MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA KWANZA WA MTUME YOHANA.
MAELEKEZO.
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.
UTANGULIZI.
Waraka wa kwanza wa Mtume Yohana ni kitabu kinachokubaliwa na waamini kwamba kiliandikwa na mtume Yohana kwenda kwenye makanisa yaliyokuwa eneo la Efeso, japo mwandishi hajataja jina lake katika maandishi ya kitabu hiki. Pamoja na kwamba ni kweli Yohana hajataja jina lake katika maandishi ya kitabu hiki, kuna viashiria kwamba waraka huu uliandikwa na yeye. Moja ya kiashiria ni ufanano mkubwa wa ujumbe na matumizi ya lugha na vitabu vingine vinavyoaminiwa kuandikwa na yeye. Vitabu hivi ni Injili ya Yohana, Waraka wa pili wa Yohana na Waraka wa tatu wa Yohana. Mfanano wa vitabu hivi ni ishara tosha kwamba viliandikwa na mwandishi mmoja
MTUME YOHANA.
Yohana alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wa Yesu, mtoto wa Zebedayo, na kaka wa Yakobo mtume (Mathayo 4:21-22). Yakobo huyu ni Yakobo mtume wa Kwanza kabisa kufa na sio Yakobo mwandishi wa waraka wa Yakobo (Matendo 12:1-2). Yohana kabla ya kukutana na Yesu alikuwa mvuvi wa samaki, kazi ambayo ilikuwa ni kazi ya familia.
Yohana anafahamika kama mwanafunzi aliyekuwa karibu sana na Yesu, na anajitaja kama mwanafunzi aliyependwa sana na Bwana Yesu (Yohana 13:23). Ni kweli kwamba Yohana alikuwa karibu sana na Yesu sababu yeye na Petro na Yakobo ndio wanafunzi pekee waliona matukio muhimu ya Bwana Yesu ambayo wanafunzi wengine hawakuyaona. Matukio haya ni kama vile, kubadilika kwa Yesu kule mlimani (Luke 9:28-36) na maombi ya Yesu katika bustani ya Gethsemane (Mathayo 26:36-46).
Baada ya kristo kufufuka Yohana alikuwa huko Jerusalem kama mmoja wa Mitume waliotambulika kama Nguzo za Kanisa (Wagalatia 2:9-10). Kwa mujibu wa mapokeo ya kihistoria kutoka kwa mababa wa Kanisa wa kuanzia karne ya pili, Yohana baada ya kufanya kazi huko Jerusalem pamoja na mitume wengine alisafiri na kwenda Efeso ambako alifanya huduma yake kwa muda wa kutosha (Kati ya mwaka 70-100 B.K).Nyaraka zake tatu ni matokeo ya huduma yake kwa kanisa lililokuwako huko Efeso. Baada ya muda, kama njia ya mateso Yohana alipelekwa katika kisiwa cha Patmo na huko aliandika kitabu cha Ufunuo. Na inaaminika kuwa Yohana ndiye mtume pekee kufa kifo cha kawaida tu bila kuuawa kama mitume wengine.
WAPOKEAJI WA AWALI WA WARAKA.
Katika kuandika kitabu hiki mwandishi hakuandika kwa mtindo wa waraka[1] ndio maana hata hakuandika wapokeaji walikuwa ni watu wa eneo gani. Kwa msaada wa kihistoria Kutoka kwenye vitabu vya waandishi ya karne ya pili na ya tatu tunajifunza kwamba Mtume Yohana, mwana wa Zebedayo, mwanafunzi Yesu aliyempenda aliishi na kufanya huduma yake kule Efeso, Asia kati ya mwaka 70-100 B.K. Hivyo inaaminika aliandika waraka huu kwa waamini wa maeneo ya Efeso ambao anawaita “watoto wake”. Kutokana na Ujumbe wa kitabu hiki ni dhahiri kuwa kitabu hiki kiliandikwa kwenda kwa waamini ambao tayari wanaijua kweli (2:7, 21), lakini katikati yao kulitokea na mgawanyiko kati yao na waalimu wa uongo. Mgawanyiko huu ukasababisha waalimu hao wa uongo kujitenga. Pamoja na kujitenga waliendelea kueneza uongo wao na ndio maana mwandishi anawaandikia waamini hawa wanaoijua kweli kujiepusha na waalimu hao wa uongo na mafundisho yao ya uongo.
KUSUDI LA WARAKA.
Katika kutafuta kusudi la kuandikwa kwa kitabu chochote basi tunatakiwa kuangalia kauli ya mwandishi inayoonyesha kusudi la kuandika ujumbe wake. Katika kitabu hiki mwandishi ana kauli zaidi ya moja zinazoashiria kusudi la kuandika ujumbe huu. Kauli hizi ni kama zifutazo
“Na haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe.” 1 Yohana 1:4
“Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,” 1 Yohana 2:1
“Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza” 1 Yohana 2:26
“Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.” 1 Yohana 5:13
Mwandishi anaonyesha kwamba alikuwa na kusudi zaidi ya moja la kuandika kitabu hiki, kwa sababu mara nyingi baada ya maelezo fulani anataja kusudi la sehemu hiyo. Baada ya kuandika mstari wa kwanza hadi wa tatu sura ya kwanza mwandishi anasema “twayaandika ili kusudi furaha yetu itimizwe” akionyesha furaha yake itatimizwa kama kutakuwa na ushirika kati yake na wapokeaji wa ujumbe huu. Baada ya kukosoa kiri zisizo sahihi katika mstari wa tano hadi wa kumi sura ya kwanza mwandishi anasema “nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi” akionyesha kwamba lengo la kuwaandikia hayo (5-10) ni kuwataka wasitende dhambi. Baada ya kueleza habari za wapinga Kristo katika mstari wa kumi na nane hadi wa ishirini na tano sura ya pili, mwandishi anasema “Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza”. Na baada ya kuelezea kuhusu ushindi wa waamini dhidi ya dunia yaani hiyo imani yao yenye ushuhuda katika mstari wa kwanza hadi kumi na mbili sura ya tano, mwandishi anasema “Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu”.
Hivyo Mwandishi alikuwa na kusudi zaidi ya moja katika kuandika ujumbe huu kwa wapokeaji. Makusudi haya yanaweza kuwekwa kwenye makundi mawili, moja ni kusudi la kichungaji na la pili ni kusudi la utetezi wa imani ya kweli.
KUSUDI LA KICHUNGAJI.
Mwandishi anawaandikia watu ambao tayari wamekwisha amini (2:12-14; 5:13) na pia wanaijua kweli (2:7, 21). Watu hawa pia anawajua na ni watu ambao ana wajibu kwao, ndio maana anawaita “watoto wangu wadogo” (2:1) au “watoto wadogo” (2:28; 3:7; 3:18; 4:4; 5:21). Anawaandikia kuwataka waendelee kwenye kuamini kweli waliyofundishwa tangu mwanzo (2:7, 24) ambayo ina ushahidi wa kweli kutoka kwa mitume waliomsikia, kumuona na kumshika Yesu (1:1-3). Kweli hiyo inawataka kuenenda katika nuru kama Mungu alivyo katika nuru (1:5-7). Kweli hiyo inawataka kupendana (3:11, 14) katika kweli na Tendo (3:18) kama Mungu alivyowapenda wao (4:10-11, 19). Na zaidi kweli hiyo inawataka kuamini kwamba Yesu ni Kristo (2:22-23), mwana wa Mungu (1:3, 7; 3:8; 4:9, 15), kipatanisho kwa dhambi zetu (4:10), aliyekuja katika mwili (4:2) na katika maji na damu (5:6). Mwandishi kama mchungaji anasema furaha yake itatimizwa kuona wapokeaji wanaishi kwenye kweli hii (1:4). Lakini pia kama mchungaji mwandishi anataka wapokeaji wa ujumbe wake wasitende dhambi (3:8-9; 5:18), na ikitokea mtu ametenda dhambi basi ajue anaye mwombezi kwa Baba ambaye ni Yesu kristo (2:1-2, 5:16-17). Na zaidi kama Mchungaji anataka kuwahakikishia kwamba wale wanaoliamini jina la Mwana wa Mungu wanao Uzima wa milele (5:13) ambao ni Yesu mwenyewe (1:2; 5:11, 20).
KUSUDI LA UTETEZI WA IMANI YA KWELI.
Sababu kubwa nyingine ya mwandishi kuandika kitabu hiki ni kupinga mafundisho potofu na maisha/mwenendo ambao uko kinyume na kweli. Mwenendo huu anaoupinga mwandishi ulikuwa dhahiri kwa watu anaowaita “wapinga Kristo” (2:18; 4:3), “manabii wa Uongo” (4:1), “watoto wa Ibilisi” (3:10) na waongo na wadanganyifu (2:4, 22; 3:7). Watu hawa walikuwa katika kundi la waamini na wakati mwandishi anaandika ujumbe huu walikuwa wamejitoa (2:19). Kujitoa kwao mwandishi anasema kumetokea ili wafunuliwe kwamba kweli hawakuwa sehemu ya waamini. Lakini watu hawa hawakuishia kujitoa tu bali walifanya jitahada kuwapotosha wengine (2:26). Kwa kuwa kitabu hiki kinakubaliwa na wasomi wengi wa Biblia kwamba kilikuwa kimekusudiwa kwa ajili ya makanisa yaliyoko Efeso na maeneo ya Karibu,basi maneno ya unabii ya mtume Paulo yalitimia kama alivyosema kwa viongozi wa Efeso (Matendo 20:29-30) na kama alivyomwambia Timotheo alipokuwa huko Efeso (2 Timotheo 3:1-7, 4:3-4)[2].
Watu hawa kwa kumsoma Mwandishi anavyowakosoa na kurekebisha fundisho lao ni dhahiri walikuwa wanafundisha yafuatayo,
a. Walikuwa wanakana kwamba “Yesu ni Kristo” (2:22) na mwandishi anasisitiza kwamba aliyezaliwa na Mungu anaamini kwamba Yesu ni Kristo (5:1).
b. Walikuwa wanakana kwamba Yesu kristo hakuja katika Mwili (4:2, Tazama pia 2 Yohana 7) na mwandishi anasisitiza kwamba Yesu kristo walimuona, walimsikia, walimtazama kwa macho na walimshika kwa mikono (1:1-3).
c. Walikuwa wanakana kwamba Yesu Kristo Mwana wa Mungu hakufa bali mwandishi anasisitiza kwamba alikufa (5:5-6).
Sasa unaweza kushangaa inakuaje watu hawa walikuwa katikati ya waamini pamoja na kwamba wanapinga kila kitu muhimu kumhusu Kristo Yesu ? Mshangao huu unaweza kutokana na sababu mbili, Moja hatujui mpangilio mzuri wa mafundisho yao na tunapata mafundisho yao kutoka katika upande wa mkosoaji tu. Jambo la pili, ni kwa sababu kwetu leo Yesu Kristo limekuwa kama Jina moja yaani Kristo limekuwa kama jina la Baba la Yesu (Kama ilivyo tamaduni yetu ya majina). Lakini tukipata mwanga kidogo kutoka katika historia tunaweza kupata angalau mpangilio wa mafundisho yao. Lakini pia tukielewa utofauti wa Jina Yesu na Cheo kristo tunaweza kuelewa fundisho lao.
Utofauti wa Jina Yesu na Cheo Kristo.
Jina Yesu ni Jina la mwokozi wetu la kupewa na wazazi kama walivyoelekezwa na malaika Gabrieli (Luka 1:31). Yesu alichukua cheo kinachoitwa Kristo (neno lililotoholewa kutoka kwenye kiyunani) au Masihi (Neno lililotoholewa kutoka kwenye kiebrania). Cheo hichi kinamaanisha yeye ni mpakwa mafuta wa Mungu aliyetabiriwa katika vitabu vya Agano la kwanza/kale kwamba atakuja kupitia ukoo wa Daudi ili kulikomboa taifa la Israeli. Hivyo Yesu ni Kristo kwa maana ya kuwa yeye ni mpakwa mafuta wa Mungu aliyekuja duniani kupitia familia ya mfalme Daudi kuleta ukombozi. Kwa utofauti huu ndio maana wayahudi mpaka leo wanakataa kwamba Yesu hakuwa kristo kwa maana wanaamini hakukidhi vigezo vya kuwa masihi/Kristo. Bado wao wanasubiri ujio wa Masihi/Kristo mpaka leo.
Mpangilio wa mfundisho ya Waalimu hawa wa Uongo.
Maandishi ya Mababa wa kanisa ya kuanzia karne ya pili ambao walitumia Kitabu hiki cha Yohana kupingana na upotofu huo yanatupa mwanga zaidi katika kutuonyesha kwamba watu hawa walikuwa na mafundisho ya namna gani.
Mababa wa kanisa wanatuonyesha kwamba mafundisho haya yalikuwa kwenye makundi kadhaa, Moja ya makundi ya waalimu hawa wa uongo lilikuwa ni kundi la Mwalimu aliyeitwa Cerinthus. Mwalimu huyu kwa mujibu wa Askofu Ireneo wa mji wa Lyon, alitenganisha kati ya Yesu na Kristo kwa kufundisha kwamba Yesu alikuwa ni mwanadamu wa kawaida tu wa kule Nazareti aliyezaliwa na Josefu na Mariam kwa njia ya kawaida tu, ambaye alikuwa na huruma na Hekima. Kwa upande mwingine Kristo alitoka kwa Mungu na kumshukia Yesu wakati wa ubatizo wake. Hivyo kwa mujibu wa mwalimu huyu, Kristo aliyekuwa ndani ya Yesu akamhubiri Baba kwa watu na akafanya miujiza mingi na mwishoe alimtoka Yesu kabla hajasulubiwa. Hivyo Cerinthus alifundisha kwamba Kristo kutoka Mbinguni hakusulubiwa bali Yesu mwanadamu wa Nazareti ndiye aliyesulubiwa na baadaye kufufuka.[3]
Kundi lingine la pili ni kundi la Udoho “Docetism”, kundi ambalo halikukubaliana na ubinadamu wa Yesu. Kwa kutokukubaliana na ubinadamu wa Yesu kundi hili walifundisha kwamba Yesu hakuwa na umbile halisi la Binadamu japo alionekana kuwa na mwili wa binadamu. Kwa lugha rahisi walifundisha kwamba Yesu alikuwa kama Mzimu. Hivyo kwa kupata mwanga huu wa mpangilio wa mafundisho yao ni rahisi kuelewa mwandishi alichokuwa anakipinga.
Kumbuka makundi haya yanatupa mwanga tu wa kile ambacho mwandishi alikuwa anapingana nacho.
Mbali na mafundisho potofu kuhusu Yesu kristo kama tulivyoeleza, pia waalimu hawa wa uongo waliishi maisha yasiyo na maadili yatokanayo na kweli. Hii ndio maana mwandishi anawakosoa sana akisema:
“Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.” 2:4
.”Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.” 2:9
“Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.” 2:11
“Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona” 4:20
“Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki” 3:7
Na kuna uwezekano mkubwa pia zile kauli za “Tukisema” za mstari wa 6, 8 na 10 sura ya kwanza zilikuwa pia ni nukuu za mwandishi kutoka kwa waalimu hawa wa uongo. Haya yote yanaonyesha waalimu hawa wa uongo waliishi tofauti na ukiri wao wa kumjua Mungu na kuwa na ushirika naye.
Hivyo mwandishi aliandika waraka huu kupinga mafundisho hayo potofu ya waalimu wa Uongo na kupinga mwenendo wao wa giza.
MPANGILIO.
Mpangilio wa kitabu hiki ni vigumu kuugundua kwa sababu Mwandishi haelezei hoja zake kwa mpangilio maalumu mwanzo mpaka mwisho. Mwandishi amechanganya changanya hoja zake mara kadhaa yaani kuna wakati anaanza jambo moja baada ya muda anaingia japo la pili kabla ya kumaliza jambo la pili anarudi tena kwenye jambo la kwanza. Mfano anazungumiza kupendana katika 3:11-24 na baada ya hapo anazungumzia wapinga kristo (4:1-6) alafu anarudi tena kuzungumza kuhusu kupendana (4:7-21).
Pia lugha anayotumia Mwandishi ni lugha ya kurudia rudia maneno yale yale kama wimbo. Maneno haya ni kama vile “kaeni ndani yake” “amri zake” “mwana wake” “kupendana”.
Hivyo mpangilio huu ni pendekezo letu tu kwa ajili ya kukusaidia kufuatilia mawazo yake.
Sehemu | Maelezo |
1:1-4 | UTANGULIZI |
1:5-2:27 | USHIRIKA NA MUNGU |
a. 1:5-2:2 | Tusijidanganye. |
b. 2:3-2:11 | Tushike amri zake. |
c. 2:12-2:14 | Kwenu watoto wadogo, wakina Baba na Vijana. |
d. 2:15-2:17 | Msiipende Dunia. |
e. 2:18-2:27 | Wapinga Kristo (Sehemu ya I) |
2:28-3:24 | WANA WA MUNGU |
a. 2:28-3:10 | Uhusiano wa Mwana wa Mungu na Dhambi na kutenda Haki |
b. 3:11-3:24 | Tupendane (Upendo sehemu ya I) |
4:1-5:17 | MSISITIZO |
a. 4:1-4:6 | Kuzitambua Roho (Wapinga Kristo sehemu ya II) |
b. 4:7-4:21 | Tupendane (Upendo Sehemu ya II) |
c. 5:1-5:13 | Kumwamini Mwana wa Mungu |
d. 5:14-5:17 | Ujasiri wetu katika Maombi |
5:18-5:21 | HITIMISHO |
a. 5:18 | Uhusiano wa Mwana wa Mungu na Dhambi |
b. 5:19 | Sisi tu wana wa Mungu |
c.5:20 | Sisi ndani ya Mwana wake |
d. 5:21 | Tujiepushe na Sanamu |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.
Kama tulivyojifunza hapo juu kwamba kitabu hiki hakikuandikwa kwa mtindo wa waraka bali kwa mtindo wa semina/hotuba, Hivyo mwandishi anaanza moja kwa moja na utangulizi wa ujumbe. Katika utangulizi mwandishi anasema kile anachokihubiri (Neno la Uzima) ana ushahidi nacho kwa njia ya kuona, kusikia, kutazama na kupapasa kwa mikono. Kwa sababu ya ushahidi huo wapokeaji wake wakishikiria anachokisema basi kutakuwa na ushirika kati yao (Mwandishi na waandikiwa). Wapokeaji wa ujumbe wakiwa na ushirika na mwandishi basi wao wote watakuwa na ushirika na Baba na mwanae Yesu. Hii ni kwa sababu yeye mwandishi yuko na ushirika na Baba pamoja na mwanae. Hilo likitokea mwandishi anasema furaha yake itatimizwa/itakamilika (1:1-4).
Baada ya utangulizi huo mwandishi anaenda kwenye sehemu ya ujumbe wake mkuu. Sehemu ya ujumbe mkuu ina sehemu tatu na mwisho kuna hitimisho la semina.
Sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu (1:5-2:27), Mwandishi anaanza kueleza jambo la kwanza walilolisikia kutoka kwa Neno la Uzima na kusahihisha kiri zinazopingana na kile walichosikia kutoka kwa Neno la Uzima (1:5-10). Lengo la kusahihisha kiri hizo tatu hapo juu mwandishi anasema ni kuwataka wasitende dhambi, lakini hata ikitokea wametenda wajue wanaye mwombezi kwa Baba ambaye ni Yesu (2:1-2). Baada ya hapo mwandishi anawaonyesha wapokeaji wa Ujumbe wake ni kwa namna gani watajua kwamba wao wanamjua huyo Neno la Uzima au wanakaa ndani yake huyo Neno la Uzima au kwamba wako nuruni (2:3-11). Mpaka hapa mwandishi anataja sababu za kuandika hiki alichoandika kwa kutaja hizo sababu kwa kuhusianisha na makundi ndani ya kanisa (2:12-14)[4]. Kabla ya kumaliza sehemu yake ya kwanza ya ujumbe mkuu mwandishi anawataka waamini wasiipende dunia na wala vitu vilivyomo katika dunia (2:15-17). Katika kuhitimisha sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu mwandishi anawaonyesha wapokeaji wa ujumbe wake kwamba wapinga kristo tayari wameshafunuliwa. Anawaonyesha wanaamini ni nini wapinga kristo hawa wanafundisha, mafundisho ambayo mwandishi anayapinga. Mwandishi pia anasema uwepo wa hawa wapinga kristo na mafundisho yao mapotofu ndio sababu aliandikia ujumbe huu, ili kusisitiza wabaki kwenye kweli waliyosikia tangu mwanzo (2:18-27). Jambo hili la kuhusu wapinga kristo mwandishi atalirudia tena kulielezea hapo mbele.
