1 Yohana – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA KWANZA WA MTUME YOHANA.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.

UTANGULIZI.

Waraka wa kwanza wa Mtume Yohana ni kitabu kinachokubaliwa na waamini kwamba kiliandikwa na mtume Yohana kwenda kwenye makanisa yaliyokuwa eneo la Efeso, japo mwandishi hajataja jina lake katika maandishi ya kitabu hiki. Pamoja na kwamba ni kweli Yohana hajataja jina lake katika maandishi ya kitabu hiki, kuna viashiria kwamba waraka huu uliandikwa na yeye. Moja ya kiashiria ni ufanano mkubwa wa ujumbe na matumizi ya lugha na vitabu vingine vinavyoaminiwa kuandikwa na yeye. Vitabu hivi ni Injili ya Yohana, Waraka wa pili wa Yohana na Waraka wa tatu wa Yohana. Mfanano wa vitabu hivi ni ishara tosha kwamba viliandikwa na mwandishi mmoja

MTUME YOHANA.

Yohana alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wa Yesu, mtoto wa Zebedayo, na kaka wa Yakobo mtume (Mathayo 4:21-22). Yakobo huyu ni Yakobo mtume wa Kwanza kabisa kufa na sio Yakobo mwandishi wa waraka wa Yakobo (Matendo 12:1-2). Yohana kabla ya kukutana na Yesu alikuwa mvuvi wa samaki, kazi ambayo ilikuwa ni kazi ya familia.

Yohana anafahamika kama mwanafunzi aliyekuwa karibu sana na Yesu, na anajitaja kama mwanafunzi aliyependwa sana na Bwana Yesu (Yohana 13:23). Ni kweli kwamba Yohana alikuwa karibu sana na Yesu sababu yeye na Petro na Yakobo ndio wanafunzi pekee waliona matukio muhimu ya Bwana Yesu ambayo wanafunzi wengine hawakuyaona. Matukio haya ni kama vile, kubadilika kwa Yesu kule mlimani (Luke 9:28-36) na maombi ya Yesu katika bustani ya Gethsemane (Mathayo 26:36-46).

Baada ya kristo kufufuka Yohana alikuwa huko Jerusalem kama mmoja wa Mitume waliotambulika kama Nguzo za Kanisa (Wagalatia 2:9-10). Kwa mujibu wa mapokeo ya kihistoria kutoka kwa mababa wa Kanisa wa kuanzia karne ya pili, Yohana baada ya kufanya kazi huko Jerusalem pamoja na mitume wengine alisafiri na kwenda Efeso ambako alifanya huduma yake kwa muda wa kutosha (Kati ya mwaka 70-100 B.K).Nyaraka zake tatu ni matokeo ya huduma yake kwa kanisa lililokuwako huko Efeso. Baada ya muda, kama njia ya mateso Yohana alipelekwa katika kisiwa cha Patmo na huko aliandika kitabu cha Ufunuo. Na inaaminika kuwa Yohana ndiye mtume pekee kufa kifo cha kawaida tu bila kuuawa kama mitume wengine.

WAPOKEAJI WA AWALI WA WARAKA.

Katika kuandika kitabu hiki mwandishi hakuandika kwa mtindo wa waraka[1] ndio maana hata hakuandika wapokeaji walikuwa ni watu wa eneo gani. Kwa msaada wa kihistoria Kutoka kwenye vitabu vya waandishi ya karne ya pili na ya tatu tunajifunza kwamba Mtume Yohana, mwana wa Zebedayo, mwanafunzi Yesu aliyempenda aliishi na kufanya huduma yake kule Efeso, Asia kati ya mwaka 70-100 B.K. Hivyo inaaminika aliandika waraka huu kwa waamini wa maeneo ya Efeso ambao anawaita “watoto wake”. Kutokana na Ujumbe wa kitabu hiki ni dhahiri kuwa kitabu hiki kiliandikwa kwenda kwa waamini ambao tayari wanaijua kweli (2:7, 21),  lakini katikati yao kulitokea  na mgawanyiko kati yao na waalimu wa uongo. Mgawanyiko huu ukasababisha waalimu hao wa uongo kujitenga. Pamoja na kujitenga waliendelea kueneza uongo wao na ndio maana mwandishi anawaandikia waamini hawa wanaoijua kweli kujiepusha na waalimu hao wa uongo na mafundisho yao ya uongo.

