MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA PILI WA MTUME PAULO KWA WAKORINTHO
MAELEKEZO
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI
Kama wewe ni kiongozi wa Kanisa la Mungu la mahali pamoja na umekuwa ukifanya utumishi wako wa kuwaongoza watu wa Mungu kwa juhudi na kwa uaminifu mkubwa, lakini umekuwa ukipata mashambulizi kutoka kwa wapinzani ambao si watumishi wa kweli wa Mungu, bali wa Shetani, lakini wanaojigeuza na kujifanya kuwa watumishi wa Mungu, basi waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho ni waraka muhimu sana kwako kuusoma kwa kina.
Ikiwa haujaishia tu kupata mashambulizi kutoka kwa wapinzani wa namna hiyo, lakini pia umepata mashambulizi kutoka kwa waamini ambao umekuwa ukiwaongoza kwa sababu wameshawishiwa na watumishi hao wa Shetani, basi waraka huu unakufaa. Inawezekana waamini hao wamekuwa wakikulinganisha na watumishi hao feki na, kwa sababu ya vipimo vya kimwili, wakakuona wewe ni mdogo na watumishi hao feki wakaonekana kuwa wakubwa. Basi kitabu muhimu cha kujifunza hekima ni waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho.
Kwa upande mwingine, kama wewe ni mwamini ambaye si kiongozi katika Kanisa la mahali pamoja na umekuwa kwenye mgogoro unaomhusisha kiongozi (au viongozi) wako ambaye, kwa sifa za kiroho, ni kiongozi anayefanya kazi ya Mungu kwa uaminifu na hafanyi kazi yake ya utumishi kwa ajili ya kujipatia kipato, wala hana namna yoyote anayofanya kuwalemea kwenye mahitaji yake, basi waraka huu ni waraka muhimu sana kukusaidia kujifunza namna ya kutokuwa upande usio wa haki.
Lakini pia, waraka huu utakusaidia kujua ni kwa viwango gani unatakiwa kupima utumishi wa viongozi wako katika kanisa. Mbali na hivyo, kwa kuwa wewe pia ni mtumishi wa Mungu, basi waraka huu ni muhimu kwako kwa kuwa utakupa sifa sahihi unazotakiwa kuzitumia pale utakapoamua kupima utumishi wako. Mwisho, lakini si kwa umuhimu, kama unataka kujifunza kuhusu utoaji kama unavyofundishwa na Agano Jipya, waraka huu ni muhimu sana kwako. Hii ni kwa sababu waraka huu una maelezo marefu zaidi kuhusu utoaji kuliko sehemu nyingine yoyote ya maandiko ya Agano Jipya. Kupitia waraka huu, utajifunza lengo la kutoa, msukumo sahihi wa kutoa, njia za kutoa, nidhamu katika utoaji, usimamizi wa matoleo na mambo mengine mengi.
KANISA LA KORINTHO NA MTUME PAULO
Kanisa la Korintho lilizaliwa katika safari ya pili ya kimishenari ya Mtume Paulo. Katika safari hii, Paulo alifika Korintho kutoka Athene akiwa peke yake. Alipofika aliungana na Akila na Prisila waliokuwa wametoka Rumi baada ya wayahudi wote kufukuzwa. Wote wakakaa pamoja na wakafanya kazi pamoja huku Paulo akihubiri injili katika sinagogi kila Jumamosi. Baadaye Timotheo na Sila walifika Korintho wakitokea Makedonia wakaungana na Paulo katika kazi ya kuhubiri injili (2 Wakorintho 1:19). Baada ya Wayahudi kukataa injili, Paulo akaacha kwenda kwenye sinagogi akaamua kuhubiria kwenye nyumba ya Tito Yusto, mmataifa aliyekuwa na imani ya Kiyahudi. Nyumba ya Tito ilikuwa karibu kabisa na sinagogi ambalo Injili ya Paulo ilikataliwa (Matendo 18:1-7). Baada ya mkuu wa sinagogi aitwaye Krispo na nyumba yake yote kuamini, Wakoritho wengi wakaamini na kubatizwa (Matendo 18:8 na 1 Wakorintho 1:14-16). Pamoja na upinzani mkubwa, Paulo na timu ya kimisheni (akiwemo Timotheo, Sila, Akila na Prisila) walikaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu katika kupanda na kulielea kanisa. Uamuzi huu ulifikiwa baada ya Paulo kuambiwa na Bwana aendelee kukaa huko kwa kuwa yeye Bwana ana watu wengi katika mji huo (Matendo 18:10).
Baada ya muda huo, Paulo na timu wakaondoka Korintho na kuelekea Efeso. Huko Efeso, Paulo akakaa kwa muda mfupi na akaamua kwenda Yerusalemu akiwaacha Prisila na Akila Efeso. Safari yake hii ya pili ya kimishenari ikaishia kwa Paulo kurejea Antiokia kutoka Yerusalemu (Matendo 18:18-22).
