Maisha Ya John G. Paton

MAISHA YA JOHN G. PATON

HISTORIA ITAYOAMSHA HARI YAKO YA KUMTUMIKIA MUNGU ZAIDI.

Shalom. Ninakukaribisha katika historia hii yenye kusisimua ya maisha ya John G. Paton mtume aliyeitwa kufanya kazi katika miongoni mwa visiwa ambavyo ni hatari zaidi kwa utumishi wake. Sehemu ambazo wengine wamechinjwa na kuliwa nyama zao mchana kweupe, sehemu ambazo watu wake hawana tofauti na wanyama ndiyo sehemu aliyoitwa naye akakubali kuitika. Watu walimhurumia, na wengine walijaa kushuhudia kama kweli Paton amekubali kwenda sehemu ya visiwa vile.

Historia hii ina mafunzo mengi ndani yake ambayo ni imani yetu yatakusogeza sehemu nzuri. 

VISIWA VYA NEW HEBRIDES

Kuna zaidi ya visiwa 80 kusini mwa bahari ya Pasifiki ambavyo visiwa hivyo vinatambulika kwa jina la New Hebrides, jina lililopewa na Kapteni James Cook mwaka 1773 kwa kile alichodai kuwa vinaufanano mkubwa na visiwa vinavyopatikana kaskazini mwa pwani ya Scotland ambavyo ni Hebrides. Visiwa vya New Hebrides vilikuwa na wakazi wasiostaharabika, wakazi wasioelimika na watu wenye mila chafu. Watu wa New Hebrides walikuwa ni watu wasiojali kwa chochote kuanzia uvaaji, ulaji, mpaka malazi yao, na mara zote walijisitiri kwa kufunika kipande cha ngozi katika sehemu zao na wengine walitembea bila chochote na hawakuonekana kuwa na walau lepe la aibu. Kibaya jamii ya watu hawa walikuwa ni watu wenye kula nyama mbichi za wanyama na ikibidi hata watu (kwa jina la kigeni hujulikana kama Cannibals)

Haitosahaulika  Novemba 20 ya mwaka 1839 wamisionari wawili wa Kiingereza waliweza kuuawa na kuliwa na wakazi wa moja ya visiwa hivi ambacho kinajulikana kwa jina la ERROMANGA, majina ya wamisionari hao ni Bwana John Williams na James Harris. Mbali na mila zao cha kula nyama za watu, pia watu wa visiwa hivi walichoshwa na wageni wa kimagharibi waliokuwa wanakuja kukalia visiwa vyao, na itakumbukwa pia mwaka 1842 ilifukuzwa timu kubwa ya wamisionari waliotoka London kutoka katika moja ya kisiwa chenye jina la TANA, wamisionari hao walidumu kisiwani hapo miezi saba tu kabla ya kuondoshwa. Sifa za visiwa hivi vilisikika sana huko ulaya na kiukweli hakukuwa na utayari wa watu kwenda kuanzisha kazi ya Mungu kule.

Mnamo kati miaka ya 1855 kanisa la REFORMED PRESBYTERIAN lililopo katika nchi ya Scotland lilitangaza uhitaji wa watu ambao wapo tayari kwenda kufanya kazi katika visiwa vya New Hebrides. Kiukweli hakukuwa na mtu mwenye utayari wa kufanya kazi hiyo kubwa, kila mtu aliogopa kwenda. Ilikuwa ni kiu ya kanisa na Dk. Bates alikuwa ndiye mtu pekee aliyeendelea kutangaza jambo hilo kwa nguvu ili apatikane mtu wa kwenda huko kumtangaza Kristo na neno lake.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida alijitokeza Bwana mmoja ambaye kanisa linamfahamu kwa jina la JOHN GIBSON PATON akijitolea kwenda katika visiwa hivyo. John Paton alikuwa ni kijana wa kati ya miaka 32 hadi 33 kipindi ambacho anaitikia wito wa kanisa katika kupeleka injili huko visiwani. Bwana John alidai kuwa na msukumo wa Mungu tangu pale alipousikia wito huo kwa mara ya kwanza na alipata muda wa kuomba ili kujihakikishia kama msukumo unatokana na Mungu au lah! Akathibitisha kuwa ulitokana na Mungu.

John Paton alikuwa ni mtumishi ambaye alishaanzisha kazi ya Mungu na kanisa la mtaani lenye jina la GREEN STREET na kazi iliyokuwa imesimama vyema. Kwa kitendo chake cha kuitikia wito ilikuwa ni jambo la furaha kwa Dk. Bates lakini lilizua minong’ono mingi kwa kanisa. Wazazi wake na John Paton walimtia moyo kuwa wao walimtoa kwa Mungu muda mrefu kutokana na agano lao na Mungu, lakini pia Dk.Bates alimtia Moyo na kuanza kumpa maelekezo ya awali.

Kipindi ambacho Paton anajitolea kwenda huko alikuwa ni mume katika ndoa changa ambayo ameifunga muda si mrefu na Bi Marry. Kipindi hicho akafuatwa na mzee Dickson ambaye kwa mshangao alimwambia WALA WATU! MNAKWENDA KUWA CHAKULA MTALIWA NA WALE WALA WATU. Baadaye John Paton akamjibu akimwambia wewe umekwisha kuzeeka sana na una muda mfupi tu wa kuishi hivi karibuni utakufa na utazikwa utakapooza kisha utaliwa na funza na minyoo kuna utofauti gani nami nitakayeliwa na hao wala nyama. KIKUBWA KWANGU NI KUMTUMIKIA KRISTO IKIWA NITAISHI AU NITALIWA, mzee Dickson akaondoa huku akirusha Nikon.

Moyo wa John Paton umezama katika kumtumikia Mungu bila kujali sehemu anayokwenda inatisha kiasi gani, bila kujali ndoa yake ni changa na wanakokwenda hawapajui alichoamua ni kuitikia wito wake na kuamua kwenda. Sasa hebu kabla ya kwenda mbele zaidi tumuangalie John G. Paton ni nani? Asili yake ni wapi? Historia yake ya nyuma ipoje? Kisha tutaendelea mbele katika maisha yake ya kitume.

