1 Wathesalonike- Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA KWANZA WA MTUME PAULO KWA WATHESALONIKE.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.

UTANGULIZI.

Waraka wa Mtume Paulo kwa kanisa la Wathesalonike ni waraka wa kipekee sana. Kwanza, huu ni waraka ambao ni miongoni mwa vitabu vya Agano Jipya ambavyo viliandikwa mwanzoni kabisa katika maisha ya kanisa. Pili, pamoja na kwamba waraka huu unaitwa waraka wa Mtume Paulo, lakini waraka huu uliandikwa na watu watatu: Paulo, Silwano (Sila), na Timotheo. Hii sio kwa sababu wametajwa katika anuani ya barua tu, bali kwa sababu waraka huu unatumia lugha ya wingi katika maeneo yote isipokuwa maeneo matatu (2:18; 3:5; 5:27) ambapo sauti ya Mtume Paulo inajitokeza kwa umoja.

KUZALIWA KWA KANISA LA THESALONIKE.

Kanisa la Thesalonike lilizaliwa wakati wa safari ya pili ya kitume ya Mtume Paulo na timu ya Injili pale walipofika katika mji wa Thesalonike na kuhubiri Injili kwa zaidi ya wiki tatu. Habari za kuzaliwa kwa kanisa la Thesalonike zinapatikana katika kitabu cha Matendo ya Mitume, sura ya 17 kuanzia mstari wa 1 mpaka 10. Lakini ili kuelewa vizuri habari hii, ni muhimu kuanzia katika sura ya 15 mstari wa 36 mpaka sura ya 18 mstari wa 22.

Baada ya kanisa kufanya kikao kule Yerusalemu na kukubaliana baada ya majadiliano (15:7) kwamba mataifa hawatakiwi kushika sheria ya Musa wala kutahiriwa ili kupata wokovu kama waamini wa Kiyahudi walivyofundisha (15:1, 5), wakaandika barua kueleza makubaliano yao. Barua hii ilikwenda kwenye makanisa yaliyoko Antiokia, Shamu na Kilikia (15:23). Katika barua hiyo, wakawatahadharisha mataifa kujiepusha na ibada za sanamu na uasherati (15:28-29). Wakawatuma mashahidi wawili ili kupeleka na kusoma barua hii pamoja na Paulo na Barnaba. Mashahidi hawa wawili walikuwa ni Yuda na Sila, watu wakuu (viongozi) miongoni mwa kanisa la Yerusalemu (15:22). Kundi hili lilifika Antiokia, mji ambao ulikuwa kama makao makuu ya kanisa kwa mataifa (15:30). Yuda na Sila walifanya kazi waliyopewa na kanisa la Yerusalemu (15:31-32) na kazi ilipoisha, Yuda alirudi Yerusalemu, Sila akabaki Antiokia (15:33-34).

Paulo na Barnaba walibaki Antiokia kwa muda wakihubiri na kufundisha Neno la Mungu pamoja na watu wengine (15:35). Baada ya muda, ndipo safari ya pili ya kimisheni ikaanza. Safari ilianza kwa Paulo kumtaka Barnaba warudi kwenye makanisa waliyoyafungua katika safari yao ya kwanza ya kimisheni ili kuona wanaendeleaje (15:36). Lakini kukatokea mgawanyiko kati ya Barnaba na Paulo, kwa sababu Barnaba alitaka Marko awepo kwenye msafara wao lakini Paulo hakutaka kwenda na Marko kwa kuwa hapo mwanzo Marko aliwaacha Pamfilia (13:13) na kurudi Yerusalemu wakati wa safari ya kwanza ya kimisheni (15:38). Barnaba akamchukua Marko (kwa jina jingine Yohana, mwandishi wa Injili ya Marko) akaenda naye Kipro na Paulo akamchukua Sila wakaenda Kilikia (15:39-41).