Sehemu ya pili ya Ujumbe mkuu (2:28-3:24). Katika sehemu hii mwandishi amezungumzia mambo mawili, moja ni Kuzaliwa na Mungu/kuwa mtoto wa Mungu (2:28-3:10) na la pili ni kupendana sisi kwa sisi (3:11-24). Katika jambo la kwanza mwandishi anaanza na kuonyesha kwamba waliozaliwa na Mungu wanatenda haki (2:28-29). Anawajulisha pia kwamba wao wamekuwa watoto wa Mungu kwa sababu ya Upendo wa Mungu (3:1-3). Baada ya hapo anawaonyesha sifa za watoto wa Mungu (3:4-6) na utofauti wa watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi (3:7-9) na hivyo kuwawezesha wapokeaji wa ujumbe kuwatofautisha watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi(3:10).
Jambo la pili mwandishi anazungumzia kupendana, jambo ambalo pia alilisikia kutoka kwa Neno la Uzima. Mwandishi anafundisha kupendana akikinzanisha na chuki. Anafanya hivyo kwa kuonyesha mifano ya Upendo na Chuki. Yesu anakuwa mfano wa Upendo na Kaini anakuwa mfano wa Chuki (3:11-18). Mwandishi anaonyesha kwamba kupendana kunatupa ujasiri mbele za Mungu (3:19-22) na anamalizia kwa kuwaonyesha wapokeaji wake kwamba kupendana ni amri aliyotupa kama alivyotupa amri ya kuliamini jina lake (3:23-24). Jambo hili la Upendo mwandishi atalirudia tena hapo mbele.
Sehemu ya tatu ya Ujumbe mkuu (4:1-5:17). Katika Sehemu hii Mwandishi anarudi kuelezea mambo ambayo tayari ameshayaeleza kwenye sehemu za nyuma lakini kwa namna/lugha nyingine. Anaanza na kueleza namna ya kuzijaribu roho ili kujua kama roho husika ni Roho wa kweli au ni roho ya upotevu. Roho ya upotevu ni roho ya wapinga kristo ambao alikwisha kuwaelezea hapo juu kwamba wameshakuwapo (4:1-6). Baada ya hapo anarudi kueleza kwa habari ya upendo/kupendana, anaeleza kwamba Mungu ni Upendo na alitupenda kwanza, hivyo imetupasa sisi tupendana, na mtu asiyempenda jirani yake huyo hakumjua Mungu (4:7-21). Baada ya hayo, mwandishi pia anarudia msisitizo wa ujumbe wake kwamba Yesu ni Kristo na kila aaminiye hilo ni mwana wa Mungu. Mwandishi anaeleza hilo kwa kueleza uhakika wa uzima wa milele uliopo kwa wote wanaomwamini mwana wa Mungu, wote wanaoamini kwamba Yesu ndiye Kristo na kuamini kwamba yeye ni mwana wa Mungu. Mambo haya yote yanayomhusu Yesu mwandishi anasema Mungu ameyashuhudia kupitia Roho wake, hivyo yeye asiyeamini ushuhuda wa Mungu kumhusu mwanaye Yesu kristo anamfanya Mungu kuwa mwongo (5:1-13). Mwisho katika sehemu hii mwandishi anaonyesha ujasiri tulio nayo katika maombi (5:14-17).
Kama tulivyojifunza tangu mwanzo kwamba kitabu hiki hakikuandikwa kwa kuzingatia muundo wa kawaida wa waraka hivyo mwandishi haitimishi kwa salamu za mwisho bali anahitimisha kwa kauli mbalimbali ambazo tayari amekwisha kuzieleza katika maeneo mbalimbali toka mwanzo na kufunga kabisa na agizo la kujilinda na sanamu (5:18-21).
FOOTNOTES
[1] Nyaraka huwa zina mpangilio ufuatao, Utangulizi, Ujumbe mkuu na Salamu za Mwisho. Utangulizi huwa unakuwa na Majina/jina la waandishi/mwandishi, Utambulisho wa wapokeaji na Salamu. Mfano mzuri wa Mpangilio huu ni waraka wa Mitume na wazee kwa makanisa ya wamataifa iliyoandikwa baada ya Mkutano wa Jerusalem (Matendo 15:23-29). Vitabu vyote vya Agano jipya vinavyoitwa Nyaraka vina sifa ya mpangilio huo isipokuwa kitabu cha Yohana wa Kwanza na Kitabu cha Waebrania.
[2] Mapendekezo haya ya uhusiano wa unabii wa mtume Paulo na hali ya kanisa mwandishi analoliandikia si mapendekezo ya uhakika, bali yanaweza kusaidia tu kuelewa kwamba kanisa ambalo mwandishi analiandikia lilikuwa katika mgawanyiko wa ndani sawa sawa na utabiri wa mtume Paulo. Mapendekezo haya yamefanywa na mwandishi John R. W Stott katika kitabu kinachoitwa “Barua za Yohana: Utangulizi na Ufafanuzi cha mwaka 1988”
(Stott, J (1988) The letters of John: An Introduction and Commentary. IVP)
[3] Kama unaweza kusoma kiingereza basi maandishi haya ya Baba Askofu Ireneo yaliyoandikwa kwa kiyunani yametafsiriwa na yanapatikana kwa ajili ya kusomwa bila malipo kabisa katika tovuti au aplikesheni ya Biblehub au tovuti ya New advent. Habari hizo za Cerinthus zinapatikana kwenye Kitabu chake kiitwacho “Against Heresies I.26.1. Askofu Ireneo anaripoti kwamba Cerinthus aliishi wakati wa Mtume Yohana na waliwahi kukutana (Against Heresies III.3.4).
[4] Mwandishi anaeleza sababu ya kuandika kwa kutaja makundi matatu ambayo ni watoto, akina Baba na Vijana. Ni vigumu kujua kwa uhakika mwandishi alitumia majina ya makundi haya kwa kuzingatia umri au hatua za ukuaji wako kiroho au alikuwa amekusudia watu wote
UFAFANUZI WARAKA WA KWANZA WA YOHANA KWA WATU WOTE.
UTANGULIZI.
Ukiwa unasoma Biblia baada ya kitabu cha waraka wa Pili wa Petro unakutana na kitabu kinachoitwa Waraka wa Kwanza wa Yohana kwa watu wote. Ukisoma kitabu hiki utagundua kwamba mwandishi hajataja Jina lake, hajataja mahali alipouelekeza ujumbe wake, hajataja utambulisho maalumu wa watu aliowaandikia na hakuna dalili inayoonyesha kwamba kitabu hiki kiliandikwa kwanza kati ya vitabu hivi vitatu vinavyofuatana (1 Yohana, 2 Yohana na 3 Yohana). Kubwa Zaidi kitabu hiki kinaitwa waraka lakini hakina mpangilio za waraka. Nyaraka huwa zina mpangilio ufuatao, Utangulizi, Ujumbe mkuu na Salamu za Mwisho. Utangulizi huwa unakuwa na Majina/jina la waandishi/mwandishi, Utambulisho wa wapokeaji na Salamu. Mfano mzuri wa Mpangilio huu ni waraka wa Mitume na wazee kwa makanisa ya wamataifa iliyoandikwa baada ya Mkutano wa Jerusalem (Matendo 15:23-29). Vitabu vyote vya Agano jipya vinavyoitwa Nyaraka vina sifa ya mpangilio huo isipokuwa kitabu cha Yohana wa Kwanza na Kitabu cha Waebrania. Sasa kichwa cha habari cha kitabu hiki ni matokeo ya mapokeo kutoka kwa mababa wa Kanisa na juhudi za wasomi wa Biblia katika kujibu maswali ya nani aliandika kitabu hiki, aliwaandikia watu wa aina gani na walioshi wapi na maswali mengi yafanayo na hayo. Tunamshukuru Mungu kwa ajili ya watu wanaofanya kazi hiyo usiku na Mchana kwa ajili yetu. Tunaposoma mara nyingi tunaweza kudhani Yohana aliandika kichwa hicho cha Habari au yeye ndiye aliyeweka sura au mistari, lakini ukweli ni kwamba haya ni matokeo ya kazi ya watu wengine mbali ya Yohana.
Sasa kwetu tutajifunza mambo yafuatayo ili kuelewa vizuri ujumbe wa Kitabu hiki na pia kuelewa kwa sehemu kuhusu taarifa mbalimbali za nyuma ya kitabu hiki. Tutajifunza kuhusu;
a. Mwandishi wa Kitabu.
b. Aina ya kitabu.
c. Sababu za kuandikwa kitabu hiki.
d. Wapokeaji wa Awali wa kitabu hiki.
e. Mpangilio wa Kitabu hiki.
a. MWANDISHI WA KITABU.
Kama tulivyoona hapo Mwanzo kwamba kichwa cha Habari kinachoonyesha kwamba Yohana ndiye mwandishi wa kitabu hiki hakitokani na Mwandishi kutaja jina lake katika Kitabu hiki wala katika Vitabu vingine vilivyopewa jina lake. Kwa kifupi Yohana hajawahi kujitaja kama yeye ndiye Mwandishi wa vitabu vinavyobeba Jina lake isipokuwa kitabu cha Ufunuo[1]. Katika Injili Mwandishi anatajwa kama “mwanafunzi aliyependwa na Yesu” (Yohana 21:20-25), katika 1 Yohana haonyeshi utambulisho wake na katika 2 Yohana na 3 Yohana Mwandishi anajiita “Mzee” (2 Yohana 1:1 na 3 Yohana 1:1).
Sasa inakubaliwa na wasomi wengi wa Biblia na Kanisa kwamba Yohana ndiye aliyeandika kitabu hiki kwa sababu zifuatazo.
i. Mwandishi anajitaja kuwa Yeye na wengine ni watu waliokuwa na uhusiano halisi na Yesu (Kwa maana ya kumsikia, kumuona, kumtazama na kumshika I Yohana 1:1-5). Hivyo mwandishi wa kitabu hiki lazima awe kati ya watu walioshuhudia maisha ya Yesu tangu mwanzo, na wenye sifa hii ni mitume kumi na wawili.
ii. Ufanano wa matumizi ya Lugha katika kitabu hiki na kitabu cha Injili. Ufanano wa Lugha kati ya kitabu hiki na kile cha Injili ni sababu kubwa ya kukubali kwamba mwandishi wa vitabu hivi ni mmoja ambaye ni Yohana mtume wa Yesu kristo.Ufananao wa Lugha uko katika namna zifuatazo
a. Kutumia maneno yale yale kwa namna ile ile. Mwandishi wa vitabu hivi viwili anatumia maneno yafutayo kwa namna ile ile.
Yesu anaitwa “Mwana pekee” (1 Yohana 4:9, Yohana 1:14, 18 3:16,18)
Yesu anaitwa “Neno” (1 Yohana 1:1, Yohana 1:1,14)
Uzima wa Milele (1 Yohana 1:2, 2:25, 3:15, 5:11,13,20 Yohana 3:15-16,36)
Roho wa kweli (1 Yohana 4:6, Yohana 14:17, 16:13)
Kutenda kweli (1 Yohana 1:6, Yohana 3:21)
b. Kufanya utofautisho unaonafana katika vitabu hivi viwili.
Utofautisho huu ni kama ufuatao
Upendo na Chuki (1 Yohana 3:11-15; Yohana 3:19-21; 15:18-25)
Uzima na Mauti (1 Yohana 3:14; Yohana 5:24)
Nuru na Giza (1 Yohana 1:5 Yohana 1:5)
Kweli na Uongo (1 Yohana 1:6,8, 2:4,21; Yohana 8:44-45)
Watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi (1 Yohana 3:10 Yohana 8:33-47 zaidi mstari 44)[2]
iii. Mababa wa Kanisa wanamtaja Mtume Yohana kuwa ndiye mwandishi wa Kitabu hiki. Mababa wa kanisa ni viongozi wa kanisa wa kipindi cha kumalizia karne ya kwanza na kipindi chote cha karne ya Pili. Mababa hawa ni kama vile Papiasi (60-130 B.K), Ireneo (130-202 B.K), Tatuliani (155-220 B.K) na klementi wa Aleksandria (150-215 B.K).Hawa wote wanamtaja Yohana mwanafunzi wa Yesu kuwa ndiye mwandishi wa kitabu hiki katika maandishi yao.
Ifuatayo ni moja ya nukuu ya Baba Ireneo kutoka kwenye maandishi yake inayoonyesha kwamba kitabu hiki na kile cha Injili kimeandikwa na Yohana.
“Basi Injili haimjui Mwana wa Adamu mwingine, isipokuwa yule wa Mariamu, aliyeteswa na hakuna kristo aliyetwaliwa kutoka kwa Yesu kabla ya mateso; Bali inamjua yeye aliyezaliwa kama Yesu kristo mwana wa Mungu, ndio yule yule aliyeteswa na kufufuka, kama Yohana, mwanafunzi wa Bwana alivyothibitisha akisema “Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.”-akiona mapema kufuru hii ambayo inamgawanya Bwana kwa kadiri ya Uwongo wao, wakisema alikuwa na miundo miwili tofauti. Kwa sababu hiyo pia alithibitisha katika waraka wake ; “Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu. Kwa hiyo jueni kila uwongo unatoka nje na si wa kweli. Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo”(Against Heresies,III. 16.5).
Katika nukuu hii Ireneo inanukuu Yohana 20:31 na 1 Yohana 2:18-22 na kuonyesha kwamba Yohana ndiye mwandishi wa hayo yote aliyoyanakuu. Hivyo kanisa wakati wa mababa wa Imani lilikuwa linajua kwamba Yohana ndiye mwandishi wa vitabu hivi viwili.
Hii ndio maana hata nakala zote za zamani zilizoandikwa kwa mkono za kitabu hiki (na barua zingine) zinabeba jina la Yohana kuwa ndiye mwandishi.[3]
Hivyo kwa sababu hizo hapo juu inakubaliwa kuwa Mtume Yohana mwanafunzi wa Yesu ndiye mwandishi wa kitabu hiki.
b. AINA YA KITABU.
Kila mtu anayejua muundo wa waraka akianza tu kusoma kitabu hiki atagundua kwamba hakina muundo wa waraka. Sasa kitabu hiki kilitambulika kama waraka kwa sababu mbili, Moja ni kurudi rudiwa kwa kutajwa kwa kusudi la kuandikwa kwa kitabu hiki na mwandishi (1:4, 2:1; 2:26; 5:13). Mwandishi kwenye maeneo hayo anasema “nawaandikia” kuonyesha aliandika kwa kusudi na kusudi hilo kwa sehemu lilikuwa ni mwitikio wa kutokana na kile kilichokuwa kinaendelea katikati ya wale aliowaandikia (2:26). Kuwepo kwa hali iliyosababisha kitabu hiki kuandikwa ni sababu nyingine inayotuonyesha kwamba kitabu hiki ni waraka kwa sababu Nyaraka nyingi za agano jipya ziliandikwa baada ya kuwepo kwa hali iliyopelekea waraka husika kuandikwa.
Lakini wasomi wengine wa Biblia wanasema kitabu hiki ni Semina/Hotuba sawa na kitabu cha Waebrania. Wengine wanaona kuwa kitabu hiki ni Risala. Yote katika yote kujua kwamba hiki kitabu ni barua au semina/hotuba au Risala hakuathiri uelewa wa ujumbe wake kwa wapokeaji wa awali na kwetu pia. Hivyo vyovyote vile utakavyoona unashawishiwa ujumbe wake hauta athiriwa na chagua utalofanya.
c. SABABU ZA KUANDIKWA KITABU HIKI.
Katika kutafuta kusudi la kuandikwa kwa kitabu chochote basi tunatakiwa kuangalia kauli ya mwandishi inayoonyesha kusudi la kuandika ujumbe wake. Katika kitabu hiki mwandishi ana kauli zaidi ya moja zinazoashiria kusudi la kuandika kwake. Kauli hizi ni kama zifutazo
“Na haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe.” 1 Yohana 1:4
“Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,” 1 Yohana 2:1
“Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza” 1 Yohana 2:26
“Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.” 1 Yohana 5:13
Mwandishi anaonyesha kwamba alikuwa na kusudi zaidi ya moja la kuandika kitabu hiki, kwa sababu mara nyingi baada ya maelezo fulani anataja kusudi la sehemu hiyo. Baada ya kuandika mstari wa 1-3 sura ya kwanza mwandishi anasema “twayaandika ili kusudi furaha yetu itimizwe” akionyesha furaha yake itatimizwa kama kutakuwa na ushirika kati yake na wapokeaji wa ujumbe huu. Baada ya kukosoa kiri zisizo sahihi katika mstari 1-10 sura ya kwanza mwandishi anasema “nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi” akionyesha kwamba lengo la kuwaandikia hayo (1-10) ni kuwataka wasitende dhambi. Baada ya kueleza habari za wapinga Kristo katika mstari wa 18-25 mwandishi anasema “Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza” na baada ya kuelezea kuhusu ushindi wa waamini dhidi ya dunia yaani hiyo Imani yao yenye ushuhuda katika mstari 1-12 sura ya Tano mwandishi anasema “Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu”.
Hivyo Mwandishi alikuwa na kusudi zaidi ya moja katika kuandika ujumbe huu kwa wapokeaji. Makusudi haya yanaweza kuwekwa kwenye makundi mawili, moja ni kusudi la kichungaji na la pili ni kusudi la utetezi wa Imani ya kweli.
Kusudi la Kichungaji.
Mwandishi anawaandikia watu ambao tayali wamekwisha amini (2:12-14; 5:13) na pia wanaijua kweli (2:7, 21), watu ambao anawajua na ni watu ambao ana wajibu kwao, ndio maana anawaita “watoto wangu wadogo” 2:1, “watoto wadogo” 2:28; 3:7; 3:18; 4:4; 5:21. Anawaandikia kuwataka waendelee kwenye kuamini kweli waliyofundishwa tangu mwanzo (2:7, 24) ambayo ina ushahidi wa kweli kutoka kwa mitume waliomsikia, kumuona na kumshika Yesu (1:1-3). Kweli hiyo inawataka kuenenda katika Nuru kama Mungu alivyo katika Nuru (1:5-7), kweli hiyo inawataka kupendana (3:11, 14) katika kweli na Tendo (3:8) kama Mungu alivyowapenda wao (4:10-11, 19) na kweli hiyo inawataka kuamini kwamba Yesu ni Kristo (2:22-23), mwana wa Mungu (1:3, 7; 3:8; 4:9, 15), kipatanisho kwa dhambi zetu (4:10) aliyekuja katika mwili (4:2) na katika maji na damu (5:6). Mwandishi kama mchungaji anasema furaha yake itatimizwa kuona wapokeaji wanaishi kwenye kweli (1:4). Lakini pia kama mchungaji mwandishi anataka wapokeaji wa ujumbe wasitende dhambi (3:8-9; 5:18) na ikitokea mtu ametenda dhambi ajue wanaye mwombezi kwa Baba ambaye ni Yesu kristo (2:1-2, 5:16-17). Na zaidi kama Mchungaji anataka kuwahakikishia kwamba wale wanaoliamini jina la Mwana wa Mungu wanao Uzima wa milele (5:13) ambao ni Yesu mwenyewe (1:2; 5:11, 20).
Kusudi la Utetezi wa Imani ya Kweli.
Sababu kubwa ya mwandishi kuandika kitabu hiki ni kupinga mafundisho potofu na maisha ambayo yako kinyume na kweli ya watu anaowaita “wapinga Kristo” (2:18; 4:3), “manabii wa Uongo” (4:1), “watoto wa Ibilisi” (3:10) na waongo na wadanganyifu (2:4,22; 3:7). Watu hawa walikuwa ni sehemu katika kundi la waamini na wakati mwandishi anaandika ujumbe huu walikuwa wamejitoa (2:19). Kujitoa kwao mwandishi anasema kumetokea ili wafunuliwe kwamba kweli hawakuwa sehemu ya waamini. Lakini watu hawa hawakuishia kujitoa tu bali walifanya jitahada kuwapotosha wengine (2:26). Kwa kuwa Kitabu hiki kinakubaliwa na wasomi wengi wa Biblia kwamba kilikuwa kimekusudiwa kwa ajili ya makanisa yaliyoko Efeso na maeneo ya Karibu (Angalia kipengele d. Wapokeaji wa Ujumbe) basi maneno ya unabii ya mtume Paulo yalitimia kama alivyosema kwa Viongozi wa Efeso (Matendo 20:29-30) na kama alivyomwambia Timotheo alipokuwa huko Efeso (2 Timotheo 3:1-7, 4:3-4)[4].