JOHN G. PATON

John G. Paton alizaliwa 24, Mey 1824 Kirkmahoe, karibia na Dumfries shire huko kusini mwa Scotland. John ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kumi na moja wa James Paton na mama yao ni Bi Janet Jardine, ambapo mzee wake alikuwa ni mtu wa hali ya kawaida akijihusisha na kilimo na kazi za utengenezaji wa Soksi. Kutokana na maisha magumu waliyokuwa wakiishi John akijikuta akikatisha masomo yake akiwa na miaka kumi na mbili tu akiungana na baba yake katika kazi ya utengenezai wa soksi. Ni ukweli kwamba hakukuwa na uwezo wa kumlipia gharama za shule hata pale mwalimu wake alipojitolea kumfundisha katika vipindi japo vya kuibia ibia.

Lakini pamoja na kukatisha masomo John hakuacha kujifunza mambo mbali mbali katika elimu isiyo rasmi ikiwa ni pamoja na kujifunza lugha ya Kilatini na Kigiriki mara mbili kwa siku. Pia John hakuacha kujifunza mambo ya imani kutoka kwa Baba yake mzee James Paton, anasema baba yake ndiye aliyemuathiri na kumfundisha kumtegemea Mungu. Mzee James Paton alikuwa jasiri na mtu mwenye imani kubwa, pamoja na shughuli nyingi alizokuwa nazo John alimshuhudia baba yake aliingia katika chuma cha maombi mara tatu kwa siku. Na mara kwa mara alimshuhudia baba yake akitoka katika chumba cha maombi akiwa na sura tofauti ikiwa ni pamoja na mng’ao mfano wa Kristo katika mlima wa mgeuko, hivi ni vitu ambavyo John alivishuhudia kwa baba yake. Na hivyo ni moja kati ya vitu vilivyochochea sana imani ya John Paton.

Aliandika John: kuna wakati baba yangu alikua akiomba mara baada ya chakula na sisi wote tulimzunguka na kupiga magoti pamoja naye, alikuwa na mzigo mkubwa wa kuomba kwa ajili ya wokovu kwa watu wasiofikiwa neema ikawafikie. Tulishuhudia machozi yakimwagika, uzuri wa maombi yale hakuna ambaye anaweza kuelezea ila tulijihisi wote kuwa Kristo anashuka isivyo kawaida kila Baba anapoomba. Nasi tukamfanya baba kuwa rafiki yetu wa imani na kumtia moyo.

Baadaye John alipofikisha umri wa miaka ya ujana alipata barua ya mwaliko wa kuhudhuria shule ya parokia kujifunza na kufundisha kwa habari za umisheni, jambo lililokuwa ni la neema na furaha kwake John pamoja na baba yake.

Kipindi hicho kukatokea moja kati ya tukio maarufu katika maisha ya John ni siku hiyo ambayo alikuwa akijiandaa kuelekea katika hiyo shule ya umisionari ambayo ilikuwa nje ya mji wao, kutoka pale wanapoishi mpaka kituoni ilikuwa ni maili 40 na baba yake ndiye aliyemsindikiza. Pamoja na kupita miaka 40 lakini John anaandika, kila ninapolikumbuka tukio hilo ni kama lilitokea jana tu, walitembea mwendo wa maili sita wakiwa wanazungumzia habari za mbinguni na kazi ya Mungu ilivyo na faida huku machozi yakimiminika mashavuni.

Katika hizo maili sita, ilifika kipindi katikati ya mazungumzo yao wakajikuta wananyamaza ghafla. Kwa takrabani nusu maili walitembea wakiwa kimya bila kuongea chochote. Walipokuwa wakiendelea John alimuangalia baba yake akagundua midomo ya mzee James inacheza cheza kumbe alikuwa akiendelea na maombi ya kimya kimya, ni machozi tu yakimwagika. Baadaye alipomuangalia tena wakagongana macho na safari hii wakashindwa namna ya kusema zaidi maneno yaliwaisha huku midomo ikiendelea kugongana kwa mzee James Paton. (Imani inaweza kurithishwa John anakuja kuwa mmisionari maarufu duniani lakini alitengenezwa na baba yake, fundisha nawe watoto wako njia iwapasayo maana hawatoiacha hata watakapokuwa wazee)

Walipofika sehemu ambayo ni ya kuagana katika stesheni ya gari moshi mzee akamshika kijana wake kisha kukawa na dakika moja ya ukimya halafu akamwambia Mungu akubariki mwanangu, Mungu wa baba yako akufanikishe na kukulinda na uovu wote. Anaandika John kuwa hakuweza kuongea tena ila midomo ikiendelea kugongana na machozi yakibubujika kisha akanikumbatia na sikuweza kubakia tena nilikimbia haraka mpaka kwenye treni nikaangalia pale nilipomuacha kama mzee ameondoka lakini alikuwa amebakia, nikampungia kofia yangu, mzee alihakikisha mpaka treni limepotea kabisa ndipo alipoondoka. Moyoni mwangu nilijisikia uchungu sana, na niliapa mara kwa mara moyoni mwangu kwamba nitajitahidi kufanya kazi ya Mungu kwa bidii na kamwe sitaweza kufanya jambo lolote litakalomuaibisha baba yangu.

Na siri moja ambayo natamani uijue ni kuwa baba yake John, mzee James alitamani sana kuingia kufanya kazi ya umisionari lakini Mungu alimzuia na hivyo akaamua kuweka agano na Mungu kuwa atamtoa mwanaye mmoja kwa ajili ya kazi hiyo, na wito ukamuangukia Paton.

Baadaye Paton akafika katika shule hizo na baadaye akawa mkufunzi wa wale wenye wito wa kutumika katika utume wa Kristo. Wengine walionyesha upinzani wa moja kwa moja lakini John Paton aliamua kukomaa na kubaki katika taaluma yake iliyomleta na kuanza kuona matunda. Ilirekodiwa ukuaji mahudhurio makubwa kipindi cha uwepo wa Paton shuleni hapo tofauti na vipindi vingi vilivyopita. Lakini pia nidhamu ya shule ilipanda na wanafunzi wengi wakiweza katika kazi ya Mungu kwa moyo wa adili. Paton akapata mafanikio makubwa yanayoonekana katika kazi yake hiyo kwa muda mfupi tu mara baada ya kuanza kazi.

