2 Timotheo- Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA PILI WA MTUME PAULO KWA TIMOTHEO.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.

UTANGULIZI.

Waraka huu ndio waraka wa mwisho kabisa kuandikwa kati ya nyaraka zote mtume Paulo alizoandika. Paulo aliandika waraka huu kwenda kwa Timotheo, mwanae katika imani ambaye bado aliyekuwepo huko Efeso. Paulo aliandika waraka huu akiwa gerezani Rumi, wakati huu ni baada ya kuandika waraka wake wa kwanza kwa Timotheo na waraka kwa Tito ambapo muda huo alikuwa huru. Kwa wakati huu Paulo alikuwa gerezani kabisa tofauti na kifungo chake cha nje alichofungwa wakati anaandika barua kama vile Waefeso, Wafilipi, Filemoni na Wakolosai. Wakati wa kifungo hicho cha kwanza huko Rumi Paulo alikuwa na watenda kazi pamoja naye pembeni yake kama vile Timotheo, Marko, Luka, Aristako na Dema (wakolosai 1:1, 4:10 na Filemoni 1:24) lakini katika kifungo hiki yuko na Luka peke yake (4:11).

TIMOTHEO.

Timotheo alikuwa ni mtoto wa Baba myunani na Mama myahudi aliyeamini aitwaye Eunike. Timotheo inawezekana aliamini wakati mtume Paulo alivyokwenda kuhubiri kule Listra katika safari yake ya kwanza ya kimishenari (Matendo 14). Paulo anamuita Timotheo Mwanae katika imani (1 Timotheo 1:2), mtenda kazi pamoja naye (Warumi 16:21), mtumishi wa Mungu katika injili ya kristo (1 Wathesalonike 3:2) mwenye nia moja na yeye ya kujali waamini (wafilipi 2:19-23) na hivyo ndivyo alivyokuwa.

Paulo na Timotheo walionana mara ya kwanza huko Listra (Matendo 16:1-2) ambapo Timotheo alikuwa na sifa njema katikati ya waamini, Hivyo Paulo akamchukua ili kufanya naye kazi ya injili. Kwa kuwa Timotheo alikuwa na Baba myunani Paulo aliamua kumtahiri ili kutokutahiriwa kwake kusiwe kikwazo katika kazi ya injili. Timotheo alifanya kazi na Paulo tangu hapo mpaka Paulo alipofungwa mara ya mwisho kabla kifo chake, hii ndio maana Timotheo anatajwa katika nyaraka zote za mtume Paulo isipokuwa waraka kwa Wagalatia, Waefeso na Tito. Hii inaonyesha Paulo na Timotheo walikuwa Baba na mwana kweli kweli na watumishi wenza kweli kweli. Kwa ujumla Timotheo alikuwa na Sifa zifuatazo

1. Alikuwa na mizizi ya imani kutoka katika familia yake na hivyo katika ujana wake alikuwa na ujuzi wa maandiko ambayo alifundishwa tangu utoto na alikuwa na sifa njema katikati ya waamini. (2 Timotheo 1:5, 3:14-17 na Matendo 16:1-2).

2. Alikuwa ni mtumishi mwaminifu aliyefanya kazi na Paulo na Paulo alikuwa na uhakika kwamba Timotheo anaweza kumuwakilisha vema na kufanya kazi ya Mungu kwa uaminifu. (Wafilipi 2:19-23, 1 Wathesalonike 3:2 na 1 Wakorintho 4:17)

3.  Alikuwa na haiba ya woga na wasiwasi hivyo alihitaji kupewa maneno ya kutiwa ujasiri (1 Wakorintho 16:10-11). Msisitizo wa Paulo pia kwenye nyaraka hizi mbili unaonyesha Timotheo alikuwa na woga (1 Timotheo 4:12, 2 Timotheo 1:7-8). Uwogo huu labda ulisababishwa na uhalisi kwamba yeye alikuwa ni kijana mdogo na Paulo alimpa majukumu makubwa.

KANISA LA EFESO.