Baada ya kukaa kwa muda kadhaa Antiokia, Paulo akaanza safari yake ya tatu ya kimishenari, ambayo alitumia muda mrefu katika mji wa Efeso. Akiwa Efeso kwa utumishi wa takribani miaka miwili, Paulo ndipo aliandika waraka ambao aliwasihi Wakorintho wasichangamane na wazinzi (1 Wakorintho 5:9), waraka ambao hatuna katika Biblia zetu. Katika kipindi hicho hicho, Paulo kwa kupata habari ya mambo yalivyokuwa yanaendelea katika kanisa la Korintho akaandika waraka wake ambao tunautambua kama waraka wa kwanza kwa kanisa la Korintho. Waraka huo mtume Paulo akautuma pamoja na Timotheo (1 Wakorintho 4:17; 16:10-11), huku akitoa ahadi kwamba yeye mwenyewe atakwenda Korintho akipita Makedonia kwanza (1 Wakorintho 16:5).

Mchoro 1. Mpango wa kwanza wa safari wa Mtume Paulo kama anavyosema katika 1 Wakorintho 16:5.
Barua hiyo, Mtume Paulo aliandika kushughulika na matatizo mbalimbali katika kanisa la Korintho, ikiwemo swala la mgawanyiko na swala la zinaa katika Kanisa. Mbali na matatizo hayo, Paulo aliandika pia barua hii kuwataka Wakorintho kuhusika na kutoa sadaka kwa ajili ya kanisa la Yerusalemu.
Pamoja na barua hiyo, hali ya Kanisa la Korintho haikurekebika, bali ilikuwa mbaya zaidi. Inaonekana mgawanyiko wala zinaa havikukoma katika kanisa (2 Wakorintho 12:20-21; 13:2). Na zaidi, kukaibuka upinzani mkubwa dhidi ya Paulo ambao inaonekana ulichochewa na adui mmoja wa Mtume Paulo (2 Wakorintho 2:5-11;7:8-13). Kutokana na hali kuwa mbaya Timotheo akarudi Efeso na kurejesha taarifa za hali ilivyo katika Kanisa. Kutokana na taarifa hizo, Mtume Paulo akasafiri kutoka Efeso mpaka Korintho ghafla, kinyume na ratiba yake aliyokuwa ameipanga na kuwajulisha Wakorintho hapo awali (1 Wakorintho 16:5). Safari hii inafahamika kama safari ya huzuni (2 Wakorintho 2:1; 12:14; 13:1), kwa kuwa uhusiano kati ya mtume Paulo na Kanisa uliingia kwenye mgogoro mkubwa. Katika mgogoro huu inaonekana mamlaka ya kitume ya Mtume Paulo yalikataliwa na adui wake mmoja katika Kanisa na Kanisa likabebwa na ushawishi wa mtu huyo (2 Wakorintho 2:1-11). Kutokana na mgogoro huo, Mtume Paulo akaamua kuondoka Korintho na kurejea Efeso, huku akiahidi atarudi tena Korintho kabla ya kwenda Makedonia, ili wao wamsafirishe kwenda huko na akitoka Makedonia atarudi tena Korintho ili tena wamsafirishe kwenda Yerusalemu (2 Wakorintho 1:15-16)

Mchoro 2. Mpango wa pili wa safari wa Mtume Paulo kama anavyosema katika 2 Wakorintho 1:15-16.
Kutokana na safari hii ya huzuni kuto kuleta matunda, Mtume Paulo aliporejea Efeso akaghairi kurudi tena Korintho (2 Wakorintho 1:23-2:1), badala yake akaandika waraka mwingine kwenda kwa Wakorintho, waraka ambao nao hatuna kwenye Biblia zetu lakini unaitwa Waraka wa huzuni (2 Wakorintho 2:3–4 na 7:8–12). Katika Waraka huo, Mtume Paulo akawajulisha Wakorintho kwamba hataenda tena kwao kabla ya kwenda Makedonia (2 Wakorintho 1:15-24). Inaonekana waraka huu ulijaa na makalipio ya Mtume Paulo kwa wakorintho, ndio maana unaitwa Waraka wa huzuni. Waraka huu akampa Tito kwenda nao Korintho. Kutokana na waraka huu kuwa na makaripio na kutokana na Mtume Paulo kuondoka kwenye safari yake ya huzuni, hii ndio sababu wapinzani wake waliweza kumsema kwamba “Nyaraka zake ni nzito, hodari; bali akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake si kitu” (2 Wakorintho 10:10).
Baada ya waraka huu, Kanisa likatubu na likamshughulikia adui wa mtume Paulo. Kwa kufanya hivyo, Kanisa likaonyesha kumaliza mgogoro wao na Mtume Paulo. Paulo alipata taarifa hizi alipokutana na Tito Makedonia baada ya kutoka Efeso (2 Wakorintho 7:5-16). Kumbuka, Efeso Mtume Paulo aliondoka baada ya ghasia zilizofanywa na wakazi wa Efeso zilizoanzishwa na Demetrio (Matendo 19:24-41).
Baada ya taarifa hizo nzuri, Mtume Paulo akaamua kuandika waraka mwingine, ambao ndio tunautambua kama waraka wa pili kwa Wakorintho. Pamoja na taarifa hizo nzuri, inawezekana pia taarifa ya Tito ilionyesha kwamba kuna ujio wa mitume wa uongo ambao pia ni maadui wa Mtume Paulo, ndiyo maana sura ya kwanza mpaka ya tisa ni sura zenye kuongelea hali iliyopita kwa lugha chanya, wakati sura ya kumi mpaka kumi na tatu ni sura zenye kuongelea hali ya udanganyifu wa mitume wa uongo unaoendelea na upinzani wao dhidi ya Mtume Paulo. Pamoja na barua hii mtume Paulo akamtuma Tito na ndugu wengine wawili ili wakalimishe ukusanyaji wa sadaka katika kanisa la Korintho kabla yeye hajafika pamoja na watu wengine kutoka makedonia ili waendenazo Yerusalemu.

