Je Mwivi Katika Yohana 10:10 Ni Nani?

JE MWIVI KATIKA YOHANA 10:10 NI NANI?

Biblia inatakiwa kusomwa kwa kufuata MUKTADHA yaani mfululizo au mtiririko wa mawazo/habari. Mstari wa biblia ukitolewa kwenye muktadha unaweza kuwa na maana yeyote anayotaka msomaji kitu ambacho sio sawa. Kusoma kwa muktadha sio rahisi kama ambavyo tunaweza kusema, kwa nini ni ngumu? Mara nyingi tunapoiendea Biblia huwa tunakuwa na majibu tayari tunayoyajua kwa kuyasikia kwa watu hivyo ni rahisi kujisoma mwenyewe kuliko kusoma Biblia.

Yohana 10:10 inasema

10.10  Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.

Bila shaka Biblia imesema mwivi anachofanya lakini haijamtaja mwivi ni nani hapo.

Mstari wa kwanza wa Yohana 10 pia anaeleza kuhusu mwizi pia. Mstari wa Kwanza unasema…

10.1  Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang’anyi.

Mstari wa nane sura hii hii pia Yesu anaelezea Mwivi lakini sasa katika Mwingi

10.8  Wote walionitangulia ni wevi na wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia.

Yesu hapa anajiweka upande wa Mchungaji wa kondoo na kundi la Pili ni Mwivi au wevi na Zaidi hili kundi la pili anatumia neno Zaidi ya wivi tu anasema Mnyang’anyi au wanyang’anyi.

Yesu anaongezea kwa kusema sifa za hawa wevi au huyu mwivi ni

10.12  Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.

Ukisoma vizuri utagundua Yesu anajielezea Yeye kama mchungaji mwema kwa kuwa atautoa uhai wake kwa ajili ya kondoo lakini upande wa pili anasema hawa wevi au huyu mwivi hawajali kondoo kwa kuwa sio mali zao/yake na Zaidi wakiona Mbwa mwitu wanakimbia.

Hii yote ni LUGHA YA PICHA Yesu anatumia akijiita mchungaji mwema na kundi ambalo liko kinyume nae ni wevi, wanyang’anyi na ni watu wa mshahara.

Kwa nini Yesu anatumia Lugha hii ya Picha?

Yesu amejifunza maandiko tangu akiwa mtoto hivyo hata mifano yake au Lugha yake ya picha haiendi mbali na maandiko. Yesu anatumia Lugha ya Picha iliyotumika katika Ezekieli 34. Katika Ezekieli 34 Mungu anamwambia Ezekieli atoe onyo kwa wachungaji wa Israeli yaani viongozi wa dini ya kiyahudi kwa kuwa hawafanyi kama Mungu anavyowataka kufanya (Soma ezekieli 34 kuelewa vizuri). Lakini Mungu haiishii kutoa onyo tu bali anatoa Ahadi kwamba…

10 Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao.

11 Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia.

12 Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza.

13 Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu.

14 Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli.

15 Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU.

16 Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.

Mungu anaahidi iko siku atakuja yeye Mwenyewe kuwalisha kondoo wake wa Israeli (Hii ndio maana Yesu anasema anao kondoo ambao sio wa zizi hili, zizi likiwa ni Israeli akionyesha kuna kundi mbali na waisraeli wapo kwenye zizi lake la sasa yaani mataifa)

Mungu atawachunga mwenyewe kwa namna gani?

Anaeleza hapo hapo

23 Nami nitaweka mchungaji mmoja juu yao, naye atawalisha, naam, mtumishi wangu, Daudi; yeye atawalisha, naye atakuwa mchungaji wao.

24 Na mimi, Bwana, nitakuwa Mungu wao, na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mkuu kati yao; mimi, Bwana, nimesema haya.

25 Nami nitafanya agano la amani nao, nami nitawakomesha wanyama wakali kati yao; nao watakaa salama jangwani, na kulala misituni.

Atamuweka Mchungaji mmoja Mtumishi wake Daudi? Daudi mbona alikufa zamani wakati wa Ezekieli?

Kuna mengi ya kusema lakini Mungu alikuwa anamaanisha Masihi ndiye atakaye kuwa mchungaji juu ya kondoo wa Israeli na wale wote wachungaji wasiofanya kama alivyowapa kufanya hawatakuwa na nafasi ya kuwasumbua kondoo

Kwa Ezekieli wachungaji sio shetani bali ni viongozi wa dini ya kiyahudi ambao walikuwa wanafanya tofauti na Mungu alivyotaka wafanye.

TURUDI YOHANA

Habari ya Yohana 10 inaanzia Yohana 9. Katika Yohana 9 habari inaanza Yesu  anamponya Kipofu tangu kuzaliwa lakini mafarisayo (Viongozi wa dini ya kiyahudi) wakamsumbua kipofu na  wazazi wake kwa kuwa walikuwa hawamwamini Yesu kama ndiye Masihi.

Usumbufu huu sio wa kumwita tu mara nyingi kumuuliza kuhusu Yesu bali nyuma yake usumbufu huu ulikuwa na agenda ya kutaka kujua kama kipofu anamwamini Yesu kuwa ndiye masihi na wao walikuwa wamekubaliana kuwa atakaye mkubali Yesu kuwa ndiye masihi atatengwa na sinagogi. (Kipofu alimwamini na mpaka Kumwabudu)

9.22  Wazazi wake waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi.

Hivyo mzozo ulikuwa kati ya Yesu na mafarisayo (Viongozi wa dini walikokuwa wanafanya tofauti na Mungu anavyotaka). Yohana 10 ina muktadha huu wa kutoka sura ya 9.

Hivyo Yesu anapoanza kuzungumza sura ya 10 anazungumza kutokana na tukio la sura ya tisa.

Anawasema mafarisayo (Viongozi wa dini ya kiyahudi) kuwa ni wanyang’anyi na wevi kwa mambo wanayoyafanya kwa kutumia Lugha ya picha kama Ambavyo Mungu alizungumza na viongozi wa dini wa kiyahudi kwa kutumia kinywa cha mtumishi wake Ezekieli.

Hivyo Yesu anajitofautisha na mafarisayo kwa kutumia tukio la kondoo (Kipofu na wale wanao mwamini).

Je ni mafarisayo tuu ndio Yesu alimaanisha ndio wevi na wanyang’anyi? Jibu sio wao tu bali tangu awali walikuwepo viongozi wa dini wa kiyahudi ambao walifanya tofauti na Mungu alivyotaka na Mungu alishawaonya.

Hivyo Katika Yohana 10;10 (Pamoja na Yohana 10:1 na 10:8) Mwivi/Wevi ni Viongozi wa Dini ya kiyahudi wanaofanya mambo tofauti na maagizo ya Mungu.

SISI LEO TUNAJIFUNZA NINI?

Kwa kuwa Hili ni neno la Mungu kwa ajili yetu ni vizuri kujua kwamba linasema na sisi leo kama lilivyosema na wayahudi karne ya kwanza. Kwetu leo andiko hili linatufundisha kutambua wevi na wanyang’anyi yaani viongozi wa dini ambao wanafanya mambo tofauti na maagizo ya Mungu. Tutawatambuaje? Kwa kuangalia sifa zao Yesu alizozitaja..

Kwamba wao ni Watu wa Mshahara, watu ambao wakiona mbwa mwitu hukimbia na kuacha kondoo, watu wenye malengo na kazi ya kuiba, kuchinja na kuharibu.

Soma Biblia taratibu kwa kuzingatia Mtiririko wa Mawazo kuepuka kupata maana isiyo sawa.