Lakini pamoja na yote haya hawakosi wapinzani, waliibuka watu waliompinga Patoni na kumshitaki kwa makosa kadha wa kadha kitu kilichokuwa kinazidi kumchafua katika ngazi za juu. Baadaye akapata barua kutoka katika bodi ya wakurugenzi wa wamisionari kumtaka ahamishwe. Kitu hicho hakikumsumbua sana Paton ambaye yeye huamini WANADAMU WANACHAGUA MUNGU ANAAMUA. Basi bodi ya wakurugenzi wa umisionari wa jiji baada ya kujiridhisha na kuchunguza juu ya sifa za bwana  Paton na kupelekwa katika moja ya wilaya korofi zaidi katika Jiji la Glasgow.

Wilaya korofi zaidi katika jiji hilo ilisifika kwa ulevi, uzinzi, uasherati, uuaji,utapeli, n.k ambapo yeye aliiita BABELI MPYA. Akiwa pale alikiri kazi ngumu aliyokutana nayo ilimfanya apate uzoefu mkubwa sana ambao ulimsaidia sana kihuduma katika siku za mbeleni. Alijifunza kumlingana Mungu na kumtumainia katika huduma ile ambayo Mungu ndiye mwenye kumpeleka. Kila alipokata tamaa aliisikia sauti ndani yake ikitaka awaokoe watu waliofungwa, amhubiri Kristo kwa kuwa anawapenda, asimame na Mungu.

Akiwa huko alihudumu kwa zaidi ya miaka tisa kama mchungaji katika jiji la Glasgow na baadaye akapata maono ya kwenda kufanya kazi ya Mungu katika sehemu nyingine. Akisukumwa na lile neno kuwa tufanye kazi ya Mungu bila kuchoka kwa sababu tutalipwa tusipozimia roho. Baada ya tangazo kutolewa kuwa anahitajika mtu wa kwenda katika visiwa vya New Hebrides akaamua kujitokeza pasipo kusita wala kuogopa.

SAFARI YA VISIWA VYA NEW HEBRIDES.

Ilikuwa ni kilio cha muda mrefu cha kanisa la Reformed Presbyterian kwa ajili ya kumpata mtu atakayekwenda New Hebrides pasipo na majibu,  walijitahidi hata kwa kupiga kura lakini ilishindikana mpaka alipojitokeza John Paton kujitolea kwenda kwa hiari yake mwenyewe. Pendekezo hilo la John lilipitishwa pasipo kupingwa ingawaje iliibuka minong’ono mingi, na safari hii minong’ono hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kumwonea huruma yeye mwenyewe kuwa kazi ni ngumu na huenda asiweze.

John alihitaji muda kwa ajili ya kujihakikishia na kuamua kutupitia mbali hofu ya kuuawa, magonjwa, ugeni wa eneo, mazingira ya huko na sifa zake na kuamua kushinda hofu ambayo ilionekana kwa watu wengi wa kipindi hicho akiwemo mzee Dickson. Hii ililichukua kanisa mwaka mzima kwa ajili ya kumuandaa John kwa ajili ya kazi iliyopo mbele yake. Walimwandaa kisaikolojia, wakamfundisha namna ya kuishi katika jamii ya wauaji na walaji wa damu bila kudhurika, wakamfundisha kazi na fani za kijamii ambazo huenda zitahitajika huko aendako ambazo zitaweza kuwa msaada kwa jamii ile na kumfanya asiishi kwa uhitaji. Na hapa ningependa tujifunze kitu;

Kanisa la Reformed Presbyterian lilitumia mwaka mzima kumfundisha na kumpika John anayekwenda kuwawakilisha huko New Hebrides,  John alikuwa na fani ya utabibu ambayo alijifunza siku nyingi. Huko anapokwenda kutahitajika huduma za kijamii nyingi sababu watu wale hawana ustaarabu wa kibinadamu hivyo ni wazi kuwa wanahitaji msaada mkubwa, wanaishi kama wanyama wanakula nyama mbichi, wanakula watu, hawana elimu n.k hivyo kuhubiri pekee hakutoshi ni lazima awe jibu la baadhi ya matatizo ya jamii ile ile watu wamuone kama malaika aliyetumwa na Mungu kwa ajili yao itakuwa ni rahisi kumsikia na kuipokea injili. Je kwetu sisi tuna utaratibu gani wa watu wanaoitwa shambani mwa Bwana? John alikuwa ni msomi wa theolojia na mchungaji wa muda mrefu lakini bado kanisa lilimkalisha chini kumuandaa. Tuwaandae vema watu wanaokwenda kupeleka injili na kuanzisha huduma sehemu tuwaandae Kiroho, kiakili, kijamii, na kiuchumi itarahisishia ugumu wa kazi.

Hayawi Hayawi yakawa! Hatimaye siku ikafika, siku ya kwenda huko New Hebrides kufanya kazi ya Mungu. Kama ilivyo ada walifanya ibada maalum kwa ajili ya kuwaweka wakfu mbele za Mungu kwa kazi hii, ambapo ilifanyika ibada ambayo kamwe haitosahaulika kwa kila mmoja aliyehudhuria mahali pale kwa maelezo ya J.G.Paton. Kulikuwa na umati mkubwa wa watu ambao ilikuwa ni shida kupata hata walau sehemu ya kukanyaga unyayo wa mguu, watu walitamani kuwa mashuhuda wa tukio hili kubwa, zaidi ilikuwa ni nguvu ya Roho Mtakatifu iliyofunikwa mahali pale pamoja na sadaka maalumu kwa ajili ya kazi hiyo. Tukio hili lilitokea 23 Machi 1858, akaagwa rasmi na kuianza safari yake akiwa sambamba na mke wake pamoja na watu wachache waandamizi.