KUSUDI LA WARAKA.

Katika kutafuta kusudi la kuandikwa kwa kitabu chochote basi tunatakiwa kuangalia kauli ya mwandishi inayoonyesha kusudi la kuandika ujumbe wake. Katika kitabu hiki mwandishi ana kauli zaidi ya moja zinazoashiria kusudi la kuandika ujumbe huu. Kauli hizi ni kama zifutazo

 “Na haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe.” 1 Yohana 1:4

Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,” 1 Yohana 2:1

Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza” 1 Yohana 2:26

Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.” 1 Yohana 5:13

Mwandishi anaonyesha kwamba alikuwa na kusudi zaidi ya moja la kuandika kitabu hiki, kwa sababu mara nyingi baada ya maelezo fulani anataja kusudi la sehemu hiyo. Baada ya kuandika mstari wa kwanza hadi wa tatu sura ya kwanza mwandishi anasema “twayaandika ili kusudi furaha yetu itimizwe” akionyesha furaha yake itatimizwa kama kutakuwa na ushirika kati yake na wapokeaji wa ujumbe huu. Baada ya kukosoa kiri zisizo sahihi katika mstari wa tano hadi wa kumi sura ya kwanza mwandishi anasema “nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi” akionyesha kwamba lengo la kuwaandikia hayo (5-10) ni kuwataka wasitende dhambi. Baada ya kueleza habari za wapinga Kristo katika mstari wa kumi na nane hadi wa ishirini na tano sura ya pili, mwandishi anasema “Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza”. Na baada ya kuelezea kuhusu ushindi wa waamini dhidi ya dunia yaani hiyo imani yao yenye ushuhuda katika mstari wa kwanza hadi kumi na mbili sura ya tano, mwandishi anasema “Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu”.

Hivyo Mwandishi alikuwa na kusudi zaidi ya moja katika kuandika ujumbe huu kwa wapokeaji. Makusudi haya yanaweza kuwekwa kwenye makundi mawili, moja ni kusudi la kichungaji na la pili ni kusudi la utetezi wa imani ya kweli.

KUSUDI LA KICHUNGAJI.

Mwandishi anawaandikia watu ambao tayari wamekwisha amini (2:12-14; 5:13) na pia wanaijua kweli (2:7, 21). Watu hawa pia anawajua na ni watu ambao ana wajibu kwao, ndio maana anawaita “watoto wangu wadogo” (2:1) au “watoto wadogo” (2:28; 3:7; 3:18; 4:4; 5:21). Anawaandikia kuwataka waendelee kwenye kuamini kweli waliyofundishwa tangu mwanzo (2:7, 24) ambayo ina ushahidi wa kweli kutoka kwa mitume waliomsikia, kumuona na kumshika Yesu (1:1-3). Kweli hiyo inawataka kuenenda katika nuru kama Mungu alivyo katika nuru (1:5-7). Kweli hiyo inawataka kupendana (3:11, 14) katika kweli na Tendo (3:18) kama Mungu alivyowapenda wao (4:10-11, 19). Na zaidi kweli hiyo inawataka kuamini kwamba Yesu ni Kristo (2:22-23), mwana wa Mungu (1:3, 7; 3:8; 4:9, 15), kipatanisho kwa dhambi zetu (4:10), aliyekuja katika mwili (4:2) na katika maji na damu (5:6). Mwandishi kama mchungaji anasema furaha yake itatimizwa kuona wapokeaji wanaishi kwenye kweli hii (1:4). Lakini pia kama mchungaji mwandishi anataka wapokeaji wa ujumbe wake wasitende dhambi (3:8-9; 5:18), na ikitokea mtu ametenda dhambi basi ajue anaye mwombezi kwa Baba ambaye ni Yesu kristo (2:1-2, 5:16-17). Na zaidi kama Mchungaji anataka kuwahakikishia kwamba wale wanaoliamini jina la Mwana wa Mungu wanao Uzima wa milele (5:13) ambao ni Yesu mwenyewe (1:2; 5:11, 20).

