MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA PILI WA MTUME PETRO.
MAELEKEZO.
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.
UTANGULIZI.
Waraka huu ni wa pili (3:1) kuandikwa na Mtume Petro kwa waamini wa mataifa, ambao hakutaja wanaishi maeneo gani. Waamini hawa walikuwa wamepokea ujumbe wa waraka wake wa kwanza (3:1) na pia walikuwa wamepokea ujumbe wa nyaraka za Mtume Paulo (3:15-16).[1].
MTUME PETRO.
Mtume Petro ni mmoja wa mitume kumi na wawili Bwana Yesu kristo aliowachagua (Luka 6:13-16) na pia ni mmoja wa wanafunzi watatu wa karibu sana wa Yesu. Wanafunzi hawa ni miongoni mwa wanafunzi wa awali kabisa wa Yesu (Luka 5:4-11) na ni wanafunzi walioona matukio adimu ya Yesu ambayo wanafunzi wengine hawakuyaona. Matukio haya ni kama vile kubadilika kwa Yesu kule mlimani (Luke 9:28-36) na maombi ya Yesu katika bustani ya Gethsemane (Mathayo 26:36-46). Mtume Petro jina lake la asili ni Simon lakini alibadilishwa jina na Yesu na kuitwa Cepha (kwa Lugha ya kiaramu) ambalo ni Petros (kiyunani), ambalo ndilo Petro kwa Kiswahili. Petro kabla ya kukutana na Yesu alikuwa ni mkazi wa Galilaya na mvuvi wa samaki katika ziwa la Genesareti (Luka 5:1-11).
WAPOKEAJI WA AWALI WA WARAKA.
Wapokeaji wa waraka huu walikuwa ni waamini wa mataifa yaani watu walioamini lakini ambao hawakuwa wayahudi, ndio maana Petro anawaita “wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani”. Mtume Petro anaposema “sisi” anamaanisha wayahudi, hivyo anawaandikia waamini wa mataifa ambao wamepokea imani sawa na ile waamini wa kiyahudi walioipokea yenye thamani. Mtume Petro hajataja maeneo ambayo waraka huu ulikusudiwa kufika, tofauti na alivyotaja katika waraka wake wa kwanza (1 Petro 1:1-2). Hii ndiyo sababu waraka huu umepewa jina la ‘waraka kwa watu wote’ kwenye Biblia zetu. Ingawa hakutaja maeneo ya wapokeaji wa awali, wapokeaji hawa walikuwa na sifa mbili. Kwanza, walipokea ujumbe wa Mtume Petro kupitia waraka wake wa kwanza (3:1). Pili, waliwahi kuandikiwa waraka na Mtume Paulo na pia walikuwa na nyaraka zingine za Mtume Paulo (3:15-16). Hivyo, waamini hawa wanaweza kuwa wale walioishi katika Asia Ndogo
KUSUDI LA WARAKA.
Mtume Petro aliandika waraka huu kwa makusudi yanayoweza kuwekwa kwenye makundi mawili kama ifuatavyo.
a. Hotuba ya kuaga.
Mtume Petro aliandika waraka huu kama Hotuba yake ya kuwaaga waamini kwa kuwa alijua wakati wake wa kufa umekaribia. Hivyo aliaandika waraka huu ili kuwakumbusha waamini kuishi maisha ya utauwa (1:3-15 na 3:11-14) na kuacha kumbukizi ya mafundisho yake (1:12-15). Kwa kuwa waraka huu ni hotuba ya kuaga Petro alitabiri ujio wa waalimu wa uongo na kutoa tahadhari kwa waamini kuhusu waalimu wa uongo watakaotokea (2:1-3a na 3:1-4). Katika kutoa tahadhari kuhusu waalimu wa uongo Petro aliwataka waamini wabaki katika kweli waliojifunza kutoka kwa mitume na yenye ushahidi wa unabii/maandiko (1:16-21 na 3:1-2).[2]
b. Utetezi wa Imani.
Kusudi la pili la mtume Petro kuandika waraka huu ni kutetea imani kuhusu tumaini letu yaani ujio wa pili wa Yesu katika utukufu wake (1:16-21 na 3:1-10). Ingawa Petro anazungumzia waalimu wa uongo kama utabiri wa mambo ya baadaye (2:1 na 3:3, 17), anafanya utetezi wa tumaini la kurudi kwa Yesu mara ya pili kana kwamba waalimu wa uongo tayari wanapinga ukweli huo (1:16 na 3:16). Aidha, Petro anataja sifa za kimwenendo za waalimu hawa wa uongo (2:11-22) na kuonyesha uhakika wa hukumu yao iliyo tayari (2:3b-10).
MPANGILIO.