Walitumia merikebu kukatiza bahari na kutokana na ubovu wa merikebu yao safari yao ilikuwa ni ngumu na ya misukosuko mingi mpaka kufika huko. Ni jambo la furaha kuona walifika salama New Hebrides ingawaje walikuwa hoi. Walipokelewa na wenyeji wao huko ambao ni waamini waliokuwa wanaishi katika visiwa hivyo. Baada ya muda kupita wakamtafutia kisiwa ambacho Bwana na Bibi Paton wataenda kuanzia katika kazi ya Mungu. Kiufupi New Hebrides ni sehemu yenye visiwa vingi vidogo vidogo ambavyo havikufikiwa bado. Basi wakapewa kisiwa kimoja kinaitwa TANNA.

JOHN PATON NDANI YA TANNA

Baada ya kupangiwa kisiwa ambacho atakikabili wenyeji wake wakajengea nyumba atakayoishi pamoja na jengo la ibada. Baada ya kufika Tanna, Bwana Paton alishangaa sana na kusema kuwa kwa macho yangu ninaishuhudia sura ya kitabu cha WARUMI 1. Anasema tabia zilizopo pale aliziona zote kwa wenyeji wa kisiwa cha Tanna, “Mungu wangu”.

Watu wale ni wanyama ambao hutembea bila mavazi na sehemu nyeti ya mwili hufunikwa na kipande kidogo cha ngozi, (mfano wa filamu ya Bushimen) na wanawake baadhi wakitengeneza mavazi ya majani na matawi ya miti. Akapaita mahali pale kilindi cha Shetani kwa jinsi alivyopakuta, anasema nilivunjika moyo kwa kiasi nilipoiona  kazi iliyopo mbele yangu, watu wale ni wajanja wajanja, wadanganyifu, wakatili na wenye kiu ya kumwaga damu. Tulishuhudia mambo hayo mbele ya macho yetu kila siku ya wanadamu bila pazia au kuzibwa (bila chenga) bila udhuru kwa miaka mingi. Katika kuwatazama watu hao katika ngozi zao, na uchi na taabu moyo wangu ukajawa na hofu kama si huruma.

Pamoja na hayo yote Bwana Paton aliiona Tanna kama shamba lililojaa mavuno mengi, ila swali alilojiuliza ataanzia wapi? Uasherati usio wa kawaida, ukatili na dhuluma viliijaza Tanna. Katika kuanza kwake kazi alilia Mungu juu ya watu wa Tanna kuwa ni nani wa kuwaokoa watu hawa wanaishi kama wanyama? Nani atakayekiponya kizazi na vizazi vinavyokuja? Ni nani wa kuondoa giza lililokuwa limetanda Tanna? Hakuna mwingine isipokuwa ni Roho Mtakatifu tu.

Kwa ujasiri usio na Kifani Paton anaanza kuikabili Tanna, anawahubiri habari za Mungu wasiomjua, anafanya kazi ya Mungu ingawa anakiri yalikuwa ni mateso yasiyo na mfano kwa kila siku moja inapokucha. Ndani ya muda waliokua wamekaa kule wakagundua kuwa mkewe ni mjamzito, lakini wakabaki kumtumikia Mungu pasipo na udhuru wowote.

KIFO CHA MKE WA PATON NDANI YA TANNA.

Wakiendelea na kazi ya Mungu visiwani humo basi kama kuna kosa moja kubwa walilolifanya walipokuwa wakiingia hapo ni kujenga nyumba katika ufukwe pasipo kuchunguza vema. Kulikuwa na mazalia ya mbu wengi maeneo yale na pia ni sehemu ambayo ilikuwa mbali na tahadhari za kiafya. Hivyo waliamua kutafuta sehemu nyingine ambayo walau itakuwa na mwinuko ili wajenge lakini walichelewa, mkewe alishikwa na homa kali ya malaria iliyoambatana na uchungu. Kipindi hicho binti huyu alikuwa ni mjamzito.

Ilikuwa ni Tar 12 Februari 1859 walipohamia makazi mapya ambayo yalikuwa sehemu ya mwinuko na siku hiyo ndiyo ambayo mkewe aliweza kujifungua mtoto wa kiume. Basi ilikuwa ni siku ya furaha isiyo na kifani ndani ya Tanna kuona baraka za Mungu zikimiminika kwao. Lakini kipindi hicho chote mkewe alikuwa na maambukizi ya maradhi mbali mbali hususan katika maeneo yale ambazo mazingira yake hawakuzoea, Malaria ikamuondoa ghafla mkewe Bwana Paton. Kitu ambacho hakukitarajia maana baada ya kujifungua mama na mtoto walikuwa salama.

Muda mfupi baadaye Bwana paton akaondokewa na mwanaye pia ambaye amezaliwa muda mfupi tu uliopita. Ilikuwa ghafla ni siku mbaya sana kwake kuondokewa na mkewe na mtoto katika sehemu kama ile na kujikuta yupo mwenyewe. Anasema ilikuwa ni huzuni ambayo kamwe hawezi kuandika uchungu wake, ni jambo linalokatisha tamaa na kuvunja moyo, linaleta simanzi na majuto tele. Alikuwa ni mkewe aliyemuoa muda mfupi tu kabla ya kuanza safari ya kuja visiwani na wakatumika pamoja kwa muda huo mfupi kabla ya Mungu kumchukua.

Alibaki kulia juu ya mwili wa mkewe na mtoto wake, na kwa kuwa hakukuwa na mtu aliyeokoka bado ilimbidi  ainuke na kutengeneza vifaa vya kuzikia (sijui kama alitengeza jeneza au sanda) ila alichimba kaburi mwenyewe na kuhifadhi miili ya mkewe na mwanaye. Na baada ya mazishi alibaki juu ya makaburi hayo usiku kucha kuyalinda ili wenyeji wa mji huo wasije kufukua na kuila nyama, ni huzuni kiasi gani.

Alibaki akila kiapo cha machozi akisema kuwa tumetoka huko kuja hapa kwa ajili ya watu wa ardhi wamrudie Mungu lakini nimemzika mke wangu hapa, sasa kifo cha mke wangu ni mbegu ambayo kwa kumlaza katika ardhi hii itamea na kuzaa watu wengi watakaomrudia Mungu. Kwa hakika Tanna inaenda kubadilika.