Katika safari yao, Paulo na Sila wakaungana na Timotheo huko Listra na wakazunguka kwenye makanisa wakiwaimarisha na kuwasomea waamini barua ya mkutano wa Yerusalemu (16:1-5). Walipopita Frigia na Galatia walitaka kuhubiri Injili katika Asia, lakini Roho aliwazuia hivyo wakapita Asia bila kuhubiri na wakafika mpaka Troa (15:6-8). Mpaka hapa, timu ilikuwa na watu watatu ambao mwandishi Luka aliwataja ambao ni Paulo, Sila na Timotheo (inawezekana walikuwa zaidi ya hao lakini mwandishi hajawataja wengine). Katika mji wa Troa, timu ikaongezeka mtu aitwaye Luka. Hii ni kwa sababu kabla ya Matendo 16:10 mwandishi anasema, “Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa” (Matendo 16:7-8). Lakini baada ya Paulo kupata maono ya mtu anayewaita Makedonia, mwandishi Luka anasema, “Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema. Basi tukang’oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia” (Matendo 16:10-12). Hii inaonyesha Luka aliungana na timu hii ya kimisheni katika mji wa Troa.

Timu ikasafiri kutoka Troa kuelekea Makedonia kwa kupita Samothrake na kufika Neapoli (bandari iliyokuwa karibu na mji wa Filipi) ndani ya Makedonia (16:11). Makedonia ilikuwa ni jimbo ambalo ndani yake kulikuwa na miji ya Filipi, Beroya, Thesalonike na mingine. Hivyo walipofika jimbo la Makedonia, walianza kazi yao mji wa Filipi (16:12). Luka ameutaja mji wa Filipi kwa sifa akiutaja kwamba ni “mji ulio mkuu katika jimbo lile” lakini ukuu huu si ukuu kwa maana ya kiutawala. Mji mkuu wa kiutawala katika jimbo la Makedonia ulikuwa ni Thesalonike.

Baada ya kufika Filipi, Injili ikahubiriwa hapo na kanisa likazaliwa. Kwa kuwa katika mji huu hakukuwa na sinagogi la Wayahudi, walienda kando ya mto, ambako walijua kungekuwa na eneo la kusali Wayahudi (16:13). Baada ya mateso, kufungwa gerezani na kufunguliwa, Paulo na Sila wakasafiri mpaka Thesalonike (Timotheo alikuwepo kwenye msafara japo hakuwepo gerezani). Luka hakufika Thesalonike kama anavyotuambia, “Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi” (Matendo 17:1).

Hapa Thesalonike, walihubiri Injili (kuhojiana nao kutoka kwenye maandiko) kwenye sinagogi la Wayahudi kwa zaidi ya Jumamosi tatu na baadhi ya Wayahudi, wamataifa waliomcha Mungu kwa dini ya Kiyahudi wengi na wanawake wenye cheo wakaamini (17:1-4). Lakini Wayahudi wengine wakaona wivu kwa kuwa watu wa dini yao wanahama, wakasababisha ghasia na kuwashitaki waamini walioamini na yule aliyekaa na timu ya Injili yaani Jasoni (inawezekana pia waamini walikuwa wanakutana kwa Jasoni kwa ajili ya ibada). Wayahudi hawa waliwashitaki waamini wa Thesalonike (Jason akiwepo) kwa kuwakaribisha watu wanaotenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema kwamba yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu (17:6-7). Hivyo hii ilikuwa ni kesi ya uhaïni (kuasi serikali ya Rumi), maana huwezi kutangaza mfalme mwingine sehemu yenye mfalme. Pamoja na Thesalonike kuwa mji huru, bado ulikuwa unatunza heshima ya Kaisari. Hii ndiyo maana wakubwa wa mji walifadhaishwa (17:8). Baada ya kushitakiwa, ikatolewa dhamana kwa Jasoni na waamini. Inadhaniwa kwamba dhamana ilihusisha Jason kukubali kutokuwapokea tena Paulo na Sila, yaani Paulo na Sila walizuiliwa kurudi tena Thesalonike kisheria, lakini zuio hili halikumhusu Timotheo, ndiyo maana Timotheo aliweza kurudi tena Thesalonike (1 Wathesalonike 2:17-3:1-5).