Kanisa la Efeso lilianzishwa na Mtume Paulo katika safari yake ya Pili ya kitume (Matendo 18:19) ambapo alikaa muda mfupi na kuwaaacha Priscila na Akila kwa ajili ya kuendeleza kazi ya kuhubiri na yeye akiahidi kurudi tena. Baada ya muda Apollo aliungana na Priscila na Akila huko Efeso. Paulo alirudi rasmi Efeso kwenye safari yake ya tatu ya kimishenari ambapo alikaa hapo Efeso kwa muda wa miaka mitatu (Matendo 19:8-10; 20:17-38 hasa 31) akihubiri na kufundisha. Hata baada ya miaka hiyo mitatu, Paulo alikuwa na ukaribu na viongozi wa kanisa la Efeso. Hii ndiyo maana kuna wakati aliwaita na kuwaonya kuhusu kulilinda kanisa huku akitabiri kwamba katikati yao kutatokea viongozi watakaofundisha mafundisho potofu (Matendo 20:17-38). Wakati wa kuandikwa kwa waraka huu wa pili, waalimu wa uongo walikuwa bado wako huko Efeso, pamoja na juhudi za Timotheo kuwapinga, kama Paulo alivyomkumbusha kufanya hivyo katika waraka wake wa kwanza. Hivyo, Paulo bado anamsisitiza Timotheo kuwapinga waalimu hao wa uongo katika waraka huu.

KUSUDI LA WARAKA.

Paulo aliandika waraka huu kwa Timotheo, kwanza kumtaka aende kwake haraka kwa kuwa alikuwa kwenye upweke na mateso ya kuwa gerezani (1:4; 4:9, 13, 21). Zaidi ya upweke na mateso ya gereza, Paulo alijua wakati wake wa kufa umekaribia (4:6), hivyo alitaka kumuona mwanawe mpendwa na mtumishi mwenza mwaminifu wa muda mrefu. Kwa kuwa alitaka Timotheo aende kwake haraka, alimpa taarifa nyingi kuhusu kile kilichomtokea na kinachoendelea kwa wakati huo (1:15-18 na 4:6-18).

Pili, Paulo alimuandikia Timotheo kumsisitiza kutunza (kubaki katika) kweli ya Injili ambayo Paulo alikuwa akiihubiri (1:13-14 na 3:14-15). Paulo alitaka Timotheo afundishe kweli hiyo kwa watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha wengine (2:1-2), na yeye mwenyewe aendelee kupingana na mafundisho potofu kwa kufundisha na kuhubiri kweli hiyo (4:1-5). Pamoja na hayo, Paulo anamtaka Timotheo asipingane na waalimu hao wa uongo kwa ugomvi wala kwa mashindano ya hoja za upumbavu, bali apingane nao kwa kuwafundisha kwa uvumilivu na upole ili yamkini Mungu awape kutubu na kuijua kweli (2:23-26).

MPANGILIO.

NambaMaandikoMaelezo
11:1-2Utangulizi
21:3-5Shukrani
31:5-18Kumtia Moyo Timotheo kwa kutumia hali yake kama mfano
 A1:5-12Chochea karama wala usionee haya injili hata kama inaleta Mateso
B1:13-14Shika na linda kweli ya Injili
C1:15-18Taarifa ya kilichotokea kwake
42:1-26Msisitizo wa kuwa hodari katika kuishindania Imani
 A2:1-7Shiriki na kubali taabu iletwayo na Injili
B2:8-13Yesu alistahimili, Mimi nastahimili na wewe stahimili
C2:14-26Usiwe kama waalimu wa Uongo
53:1-4:8Mwito wa kuhubiri na kuishi kweli katika picha ya wakati wa mwisho.
 A3:1-9Sifa za watu walio upande wa upinzani katika siku za mwisho
B3:10-17Sifa zako Timotheo na za wale walio upande wa kweli
C4:1-5Hubiri hata kama watakataa kweli
D4:6-8Mimi nimefanya vizuri na kazi nimemaliza
64:9-18Taarifa kwa Timotheo
74:19-22Salamu za Mwisho

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.

Waraka huu una muundo kama waraka ulivyotakiwa kuwa, yaani una Utangulizi (1:1-2), Shukrani (1:3-5), Ujumbe mkuu (1:6-4:8) na Mwisho wa Barua (4:9-22). Mwisho wa Barua una sehemu mbili yaani Taarifa kwa Timotheo (4:9-18) na Salamu za Mwisho (4:19-22). Utanguzili una sehemu Tatu kama ilivyokuwa kawaida yaani kuna anuani ya Mtuma waraka (1:1), anuani ya mpokeaji (1:2a) na Salamu (1:2b). Japo si kila waraka ulikuwa na Shukrani lakini nyaraka nyingi zilikuwa na shukrani baada tu ya utangulizi kama waraka huu (1:3-5).