Binafsi nimeipenda sana imani ya John G. Paton ambaye pamoja na majaribu yote lakini hakuwa na wazo la kuiacha kazi yake, kwa muda wote aliokaa huko hakuna aliyeokoka ila bado hakuwa na wazo la kurudi mpaka anampoteza mkewe hakuwa na wazo la kukimbia kazi ya Mungu bali hasira zake zote aliwekeza kazini mwa Bwana. Mungu atusaidie kuifikia imani hii na ufahamu kama wa Paton.

MATUNDA YANAANZA KUONEKANA TANNA.

Akiwa na mwaka mmoja katika kisiwa cha Tanna aliweka jiwe la msingi na kuamua kujikita na huduma Rasmi, na hapo Idadi ya waongofu ikafikia watu ishirini kitu ambacho J.Paton alimshukuru Mungu kwa ukombozi wa watu hawa. Moja kati ya changamoto za kihuduma alizokutana nazo ilikuwa ni lugha. Lugha ambazo zilitumika katika visiwa vya New Hebrides zilikua tofauti tofauti na ndani ya Tanna upande huu waliongea lugha hii na upande ule waliongea nyingine.

Ndani ya Tanna kulikuwa ni desturi zao kwa nyakati kadhaa kuwatoa baadhi ya wanawake kama dhabihu katika kisiwa chao, jambo ambalo Paton na timu yake walilishuhudia mara kwa mara kipindi walipokuwa kisiwani. Ni umwagaji wa damu lakini hawakuthubutu kuwazuia wenyeji katika unyama wa aina hii wakijua kufanya hivyo ni kujitoa wao wenyewe kuchinjwa  na kugeuza chochote kisiwani, hivyo walinyamaza. Nyama za watu zililiwa na wanakijiji, wajane walinyongwa na mambo yote yalifanya hadharani kweupe bila chembe ya aibu.

 Wakiwa katika nyakati za mateso kama hizo za tamaduni, mila, na imani potofu bado Mungu hakuacha kuwaleta wenyeji kwa siri nyakati za usiku ili kupeleleza juu ya imani hii mpya ambayo imeletwa na Paton. Bwana Paton alikiri kuwa kuna kipindi moyo wake uliingia na hofu kuu akiwa kisiwani lakini alijitia nguvu kwa Bwana.  Na kutokana na aina ya maisha waliyoishi pale kisiwani na kafara walizokuwa wakizitoa Paton alijikita kufundisha kwa habari za sadaka ya Kristo pale msalabani na kuwa aina haja ya kuendelea na kafara. Na hapo akampata mwongofu mmoja aliyempa jina la Abraham ambaye alikuwa ni mlaji wa nyama za watu, muuaji huko nyuma lakini Kristo akamfanya kuwa kiumbe kipya. Bwana Abraham akasimama kweli kweli katika Bwana na akawa ni rafiki mkubwa wa Paton.

Akiwa anaendelea na huduma alitembelewa na viongozi ambao ni Kapten Vernon pamoja na Askofu Selwyn waliokiri kupata mapumziko mafupi na kuamua kumtembelea visiwani. Paton alijikuta ni mwenye furaha na kuuona upendo wao na kumtia moyo sana katika huduma. Pamoja na yote walimshahuri ahamie sehemu ya juu kabisa na aweke makazi huko kwa sababu za kiusalama kutokana na mazingira ya kisiwa yalivyo.

Paton aliamua kukamilisha mapema sana ujenzi wake katika sehemu kuishi kama alivyoshauriwa. Alifanya kazi ngumu upesi na akiwa katika robo ya maandalizi yake juu ya makazi mapya alishambuliwa na homa kali ambayo ingeweza kumuondoa. Lakini Abraham na mke wake walisimama kumuuguza na kukamilisha ujenzi wa makazi mapya. Bwana Abraham alijitokeza na kuwahubiri ndugu zake neema ipatikanayo kupitia Kristo Yesu. Na baadaye wakajenga rasmi nyumba ya ibada.

Kulifanyika majaribio mengi yasiyo na ukomo ya kumuua Paton lakini Mungu alikuwa anamlinda katika namna isiyo ya kawaida, alimponya na hatari zote. Baadae walipata msaada wa suruali kama jozi (pair) hamsini kutoka Glasgow kumbuka wanakijiji hawakuwa na mavazi waliyokuwa wanavaa zaidi ya kipande cha ngozi na manyasi. Lakini kama aitoshi Glasgow walichapisha kitabu cha kwanza katika lugha ya kitana. Yalikuwa ni mafanikio makubwa ya Paton kuona maandiko yanafasiriwa katika lugha mama ya kisiwani humo.

Moja kati ya vitu alivyovigundua Paton juu ya ugumu wa kupenyeza neno la Mungu kwa watu hawa na biashara za utumwa zilizoshamiri miaka hiyo. Watu wa visiwa hivi walinyanyaswa na nchi za magharibi juu ya utumwa na ukoloni kiasi cha kuwachukia wageni wote waliokuwa wanatembelea visiwani, walitafuta kujilipiza visasi kwa wazungu kumbuka hawa watu hawakuwa wazungu. Kazi yake ya kumhubiri Kristo ilikuwa ngumu kwa sababu wenyeji walikuwa wakimshuku kuwa anawapeleleza. Hivyo ikamfanya kukemea vikali sana vitendo vinavyofanywa na nchi hizi za magharibi juu ya kushiriki katika biashara za ukoloni na utumwa.

Kazi ya Mungu ikazidi kukua taratibu na hatimaye sasa hivi Paton alikuwa ana matawi sita ndani ya kisiwa cha Tanna na waliohudumu  walikuwa ni wazawa, unaweza ona jinsi kazi inavyoendelea kustawi. Tunapokumbuka kuwa walimu hawa waliwahi kuwa walaji watu, kuna sababu kubwa ya kumsifu Mungu. Paton aliendelea kuona mavuno jinsi yalivyo mengi visiwani lakini watendakazi walikuwa ni wachache na vijiji vingi vilikuwa havikufikiwa, hivyo aliweka mpango wa kuendelea kufundisha wenyeji neno na kumuweka Abraham na mkewe kama wasimamizi wa matawi hayo yote. Ilifika kipindi aliona makundi makubwa mawili yanayohitaji msaada, kundi la kwanza ni watu waliokuwa wanakuja kuulizia juu ya habari za Kristo na uweza wa Mungu na kundi la pili ni vijana waliokuwa tayari kutupa vinyago na miungu ya kipagani. Ilifika kipindi wanaume waliokwenda vitani badala ya kutoa kafara safari hii walikwenda kwa Paton na kupiga magoti ili wawekewe mkono.