Mchoro 3. Safari ya Mtume Paulo baada ya kuandika waraka wa pili kwa Wakorintho. Safari hii ni tofauti na mpango wake kama ulivyooneshwa katika mchoro 2.
KUSUDI LA WARAKA.
Barua hii, Mtume Paulo aliandika kwa makusudi makubwa matatu. Moja, kuwathibitishia Wakorintho upendo wao (yeye, Timotheo na Tito) hata baada ya kuwepo kwa mgogoro kati yao, ambao ulikuwa umeisha baada ya taarifa njema za Tito (2 Wakorintho 1-7). Pili, ni kuwahimiza Wakorintho kumaliza kazi ya utoaji kwa ajili ya kanisa la Yerusalemu, jambo ambalo walikuwa wameanza toka mwaka uliopita (2 Wakorintho 8-9). Tatu, kuwapinga mitume wa uongo waliovamia Kanisa na kumshambulia yeye (2 Wakorintho 10-13).
MPANGILIO WA KITABU
| MAELEZO | 2 WAKORINTHO |
| UTANGULIZI Salamu na Shukrani | 1:1-11 |
| SEHEMU YA KWANZA YA UJUMBE | |
| Utetezi wa nia, mwenendo na maamuzi ya Paulo | 1:12-2:13 |
| Utumishi wa kweli jinsi ulivyo | 2:14-7:4 |
| Utetezi wa waraka wa Huzuni | 7:5-16 |
| SEHEMU YA PILI YA UJUMBE | |
| Kutoa kwa ajili ya wakatifu | 8:1-15 |
| Kazi na kusudi la Tito kwenda Korintho | 8:16-9:5 |
| Faida za kutoa kwa ajili ya Watakatifu | 9:6-15 |
| SEHEMU YA TATU YA UJUMBE | |
| Utofauti wa Paulo na wapinzani wake | 10:1-18 |
| Utangulizi kabla ya kujisifu kama mpumbavu | 11:1-21 |
| Kujisifu kama mpumbavu | 11:22-12:13 |
| SEHEMU YA NNE YA UJUMBE | |
| Nitakapokuja sitawalemea | 12:14-21 |
| Wasio tubu dhambi sitawahurumia | 13:1-10 |
| MWISHO WA BARUA | |
| Mausia ya mwisho na salamu za mwisho | 13:11-14 |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI
Barua hii kama barua nyingine inaanza na anuani na salamu (1:1-2). Baada ya anuani na salamu, Mtume Paulo anamtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tofauti na kawaida yake ya kumtukuza Mungu au kumshukuru kwa ajili ya yale aliyoyafanya kwa wapokeaji wa ujumbe wake,[1] katika barua hii anamtukuza Mungu kwa ajili ya faraja yake juu yake yeye na timu nzima ya injili, waliyoipata katikati ya mateso makali (1:3-7). Katika kumtukuza Mungu kwa faraja, anawajulisha Wakorintho jinsi dhiki waliyoipata Asia ilivyokuwa kubwa. Katika ukubwa wake, dhiki hiyo iliwafanya Paulo na timu ya injili kuacha kujitegemea wenyewe na kumtegemea Mungu pekee, “awafufuaye wafu,” (1:8-11).[2]
Sehemu ya kwanza ya Ujumbe mkuu
Baada ya utangulizi huo, Mtume Paulo anakwenda kwenye ujumbe mkuu wa barua yake. Katika sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu, Paulo anatetea utume wake dhidi ya mashtaka ya wakosoaji wake (1:12–7:16). Lengo la utetezi huu ni kuendelea kuwataka Wakorintho wapatane na yeye kwa dhati na pamoja na timu nzima ya injili. Katika utetezi wake, Paulo anatumia hoja mbili za msingi: kwanza, anatetea nia, mwenendo, na maamuzi yake (1:12–2:13); kisha anaeleza kwa ufasaha utumishi wa kweli katika Kristo ukoje (2:14–7:16).