Baada ya shukrani Paulo anaingia kwenye ujumbe wake mkuu (1:6-4:8). Ujumbe mkuu wa barua hii unaweza kugawanywa katika sehemu kuu tatu.

Sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu (1:6-18), Paulo anamkumbusha Timotheo kuchochea/ kuendelea kutumia karama yake ya kuhubiri injili na kumsisitiza asiionee haya hiyo injili (Ushuhuda wa Yesu) hata kama inaleta mateso, ambapo Paulo yeye amekwisha yapata na anayastahimili (1:6-12). Pili, Paulo anamtaka Timotheo kuendelea kuishika na kuilinda kweli hiyo ambayo ameisikia kutoka kwa Paulo kwa muda mrefu kwa msaada wa Roho mtakatifu (1:13-14). Mwisho katika sehemu hii ya kwanza Paulo anampa taarifa Timotheo ya kumuonyesha kuwa watu wa Asia walimtelekeza (waliomuonea haya na kumuepuka) lakini Onesiforo hakumuonea haya wala hakumuepuka (1:15-18). Hivyo Paulo anamtaka Timotheo pia asimuonee haya.

Sehemu ya Pili ya Ujumbe mkuu (2:1-26), Paulo anamtaka Timotheo akubali kushiriki mateso yatokanayo na injili na awafundishe watu waaminifu injili hiyo ili wao nao wawafundishe wengine. Hii ni kwa sababu Timotheo yuko kwenye upinzani mkali na waalimu wa uongo. Paulo anatumia mifano mitatu ya kumtaka yeye pia apigane vita hii vizuri, mfano wa kwanza ni wa askali wa vita, wa pili, ni wa mwanariadha mshindani na wa tatu ni wa mkulima (2:1-7). Paulo pia anamtaka Timotheo amkumbuke Yesu aliye mfano halisi wa ustahilivu wa mateso, ambaye pia amemfanya Paulo kuingia kwenye mateso hata kufungwa gerezani lakini anastahimili mambo hayo yote (2:8-10). Katika kuendelea kumsisitiza kustahimili mateso anamuandikia ushairi huu;

Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia;

Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye;

Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi;

Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. (2:11-13)

Paulo anamalizia sehemu hii ya pili ya ujumbe mkuu kwa kumtaka Timotheo na watu walio upande wake wajiepushe na mashindano ya maneno yasiyo na maana, wajiepushe na mafundisho ya uongo wa waalimu wa uongo na wajiepushe na magomvi yatokanayo na maswali ya  upumbavu. Kwa kufanya hivyo wao watakuwa vyombo vyenye heshima, vilivyosafishwa, vimfaavyo Bwana, vimetengenezwa kwa ajili ya kila kazi iliyo njema.  Upande wa pili, Paulo anamuonyesha yeye Timotheo aweje, atumie neno la kweli kwa halali, azikimbie tamaa za ujanani, ukafuate haki, imani, upendo, na amani na awaonye kwa upole wao washindanao naye/waalimu wa Uongo (2:14-26).

Sehemu ya tatu ya Ujumbe mkuu (3:1-4:8), Paulo anaanza na kumuonyesha Timotheo kwamba hali ya watu itaendelea kuwa mbaya zaidi, hali hiyo mbaya ni wale wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake. Kukana nguvu zake ni kuipinga injili ya kweli kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa[[1]]. Watu hawa wanapingana na kweli kwa kuwa wameharibika akili zao na wamekataliwa kwa mambo ya imani. Pamoja na kwamba uongo wa watu hawa utadhihirika kwa watu wote lakini tayari wameshawateka wanawake kadhaa na uongo wao (3:1-9)[[2]]. Paulo anasema anajua Timotheo yeye hayuko kama hao maana yeye amefuata mafundisho yake, mwenendo wake, makusudi yake, imani, Upendo, uvumilivu, saburi na mateso (3:10-11). Paulo anamwambia Timotheo njia hii aliyoifuata ina mateso sio kwake tu bali kwa wote watakaokuishi maisha ya utauwa, lakini njia ya upande wa pili hiyo ni ya kuzidi katika Uovu, kudanganyana na kudanganyika tu. Paulo anamtaka Timotheo aendelee kwenye njia ya kwanza, njia ya kweli na ya mateso kwa kuwa anawajua waliyomfundisha njia hiyo na zaidi amejifunza njia hiyo kupitia maandiko matakatifu tangu utoto. Maandiko hayo Paulo anasema yana pumzi ya Mungu na yanafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki, ili watu wa Mungu wawe kamili, wamekamilishwa wapate kutenda kila tendo jema (3:12-17).[[3]]

