MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA PILI WA MTUME YOHANA.
MAELEKEZO.
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI.
Waraka wa pili wa Mtume Yohana ni kitabu kinachokubaliwa na waamini kwamba kiliandikwa na mtume Yohana kwenda kwenye makanisa yaliyokuwa eneo la Asia ndogo japo mwandishi hajataja jina lake katika maandishi ya kitabu hiki. Pamoja na kwamba ni kweli Yohana hajataja jina lake katika maandishi ya kitabu hiki zaidi ya kujiita “Mzee” kuna viashiria kwamba waraka huu uliandikwa na yeye. Moja ya kiashiria ni ufanano mkubwa wa Ujumbe na matumizi ya Lugha na Vitabu vingine vinavyoaminiwa kuandikwa na yeye, vitabu hivi ni Injili ya Yohana, Waraka wa kwanza wa Yohana na Waraka wa Tatu wa Yohana. Mfanano wa vitabu hivi ni ishara tosha kwamba viliandikwa na mwandishi mmoja.
MTUME YOHANA.
Yohana alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wa Yesu, mtoto wa Zebedayo, na kaka wa Yakobo mtume (Mathayo 4:21-22). Yakobo huyu ni Yakobo mtume wa Kwanza kabisa kufa na sio Yakobo mwandishi wa waraka wa Yakobo (Matendo 12:1-2). Yohana kabla ya kukutana na Yesu alikuwa mvuvi wa samaki, kazi ambayo ilikuwa ni kazi ya familia.
Yohana anafahamika kama mwanafunzi aliyekuwa karibu sana na Yesu na anajitaja kama mwanafunzi aliyependwa sana na Bwana Yesu (Yohana 13:23). Ni kweli kwamba Yohana alikuwa karibu sana na Yesu sababu Yeye na Petro na Yakobo ndio wanafunzi pekee waliona matukio muhimu ya Bwana Yesu ambayo wanafunzi wengine hawakuyaona. Matukio haya ni kama kubadilika kwa Yesu kule mlimani (Luke 9:28-36) na maombi yake katika bustani ya Gethsemani (Mathayo 26:36-46).
Baada ya kristo kufufuka Yohana alikuwa huko Jerusalem kama mmoja wa Mitume waliotambulika kama Nguzo za Kanisa (Wagalatia 2:9-10). Kwa mujibu wa mapokeo ya kihistoria kutoka kwa mababa wa Kanisa wa kuanzia karne ya pili Yohana baada ya kufanya kazi huko Jerusalem pamoja na mitume wengine alisafiri na kwenda Efeso ambako alifanya huduma yake kwa muda wa kutosha (Kati ya mwaka 70-100 B.K) na nyaraka zake tatu ni matokeo ya huduma yake kwa kanisa lililokuwako huko Efeso. Baada ya muda kama njia ya mateso Yohana alipelekwa katika kisiwa cha Patmo na Huko aliandika kitabu cha Ufunuo. Na inaaminika kuwa Yohana ndiye mtume pekee kufa kifo cha kawaida tu bila kuuawa kama mitume wengine.
WAPOKEAJI WA AWALI WA WARAKA.
Kitabu hiki tofauti na waraka wa kwanza, kinataja mpokeaji/wapokeaji wa ujumbe huu. Wapokeaji wa ujumbe huu ni mwanamke mteule (Mama mteule) na Watoto wake. “Mwanamke mteule” ni lugha ya picha inayomaanisha kanisa na “watoto wake” ni waamini wa kanisa hilo.[1] Hii ni kwa sababu kanisa mara nyingi lilifahamika kama Bibi harusi wa Kristo na waamini kuitwa Watoto na Yohana ni kitu cha kawaida hasa katika waraka wake wa kwanza. Sifa ya waandikiwa wa barua hii ni kwamba baadhi yao walikuwa wanaenenda katika kweli kama walivyofundishwa (2Yohana1:4).
KUSUDI LA WARAKA.
