Jacob Deshazer -Jifunze Msamaha

Neno msamaha ni neno ambalo lina maana kubwa kuliko wakati fulani tunavyoweza kulielezea, yapo masomo mengi sana yanayofundisha kusamehe na kusamehewa lakini bado hayamalizi ukubwa na upana wa neno msamaha. Na leo katika makala hii tumekuandalia historia ya maisha ya mtu mmoja anayeitwa Jacob DeShazer ambayo itakuacha na somo kubwa sana la msamaha katika moyo wako, karibu.

JACOB DESHAZER (Familia)

Jacob DeShazer ambaye watu wengi walipenda kumuita Jack, ni mzaliwa na Raia wa Marekani huko West Stayton, Oregon, Salem ambapo alizaliwa tarehe 15 Novemba, 1912. Katika makuzi ya Jacob hakuwahi kumjua baba yake kwa kile alichoelezwa kuwa alifariki alipokuwa na umri usiozidi miaka miwili. Baba yake na Jacob alikuwa ni mchungaji aliyesimamia kanisa la Church of God, na mama yake Jacob alikuwa ni mwamini mzuri wa Mungu. Jacob ni mtoto wa tatu kwa mama yake lakini Baba yake alikuwa na watoto wengine wanne ambao aliwapata kabla ya Jacob. Kiufupi baba yake na Jacob aliwahi kuoa kabla ya kukutana na mama yake Jacob ila mkewe alifariki akiwa mdogo na kumuachia watoto wanne; wakike watatu na mmoja wa kiume. Hivyo mama yake Jacob akawajibika kuwatunza kama mama yao kipindi chote cha ndoa yake.

Baada ya kuolewa Hulda mama yake na Jacob aliweza kuzaa watoto wanne ambao watatu wa kike na mmoja ni wa kiume ambaye ndiye Jacob, Jacob kwa mama yake alitanguliwa na dada zake wawili na kufuatiwa na mdogo wake wa mwisho ambaye ni wa Kike. Hivyo wakajikuta wakiishi kwenye familia ya watoto nane pamoja na hao ndugu zao wa kambo ambao kati yao sita ni wa kike.

Huzuni ilijitokeza katika familia hii kubwa mjini Salem baada ya kuondokewa na Baba ambaye alisumbuliwa na ugonjwa wa tumbo. Familia yote inabaki kumuangalia mama yake na Jacob. Kutokana na mzigo kuwa mkubwa ilishindikana Hulda kuwalea watoto hao wote nane, hivyo akawarudisha watoto wale wanne wa kambo upande wa baba yao naye akawajibika kuwalea wale wanne wa kuwazaa. Bado watoto wanne ilikuwa ni mtihani mkubwa sana kwa Hulda ambaye kuna wakati walikosa chakula, na mahitaji mengine ya muhimu kutokana na hali ngumu ya kimaisha aliyokuwa akikabiliwa nayo.

Baada ya miaka mitatu kipindi ambacho Jacob ana miaka mitatu mama yake aliolewa tena na bwana Hiram Andrus mwanaume wa miaka 47 ambaye walikutana kanisani huko Salem. Ambapo baada ya miaka michache mbele walifanikiwa kupata watoto wengine wanne ambao watatu walikuwa wa kike na mmoja wa kiume kitu kilichomfanya Jacob awe na aibu kutokana na familia kuwa na mabinti wengi kuliko watoto wa kiume.

KIIMANI

Kwa upande wa imani familia yao ilikuwa vizuri ambapo baba yake wa kambo alikuwa ni mtu mwenye kufundisha watoto neno la Mungu na kuwasomea sura kadhaa za maandiko kila siku baada ya chakula. Alijitahidi kuijenga familia katika misingi mizuri ya kiimani na hapo Jacob alianza kuhudhuria vipindi mbalimbali vya kikanisa ikiwemo Sunday School. Lakini ajabu ni kwamba Jacob alijikuta akitofautiana na mwalimu wake wa sunday school na kuanza kuchukia na imani yenyewe. Hali mbaya ya kutokuamini ikazidi kupata nafasi ndani ya Jacob akiwa bado mdogo na kujikuta anaingia katika kundi la watu wasioamini kabisa uwepo wa Mungu.

