Hagai – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA UJUMBE WA NABII HAGAI.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.

UTANGULIZI.

Ujumbe wa Nabii Hagai uliopo kwenye kitabu hiki ulitolewa kwa kipindi cha wiki kumi na tano tu, yaani miezi mitatu na wiki tatu. Ujumbe huu, uliotolewa katika semina nne tofauti, ulianza tarehe mosi ya mwezi wa sita (Hagai 1:1) na kumalizika tarehe ishirini na nne ya mwezi wa tisa (Hagai 2:10, 20), katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario katika Dola ya Uajemi.[1] Ujumbe wa nabii ulikuwa kwanza kwa viongozi wawili, yaani Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu. Pili, ujumbe huo ulikuwa kwa ajili ya Waisraeli waliorudi nyumbani kutoka utumwani. Baada ya kazi hii ya muda mfupi ya nabii Hagai, nabii Zekaria aliendeleza kazi ya kuwasukuma na kuwatia moyo viongozi hawa wawili na Waisraeli ili kujenga tena Hekalu (Ezra 5:1, 6:14).

MUKTADHA WA KIHISTORIA WA UJUMBE WA NABII HAGAI.

Baada ya utawala wa Suleimani kuisha, taifa la Israeli liligawanyika na kuwa mataifa mawili: Israeli na Yuda (1 Wafalme 12:1-22). Israeli walianza kuabudu sanamu mara tu baada ya kutengana na Hekalu la Jerusalem (1 Wafalme 12:23-33). Hivyo, Mungu akawatuma manabii kuwaonya kwa mabaya waliyoyafanya. Kati ya manabii wengi Mungu aliowatuma, wapo Hosea na Amosi. Kwa kuwa Israeli haikusikia sauti ya Bwana kupitia manabii hao, Mungu aliruhusu Israeli kupigwa na kuchukuliwa mateka na Dola ya Ashuru. Dola ya Ashuru iliwatawanya Waisraeli kwenye maeneo mbalimbali na kuwachukua watu wengine kutoka maeneo mengine na kuwaleta kwenye ardhi ya Israeli, na hivyo Israeli ikapoteza utaifa wake (1 Wafalme 17).

Pamoja na hayo, taifa la Yuda halikujifunza kutoka kwa ndugu zao; nao walifanya mabaya mbele za Mungu (1 Wafalme 17:19). Mungu pia aliwatuma manabii kwa taifa la Yuda kuwaonya kutokana na dhambi zao, hasa ibada ya sanamu na udhalimu wa kijamii/ukiukaji wa haki katika jamii (1 Wafalme 17:13). Kati ya manabii wengi Mungu aliowatuma, wapo Mika, Isaya, na Yeremia. Kwa kukosa kutubu, Mungu aliruhusu taifa la Yuda kupigwa na watu wake kupelekwa utumwani Babeli kwa awamu mbili: awamu ya kwanza chini ya ufalme wa Yehoyakimu (2 Wafalme 23:34-24:1-7) na awamu ya pili wakati wa ufalme wa Yehoyakini (2 Wafalme 24:8-20). Pamoja na watu wengine kubaki Yuda na mfalme Nebukadneza kuweka mfalme juu ya Yuda, Israeli waliobaki hawakumrudia Mungu, na hivyo Nebukadneza akarudi tena na kuupiga mji wa Jerusalemu na kuuchoma moto (2 Wafalme 25). Hili lilitokea baada ya nabii Ezekieli kutabiri hivyo kwa wale waliokuwa utumwani tayari wakati na yeye akiwa utumwani. Mpaka hapa, Israeli na mataifa mengine mengi yalikuwa yanatawaliwa na Dola ya Babeli.

Kama Mungu alivyotabiri kupitia kinywa cha nabii Danieli (na Isaya pia) kwamba atainua ufalme mwingine baada ya Babeli, basi Mungu akainua Dola ya Umedi na Uajemi (Danieli 2, 7, na 8). Umedi na Uajemi walipiga Dola ya Babeli na hivyo mateka wote na makoloni yote ya Babeli yakawa chini ya utawala wa Umedi na Uajemi. Mungu akatumia utawala huu kuwaruhusu taifa la Yuda kurudi nyumbani kwao na kuwa na shughuli zao za ibada kama ilivyokuwa mwanzo (2 Nyakati 36, Ezra 1:1-4). Hii ni baada ya taifa la Yuda kuwa utumwani Babeli kwa muda wa miaka sabini kama ilivyotabiriwa na nabii Yeremia (Yeremia 25:1). Sera ya utawala wa Umedi na Uajemi iliwaruhusu mateka kurudi kwenye mataifa yao na kuendelea na shughuli zao za kuabudu pamoja na kwamba waliendelea kuwa chini ya utawala huu.