KUSUDI LA UTETEZI WA IMANI YA KWELI.

Sababu kubwa nyingine ya mwandishi kuandika kitabu hiki ni kupinga mafundisho potofu na maisha/mwenendo ambao uko kinyume na kweli. Mwenendo huu anaoupinga mwandishi ulikuwa dhahiri kwa watu anaowaita “wapinga Kristo” (2:18; 4:3), “manabii wa Uongo” (4:1), “watoto wa Ibilisi” (3:10) na waongo na wadanganyifu (2:4, 22; 3:7). Watu hawa walikuwa katika kundi la waamini na wakati mwandishi anaandika ujumbe huu walikuwa wamejitoa (2:19). Kujitoa kwao mwandishi anasema kumetokea ili wafunuliwe kwamba kweli hawakuwa sehemu ya waamini. Lakini watu hawa hawakuishia kujitoa tu bali walifanya jitahada kuwapotosha wengine (2:26). Kwa kuwa kitabu hiki kinakubaliwa na wasomi wengi wa Biblia kwamba kilikuwa kimekusudiwa kwa ajili ya makanisa yaliyoko Efeso na maeneo ya Karibu,basi maneno ya unabii ya mtume Paulo yalitimia kama alivyosema kwa viongozi wa Efeso (Matendo 20:29-30) na kama alivyomwambia Timotheo alipokuwa huko Efeso (2 Timotheo 3:1-7, 4:3-4)[2].

Watu hawa kwa kumsoma Mwandishi anavyowakosoa na kurekebisha fundisho lao ni dhahiri walikuwa wanafundisha yafuatayo,

a. Walikuwa wanakana kwamba “Yesu ni Kristo” (2:22) na mwandishi anasisitiza kwamba aliyezaliwa na Mungu anaamini kwamba Yesu ni Kristo (5:1).

b. Walikuwa wanakana kwamba Yesu kristo hakuja katika Mwili (4:2, Tazama pia 2 Yohana 7) na mwandishi anasisitiza kwamba Yesu kristo walimuona, walimsikia, walimtazama kwa macho na walimshika kwa mikono (1:1-3).

c. Walikuwa wanakana kwamba Yesu Kristo Mwana wa Mungu hakufa bali mwandishi anasisitiza kwamba alikufa (5:5-6).

Sasa unaweza kushangaa inakuaje watu hawa walikuwa katikati ya waamini pamoja na kwamba wanapinga kila kitu muhimu kumhusu Kristo Yesu ? Mshangao huu unaweza kutokana na sababu mbili, Moja hatujui mpangilio mzuri wa mafundisho yao na tunapata mafundisho yao kutoka katika upande wa mkosoaji tu. Jambo la pili, ni kwa sababu kwetu leo Yesu Kristo limekuwa kama Jina moja yaani Kristo limekuwa kama jina la Baba la Yesu (Kama ilivyo tamaduni yetu ya majina). Lakini tukipata mwanga kidogo kutoka katika historia tunaweza kupata angalau mpangilio wa mafundisho yao. Lakini pia tukielewa utofauti wa Jina Yesu na Cheo kristo tunaweza kuelewa fundisho lao.

Utofauti wa Jina Yesu na Cheo Kristo.