Kwa sababu ya tukio hilo, timu ya umisheni ikalazimika kuondoka usiku na kwenda mpaka Beroya (17:10). Wayahudi wa Beroya walikuwa waungwana, walijifunza na wengine wakaamini, lakini Wayahudi wa Thesalonike waliposikia habari hizo wakawafuata timu ya umisheni huko Beroya na kufanya ghasia pia huko, kiasi cha kusababisha Paulo kuondoka Beroya kwenda mpaka Athene (17:11-14). Timotheo na Sila wakabaki Beroya, lakini wale waliomsindikiza Paulo mpaka Athene walipokuwa wanarudi, Paulo akawaagiza kuwaambia Sila na Timotheo kwamba wasikawie wamfuate Athene (17:15). Barua ya Wathesalonike inaonyesha kwamba Paulo na Timotheo (pamoja na Sila) walionana Athene kwa muda mfupi ambapo kutoka Athene Paulo alimtuma Timotheo kwenda Thesalonike (1 Wathesalonike 3:1-5). Na kutoka Athene inadhaniwa Sila akarudi Filipi. Kutoka Athene, Paulo akaenda Korintho ambako akaonana na Timotheo na Sila, Timotheo akitoka Thesalonike na habari njema ya maendeleo ya kanisa (Matendo 18:5). Hivyo, timu hii ya kimisheni ikafanya kazi ya Injili katika mji wa Korintho (2 Wakorintho 1:19). Mji wa Korintho ulikuwa ni mji wa jimbo jingine la Akaya, wakati miji ya Filipi, Beroya na Thesalonike ilikuwa kwenye jimbo moja la Makedonia.

Kuna mambo ya msingi ya kuzingatia hapa kuhusu uanzishwaji wa kanisa katika mji huu wa Thesalonike: Moja, kanisa katika mji huu wa Thesalonike lilizaliwa katikati ya upinzani mkubwa wa Wayahudi. Kwa kuwa Wayahudi hawa wa Thesalonike walifanya ghasia kwa timu ya umisheni na hii inaonyesha kwamba waliwatesa pia waamini waliobaki baada ya timu hii ya umisheni kuondoka (1 Wathesalonike 3:3-4).

Jambo la pili la msingi ni kujua kuwa kanisa lilipata muda mdogo sana wa kulelewa na timu hii ya kimisheni kwa kuwa walikaa muda mfupi sana.

Jambo la tatu ni kwamba viongozi wao waliomtangaza Yesu kama mfalme walitoroshwa usiku kwenda Beroya (Matendo 17:10). Hili linaweza kuonekana kama kuwatelekeza waamini.

Huko Korintho, Paulo alikaa kwa muda wa mwaka mmoja na nusu (18:11), na kutoka huko ndiyo aliandika barua zote mbili kwa Wathesalonike (pamoja na Sila na Timotheo). Kutoka Korintho, Paulo akasafiri mpaka Yerusalemu akipitia Efeso (akiwaacha Priscila na Akila) na hatimaye akarudi Antiokia kule alikoanzia safari pamoja na Sila (18:18-22). Na hapa ndio mwisho wa safari ya pili ya kitume ya Mtume Paulo.

SABABU ZA KUANDIKWA KWA BARUA YA KWANZA KWA WATHESALONIKE.

Matendo ya Mitume 17 inatuonyesha kwamba timu ya kimishenari haikukaa kwa muda mrefu Thessalonike, na hili halikuwa kwa hiari yao. Kwa sababu ya ghasia za Wayahudi, timu hii iliondoka Thessalonike haraka, hivyo kuacha Kanisa likiwa changa. Tunajua timu hii ilitoka Thessalonike na kwenda Beroya, na huko Beroya pia Wayahudi wa Thessalonike wakawafanyia ghasia na kusababisha waende mpaka Athene (Paulo akitangulia). Paulo anasema kwamba, “Basi kwa hiyo, tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliona vema kuachwa Athene peke yetu. Tukamtuma Timotheo ndugu yetu, mtumishi wa Mungu katika Injili ya Kristo, ili kuwafanya ninyi imara na kuwafariji kwa habari ya imani yenu;” 1 Wathesalonike 3:1-2. Hivyo, kutoka Athene, Timotheo alirudi tena Thessalonike kwa ajili ya kuwafanya imara na kuwafariji kanisa baada ya Paulo kujaribu na kuzuiliwa na shetani zaidi ya mara moja (1 Wathesalonike 2:18). Huko Athene, Paulo hakukaa muda mrefu akaenda Korintho, ambako Timotheo alileta habari njema kuhusu maendeleo ya Kanisa la Thessalonike pamoja na kuwa na changamoto za mateso ya Wayahudi. Paulo anasema, “Lakini Timotheo alipotujia hivi sasa kutoka kwenu, alituletea habari njema za imani yenu na upendo wenu, na ya kwamba mnatukumbuka vema siku zote; mkitamani kutuona sisi vile vile kama sisi kuwaona ninyi.” 1 Wathesalonike 3:6. Habari njema hizi ndizo ziliwafanya timu hii ya kimishenari kuandika barua hii inayoelezea shukrani zao kwa Mungu (1 Wathesalonike 1:2, 2:13 na 3:9) kwa ajili ya ukuaji wa Kanisa la Thessalonike katika imani, upendo, na tumaini pamoja na kuwepo kwa mateso kutoka kwa Wayahudi (1 Wathesalonike 1:16 na 2:14). Ukuaji huu wa kanisa la Thessalonike ulikuwa ni sauti ya ushuhuda kwa makanisa mengine katika jimbo la Makedonia na jimbo la Akaya pia (1 Wathesalonike 1:7-8).

