio maana Wakorintho walimuuliza Paulo kuhusu kushiriki au kutokushiriki katika sherehe hizo (1 Wakorintho 8-10). Lakini pia nyama zingine kutoka kwenye mahekalu haya zilipelekwa sokoni na kuuzwa. Kwa sababu hiyo pia, ndio maana Mtume Paulo aliandika kwa kirefu juu ya jambo hili.
Jambo jingine la msingi kufahamu kuhusu Korintho ni kwamba huko Korintho kulikuwa na mashindano ya michezo yaliyoitwa “Michezo ya Isthmia”, yaliyofanyika kila baada ya miaka miwili. Mashindano haya yalihusisha michezo kama mbio, kuruka viunzi, mashindano ya farasi, na mingine mingi, ikifanana na michezo ya Olimpiki ya hivi sasa. Hii ndiyo sababu Paulo aliandika: “Kila ashindaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo, bali sisi tupokee taji isiyoharibika” (1 Wakorintho 9:25). Ujumbe huu ulikuwa wa kueleweka kwa urahisi kwa Wakorintho kwa kuwa walikuwa katika muktadha huu wa kimichezo.
Kwa ujumla, Korintho ulikuwa ni mji mkubwa uliojaa watu kutoka mataifa mbalimbali, mji wenye uchumi wa biashara, na ulikuwa na maisha ya starehe nyingi kama ilivyo miji mikubwa ya leo.
Athari za mji wa Korintho ya kigiriki kwenye Korintho ya kirumi.
Kama tulivyojifunza hapo juu kwamba Korintho ya Kwanza (Korintho ya Kigiriki) ilibomolewa na Korintho mpya ya Kirumi ikajengwa. Korintho hii mpya ilibeba athari kadhaa kutoka Korintho ya zamani. Pamoja na Korintho ya Kigiriki kubomolewa, kuna ushahidi kwamba kulikuwa na masalia ya watu walioendelea kuishi hapo. Kutokana na masalia hawa, kuna uwezekano mkubwa kwamba Korintho mpya ya Kirumi ilikuwa na sifa kama Korintho ya kwanza.
Moja, ya mambo ambayo yalikuwa ni athari za Korintho ya zamani ni uwepo wa zinaa iliyokithiri. Katika Korintho ya Kigiriki, mji ulikuwa na kiwango cha juu cha uasherati kiasi kwamba kufanya zinaa kuliitwa “Kukorinthia”, na istilahi “Msichana wa Korintho” ilitumika kama tamathali ya usemi kumaanisha kahaba. Kama ambavyo leo makahaba wanapewa majina tofauti tofauti, ndivyo hivyo hivyo makahaba katika nyakati hizo, nje na ndani ya Korintho, waliitwa “Wasichana wa Korintho.”
Kwa sababu ya athari hizi, ndiyo maana kanisa la Korintho lilikuwa na changamoto kubwa ya zinaa, jambo ambalo Mtume Paulo alilipinga kwa nguvu zote.
KUSUDI LA WARAKA
Mtume Paulo aliandika barua hii akiwa Efeso wakati wa safari yake ya tatu ya kimishenari. Kutoka huko, Paulo aliandika barua hii kwa sababu kubwa mbili.
Moja, aliandika kutoa suluhisho kutokana na matatizo yaliyokuwa yanaendelea katika kanisa. Taarifa za matatizo haya Paulo alizipata kutoka kwa familia ya Kloe (1 Wakorintho 1:11). Matatizo yaliyokuwa yamelikumba kanisa ni kama vile mgawanyiko katika kanisa (1 Wakorintho 1-4), maisha ya zinaa ndani ya kanisa (5:1-13; 6:12-25), na waamini kupelekana mahakamani (6:1-11).
Sababu ya pili ya Mtume Paulo kuandika barua hii ni kutoa majibu kwa maswali ambayo Wakorintho walimuandikia. Mambo haya yalihusu ndoa (7:1-40), uhuru wa Kikristo (8:1–11:1), kusanyiko (11:2–14:40), na kuhusu ufufuo (15:1-58). Kumbuka kwamba, pamoja na kuitwa ya kwanza, hii haikuwa barua ya kwanza, hivyo kuna mambo mengine ambayo Mtume Paulo anatoa ufafanuzi kwa sababu Wakorintho walimuelewa vibaya katika barua yake ya kwanza (5:9).