Jina Yesu ni Jina la mwokozi wetu la kupewa na wazazi kama walivyoelekezwa na malaika Gabrieli (Luka 1:31). Yesu alichukua cheo kinachoitwa Kristo (neno lililotoholewa kutoka kwenye kiyunani) au Masihi (Neno lililotoholewa kutoka kwenye kiebrania). Cheo hichi kinamaanisha yeye ni mpakwa mafuta wa Mungu aliyetabiriwa katika vitabu vya Agano la kwanza/kale kwamba atakuja kupitia ukoo wa Daudi ili kulikomboa taifa la Israeli. Hivyo Yesu ni Kristo kwa maana ya kuwa yeye ni mpakwa mafuta wa Mungu aliyekuja duniani kupitia familia ya mfalme Daudi kuleta ukombozi. Kwa utofauti huu ndio maana wayahudi mpaka leo wanakataa kwamba Yesu hakuwa kristo kwa maana wanaamini hakukidhi vigezo vya kuwa masihi/Kristo. Bado wao wanasubiri ujio wa Masihi/Kristo mpaka leo.

Mpangilio wa mfundisho ya Waalimu hawa wa Uongo.

Maandishi ya Mababa wa kanisa ya kuanzia karne ya pili ambao walitumia Kitabu hiki cha Yohana kupingana na upotofu huo yanatupa mwanga zaidi katika kutuonyesha kwamba watu hawa walikuwa na mafundisho ya namna gani.

Mababa wa kanisa wanatuonyesha kwamba mafundisho haya yalikuwa kwenye makundi kadhaa, Moja ya makundi ya waalimu hawa wa uongo lilikuwa ni kundi la Mwalimu aliyeitwa Cerinthus. Mwalimu huyu kwa mujibu wa Askofu Ireneo wa mji wa Lyon, alitenganisha kati ya Yesu na Kristo kwa kufundisha kwamba Yesu alikuwa ni mwanadamu wa kawaida tu wa kule Nazareti aliyezaliwa na Josefu na Mariam kwa njia ya kawaida tu, ambaye alikuwa na huruma na Hekima. Kwa upande mwingine Kristo alitoka kwa Mungu na kumshukia Yesu wakati wa ubatizo wake. Hivyo kwa mujibu wa mwalimu huyu, Kristo aliyekuwa ndani ya Yesu akamhubiri Baba kwa watu na akafanya miujiza mingi na mwishoe alimtoka Yesu kabla hajasulubiwa. Hivyo Cerinthus alifundisha kwamba Kristo kutoka Mbinguni hakusulubiwa bali Yesu mwanadamu wa Nazareti ndiye aliyesulubiwa na baadaye kufufuka.[3]

Kundi lingine la pili ni kundi la Udoho “Docetism”, kundi ambalo halikukubaliana na ubinadamu wa Yesu. Kwa kutokukubaliana na ubinadamu wa Yesu kundi hili walifundisha kwamba Yesu hakuwa na umbile halisi la Binadamu japo alionekana kuwa na mwili wa binadamu. Kwa lugha rahisi walifundisha kwamba Yesu alikuwa kama Mzimu. Hivyo kwa kupata mwanga huu wa mpangilio wa mafundisho yao ni rahisi kuelewa mwandishi alichokuwa anakipinga.

Kumbuka makundi haya yanatupa mwanga tu wa kile ambacho mwandishi alikuwa anapingana nacho.

Mbali na mafundisho potofu kuhusu Yesu kristo kama tulivyoeleza, pia waalimu hawa wa uongo waliishi maisha yasiyo na maadili yatokanayo na kweli. Hii ndio maana mwandishi anawakosoa sana akisema:

Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.” 2:4

.”Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.” 2:9

Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.” 2:11

“Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona” 4:20

Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki” 3:7

Na kuna uwezekano mkubwa pia zile kauli za “Tukisema” za mstari wa 6, 8 na 10 sura ya kwanza zilikuwa pia ni nukuu za mwandishi kutoka kwa waalimu hawa wa uongo. Haya yote yanaonyesha waalimu hawa wa uongo waliishi tofauti na ukiri wao wa kumjua Mungu na kuwa na ushirika naye.

Hivyo mwandishi aliandika waraka huu kupinga mafundisho hayo potofu ya waalimu wa Uongo na kupinga mwenendo wao wa giza.

MPANGILIO.