Watu hawa kwa kumsoma Mwandishi anavyowakosoa na kurekebisha fundisho ni Dhahiri walikuwa wanafundisha yafuatayo,
a. Walikuwa wanakana kwamba Yesu ni Kristo (2:22) na mwandishi anasisitiza kwamba aliyezaliwa na Mungu anaamini kwamba Yesu ni Kristo (5:1).
b. Walikuwa wanakana kwamba Yesu kristo hakuja katika Mwili (4:2, Tazama pia 2 Yohana 7) na mwandishi anasisitiza kwamba Yesu kristo walimuona, walimsikia, walimtazama kwa macho na walimshika kwa mikono (1:1-3).
c. Walikuwa wanakana kwamba Yesu Kristo Mwana wa Mungu hakufa bali mwandishi anasisitiza kwamba alikufa (5:5-6).
Sasa unaweza kushangaa inakuaje watu hawa walikuwa katikati ya waamini pamoja na kwamba wanapinga kila kitu muhimu kuhusu Yesu kristo ?, Mshangao huu unaweza kutokana na sababu mbili, Moja hatujui mpangilio mzuri wa mafundisho yao na tunapata mafundisho yao kutoka upande wa wakosoaji tu. Jambo la Pili kwa sababu kwetu leo Yesu Kristo limekuwa kama Jina moja yaani Kristo limekuwa kama jina la Baba la Yesu. Lakini tukipata mwanga kidogo kutoka katika historia tunaweza kupata angalau mpangilio wa mafundisho yao. Lakini pia tukielewa utofauti wa Jina Yesu na Cheo kristo tunaweza kuelewa fundisho lao. Sasa mwokozi wetu Yesu (Jina lake) aliyezaliwa Bethelehemu alichukua Cheo kinachoitwa Kristo (neno lilotohorewa kutoka kwenye kiyunani) au Masihi (Neno lililotohorewa kutoka kwenye kiebrania) ambacho kina maanishani yeye ni mpakwa mafuta wa Mungu aliyetabiriwa kwamba atakuja kupitia ukoo wa Daudi. Hivyo Yesu ni Kristo kwa maana ya kuwa yeye ni mpakwa mafuta wa Mungu aliyekuja duniani kupitia familia ya mfalme Daudi. Hivyo wapinga Kristo walikuwa wanakana kwamba Yesu ni Kristo.
Lakini pia Maandishi ya Mababa wa kanisa ya kuanzia karne ya Pili ambao walitumia Kitabu hiki cha Yohana kupingana na upotofu huo yanatupa mwanga zaidi katika kutuonyesha kwamba watu hawa walikuwa na mafundisho ya namna gani.
Mababa wa kanisa wanatuonyesha kwamba Moja ya makundi ya walimu wa Uongo lilikuwa ni kundi la Mwalimu Cerinthus, ambaye kwa mujibu wa Askofu Ireneo wa mji wa Lyon, Cerinthus alitengenisha kati ya Yesu na Kristo kwa kufundisha kwamba Yesu alikuwa ni mwanadamu wa kawaida tu wa kule Nazareth aliyezaliwa na Joseph na Mariam kwa njia ya kawaida tu, ambaye alikuwa na Huruma na Hekima na Kristo alitoka kwa Mungu na kumshukia Yesu wakati wa Ubatizo wake, hivyo Kristo aliyekuwa ndani ya Yesu akamhubiri Baba ambaye alikuwa hafahamiki na akafanya miujiza mingi na mwishoe alimtoka Yesu kabla hajasurubiwa. Hivyo Cerinthus alifundisha kwamba Kristo kutoka Mbinguni hakusurubiwa bali Yesu mwanadamu wa Nazareth ndiye aliyesurubiwa na baadaye kufufuka.[5]
Kundi lingine ni lile la Docetism, ambao hawa hawakukubalina na ubinadamu wa Yesu hivyo walifundisha kwamba Yesu hakuwa na umbile halisi la Binadamu japo alionekana kuwa na mwili wa binadamu. Kwa lugha rahisi walifundisha kwamba Yesu alikuwa kama Mzimu. Makundi haya yalikuwa ni matawi ya Mafundisho wa Unostiki ambao msingi wao wa Imani ulikuwa kwamba vitu vinavyoonekana na kushikika ni viovu kwa asili na vitu vya kiroho ni vyema kwa asili. Hii ndio maana hawakukubali kwamba Yesu alikuwa mwanadamu wa kawaida (Docetism) na hawakukubali kwamba Yesu ni Kristo (Cerinthian).
Kumbuka makundi haya yanatupa mwanga tu wa kile ambacho mwandishi alikuwa anapingana nacho.
Mbali na mafundisho potofu kuhusu Yesu kristo kama tulivyoeleza pia waalimu hawa wa uongo waliishi maisha yasiyo na maadili yatokanayo na kweli. Hii ndio maana mwandishi anawakosoa sana akisema:
“Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.” 2:4
.”Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.” 2:9
“Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.” 2:11
“Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona” 4:20
“Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki” 3:7
Na kuna uwezekano mkubwa zile “Tukisema” za mstari wa 6, 8 na 10 sura ya kwanza zilikuwa pia ni nukuu za mwandishi kutoka kwa waalimu hawa wa Uongo. Haya yote yanaonyesha waalimu hawa wa Uongo waliishi tofauti na ukiri wao wa kumjua Mungu na kuwa na ushirika naye.
d. WAPOKEAJI WA AWALI WA KITABU.
Kwenye sehemu ya kuelezea sababu za kuandikwa kitabu hiki tumeona kwamba kitabu hiki kiliandikwa kwenda kwa waamini ambao tayali wanaijua kweli lakini kwenye jamii yao kumetokea mgawanyiko, kuna kundi la wanaoijua kweli na kundi la waalimu wa uongo ambao walijitenga. Mwandishi Yeye hajataja mahali kitabu hiki alipokielekeza hivyo imewafanya wasomi wengi wa Biblia kuamini kwamba kitabu hiki kiliandikwa kwa ajili ya kusomwa kwenye makanisa mengi ambayo yalikuwa yameathiriwa na mafundisho ya waalimu hawa wa uongo.
Na kutoka kwenye vitabu vya waandishi wa karne ya Pili na ya Tatu tunajifunza kwamba Mtume Yohana, mwana wa Zebedayo, mwanafunzi Yesu aliyempenda aliishi na kufanya huduma yake kule Efeso, Asia kati ya mwaka 70-100 B.K.
Mmoja wa watu wanatoa taarifa hizo ni Ireneo Askofu wa Mji wa Lyon, ambaye yeye alimsikia na kumuona Askofu Polycap ambaye alikuwa mwanafunzi wa Yohana mtume na aliyejifunza Injili kutoka wengine waliomuona Yesu. Ireneo anasema Yohana mwanafunzi wa Yesu aliandika Injili akiwa Efeso huko Asia.[6]
Pia Ireneo anasema kanisa la Efeso lilianzishwa na mtume Paulo na Yohana mwanafunzi wa Yesu alibaki huko mpaka muda wa utawala wa Trajan. Na pia anaripoti kwamba Yohana aliwahi kujitoa kwenye sehemu ya kuoga baada ya kugundua mwalimu wa Uongo (Cerinthus) ameingia pia kuoga sehemu hiyo huko Efeso, kama walivyomsikia Polycarp akisimulia.[7]
Baba Askofu Eusebio katika kitabu chake cha Historia ya Kanisa anawataja na kuwanukuu mashaidi wawili ambao wanatoa taarifa kwamba Yohana aliishi huko Efeso, Asia. Mashahidi hawa ni Ireneo wa Lyon na Klementi wa Aleskanda.[8] Kuna ushahidi mwingi wa kutoka kwa waandishi wengine wa karne ya Pili ambao sijawataja, unaonyesha kwamba Yohana aliishi na kufanya huduma yake huko Efeso.
Hivyo ina aminika kwamba kitabu hiki kiliandikwa kwa ajili ya makanisa ya efeso na yale ya maeneo ya karibu. Makanisa ya maeneo ya karibu yakiwa ni kama vile Smirna, sardi, laodokia, pergamo, Thyatira na Philadephia makanisa yaliyoandikiwa barua katika kitabu cha ufunuo.
e. MPANGILIO WA KITABU.
Mpangilio wa Kitabu hiki ni vigumu kuugundua kwa sababu Mwandishi haelezei hoja zake kwa mpangilio maalumu mwanzo mpaka mwisho yaani anaanza jambo moja baada ya muda anaingia japo la pili kabla ya kumaliza la pili anarudi tena kwenye jambo la kwanza. Mfano anazungumiza kupendana katika 3:11-24 na baada ya hapo anazungumzia wapinga kristo (4:1-6) alafu anarudi tena kuzungumza kuhusu kupendana (4:7-21).
Pia lugha anayotumia Mwandishi ni lugha ya kurudia rudia maneno yale yale kama wimbo. Maneno haya ni kama vile “kaeni ndani yake” “amri zake” “mwana wake” “kupendana”.
Hivyo mpangilio huu ni pendekezo letu tu kwa ajiri ya kutusaidia kufuatilia mawazo ya mwandishi.
Sehemu | Maelezo |
1:1-4 | UTANGULIZI |
1:5-2:27 | USHIRIKA NA MUNGU |
a. 1:5-2:2 | Tusijidanganye. |
b. 2:3-2:11 | Tushike amri zake. |
c. 2:12-2:14 | Kwenu watoto wadogo, wakina Baba na Vijana. |
d. 2:15-2:17 | Msiipende Dunia. |
e. 2:18-2:27 | Wapinga Kristo (Sehemu ya I) |
2:28-3:24 | WANA WA MUNGU |
a. 2:28-3:10 | Uhusiano wa Mwana wa Mungu na Dhambi na kutenda Haki |
b. 3:11-3:24 | Tupendane (Upendo sehemu ya I) |
4:1-5:17 | MSISITIZO |
a. 4:1-4:6 | Kuzitambua Roho (Wapinga Kristo sehemu ya II) |
b. 4:7-4:21 | Tupendane (Upendo Sehemu ya II) |
c. 5:1-5:13 | Kumwamini Mwana wa Mungu |
d. 5:14-5:17 | Ujasiri wetu katika Maombi |
5:18-5:21 | HITIMISHO |
a. 5:18 | Uhusiano wa Mwana wa Mungu na Dhambi |
b. 5:19 | Sisi tu wana wa Mungu |
c.5:20 | Sisi ndani ya Mwana wake |
d. 5:21 | Tujiepushe na Sanamu |
1 Yohana 1:1-4
1.1 Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima;
1.2 (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);
1.3 hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.
1.4 Na haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe.
Mpangilio wa mfululizo wa mawazo ya Mwandishi.
1:1 Mwandishi anaanza na kueleza uhusiano wake wa Neno la Uzima.
1:2 Mwandishi anauelezea Uzima
1:3 Mwandishi anaendelea kuelezea Uhusiano wake na Neno la Uzima na utangazaji wake Neno Hilo kwa wapokeaji wa ujumbe wa kitabu hiki
1:4 Mwandishi anaeleza kusudi la kuandika.
UFAFANUZI- UTANGULIZI.
Mwandishi anaanza na kuelezea uhusiano kati yake na Neno la Uzima (1:1). Lakini uhusiano huu ana ueleza kwa kutumia lugha ya wingi, maana yake hayuko peke yake mwenye uhusiano huu na Neno la Uzima. Neno hilo la Uzima ndilo (a) Lile lililokuwako tangu mwanzo, (b) Lile tulilolisikia, (c) Lile tuliloliona kwa macho yetu, (d) Lile tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa. Kabla ya kuendelea kueleza Zaidi kuhusu Neno la Uzima, Yohana anaelezea kuhusu huo Uzima (1:2). Uzima huo ulidhihirika na Yohana na wenzie waliuona (Tazama Yohana 2:11, 21:1 na 21:14)[9]. Baada ya kuuona Uzima walifanywa mashahidi na sasa wanatoa ushahidi kuhusu Uzima huo (shuhudia) na wanawatangazia (hubiri) wapokeaji wa ujumbe huu uzima huo ambao ni Uzima wa Milele. Uzima huu wa Milele kabla haujadhihirika Ulikuwa kwa Baba (Tazama Yohana 1:1,14).
Baada ya kuelezea kuhusu Uzima/Uzima wa Milele Yohana anarudi kuelezea habari za mstari wa kwanza, zinazohusu Neno la Uzima. Neno hilo la Uzima anasisitiza kwamba waliliona na kulisikia (Alisema pia mstari wa 1) na wanawatangazia/wanawahubiri wapokeaji wa Ujumbe huu ili wapokeaji wawe na ushirika na wao, wao yaani Yohana na kundi lililo upande wake. Yohana na kundi lililo upande wake wana uhakika kwamba wao wana Ushirika na Baba pamoja na Mwana wake Yesu Kristo (1:3). Kwa Lugha nyingine Yohana anawataka wapokeaji wa ujumbe huu wawe na ushirika naye pamoja na kundi lililo upande wake, ambao wao wana uhakika kwamba wana Ushirika na Baba na mwana wake Yesu kristo. Na wapokeaji wakiwa na Ushirika na Yohana na kundi lake basi Furaha yao itatimizwa, na hilo ndio lengo la kuwaandikia (1:4).
Walio Upande wa Yohana
Kwa uhusiano Yohana anaoutaja kuhusu Neno la Uzima kundi lililo upande wake ni Dhahiri kwamba ni kundi la Mitume, wale waliomuona kwa macho, kumsikia, kumtazama na kumshika kwa mikono yao. Pamoja na kwamba Yohana anaandika ujumbe huu peke yake (Matumizi ya Lugha ya umoja 2:1, 7, 8, 12, 13, 14, 21, 26, 4:20, 5:13) ila anatumia kundi la mitume kuonyesha kwamba yeye yuko kwenye upande wa ukweli (Matumizi ya Lugha ya wingi anazungumzia kusikia, kuona na kushika neno la Uzima 1:1-3,5; 3:11; 4:14;5:20).
Neno la Uzima.
Neno la Uzima ni ujumbe uliofanyika mwili katika Yesu kristo Bwana wetu ambao Yohana anauhubiri kwa wapokeaji wa kitabu hiki. Sifa za ujumbe Yohana anazosema anawahubiri wapokeaji ni sifa za kitu chenye uhai, hivyo ujumbe huu Yohana anaousema ni ujumbe ambao alikuwa na mwili wa kushikika, umbile la kuonekana na ujumbe uliongea na wakasikia.
Ushirika.
Yohana anasema anawahubiri wapokeaji wa ujumbe huu wa maandishi ili wawe na ushirika naye na watu walio upande wake na wao wana uhakika wako na ushirika na Baba na mwanae Yesu kristo. Swali la msingi litakuwa nini maana ya Ushirika katika sentensi hii? Je Yohana anamaanisha anahubiri ili waokoke? Au wawe upande wake mbali na upande mwingine?. Sasa Neno hili “ushirika” (kiyunani; Koinonia) limetumika mara nne tu katika waraka huu na halijatumika kabisa katika 2 Yohana, 3 Yohana wala katika Injili ya Yohana. Neno hili kama lilivyotumika katika mstari wa 3, 6 na 7 lina maanisha Ushirika ni kitu kinachotokea pale watu wanapoenenda katika kweli (6) yaani wanapoenenda nuruni kama Mungu alivyo katika Nuru (7). Kwa hiyo Yohana anawahubiri wapokeaji wa ujumbe ili waenende katika kweli yaani Kuenenda Nuruni kama Mungu alivyo na hilo likitokea Yohana furaha yake itatimizwa (Tazama 2 Yohana 4 na 3 Yohana 4). Kwa hiyo Yohana na kundi lake wao wana uhakika kwamba wanaenenda katika kweli yaani wanaenenda nuruni kama Mungu alivyo, hiyo kinyume na kundi kinzani (Kundi la wapinga Kristo).
TUNAJIFUNZA NINI.
1. Imani juu ya Yesu kristo ina ushahidi uliokamilika. Kwa kusoma lugha ya Yohana Uzima au Uzima wa milele ni Yesu mwenyewe (2) na Neno la Uzima ni Yesu mwenyewe katika mwili wa kibinadamu, Ujumbe Yesu aliofundisha na ujumbe unaohusu maisha yake ya hapa duniani yaani kuzaliwa, kuteswa, Kufa na kufufuka kwake. Yesu na ujumbe wake havipaswi kutenganishwa kama Yohana anavyochanganya katika Lugha yake, anasema Neno la Uzima waliliona kwa macho, walilisikia, walitazama na kulipapasa kwa mikono(1) na wanalibubiri kwa wapokeaji wa ujumbe (3) na pia Uzima wenyewe waliuona na wanawahubiri wapokeaji (2). Hivyo kwa upande mmoja Yohana anatofautisha kati ya Ujumbe na Yesu mwenyewe na Upande wa pili hatofautishi Ujumbe na Yesu mwenyewe.
Sasa duniani kote ushahidi wa kujitosheleza ni ule wa kuona au kuhusika katika tukio, Yohana anatuhakikishia kwamba Yeye na wenzie (Mitume) waliona kwa Macho, walisikia, walitazama na walishika kwa mikono mambo wanayoyatolea Ushahidi. Yaani habari za Yesu na Yesu mwenyewe sio hadithi wala sio tungo bali ni ushahidi wa watu wanaokidhi vigezo vya kuwa mashahidi wa kweli.
Mwamini mwenzangu usiwe na wasi wasi wala mashaka kuhusu kumwamini Yesu, maana mwandishi Yohana ni shahidi wa kuona, kusikia na kugusa. Na Yohana anatumia wingi kuonyesha kwamba hayuko peke yake, yuko na wengi. Mmoja wa wenzie na Yohana aliwahi pia kusema “Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu” 2 Petro 1:16-18
Hivyo Imani yetu sio matokeo ya utunzi wa mtu au ushahidi wa mtu mmoja tu, hapana. Mara nyingi watu husema kwenye maswala ya Imani hakuna mtu mwenye uhakika asilimia mia, lakini wewe mwamini hautakiwi kuwa kwenye kundi la Namna hilo. Unapokuwa jaji au mmoja wa watu wa baraza la mahakama na ukasikiliza ushahidi mwisho wa siku unapoamua kumtaja mtu kuwa ni mtuhumiwa au sio mtuhumiwa hautakiwi kuwa na mashaka na uamuzi wako. Unatakiwa kuwa na uhakika kutokana na ushahidi uliousikia kutoka kwa mashahidi wenye vigezo vya kutoa ushahidi wa kweli. Hivyo sikiliza ushahidi wa Yohana Imani yako iwe thabiti.
Unaweza kujiuliza kwa nini Mitume Yohana na Petro wanatetea Ushahidi wao kwamba waliona, walisikia na kushika wakati waliishi miaka michache tu baada ya Yesu kuwepo? Jibu ni kwamba tayali watu walipinga ukweli wa habari ya Yesu tangu mwanzoni mwa Imani hii, Hivyo hakuna jipya leo. Wanadamu wanapopiga ukweli wa habari za Yesu jua kwamba hicho wanachokifanya wao sio wa Kwanza. Kazi yetu sisi ni kufanya kama Yohana na Petro kutetea ukweli wa Maisha ya Bwana wetu Yesu.