Utetezi wa nia, mwenendo na maamuzi yake
Paulo anaanza kujitetea dhidi ya mashtaka waliyopewa kwa kueleza kwamba wao wanaujasiri wa kujisifu kutoka kwenye dhamira zao kwamba walienenda kwa utakatifu na kwa weupe wa moyo kwao Wakorintho na kwa dunia, kama Wakorintho wanavyokubali kwa sehemu (1:12-14). Paulo anasema kutokana na sifa zake hizo, alipanga kwenda Korintho kabla ya kwenda Makedonia ili aweze kurudi tena Korintho kabla ya kwenda Yudea/Yerusalemu. Kutokutimia kwa mpango huu haikuwa kwa sababu yeye ni kigeugeu, kwa kuwa, Mungu na injili waliyoihubiri sio kigeugeu (1:15-22). Sababu ya kughairi mpango huo ilikuwa ni kutokutaka kuwatembelea kwa ziara nyingine ya huzuni. Hata lengo la kuandika waraka wa huzuni ilikuwa ni hivyo hivyo; kutokuwahuzunisha tena watakapoonana (1:23-2:4). Anaongeza kwa kusema, jambo alilolipitia lililosababishwa na yule adui aliyempinga halikumhuzunisha yeye tu, bali Kanisa zima pia. Pamoja na hivyo, Paulo anasihi Kanisa kumsamehe adui huyo maana amekwisha pata adhabu ya kutosha. Baada ya kuwasihi kufanya hivyo anaeleza lengo lingine la kuandika waraka wa huzuni: aliandika ili kuujaribu utii wao. Kisha, anasisitiza kwamba amemsamehe yule adui, na kwamba amefanya hivyo kwa ajili ya manufaa ya Kanisa, kwa kuwa hataki Shetani, mwenye hila, aitumie hali hiyo kujipatia nafasi (2:5-11). Mwisho, Paulo anatoa taarifa kwamba alipofika Troa hakuwa na raha nafsini mwake, kwa kuwa hakuonana na Tito kama alivyotarajia. Alipomkosa Tito akaamua kuendelea na safari mpaka Makedonia (2:12-13). Taarifa hizi zitaendele sura ya 7:5-16, hapa katikati, yaani 2:14-7:4 ni mchepuko wa kifasihi.

Mchoro 4. Mchepuko wa kifasihi katika 2 Wakorintho.
Utumishi wa kweli katika Kristo ukoje?
Paulo, kabla ya kuendelea na kueleza nini kilifuata baada ya kufika Makedonia, anaamua kueleza kwanza kwa kirefu kuhusu utumishi wa kweli ulivyo, huku akijielezea yeye na watumishi wenza kama mfano bora wa utumishi huo. Lengo la kueleza hivyo ni kuendelea kuwataka Wakorintho wapatane naye kwa dhati pamoja na timu nzima ya injili.
Paulo anasema, pamoja na kukosa raha nafsini mwake anamshukuru Mungu ambaye anawaongoza daima katika msafara wa ushindi katika Kristo. Mungu kwa kufanya hivyo, anaeneza harufu ya kumjua yeye kwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea. Kwa wanaopotea harufu hii huleta mauti na kwa wanaookolewa huleta uzima. Kwa ujumla Paulo anasema matukio yote ya maisha yake yanaongozwa na Mungu ambaye anaeneza harufu ya kumjua yeye ambayo inawagawa watu katika uzima na mauti (2:14-16a). Baada ya kutaja matokeo hayo ya injili, mtume Paulo anauliza, Nani anafaa kwenye kazi ya namna hiyo? (2:16b). Kwa kujitofautisha na “walighoshio neno la Mungu” Paulo anajibu kwamba, wenye weupe/unyoofu wa moyo ndio wanafaa kwa kazi hiyo na anajiweka yeye na wenzie katika kundi hili (2:17). Baada ya kujiweka katika kundi la watu wanaofaa kwa kazi ya injili, anatoa utetezi kwamba wao wanastahiri kujiweka kwenye kundi hilo kwa kuwa wao hawahitaji barua iliyoandikwa kwa mkono kuthibitisha unyoofu wao katika injili, kwa kuwa Wakorintho wao wenyewe ni barua ya kuthibitisha unyoofu wao, iliyoandikwa kwa Roho wa Mungu aliye hai na si katika vibao vya mawe (3:1-3). Mwisho anakiri unyoofu huo hautokani na wao wenyewe bali na Mungu (3:4-6).
Hapo juu, Paulo ametofautisha kati yake na wahubiri wenzake kwa upande mmoja, na wahubiri wengine wanaoghoshi Neno la Mungu kwa upande mwingine, ambao wao wanategemea barua za uthibitisho zilizoandikwa kwa mikono. Anaonyesha kwamba yeye na watumishi wenzake ni wanyoofu, hawaghoshi Neno la Mungu, wala hawahitaji barua za uthibitisho, kwa kuwa uwepo wa kanisa la Korintho ni barua ya kweli ya uthibitisho wa kazi yao, ambayo imeandikwa na Roho wa Mungu na si kwa maandishi ya mikono.[3]
Kwa kuwa mada hii ya kuandikwa kwa Roho na kuandikwa kwa mikono inaweza kufananishwa na Agano la kwanza la sheria, lililoandikwa kwa mkono wa Mungu, na Agano la pili, ambalo manabii walitabiri kuwa litaandikwa na Roho katika mioyo (tazama, Yeremia 31:31–34 na Ezekieli 36:26–27), basi Paulo anaingia katika kutofautisha maagano haya mawili, huku akionyesha Agano jipya ni bora. Na lengo la kuonyesha kwamba Agano jipya ni bora ni kuonyesha kwamba utumishi wao ni bora kuliko ule wa wapinzani wao.[4]
Paulo anasema, ikiwa huduma ya Agano la kwanza, iliyoleta mauti, ilikuja na utukufu kiasi kwamba Waisraeli hawakuweza kumtazama Musa, pamoja na kwamba utukufu huo haukuwa wa kudumu (ulikuwa unabatilika), basi huduma ya Agano jipya, ambayo inaleta uzima, ina utukufu zaidi. Kutokana na utukufu zaidi wa huduma ya Agano Jipya, wao (Paulo na wenzake) wananena kwa ujasiri, si kama Musa aliyejifunga utaji juu ya uso wake (3:7–12). Paulo anaongeza kwamba, kwa Waisraeli kumtazama Musa mwenye utaji, mioyo yao ilitiwa uzito wa kuelewa Agano la kwanza, na hivyo hata leo hawalielewi linaposomwa. Kinyume na wao, wale walioamini, ambao kati yao na Bwana hakuna utaji, wanautazama utukufu wa Bwana kama vile wanavyotazama kwenye kioo, na hivyo wanabadilishwa ili wafanane na Bwana kutoka utukufu hadi utukufu (3:13–18).