Mpangilio wa kitabu hiki ni vigumu kuugundua kwa sababu Mwandishi haelezei hoja zake kwa mpangilio maalumu mwanzo mpaka mwisho. Mwandishi amechanganya changanya hoja zake mara kadhaa yaani kuna wakati anaanza jambo moja baada ya muda anaingia japo la pili kabla ya kumaliza jambo la pili anarudi tena kwenye jambo la kwanza. Mfano anazungumiza kupendana katika 3:11-24 na baada ya hapo anazungumzia wapinga kristo (4:1-6) alafu anarudi tena kuzungumza kuhusu kupendana (4:7-21).

Pia lugha anayotumia Mwandishi ni lugha ya kurudia rudia maneno yale yale kama wimbo. Maneno haya ni kama vile “kaeni ndani yake” “amri zake” “mwana wake” “kupendana”.

Hivyo mpangilio huu ni pendekezo letu tu kwa ajili ya kukusaidia kufuatilia mawazo yake.

SehemuMaelezo
1:1-4UTANGULIZI
 
1:5-2:27USHIRIKA NA MUNGU
a. 1:5-2:2Tusijidanganye.
b. 2:3-2:11Tushike amri zake.
c. 2:12-2:14Kwenu watoto wadogo, wakina Baba na Vijana.
d. 2:15-2:17Msiipende Dunia.
e. 2:18-2:27Wapinga Kristo (Sehemu ya I)
  
2:28-3:24WANA WA MUNGU
a. 2:28-3:10Uhusiano wa Mwana wa Mungu na Dhambi na kutenda Haki
b. 3:11-3:24Tupendane (Upendo sehemu ya I)
 
4:1-5:17MSISITIZO
a. 4:1-4:6Kuzitambua Roho (Wapinga Kristo sehemu ya II)
b. 4:7-4:21Tupendane (Upendo Sehemu ya II)
c. 5:1-5:13Kumwamini Mwana wa Mungu
d. 5:14-5:17Ujasiri wetu katika Maombi
 
5:18-5:21HITIMISHO
a. 5:18Uhusiano wa Mwana wa Mungu na Dhambi
b. 5:19Sisi tu wana wa Mungu
c.5:20Sisi ndani ya Mwana wake
d. 5:21Tujiepushe na Sanamu

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.

Kama tulivyojifunza hapo juu kwamba kitabu hiki hakikuandikwa kwa mtindo wa waraka bali kwa mtindo wa semina/hotuba, Hivyo mwandishi anaanza moja kwa moja na utangulizi wa ujumbe. Katika utangulizi mwandishi anasema kile anachokihubiri (Neno la Uzima) ana ushahidi nacho kwa njia ya kuona, kusikia, kutazama na kupapasa kwa mikono. Kwa sababu ya ushahidi huo wapokeaji wake wakishikiria anachokisema basi kutakuwa na ushirika kati yao (Mwandishi na waandikiwa). Wapokeaji wa ujumbe wakiwa na ushirika na mwandishi basi wao wote watakuwa na ushirika na Baba na mwanae Yesu. Hii ni kwa sababu yeye mwandishi yuko na ushirika na Baba pamoja na mwanae. Hilo likitokea mwandishi anasema furaha yake itatimizwa/itakamilika (1:1-4).

Baada ya utangulizi huo mwandishi anaenda kwenye sehemu ya ujumbe wake mkuu. Sehemu ya ujumbe mkuu ina sehemu tatu na mwisho kuna hitimisho la semina.

Sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu (1:5-2:27), Mwandishi anaanza kueleza jambo la kwanza walilolisikia kutoka kwa Neno la Uzima na kusahihisha kiri zinazopingana na kile walichosikia kutoka kwa Neno la Uzima (1:5-10). Lengo la kusahihisha kiri hizo tatu hapo juu mwandishi anasema ni kuwataka wasitende dhambi, lakini hata ikitokea wametenda wajue wanaye mwombezi kwa Baba ambaye ni Yesu (2:1-2). Baada ya hapo mwandishi anawaonyesha wapokeaji wa Ujumbe wake ni kwa namna gani watajua kwamba wao wanamjua huyo Neno la Uzima au wanakaa ndani yake huyo Neno la Uzima au kwamba wako nuruni (2:3-11). Mpaka hapa mwandishi anataja sababu za kuandika hiki alichoandika kwa kutaja hizo sababu kwa kuhusianisha na makundi ndani ya kanisa (2:12-14)[4]. Kabla ya kumaliza sehemu yake ya kwanza ya ujumbe mkuu mwandishi anawataka waamini wasiipende dunia na wala vitu vilivyomo katika dunia (2:15-17). Katika kuhitimisha sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu mwandishi anawaonyesha wapokeaji wa ujumbe wake kwamba wapinga kristo tayari wameshafunuliwa. Anawaonyesha wanaamini ni nini wapinga kristo hawa wanafundisha, mafundisho ambayo mwandishi anayapinga. Mwandishi pia anasema uwepo wa hawa wapinga kristo na mafundisho yao mapotofu ndio sababu aliandikia ujumbe huu, ili kusisitiza wabaki kwenye kweli waliyosikia tangu mwanzo (2:18-27). Jambo hili la kuhusu wapinga kristo mwandishi atalirudia tena kulielezea hapo mbele.

Sehemu ya pili ya Ujumbe mkuu (2:28-3:24). Katika sehemu hii mwandishi amezungumzia mambo mawili, moja ni Kuzaliwa na Mungu/kuwa mtoto wa Mungu (2:28-3:10) na la pili ni kupendana sisi kwa sisi (3:11-24). Katika jambo la kwanza mwandishi anaanza na kuonyesha kwamba waliozaliwa na Mungu wanatenda haki (2:28-29). Anawajulisha pia kwamba wao wamekuwa watoto wa Mungu kwa sababu ya Upendo wa Mungu (3:1-3). Baada ya hapo anawaonyesha sifa za watoto wa Mungu (3:4-6) na utofauti wa watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi (3:7-9) na hivyo kuwawezesha wapokeaji wa ujumbe kuwatofautisha watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi(3:10).

Jambo la pili mwandishi anazungumzia kupendana, jambo ambalo pia alilisikia kutoka kwa Neno la Uzima. Mwandishi anafundisha kupendana akikinzanisha na chuki. Anafanya hivyo kwa kuonyesha mifano ya Upendo na Chuki. Yesu anakuwa mfano wa Upendo na Kaini anakuwa mfano wa Chuki (3:11-18). Mwandishi anaonyesha kwamba kupendana kunatupa ujasiri mbele za Mungu (3:19-22) na anamalizia kwa kuwaonyesha wapokeaji wake kwamba kupendana ni amri aliyotupa kama alivyotupa amri ya kuliamini jina lake (3:23-24). Jambo hili la Upendo mwandishi atalirudia tena hapo mbele.

Sehemu ya tatu ya Ujumbe mkuu (4:1-5:17). Katika Sehemu hii Mwandishi anarudi kuelezea mambo ambayo tayari ameshayaeleza kwenye sehemu za nyuma lakini kwa namna/lugha nyingine. Anaanza na kueleza namna ya kuzijaribu roho ili kujua kama roho husika ni Roho wa kweli au ni roho ya upotevu. Roho ya upotevu ni roho ya wapinga kristo ambao alikwisha kuwaelezea hapo juu kwamba wameshakuwapo (4:1-6). Baada ya hapo anarudi kueleza kwa habari ya upendo/kupendana, anaeleza kwamba Mungu ni Upendo na alitupenda kwanza, hivyo imetupasa sisi tupendana, na mtu asiyempenda jirani yake huyo hakumjua Mungu (4:7-21). Baada ya hayo, mwandishi pia anarudia msisitizo wa ujumbe wake kwamba Yesu ni Kristo na kila aaminiye hilo ni mwana wa Mungu. Mwandishi anaeleza hilo kwa kueleza uhakika wa uzima wa milele uliopo kwa wote wanaomwamini mwana wa Mungu, wote wanaoamini kwamba Yesu ndiye Kristo na kuamini kwamba yeye ni mwana wa Mungu. Mambo haya yote yanayomhusu Yesu mwandishi anasema Mungu ameyashuhudia kupitia Roho wake, hivyo yeye asiyeamini ushuhuda wa Mungu kumhusu mwanaye Yesu kristo anamfanya Mungu kuwa mwongo (5:1-13). Mwisho katika sehemu hii mwandishi anaonyesha ujasiri tulio nayo katika maombi (5:14-17).