MPANGILIO WA KITABU
| MAELEZO | 1 WAKORINTHO |
| UTANGULIZI Salamu, Shukrani na Maombi | Sura ya 1:1-9 |
| MAJIBU YA YALE ALIYOSIKIA | SURA YA 1 HADI YA 6 |
| a) Mgawanyiko katika kanisa | Sura ya 1:9-4:21 |
| b) Mtu anayeishi na mama yake wa kambo kimapenzi. | Sura ya 5:1-13 |
| c) Wapendwa kupelekana mahakamani | Sura ya 6:1-11 |
| d) Wanaume kufanya zinaa na makahaba | Sura ya 6:12-25 |
| MAJIBU YA YALE WALIYOMUANDIKIA | SURA YA 7 HADI YA 15 |
| e) Tabia ndani ya Ndoa | Sura ya 7:1-24 |
| f) Tabia kwa ambao hawajawahi kuoa/kuolewa | Sura ya 7:25-40 |
| g) Chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu. | Sura ya 8:1-13 |
| h) Kuabudu sanamu (Kwenda kwenye sherehe za waabudu sanamu) | Sura 9-10:18 |
| i) Chakula kinachouzwa sokoni lakini kilitolewa sadaka kwa sanamu | Sura ya 10:18-11:1 |
| j) Wanawake kufunika vichwa katika kusanyiko | Sura ya 11:2-16 |
| k) Mgawanyiko wakati wa meza ya Bwana | Sura 11:17-34 |
| l) Karama za rohoni | Sura ya 12-14 |
| m) Ufufuo wa miili yetu | Sura ya 15 |
| HITIMISHO | SURA 16:1-24 |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI
Barua hii kama barua nyingine inaanza na utangulizi (1:1-9). Utangulizi huu una anuani, salamu na shukrani. Katika anuani kuna mambo mawili, Moja, Paulo anajitambulisha akiwa pamoja na Sosthene (1:1) na pili anatambulisha wapokeaji wa barua yake (1:2). Kabla ya shukrani Paulo anatoa salamu kwa Wakorintho (1:3). Baada ya hayo, Paulo anatoa shukrani zake kwa Mungu kwa ajili ya yale aliyoyafanya kwa Wakorintho (1:4-9). Pamoja na neema ya Mungu na uaminifu wake kwao, kuna jambo moja la msingi sana katika kuelewa barua nzima ambalo mtume analisema katika shukrani hii. Mtume anasema “kwa kuwa katika kila jambo mlitajirika katikayeye, katika maneno yote, na maarifa yote“ na “hata hamkupungukiwa na karama yo yote.” Kwa kauli hizi, mtume Paulo anaonyesha kwamba Wakorintho walikuwa na utajiri wa karama za Roho hasa zinahusisha maneno, hekima na maarifa.
Baada ya utangulizi huo, Paulo anakwenda moja kwa moja kwenye sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu (1:10-6:25). Katika sehemu hii kuna matatizo makubwa manne: Mgwanyiko katika kanisa (1:10-4:21), Kanisa kutochukua hatua yeyote katikati ya zinaa (5:1-13), waamini kupelekana mahakamani (6:1-11) na Wanaume kufanya zinaa na makahaba (6:12-20).
Katika tatizo la kwanza, Paulo anaanza kwa kuwaita Wakorintho kuishi kwa umoja. Paulo anawaita kuishi kwa umoja kwa sababu amepewa taarifa kwamba kati yao kuna mgawanyiko (fitina/faraka). Mgawanyiko huu unadhihirika kwa Wakorintho kujichagulia utambulisho kutokana na waalimu/viongozi wanaowapenda au kuwakubali zaidi. Kwa nguvu zote, Paulo anawaonyesha kwamba Kristo hajagawanyika, hakuna mtumishi aliyekufa kwa ajili yao, na hawakubatizwa kwa jina la kiongozi yeyote—siyo yeye, wala Apolo, wala Petro (1:10-17).
Wakorintho walijichagulia waalimu hao kwa sababu waliiga tabia hiyo kutoka katika jamii (au walibeba utamaduni waliokuwa nao kabla ya kuamini), ambapo wanafalsafa (walimu wa hekima) walikuwa na wanafunzi, na wanafunzi walijitambulisha kwa kubeba utambulisho wa majina ya wanafalsafa husika. Wanafunzi walichagulia wanafalsafa kwa kupima hekima zao na namna wanavyoweza kuwasilisha kwa ufasaha hekima hizo. Hivyo, mzizi wa tatizo la mgawanyiko kwa Wakorintho ni hekima ya kidunia. Na tatizo hili la mgawanyiko lilidhihirika kwa kila kundi ndani ya kanisa kuchagua mwalimu/kiongozi linayemkubali kwa viwango vyao.
Katika kushughulikia mzizi wa tatizo, Paulo anawaonyesha Wakorintho kwamba wao (Paulo, Apolo na Kefa) si wanafalsafa bali ni wahubiri wa Injili. Injili ambayo yeye aliihubiri kwao (Neno la msalaba), tofauti na hekima ya kibinadamu (falsafa), ni uweza wa Mungu kwa wale wanaookolewa. Paulo anasisitiza kwamba ujumbe wa msalaba, unaoonekana kuwa upuuzi (kinyume cha hekima) kwa wanaopotea, ni nguvu na hekima ya Mungu kwa waaminio (1:18-25).[2] Kwa kutaka kuwathibitishia Wakorintho kwamba Mungu anafanya kazi tofauti na hekima ya dunia hii, Paulo anawathibitishia kwa kuwatazamisha maisha yao wenyewe. Wao wenyewe Mungu aliwachagua kuokolewa, pamoja na kwamba hawakuwa miongoni mwa wenye hekima, wenye nguvu, wala miongoni mwa wenye vyeo (1:26-31). Baada ya kueleza kuhusu wao, Paulo anaelezea jinsi alivyokuwa kwao na jinsi alivyohubiri. Kuhubiri kwake hakukuwa kwa hekima wala kwa ufasaha wa uwasilishaji (kama wanafalsafa) bali kuhubiri kwake kulihusu Kristo na kusubiwa kwake, tena kulifanyika kwa Roho ili imani yao isijengwe kwenye hekima ya kibindamu (2:1-5).