Pamoja na ripoti nzuri ya ukuaji wa kanisa, pia ripoti hizi za Timotheo zilionyesha yale yaliyopungua katika Kanisa la Thessalonike. Mambo hayo yalisababisha timu hii ya kimishenari kuendelea kumuomba Mungu awape nafasi ya kwenda ili kuwaimarisha (1 Wathesalonike 3:10). Hivyo, Paulo na timu hii ya kimishenari wanatumia barua hii pia kuwaimarisha Wathesalonike katika maeneo yenye mapungufu na kuwasisitiza katika maeneo ambayo waliwafundisha wakiwa pamoja nao (4:1-5:28).

MPANGILIO.

11:1Anuani
21:2-3:13Shukrani Na Maombi
A                           1:2-1:10Shukrani kwa Mungu kwa jinsi ile Wathesalonike walivyolipokea Neno.
B                           2:1-2:12Maisha ya Waandishi wa Barua/wahubiri injili walipokuwa Thesalonike
C                         2:13-2:16Shukrani kwa Mungu kwa jinsi ile Wathesalonike walivyolipokea Neno.
D                         2:17-3:10Mtazamo wa waandishi wa Barua/wahubiri injili baada ya kuondoka Thesalonike kwa lazima.  
E                         3:11-3:13Maombi
34:1-5:15Kuimarisha Yaliyopungua
A                          4:1-4:1-2Utangulizi
B                             4:3-4:8Kuepuka Uchafu na Uasherati
C                           4:9-4:12Kupendana
D                         4:13-5:11Tumaini Letu  
45:12-22Maagizo ya Mwisho
A                         5:12-5:13Kuwatambua Viongozi
B                         5:14-5:15Wajibu wao kati yao Wanaoamini
C                         5:16-5:18Mapenzi ya Mungu kwao
D                         5:19-5:22Wajibu wao kuhusu Unabii
55:23-5:28Hitimisho La Barua

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.

Waraka huu una muundo kama waraka wa kawaida katika karne ya kwanza, yaani una Utangulizi (1:1-3:13), Ujumbe Mkuu (3:14-5:22), na Salamu za Mwisho (5:23-28). Utangulizi una sehemu tatu: anuani ya mtuma waraka, anuani ya mpokeaji, salamu (1:1), na shukrani na maombi (1:2-3:13).

Mara nyingi barua huwa na shukrani fupi, lakini katika barua hii, shukrani ni ndefu na ndani yake ina maelezo ya matukio kati ya waandishi hawa na Wathesalonike. Waandishi wanaanza kwa kuwajulisha Wathesalonike kwamba huwa wanawaombea, na katika kuwaombea huwa wanamshukuru Mungu kwa sababu ya imani yao, upendo wao, na tumaini lao lilipo katika Kristo Yesu (1:2-3). Imani yao, upendo, na tumaini ni matokeo ya uteule wao ambao ulithibitika baada ya kupokea Injili iliyohubiriwa kwao kwa nguvu, katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi (1:4-5). Pamoja na kupokea Injili hii katika upinzani mkali, Wathesalonike walifanyika wafuasi wa Bwana na wafuasi wa waandishi na hivyo kuwa kielelezo katika majimbo ya Makedonia na Akaya (1:6-8). Watu wa majimbo haya walipeana habari jinsi Injili ilivyowafanya Wathesalonike watoke katika sanamu na kumgeukia Yesu Kristo ambaye sasa wanamngoja arudi mara ya pili (1:9-10).