Kama ambavyo huduma ya Agano Jipya ilivyo na utukufu bora zaidi, ndivyo walivyo pia watumishi wake. Watumishi wake ni wenye haki; hawaenendi kwa hila, wala hawalichanganyi Neno la Mungu na uongo (4:1–2). Lakini pamoja na sifa hizo, Injili yao haikubaliwi na wote, kwa kuwa wapo waliopofushwa fikra na mungu wa dunia hii (4:3–4). Injili ambayo mungu wa dunia hii amewapofusha wengine wasiiamini inahusu Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana na haihusu habari za wahubiri (4:5–6).
Pamoja na kuwa na huduma yenye utukufu uzidio, Paulo anakiri kwamba huduma hii (hazina) wanayo katika miili yenye udhaifu (yaani, vyombo vya udongo) ili nguvu izidio ya huduma hii itoke kwa Mungu na sio kwao wanadamu. Hii ndio sababu wanapitia changamoto katika mwili kama vile kudhiakiwa, kuona shaka, kuudhiwa na kutupwa chini, yote haya yakiwa kwa ajili ya Wakorintho. Pamoja na changamoto hizo, Paulo anasema hawakati tamaa. Moja, ni kwa sababu wanajua kwamba mateso yao ya sasa ni ya muda tu na kazi yake ni kuwafanyia utukufu uzidio katika maisha ya umilele (4:7-18). Pili, ni kwa sababu wanajua hata kama mwili huu wa duniani utaharibiwa, wanao na wanatarajiwa kuvikwa mwili utokao mbinguni kwa Mungu aliyewapa Roho sasa kama malipo ya awali (5:1-5). Baada ya kueleza sababu hizo, ambazo zote zinaonyesha tumaini lao liko kwenye maisha baada ya ufufuo, Paulo anakiri kwamba wanatamani watoke katika mwili huu ili waende kuwa na Bwana, kwa kuwa sasa wako mbali naye. Lakini pamoja na kuwa mbali naye sasa, bado wanafanya jitihada kumpendeza yeye kwa kuwa imewapasa kwenda mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo kwa ajili ya malipo ya jinsi walivyoishi katika mwili huu wa sasa (5:6-10).
Baada ya Mtume Paulo kueleza kuhusu ubora wa huduma ya Agano Jipya, udhaifu walionao sasa wahudumu wake na tumiani walilonalo, anaingia kwenye kilele cha kusisitiza Wakorintho kupatana naye kwa kuwa anasifa za utumishi wa kweli.
Paulo anaanza kwa kusema, kwa sababu ya uhalisia wa hatima yetu mbele za Mungu,yeye pamoja na wale walio pamoja naye wanawashawishi watu kwa uwazi na unyoofu ambao Mungu anauona, na ambao wanatumaini kuwa Wakorintho wanauona pia. Kusema kwamba wanatumaini kwamba unyoofu wao Wakorintho wanauona, hawajasema ili wajisifu wenyewe mbele za Wakorintho tena, bali kuwapa nafasi ya kuwa na mambo ya kujisifu kwa ajili yao dhidi ya wale wanaojisifia mambo ya utu wa nje tu (5:11-13). Zaidi, kinachowafanya Paulo na wenzie kuwashawishi watu kwa unyoofu na kutokujisifu kwa mambo ya nje ni upendo wa Kristo ambao umewafanya wao kutokuwatazama watu kwa jinsi ya mwili/utu wa nje, kwa kuwa mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, kwa hiyo hawezi kutazamwa kwa namna ya nje tu (5:14-17). Mambo yote Paulo aliyoyataja hapo juu, yaani upendo wa Kristo, mabadiliko ya namna ya kuwatazama watu na uumbaji mpya ndani ya Kristo, vyatokana na Mungu aliyewapatanisha Paulo na wenzie na nafsi yake, na kuwapa huduma ya upatanisho. Na kwa sababu wanafanya kazi pamoja na Mungu ndiyo maana wanawasihi Wakorintho wasiipokee neema ya Mungu bila kuleta matokeo kwa kuwa wakati sahihi ni sasa (5:18-6:2).[5]
Ili kusisitiza kwamba Wakorintho wanatakiwa kupatana naye, Paulo anaeleza sifa za utumishi wa kweli walizanazo yeye na watumishi wenzake (6:3-10). Kufikisha kwenye kilele ujumbe wake, Paulo anawasihi Wakorintho kufungua mioyo yao (kuelekea upatano wa dhati) kama wao, yaani Paulo na wenzie walivyofungua vinywa vyao kwa uwazi na mioyo yao pia (6:11-13). Baada ya kuwasisitiza Wakorintho kutokuweka mapatano na wale wasioamini na zaidi kujitenga nao (6:14-7:1), Paulo anarudi tena kuwasisitiza Wakorintho kufungua mioyo yao kwake na kuruhusu aingie mioyoni mwao kama yeye na timu yake walivyowajawa na Wakorintho mioyoni mwao (7:2-4).