Paulo mwisho wa sehemu hii ya tatu anamtaka Timotheo atimize kazi yake ya uhubiri wa injili kwa kufundisha, kukaripia, kukemea na kuonya pamoja na uhalisia kwamba watu watajiepusha wasisikie kweli na hata wakisikia watakataa mafundisho hayo yenye Uzima na kuzigeukia hadithi za Uongo na hivyo watajipatia waalimu makundi makundi (4:1-5). Paulo anamtaka Timotheo afanye hivyo kwa kuwa yeye amefanya kwa sehemu yake, imani ameilinda na kazi ya kuhubiri ameimaliza anachosubiri ni taji ya haki tu kutoka kwa Bwana ambaye atawapa wote wanaomsubiri (4:6-8).

Baada ya kumaliza Ujumbe wake mkuu Paulo anafunga waraka wake kwa kumpa Timotheo taarifa mbalimbali (4:9-18) na anahitimisha kwa salamu (4:19-22). Kwenye taarifa hiyo Paulo anamuonyesha Timotheo tena kwamba watu wamemtelekeza (Dema mmoja wapo), wengine amewatuma kwenye kazi (Tito mmoja wapo) na Luka peke yake ndio yuko pamoja naye. Hivyo anamtaka Timotheo aje kwake upesi na aje na vitu alivyoviacha huko Troa. Paulo anasema kwenye kusikilizwa kesi yake kwa mara ya kwanza (jawabu langu la kwanza) wote hawakusimama upande wake lakini Bwana Yesu alisimama pamoja naye akamtia nguvu na Bwana huyo huyo atamhifadhi hata afike katika ufalme wa Mbinguni. Lakini pia anamjulisha Timotheo kwamba ajiepushe na mtu hatari aitwaye Iskanda anayefua shaba (4:9-18).

Katika salamu za mwisho, Paulo anamtaka Timotheo awasalimie watu walioko huko Efeso na pia anampa Timotheo salama za watu wa kanisa la Rumi na anawataja majina watu wanne. Watu hawa hawakuwa sehemu ya timu ya watenda kazi pamoja naye, ndio maana alisema Luka pekee yuko pamoja naye. Na anamaliza na usemi wa mwisho wa neema (4:19-22).



FOOTNOTES


[1] Yane na Yambre ni majina ya waganga wa Kimisri walioshindana na Musa wakati Mungu alipomtuma kumpa ujumbe Pharao wa kutaka kuwaruhusu waisraeli waondoke Misri (Kutoka 7:10-13, 20-22 na 8:5-7, 17-18).

[2] Ni dhahiri kwamba wanawake wa Efeso walikuwa wameathiriwa sana na waalimu hawa wa uongo. Ndio maana barua zote mbili kwa Timotheo zinaonyesha wanawake wameathiriwa na Uongo huo na wanatumika kuueneza pia (Soma 1 Timotheo 5:11-15 hasa 13 na 15 na 2 Timotheo 3:6). Ujuzi huu utakusaidia kuelewa kwa nini Paulo anakaza wanawake kufundisha katika kanisa (1 Timotheo 2:11-15).

[3] Maandiko haya Paulo anayoyasema ni maandiko ambayo leo tunayaita Agano la kale. Kwa wakati huu kanisa lilitumia Maandiko hayo kufundisha na kuhubiria kwa kuwa hakukuwa na maandiko ambayo Leo tunayaita Agano jipya.

UFAFANUZI WA WARAKA WA PILI WA MTUME PAULO KWA TIMOTHEO..

Unakuja hivi karibuni…….