Waliporuhusiwa kurudi, watu wa Yuda hawakurudi wote kwa wakati mmoja; walirudi kwa makundi matatu tofauti. Kundi la kwanza lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Sheshbaza na Zerubabeli, na kusudi lao lilikuwa ni kujenga Hekalu kwanza (Ezra 1-6). Baada ya hatua za kwanza za ujenzi, yaani ujenzi wa msingi (Ezra 3:8-13), upinzani kutoka nje na ndani ulisimamisha kazi kwa muda wa miaka 14. Kwa kusimamishwa kwa kazi ya Hekalu, watu walianza kufuata maslahi yao ya kibinafsi na kujijengea wenyewe majumba mazuri ya kuishi, wakisahau kabisa ujenzi wa Hekalu waliouachia njiani. Hapo ndipo Mungu alipomtuma nabii Hagai kuwarudisha Yuda katika ujenzi wa Hekalu. Baada ya nabii Hagai, nabii Zekaria aliendeleza kazi, na mwishowe Hekalu likajengwa na kukamilika miaka minne baadaye (Ezra 6:14-15).

Kundi la pili la Waisraeli lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Ezra, ambaye alirudisha usomaji na ufuataji wa torati ya Musa (Ezra 7-10). Kundi la tatu lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Nehemia, ambaye alirudi kwa lengo la kujenga tena ukuta wa Yerusalemu uliobomolewa (Nehemia 1-13).

.

UJUMBE MKUU WA NABII HAGAI.

Ujumbe wa Nabii Hagai unasisitiza umuhimu wa kutanguliza ujenzi wa Hekalu la Mungu kule Yerusalemu baada ya Waisraeli kurudi kutoka utumwani/uhamishoni. Hagai anawataka watu wazingatie njia zao na kutanguliza nyumba ya Mungu kuliko mambo yao wenyewe (1:1-15). Licha ya kufikiri kwamba Hekalu hili jipya halitakuwa na utukufu kama lile la kwanza, Hagai anawahakikishia watu kwamba Mungu yuko pamoja nao na hivyo Hekalu hili litakuwa na utukufu kuliko lile la kwanza (2:1-9). Pia Mungu anawaonyesha watu wake kwamba dhambi ya kukataa kujenga Hekalu lake iliwafanya kila wanachokifanya kuwa najisi mbele zake, lakini sasa kwa kuwa wamekubali kujenga Hekalu, atawabariki (2:10-19). Hatimaye, Hagai anahitimisha kwa ahadi kwa Zerubabeli, akithibitisha jukumu lake na hatima yake kama kiongozi aliyechaguliwa (2:20-23). Kwa ujumla, kuna mambo matatu ya msingi katika ujumbe wa nabii Hagai: kujengwa kwa Hekalu la pili lenye utukufu kuliko lile la kwanza (2:6-9), falme kupinduliwa na kupigwa (2:20-22), na kurejeshwa kwa uongozi wa ukoo wa Daudi katika Israeli (2:23).

MPANGILIO WA KITABU.

NambaMaandikoMaelezo
11:1-15Hotuba ya Kwanza
22:1-9Hotuba ya Pili
32:10-19Hotuba ya Tatu
42:20-23Hotuba ya nne

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.

Hotuba ya kwanza ya nabii Hagai ilitolewa siku ya kwanza ya mwezi wa sita mwaka wa pili wa mfalme Dario juu ya Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki (1:1). [2] Hotuba hii inaanza na kukosoa mtazamo mbaya wa waisraeli uliowafanya wasijenge nyumba ya Mungu (1:2), na badala yake wakajenga nyumba zao wenyewe na kutelekeza nyumba ya Mungu (1:3-4). Hivyo, Bwana anawaita kutafakari chaguo hili walilolifanya (1:5). Baada ya hilo, Bwana anawaonyesha madhara waliyoyapata tayari kwa sababu tu waliacha kujenga nyumba yake (1:6-11). Madhara haya ni pamoja na kukosa utoshelevu katika maeneo mbalimbali (1:6). Kabla ya kuendelea kuwaonyesha madhara yaliyowapata, Mungu anawaita kutafakari na kuwataka wamjenge yeye nyumba (1:7-8). Madhara mengine yaliyowapata ni kupata matokeo wasiyoyapenda (1:9), kukosa mvua na mazao (1:10), na kupata ukame katika hali na kazi zote za mikono (1:11). Baada ya hotuba hii ya kwanza, Viongozi hawa wawili pamoja na waisraeli walitii sauti ya Mungu wakaanza kujenga tena Hekalu siku ya ishirini na tatu toka siku ya kutolewa ujumbe huu (1:12-15).