Baada ya mchepuko wa kifasihi kuisha, Mtume Paulo anarejea pale alipoishia kueleza kuhusu hali yake na safari yake baada ya kufika Makedonia (tazama mchoro 4). Paulo anasema kwamba alipofika Makedonia, hali haikuwa nzuri pia kwa sababu ya upinzani wa nje na wa ndani. Hali hii ilibadilika pale walipopata faraja baada ya Tito kuungana nao, akiwa na taarifa njema za Wakorintho kutubu baada ya kupokea waraka wa huzuni (7:5–7). Paulo anaongeza kusema kwamba, pamoja na ukweli kwamba waraka huo uliwahuzunisha, hajuti kwa sababu huzuni hiyo ilikuwa ya muda mfupi na, mwisho wa siku, ilizaa toba kwa Wakorintho, jambo ambalo liliwafariji (7:8–13a). Paulo anamalizia kwa kuonyesha kwamba si tu taarifa njema za Tito zilizowapa faraja, bali pia furaha aliyokuwa nayo Tito baada ya Wakorintho kuitikia vizuri waraka wa huzuni iliongeza faraja kwa Mtume Paulo (7:13b–16).
Sehemu ya pili ya ujumbe mkuu
Baada ya sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu ambayo Paulo alijikita kutetea utume wake dhidi ya mashtaka ya wakosoaji wake, sehemu ya pili Mtume Paulo anajikita katika kuwataka Wakorintho kukamilisha utoaji wao kwa ajili ya wakatifu walioko Yerusalemu. Katika jambo hili, Mtume Paulo anaanza kwa kutoa mfano chanya wa utoaji ulioonyeshwa na makanisa ya Makedonia (8:1-5) kwa lengo la kuwataka Wakorintho kuwa na wingi wa ukarimu kama walivyo na wingi katika mambo mengine (8:6-7). Baada ya mwito huo wa kutoa, Paulo anatoa ufafanuzi wa maelekezo yake ya kuhusu kutoa ili asieleweke vibaya. Anasema kwamba, mwito wake wa kuwataka wao kutoa si amri, bali ni mwito wa kufuata mfano bora wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye aliacha utajiri wake kwa ajili yetu. Anaendelea kufafanua kwa kuwataka Wakorintho watoe sawasawa na walivyo navyo, huku wakitambua kwamba utoaji si kwa ajili ya kufaidisha kundi moja na kulielemea kundi jingine, bali ni kwa ajili ya kuleta usawa kwa kuzingatia mahitaji (8:8–15).
Baada ya hatua hiyo, Paulo anaeleza sababu za Tito kuja kwao akiwa pamoja na waamini wengine wawili ambao hajawataja majina yao. Zaidi ya hayo, akitarajia upinzani, anaeleza sifa bora za watu hawa ili Wakorintho wawapokee (8:16–24). Baada ya kutaja sifa zao, Paulo anaeleza kwamba kusudi la kuwatuma watu hawa kabla ya yeye kwenda ni kuhakikisha kwamba Wakorintho wanakamilisha utoaji wao, kama walivyokuwa tayari kufanya kwa mwaka mzima. Lengo la kukamilisha matoleo haya kabla ya Paulo kufika Korintho ni ili asiaibike mbele ya watu wa Makedonia, ambao amekuwa akijisifia utayari wa Wakorintho (9:1–5).
Mwisho wa sehemu hii ya pili ya ujumbe mkuu, Mtume Paulo anaeleza faida za utoaji ambao amekuwa akiwasisitiza Wakorintho kuufanya. Faida hizi ziko kwa yule anayetoa (9:6-11) na kwa Mungu pia (9:12-15).