Baada ya kukosoa hekima ya kibinadamu kwa kirefu (hekima iliyotumiwa na Wakorintho na mwishowe ikasababisha mgawanyiko), Paulo anawajulisha Wakorintho kwamba kuna hekima itokayo kwa Mungu, tofauti na hekima ya kidunia. Hekima hii ni ile ambayo inapatikana kwa ufunuo wa Roho, ambayo wakuu wa dunia hii hawana kwa kuwa ni siri ya waamini tu (2:6–10). Hekima hii, kwa kuwa inapatikana kwa ufunuo wa Roho, inaeleweka vizuri kwa waamini waliokomaa / watu wa Roho. Watu wa tabia za mwilini hawawezi kuipokea (2:11–16). Baada ya kuelezea sifa hizo za hekima ya kimungu, Paulo anawaweka wazi Wakorintho kwamba yeye hakuwafundisha hekima hii ipasavyo kwa kuwa wao walikuwa na tabia za mwilini, na hata sasa bado hawawezi kuipokea hekima hii ya kimungu ipasavyo kwa kuwa bado ni watu wa tabia za mwilini, na mgawanyiko kati yao unathibitisha hilo (3:1-4).
Baada ya kumalizana na mzizi wa tatizo, Paulo anarudi kwenye tatizo lililokuwa linaonekana, yaani mgawanyiko kutokana na watumishi/viongozi waliowatumikia. Kwa kutumia mifano miwili — mfano wa ukulima na wa ujenzi — Paulo anawakumbusha Wakorintho kwamba wao ni watumwa tu wa Bwana Yesu kwa ajili yao, ambao wanafanya kazi tofauti tofauti kulingana na Bwana alivyowapa kufanya na ambao kazi zao zitapimwa na Bwana kwa moto siku ya hukumu. Wao wasiwe sababu ya kuligawanya kanisa (3:5–15). Kusisitiza umuhimu wa umoja wa kanisa, Paulo anawajulisha Wakorintho kwamba wao ni hekalu la Mungu, kwa kuwa Roho wa Mungu anakaa katikati yao, na Mungu yuko tayari kumharibu mtu yeyote ambaye yuko tayari kuliharibu hekalu hilo (3:16–17).
Katika kuhitimisha, Paulo anatoa maelekezo tena juu ya kiini cha tatizo (hekima), juu ya tatizo lenyewe (mgawanyiko kutokana na waalimu) na kuhusu kuhukumu (kupima) utumishi. Mambo haya yote matatu ni marudio ya kile ambacho ameshakisema hapo juu na yana uhusiano mkubwa. Katika jambo la kwanza, anawasihi waachane na hekima ya kidunia, wanyenyekee ili wapate hekima ya kimungu (3:18–20). Katika jambo la pili, anatoa maelekezo wasijifie wanadamu kabisa, kwa kuwa wote wapo kwa ajili yao (3:21-23). Na mwisho anawaambia Wakorintho waache hukumu (upimaji wa kazi) ya utumishi kwa Mungu. Yeye Paulo hastahili kuhukumiwa na wao, wala na mwanadamu yeyote; hata yeye mwenyewe hawezi kujihukumu, kwa kuwa anayestahili kuhukumu ni Bwana (4:1-5).
Katika kupambana na tatizo hili la mgawanyiko Paulo amemhusisha sana Apolo (Petro amemtaja tu jina bila maelezo ya kazi yake tofauti na Apolo), hivyo anawajulisha Wakorintho kwamba hakuwa anamkosoa Apolo, bali alikuwa akizungumza kuhusu Apolo na yeye ili kuwaonya wao wasijivune kwa chochote (4:6-7). Baada ya hapo, Paulo anafafanua zaidi onyo lake kuhusu kujivuna kwa Wakorintho. Kwa kutumia kejeli anawadhihaki Wakorintho kwa madai yao kwamba “wameshiba,” “wametajirika,” na kwamba “wameanza kutawala.” Kujiona kwao namna hiyo kunaonyesha jinsi mtazamo wao ulivyopotoka kabisa, kwani hali ya mitume inaonyesha tofauti na madai yao. Paulo na mitume wengine wanaonekana kama “wapumbavu,” “watu dhaifu,” na “wasiostahili heshima.” Kama mitume wanaonekana hivyo wao watajisifiwe kinyume chake? Yaani wao walitakiwa kujisifia sifa zile walizonazo mitume (4:8-13). Katika kuhitimisha hoja yake kuhusu tatizo hili la kwanza, Paulo anawaita Wakorintho kumfuata yeye katika njia zake kwa kuwa yeye ndiye Baba yao. Kwa kuwa yeye ni Baba yao, ndio maana anamtuma Timotheo kwao ambaye ni mtoto wake mwaminifu ambaye atawakumbusha mwenendo wake, na baadaye yeye mwenyewe ataenda pamoja na kuwepo kwa watu wanaosema kwa kiburi kwamba hatarejea kwao (4:14-21).