Ndiyo, Jacob hakuamini kabisa uwepo wa Mungu na kujikuta akiwahurumia familia yake kwa kupoteza muda mwingi na nguvu kubwa kwa ajili ya Mungu ambaye hayupo. Kuna wakati aliwaona watu wa familia yake kama wana kichaa cha kiimani, wamechanganyikiwa katika masuala hayo.

UJANA

Maisha daima yanasonga mbele na umri unazidi kusogea, Jacob akiwa shule alikuwa anapenda sana mpira wa miguu na Baseball pamoja na kwamba hakuwa na kimo kikubwa lakini alikuwa ni mchezaji mzuri. Lakini hakufanikiwa kujiunga hata na timu ya shule kwa kuwa baba yake aliwekeza zaidi kazi kama kipaumbele chake cha kwanza hivyo kujikuta anatumikia shambani muda mwingi baada ya masomo. Kwa upande wa masomo alikuwa akipenda zaidi hesabu na alikuwa mwanafunzi mzuri ambaye aliweza kuchaguliwa kujiunga na high school, ilipofika mwaka 1931 Jacob alihitimu masomo yake akitarajia kujiunga na elimu ya juu.

Lakini mwaka huo kulitokea na msukosuko mkubwa wa kiuchumi kule Marekani, kitu ambacho kilipelekea familia nyingi za chini kushindwa kukidhi baadhi ya mahitaji. Na hapo ndipo safari ya elimu kwa Jacob ilipokwisha rasmi na kuangukia kutafuta ajira zisizo rasmi mitaani.

Akiwa mitaani Jacob alijikuta akifanya hiki na kile na alifurahia maisha yake mapya na hapo ndipo Jacob aliacha rasmi kwenda kanisani. Jacob alikuwa mjanja wa mjini hivyo aliweza kufanya kazi tofauti tofauti kwa vipindi tofauti tofauti lakini pesa aliyokuwa akipokea nayo ilikuwa ya kawaida tu.

Ilipofika mwaka 1940 Jacob aliamua kuchangamkia fursa ya kujiunga na Jeshi, kwa vile aliamini kutokana na vuguvugu la vita linaloendelea Marekani itahitaji kujiimarisha. Jacob akaamua kutuma maombi ya nafasi za jeshi na hatimaye akakubaliwa, na hapo ndipo maisha ya Jacob yakabadilika rasmi.

Akiwa jeshini alitamani zaidi kujiunga na kikosi cha anga, matamanio yake yalikuwa ni urubani. Ingawa alikatishwa tamaa na wenzake wengi lakini yeye alidhamiria kuwa rubani wa ndege za vita, umri wake ulikuwa umevuka miaka 25 ambapo kwa sheria za jeshi enzi hizo huwezi kujifunza mafunzo hayo ila kama alivyodhamiria alifanikiwa kupata na kujifunza kwa bidii mpaka kufuzu. Mpaka sasa katika historia yetu Jacob ni mwanajeshi wa Marekani.

MGOGORO KATI YA JAPANI NA MAREKANI.

Tukirejea miaka hiyo kulikuwa na mgogoro mkubwa ulioendelea kati ya Marekani na Japani kutokana na mustakabali wa bahari ya Pasifiki, Mgogoro ambao haukuwa na muafaka wa kuelewena. Na kufikia mwaka 1940 vita kuu ya pili ya dunia ilikuwa ikilindima huko katika mataifa makubwa ya Ulaya, ambapo Marekani iliombwa sana nayo iwe mmoja kati ya washiriki wa vita hiyo dhidi ya Ujerumani, lakini Marekani hakuwa na msimamo wa moja kwa moja kuingia katika vita hiyo, hivyo alikaa pembeni.