2. Tushirikiane na upande wenye ukweli.
Lengo la Yohana kuonyesha kwamba wao ni mashahidi wa kuona, kusikia na kugusa ni kuwataka wapokeaji wajue kwamba wao ni mashahidi wa kweli wa kile wanachokihubiri. Tena Yohana alikusudia ujumbe huu ulete Ushirika kati ya wapokeaji wa ujumbe na upande wake. Kwa sababu wao (mitume) wana uhakika wa kuwa na ushirika na Baba pamoja na mwanae Yesu kristo. Ushirika huu una maana kama tulivyoelezea hapo juu, kwamba Yohana anataka wapokeaji wa ujumbe huu waenende katika kweli yaani kuenenda nuruni kama Mungu alivyo. Upande huu ndio upande ambao Yohana na mitume wapo. Kwa usomaji wa ujumbe huu utagundua kwamba kuna upande Yohana alikuwa anapingana nao. Upande huo Yohana anaopingana nao una mafundisho na maisha kinyume na kweli (Upande wa wapinga Kristo). Na upande huo unataka kujipatia wafuasi (Ushirika) kwa wapokeaji wa Ujumbe huu wa Yohana, ndio maana katika waraka mzima ataendelea kupingana na upande huo pinzani wenye mafundisho potofu.
Hata Leo kuna mafundisho potofu kinyume na mafundisho ya Bwana Yesu na mitume tunatakiwa kuepukana na watu wa namna hiyo na kuwa na ushirika na watu wanaoshika mafundisho na mfano wa maisha ya Bwana Yesu pamoja na mitume wake. Mafundisho ya Bwana wetu Yesu kristo na mitume yanatutaka tuenende katika kweli kwa kuenenda nuruni kama Mungu alivyo. Changua upande huu na upinge upande ulio kinyume na mafundisho ya kweli.
1 Yohana 1:5-2:2
1.5 Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake.
1.6 Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli;
1.7 bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
1.8 Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
1.9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
1.10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.
2.1 Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,
2.2 naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.
Mpangilio wa mfululizo wa mawazo ya Mwandishi.
1:5 Mwandishi anaanza na kauli (kweli) inayojumuisha hoja yake. Kila mwandishi atakachoeleza mstari wa 6 sura ya kwanza mpaka mstari wa 2 sura ya pili kinabebwa na kweli hii.
1:6 Mwandishi anaelezea kweli hiyo kwa mara ya kwanza akihusianisha na mwenendo wa waamini. Hili analifanya mstari wa 6 mpaka wa 7
1:8 Mwandishi anaelezea kweli hiyo kwa mara ya pili akihusianisha na mtazamo wa waamini kuhusu hali ya dhambi na matendo ya dhambi. Hili analifanya mstari wa 8 mpaka wa 9.
1;10 Mwandishi anaeleza kweli hiyo kwa mara ya tatu akihusianisha na uhalisia wa maisha ya nyuma ya waamini. Hili analifanya mstari wa 10.
2:1 Mwandishi anahitimisha kwa kutoa sababu ya kuandika hayo yote (1:5-1:10). Na hili analifanya mstari wa 1 na 2 sura ya pili.
UFAFANUZI.-TUSIJIDANGANYE.
Yohana baada ya kuonyesha kwamba Yeye (pamoja na mitume) ni shahidi wa kweli wa kuona, kushika na kusikia kwa habari ya Neno la Uzima anaanza kwa kusema “hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake” kwamba “Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake” na habari hii wanaihubiri kwa wapokeaji (1:5). Mungu ni nuru ni Lugha ya picha kutoka agano la kale inayoonyesha utakatifu, usafi na “ukamilifu katika wema” wa Mungu. Kwa sifa hii ndani yake hakuna giza kabisa yaani hakuna uovu wala kutokukamilika katika wema. Kwa kuwa Mungu ana sifa hiyo kama walivyosikia kutoka kwa Yesu, mtu yeyote anayesema ana ushirika na Mungu hatakiwi kuenenda gizani maana akifanya hivyo anakuwa mwongo na wala haiishi kweli (1:6). Bali mtu anayesema ana ushirika na Mungu anatakiwa kuenenda Nuruni kama Mungu yeye alivyo Nuru, na waenenda nuruni wana ushirika miongoni mwao na damu ya Yesu huwasafisha dhambi yote (1:7). Mwandishi anatumia Lugha ya wingi akijiambatanisha na wapokeaji. Sasa mwandishi anavyoeleza mambo ni wazi kwamba kuna kundi anapingana nalo ambalo ananukuu wanayoyasema au kuyaishi (Tazama 2:19, 26). Kundi hilo haliishi kweli kwa kuwa wanasema wana ushirika na Mungu lakini wanaishi gizani. Kundi hilo ni waongo kwa kuwa wanakiri ushirika na Mungu lakini wanaishi gizani. Hii ndio maana mwandishi alianza kuandika kitabu hiki kwa kueleza kwamba yeye ni shahidi wa kweli wa Neno la Uzima akionyesha utofauti wake na kundi hilo (1:1-3). Lakini pia ndio maana anataka wapokeaji wa Ujumbe wawe na ushirika naye na sio hilo kundi linalokiri kuwa na ushirika na Mungu na wakati wanaenenda katika giza (1:3). Kwa mwanga wa Yohana 3:19-21 kuenenda katika giza ni kuwa na maisha ya matendo maovu na kuchukia nuru ili matendo hayo maovu yasikemewe[10]. Hii ndio maana waenenda gizani wanaweza kusema hawana dhambi kitu ambacho pia Mwandishi anakipinga (1:8). Hivyo wapinzani wa Yohana pamoja na kuwa wana maisha ya matendo maovu kinyume na sifa ya Mungu lakini pia wanasema hawana dhambi ili maovu yao yasikemewe. Yohana anasema na sisi tukisema hivyo “twajidanganya wenyewe,wala kweli haimo mwetu”. Hivyo kuenenda Nuruni sio tu kuishi katika maisha ya usafi na utakatifu kama Mungu alivyo bali pia ni kukubali matendo ya maisha yetu yamulikwe na yawe wazi ili kuonekana kama yametendwa katika Mungu au la. Na kama hayajatendwa katika Mungu (sawa na sifa ya Mungu) tunatakiwa kuungama, tukiungamaYeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote (1:9). Dhambi kuondolewa ni kusamehewa na kusafisha udhalimu ni kuondoa kile dhambi imezalisha au mabaki yaliyosababishwa na Dhambi.
Ukiri wa kutokuwa na dhambi wa wapinzani wa Mwandishi umekwenda mbali Zaidi na kufikia kusema “hatukutenda dhambi” na sisi tukiungana nao tunamfanya Yesu kuwa mwongo na kitendo hicho kinaonyesha dhahiri kweli yake haimo ndani yetu (1:10). Mwandishi anasema Lengo la kuandika haya (mstari wa 5-10) ni ili wapokeaji wa kitabu hiki wasitende dhambi (sawa na fundisho la 1:6-7) na ikitokea mtu ametenda dhambi ajue tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki (sawa na fundisho la 1:8-8) (2:1). Yesu kristo ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote (2:2).
Kuungama
Kuungama dhambi katika Agano jipya kunapatikana katika maeneo mengine manne. Sehemu ya kwanza na ya pili ni watu walikuwa wanaenda kwa Yohana kuungama dhambi zao (Mathayo 3:6 na Marko 1:5) na kubatizwa. Sehemu ya Tatu ni Yakobo anawaambia waamini waungame dhambi zao kati yao wenyewe (Yakobo 5:16). Sehemu ya nne ni kule Efeso watu walipoamini wakaja wakaungama (Matendo 19:18) wakidhihirisha matendo yao. Sehemu zote hizo zinaonyesha kuungama ni kukiri kwa kukubali kwamba kilichofanyika ni dhambi. Na sehemu zote hizo watu/mtu alikiri kwa kukubali kwamba alichofanya ni dhambi mbele ya watu/mtu wengine. Mwandishi wa kitabu hiki yeye hajatuonyesha kwamba tuungame kwa mtu mwingine au la, yeye msisitizo wake uko katika kukiri kwa kukubali kwamba kile kilichofanyika ni dhambi.
TUNAJIFUNZA NINI.
1. Ukiri unaokinzana na Uhalisia wa Maisha.
Ushirika na Mungu mwandishi anasema ni halisi na huzaaa mwenendo wa Nuruni kwa maana Mungu ni Nuru. Hivyo kwa mujibu wa mwandishi hakuna mtu aliye na ushirika na Mungu na mwenendo wake ni wa gizani. Ukiri wetu wa kuwa na ushirika na Mungu unatakiwa kuendana na namna tunavyoishi. Tukiishi maisha ya gizani na kukiri kwamba tuna ushirika na Mungu mwandishi anasema hapo tunakuwa Waongo na wala hatuiishi kweli.
2. Tunaye Mwombezi kwa Baba.
Kwa kile mwandishi alichokisema kuhusu mwamini na maisha yake ni rahisi kujiuliza kwamba Je mwandishi anamaanisha mwamini akifanya dhambi ina maana hana ushirika na Mungu?. Swali hili litajirudia mara nyingi kwa sababu mwandishi atarudia rudia msisitizo wake wa kuwataka waamini kuishi maisha masafi ya utakatifu (Mwenendo wa Utakatifu). Mwandishi anachokisema ni mfumo wa maisha unaoendana na giza ni ishara ya uhalisia kwamba mtu huyo hana ushirika na Mungu ambaye ni nuru. Hii ndio maana pia mwandishi anakataa mwamini kusema sina dhambi kwa sababu anajua mwamini anaweza kufanya dhambi, hivyo mwamini anaweza kufanya dhambi. Mwisho mwandishi anatoa nini kifanyike mwamini anapokuwa amefanya dhambi. Mwandishi hasemi mwamini akifanya dhambi afanye kama hakuna kilichotokea, hapana. Bali mwamini anatakiwa kukiri kwa kukubali kwamba alichofanya ni dhambi (Kuungama) hili linaweza kufanyika mbele ya mwamini/waamini wenzie au kwa Mungu. Mwamini akifanya hilo Mungu ni mwaminifu na wa haki kumsamehe dhambi yote na kuondoa kila mabaki yaliyosababishwa na dhambi. Uaminifu wa Mungu unatuhakikishia msamaha ambao upo tayali ni sisi tu kuungama.
3. Tusitende Dhambi.
Lengo la mwandishi katika sehemu hiyo ya maandiko ni kututaka sisi waaamini tusitende dhambi. Na pia jambo hili mwandishi atarudia rudia kama ilivyo kawaida yake. Mwamini mwenzangu kwa kuwa lengo la kujifunza maandiko ni kuishi sawa sawa na Ufunuo wa Mungu kwetu, basi tunatakiwa kuishi maisha ya kutotenda dhambi hili ndio lengo la Mwandishi. Lakini ikitokea tumetenda dhambi tunatakiwa kufanya kama tulivyoeleza hapo juu kwamba tunaye mwombezi kwa Baba maybe ni Yesu kristo.
1 Yohana 2:3-11
2.3 Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake.
2.4 Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.
2.5 Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake.
2.6 Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.
2.7 Wapenzi, siwaandikii amri mpya, ilaamri ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Na hiyo amri ya zamani nineno lile mlilolisikia.
2.8 Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu; kwa kuwa giza linapita na ile nuru ya kweli imekwisha kung’aa.
2.9 Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.
2.10 Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.
2.11 Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.
Mpangilio wa mfululizo wa mawazo ya Mwandishi.
2:3 Mwandishi anaanza ya kauli inayojumuisha hoja yake. Kila anachoeleza katika mstari wa 4-11 kinabebwa na kauli ya mstari wa 3.
2:4 Mwandishi anaelezea hoja yake kwa kunukuu “yeye asemaye” mara ya kwanza katika mstari wa 4-5.
2:6 Mwandishi anaelezea hoja yake kwa kunukuu “yeye asemaye” mara ya pili katika mstari wa 6-7
2:9 Mwandishi anaelezea hoja yake kwa kunukuu “yeye asemaye” mara ya tatu katika mstari wa 7-11.
UFAFANUZI-TUSHIKE AMRI ZAKE.
Mwandishi anaanza kwa kueleza kauli ya ujumla kwamba ikiwa tunashika amri zake basi tunajua kwamba tumemjua yeye (2:3). Yeye kwa muktadha huu inamaanisha Yesu lakini pia inaweza kumaanisha Mungu kwa kuwa kwa Mwandishi Yesu na Mungu hawatenganishwi. Kushika amri ni kuishi kwa kufuata maelekezo ya amri hizo. Mwandishi anaelezea vizuri zaidi kwa kunukuu mtu anayekiri kwamba amemjua yeye lakini hazishiki amri zake. Mwandishi anasema mtu wa namna hiyo ni mwongo na wala kweli haimo ndani yake (2:4). Kinyume cha mtu mwongo mwandishi anamuelezea mtu anayeshika amri zake (Hapa imeziita amri Neno lake) kwamba mtu huyo upendo wa Mungu umefikia kilele (umekamilika) kweli kweli (2:5a). Na kwa kushika amri zake mwandishi anasema twajua kwamba tumo ndani yake, yaani ndani ya Yesu (2:5b). Mwandishi ananukuu mara ya pili mtu ambaye anasema anakaa ndani yake. Mwandishi anasema yeye anayekiri kwamba anakaa ndani ya Yesu imempasa kuenenda kama Yesu alivyoenenda (2:6). Mwandishi anamtaja Yesu kuwa kielelezo cha aina ya maisha ya mtu anayesema anakaa ndani yake anayotakiwa kuishi. Bado mwandishi anasisitiza kuishi maisha yanayoendana na kufuata amri/Neno/Mfano wa Yesu. Mwandishi anajua wapokeaji wa kitabu hiki wanazijua amri za Yesu tangu mwanzo kwa kuwa walisikia Neno lake hivyo anachowaandikia sio amri mpya (2:7). Mwandishi bado unachanganya kati ya amri za Yesu na Neno lake, Hivyo havitenganishwi. Na wazo lake kubwa kuanzia mstari huu wa 7 mpaka 11 ni amri ya Yesu ya kupendana (Tazama Yohana 13:34 na 15:12,17). Lakini kwa upande mwingine mwandishi anasema anawaandikia amri mpya japo ni amri ile ile aliyosema sio mpya (Anatumia Lugha Yesu aliyotumia Yohana 13:34), neno lililo kweli ndani yake (Yesu) na ndani yenu (waamini) (2:8a). Anawaandikia amri hii kwa sababu giza linapita na nuru ya kweli imekwisha kung’ara (2:8b). Nuru ya kweli ni Mungu ambaye amejifunua duniani kupitia Yesu kristo (Tazama Yohana 1:4-5).
Katika kuelezea kushika amri hii ya Upendo mwandishi anafafanua kwa kumnukuu mtu anayesema kwamba yuko Nuruni lakini anamchukua ndugu yake, mtu huyo mwandishi anasema yuko gizani (2:9). Lakini yeye anayempenda ndugu yake mwandishi anasema huyo anakaa katika Nuru na ndani yake hamna kikwazo/kinachomzuia (2:10).Mwandishi anarudi kumuelezea mtu aliyemuelezea mstari wa 9 kwa msisitizo zaidi kwamba mtu huyo “yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho” (2:11). Kuwa nuruni ni kuwa ndani ya Mungu ambaye ni nuru na kuwa gizani ni kuwa nje na Mungu ambaye ndani yake hakuna giza (Kumbuka 1:5).
Amri zake.
Amri ni maagizo Yesu aliyoyatoa kwa wanafunzi wake, ambayo aliyatoa kwa kuzungumza ndio maana hizo amri pia zinaitwa Neno lake. Na wanafunzi wake waliwafundisha wengine ambao waliamini pasipo kumsikia Yesu mwenyewe. Waliwafundisha kwa mazungumzo au kwa maandishi. Neno lake hapa haimaanishi Biblia kwa sababu wapokeaji wa ujumbe huu hawakuwa na Biblia kama sisi tulivyonayo leo. Lakini kwa sababu maneno hayo ya Yesu tunayapata katika Biblia hivyo ni sawa kuita Biblia neno lake.
TUNAJIFUNZA NINI.
1. Kuzishika amri zake.
Mara nyingi ukizungumza amri, waamini wanafikiri kuhusu kurudishwa kwenye torati lakini Mtume Yohana anajua kwamba Yesu alitoa maagizo mengi kwao ili pia wao wafikishe kwa kila atakaye amini na maagizo hayo yalikuwa ni matakwa ya Bwana wala sio mapendekezo. Tuna mengi ambayo Bwana ametuamuru kuyafanya au kutokufanya ni wajibu wa kila anayesema ameamini kuishi kwa kufuata amri hizo. Na kuishi kwa kufuata Neno/amri za Kristo ni Ushahidi kwamba mwamini anamjua Kristo na upendo wa Mungu unafanya kazi ndani yake kwa kiwango kinachotakiwa.
2. Kuenenda kama Yesu alivyoenenda.
Mwandishi anatufundisha kufanya ukiri wetu ufanane na vile tunaishi. Kwa kuwa wote tulioamini tunatambulika kwamba tuko ndani ya Yesu na ndivyo ilivyo, hivyo sisi tunadaiwa kuishi kama Kristo katika mwenendo wetu. Yesu ndiye mfano bora wetu wa namna ya kuishi kwa wote tunaoamini na kukiri kwamba tuko ndani yake.
3. Kupendana.
Yohana katika aya hii amesisitiza sana kufuata/kuishi sawasawa na neno/amri/maagizo ya Yesu, Na Yohana katika Injili ametusaidia kunukuu moja ya amri kati ya nyingi Yesu alizoziacha, amri hii ni kupendana (Yohana 13:34-35). Hivyo Yohana tena anasisitiza kwamba kupitia upendo tunaweza kujua nani yuko nuruni nan ani yuko gizani. Hivyo upendo ni hali ya waamini kwa kuwa wo wako nuruni. Kwa upande mwingine mwandishi anatuambia kwamba hakuna kuchukiana kwa waamini/watu walioko nuruni.
1 Yohana 2:12-14
2.12 Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake.
2.13 Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa sababu mmemjua Baba.
2.14 Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.
Mpangilio wa mfululizo wa mawazo ya mwandishi.
Mwandishi ameandika sababu za kuandika ujumbe huu kwa kutaja makundi husika. Ameanza na watoto, akafuata akina Baba na mwisho kumalizia na Vijana. Amelifanya hili kwa awamu mbili.
2:12-13 Awamu ya kwanza. Ametumia lugha ya wakati uliopo “Nawaandikia”.
2:13-14 Awamu ya Pili. Ametumia Lugha ya wakati uliopita “Nimewaandikia”
UFAFANUZI-WATOTO, WAKINA BABA NA VIJANA.
Baada ya hayo mwandishi aliyoyaandika mpaka sasa, anaeleza sababu ya kuandika kwa kutaja makundi matatu ambayo ni watoto, akina Baba na Vijana. Ni vigumu kujua kwa uhakika mwandishi alitumia majina ya makundi haya kwa kuzingatia umri au hatua za ukuaji wa kiroho au alikuwa amekusidia watu wote. Mwandishi anasema anawaandikia watoto kwa sababu wamesamehewa dhambi zao kwa ajili ya jina lake (2:12). Mwandishi anawaandikia akina Baba kwa sababu wamemjua yeye aliye Tangu mwanzo (2:13a). Hii ikimaanisha wamemjua Yesu tangu mwanzo wa kuamini kwao, na hili linaweza kuashiria kwamba wakina Baba ni waamini mwenye muda mrefu katika Imani yao. Vijana mwandishi amewaandikia kwa sababu wamemshinda yule mwovu/shetani (2:13b). “mmemshinda” ni lugha inayoonyesha jambo lililotokea wakati uliopita na matokeo yake yanaonekana mpaka sasa. Baada ya kumaliza awamu ya kwanza mwandishi anarudia tena kusisitiza sababu za kuandika lakini sasa anatumia lugha ya wakati uliopita. Kwa watoto mwandishi anasema Nimewaandikia kwa sababu wamemjua Baba (2:13c), hii inaweza kuashiria kwamba wamemjua hivi karibuni tofauti na akina Baba. Kwa akina Baba mwandishi anarudia yale yale aliyoyasema katika sehemu ya kwanza (2:14a). Mwisho mwandishi anasema amewaandikia vijana sababu wana nguvu na Neno la Mungu linakaa ndani yao na wamemshinda shetani (2:14b).
Kumshinda Yule mwovu.