Kabla ya kuendelea kuelezea shukrani zao kwa Mungu, waandishi wanawakumbusha Wathesalonike jinsi walivyoishi katikati yao, jinsi walivyoishi maisha ya kuwa vielelezo, na jinsi walivyohubiri kwa bidii licha ya mateso. Kuhubiri kwao kulikuwa bila udanganyifu huku wakilenga kumpendeza Mungu pekee (2:1-5). Wanasema hawakutafuta utukufu wa wanadamu bali walikuwa wapole na wenye upendo mkubwa, wakijitoa kwao kwa furaha kama mlezi anavyofanya kwa watoto wake (2:6-8). Walifanya kazi za mikono mchana na usiku ili wasiwalemee Wathesalonike. Walihubiri kwa utakatifu na haki na kuwaonya Wathesalonike waenende kama ilivyo wajibu wao kwa Mungu aliyewaita (2:9-12).

Baada ya kuwakumbusha Wathesalonike jinsi walivyoishi katikati yao, waandishi wanarudi tena katika kuelezea shukrani zao kwa Mungu kwa ajili yao. Wanamshukuru Mungu kwa kuwa Wathesalonike walilipokea neno la Mungu kama kweli kutoka kwa Mungu na si kama maneno ya wanadamu, neno ambalo linafanya kazi ndani yao. Wanawapongeza kwa kuiga mfano wa makanisa ya Mungu yaliyokuwa katika Uyahudi, makanisa haya yalipata mateso kutoka kwa watu wa taifa lao wenyewe kama Wathesalonike wanavyopata mateso sasa (2:13-14). Wanaowatesa waamini wa Uyahudi ndio hao hao waliomtesa Bwana Yesu, manabii wengine, na ndio wanaowapinga waandishi katika kuhubiri Injili kwa mataifa (2:15-16).

Kabla ya kumalizia sehemu hii ya shukrani na maombi, waandishi wanawaeleza Wathesalonike nini kilitokea baada ya wao kulazimika kuwaacha. Baada ya kutengana, wahubiri hawa walitamani sana kuwaona tena Wathesalonike. Walijaribu kurudi tena Thesalonike lakini hawakuweza, na Paulo anajitaja kwamba yeye peke yake alijaribu lakini ilishindikana (2:17-18). Waandishi walitamani kuwaona tena ili wawaimarishe katika imani, kwa sababu wao ndio furaha yao na utukufu wao wakati wa kurudi Bwana Yesu Kristo (2:19-20).

Paulo na Sila waliposhindwa kurudi tena wakaamua kumtuma Timotheo ili awafanye imara Wathesalonike katika imani na kuwatia moyo kutokana na mateso wanayopitia. Na Timotheo aliporudi sasa alileta habari njema ya maendeleo ya Wathesalonike na ya kwamba Wathesalonike pia walitamani kuonana na timu nzima ya wahubiri hawa (3:1-6). Habari njema za Timotheo ziliwapa faraja na wakapatia ahueni ya mawazo makali waliyokuwa wanayapitia, hii ni kwa sababu walipata uhakika kwamba Wathesalonike wanaendelea na imani (3:7-10).

Waandishi wanafunga sehemu hii ya shukrani na maombi kwa kuomba mambo matatu mbele za Mungu. Moja, wanaomba Mungu awape nafasi ya wao wote kwenda tena Thesalonike. Pili, wanawaombea Wathesalonike wazidi kuwa na upendo katikati yao na kwa watu wengine. Na mwisho, wanawaombea Wathesalonike kwamba Mungu awafanye kuwa imara, wawe watakatifu bila lawama hata siku ya kurudi Bwana Yesu Kristo (3:11-13).

Sehemu ya ujumbe mkuu kwa Wathesalonike inakuja baada ya kuwa na utangulizi mrefu. Katika sehemu hii, waandishi wanawaonya Wathesalonike waishi kama wanavyotakiwa kuenenda katika Bwana kama walivyowaagiza tangu mwanzo (4:1-2). Katika mwenendo wanazungumzia mambo matatu: uasherati, upendo, na uwajibikaji katika kazi. Kama waamini wanatakiwa kuepukana na uasherati na uchafu (4:3-8). Wanatakiwa kuongeza upendo kwa kuwa hilo tayari wanaliishi (4:9-10). Pia wanatakiwa kufanya kazi za mikono ili wasiwe na uhitaji na ili wawe mfano mzuri kwa wasioamini (4:11-12).