Sehemu ya tatu ya ujumbe mkuu[6]
Baada ya kumaliza kuwataka Wakorintho kukamilisha utoaji kwa ajili ya watakatifu wa Yerusalemu, Paulo anarudi kwenye kutetea utume wake dhidi ya wapinzani wengine (tofauti na wale wa sura ya 1-7) ambao amewaita “mitume wakuu.” Paulo anaanza kwa kuwasihi Wakorintho kuwashughulikia wapinzani wake hao ili yeye akienda asitumie ukali (ujasiri kwa uthabiti) kwa wale ambao wanadhania yeye anaenenda kwa mwili, yaani wapinzani wake (10:1-2). Paulo anafafanua kwamba pamoja na kwamba yeye na wenzie wanaenenda kwa mwili, hawapigani kwa mwili, kwa kuwa silaha zao si za mwili bali za rohoni. Kwa kutumia lugha ya kivita ya wakati huo (yaani, kuangusha ngome na kuteka nyara), Paulo anaelezea uwezo wa silaha hizo, huku akimalizia kwa kuwaambia Wakorintho kwamba wao (yaani, Paulo na wenzie) wako tayari kuwahukumu hao wapinzani ikiwa Wakorintho watawakubali wao, yaani pale Wakorintho wakapoacha kuwasikiliza wapinzani wa Paulo na kurudi kumsikiliza yeye na watumishi wenzake (10:3-6). Juu ya hilo, Paulo anawataka Wakorintho kutathmini mambo jinsi yanavyojionyesha wazi, badala ya kuwasikiliza wapinzani wake. Wao wanajiita watu wa Kristo (yaani, wenye mamlaka kutoka kwa Kristo), naye pia kama ilivyo wazi. Baada ya kukubali kwamba yeye pia ana mamlaka kutoka kwa Kristo, Paulo anakiri kwamba haoni haya kujisifu kwa hilo, wala hafanyi hivyo kwa lengo la kuwaogopesha Wakorintho, kama wapinzani wake wanavyodai kwamba katika nyaraka zake ni mkali na mwenye mamlaka, lakini akiwa katika mwili ni dhaifu. Dhana hiyo pia, ya kusema yeye ni mkali kwenye nyaraka lakini akiwa katika mwili ni dhaifu, Mtume anaipinga kwa kuwataka wajue kwamba jinsi alivyo katika nyaraka zake, ndivyo alivyo pia akiwa katika mwili pamoja nao (10:7-11). Katika kuendelea kujitetea dhidi ya wapinzani wake, Paulo anajitofautisha nao katika mambo kadhaa. Moja, yeye na wahubiri wenzake hawajipimi wala kujilinganisha na wao (“mitume wakuu”), ambao wanajipima wao wenyewe; kwa sababu kufanya hivyo ni kukosa akili. Pili, hawajisifu kwa kazi nje ya mipaka ile waliopewa na Mungu. Lakini Korintho iko ndani ya mipaka yao ya kujisifia kwa kuwa wao ndio waliowapelekea injili ya Kristo kwanza. Tatu, hawajisifii kazi (taabu) za watu wengine, lakini wanatumiani imani ya Wakorintho ikikua wao watatukuzwa na watapata nafasi ya kuhubiri kwenye nchi za mbele zaidi ya Korintho. Pamoja na kujitofautisha huko, Paulo anamalizia kwa kusisitiza kujisifu kunatakiwa kuwa katika Bwana (na sio katika hekima, nguvu wala utajiri[7]) kwa kuwa anayekubaliwa sio yule anayejisifu bali anayesifiwa na Bwana (10:12-18).
Baada ya kujitofautisha na “mitume wakuu” hasa kwenye swala la kujisifu, Paulo anaamua kuingia kwenye kujisifu. Kabla hajajisifu, Paulo anaeleza kwa nini ameamua kuingia kwenye upumbavu huu. Paulo anasema ni kwa sababu ana wivu wa kimungu juu ya Wakorintho na ana wasi wasi wasije wakawa wamedanganywa na mitume wakuu kama Shetani alivyomdanganya Eva. Hii ni kwa sababu wanakubaliana na mitume hawa wanaomhubiri Yesu mwingine, Roho mwingine na injili nyingine (11:1-4). Tenakabla ya kuingia kwenye upumbavu wa kujisifu Paulo anapambana kwanza na shutuma za wapizani wake. Pale walipomtuhumu kwamba yeye sio mzungumzaji wa hadhara aliyepata mafunzo kuliko wao, yeye anajibu kwamba hakupungukiwa chochote walichonacho wo, na hata kama hakuwa na ustadi wa kuzungumza hakupungukiwa elimu (11:5-6). Pale wanapomtuhumu kwamba hakupokea fedha yeyote kutokana na kazi yake, yeye anajibu kwamba alifanya hivyo kwa upendo ili Wakorintho watukuzwe, mwenendo ambao ni tofauti na mitume hawa wa uongo, ambao wanajigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo kama Baba yao shetani anavyofanya (11:7-15). Na kwa kuwa Wakorintho wameweza kuchukuliana na mitume wakuu katika upumbavu wao wa kujisifu katika mambo ya mwili, Paulo anawaomba Wakorintho wachukuliane naye katika kujisifu kama mpumbavu, pamoja na kwamba yeye sio mpumbavu (11:16-21).
Baada ya kusema hayo, Paulo anaamua kujisifu, pamoja na kwamba anajua kufanya hivyo ni upumbavu. Kwanza anakubaliana kwamba kama walivyo mitume wakuu, yeye pia ni mwisraeli kweli kweli. Lakini ikifika kwenye utumishi wa Kristo, Paulo anajisifu kwamba yeye ni zaidi ya mitume hao wakuu. Ubora wake unathibitishwa na mateso na mambo yake ambao mitume wakuu wanayaona kuwa ni udhaifu. Mambo haya ni kama kufungwa, kupigwa bakora, kunusurika kufa na hatari mbalimbali alizokutana nazo (11:22-33). Tena pamoja na kuwa na maono na mafunuo kutoka kwa Bwana, Paulo anajisifu kwamba Bwana amemuwekea mwiba katika mwili ili asijisifu kupita kiasi, ili uweza wa Mungu utimilike katika udhaifu wake, ndiyo maana unafurahia udhaifu (12:1-10). Mwisho wa kujisifu Paulo anawakemea Wakorintho kwa kushindwa kumtetea na kuthibitisha utume wake mbele ya mitume wakuu, pamoja na wao wenyewe kuwa mashahidi wa uthibitisho wa utume wake uliothibitishwa kwa ishara, maajabu na miujiza (12:11–13).