Namba | Maandiko | Maelezo | |
1 | 1:1-2 | Utangulizi wa Waraka | |
2 | 1:3-15 | Utangulizi wa Ujumbe mkuu wa waraka | |
A | 1:3-11 | Ujumla wa Ujumbe wa Petro kwa waamini | |
B | 1:12-15 | Sababu ya kuandika waraka huu | |
3 | 1:16-21 | Ujio wa Yesu mara ya Pili katika Utukufu ni wa uhakika | |
A | 1:16-18 | Ukuu na utukufu wa Yesu tunaoutarajia katika ujio wake tuliuona | |
B | 1:19-21 | Ushahidi wa maneno ya unabii | |
4 | 2:1-22 | Waalimu wa Uongo | |
A | 2:1-3a | Ujio wa waalimu wa Uongo | |
B | 2:3b-10 | Uhakika wa Hukumu kwa waalimu hawa wa Uongo | |
C | 2:11-22 | Sifa za waalimu hawa wa Uongo | |
5 | 3:1-16 | Ahadi ya kuja kwake ni hakika | |
A | 3:1-5 | Ujio wa wenye kudhihaki ahadi ya kuja kwake | |
B | 3:6-10 | Uhakika wa utimilifu wa Ahadi ya kuja kwake | |
C | 3:11-16 | Namna ya kuishi waamini kwa sababu ya kujua uhakika wa ujio wake | |
6 | 3:17-18 | Mwisho wa Waraka |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.
Waraka huu una mpangilio wa kawaida wa waraka, yaani una utangulizi wa waraka (1:1-2), ujumbe mkuu (1:3-3:16) na mwisho wa waraka (3:17-18). Utangulizi una sehemu tatu kama ilivyokuwa kawaida yaani kuna Anuani ya Mtuma waraka (1:1a), anuani ya mpokeaji (1:1b) na Salamu (1:2).
Ujumbe mkuu umegawanyika katika sehemu nne ambazo ni:
Utangulizi wa Ujumbe mkuu (1:3-15). Katika sehemu hii mtume Petro anawajulisha waamini kwamba uweza wa Uungu wa Yesu umewapa bure kila kitu wanachokihitaji ili kuishi maisha ya utauwa. Na hivyo vyote vinapatikana kwa njia ya kumjua yeye aliyewaita (1:3). Tena amewapa ahadi kubwa mno za thamani ili washiriki tabia ya Uungu (1:4). Hivyo wanatakiwa kufanya bidii kuishi iwapasavyo (1:4-9) na kwa kuishi hivyo hawatajikwaa kamwe na mwisho watapewa kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo (1:10-11). Petro anasema lengo la kuandika waraka huu ni kuwakumbusha waamini kuishi kama alivyoelezea hapo juu pamoja na kwamba anajua wanaishi hivyo tayari (1:12-14). Sio tu kuwakumbusha kuishi hivyo bali pia kuacha kumbukumbu ya mafundisho yake (1:15).
Sehemu ya kwanza ya Ujumbe mkuu (1:16-21), Petro anawahakikishia waamini kwamba walivyowafundisha kuhusu ukuu wa Yesu na ujio wake mara ya Pili hawakuwafundisha hayo kwa sababu ya kufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu[3], bali wana uhakika na habari hizo kwa sababu mbili. Moja, Petro na wenzake walimuona Yesu kristo katika utukufu wake katika mlima ule ambapo alibadilika na kung’aa na sauti ya Mungu akasikika ikisema “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (1:16-18)[4]. Sababu ya Pili ni uwepo wa neno la Unabii uliopo katika maandiko unaotabiri ujio wa wakati ambao Mungu atafanya upya mambo yote kupitia Ujio wa pili wa Yesu (1:19-21)[5]. Ushahidi huu Petro anaoutoa sio wa peke yake ndio maana anatumia lugha ya wingi katika sehemu hii ( “…hatukufuata… tulipowajulisha… tuliisikia…”) japo sehemu ya nyuma (1:3-15) alitumia lugha ya umoja (…nitakuwa tayari…. Walakini nitajitahidi……). Huu ni ushahidi wa yeye Petro na Mitume wengine.
Sehemu ya pili ya Ujumbe mkuu (2:1-22), Petro anawajulisha waamini kwamba watatokea waalimu wa uongo miongoni mwao ambao wataingiza uzushi wa kupoteza kwa werevu (kwa namna ambayo ni ngumu kutambua kama huo ni uongo) na watamkana hata Bwana aliyewanunua[6]. Mwenendo wao wa kumkana Bwana utawafanya wengi wawafuate na hivyo njia ya kweli itatukanwa na wao watajipatia faida (2:1-3a). Petro anawaonyesha waamini kwamba waalimu hao wa Uongo Mungu atawahukumu. Uhakika wa hukumu kwa waalimu hawa wa uongo Petro anautoa kwa kuonyesha hukumu ya Mungu katika historia (2:3b-8). Katika kuonyesha uhakika wa hukumu ya waalimu hawa wa uongo Petro anaonyesha kwamba Mungu amekuwa akiwaokoa watauwa wasipate hukumu pamoja na wasio haki (2:9-10). Baada ya hapo Petro anaeleza kwa urefu sifa na tabia za waalimu hawa wa uongo (2:11-22).