Baada ya kuzungumzia mwenendo, waandishi wanahama na kuanza kuzungumzia tumaini la waamini. Wanawaambia Wathesalonike wasihuzunike kwa sababu ya waamini waliokufa, hii ni kwa sababu watapata ufufuo wakati wa kurudi Yesu mara ya pili. Ufufuo utakuwa kwa waliokufa lakini kwa watakaokuwa hai ni kubadilishwa, ili wote kwa pamoja katika miili ya utukufu waende kumlaki Bwana mawinguni na hatimaye kuishi naye milele. Jambo hili ni tumaini kwao na linatakiwa liwe jambo la kufarijiana (4:13-18).

Kwa kuwa tumaini la waamini liko kwenye ujio wa Yesu mara ya pili, waandishi wakaona vema kuwaandikia Wathesalonike kuhusu majira na wakati wa tukio hili. Wanaanza kwa kuwaambia Wathesalonike kwamba, wao hawana haja ya kuwaandikia kuhusu jambo hili kwa sababu tayari wanajua kwamba ujio wa Bwana utakuwa katika wakati usiotarajiwa kama vile wakati wa mwizi kuja (5:1-3). Hata hivyo, kwenye ujio wa Bwana kuna makundi mawili; kundi la kwanza ni la watu wa gizani na ujio huu utawajia ghafla na utakuwa wa mateso kwao, kama mama mjamzito. Kundi la pili ni la Wathesalonike, wao ujio wa Bwana sio jambo lisilotarajiwa kwa kuwa wao ni wana wa nuru, na hivyo wanatakiwa kukesha (5:4-7). Kuwa wa nuru ni kuishi katika kiasi, kujivika kifuani imani na upendo na kuwa na chepeo iitwayo tumaini la wokovu. Hii ni kwa sababu Bwana hakuwaweka Wathesalonike kwa ajili ya ghadhabu kama kundi la kwanza bali waliwekwa kwa ajili ya wokovu kupitia Yesu Kristo aliyekufa kwa ajili yao. Basi kwa tumaini hili wanaagizwa kufarijiana kila mmoja na mwenzake kama wanavyofanya tayari (5:8-11).

Sehemu ya ujumbe mkuu inafikia tamati kwa waandishi kutoa maagizo ya mwisho kwa Wathesalonike. Moja, wanawaagiza kanisa kuwatambua viongozi wao (5:12-13). Pili, wanawaagiza namna gani wanatakiwa kuhusiana na kusaidiana kama waamini (5:14-15). Tatu, wanawataka waishi maisha yenye furaha, shukrani, na maombi maana hayo ndio mapenzi ya Mungu kwa watu wake (5:16-18). Mwisho, wanawataka Wathesalonike wasiukatae unabii bali waujaribu kila unabii na hivyo kuambatana na unabii mwema/wa kweli (5:19-21).

Waraka huu unafika tamati kwa salamu za mwisho. Salamu hizi za mwisho zina maombi ya waandishi kwa Mungu kwa ajili ya Wathesalonike (5:23-24), hitaji la waandishi kuombewa na Wathesalonike (5:25), salamu kwa ndugu wote (5:26), agizo kuhusu ndugu wote kusomewa waraka huu (5:27), na salamu za kufunga waraka (5:28).




FOOTNOTES

UFAFANUZI WARAKA WA KWANZA WA WATHESALONIKE

UTANGULIZI

1 WATHESALONIKE 1:1

1 WATHESALONIKE 1:2-10

1 WATHESALONIKE 2:1-12

1 WATHESALONIKE 2:13-16

1 WATHESALONIKE 2:17-20

1 WATHESALONIKE 3:1-6

1 WATHESALONIKE 3:7-10

1 WATHESALONIKE 3:11-13

MAELEZO YA ZIADA: MATESO YAKOJE KWETU SISI LEO?

1 WATHESALONIKE 4:1-12

1 WATHESALONIKE 4:13-18

1 WATHESALONIKE 5:1-11

MAELEZO YA ZIADA: WAAMINI WAKIFA WANAENDA WAPI?

1 WATHESALONIKE 5:12-15

1 WATHESALONIKE 5:16-22

1 WATHESALONIKE 5:23-28

MAELEZO YA ZIADA: KUSALIMIANA KWA BUSU TAKATIFU

VITABU REJEA