Neno Kushinda (Kiyunani Nikao) zaidi ya sehemu hii (2:12-14) limetumika mara nne zaidi katika kitabu hiki. Sehemu ya kwanza mwandishi anawataja wapokeaji wa ujumbe kwamba wamewashinda manabii wa uongo, wenye Roho ya mpinga kristo, kwa sababu Mungu aliye mkuu kuliko aliye katika dunia yuko ndani yao (4:4). Sehemu ya Pili mwandishi anasema kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu (5:4a). Sehemu ya Tatu mwandishi anasema hiyo Imani yetu ndio kuushinda Ulimwengu (5:4b) na Sehemu ya mwisho mwandishi anasema kuushinda ulimwengu ni kuamini kwamba Yesu ndiye mwana wa Mungu aliyekuja kwa maji na damu. Kwa ujumla kumshinda mwovu ni kumwamini Yesu mwana wa Mungu na hivyo ni kuzaliwa na Mungu ambaye ni mkuu kuliko yeye aliyeko ulimwenguni. Hii ndio maana mwandishi anavyowaambia vijana kuhusu kumshinda yule mwovu. Anawaambia kwa lugha ya wakati uliopita kwa kuwa ushindi huu unapatikana wakati wa kuamini na matokeo yake hudhihirika mpaka wakati wa sasa (5:18).
TUNAJIFUNZA NINI.
1. Msamaha wa Dhambi.
Kama tulivyosema katika ufafanuzi kwamba ni vigumu kujua kwa hakika kwamba makundi haya aliyoyataja mwandishi ni makundi ya umri au ukuaji kiroho au ni mbinu tu ya lugha lakini mwandishi alikusudia kila mwamini, hii ni kwa sababu mambo mwandishi anayoyataja kwenye makundi husika yanawahusu waamini wote. Msamaha wa dhambi kupitia Yesu ni jambo muhimu kwa kila mwamini kulijua na kuliamini pasipo shaka. Kila aliyemwamini Yesu anatakiwa kuwa imara katika kuamini kwamba yeye amesamehewa dhambi zake kupitia jina la Yesu. Kama huwa unapata mashaka kwa habari ya kusamehewa basi ujumbe huu ni wako kila wakati mashaka yanapokujia.
2. Kumjua Yeye tangu mwanzo.
Mwandishi anasema wakina Baba wamemjua yeye tangu mwanzo sifa ambayo tumesema inaweza kuashiria kwamba kundi hili linawahusu watu ambao muda umepita toka walipoamini. Na kujua kwa mwandishi sio kuwa na kumbukumbu za kichwani bali kujua kwa Yohana kunahusisha kuhusiana kwa karibu. Katika kizazi chetu kuna msisitizo mkubwa wa kujua jambo kwa namna ya kuwa na kumbukumbu za kichwani lakini maneno haya yatupe hamasa sisi ambao tumekuwa na muda tangu tumeamini kwamba tuna uhusiano wa karibu na Mungu kwa kumpa muda mwingi yeye katika kuzungumza naye na kwa kutii yale anayotuambia.
3. Ushindi dhidi ya yule mwovu.
Yohana anawaambia vijana wamemshinda yule mwovu na kama ambavyo tumefafanua katika ufafanuzi kwamba ushindi huu Yohana anaozumgumza ulikwisha tokea na matokeo yake yanaendelea sasa. Ushindi ulitokea wakati tunaweka Imani yetu kwa sasa na tokea hapo sisi ni washindi. Kwa sababu ushindi ulikwisha kutokea hivyo mwamini hapaswi kuogopa chochote wala kushindana na chochote kana kwamba kina uwezo wa kupindua ushindi wetu. Mara nyingi waamini wameingia kwenye hofu, mashaka na wasiwasi kwa kuwa hawajajua kwamba wao ni washindi tayali, Hivyo ikiwa wewe ni mwamini jua basi wewe ni mshindi na ushindi huo ulionao una matokeo yanayodumu.
1 Yohana 2:15-17
2.15 Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.
2.16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.
2.17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.
Mpangilio wa mfululizo wa Mawazo wa mwandishi.
2:15 Mwandishi anatoa ujumla wa Hoja yake “Msiipende dunia wala mambo yaliyomo katika dunia”
2:16 Mwandishi anataja mambo yaliyokatika dunia.
2:17 Mwandishi anataja sifa ya dunia na mambo yake.
UFAFANUZI-MSIIPENDE DUNIA.
Baada ya kutaja sababu za kuandika, mwandishi anarudi kwenye ujumbe tena. Mwandishi ananza kwa kutoa amri ambayo ndio hoja yake ya msingi kwamba “msiipende dunia, wala mambo yaliyo katika dunia” (2:15a). Dunia hapa inamaanisha uumbaji ambao haujakombolewa ambao mfumo wake wa maisha uko chini ya yule mwovu na uko kinyume na Mungu (Tazama 4:3-5; 5:19). Baada ya amri hiyo mwandishi anatoa sababu, sababu ya kwanza, Mtu hawezi kuwa na upendo kwa dunia na kwa Baba, anayeipenda dunia ni dhahiri kumpenda Baba hakumo ndani yake (2:15b). Hii ndio maana kutokuipenda dunia sio pendekezo bali ni amri. Sababu ya Pili, Kila kilichomo duniani yaani tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima vyatokana na dunia, havitokani na Baba (2:16). Waamini hawatakiwi kuvipenda vitu visivyotokana na Baba. Sababu ya Mwisho, dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele (2:17). Dunia inapita maana yake imeshaanza kupita na iko kwenyee mchakato wa kupita kwa sababu nuru imekwisha kunga’aa yaani Yesu amekwisha kuja (Tazama 2:8). Yeye afanye mapenzi ya Mungu katika muktadha huu ni yule asiyeipenda dunia.
Tamaa ya Mwili.
Neno lililotafsiriwa mwili ni neno Sarx (Kiyunani) lina maana nyingi kutokana na mahali lilipotumika. Kati ya maana nyingi moja, Mwili ni hali ya ndani ya mwanadamu iliyo na Lengo la kumuasi Mungu na Pili, ni Mwili wa nyama wa mwanadamu. Maana zote mbili zinaweza kubeba mwandishi anachotaka kutujulisha lakini hasa anachokisema ni ile hali ya ndani ya mwanadamu iliyo na Lengo la kumuasi Mungu.
Tamaa ya Macho.
Tamaa ya Macho ni hali ya kutaka kuwa na vitu tunavyoviona kwa namna yeyote iliyopo. Huu ni ushawishi mwanadamu anaoupata kwa kutazama na hivyo kupelekea kutaka vitu hivyo kwa gharama yeyote
Kiburi cha Uzima.
Neno lililotafsiriwa Uzima ni neno Bios (Kiyunani) ambalo lina maana ya Uzima, maisha, mali au riziki. Neno hili pia Mwandishi amelitumia katika mstari wa 7 sura ya 3 akisema “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia (Biov)…….”. Kwa hiyo kiburi hiki kinachoitwa cha Uzima ni hali ya kujiona kuwa katika hadhi ya juu inayotokana na kuwa na mali za dunia.
TUNAJIFUNZA NINI
1. Tusiipende dunia.
Kama tulivyofunza, dunia hapa mwandishi hamaanishi uumbaji wa Mungu wa mbingu na Nchi (Ardhi na anga) bali ni uumbaji wa Mungu ulioathiriwa na anguko na hauja kombolewa. Mfumo huu wa dunia ulioathiriwa na shetani ni wanadamu wanaouendeleza sasa. Roho wa Mungu kupitia mwandishi anatutaka tusiipende dunia kwa kuwa hatuwezi kuchanganya upendo wa kupenda Mungu na wakati huo huo tukampemda Mungu. Dunia ina mambo yake ambayo kwa hali ya mwili ambao haujakombolewa ni mambo mazuri na raha lakini hayo ni machukizo kwa Baba mfano wa mambo hayo ni kama kujipatia mali kwa dhuruma, wizi, utapeli, wivu, husuda, mashindano, chuki na uadui. Mambo haya yote Mungu anataka waamini tusiwe sehemu yake. Moja ya majaribu ya Yesu ambayo shetani aliyatumia ni kumuonyesha Yesu milk izote za ulimwengu na Shetania akaahidi kwamba atampa Yesu ikiwa tu Yesu atakubali kumsujudia, lakini Yesu akakataa, Hii ni njia moja wapo shetani anaitumia kutushawishi waamini kuingia na kuishi kwenye mfumo wa dunia. Huwa anatuonyesha Fahari ya dunia na mambo yake yaani anatuonyesha uzuri, matokeo makubwa pasipo taabu yeyote, majibu ya haraka, raha tutakayopata na mengineyo lakini maandiko yanatutaka kusipende vitu hivyo vya dunia hata kama vinavutia kwa kiasi gani.
2. Dunia inapita.
Moja ya sababu ambayo inatakiwa kututia nguvu kila tunapofanya maamuzi ya kuikataa dunia ni kujua kwamba dunia haitadumu. Uzuri wote shetani anaotuonyesha, raha yote inayoahidiwa na shetani na kila kitu ndani ya uumbaji huu ambao haujakombolewa kina mwisho na hakitaonekana tena katika uumbaji ujao. Jambo hili litutie moyo hata tunapopata shida wakati wa kuikataa dunia na mabo yake, tujue kila kinachotokea kinapita ila sisi tukidumu katika mapenzi ya Baba tutadumu milele pamoja na yeye.
1 Yohana 2:18-27
2.18 Watoto, niwakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa niwakati wa mwisho.
2.19 Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.
2.20 Nanyi mmepakwa mafutana Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote.
2.21 Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana uongo wo wote utokao katika hiyo kweli.
2.22 Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana.
2.23 Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia.
2.24 Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba.
2.25 Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.
2.26 Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza.
2.27 Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.
Mpangilio wa mfululizo wa mawazo ya mwandishi.
Sehemu hii tunaweza kuigawa katika makundi mawili
Sehemu ya Kwanza. Mwandishi anatofautisha “Wapinga kristo” na “wanaoijua kweli”
2:18 –Kauli inayojumuisha hoja yake. (Wapinga kristo)
2:19-Maelezo kuhusu wapinga kristo (Walitoka katikati ya Waamini)
2:20-21 Wapokeaji wa Ujumbe (Wanaijua kweli)
2:22-23 Wapinga Kristo (Namna ya kuwatambua)
Sehemu ya Pili. Mwandishi anawasisitiza “wanaoijua kweli” kubaki ndani ya kweli.
2:24-25 Wapoakeaji wa Ujumbe (Wakae na kweli walioisikia tangu mwanzo)
2:26-Lengo la kuandika mambo haya
2:27 Wapokeaji wa Ujumbe (Mafuta yanakaa ndani yenu).
UFAFANUZI-WAPINGA KRISTO I.
Mwandishi sasa anaeleza kwa uwazi kwa kwamba aliandika barua hii kupingana na kundi la waalimu wa uongo (ambao yeye hapa anawaita wapinga kristo na katika 4:1-6 anawaita manabii wa Uongo) ambao walikuwa wanataka kuwapotosha wapokeaji wa kitabu hiki. Tangu mwanzo alianza kwa kutaja sifa za maisha yao (Kiri zao zinazopingana na vile wanavyoishi, 2:3-11) lakini sasa anataja fundisho lao (Yesu si Kristo) na anawataka wapokeaji wa kitabu hiki wawatambue na kuwasisitiza wao kubaki ndani ya kweli (Yesu ni Kristo). Mwandishi anaanza na kutaja hoja yake ya msingi kwamba wapinga kristo wapo na kwa sababu wapo basi huu ni wakati wa mwisho (2:18). Mwandishi ameambatanisha wakati wa mwisho na uwepo wa wapinga kristo kwa sababu anajua wapokeaji wa ujumbe wake walifundishwa kwamba wakati wa mwisho Mpinga kristo atakuja[11]. Mwandishi hakatai ukweli kwamba mpinga kristo (Mtu mmoja) anakuja bali anataka kuwaonyesha kwamba hata sasa wanaompinga kristo wapo tayali. Mwandishi anawataja wapinga kristo hawa kwamba walikuwa miongoni mwa waamini lakini hawakuwa waamini wa kweli na mwishowe wakatoka katika kundi la waamini. Kwa nini mwandishi anasema hawakuwa waamini? Sio kwa sababu nyingine isipokuwa kwa sababu hawakuendelea kuwa sehemu ya waamini. Na kule kutoka kwao ni kufunuliwa kwao kunakoonyesha kwamba hawakuwa sehemu ya waamini (2:19). Tofauti na wapinga kristo wapokeaji wa ujumbe huu mwandishi anasema wao wamepakwa mafuta na yeye aliye mtakatifu, hivyo wanajua yote (2:20). Kupakwa mafuta ni kupokea Roho mtakatifu kutoka kwa aliye mtakatifu. Roho mtakatifu Yesu aliahidi atawafundisha kweli yote wanafunzi wake na kuwakumbusha yale yeye aliwafundisha (Yohana 15:26; 16:7, 12-15), hii ndio maana Yohana katika maandishi yake anamuita Roho mtakatifu Roho wa kweli (Yohana 15:26; 16:13 1 Yohana 4:6) akionyesha Roho mtakatifu anaambatana na kweli. Hivyo kwa kuwa wapokeaji wa Ujumbe huu walipokea Roho mtakatifu Mwandishi anajua wanaijua kweli, ndio maana anasema hakuwaandikia kwa sababu hawaijui kweli bali kwa sababu wanaijua kweli na hiyo kweli haina Uongo ndani yake (2:21). Mwandishi anarudi tena kuwaelezea wapinga kristo, sasa anataja sifa ya kuwatambua. Wapinga kristo ni wale wanaokana kwamba Yesu ni kristo (2:22)[12].Kukana kwamba Yesu ni kristo ni sawa kabisa na kumkana Baba kwa sababu kila anayemkana Mwana hanaye Baba na amkiriye mwana (Yesu ni kristo) anaye Baba (2:23). Kweli katika muktadha huu inahusiana na Fundisho la kuhusu Ukristo wa Yesu (Umasihi wa Yesu) japo kweli anaweza kuwa na maana pana zaidi ya hiyo.
Mwandishi sasa anahamia katika kuwasisitiza wapokeaji wa ujumbe huu kwamba wabaki ndani ya kweli, kweli ikiwa ni kwamba Yesu ni kristo. Mwandishi anawasisitiza lile walilosikia Tangu mwanzo likae ndani yao. Kwa sababu wanajua kweli anachosisitiza ni kuendelea kukaa ndani yake. Na mwandishi anasema ikiwa hilo walilolisikia tangu mwanzo (Kwamba Yesu ni Kristo) linakaa ndani yao basi wataendelea kukaa ndani ya Mwana na ndani ya Baba (2:24).Lile walilosikia Tangu mwanzo ina maanisha ujumbe wa injili waliousikia tangu wakati wanaamini ambao unatambua kwamba Yesu ni Kristo. Kwa kuwa mwandishi anawasisitiza kuendelea kukaa katika kweli walioisikia basi anasema Mungu amehaidi Uzima wa Milele kwa wale watakaoendelea kukaa katika kweli (2:25).[13]
Mwandishi anasema aliwaandikia haya (2:18-27) kwa sababu kuna watu wanataka kuwapoteza (2:26), wanawafundisha kwamba Yesu sio kristo. Hawa watu wanaotaka kuwapoteza ndio wapinga Kristo. Mwandishi anamalizia sehemu hii kwa kusema kwa sababu mafuta waliyoyapokea yanakaa ndani yao hawana haja ya mtu kuwafundisha. Lakini kama mafuta yanavyowafundisha sasa na yalivyowafundisha hapo nyuma anawataka wakae ndani yake (2:27). Mwandishi haipingi wapokeaji wa ujumbe huu kufundishwa au kufundishana mambo ya Imani yao bali anapinga kufundishwa na wapinga kristo ambao amewataja sifa zao ili waweze kuwatambua (2:22), lakini pia kwa sababu wapokeaji wanajua kweli (Yesu ni kristo) hawahitaji mtu kuwafundisha tena jambo hilo (Yesu ni Kristo) ndio maana hata yeye hajaandika kuwafundisha bali kuwasisitiza kubaki kwenye kweli (2:21).
TUNAJIFUNZA NINI.
1. Uwepo wa wapinga Kristo.
Kama mwandishi alivyowafundisha wapokeaji wa awali wa ujumbe wake hivyo hivyo Roho wa Mungu anatufundisha na sisi kwamba Roho yeyote inayepinga ukweli kwamba Yesu ni Kristo/masihi[14], huyo mpinga Kristo. Roho yeyote inayokataa kwamba Yesu sio mpakwa mafuta wa Mungu hiyo ni Roho ya Mpinga Kristo. Moja ya mfano wa wazi kabisa ya aina ya watu wanaokataa kwamba Yesu ni Kristo ni wayahudi. Wayahudi wanaamini mwamba Yesu sio Kristo na ndio sababu bado wanasubiri ujio wa Kristo mwingine. Sasa Pamoja na kuwa mfano wa wazi, mtu yeyote ambaye anakataa kwamba Yesu ndiye masihi/Kristo huyo ni mpinga Kristo. Ni muhimu kujua hilo ili usije ukadanganyika.
2. Kubaki katika Kweli.
Kwa kuwa Imani ni jambo la muendelezo na sio tukio la mara moja na Imani ndio inaleta wokovu ni muhimu kuhakikisha unabaki katika kweli ya Neno la Mungu na sio kubebwa na upepo wa kila aina ya mafundisho. Tangu karne ya kwanza kulikuwa na waalimu na manabii wa uongo na jambo hilo halijabadilika hivyo ni muhimu kwa waamini kuwa tabia ya kuchunguza mafundisho na kujihakikishia kama kweli yanaendana na kila hasa maandiko yanachofundisha. Kwa kufanya hivyo, itatusaidia kubaki kwenye kweli ya Mungu.
3. Roho Mtakatifu anafundisha.
Kwa waamini wengi wanaposikia “Roho mtakatifu kufundisha” huwa wana pata maana ya kwamba Roho mtakatifu kutoa ufunuo wa mambo mapya ambayo watu wengine hawayajui. Lakini hapa tunajifunza Roho mtakatifu, Roho wa kweli huwafundisha waamini mambo yale yale aliyowafundisha tangu mwanzo, kwa hiyo Roho mtakatifu haimaanishi tu kupata mambo mapya kutoka kwa Roho mtakatifu bali huusisha kupata kujifunza zaidi katika kile ambacho ameshakufundisha tangu mwanzo.
Kwa upande mwingine, waamini wengine wakisikia Kufundishwa na Roho mtakatifu huwa hudhani ni kupata ujuzi wa jambo bila kusaidiawa na mtu mwingine yeyote, ikitokea wanasaidiwa na mtu mwingine hudhani huyo sio Roho mtakatifu, lakini ukweli ni kwamba Roho mtakatifu hutumia watu wake kufundisha watu wake. Ukipata mwamini mwingine anakufundisha jambo kaa jifunze kwa kuwa Roho mtakatifu yuko kazini kukufundisha.
1 Yohana 2:28-3:10
2.28 Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake.
2.29 Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye.
3.1 Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.
3.2 Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.
3.3 Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu.
3.4 Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.
3.5 Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake.
3.6 Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua.
3.7 Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki;
3.8 atendaye dhambini wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.
3.9 Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu.
3.10 Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.
Mpangilio wa mfululizo wa mawazo ya mwandishi.
2:28-29 Kuzaliwa na Mungu na kuishi katika kutenda haki.
3:1-3 Watoto wa Mungu kwa sababu ya Upendo wa Mungu
3:4-6 Watoto wa Mungu hawatendi dhambi
3:7-9 Utofauti wa Watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi
3:10 Hitimisho (Utambuzi wa watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi)
UFAFANUZI.-WANA WA MUNGU.
Mwandishi katika sehemu hii inazungumzia mambo mawili makubwa moja likiwa ni kuzaliwa na Mungu na la pili likiwa ni kutenda haki, kinyume na kutenda dhambi. Mwandishi anasema kwa ujumla kwamba waliozaliwa na Mungu ambao ndio watoto wa Mungu wao wanatenda haki (Hawatendi dhambi) na wale wasiozaliwa na Mungu ambao ni watoto wa Ibilisi wanatenda dhambi (hawatendi haki). Hivyo kupitia maelezo hayo watoto wa Mungu ni Dhahiri na watoto wa Ibilisi ni Dhahiri, pia maana yake watoto wa Mungu wanatambulika na watoto wa Ibilisi wanatambulika.