Baada ya kumaliza kwenye tatizo la kwanza, Mtume anahamia kwenye tatizo la pili. Tatizo la pili lilikuwa ni kanisa kutochukua hatua yeyote kwa mtu aliyekuwa anaishi katika maisha ya zinaa na mama yake (mke wa baba yake). Kanisa lilijivuna (kujisifu) badala ya kusikitishwa. Katika tatizo hili, Paulo anatoa suluhisho kwa kanisa; wanapokusanyika pamoja kwa jina la Yesu, wamtoe mtu huyo katika ushirika na wamkabidhi mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uangamizwe, lakini roho yake ipone siku ya kuja kwa Bwana. Lengo la kufanya hivyo ni kulisafisha kanisa, yaani, kanisa lisiharibike kwa kuiga mwenendo mbaya (5:1-13).
Tatizo la tatu ambalo Mtume Paulo alipewa taarifa na watu wa nyumbani mwa Kloe ni waamini kupelekana kwenye mahakama za wasioamini. Ni wazi kwamba hili lilitokana na mtazamo wao potofu kuhusu hekima (Kama tatizo la kwanza); kwa kuwa walidhani kwamba mahakimu wa kidunia walikuwa na hekima zaidi kuliko wao katika kutatua migogoro. Katika tatizo hili, Mtume Paulo anatoa suluhisho kwamba, waamini wanatakiwa kutatua migogoro yao wenyewe na siyo kwenda kwenye mahakama za kidunia. Sababu ya kutakiwa kufanya hivyo ni kwamba, wao watahusika katika kuhukumu wasioamini katika hukumu ijayo. Kama wao watahusika katika hukumu ijayo, kuhukumiana katika mahakama za wasioamini ni kutokujua nafasi yao katika Mungu (6:1-11).
Tatizo la mwisho alilopewa habari zake ni kuhusu wanaume waliotaka kuendelea kuishi maisha ya kufanya zinaa na makahaba. Walitaka kuishi hivyo kwa kuwa waliamini, kutokana na uhuru waliokuwa nao ndani ya Kristo “vitu vyote ni halali,” na kama ambavyo “vyakula ni kwa ajili ya tumbo,” basi mwili pia ni kwa ajili ya zinaa. Maelekezo ya Paulo kutokana na tatizo hili ni kwamba, kila mtu akimbie zinaa. Kwa nini wakimbie zinaa? Kwanza, uhuru wa Kikristo maana yake ni kutokuongozwa au kutawaliwa na kitu chochote na sio kufanya kila kitu. Pili, kwa kuwa miili ya waamini ni viungo vya Mwili wa Kristo na pia ni hekalu la Roho Mtakatifu, haiwezekani miili hiyo ikaunganishwa na makahaba. Hii ni kwa sababu zinaa inaunganisha watu wawili na kuwafanya kuwa mwili mmoja (6:12-20).
Baada ya Paulo kumaliza kutoa mwitikio wake kuhusu yale aliyosikia yakiendelea kwenye kanisa, anaingia kujibu maswali ambayo Kanisa la Korintho lilimuandikia. Maswali hayo yalihusu mambo makubwa manne ambayo ni; ndoa na useja (7:1-40), uhuru wa Kikristo katikati ya ibada za sanamu (8:1–11:1), mwenendo katika kusanyiko (11:2–14:40) na Ufufuo wa wafu (15:1-58).
Kuhusu ndoa na useja, Paulo anaanza kutoa majibu kwa kukosoa baadhi ya Wakorintho waliokuwa wanasema “ni heri mwanamume asimguse mwanamke.” Paulo anasema kwa walioko katika ndoa tayari wasinyimane (yaani, wagusane); badala yake, kila mmoja ampe mwenza wake haki kamili za ndoa (7:1-7). Kwa ambao hawajaoa na wajane, Paulo anawashauri wabaki hivyo hivyo, yaani bila ndoa (7:8-9). Kwa waamini wenye ndoa, Bwana anaagiza wasiachane na ikitokea wameachana, wabaki hivyo hivyo bila kuoa/kuolewa tena au warudiane tena (7:10-11). Kwa wenye ndoa ambao mmoja wao sio mwamini, wasitafute kuachana isipokuwa asiyeamini ametaka (7:12-16). Yote katika yote, kila mmoja abaki kwenye hali ile ile ambayo Bwana alimwita nayo, lakini kama itabadilika ni sawa pia (7:17-24).
Kutokana na usemi wa “ni heri mwanamume asimguse mwanamke,” Wakorintho waliona pia mabikira waliochumbiwa wasiolewe tu. Paulo anakubaliana na ukweli kwamba ni vizuri watu hawa wasiolewe, lakini sio kwa sababu theologia ya mbovu ya Wakorintho. Paulo anatoa sababu mbili za yeye kukubali kwamba ni vizuri wanawali hawa wasiolewe. Moja, kwa sababu ya shida (inawezekana mateso) iliyokuwa inaendelea Korintho. Pili ni kwa sababu mtu akiolewa/kuoa, umakini wake unagawanyika. Kwa upande mmoja hujishughulisha na mambo ya Bwana, na upande mwingine hujishughulisha na mambo ya mumewe/mkewe. Hivyo ni vizuri mabikira hawa wasioolewe. Pamoja na Paulo kupendekeza useja, anamaliza kwa kusema, mtu akiona hawezi kubaki bila ndoa, aoe, kwa kuwa hilo nalo ni mapenzi ya Mungu (7:25-40).