Hotuba ya pili ya nabii Hagai ilitolewa mwezi mmoja baadaye, yaani siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba wa mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario (2:1-2). Katika Hotuba hii, Mungu anawaonyesha kwamba kwa mtazamo Hekalu hili wanalojenga sasa halina viwango ukilinganisha na Hekalu la mwanzo lililojenga na Suleiman (2:3). Lakini pamoja na muonekano huo, Mungu anawatia moyo kwamba yeye yuko pamoja nao (2:4-5). Kwa kuwa yuko pamoja nao, yeye atalifanya Hekalu hili kuwa bora zaidi ya lile lililojengwa na Suleimani kwa kuwafanya mataifa walete vitu vya thamani katika hekalu hili, kwa kuwa vitu hivyo ni mali yake yeye. Vitu hivyo ni kama fedha na dhahabu (2:6-9).

Hotuba ya tatu ilitolewa siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa ya mwaka huo huo, yaani miezi mitatu baada ya kuanza kulijenga tena Hekalu la Bwana (2:10). Katika Hotuba hii Mungu anawauliza makuhani maswali mawili ili kupitia majibu yao awajulishe Israeli hali yao (2:11). Swali la kwanza, Je, kitu kitakatifu kikigusa vyakula , vyakula hivyo vinatakasika? Jibu ni hapana (2:12). Swali la pili, Je, ikiwa kitu najisi kikigusa vyakula, vyakula vinakuwa najisi? Jibu ni ndio (2:13). Kwa kanuni hii, ni dhahiri utakatifu hauji kwa kugusana ( hauwezi kuhamishwa), lakini unajisi unaletwa kwa kugusana (unahamishika). Kupitia kanuni hii Mungu anawaonyesha Israeli hali yao. Kwa sababu ya kukataa kujenga nyumba yake (Unajisi) hivyo kazi zote wanazozinfanya ni najisi (2:14). Hivyo Bwana anawaambia watafakari yaliyowapata wakati ambao hawakuwa watiifu, Mungu aliwazuia wasifanikiwe (2:15-16), na akawapiga kwa upepo, ukungu na mvua ya mawe (2:17). Bwana anawaita tena kutafakari jinsi ilivyo tangu walivyoanza kujenga nyumba yake, kwamba yeye ameanza kuwabariki ndio maana wameweza kupanda na hivyo sasa wanasubiria mavuno ambayo yatakuwa ni ya baraka (2:18-19).

Siku hiyo hiyo ambayo Hagai ilitoa hotuba yake ya tatu, akatoa hotuba ya nne (2:20). Hotuba hii ni fupi kuliko zote zilizopita na ni utabiri kwa Zerubabeli, liwali wa Yuda. Mungu anasema kwamba, kupitia Zerubabeli, liwali wa Yuda Mungu atapindua na kuzipiga falme zingine (2:21-22). Na baada ya hilo Mungu anaahidi kumfanya Zerubabeli kuwa mtawala teule mwenye mamlaka yake (2:23).

FOOTNOTES


[1] Kwa kalenda huu ulikuwa ni mwaka 520 K.K.

[2] Kwa kalenda ilikuwa ni tarehe 29 mwezi wa nane mwaka 520 K.K.

UFAFANUZI UJUMBE WA NABII HAGAI

UTANGULIZI

MWANDISHI WA KITABU

AINA YA KITABU/UANDISHI

MUKTADHA WA KIHISTORIA WA KUTOLEWA UJUMBE

WAPOKEAJI WA AWALI WA UJUMBE

MPANGILIO WA KITABU

HAGAI 1:1-11

HAGAI 1:12-15

HAGAI 2:1-9

HAGAI 2:10-19

HAGAI 2:20-23