Mzee Yohana anaandika waraka huu kwa kanisa ambalo anajua ndani yake lina waamini wanaoenenda katika kweli hivyo anaandika kulipa tahadhari kanisa juu ya kutokuwapokea waalimu wa uongo (2Yoh1:7). Anawakataza vikali kuwapokea waalimu wa uongo na kuwapa ukarimu wa aina yeyote (2Yoh1:10). Waalimu hawa wa uongo walikuwa wanafundisha sawa na waalimu wa uongo katika waraka wake wa kwanza (2 Yoh 1:7 na 1 Yoh 4:1-3), lakini tofauti ni kwamba kwa waraka wa kwanza, waalimu hawa walijitenga baada ya kuwa sehemu ya kanisa (1 Yoh 2:19) lakini katika waraka huu waalimu hawa si sehemu ya kanisa ila ni waalimu wanaozunguka na kutembelea makanisa mbalimbali na hivyo wakati wowote watafika katika kanisa hili. Pamoja na jambo hilo pia mwandishi anawakumbusha kanisa kuhusu mambo mawili ya msingi Kwenda Pamoja yaani Upendo na kweli.
MPANGILIO.
Sehemu | Maelezo |
1:1-3 | Utangulizi |
1:4-6 | Kweli na upendo |
1:7-11 | Kusiwepo na ushirika na waalimu wa uongo |
1:12-13 | Salamu za mwisho |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.
Waraka huu una muundo kama waraka/barua ya karne ya kwanza ilivyotakiwa kuwa, yaani kuna Utangulizi (1:1-3), Ujumbe mkuu (1:4-11) na Salamu za Mwisho (1:12-13). Utanguzili una sehemu Tatu kama ilivyokuwa kawaida yaani Kuna Anuani ya Mtuma waraka (1:1a), anuani ya mpokeaji (1:1b-2) na Salamu (1:3).
Sehemu ya ujumbe mkuu inaweza kugawanywa katika sehemu nyingine mbili. Katika sehemu ya kwanza mwandishi anaanza na kuwapa sifa kanisa ya kwamba kati yao kuna wanaoenenda katika kweli (1:4). Pamoja na kuenenda katika kweli Yohana anawakumbusha waamini kupendana (1:5). Upendo Yohana anaouzungumza unahusu kuzishika amri za Mungu, ambazo moja wapo ndio hii ya kupendana waamini (1:6). Sehemu ya pili, mwandishi anaanza na kutoa taarifa kwamba wadanganyifu ambao ni wapinga Kristo wameshatokea, na wanafundisha kwamba Yesu hakuja katika mwili (1:7).[2] Kwa kuwa wadanganyifu wapo na udanganyifu wao unaathiri Imani yako mwandishi anasisitiza waamini wabaki katika kile wanachoamini ili wasipoteza thawabu ya waliyoyafanya mpaka sasa (1:8). Wdanganyifu hawa hawana Mungu kwa kuwa hawajadumu katika mafundisho ya Kristo ila yeyote aliyedumu katika mafundisho ya Kristo huyo ana Baba na Mwana (1:9). Kwa kuwa wadanganyifu hawa hawana Mungu na wanaweza kuwatoa waamini katika thawabu zao kanisa halipaswi kuwakaribisha wala kuwapa salamu (1:10)[3]. Kwa maana mtu akiwapa salamu au kuwakaribisha mtu huyo pia anashirki kazo zao za udanganyifu (1:11).
Mwisho Yohana anawajulisha kanisa kwamba ana mambo mengi ya kuwaambia lakini atafanya hivyo wakionana uso kwa uso kwa kuwa anatarajia Kwenda kwao hivi karibuni (1:12). Mwisho kabisa anatoa salamu kwa kanisa kutoka kwa waamini waliokokaribu nae (1:13).
FOOTNOTES
[1] Kwa kuwa jambo hili halina uhakika wa asilimia 100 kuna mtazamo kwamba mwanamke mteule ni kiongozi wa kanisa aliyekuwa jinsia ya kike.
[2] Mwandishi pia aliwaonya kanisa aliloliandikia waraka wake wa kwanza kuhusu waalimu hawa ambao walikuwa wanapinga kwamba Yesu hakuja katika mwili. Kundi hili halikukubaliana na ubinadamu wa Yesu hivyo walifundisha kwamba Yesu hakuwa na umbile halisi la Binadamu japo alionekana kuwa na mwili wa binadamu. Kwa lugha rahisi walifundisha kwamba Yesu alikuwa kama Mzimu.
[3] Waalimu hawa walikuwa wanasafiri huku na kule kama watumishi wengine wa Mungu wa kweli. Hii iliwahitaji wakaribishwe na mwenyewe. (kupewa chakula na malazi) ili wafanye kazi yao ya kufundisha ndio maana Yohana anasema wasikaribishwe
Unakuja hivi karibuni….