Jambo la pili ambalo Wakorintho walimuandikia Mtume Paulo ni kuhusu uhuru wa kikristo katikati ya ibada ya sanamu. Kuhusu waamini kwenda kula chakula kilichotolewa sadaka kwenye mahekalu ya miungu (Rejea maelezo ya mji wa Korintho katika utangulizi), Paulo anasema ni kweli ile miungu inayotolewa hizo sadaka si kitu kwa waamini, kwa hiyo kula chakula huko “inaweza kuwa si shida” kwa waamini wenye ujuzi. Lakini Paulo anasema mwenendo wetu haongozwi na ujuzi tu bali na upendo. Kwa mwamini yule ambaye hajafikia uelewa huu; kujua kwamba vile vinavyoabudiwa katika mahekalu hayo sio Mungu, na kama mwamini huyo alitoka kwenye ibada hizo kabla ya kuamini, akiona mwamini mwenye ujuzi anakula hicho chakula, yeye ataiga, lakini yeye atakula kwa kushiriki kabisa ibada ya sanamu kutokana na udhaifu wake wa imani. Kitakachokuwa kimesababisha mwamini huyu kufanya dhambi (kufanya ibada ya sanamu) ni mfano mbaya wa mwamini mwenye ujuzi. Kwa sababu hiyo, Paulo anasema waamini wenye ujuzi wajizuie kula chakula hicho ili wasiwakwaze[3] waamini wadhaifu (8:1-13). Mpaka hapa Paulo anawazuia Wakorintho wanaodai kuwa wana haki na uhuru wa kwenda kushiriki chakula katika mahekalu ya miungu kwa kutumia kanuni ya upendo.
Katika kusisitiza ujumbe wake, Paulo anajielezea jinsi ambavyo yeye amekuwa mfano halisi wa hiki anachokisema kwa Wakorintho. Paulo anasema, ingawa yeye ni mtume na ana haki kadhaa kama vile kuoa, kutofanya kazi za mikono na kupokea fedha kutoka kwao kwa sababu ya kazi yake ya injili (9:1-14), lakini amejizuia kutumia haki hizo kwa ajili ya wengine (9:15-23). Mwishoni, katika kueleza mfano wa maisha yake, anatoa mfano: Paulo anasema kwamba kama ambavyo wanariadha washindi huwa na nidhamu ya hali ya juu ya kujizuia vitu vyote ili tu wapokee taji iharibikayo, yeye anajitesa (kama alivyoelezea hapo juu kuhusu kunyima haki zake) ili asije akawahubiri wengine yeye akakataliwa mwishoni (9:24-27). Kwa mfano huo Paulo anawaita Wakorintho kuishi kwa kanuni ya upendo (kujizuia kwa ajili ya wengine) mpaka mwisho kama wanariadha ili mwishoni wasije wakakataliwa.
Kwa sababu hili ni jambo la msingi, Paulo anatoa mfano wa watu waliokataliwa mwishoni, yaani kizazi kilichookolewa kutoka Misri na kufia jangwani.Wao waisraeli waliokolewa na Mungu, walibatizwa wawe na Musa, walishiriki chakula na kinywaji cha kiroho (kutoka kwa kristo)[4] lakini mwishoni walifia jangwani bila kuingia kwenye nchi ya ahadi. Sababu ya kutokufika nchi ya ahadi ilikuwa ni; walitamani mabaya, waliabudu sanamu, walifanya uasherati, walimjaribu Bwana na kumng’unikia. Hayo yote, Paulo anasema yaliandikwa ili kuwaonya waamini wa nyakati hizi ili kila anayedhani amesimama angalie asianguke. Pamoja na hayo, Mungu hataruhusu Wakorintho wajaribiwe kupita uwezo wao, na zaidi atawapatia njia ya kutokea, ili waweze kudumu hadi mwisho (10:1-13).
Toka mwanzoni wa sura ya nane mpaka hapa Paulo alikuwa anajenga hoja ya kuwakataza Wakorintho kwenda kula chakula kwenye mahekalu ya miungu. Mwishoni anatoa jibu la wazi kwamba wakimbie ibada ya sanamu. Pamoja na hoja ya kutumia kanuni ya upendo na maonyo kutoka kwenye mfano wa kizazi cha jangwani, hapa napo anatoa ufafanuzi kwa namna mbili kuhusu kwa nini wanatakiwa kukimbia ibada ya sanamu (kula chakula kwenye mahekalu ya miungu). Moja, haiwekani kushiriki damu na mwili wa Yesu na tena kushiriki meza ya miungu, ushirika ni wa upande mmoja tu. Pili, waisraeli (hasa walawi) waliokuwa wanakula dhabihu sawa na maagizo ya Mungu walikuwa na ushirika na hiyo madhabahu, hivyo kula kwenye madhabahu hizo za miungu ni kutengeneza ushirika nazo (10:14-18).[5]
Kwa kuwa mwanzoni Paulo alikubaliana na Wakorintho wenye ujuzi kwamba ile miungu si kitu, sasa anaposema kula kwenye madhabahu za miungu hiyo kunatengeneza ushirika, ina maana hiyo miungu ni hai? Au kile kilichotolewa sadaka ni hai? Paulo anasema hapana, ile miungu kweli haina uhai, ila nyuma yake kuna nguvu ya mashetani (mawakala wa shetani), na hivyo hataki Wakorintho washirikiane na mashetani. Hata hivyo, kushirikia na miungu kunamtia Mungu wivu (10:19-21).