Sehemu ya tatu ya Ujumbe mkuu (3:1-16), Petro anawasisitiza waamini kukumbuka maneno ya manabii watakatifu na mafundisho ya Bwana Yesu waliyoyapata kupitia mitume. Anawajulisha kwamba watakuja watu wenye kudhihaki maneno haya, ambayo yana ahadi ya Yesu kurudi mara ya pili, kutakako ambatana na kufanywa upya kwa vitu vyote (3:1-5). Petro anawathibitishia waamini kwamba siku hiyo inakuja kwa hakika na mbingu na nchi wanayoiona sasa itafumuliwa na kuteketea na vitu vilivyondani yake (3:6-10). Lakini baada ya hayo waamini Mungu amewaahidi mbingu mpya na nchi mpya ambayo haki yakaa. Kutokana na ujuzi wa kile Mungu atafanya kwenye mbingu na nchi ya sasa (pamoja na wasiomcha Mungu) na kutokana na ujuzi wa ahadi ya mbingu mpya na nchi mpya waamini wanatakiwa kuwa watu wa mwenendo wa utauwa na wawe na bidii ili waonekane katika amani kuwa hawana mawaa wala aibu mbele yake. Na wanatakiwa kujua kwamba uvumilivu wa Bwana (kutokuwahi kurudi kwa Bwana) ni kwa ajili ya wokovu. Mtume Petro anasema kwamba mambo hayo (ya Mstari wa 14 na 15) ni mambo ambayo Mtume Paulo pia ameyazungumzia kwenye nyaraka zake (3:11-16).[7]
Mwisho wa waraka Petro anawasisitiza waamini kwamba kwa kuwa wameyajua hayo yote walinde nafsi zao waangalie wasije wakachukuliwa na waalimu hawa wa Uongo (wahalifu), wakaanguka na kuuacha uthibitifu wao ila wakue katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo (3:17-18).
FOOTNOTES
[1] Hakuna anayejua idadi ya nyaraka za mtume Paulo Petro anazozizungumzia katika sehemu hii. Kumbuka wakati huu Petro anazungumza Vitabu vya Agano jipya vilikuwa havijakusanywa kwa pamoja kama tulivyonavyo hivi leo.
[2] Kutoa Hotuba ya kuaga ilikuwa ni jambo la kawaida katika Israeli na katika kipindi cha kanisa. Mfano Kitabu cha kumbukumbu la Torati ni Hotuba ya Kuaga ya Musa kwa kizazi kipya cha Israeli, Yohana 13:31-17:26 ni Hotuba ya Yesu ya Kuaga wanafunzi wake, Matendo 20:17-38 ni Hotuba ya Mtume Paulo kuaga viongozi wa kanisa la Efeso na 2 Timotheo ni Hotuba ya Kuaga ya Mtume Paulo. Hotuba hizi za kuaga zote zinahusisha mambo mawili makuu, moja maelekezo ya namna ya kuishi/kuenenda na Pili utabiri wa mambo ya mbele baada ya mhusika kuondoka.
[3] Utetezi huu Petro anaoufanya unaweza kuwa ishara ya kwamba kuna watu waliwatuhumu mitume kwamba hili fundisho la kurudi kwa Yesu mara ya Pili katika utukufu wake ni hadithi zilizotungwa kwa werevu na mitume wakazifuata.
[4] Tukio hili la Yesu kubadilika Petro analolizungumzia linapatikana katika Mathayo 17:1-8, Marko 9:2-8 na Luka 9:28-36.
[5] Petro kwa kuwa ni myahudi Neno la unabii analolisema ni maandiko ambayo leo tunayaita Agano la kale kwa kuwa kwa wakati wake hakukuwa na maandiko yanayoitwa Agano jipya. Maandiko haya yanatabiri ujio wa wakati ambao Mungu atayafanya upya vitu vyote na baada ya kumwamini Yesu Petro anajua kwamba tukio hili litatokea pale Yesu atakaporudi mara ya Pili. Hivi ni sawa na Petro alivyofundisha watu kule hekaluni baada ya kiwete kutembea (Angalia Matendo 3:19-21)
[6] Kumkana Bwana kwa waalimu hawa wa uongo sio kwa njia ya kutamka kwamba Yesu sio Bwana wao bali ni kwa mwenendo wao. Kama ni kwa njia ya kutamka basi isingekuwa vigumu kutambua uzushi wao
[7] Mtume Paulo amezungumzia sana kuhusu kuishi Maisha ya utauwa katika mwenendo kunakotokana na mwamini kujua siku ya kurudi Bwana imekaribia kama ambavyo Petro amekiri. Moja ya maeneo amezungumzia hilo ni katika Warumi 13:11-14. Lakini pia amezungumza kuhusu uzumilivu wa Mungu ambao unatoa nafasi ya watu kutubu. Maeneo aliyozungumzia hili ni kama Warumi 2:4, 9:22
UFAFANUZI WA WARAKA WA PILI WA MTUME PETRO..
Unakuja hivi karibuni…….