Mnamo Septemba 1860 walikuja wamisionari wawili Bwana na Bi Jonsoni waliamua kuamia Tanna kwa ajili ya huduma wakitokea Nova Scotia na kupokelewa na mwenyeji wao Bwana Paton, ilikuwa ni furaha ilioje Mungu kuzidi kuisimamia kazi ya Tanna. Watu hawa walikuwa wajanja na kwa haraka walielewa lugha ya Tanna na kuchukuliana na wenyeji wa visiwani. Waliwatia moyo kwa kipindi ambacho walikuwepo visiwani hapo.

MAJANGA MAKUBWA KISIWANI TANNA

Na baadaye kipindi ambacho huduma inazidi kukua na furaha ya huduma ilipokuwa inazidi kushamiri ndipo kukatokea janga kubwa la ugonjwa WA SURUA. Surua ilikuwa ni hatari kipindi kile (kumbuka miaka hiyo hakukuwa na dawa rasmi na chanjo kama sasa hivi) kiasi cha kuua watu wengi sana kipindi hicho. Watu wengi wakaanza kukimbia visiwani, kazi ikawa ngumu sana.

Kila siku walikuwa wakichimba makaburi, wakina mama walikufa na wengine wakabaki wajane ilikuwa ni huzuni, hofu ya kifo, na uchungu usio wa kawaida. Lakini Paton akabainisha kuwa hawezi kukimbia kwa sababu ya hatari ya aina yoyote ikiwa Bwana hajamtaka aondoke. Akasimama imara na Abraham katika kipindi kigumu cha namna ile, moja la tukio ambalo John alilikumbuka vyema kuwa tarehe 21 January wakati wa jioni walichimba kaburi la mwanaume mmoja ambapo pembeni yake alisimama mjane wa marehemu, na wakati huo amesimama kama mchungaji katika ibada ya kuaga na kuulaza mwili akisema kuwa “anatumika mara baada ya taabu zake na kazi zake zikimfuata” ama kwa hakika unaweza ona ugumu wa kazi ya kuzika kila siku wapendwa, marafiki, majirani na ndugu kiasi cha kukosa neno la faraja na kuacha Mungu awe mfariji.

Kipindi hiki cha ugonjwa wa surua ulipokuwa ukitesa wakazi wa Tanna kukatokea majanga mengine makubwa zaidi na safari hii ni TUFANI NA VIMBUNGA vilivyozidi kuchukua maisha mengi, mambo hayo yalifuatana kwa uharaka mkubwa. Baadhi ya wakazi wakaeneza uvumi kuwa hayo yametokea kwa sababu miungu yao imekasirika kutokana na ibada nyingi za kikristo zilizoshika kasi visiwani. Hivyo wakaendelea kupandikiza chuki kwa watu juu ya wakristo wa visiwani humo.

Hatari ikazidi kunukia huko Tanna kwa ajili ya Paton na Rafiki yake Ibrahimu, ikichochewa na vifo vya wamisionari katika visiwa vya jirani kuwa ndiyo sababu ya mabaya yote haya. Hivyo katika Tanna Paton na Ibrahimu ndiyo waliohofiwa zaidi kuwa katika hatari ya kuuawa. Wakapokea barua kutoka kwa A.Clark iliyokuwa inasema kuwa Askofu Selwyn amewasiliana na baadhi ya watu waliomuelezea hali mbaya na machafuko huko Tanna na ya kwamba anamtumia meli itakayomchukua na kumtoa hapo Tanna ili kumpeleka sehemu salama zaidi.

Lakini Paton baada ya kuipata barua hile akifikiria juu ya hali ya Tanna katika uendelevu wa neno la Mungu, kuwa akiondoka neno la Mungu na huduma itakuwaje? akaona itakufa basi haina maana ya muda wote waliokaa huko kupotea bila matokeo. Akaamua kubaki, akamtuma Clark kumwambia Askofu kwamba atabaki, na Mungu anajua ataishi katika nchi ya watu walio hai. Lakini jambo hili linazidi kuwa kubwa kuwa akiendelea kubaki atairuhusu mauti yake kabla ya wakati.

Baadaye kama alivyokuja kwa hiari na dhamira safi kutoka ndani ndivyo alivyoshuhudiwa kuwa wakati wake wa kukaa Tanna umeshafika mwisho. Kitu ambacho kila akikiangalia kisiwa cha Tanna machozi yanamtoka kukiacha. Akiikumbuka kazi aliyoifanya anaamini kabisa imepandwa mbegu itakayoota na kumea kwa miaka mingi ijayo, na siku ya Bwana wataashwa wengi zaidi katika Tanna. Hivyo aliondoka kwa dhamira safi na si kwa kukimbia wala kuogopa kifo, japo kuna wengine walimdhiaki kuwa hana moyo kama wa Kristo na kuiacha huduma na kurudi mjini.

Ilikuwa ni mwaka 1862 alipoondoka Tanna baada ya kukaa kwa miaka minne, akapitia Australia na huko akawachangisha wakristo wa huko pesa kwa ajili ya kupata meli kubwa kwa ajili ya utumishi aliyoipata jina la Dayspring (mchana) na kurejea nyumbani huko Scotland. Na huko Scotland anapata wamisionari wengi zaidi wenye moyo na shauku ya kumtumikia Mungu tena.

KUREJEA SCOTLAND.

Mei 16, 1863 aliweza kufika London na kupokelewa vizuri, na kufikia Agost 26, 1863 alifika katika mji wa nyumbani Glasgow na kupokelewa kwa heshima. Alipoondoka alikwenda na mkewe na safari hii amerudi akiwa mwenyewe, alipokelewa kama shujaa kwa kuwa alisubiriwa kwa hamu kubwa mno. Ni heshima ambayo yeye mwenyewe hakuitarajia na kanisa likamchagua na kumpa uongozi mkubwa pale Glasgow.