Mpaka hapa Paulo amewakataza Wakorintho kwenda kwenye mialiko ya kula chakula kilichotolewa sadaka kwenye mahekalu ya miungu. Kwa kuwa chakula hiki kilichotolewa kwa miungu, baada ya kubaki katika sherehe zilizofanyika kwenye hekalu husika, kilipelekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa, na watu walinunua, Mtume Paulo anatoa maelekezo ya nini kifanyike kwenye muktadha huu pia. Hapa kuna hali halisi mbili; Moja, Wakorintho wafanye nini kuhusu chakula hicho kinachouzwa sokoni? Na pili, kama mtu asiyeamini amewaalika nyumbani kwake, wafanye nini? (Kumbuka hoja ya mwanzo ilikuwa ni kwenda kwenye mahekula kushirikia chakula, sasa ni kununua sokoni na kula nyumbani kwa asiyeamini). Paulo anasema, wako huru kula kila kitu kinachouzwa sokoni bila kuulizauliza kilikotokea kwa kuwa vitu vyote ni mali ya Mungu (10:22–26). Pia, kama wamealikwa na mtu asiyeamini nyumbani kwake, wale chakula bila kuuliza chanzo cha chakula hicho. Lakini kama wataambiwa kwamba chakula hicho kilitolewa kiwe sadaka, wasile. Wasile kwa sababu ya yule aliyetoa taarifa. Mtume anasema hivyo kwa kuwa aliyetoa taarifa ametoa taarifa kwa kuwa anajua kuwa kwa waamini kula chakula hicho si sawa.
Pamoja na kuwa na uhuru wa kula na pamoja na kula kwa shukrani, wasile ili wasiwakoseshe Wayahudi wala Wayunani wala kanisa la Mungu, kama ambavyo yeye Paulo anawapendeza watu wengine pasipo kutafuta faida yake mwenyewe. Mwisho, Paulo anasisitiza Wakorintho kumfuata yeye kama anavyomfuata Kristo, yaani, wajizuie kwa faida ya wengine kama yeye anavyofanya hivyo akiiga mfano wa Kristo (10:27-11:1).
Baada ya kumaliza jambo hilo la kuhusu kula chakula kilichotolewa kama sadaka kwa miungu, Paulo anajikita kwenye kueleza mwenendo unaotakiwa kwa waamini wanapokutana kwa pamoja. Katika hili, tatizo la Wakorintho lilikuwa ni kutafuta umoja mahali ambapo walihitaji utofauti, na utofauti mahali ambapo walipaswa kuwa na umoja.
Mtume anaanza kwa kufundisha namna gani wanawake wavae (tofauti na wanaume) wanapofanya maombi au kuhutubu katika kusanyiko. Wanawake wanapaswa kufunika vichwa kwa sababu mwanamke ni utukufu wa mwanamume (11:2–10), lakini pia kwa sababu za kitamaduni, na zaidi, hiyo ndiyo desturi ya makanisa ya Mungu (11:11–16). Katika eneo hili, wao walitaka umoja wakati ilitakiwa kuwe na utofauti kati ya mwanamke na mwanamume.
Wakorintho, badala ya kuwa na umoja kwenye Meza ya Bwana, wao wakagawanyika. Mgawanyiko ulikuwa kati ya matajiri na maskini, walioshiba na wenye njaa. Mtume anakemea mgawanyiko huo kwa kuwa Meza ya Bwana kusudi lake ni ushirika na siyo kushiba. Na kwa sababu walishasababisha mgawanyiko, ndiyo maana wengine miongoni mwao walikufa, wengine wanaumwa kwa kuwa walishiriki Meza ya Bwana isivyostahili, yaani walishiriki kwa kuligawanya kanisa (11:17–34).
Tena, badala ya kuwa na mgawanyiko wa karama, Wakorintho wao walitaka wote watumie karama moja, yaani karama ya kunena kwa lugha. Katika hili, Paulo anaanza kwa kueleza kwamba kuna utofauti wa karama za kiroho na anataja mifano ya karama hizo. Ingawa karama hizo ni tofauti, zote zinatoka kwa Roho mmoja. Tena, Paulo anasisitiza kwamba kusudi la karama hizi ni faida ya wote, na si kwa ajili ya kujitukuza. Pia, Paulo anasema hakuna karama iliyo bora zaidi ya nyingine kwa thamani au umuhimu. Kwa kutumia mfano wa mwili wa mwanadamu, Paulo anasisitiza utofauti wa karama na kutegemeana kwa waamini wote wenye karama tofauti tofauti. Kwa kutaja tena karama zingine, Paulo anasisitiza kwamba karama ziko tofauti tofauti (12:1–31). Sababu ya mtume Paulo kupinga vikali kujitukuza au kutukuza karama fulani ni kwa sababu Wakorintho waliona kuwa na karama ya kunena kwa lugha ndiyo bora.
Sasa kabla hajapindua mtazamo huo na kueleza karama ipi ni bora zaidi, anawaeleza Wakorintho nini ni bora kuliko karama. Upendo ndiyo bora kuliko karama. Karama yoyote pasipo upendo ni bure (13:1–3). Upendo ni kipaumbele kuliko karama kwa sababu, kwa sifa zake, upendo unafaidisha wengine (13:4–7). Kwa muktadha huu, karama zinaweza kufanya kazi bila kuleta manufaa kwa wengine kama zitafanya kazi nje ya upendo. Mwisho, upendo ni kipaumbele kwa kuwa huo utadumu milele (13:8–13).