Ni vigumu kuamua kwa uhakika kabisa kwamba mstari wa 28 ni hitimisho la sehemu ya juu (2:18-27) au ni utangulizi wa sehemu hii (2:28-3:10), hivyo sisi tunaona ni kiungo cha sehemu iliyopita na sehemu hii. Mwandishi anawasisitiza wapokeaji wa ujumbe wake kuendelea kukaa ndani yake (Yesu) ili atakapofunuliwa wawe na ujasiri, wasiaibike mbele zake katika kuja kwake (2:28). Mwandishi anatumia lugha mbili tofauti kuelezea kitu kile kile “atakapofunuliwa wawe na ujasiri” ni sawa na kusema “wasiaibike mbele zake katika kuja kwake”. Hivyo kuja kwa Yesu ndio kufunuliwa kwake. Hivyo wakiendelea kukaa ndani yake yaani wasipodanganywa (2:26, 3:7) basi watakuwa na ujasiri na hawataibika siku ya kuja kwa Yesu. Kudanganywa huku ni kwa kuacha kuamini kwamba Yesu ni Kristo (2:18-17 hasa mstari 26) na kutoendelea kutenda haki kama yeye alivyo na haki (2:29-3:10 hasa 3:7). Sehemu iliyopita (2:18-27) aliwasisitiza kubaki kwenye Fundisho na sehemu hii ya pili atawasisitiza kutenda haki (2:29-3:10). Haya maeneo mawili wapinga kristo walikuwa wanayapotoa ndio maana mwandishi anataka wasidandanywe (2:26, 3:7). Mwandishi anawaambia wapokeaji wa ujumbe wake kwa kuwa wanajua yeye ni mwenye haki wajue pia kila atendaye haki amezaliwa na yeye (2:29). Yeye ni Mungu kwa sababu kila mahali Yohana anapozungumza kuhusu Kuzaa, Mungu ndiye anayezaa (3:9; 4:7; 5:1, 4, 18). Hivyo mwandishi anasema kwa kuwa wanajua Mungu ni mwenye haki kila atendaye haki amezaliwa na Mungu. Kabla ya kuendelea kuelezea kwa urefu jambo hili la kuhusu waliozaliwa na Mungu kutenda haki mwandishi anaelezea kuhusu Upendo walioupata hawa waliozaliwa na Mungu (3:1-3). Baada ya kuelezea Upendo wa Mungu kwa hawa waliozaliwa na Mungu ataendelea na kuelezea kuhusu kutenda haki kwa waliozaliwa na Mungu (3:4-10).
Kwa kuwa wapokeaji wa Ujumbe huu mwandishi anajua wamezaliwa na Mungu anawaambia tazameni (Kuangalia kitu cha thamani kwa mshangao) upendo ambao Baba (Mungu) amewapa, upendo huo umewapa wao (pamoja na mwandishi) kuitwa Wana wa Mungu na hivyo ndivyo walivyo. Na kwa sababu wao ni wana wa Mungu ulimwengu hauwatambui kwa sababu haukumtambua yeye (3:1). Yeye hapa ni Yesu kwa kuwa Yohana anafundisha kwamba Mungu alikuja katika mwili (Yesu) hapa duniani na dunia haikumtambua (Yohana 1:10). Yohana 1 hiyo hiyo pia mstari wa 12 na 13 unatupa picha ya njia ya kufanyika kuwa mwana wa Mungu, ambayo ni kumpokea kwa kuliamini Jina lake. Mwandishi anathibitisha kwamba sasa tu wana wa Mungu lakini haijadhihirishwa bado vile tutakavyokuwa, yaani bado haijawekwa wazi kwetu jinsi tutakavyokuwa hapo mbele. Lakini mwandishi na wapokeaji wa ujumbe wake wote wanajua kwamba Yesu atakaporudi tena mara ya Pili (Atakapodhihirishwa) watafanana naye kwa maana watamuona kama alivyo (3:2). Mwandishi anamaanisha sasa tu wana wa Mungu lakini bado tunasubiri kubadilishwa miili yetu ya nyama ili ifanane na mwili wa Yesu wa Utukufu (Tazama Wafilipi 3:21) na hili jambo litatokea atakaporudi mara ya pili. Kufanana naye ni tukio linalosubiriwa, hivyo kufanana naye ni tumaini (kitu kinachotarajiwa). Kila mwenye matumaini ya kufanana naye hujitakasa kama yeye alivyo mtakatifu (3:3). Wenye matumaini haya ni wale tu ambao sasa ni wana wa Mungu (3:2), hivyo hawa wana wa Mungu ndio wanatakiwa kujitakasa kama yeye alivyo mtakatifu. Kujitakasa katika muktdha huu ni kuacha kutenda dhambi na kutenda haki (2:29 na 3:4-10). Mwandishi anarudi katika mada aliyoiacha njiani katika 2:29, mada mbayo inayowataka wana wa Mungu kutenda haki sawa na msisitizo wa 3:3. Lengo la sehemu hii ni kuwataka wana wa Mungu (Wapokeaji wa ujumbe) kutenda haki na kuwaonyesha kwamba wana wa Mungu ni dhahiri kama walivyo wana wa Ibilisi.
Mwandishi anawaambia kwamba kila anayetenda dhambi anafanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi (3:4). Uasi ni kuwa mpinzani/kinyume na katika Muktadha huu ni kuwa mpinzani/kinyume na Mungu. Kwa kuwa wapokeaji wanajua kwamba Yesu alikuja duniani katika mwili (1:2) ili aziondoe dhambi pamoja na kwamba ndani yake hakuna dhambi (3:5), basi akaaye ndani yake (Yesu) hatendi dhambi (3:6a). Anayetenda dhambi hakumuona yeye wala hakumtambua (3:6b). Kauli hii ya kutokutenda dhambi kwa wakaao ndani yake Yesu inaonekana kukinzana na kile mwandishi alichokisema mwanzoni kwamba “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe…” (1:8) na msisitizo wake wa kuwataka wapokeaji (pamoja na mwandishi) wawe wana ungama dhambi unakosa maana pia (1:9). Na mwandishi pia alionyesha huko nyuma kwamba anakubari kwamba wapokeaji wake waliozaliwa na Mungu wanaweza kutenda dhambi na wakitenda wanae mwombezi kwa Mungu, aitwaye Yesu (2:1). Sasa namna ambayo inaweza kutusaidia kuelewa Ujumbe huu ni kuangalia matumizi ya nyakati katika vitenzi alivyovitumia mwandishi katika kuwapa wapokeaji wake ujumbe huu. Vitenzi vilivyotumika katika kueleza “hatendi dhambi” na “atendaye dhambi” (3:6) vinatumia nyakati ya mazoea (Nyakati endelevu), Hivyo tunaweza kusema mwandishi anasema Kila akaaye ndani yake haendelei kutenda dhambi na kila anayeendelea kutenda dhambi hakumuona yeye wala hakumtambua. Kwa lugha rahisi zaidi kila akaaye ndani yake haishi maisha ya dhambi na anayeishi maisha ya dhambi hakumuona yeye wala hakumtambua.
Mwandishi anaendelea kusema kwa wapokeaji wa ujumbe wake kwamba mtu asiwadanganye atendaye haki (sio tendo moja bali mfumo wa maisha) huyo mtu ana haki kama yeye (Yesu) alivyo na Haki (3:7). Kama tulivyoanisha pale juu kwamba mstari wa 7 mpaka 9 unaonyesha tofauti ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi, hivyo mwandishi anataja sifa ya watoto wa ibilisi tofauti ya sifa ya watoto wa Mungu aliyoitaja katika mstari wa 7. Mwandishi anasema watoto wa ibilisi ndio wale watendao dhambi (wanaendelea kuishi maisha ya dhambi) kwa kuwa Ibilisi yeye hutenda dhambi tangu Mwanzo (3:8a). Ibilisi alianza kutenda dhambi tangu mwanzo na mpaka sasa anatenda dhambi, bado mwandishi anazungumza kwa kutumia lugha ya nyakati ya mazoea (Muendelezo). Kwa kuwa kazi ya shetani imekuwa kuwafanya wanadamu kuishi maisha ya dhambi kama yeye, Mwana wa Mungu alifanyika mwili akaja duniani (alidhihirishwa) ili kuvunja hiyo kazi (3:8b). Na kila ambaye kazi hii ya Mwana wa Mungu imemfikia basi hawezi kuendelea kuishi maisha ya dhambi. Hii ni kwa sababu uzao/mbegu ya Mungu inakaa ndani yake na pia hawezi kuendela kuishi maisha ya dhambi (kutenda dhambi) kwa kuwa amezaliwa kutokana na Mungu (3:9). Uzao/Mbegu ya Mungu iliyondani ya waamini ni Roho mtakatifu (2:27) au neno la Mungu lile walilolisikia (2:24) au vyote kwa pamoja. Mwisho mwandishi anaweka hitimisho kwamba watoto wa Mungu wanatambulika (dhahiri) na watoto wa Ibilisi pia wanatambulika. Mtu ambaye hatendi haki (haishi maisha ya haki) huyo hatokani na Mungu na pia yule asiyempenda ndugu yake hatokani na Mungu (3:10). Kuhusu kupenda mwandishi ametaja tu hapa katika hitimisho ili kutukaribisha kwenye ujumbe wake unaofuata unaohusu kupendana (3:11-24). Kwa ujumla sifa kuu za utambuzi kati ya Watoto wa Mungu na wa iblisi ni; kutenda haki na kuwa na Upendo. Watoto wa Ibilisi hawatendi haki na hawana upendo na watoto wa Mungu ni kinyume cha watoto wa Ibilisi, wanatenda haki na wanapenda.
TUNAJIFUNZA NINI
1. Kuishi maisha ya Haki.
Msisitizo mkubwa wa Mwandishi katika ay ani kuwataka waamini kuishi Maisha ya haki katika Baba yao alivyo mwenye haki. Ni wajibu wetu sisi kama waamini kuishi Maisha yanayomfunua Baba yetu. Kuishi kwa haki ni eneo pana lakini nitaongelea tu kwenye kuwafanyia watu vile anavyotakiwa. Sisi kama waamini tunatakiwa kufanyia watu sawa na inavyostahiri katika maeneo mbalimbali ya Maisha yetu. Tunapotafuta fedha na mali tuwafanyie watu vile inavyostahiri (kutenda haki), tunapotoa huduma tutoe kama inavyostahiri bila kupendelea wala kuonea watu, tunapohusiana na watu tuhusiane nao vile inavyostahiri na kadhalika.
2. Upendo wa Mungu.
Kila anayeamini kwamba Yesu ndiye mwokozi wake huyo ni mtoto wa Mungu, lakini kibali hiki cha kufanyika kuwa Watoto wa Mungu kinatokana na Upendo wa Mungu na sio sababu nyingine yeyote. Kwa uweza Mungu alio nao angeweza kufuta uumbaji wote na kuumba tena lakini kwa upendo wake akaamua kuja duniani kufa na kulipa gharama ya ukumbozi na kufanya watu wote wanaoamini kuwa ni Watoto wake. Ujuzi huu utusaidie kutufanya sisi waamini kuwa wanyenyekevu kwa kuwa tunajua tulichopata tumepata kwa upendo tu wa Mungu sio jambo ambalo tumelifanyia kazi au tunalistahiri.
3. Kutofautisha Wana wa Mungu na Wana wa Ibilisi.
Kwa ujumla kwenye bara letu la Afrika kuna watu wengi sana wanaojitambulisha kuwa ni Watoto wa Mungu au waabudu Mungu lakini cha kushangaza pia ni kwamba pia katika jamii hii hii ya watu wanaojitambulisha kuwa ni Watoto wa Mungu kuna uovu mkubwa uliokithiri. Kwa mfano ukiingia kwenye huduma za jamii utakutana na rushwa karibu kila kona kana kwamba huko kote hakuna wanaojitambulisha kuwa ni Watoto wa Mungu. Ukiacha hilo, ukiangalia uongo unaoenezwa/kuzungumza katika mataifa yetu ni mkubwa kiasi cha kudhani kwamba hakuna watu wanaojitambulisha kama waabudu Mungu.Mifano ni mingi lakini hayo ni machache tu. Sasa tunajifunza kupitia kitabu hiki kwamba utambuzi sahihi wa Watoto wa Mungu na Watoto wa Ibilisi uko kwenye namna gani watu wanaishi na sio vile wanavyojitambulisha. Mwandishi anasema watendao haki ni wana wa Mungu na wako Dhahiri na wasiotenda haki, wan awa Ibilisi pia wako Dhahiri kupitia Maisha yao. Hivyo ni wito wa Roho wa Mungu kwamba tuishi jinsi tulivyo, kwa kuwa sisi ni Watoto wa Mungu tuishi kwa haki na tusiishi kwama Watoto wa Ibilisi.
Lakini pia tunajifunza namna tunavyoweza kutambuana. Mtu hata akijitambulisha kwa lugha nzuri kiasi gani ya kwamba yeye ni mtoto wa Mungu ni vizuri kuangalia mwenendo wake ili kujua kama ni kweli anachoikiri au ni mwongo. Hili litatusaidia waamini ili tusitapeliwe na watu anaojiingiza kwa siri katika makusanyiko yetu. Vijana wanaotaka kuoa au kuolewa wasisikilize ujambulisho wa maneno bali watazame mwenendo ili kujua kwa hakika nani ni nani. Wanaotaka kufanya ushirika katika fedha na mali wasisikilize utambulisho wa mtu wa maneno bali watazame mwenendo wa watu hao ili kujua kama hao kweli ni Watoto wa Mungu au ni wa Ibilisi.
4. Tumaini letu.
Moja ya jambo la muhimu kwa waamini kujua ni kwamba tunalo tumaini, kwamba Mungu atafanya mambo kuwa sawa pale Kristo Yesu atakaporudi mara ya pili. Miili yetu yenye changamoto itabadilishwa na kufanana na mwili wa Yesu wa utukufu, ule aliokuwa nao baada ya kufufuka. Na uumbaji huu tunaouona Mungu pia ataufanya upya na Maisha kwa ujumla katika umilele wetu yatakuwa mapya. Ujuzi wa jambo hili hutusaidia kufanya bidii ya kumuishia Mungu pale tunapojisika kuchoka kutokana na changamoto za ulimwengu huu. Kujua kile unachokitumainia mara nyingi humfanya mwanadamu asikate tamaa katika kile anachokifanya.
1 Yohana 3:11-24
3.11 Maana, hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi;
3.12 si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.
3.13 Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia.
3.14 Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapendandugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti.
3.15 Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake.
3.16 Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.
3.17 Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?
3.18 Watoto wadogo, tusipendekwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli.
3.19 Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake,
3.20 ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote.
3.21 Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu;
3.22 na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.
3.23 Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, nakupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri.
3.24 Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.
Mpangilio wa mfululizo wa mawazo ya mwandishi.
3:11-18 Tupendane sisi kwa sisi
3:19-22 Ujasiri tunaoupata katika kupendana
3:23-24 Hitimisho.
UFAFANUZI-TUPENDANE I.
Mwandishi katika kumalizia sehemu ya juu (2:28-3:10) ambayo alikuwa anaonyesha utofauti wa wana wa Mungu na wana wa Ibilisi alimalizia kwa kuonyesha kwamba “yeye asiyempenda ndugu yake” hatokani na Mungu, maana yake huyo ni mtoto wa Ibilisi. Hivyo sehemu hii (3:11-24) anaandika kuwasisitiza wapokeaji wa ujumbe wake kupendana wao kwa wao kwa kuwa hiyo ndio amri ya Kristo. Mwandishi anaanza kueleza kuhusu kupendana kama alivyoanza kueleza Habari ya kwamba Mungu ni Nuru (1:5). Mwandishi alisema “Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake na kuihubiri kwenu….” (1:5) na sasa anasema “hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo” (3:11). Habari hii inayosema Mungu ni Nuru mwandishi na wenzie (Mitume) waliisikia kwa Yesu (1:5) na Habari ya kupendana pia waliisikia kwa Yesu (Tazama Yohana 15:17). Hii ndio maana wasomi wengine wa Biblia wamegawanya kitabu hiki katika mpangilio wa sehemu kuu mbili yaani 1:5-3:10 ambayo inaongelea sana Kwamba Mungu ni Nuru na wana wa Mungu wanatakiwa kuenenda nuruni na 3:11-5:12 ambayo inaongelea kwamba Mungu ni Upendo na hivyo watoto wake wanatakiwa kupendana. Ni kweli kwamba Mambo haya mawili ndio habari kuu ya Yohana katika kitabu hiki japo hajayaongelea kwa mapangilio wa kuyatenganisha moja kwa moja.
Mwandishi anawakumbusha ujumbe ambao tangu mwanzo waliusikia ambao unahusu kupendana wao kwa wao (3:11). “Sisi kwa sisi” mwandishi anamaanisha waamini. Kinyume cha upendo kwa mwandishi ni chuki, ndio maana anawapa mfano wa chuki ambao anawataka wapokeaji wa ujumbe wake wasiige. Mfano huu ni wa kaini ambaye alimuua ndugu yake (Mwanzo 4:1-8). Mwandishi anamuita Kaini ni“wa yule mwovu” kwa sababu tayali alishasema namna watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi wanavyotambulika (3:7-10 hasa mstari wa 10). Kwa sababu Kaini alikuwa na chuki basi hivyo ni dhahiri alikuwa ni wa yule mwovu. Mwandishi anatoa sababu ya Kaini kumuua ndugu yake: Kaini alimuua ndugu yake kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya na ndugu yake matendo yake yalikuwa ya Haki (3:12). Huu si tu mfano wa chuki bali pia ni mfano wa kuwaonyesha kwamba hata wao watachukiwa na Ulimwengu, kwa sababu Ulimwengu kama Kaini una matendo mabaya na Waamini wana matendo ya haki kama ndugu yake Kaini na watenda mabaya huwachukia mwenye haki. Hii ndio maana mwandishi anasema wasistaajabu/wasishangae ulimwengu ukiwachukia maana ni lazima tu ulimwengu utawachukia[15] (3:13). Mwandishi anawaambia wapokeaji kwamba wao (pamoja na yeye) wanajua kwamba wametoka mautini kuingia uzimani kwa sababu wanawapenda ndugu. Maana yeye asiyependa akaa katika Mauti. Mwandishi anachosema ni kwamba kupendana kunaonyesha kwamba wao ni waamini ambao wana Uzima wa milele (Tazama Yohana 5:24). Kwa lugha nyingine kuamini na kupendana ni vitu visivyoweza kutenganishwa (3:14). Kwa kusisitiza hilo anamalizia kwa kusema yeye amchukiaye ndugu yake ni mwuaji[16], na wao wanajua kwamba kila mwuaji hana Uzima wa milele ndani yake (3:15). Mwuaji ambaye hana Uzima wa Milele ndani yake huutoa uhai wa mwenzake lakini wao wenye Uzima wa Milele mwandishi anawataka wautoe uhai wao kwa ajili ya ndugu, kwa sababu huo ndio Upendo Yesu aliuonyesha (3:16). Yesu alionyesha Upendo kwa kuutoa uhai kwa ajili yao na waamini wanatakiwa kuutoa uhai wao kwa ajili ya ndugu. Mwandishi anatoa mfano halisi wa namna ya kuishi upendo huo Yesu aliouonyesha kwa kutumia swali la balagha[17]. Mwandishi anauliza mtu akiwa na riziki ya dunia na akamuona ndugu yake ana uhitaji, akamzuilia kumpa riziki hiyo ili kukutana na uhitaji wake, Je huyo mtu aliyemzuilia ndugu yake riziki ya dunia Upendo wa Mungu unakaa ndani yake? Jibu ni hapana kwa kuwa hili ni swali la balagha, upendo wa Mungu haukai ndani yake (3:17). Mwandishi anamalizia kwa kusisitiza kwamba wasipende kwa neno au kwa kuongea (Ulimi) bali Upendo uwe katika tendo na kweli (3:18). Mfano wa kupenda kwa tendo umeshaonyeshwa katika swali la balagha (3:17). Msisitizo wa tendo kwa mwandishi haukatazi kuongea lugha ya upendo bali unasisitiza Upendo kutoishia kwenye maneno. Upendo pia mwandishi anasisitiza uwe katika kweli yaani uendane na fundisho na mfano wa Kristo.