Ilipofika mwaka 1864 John Paton aliweza kumuoa Bi Margaret Whitecross aliyekuwa binti wa mwandishi maarufu sana wakati huo. Na jambo kubwa sana alilokuwa nalo John Paton ni kurudi tena kule visiwani kuendelea na kazi ya umisionari. Na ni azimio ambalo liliafikiwa na mke wake mpya kwa ajili ya kazi iliyokuwa mbele yao. Hivyo wakaanza ziara ya kuliaga kanisa kwa ajili ya utumishi wake, mara baada ya kumaliza ziara zao zote yeye na mke wake wakaamua kurudi nyumbani kwao kwa mzee Paton huko Torhorwald, na kuikuta familia ikiwa inaendelea vyema na Mungu.

Mzee Paton aliwapokea vizuri kwa furaha mwanae na mkewe, na kama kawaida yake hakuificha furaha yake kwao na kawahusia maneno ya faraja katika safari yao mpya. Basi siku ya mwisho pale nyumbani walipiga magoti wawekewe mikono na wazazi wao, kwa machozi yaliyojaa upendo wazee wakawakabidhi mikononi mwa Mungu, na kuomba Mungu awape neema na nguvu mara mbili zaidi ya waliyokuwa nayo wao. John Paton alimhesabu baba yake kama kuhani wa familia,  hivyo mara zote husema mzee alikuwa anafanya kazi ya kikuhani na maombi hayo anasema ni maombi ya kikuhani.

Baada ya maombi hayo akiwa anajiandaa kuinuka kutoka magotini, John alitamani kuwaangalia wazazi wake usoni akiwa anajua hii ndiyo itakuwa siku ya mwisho kuwaona katika dunia hii. Alijisemea moyoni John “kwa heri ya kuonana macho yetu hayatoonana tena mpaka siku ya makutano katika kiyama” Basi mama akawatia moyo wakiwa wanaondoka huku kwa pamoja wakiwaombea sehemu ya Roho yao mara mbili kwa wamisionari hawa.

Kama mawazo ya John Paton yalivyokuwa kuwa inawezekana asionane tena na wazazi wake ndivyo ilivyokuwa, mwaka huo 1865 mara baada ya homa ya muda mfupi mama yake John alifariki. Na mwaka 1868 mzee John Paton alifariki na kuacha tumaini kubwa kwa wanawe na wapendwa wao kuwa amepumzika na wataonana tena katika siku ya Bwana. Kipindi hicho chote John Paton alikuwa katika huduma ya kimisionari huko katika visiwa vya ANIWA.

Walipotoka nyumbani Bwana na Bi John Paton walianza safari katika utumishi mpya kwenda katika visiwa vya Aniwa ambavyo havipo mbali sana na visiwa vya Tanna kuanzia umbali, tamaduni, imani, na mabalaa yote. Walifika Australia mwishoni mwa mwaka 1864, wakawasili Sydney mwaka mpya wa 1865. Wakiwa safarini kuelekea Aniwa alizipata habari za Ibrahimu kijana wake aliyemuacha huko Tanna akiendelea na kazi ya Mungu kwa ujasiri wa hali ya juu na kazi ya Mungu ikisonga mbele. Lakini yeye Paton hakuwa na wazo la kuelekea Tanna tena kwa sababu maelekezo yake yote ni juu ya Aniwa.

HUDUMA NDANI YA KISIWA CHA ANIWA

Kutokana na uzoefu alioupata  wa kufanya kazi katika visiwa hivi vya New Hebrides, John Paton hakua na muda wa kupoteza tena kuanza kazi ndani ya Aniwa. Walianza katika kujenga nyumba yao ya makazi yao pamoja na watenda kazi waliokuja nao, wakajenga nyumba ya ibada pamoja na majengo mengine yote yanayohitajika. Wakaanza kazi kwa wapagani wa Aniwa ambao walikuwa wamekidhiri katika mauaji ya watoto wachanga kama sadaka na wakina mama, akiamini kuwa Mungu anao uwezo wa kuwaokoa.

Kisiwa cha Aniwa kilikuwa kinakabiliwa na ukosefu wa maji safi kwa kipindi kirefu. Wenyeji wa kisiwa walitegemea maji ya mvua pekee kama chanzo pekee cha maji, hawakuwa na elimu yeyote nyingine ambayo ingeweza kuwafanya wapate maji safi,  hivyo kukakabiliwa na ukame pamoja na maji machafu ambayo hayafai ndiyo yaliyotumika. Paton aliwahurumia jinsi ambavyo walikuwa wanateseka tu kutokana na ukosefu wa maji safi, hivyo akaamua kutengeneza mpango wa kuchimba kisima.

Aliitumia njia hii ya kuchimba kisima ili apate usikivu (tension) kwa wenyeji pale ambapo anakuwa akihubiri injili juu ya Mungu mgeni kwao ambaye hawajawahi kumsikia. Hii ilileta upinzani mkubwa mkubwa sana katika jamii ambapo baadhi yao walikataa kata kata mpango wake wa kuchimba kisima, kwa kuwa hawakuamini kama kuna uwezekano wa maji safi yakatoka chini ya ardhi, wao waliamini maji safi hushushwa kutoka juu kwa miungu yao. Na ukame ule ulisababishwa na kukaidi miungu yao. Na Paton alikuja kwa habari ya kumhubiri Mungu mwingine wasiyemjua, hivyo wapinzani wakakaza katika kuwataka watu wafanye ibada kwa ajili ya kuomba mvua.

Baadhi ya wenyeji walilipenda tumaini la Paton kuwa anaweza kufanya maji yakatoka chini ya ardhi, japo hawakuamini lakini walikuwa tayari kujua ukweli wa jambo hili. Hivyo suala la maji lilikuja kuwa ni ajenda kubwa kisiwani kuliko injili aliyohubiri, watu walitaka matokeo. Hivyo kazi ikaanza na baadhi ya wanakijiji waliojitokeza walisaidia kazi hiyo, huku wale wengine wakiendelea kuomba mvua. Ikatokea wamechimba kisiwa umbali mrefu kwenda chini pasipo kupata maji kitu kilichomtia hofu kidogo Paton, na watu wa kisiwani wakaanza kuwa na hasira juu yake. Ikafika sehemu kitakachomuokoa Paton na timu yake yote aliyokuja nayo ni maji tu na wala si jambo lingine.  Watu walijipanga wakiendelea kufuatilia kwa sababu hakukuwa na dalili yeyote ya maji. Hapo ndipo wapinzani wakashika hatamu kuwarudisha nyuma hata wale walianza kuamini kuwa warejee kwa miungu yao.