Baada ya kueleza ukweli huu, kwamba upendo ndiyo kipaumbele, Paulo anarudi kurekebisha mtazamo wa Wakorintho wa kudhani karama ya kunena kwa lugha ndiyo bora kuliko karama nyingine. Paulo anasema karama ya kuhutubu (yaani, karama ya kutumia lugha ya kawaida kulifundisha kanisa) ndiyo bora kuliko kunena kwa lugha, isipokuwa pale lugha inapotasfiriwa ili kanisa lijengwe (14:1–5). Kwa Paulo, kinachofanya karama kuwa bora ni faida ya karama hiyo kwa kanisa, siyo kumtukuza mwenye karama. Kumbuka, sura ya kumi na mbili amesisitiza hakuna karama bora au yenye umuhimu zaidi; hivyo, anachofundisha hapa ni kurekebisha upimaji wa umuhimu au ubora wa karama uliokuwa unafanywa na Wakorintho.
Paulo anatumia mifano mitatu katika kufafanua alichokisema. Mfano wa kwanza ni wa yeye mwenyewe, mfano wa pili ni wa filimbi na kinubi, na wa tatu ni wa baragumu. Mifano hii yote ni ya kusisitiza kwamba Wakorintho watamani karama za kunena maneno yanayoeleweka na kanisa ili kanisa lijengwe (14:6–19). Kwa kuwa Paulo hapingi kunena kwa lugha, anaweka wazi kwamba kunena kwa lugha ni ishara kwa ajili ya wasioamini, lakini kuhutubu ni kwa ajili ya waamini. Hii ndiyo maana anatamani wanapokutana pamoja wanaohutubu wawe wengi kuliko wanaonena kwa lugha (14:20–25). Pamoja na hayo yote, mambo yote katika kusanyiko yafanyike kwa mpangilio ili kanisa lijengwe na si kwa machafuko (14:26–33). Katika kupinga machafuko na kusisitiza mpangilio, Mtume Paulo anaelekeza macho yake kwa wanawake. Anaagiza wanawake wasinene katika kanisa, hasa wasiulize maswali, bali waulize waume zao nyumbani wakitaka kujifunza (14:34–36). Kumbuka hapo juu, Mtume alisema wanawake wanapohutubu wafunike vichwa vyao (11:5), kwa hiyo maneno haya si katazo la wanawake kuhutubu. Katazo liko kwenye kuzungumza wakati wa kujifunza, tena hasa kuhusu kuuliza maswali.
Katika kuhitimisha fundisho hili la namna gani waamini wanatakiwa kuenenda wanapokutana, Paulo anamaliza kwa maagizo matatu ambayo ni marudio ya yale aliyoyasema tayari. Moja, wote, pamoja na wale wanaojiona kuwa ni wa kiroho, watambue kuwa anayoyaagiza ni maagizo ya Bwana. Pili, wote watake sana kuhutubu bila kuzuia kunena kwa lugha. Tatu, mambo yote katika kusanyiko yafanyike kwa uzuri na kwa utaratibu (14:37–40).
Baada ya kumaliza jambo hilo, Paulo anaingia kwenye kutetea ufufuo wa miili. Baadhi ya Wakorintho walikuwa na mashaka kuhusu ulazima na uwepo wa ufufuo wa wafu mwisho wa ulimwengu huu. Kama kawaida, Wakorintho waliiga au walitoka na mtazamo huu kutoka kwenye upagani. Katika upagani kulikuwa na mafundisho ya wanafalsafa ambayo yalikuwa yanaonyesha kwamba mwili (na vitu vyote vinavyoonekana) ni mwovu bali roho ni safi. Katika mafundisho haya wokovu ulikuwa ni kutoka katika mwili na kurejea katika roho ambayo ni safi. Hivyo, kwa mafundisho haya Wakorintho hawakuona umuhimu au ulazima wa ufufuo kwa kuwa kwa wao mwili ni mwovu. Kutatua theologia hii mbaya, Paulo anaanza na ufufuo wa Yesu. Paulo anawakumbusha Wakorintho injili aliyowafundisha, ambayo ilijikita kwa Kristo aliyesulubiwa na kufufuka, kisha anatoa ushahidi wa mashuhuda waliomwona Kristo baada ya kufufuka (15:1–11). Katika kuendelea kujenga hoja, Paulo anatumia upande hasi na upande chanya. Kwa upande hasi, Paulo anasema kama Kristo hakufufuka basi imani yetu yote ni bure (15:12-19). Upande chanya Paulo anasema, Kristo amefufuka na hivyo yeye ni limbuko katika ufufuo. Kwa kuwa Yesu ni limbuko ni hakika waamini watafufuka kama Yesu alivyofufuka. Pamoja na hilo kufufuka kwa Yesu ndio njia ya Mungu kushughulika na adui aitwaye kifo (15:20-28). Lakini pia, Paulo anatumia maisha na matendo ya Wakorintho (kubatizwa kwa ajili ya wafu) na ya kwake mwenyewe (kuhatarisha maisha yake kwa ajili ya injili) kuonyesha kwamba yote hayo yanaonyesha kwamba kuna ufufuo wa wafu, kama ungekuwa haupo basi wanayofanya hayana maana kabisa (15:29-34).