Mwandishi anahamia sasa kuonyesha kwamba Upendo/kupendana katika tendo na kweli kutawapa kujua kwamba wao wako katika kweli yaani wako katika upande wenye kweli tofauti na upande wa watoto wa Ibilisi (Upande wa wapinga Kristo, 2:9-11). Kwa kupendana katika tendo na kweli mwandishi na wapokeaji wa ujumbe wake watapata kufahamu kwamba wako katika upande wa kweli, na hivyo wataituliza mioyo yao mbele zake/mbele za Mungu (3:19) ikiwa mioyo yao inawahukumu .Wataituliza mioyo yao kwa Mungu kwa sababu Mungu ni mkuu kuliko mioyo yao naye anajua yote (3:20). Mwandishi anachosema ni kwamba upendo katika tendo na kweli utawapa waamini kufahamu kwamba wako katika upande wa kweli. Na kwa kuwa wako upande wa kweli/upande wa watoto wa Mungu basi wataituliza mioyo yao kwa Mungu ikiwa mioyo yao itawahukumu. Pale mwamini atakapohukumiwa na Moyo wake atautuliza moyo wake kwa Mungu kwa kuwa Mungu ni mkuu kuliko moyo wake na anajua yote. Mwamini anapohukumiwa na Moyo wake asiunyamazishe moyo bali autulize moyo kwa Mungu, hili linafanana na kuungama (1:8-9).
Mwandishi anageukia upande wa Pili sasa, upande ambao mioyo yao haiwahukumu. Upande huo mwandishi anasema basi hapo wana ujasiri mbele za Mungu (3:21) na hivyo lolote watakaloliomba watalipokea kwake. Ujasiri mbele za Mungu na kupokea kwake mwandishi amekuambatanisha na kigezo, kigezo kikiwa ni kushika amri zake na kuyatenda yapendazayo machoni pake (3:22). Moja ya amri zake mwandishi anataja ni kuliamini jina la mwana wake Yesu kristo na kupendana wao kwa wao kama alivyoamuru (3:23). Mwandishi anahitimisha sawa na alichokuwa akikizungumza kwamba anayezishika amri zake hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake (3:24a). Na watajuaje kwamba Mungu anakaa ndani yao?, watajua Mungu yuko ndani yao kwa uwepo wa Roho, Mungu aliowapa (3:24b).
TUNAJIFUNZA NINI.
1. Upendo/Kupendana kwa vitendo na kweli.
Moja ya jambo ambalo Yohana analizungumza sana kwenye vitabu vyake ni Upendo katikati ya waamini nah ii ni kwa sababu Mungu mwenyewe ni upendo. Tunapaswa waamini kupendana sisi kwa sisi tena kwa vile tunavyoishi (Kwa matendo). Kunapokuwa na mtu mwenye changamoto katikati yetu basi tuwe tayali kusaidiana kutatua na kunapokuwa na uhitaji katikati yetu basi tuwe tayali kukutana na uhitaji huo. Tusiwe watu wa kuangalia Maisha yetu mwenyewe tu bali tuangaliane sisi kwa sisi. Tupendane kwa kufuata mfano wa Yesu wa kuacha Fahari ya Uungu na kushuka chini ili kututumikia. Tushuke kwenye utofauti tulio nao na kufika kwenye kiwango cha kutumikiana. Tupendane kwa kufuata mfano wa Baba wa kumtoa mwanae wa pekee kwa ajili yetu. Tuwe tayali kulipa gharama katika kutumikiana kama waamini.
Katika kanisa sasa kuna changamoto sana katika jambo hili la muhimu kwa kuwa ubinafsi unasisitizwa kwa maneno, mafundisho na mifumo. Waamini wengi hata kukusanyika wanakusanyika ili wapate vitu wao wanavyovitaka na hawana haja na waamini wengine, hili ni kinyume na tunachojifunza kupitia Yohana. Mungu anataka tutumikiane na sio kila mtu kutafuta kile anachokitaka.
1 Yohana 4 : 1-6
4.1 Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.
4.2 Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu.
4.3 Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.
4.4 Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.
4.5 Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia
4.6 Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.
Mpangilio wa mfululizo wa Mawazo ya Mwandishi.
4:1 Manabii wa Uongo/wapinga kristo wapo sasa
4:2-3 Kuwatambua wapinga Kristo
4: 4-6 Sisi na Ninyi ni wa Mungu wao ni wa dunia.
UFAFANUZI-WAPINGA KRISTO II.
Sehemu hii ni sehemu ya pili kwa mwandishi kuzungumza kuhusu uwepo wa wapinga Kristo ambao sasa mwandishi anawaita manabii wa uongo. Kama alivyofanya mwanzo (2:18-27) aliwatofautisha wapinga Kristo na wanaoijua kweli, hapa pia anawatofautisha wapinga Kristo na Watoto wa Mungu. Mwandishi anatoa tahadhari kwa wapokeaji wa ujumbe wake kwamba wasiamini kila roho. Na sababu ya tahadhali hiyo ni kwamba manabii mwenye roho ya uongo wametokea tayari (4:1). Baada ya tahadhari mwandishi anawapa wapokeaji wa ujumbe wake namna ya kuzijaribu roho. Kwa upande Chanya, kila roho inayokubali kwamba Yesu alikuja (alizaliwa na kuishi) katika mwili wa kibinadamu yatokana na Mungu (4:2). Na kwa upande hasi kila roho isiyokubali kwamba Yesu alikuja katika mwili, hiyo ni roho ya mpinga Kristo ambayo ipo duniani tayari (4:3).Kwa kuwa mwandishi anawajua wapokeaji wa ujumbe wake anajua wanakubali kwamba Yesu alikuja katika mwili, hivyo anawathibitishia kwamba wao wanatokana na Mungu yaani wako upande wa Mungu na wamewashinda manabii wa uongo/wapinga Kristo. Na ushindi wao ni kwa sababu ndani yao kuna aliye mkuu kuliko aliye katika dunia; huko ambako ni eneo la utawala la wapinga Kristo (4:4). Ushindi wao hautafsiriwi kwa kupewa sikio na dunia, kwa kuwa dunia itawapa tu sikio manabii wa uongo/wapinga Kristo kwa kuwa mambo wanayoyanena yanaendana na dunia (4:5). Kinyume na manabii wa uongo, mwandishi na wapokeaji wa ujumbe wake wanatokana na Mungu na yeyote anayemjua Mungu ndiye atakaye wasikia na asiyemjua Mungu hawezi kuwasikia (4:6a). Mwandishi anamaliza aya hii kwa hitimisho kwamba katika hili ndio tunaweza kutambua Roho wa Kweli na roho ya upotevu (4:5b). “Hili” ni mjumuisho wa mambo aliyoyazungumza hapo juu yaani mambo mawili; Moja ukiri wa roho husika juu ya Yesu kuja katika mwili na Pili, ni aina gani ya watu wanaosikia ujumbe wa hiyo roho. Hivyo mwandishi anasema kwamba kupitia ukiri wa roho husika kuhusu ujio wa Yesu katika mwili na kupitia aina ya watu wanaosikia hiyo roho (Watu wa dunia au wanaomjua Mungu) wapokeaji wake wanaweza kutambua kati ya Roho ya kweli na roho ya upotevu.
TUNAJIFUNZA NINI.
1. Uwepo wa wapinga Kristo.
Kwa tafsiri ya Mwandishi ya neno Mpinga Kristo, ni dhahiri hata leo kanisa lina changamoto ya uwepo wa wapinga kristo. Kwa kipindi cha mwandishi wapinga kristo walifundisha kwamba Kristo hakuja katika mwili kwa kuwa wao waliamini kwamba dunia na vyote vilivyomo ndani yake ni viovu, hivyo Kristo mwana wa Mungu asingeweza kuja katika mwili katika dunia ovu. Ukisiliza fundisho hilo linaonekana kama linamtetea Kristo na utukufu wake, yaani linaonyesha kwamba kwa Utakatifu wa Kristo asingeweza kuja katika dunia iliyo ovu. Lakini ukweli ni kwamba linaharibu na kukinzana na Imani yetu. Sasa kwetu leo kuna mafundisho mengi kuhusu kristo ambayo ukiyasikiliza ni kama yana mtetea Kristo lakini ukiyapima kwa maandiko (Yale waliyoyasikia wenzetu tangu mwanzo) unaona yanapingana na kweli. Mafundisho hayo tusiyakubali sisi kama waamini.
2. Kila ujumbe una wapokeaji wake.
Mwandishi ametuonyesha kwamba hawa manabii wa uongo wapo na pia dunia inawasikia. Ni dhahiri kwamba dunia inawasikia sana wao kwa sababu wananena mambo ambayo asili yake ni duniani na watu wa duniani wanayapenda na kuyakubali mambo yao. Kwa upande wa pili watu wa Mungu wanaisikia kweli. Moja ya jambo la msingi kujifunza hapa ni ukweli kwamba uongo wa ibilisi na manabii wake utasikiwa sana na utapendwa na watu wengi wa dunia hii na ukweli wa neno la Mungu utasikiwa na kupendwa na watu wachache wa Mungu. Hivyo katika kutimiza wajibu wetu kama waamini wa kujaribu kila roho tusiangalie idadi ya watu unaoisikia roho husika. Tukiangalia wingi tutapotea kwa urahisi kwa kuwa ni dhahiri wanabii wa uongo watasikiwa na watu wengi kwa kuwa wananena mambo ya duniani na dunia inayapenda mambo yake. Na upande wa pili kama unafundisha kweli usikate tamaa kama watu wengi hawakusikilizi/hawakubali ujumbe wako, jua kwamba hao wachache watakaokubali ujumbe wako hao ndio wa Mungu na wengine hawaukubali kwa kuwa hawako upande wa Mungu.
3. Ni wajibu wa kila mwamini kufanya utambuzi.
Mwandishi aliandika ujumbe wake kwa ajili ya kila mwamini kupokea ujumbe huo na sisi leo Roho wa Mungu anasema na sisi wote kwamba tusiamini kila roho inayonena nasi, hata kama inakiri kwamba roho hiyo imetoka kwa Mungu, tuna wajibu wa kupima na kuangalia kwamba ni kweli roho hiyo imetoka kwa Mungu au la. Kwa wakati wa mwandishi hakukuwa na Biblia kama tulivyonayo leo ndio maana aliandika hata namna ya kutambua, lakini sisi leo tuna Biblia ambayo ni msaada mkubwa katika kutusaidia kutambua Roho ya kweli ni ipi na roho ya upotevu ni ipi. Hivyo ni wajibu wa kila mwamini kutambua roho na kuiamini Roho ya kweli tu na kutokuamini roho ya mpinga Kristo.
1 Yohana 4:7-21
4.7 Wapenzi, nampendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu.
4.8 Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo.
4.9 Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye.
4.10 Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.
4.11 Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana.
4.12 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu.
4.13 Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake.
4.14 Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu.
4.15 Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu.
4.16 Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu niupendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.
4.17 Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu.
4.18 Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.
4.19 Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.
4.20 Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.
4.21 Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.
Mpangilio wa mfululizo wa Mawazo ya Mwandishi.
4:7-8 Tupendane kwa kuwa Upendo hutoka kwa Mungu.
4:9-10 Upendo wa Mungu umeonekana.
4:11-12 Kama Mungu alitupenda anatupasa kupendana.
4:13-16 Uhakika wa kukaa ndani ya Mungu.
4:17-18 Pendo huleta ujasiri na halichangamani na hofu.
4:19-21 Hitimisho
UFAFANUZI-TUPENDANE II.
Mwandishi katika sehemu hii unazungumza kuhusu kupendana jambo ambalo analisisitiza hii mara ya pili (Mara ya kwanza amezungumza katika 3:11-24). Hata kujenga hoja kwake katika aya hii kuna fanana sana na aya hiyo iliyopita. Mwandishi anasisitiza kupendana kwa wapokeaji wa ujumbe wake na katika kusisitiza huko anataja chanzo cha upendo ambacho ni Mungu. Katika kutaja chanzo cha upendo, Mwandishi pia anazungumza ukweli ulio wazi kwamba kila apendaye amezaliwa na Mungu, na mtu huyo apendaye anamjua Mungu (4:7). Kinyume na ukweli ulio wazi wa kwanza, mwandishi anasema ukweli mwingine ulio wazi kwamba asiyependa hamjui Mungu. Na ni kwa nini asiyependa hamjui Mungu? Hii ni kwa sababu sio tu Mungu ni chanzo cha Upendo lakini Mungu ni upendo (4:8). Kwa kuwa mwandishi ameonyesha kwamba Mungu ni Upendo na ndiye chanzo cha upendo, basi akaamua kuonyesha ni kwa namna gani Mungu amefanya upendo kudhihirika. Mungu alifanya kwa kumtuma mwanae wa pekee ulimwenguni ili sisi tupate uzima (4:9). Ni lugha nyepesi, Mungu alifanya jambo lenye gharama kwake lakini lenye manufaa kwa ulimwegu. Mwandishi anasisitiza Mungu alivyoonyesha pendo lake kwetu kwa kuanza yeye kutupenda kwa kumtoa mwanae ili kutupatanisha na yeye (4:10). Msisitizo wa mwandishi haukuwa katika kuwajulisha tu waamini sifa ya Mungu bali ilikuwa ni kuonyesha sifa ya Mungu ya Upendo uliodhirika ambayo inatufanya waamini kuwa wadeni wa kupendana (4:11). Mungu ameonyesha jinsi alivyo kwa kumtoa mwanae na sisi tunatakiwa kupendana kwa mfano huo. Mwandishi haiishii hapo tu kusisitiza bali anaenda mbele zaidi kusema waamini wakipendana basi huo ni mwonekano wa Mungu akaaye ndani yao ambaye hakuna mtu aliyewahi kumuona. Na Zaidi waamini wakipendana ni udhihirisho kwamba upendo wa Mungu kwao umefikia matokeo yake kamili katika kuumba aina ile ile ya upendo kama wake ndani yao (4:12). Mwandishi bado anaendelea kusisitiza kuhusu upendo lakini sasa anapanua kidogo mada yake kwa kuelezea kwa pembe nyingine. Mwandishi sasa anaelezea kwa kuwapa wapokeaji wa ujumbe namna ya kujua kwa hakika kwamba wanakaa ndani ya Mungu na Mungu anakaa ndani yao. Anataja mambo matatu, jambo la kwanza ni kupewa Roho wake yaani Roho wa Mungu kukaa kwa waamini (4:13). Jambo la Pili ni ukiri wa kukubali kwamba Yesu ni mwana wa Mungu (4:14) sawa sawa na ushuhuda wa mwandishi kwamba Mungu alimtuma mwanae kuwa mkombozi wa ulimwengu (4:13). Na jambo la tatu ni kukaa katika pendo sawa sawa na ufahamu na kuamini kwamba Mungu ni upendo na upendo huo umeelekea kwetu (4:15). Kwa kukaa katika pendo (kupendana sisi kwa sisi) basi upendo wa Mungu umefikia matokeo yake kamili katika kuumba aina ile ile ya upendo kama wake ndani yetu na hivyo hutupa ujasiri siku ya hukumu mbele zake (4:17). Baada ya kueleza kwamba pendo hutupa ujasiri siku ya hukumu, mwandishi anaelezea ukweli ulio wazi kwamba Upendo na hofu havichangamani (4:18). Mwandishi sasa anahitimisha aya hii ya kuhusu upendo kwa kurudia ambayo amekwisha kuyafudisha. Moja, tunapenda/tunatakiwa kupenda kwa kuwa Mungu alitupenda kwanza (4:19) kama alivyofundisha katika 4:9-11. Na pili kusema “nampenda Mungu” na wakati huo huo unamchukia Jirani yako, ile kauli ya kumpenda Mungu inakuwa ni Uongo. Hii kwa sababu huwezi kupenda Mungu usiyemuona na kumchukia Jirani umwonaye (4:20), mawazo sawa na wazo la 4:12. Na mwisho kumpenda Jirani kwa kila asemaye anampenda Mungi ni amri; yaani ni jambo la lazima (4:21).
TUNAJIFUNZA NINI.
- Mfano wa Upendo ni Mungu mwenyewe.
Kama ilivyo msisitizo wa mwandishi Mungu anatutaka waamini kupendana na namna ya kupenda yeye mwenyewe ameonyesha mfano bora kuliko yote. Mungu ameonyesha mfano kwa kumtoa mwanae wa pekee ili sisi tupate faida yaani tupate ukombozi, tupatanishwe na tusamehewe dhambi. Kwa ujumla upendo ulioonyesha na Mungu ni wa kufanya kitu cha gharama kwa manufaa ya wengine. Na sisi tunatakiwa kuiga mfano kwa kufanya mambo mema yanayotugharimu lakini yana manufaa kwa watu wengine. Kila mwamini anatakiwa kulenga kufanya jambo linalomgharimu yeye lakini lina manufaa kwa wengine.
1 Yohana 5 : 1-13
5.1 Kila mtu aaminiye kwamba Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye.
5.2 Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu, tumpendapo Mungu, na kuzishika amri zake.
5.3 Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.
5.4 Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.
5.5 Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?
5.6 Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu.
5.7 Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli.
5.8 Kwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja.
5.9 Kisha wako watatu washuhudiao duniani], Roho, na maji, na damu; na watatu hawa hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe.
5.10 Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe.
5.11 Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe.
5.12 Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.
5.13 Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.
Mpangilio wa mfululizo wa Mawazo ya Mwandishi.
5:1-5 Waliozaliwa na Mungu.
5:6-10 Ushuhuda wa Mungu juu ya Mwanae
5:11-13 Uzima wa milele kwa wanaoliamini jina la mwana wa Mungu.
UFAFANUZI-KUMWAMINI MWANA WA MUNGU
Baada ya kuelezea kuhusu waalimu/manabii wa uongo na upendo kwa mara ya pili katika haya zilizopita, mwandishi anaendelea kusisitiza mambo aliyoyafundisha tangu mwanzo wa waraka huu. Mambo haya ni imani kwamba Yesu ndiye Kristo, kuzaliwa na Mungu, kumpenda Mungu na watoto wake, kushika amri za Mungu, na kuushinda ulimwengu. Pia inasisitiza ushuhuda wa Mungu kwa Roho kuhusu Yesu ni nani na uzima wa milele ambao ametupa.
Mwandishi anaanza na kusisitiza kwamba kila anayeamini kwamba Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu (5:1a)[18] na mtu huyo ni tofauti na wapinga Kristo ambao wao hawaamini kwamba Yesu ni Kristo (Angalia 2:2). Baada ya kueleza kuhusu kweli hiyo mwandishi anarudi tena kuelezea kuhusu kupendana. Anaanza na ukweli ulio wazi kwamba kila mwenye kumpenda mzazi anampenda na mtoto aliyezaliwa na huyo mtoto (5:1b). Mwandishi anatumia ukweli huo ulio wazi kuonyesha kwamba tutajua kama tunawapenda watu pale tunapompenda Mungu na kuzishika amri zake (5:2). Kauli hii ni sawa kabisa na alichosema katika 4:20-21, Kauli zote mbili zina ukweli kwamba Kumpenda Mungu na kuwapenda Watoto wake (Kupendana) vinaenda Pamoja. Katika mwendelezo huo huo mwandishi anasisitiza tena kwamba kumpenda Mungu ni kuzishika amri zake na hizo amri sio nzito (5:3). Baada ya hapo mwandishi anaarudi tena kwenye jambo lake alilofungua nalo aya hii. Anaelezea kwamba sifa ya kile kilichozaliwa na Mungu ni kuushinda ulimwengu na ushindi huu juu ya ulimwengu sio jambo jingine lolote isipokuwa Imani yetu ambayo ni Imani kuhusu ukristo wa Yesu (5:4). Mwandishi anasisitiza kwamba ushindi juu ya ulimwengu ni Imani yetu, lakini Imani hii haiku tu kwenye kuamini katika ukweli kwamba Yesu ni Kristo kama alivyosema katika 5:1 bali pia Imani yetu inahusisha kuamini kwamba Yesu ni mwana wa Mungu (5:5). Kwa sababu kuamini kwamba Yesu ni Kristo na ni mwana wa Mungu ndio kunamfanya mtu azaliwe na Mungu na hivyo kuwa mshindi wa Ulimwengu, mwandishi akaona vema kumuelezea huyo Yesu zaidi. Mwandishi anasema Yesu Kristo alikuja kwa maji na kwa damu na kusisitiza kwamba hakuja tu kwa maji bali kwa damu pia (5:6). Hii ni ishara kwamba kuna watu walikuwa wanaamini kwamba Yesu alikuja kwa maji tu na si kwa damu. Mwandishi ametumia lugha ya picha hapa katika kumuelezea Yesu na lugha hii ya picha kwa waandikiwa wa awali ilikuwa ni lugha inayoeleweka kwa wazi lakini kwa sababu ya kupita kwa wakati imekuwa ni vigumu kujua kwa hakika pasipo shaka maana ya lugha hii ya picha. Kuna mapendekezo mengi ya nini maana ya lugha hii ya picha lakini mimi nakubaliana na mapendekezo kwamba lugha hii ya picha ya maji na damu ina maana ya kubatizwa na kufa kwa Yesu. Hii ni kwa sababu baada ya kutaja maji na damu mwandishi anamtaja Roho mtakatifu kuwa naye ni shahidi anayemshuhudia Yesu (5:7), na inafahamika kwamba Roho mtakatifu alimshuhudia Yesu kuwa ni mwana wa Mungu wakati wa tukio la Ubatizo (Yohana 1:32-34). Mwandishi pia anasema hawa wote watatu yaani maji, damu na Roho wanapatana katika habari moja yaani wote wanamshuhudia Yesu kwamba ni mwana wa Mungu na yeyote amwaminiye atapata uzima (5:8)[19]. Ushuhuda huu wa maji, damu na Roho ni ushuhuda wa Mungu juu ya mwanae, kama tunaweza kuuamini ushuhuda wa mwanadamu basi inatakiwa kuuamini ushuhuda wa Mungu kwa kuwa ushuhuda wake ni mkuu kuliko wa wanadamu (5:9). Anayemwamini Yesu huyo ameukubali ushuhuda wa Mungu ambao ameshuhudia kuhusu mwanaye na asiyeamini anamfanya Mungu kuonekana muongo kwa kuwa ni kawaida kwa wanadamu kutokuamini ushuhuda usio wa kweli (5:10).