Paton akajiona nafsi yake mfano wa Eliya katikati ya manabii wa baali kwa Mungu atakayeshusha moto. Ndipo Paton akagundua hapa si suala la kuchimba tu bali hii imekuwa ni vita kati ya ufalme wa Mungu na wa giza, ndipo akaingia yeye na watu wake katika maombi ya kina kwamba na ijulikane katikati ya watu wa Aniwa kama Mungu hupo. Na kwa ujasiri akawaambia watu kuwa anamuomba Mungu wake awaletee maji na watayaona, akazidi kuwaaminisha watu wale kwa Mungu. Ile habari ilikua ndiyo habari kubwa katika kisiwa kwa wakati huo iliyofuatiliwa na watu wa rika zote.

Wakati wa kazi ikiwa inaendelea hatimaye wakaona chemichemi za maji yakibubujika kutoka katika kile kisima walichokuwa wanachimba. Wanaaniwa wote wakakutanika hapo kukawa na mshangao ambao si wa kuelezea. Furaha kubwa isiyo kifani ilionekana katika watu wote wa kisiwa, baadhi yao wakamuona Paton na watu wake ni miungu waliohusika. Wakiwa katika kilele cha furaha ndipo watu wote wakaiamini injili ya Paton wakamuamini Mungu, wakakubali kuokoka wote wakubwa kwa wadogo. Upagani wote ulikomeshwa kabisa na kuzimwa katika kisiwa, watu wakapenda kusikia hadithi tamu za zamani za Kristo na fundisho la Mungu linaloteta uhuru wa nafsi.

Wakaleta vinyago, hirizi, na manyanga yao yote yachomwe kwa kumuamini Mungu, wote wakageuka na kumrudia Mungu tangu wakati huo. Sanamu zile zilizokuwa kubwa zilivunjwa na nyingine zilizikwa na wengine wakazitupa baharini, na kila mmoja hakuacha kushuhudia jinsi alivyokuwa amefungwa katika vifungo vya ushirikina.

Watu wa Aniwa walijifunza mwenendo mzuri na adabu ya familia kama maandiko yanavyotufundisha na vipawa vya Roho Mtakatifu viliendelea kurahisisha utendaji wa watu wa Aniwa katika maisha mapya ya wokovu. Pamoja na kwamba hakukua na urahisi kama ilivyo sasa lakini Bi.Paton aliandika kitabu cha nyimbo za kumsifu na kumuabudu Mungu kichotumiwa katika mikusanyiko yao.

Wakaamua kwa pamoja kujitolea kujenga jengo kubwa la ibada, wakajitokeza wote kwa pamoja kufanya kazi na kujitoa na baada ya wiki jengo likakamilika. Na ibada ya kwanza katika jengo hili ilikuwa ni ya masaa matatu mnamo mwaka 1869. Baada ya hapo wakawapokea waalimu waliokuja kuwafundisha watu wa kisiwani katika mitaala maalum, ambapo waliwafundisha neno lakini pia waliwafundisha ustaarabu na elimu tofauti. Wakatenga madarasa ya kina mama, watoto na kina baba ambapo wakaiona Aniwa katika sura mpya. Kutoka katika watu waliokuwa wakitembea bila nguo na kuona kawaida mpaka kuwa katika watu waliojisitiri vizuri na kuwa na heshima ya kifamilia.

Baadaye Paton alirudi Uingereza na kukaa mwaka mmoja na nusu na kuwaelezea huduma ya Aniwa. Aliadhimia kupata michango ya £ 6000, lakini alikabidhiwa £ 9000 alipofika Australia hii ni kwa ajili ya misaada na kazi ya Mungu kwa watu wa Aniwa.

KALENDA YA JOHN

24 mei 1824, siku ya kuzaliwa kw John,

1836, John aliacha shule akiwa na miaka 12

2 April 1858, John alimuoa Bi Marry Ann Robson, ambapo siku 14 zilizofuata John alianza safari ya kuvuka maji kuvifuata visiwa.

16 April 1858, John alianza safari rasmi ya kwenda visiwani.

5 Novemba 1859 John anaingia rasmi katika visiwa vya Tanna,

12 Februari 1859 John anapata mtoto wa kiume aliyempa jina la Peter,

Kati ya tarehe 1 au 2 Machi 1859 mama yake na Peter na mkewe na John anafariki kutokana na homa kali kisiwani hapo, kumbuka ni siku 19 tu tangu ajifungue, na hakufikisha hata mwaka tangu aolewe. John anamzika visiwani na kuulinda mwili wake usiliwe.

21 Aprili 1859 Peter mtoto wa John anafariki. Kumbuka alidumu katika siku 39 tu John anamzika pembeni mwa kaburi la mama yake.

1862 John anarudi Scotland

17 Juni 1864, John anamuoa Bi Margaret (Maggie) Whitecross.

24 Machi 1865 Wanapata mtoto wa kiume Robert

Agosti 1866 waliweza kurudi New Hebrides sasa hivi katika kisiwa cha Aniwa.

16 Mei 1905 Maggie Whitecross mkewe Paton alifariki akiwa na umri wa miaka 64 huko Australia

28 January 1907 John Paton alifariki akiwa na miaka 82 huko Australia kumbuka ni miaka miwili baada ya kifo cha mkewe.

REJEA

“You will be eaten by cannibals” posted February 8, 2000. Accessed though https://www.desiringgod.org/messages/you-will-be-eaten-by-cannibals-lessons-from-the-life-of-john-g-paton.

Paton, G John., Kent Albert and Paton James. The Story of Dr. John G. Paton’s, Thirty Years with South Sea Cannibals, New York: Doran. 1907.

Paton, G John. Mission to The New Hebrides, New York: Chicago Fleming H. Revell Co. 1889.