Kama tulivyojifunza tangu mwanzo kwamba kitabu hiki hakikuandikwa kwa kuzingatia muundo wa kawaida wa waraka hivyo mwandishi haitimishi kwa salamu za mwisho bali anahitimisha kwa kauli mbalimbali ambazo tayari amekwisha kuzieleza katika maeneo mbalimbali toka mwanzo na kufunga kabisa na agizo la kujilinda na sanamu (5:18-21).



FOOTNOTES

[1] Nyaraka huwa zina mpangilio ufuatao, Utangulizi, Ujumbe mkuu na Salamu za Mwisho. Utangulizi huwa unakuwa na Majina/jina la waandishi/mwandishi, Utambulisho wa wapokeaji na Salamu. Mfano mzuri wa Mpangilio huu ni waraka wa Mitume na wazee kwa makanisa ya wamataifa iliyoandikwa baada ya Mkutano wa Jerusalem (Matendo 15:23-29). Vitabu vyote vya Agano jipya vinavyoitwa Nyaraka vina sifa ya mpangilio huo isipokuwa kitabu cha Yohana wa Kwanza na Kitabu cha Waebrania.

[2] Mapendekezo haya ya uhusiano wa unabii wa mtume Paulo na hali ya kanisa mwandishi analoliandikia si mapendekezo ya uhakika, bali yanaweza kusaidia tu kuelewa kwamba kanisa ambalo mwandishi analiandikia lilikuwa katika mgawanyiko wa ndani sawa sawa na utabiri wa mtume Paulo. Mapendekezo haya yamefanywa na mwandishi John R. W Stott katika kitabu kinachoitwa “Barua za Yohana: Utangulizi na Ufafanuzi cha mwaka 1988”

(Stott, J (1988) The letters of John: An Introduction and Commentary. IVP)

[3] Kama unaweza kusoma kiingereza basi maandishi haya ya Baba Askofu Ireneo yaliyoandikwa kwa kiyunani yametafsiriwa na yanapatikana kwa ajili ya kusomwa bila malipo kabisa katika tovuti au aplikesheni ya Biblehub au tovuti ya New advent. Habari hizo za Cerinthus zinapatikana kwenye Kitabu chake kiitwacho “Against Heresies I.26.1. Askofu Ireneo anaripoti kwamba Cerinthus aliishi wakati wa Mtume Yohana na waliwahi kukutana (Against Heresies III.3.4).

[4] Mwandishi anaeleza sababu ya kuandika kwa kutaja makundi matatu ambayo ni watoto, akina Baba na Vijana. Ni vigumu kujua kwa uhakika mwandishi alitumia majina ya makundi haya kwa kuzingatia umri au hatua za ukuaji wako kiroho au alikuwa amekusudia watu wote

UFAFANUZI WARAKA WA KWANZA WA YOHANA KWA WATU WOTE.

UTANGULIZI.

1 Yohana 1:1-4

1 Yohana 1:5-2:2

1 Yohana 2:3-11

1 Yohana 2:12-14

1 Yohana 2:15-17

1 Yohana 2:18-27

1 Yohana 2:28-3:10

1 Yohana 3:11-24

1 Yohana 4 : 1-6

1 Yohana 4:7-21

1 Yohana 5 : 1-13

1 Yohana 5:14-17

1 Yohana 5:18-21

VITABU REJEA

Footnotes