Sehemu ya nne ya Ujumbe mkuu
Baada ya kutetea kwa kirefu utume wake, Paulo anamalizia barua hii kwa kuwaanda Wakorintho kwa ujio wake, ambapo safari hi itakuwa ni safari yake ya tatu kwao. Kwanza, anaanza na kuwahakikishia kwamba akienda kama kawaida yake hatawalemea kwa chochote, kama ambavyo yeye na watumishi wenzake akiwepo Tito walivyokuwa wanafanya. Na ameamua kuishi hivyo kwa sababu hatafuti vitu kutoka kwao, bali anawatafuta wao kama ilivyo kwamba wazazi ndiyo wanaweka akiba kwa watoto na sio watoto kwa wazazi (12:14-19). Pili, Paulo anaelezea wasiwasi wake kwamba isije ikiwa baadhi ya Wakorintho hawajatubu bado dhambi zao, jambo ambalo litamlazimisha kuchukua hatua ambazo hazitawapendeza (12:20–21).
Tatu, baada ya kueleza wasi wasi wake huo, Paulo anaeleza wazi kwamba wale ambao bado hawajatubu, atakapoenda Korintho hatawahurumia, yaani atachukua hatua kali dhidi yao kama mtume ambaye Kristo anafanya kazi ndani yake (13:1-4). Baada ya kuthibitisha kwamba yeye ni mtume wa kweli na ana mamlaka ya kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa Wakorintho ambao hawajatubu, Paulo anawataka Wakorintho kujichunguza kama kweli wako kwenye imani au la. Paulo anawataka kufanya hivyo kabla yeye hajaenda kwao, ili akienda kwao asitumie ukali kwa kadiri ya uwezo ule aliopewa na Bwana, kwa ajili ya kujenga wala si kwa ajili ya kubomoa (13:5-10).
Paulo anahitimisha waraka wake kwa mausia ya mwisho na salamu (13:11–14).
FOOTNOTES
[1] Kwa kawaida Mtume Paulo huwa anamshukuru Mungu kwa ajili ya ukuaji wa maisha ya imani ya waandikiwa wake, lakini katika barua hii anamtukuza Mungu kwa yale aliyofanya kwake na kwa timu ya injili alio nao pamoja naye (Linganisha na 1 Wakorintho 1:3-9, Waefeso 1:3-14).
[2] Pia, ni kawaida ya mtume Paulo baada ya shukrani kutoa taarifa za maombi yake au kuwaombea moja kwa moja wapokeaji wa barua zake, na mara kadhaa huomba kuombewa mwishoni mwa barua (Angalia Warumi 15:30–32; 1 Wathesalonike 5:25; na Filemoni 1: 22), lakini katika barua hii anaomba kuombewa na Wakorintho mwanzoni tu mwa barua.
[3] Ilikuwa ni kawaida kwa Kanisa la kwanza kupokea wahubiri wanaosafiri huku na kule kwa njia ya kupokea barua ya uthibitisho, kutoka kwenye kanisa la mahali pamoja anakotoka mhubiri husika. Hii ilikuwa ni kwa ajili ya kuepuka kupokea wahubiri wenye mafundisho potofu (Matendo 18:27). Paulo anasema yeye na Tito na Timotheo hawahitaji barua kwa kuwa kuwepo kwa Kanisa la Korintho ni uthibitisho tosha, kwa kuwa wao ndio waliopanda hilo Kanisa. Kwa lugha nyingine wao wasingekwenda Korintho basi kusingelikuwa na Kanisa la Korintho.
[4] Inawezekana wapinzani wa Mtume Paulo walikuwa wanajivunia sheria ya Musa ndiyo maana Paulo anataka kuonyesha kwamba Agano jipya ambalo linaandikwa na Roho katika mioyo ya waamini ndilo lenye utukufu zaidi kuliko Agano la kwanza lililoandikwa kwa mikono ya Mungu.
[5] Paulo anachosema hapa kwa Wakorintho ni kwamba, kama Mungu amewapa Paulo na wenzake ujumbe wa upatanisho baada ya wao kupatanishea hivyo Wakorintho wanatakiwa kupatana nao, kwa kuwa kutokufanya hivyo ni sawa na kupokea neema ya Mungu bure.
[6] Unaposoma sura ya 10-13 ni muhimu kuzingatia kwamba Mtume Paulo anajibu tuhuma za moja kwa moja zilizotolewa na wapinzani wake kwa upande mmoja. Mfano, kwa kusoma 10:1,10 utagundua kwamba wapinzani wake walikuwa wanamtuhumu kuwa mkali na mwenye mamlaka katika nyaraka zake, lakini akiwa ana kwa ana ni dhaifu. Kwa upande mwingine anawakosoa kile wapinzani wake wanafanya. Mfano, kwa kusoma 10:12-18 utagundua kwamba Paulo anakosoa tabia ya wapinzani wake kujisifu kupita kiasi.
[7] Namna sahihi na namna isiyosahihi ya kujifisu ni wazo linalotoka kwenye Yeremia 9:23-24. Kuna uwekezako mkubwa Paulo alipokuwa anaandika mstari wa kumi na saba (2 Wakorintho 10:17) alikuwa anaelezea wazo la Yeremia 9:23-24.
Unakuja hivi karibuni…