Baada ya kumaliza kuelezea uhakika na ulazima wa ufufuo, Paulo anaulizwa, ufufuo utakuaje? Na miili ya ufufuo itakuaje? (inaonekana swali lenyewe lililenga kuthibitisha kwamba ufufuo hautakuwepo). Paulo anajibu kwa kutumia mfano wa mbegu. Kama ambavyo mbegu inakufa ili izae kitu kipya lakini chenye uhusiano nayo, ndivyo hivyo hivyo mwili wa sasa utakufa na kuzikwa katika hali ya udhaifu, lakini Mungu ataufufua na kuwa mwili tofauti kwa sifa, lakini unaoendana na wa zamani (15:35-38). Baada ya hapo, Paulo anasisitiza utofauti wa miili ya sasa na ule baada ya ufufuo kwa kuonyesha ubora wa mwili baada ya ufufuo. Maeneo saba yanaonyesha ubora wa miili ya ufufuo, manne yanahusiana na miili yenyewe (kuharibika/kutokuharibika; aibu/fahari; udhaifu/nguvu; asili/roho) na matatu yanahusiana na chanzo cha miili hiyo (Adamu wa kwanza/wa mwisho; mtu wa udongo/wa mbinguni; sura ya yule wa udongo/sura ya yule wa mbinguni (15:39-49). Mwisho, Paulo anahitimisha kwa kuelezea mabadiliko ya miili Mungu atakayoyafanya katika kuishinda mauti kabisa (15:50-58).
Baada ya fundisho hilo, barua inafikia tamati. Katika hitimisho la barua, Paulo anatoa maelekezo na taarifa kwa Wakorintho kuhusu mambo mbalimbali. Moja, anatoa maelekezo kuhusu kutoa sadaka kwa ajili ya watakatifu wa Jerusalemu. Wakorintho watoe sadaka hiyo kila siku ya kwanza ya juma, na yeye atatuma wawakilishi watakaoibeba sadaka hiyo na kuipeleka Yerusalemu, na yeye ataungana nao ikiwezekana (16:1-4). Pili, Paulo anawaambia Wakorintho mipango yake ya safari na ya kwenda kwao (16:5-9). Tatu, Mtume Paulo anawajulisha kanisa kuhusu Timotheo na Apolo; Timotheo ataenda kwao sasa hivi, lakini Apolo mpaka baadaye akipata nafasi (16:10-12). Nne, Mtume anatoa hamasa fupi fupi za kuishi maisha ya imani (16:13-18). Baada ya hapo, anamaliza waraka wake kwa salamu za mwisho (16:19-24).
FOOTNOTES
[1] Kumbuka, Wagiriki walitangulia katika utawala, wakifuatiwa na Warumi. Hivyo, Korintho iliyobomolewa ni ile iliyokuwa chini ya utawala wa Wagiriki.
[2] Katika aya hii (1:18-25), kuna maneno mawili (pamoja na maneno ya kinyume chake) yanayorudiwa mara nyingi na Mtume Paulo. Mtume anataja sana hekima (na upuuzi/upumbavu) na nguvu (udhaifu). Hii inaonyesha jinsi ambavyo Mtume Paulo alikuwa akipambana na hekima ya dunia hii kwa kumtambulisha Yesu (ujumbe wa msalaba) kama Hekima na Nguvu ya Mungu. Katika Biblia ya Kiswahili (SUV) neno “hekima” linatajwa mara 6 (upumbavu/upuuzi mara 4), na “nguvu” linatajwa mara 3 (udhaifu mara 1). Maneo haya yanaendelea kujirudia kwenye aya zinazofuata mpaka 4:21.
[3] Mara nyingi neno “kukwaza” limetumika kumaanisha kumhuzunisha mtu au kumtendea kitu asichokipenda. Lakini maana ya neno hili katika muktadha wa Biblia ni kumsababisha mtu kufanya dhambi. Hivyo, Paulo anakataza waamini wenye ujuzi kufanyika mfano mbaya utakaowasababisha waamini wadhaifu kufanya dhambi ya kuabudu miungu.
[4] Katika kipengele hiki cha maandiko, mtume Paulo anafananisha kanisa na taifa la Israeli. Kama ambavyo waamini waliokolewa kutoka kwenye utumwa wa dhambi, ndivyo Israeli waliokolewa kutoka kwenye utumwa wa Misri kupitia kuvuka bahari. Kama ambavyo waamini wanabatizwa, ndivyo Waisraeli walibatizwa. Kama ambavyo waamini wanakula na kunywa mwili na damu ya Yesu kupitia meza ya Bwana, ndivyo Waisraeli walikula na kunywa kutoka kwa Kristo.
[5] Wakati watu wa Israeli walipotoa dhabihu, mara nyingi dhabihu haikuteketezwa yote na sehemu iliyobaki ilikuwa inahifadhiwa na kuliwa na makuhani (Walawi 7:6) au na mtu aliyetoa sadaka hiyo (Walawi 7:15). Wale waliokula chakula hicho walishiriki ushirika na Mungu na walikuwa na ushirika na madhabahu. Hivyo, kula chakula kwenye hekalu sio jambo la tumbo ni jambo la ushirika.
Unakuja hivi karibuni…