Katika kumalizia aya hii mwandishi anasisitiza kwamba Mungu ameshatoa taarifa kwamba uzima wa milele upo na unapatikana kwa njia ya kumwamini mwanae Yesu Kristo (5:11). Hivyo anayemwamini Yesu anao uzima wa milele na asiye mwamini hana huo uzima wa milele (5:12). Na mwisho mwandishi anasema ameandika haya ili wanaomwamini Yesu wajue kwamba wanao uzima wa milele (5:13). Kuna mfanano wa karibu sana kati ya lugha ya 5:13 na lugha katika Injili ya Yohana 20:31. Sehemu zote mbili zinataja kuhusu kusudi la yaliyoandikwa, zote zinahusu uzima (wa milele), zote yanarejelea kuamini, na zote zinataja maneno “Mwana wa Mungu” na “katika jina lake.” Utofauti wake ni kwamba Yohana 20:31 imeandikwa ili wasomaji wa Yohana waweze kuamini, ilihali 1 Yohana 5:13 inaeleza kwamba wasomaji wake tayari wamekwisha kuamini na hivyo kusudi lake ni kwamba wapate kujua kwamba wana uzima huu.
TUNAJIFUNZA NINI
1. Uzao wa Mungu.
Mwandishi anatufundisha kwamba ili mwanadamu afanyike kuwa mwana wa Mungu anatakiwa kuamini tu kwamba Yesu ni Kristo. Na kila aliyezaliwa na Mungu yeye ni mshindi kwa kuwa ameamini. Ushindi kwa mwandishi sio jambi lolote lile isipokuwa Imani yetu. Kwa kutokujua au kutokuamini kwa hakika mara nyingi waamini tumejiona kuwa sio washindi au sisi sio Watoto kamili wa Mungu lakini mwandishi ametupa namna ya kujua kama sisi ni Watoto wa Mungu au la. Kuna picha ambayo imeingia ndani ya kanisa ya kuonyesha kwamba wale wasio na magonjwa, wenye fedha, vyeo na mali hao ndio wanaonyesha dhahiri kwamba wao ni Watoto wa Mungu na washindi lakini picha hiyo sio picha sahihi tunayojifunza kutoka katika Biblia.
2. Uzima wa milele sasa.
Mara nyingi tukizungumza uzima wa milele kwenye fahamu zetu inakuja maana ya Maisha ya kutokufa ya waamini baada ya kufufuliwa. Jambo ni kweli kabisa, maandiko yanaeleza kuwa huo ni uzima wa milele. Lakini pia kwa upande wa pili maandiko yaonyesha kwamba Yesu ndiye uzima wa milele na yeyote aliye na Yesu anao uzima wa milele mara tu baada ya kuamini. Kwa hiyo kila mwamini anao uzima wa milele ndani yake.
3. Ushuhuda wa Mungu ni mkuu.
Mwandishi anapozungumzia kwamba Mungu amemshuhudia mwanae anatupeleka kwenye lugha ya kimahakama, yaani Mungu alitoa Ushahidi kwamba amemtuma mwanae aje ulimwenguni kwa ajili ya kutoa uzima kwa kila atakaye mwamini nay eye ndiye pekee wa kuaminiwa. Ushuhuda huo Mungu aliutoa akikusudia kila atakayeusikia aukubali kwa kumwamini Yesu. Sasa pale ambapo watu hawamwamini Yesu mwandishi anasema watu wao wanamfanya Mungu kuwa mwongo. Hii ni kwa sababu sisi sote huwa tunaamini Ushahidi/ushuhuda ambao huwa tunadhani ni wa kweli na huwa hatuamini kile ambacho tunadhani ni uongo. Ni mwito wa Mungu kwamba sisi sote tuamine ushuhuda wake kwa kuwa kama tunaweza kuamini ushuhuda wa wanadamu tunashindwaje kuamini Ushuhuda wa Mungu ambaye ni mkuu kuliko binadamu?. Kama bado hujamwamini Yesu basi fanya hivyo, usimfanye Mungu kuwa mwongo.
1 Yohana 5:14-17
5.14 Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.
5.15 Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.
5.16 Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo.
5.17 Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti.
Mpangilio wa mfululizo wa Mawazo ya Mwandishi.
5:14-15 Ujasiri katika Maombi
5:16-17 Maombezi
UFAFANUZI-UJASIRI KATIKA MAOMBI
Wale wote wanaomwamini mwana wa Mungu wana ujasiri kwamba Mungu anasikia maombi yao pale wanapoomba sawa sawa na mapenzi yake (5:14). Na kwa sababu Mungu anasikia basi huu ni uhakika kwamba tutapokea haja zile tulizomwomba Mungu (5:15). Moja ya jambo ambalo linaweza kuwa haja yetu ambayo tunauhakika Mungu atatusikia kwa sababu iko kwenye mapenzi yake ni kumuombea ndugu ambaye anatenda dhambi “isiyo ya mauti”, na tukifanya hivyo mwandishi anasema Mungu atampa uzima yule anayetenda dhambi “isiyo ya Mauti”. Baada ya kusema hilo mwandishi anaonyesha tofauti ya dhambi; ambapo kuna dhambi isiyo ya mauti na dhambi ya mauti, mwandishi anasisitiza maombi haya hayafanywi kwa mtu anayetenda dhambi ya mauti (5:16). Kwa kupanua uwanja mwandishi anasema kila jambo ambalo si la haki ni dhambi na dhambi iko isiyo ya mauti (5:17). Kwa tasfiri nzuri Zaidi neno “dhambi ya mauti” huweza kutasfiriwa kama dhambi inayopelekea kwenye mauti. Na mauti katika kitabu hiki sio kifo cha mwili bali ni mauti ya kiroho. Mwandishi ametupa tu aina ya dhambi lakini hajataja ni dhambi ipi ni ile inayopelekea Mauti na ipi sio ya mauti lakini kwa kufuatilia Mawazo na msisitizo wa mwandishi tunaona kuwa kuna aina ya dhambi ambazo amezitaja ambazo amekiri kwamba wanaofanya hivyo hawana Baba (2:18-19), wamo gizani (2:9) na wanakaa mautini (3:14-15), hizo zaweza kufikiriwa kuwa ni dhambi za Mauti.
TUNAJIFUNZA NINI.
1. Kujibiwa maombi.
Ujumbe huu wa Yohana ni muhimu sana kwenye Maisha yetu kama waamini, kwa kuwa hakuna jambo muhimu sana na linaloongeza Imani yetu kwa Mungu kama kuomba na kujibiwa. Roho wa Mungu anatuonyesha kwamba kama tukiomba vitu sawa saw ana mapenzi ya Mungu, yeye hutusikia na kama anatusikia basi ni dhahiri tutapata majibu ya yale tuliyomwomba. Swali la msingi linaweza kuwa mimi nitajuaje mapenzi ya Mungu ili niombe sawa sawa na hayo? Jibu ni kwamba Mapenzi ya Mungu yapo kwenye Neno la lake, ndio maana ni muhimu kuwa msomaji wa neno la Mungu ili uweze kujua mapenzi yake. Lakini pia Mungu hajaishia hapo, pia husema na sisi katika mahusiano yetu nay eye. Hutujulisha mapenzi yake kupitia sauti ya ndani ya moyo, sauti ya kusikika, ndoto, maono, maonyo kutoka kwa watu wengine nan jia nyingine mbalimbali. Kwa hiyo sisi kama waamini tunatakiwa kujua mapenzi ya Mungu na kuhakikisha tunaomba sawa sawa na mapenzi hayo.
2. Kuombeana.
Najua kuna mahitaji mengi sana ambayo mwandishi angeyatolea mfano lakini ametoa mfano wa maombi ya kuombeana ili sisi pia tujifunze kwamba maombi sio jambo la kibinafsi. Tunatakiwa kuombeana sisi kwa sisi kama tunavyojiombea wenyewe. Ni mara ngapi umewaombea watu wengine? Hili ni swali la kujiuliza na kama majibu yako sio Chanya basi anza leo kuwa mtu unayewaombea wengine. Waamini wanapoingia kwenye dhambi mimi nisifurahi wala kunyamaza bali ni wajibike kwa kumuombea kama mwandishi alivyotufundisha.
1 Yohana 5:18-21
5.18 Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi.
5.19 Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.
5.20 Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.
5.21 Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.
Mpangilio wa mfululizo wa Mawazo ya Mwandishi.
5:18-20 Wana wa Mungu hulindwa
5:21 Mwisho
UFAFANUZI-HITIMIHO.
Kama ilivyo kawaida yake mwandishi kwa kuwa ametaja kuhusu dhambi (5:17) akaamua kurudia kwa msisitizo Jambo alilolisema tayali (3:5-10) kwamba waliozaliwa na Mungu hawawezi “kuendelea” kuishi katika dhambi, kwa kuwa waliozaliwa na Mungu hujilinda na mwovu hawagusi (5:18). Mwandishi ameshasema kwenye aya ya juu kwamba mwamini anaweza kutenda dhambi isiyo ya mauti na maombi ya mwamini mwingine yanahitajika wakati huo, hivyo hajipingi anaposema aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi. Tena mwandishi anasema yeye, walioupande wake na waandikiwa wa ujumbe wake wao ni wa Mungu na dunia ni ya yule mwovu (5:19). Pia mwandishi na kundi lake wanajua kwamba Yesu, mwana wa Mungu amekwisha kuja na kujifunua kuwa yeye ni wa kweli, na mwandishi na kundi lake wamo ndani yake. Na hapa mwandishi anasema wazi kwamba Yesu ndiye Mungu wa kweli na Uzima wa milele (5:20). Kwa kuwa mwandishi amesema kwa wazi kwamba Yesu ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele inaweza kudhaniwa kwamba “huyu ndiye” inamhusu Baba na sio Yesu lakini Mstari mzima wa 20 inamuelezea Yesu na sio Baba na pia katika barua hii Yesu ndiye anayeitwa Uzima/uzima wa Milele na sio Baba (Angalia 1:2 na 5:11-13 ). Mwisho mwandishi anamaliza na kauli moja tu ya jambo ambalo hajalizungumzia kabisa katika ujumbe wake wote mpaka sasa, yaani waamini wajilinde na sanamu. Kwa lugha nyepesi na kwa mazingira ya karne ya kwanza mwandishi anawahasa kwamba wajiweke mbali na ibada ya sanamu (5:21).
TUNAJIFUNZA NINI.
1. Wana wa Mungu hujilinda.
Biblia inafundisha kwamba sisi waamini tunalindwa na Mungu kwa njia ya Imani. Hili ni jambo la kweli na hakika, lakini pia Biblia inafundisha kwamba mwamini hujilinda yaani hujiweka mbali na yule mwovu na mwisho wa siku yule mwovu hamgusi. Kumgusa ina maana ya mwovu hawi na nafasi katika Maisha ya mwamini huyu.
2. kujitenga na ibada ya sanamu.
Katika karne ya kwanza ibada ya sanamu ilifanyika kwa watu Kwenda kwenye mahekalu/sehemu maalumu ya kufanyia ibada hizo lakini kwa sasa hili linaweza lisiwe kwa wazi kwa kiasi hicho. Lakini hii haimaanishi kwamba hakuna ibada ya sanamu sasa. Ibada ya sanamu ipo sasa kwa namna ya kuviabudu vitu ambavyo vinaambatanishwa katika ibada zetu mfano wa vitu hivi ni sanamu zilizopo kwenye majengo ya kukutania waamini, kuabudu viongozi wetu wa makanisa, kuabudu wenye fedha na mali na vyeo na kwa njia nyingine mbalimbali.
VITABU REJEA
Campbell, Constantine R. 1, 2, and 3 John. Grand Rapids, MI : Zondervan, 2017
Burge, Gary M. The letters of John: from biblical text to contemporary life. Grand Rapids, Michigan: Zondervan Publishing House, 1996.
Stott, John R.W. The Letters of John: An Introduction and Commentary.
Jobes, Karen H. 1, 2, and 3 John. Grand Rapids, Michigan: Zondervan, 2014.
Yarbrough, Robert W. 1-3 John. Grand Rapids: Baker Academic, 2008.
Marshall, I Howard. The Epistles of John. Grand Rapids, Michigan: William B. Eerdmans, 1978.
Köstenberger, Andreas J. A theology of John’s Gospel and letters. Grand Rapids, Michigan : Zondervan, 2009.
Footnotes
[1] Yohana anataja jina lake katika kitabu cha Ufunuo mara kadhaa kama vile Ufunuo 1:1,4,9 na 22:18
[2] Pointi a na b zimenukuliwa kutoka kwenye kitabu kinachoitwa; Theologia ya Injili ya Yohana na Barua: Theologia ya kibiblia ya Agano jipya kilichoandikwa na mwandishi Andreas J. Kostenberger, 2009.
(Andreas J. K (2009), A theology of John’s Gospel and Letters: Biblical theology of the New Testament. Epub edition).
[3] Kwa kuwa teknologia ya kuchapa iligunduliwa karne ya 14, hapo nyuma maandiko yalikuwa yanaandikwa kwa mkono na nakala zilitengenezwa kwa kukopiwa kwa mkono. Hivyo zile nakala zilizoandikwa kwa mikono za vitabu hivi vitatu vinabeba jina la Yohana kuonyesha kwamba ilijulikana tangu awali kwamba yeye ndiye mwandishi wa Vitabu hivi.
[4] Mapendekezo haya ya uhusiano wa unabii wa mtume Paulo na hali ya kanisa mwandishi analoliandikia si mapendekezo ya uhakika, bali yanaweza kusaidia tu kuelewa kwamba kanisa ambalo mwandishi analiandikia lilikuwa katika mgawanyiko wa kutoka ndani. Mapendekezo haya yamefanywa na mwandishi John R. W Stott katika kitabu kinachoitwa “Barua za Yohana: Utangulizi na Ufafanuzi cha mwaka 1988”
(Stott, J (1988) The letters of John: An Introduction and Commentary. IVP)
[5] Kama unaweza kusoma kiingereza basi maandishi haya ya Baba Askofu Ireneo yaliyoandikwa kwa kiyunani yametafsiriwa na yanapatikana kwa ajili ya kusomwa bila malipo kabisa katika tovuti au aplikesheni ya Biblehub au tovuti ya New advent. Habari hizo za Cerinthus zinapatikana kwenye Kitabu chake kiitwacho “Against Heresies I.26.1. Askofu Ireneo anaripoti kwamba Cerinthus aliishi wakati wa Mtume Yohana na waliwahi kukutana (Against Heresies III.3.4).
[6] Ireneo, Against Heresies III. 1.1
[7] Ireneo, Against heresies III. 3.4
[8] Eusebio, Historia ya Kanisa III.23
[9]Yohana anatumia neno hili Kudhihirika akionyesha jinsi Yesu alivyokuwa anajionyesha yeye ni nani kwao wakati wa Maisha yake (Yoh 2:11) na jinsi alivyowatokea baada ya kufufuka kwake (Yoh 21:1,14)
[10] Japo Yohana anazungumzia picha ya Nuru na Giza katika maeneo mengi (Yohana 1:5,8:12, 11:10, 12:35-36,46), Nimetumia Yohana 3:19-21 kwa sababu inaonyesha uhusiano mzuri wa Giza na Nuru hasa kuhusiana na mwitikio wa watu. Inaeleza watu wa gizani wakoje na mwitikio wao kwa Nuru na watu wa nuruni wakoje na mwitikio wao kwa hiyo nuru ukoje.
[11]Fundisho la kuwepo kwa mtu aitwaye Mpinga kristo lilifundishwa kwa waamini mapema sana kwa sababu liliambatana na fundisho la Ujio wa Yesu mara ya Pili. Hivyo inaonekana wapokeaji wa ujumbe huu walikwisha fundishwa habari za mtu ajaye aitwaye Mpinga kristo. Maandishi ya kwanza kabisa kuonyesha kwamba kanisa lilifundishwa kuhusu mpinga kristo ni barua ya Mtume Paulo kwa Wathesalonike (2 Wathesalonike 2:1-10). Kumbuka kwamba nyaraka kwa wathesalonike ndio nyaraka zenye uhakika kabisa kwamba ziliandikwa mapema Zaidi kuliko vitabu vyote vya Agano jipya.
[12]Kukana kwamba ukristo/umasihi kwa watu hawa hakufanani na vile wayahudi walivyokana umasihi wa Yesu, wao walikuwa wanakana kwamba Kristo hakuja katika Mwili (Tazama 1 Yohana 4:1-6, 2 Yohana 7). Hii ilitokana na kumtenganisha Kristo wa Mbinguni na Yesu mwanadamu wa Nazareth (Tazama Utangulizi, Sababu za kuandikwa kitabu hiki)
[13]Mwandishi ametumia neno “Uzima wa milele” kwa namna mbalimbali. Moja Yesu mwenyewe ndio uzima wa milele (1 Yohana 1:2, 5:20), Pili ni uzima tunaoupata sasa baada tu ya kumwamini Yesu (Yohana 5:11-13) na Tatu ni Jambo ambalo tunalisubiri kwa kuwa tumeahidiwa (1 Yohana 2:25). Ahadi ni jambo ambalo hatujalipata. Hivyo kwa mwandishi Uzima wa Milele tunao sasa na tutaupata badae, vyote kwake ni kweli.
[14] Kama ambavyo tumejifunza katika utangulizi kwamba Yesu ni jina Jina la Mwokozi wetu na Kristo ni Cheo ambacho kinamaanishani yeye ni mpakwa mafuta wa Mungu aliyetabiriwa kwamba atakuja kupitia ukoo wa Daudi. Hivyo Yesu ni Kristo kwa maana ya kuwa yeye ni mpakwa mafuta wa Mungu aliyekuja duniani kupitia familia ya mfalme Daudi.
[15]Soma pia Yohana 15:18-19
[16]Bado tunaona Yohana anafundisha kutokana na Yesu alivyofundisha. Yesu ndiye Mwalimu wa kwanza kufafanua sheria kwa namna ya kuonyesha kwamba Hasira na Chuki zinafafana tu na uuaji (Mathayo 5:21-22)
[17]Swali la balagha ni swali lisilohitaji jibu kwa maana tayali lina jibu ndani yake.
[18] Mwandishi ametumia sifa nyingine nne kuwaelezea watu waliozaliwa na Mungu. Angalia (2:29; 3:9; 4:7; 5:4, 18).
[19] Maneno yaliyowekwa kwenye mabano [mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja. Kisha wako watatu washuhudiao duniani] ni maneno yanayoonekana kwenye nakala chache za agano jipya zilizoandikwa kwa mikono na hivyo hakuna uhakika kwamba maneno haya yaliandikwa na mwandishi au yaliongezwa wakati wa kunakiri ujumbe huu.Na pia yanakosekana kwenye nakala za zamani Zaidi za agano jipya.