SHAMBULIZI KATIKA BANDARI YA LULU (PEARL HARBOR).

Kutokana na mgogoro uliodumu muda mrefu kati ya Marekani na Japani bila kuwa na muafaka, Japan Ikaamua kuishambulia Kambi ya Marekani katika kisiwa cha Hawaii ambapo walishambulia mpaka makazi ya raia walikuwa wakiishi humo. Ilikuwa ni December 7, 1941 ambapo Japani kupitia ndege zao walifanya uharibifu mkubwa wa mali na kugharimu maisha ya watu pia. Ilirekodiwa watu zaidi ya 2,300 walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.

Kutokana na shambulio hili, ifikapo Desemba 7 kila mwaka Marekani hufanya maadhimisho ya tukio hilo kwa ajili ya kuwaenzi wale wote waliopoteza maisha yao.

Baada ya tukio hili ilipelekea Marekani kutangaza kuingia katika vita ya pili ya dunia rasmi kwa lengo la kumkabili mjapani. Japani pia waliharibu meli kadhaa za jeshi pamoja na ndege nyingi za jeshi la Marekani.

HALI YA VITA

Habari za shambulio hilo la ghafla lilichukua sura nyingine huko Marekani, ambapo vilio,huzuni na hasira nyingi viliambatana pamoja na uchungu kwa wamarekani wote. “Lazima walipe! Japani lazima walipe kwa hili! Na watalipa” ilikuwa ni sauti ya Jacob DeShazer aliyesikia taarifa hii katika spika ya matangazo yaliyokuwepo kambini wakati huo alikuwa akimenya viazi. Alipiga kelele akiwa na hasira kali huku akisema watalipa kwa hakika lazima walipe.

Jacob akasainiwa kama mwanajeshi wa kikosi cha anga rasmi Januari 1942 akahamishwa kutoka mji wa California mpaka kwenye kambi ya kikosi cha anga Culumbia, kusini mwa mji wa Carolina. Akiwa katika majukumu yake pale akapokea ujumbe kuwa Kapteni anataka kumuona, akaanza kuogopa na kujikagua yamkini atakuwa amefanya kosa lakini wapi! Aliporipoti ofisini kwa Kapteni akashangaa kuona wanajeshi wenzake kama 20 hivi wa kikosi cha anga wakiwa katika ofisi ya Kapteni. Kapteni alionekana kusubiri ujio wa Jacob kabla ya kuanza kuzungumza na alipoingia tu Jacob akaanza kwa kusema, vijana nimetaarifiwa kuwa tunakabiliwa na misheni ya hatari sana mbele yetu, hivyo nahitaji watu watakaoweza kujitolea katika hili, kisha akawaangalia watu wote usoni na kusema, kama nilivyosema watu watakaojitolea. Hii si lazima hivyo mtu awe huru kwangu mimi sina shida kabisa mtu akikataa kulingana na misheni iliyo mbele yetu. Misheni hiyo inatakiwa kufanyika wapi? Mtu mmoja aliuliza, na itakuwa ni kwa muda gani? Mtu wa pili akadakia. Na tunahitajika watu wangapi? Maswali lukuki yakaendelea kutupwa bila mpangilio mpaka pale Kapteni alipoinua mikono yake ishara ya kutaka utulivu.

Jamani nimewaambia yale ambayo ninayafahamu kwa sasa, hii misheni ni misheni iliyotoka ngazi za juu na inaendeshwa kwa usiri mkubwa.Mengi mtayajua mpaka pale ambapo mtakubali kuingia katika jambo hili. Waliendelea kuuliza maswali mengi ya sintofaamu na wakapata majibu ya aina hiyo hiyo. Ukafika wakati wa kufanya maamuzi na watu wote waliokuwepo walinyoosha mkono ishara ya kukubaliana na suala la kujitolea, lakini Jacob alikuwa wa mwisho kunyoosha mkono wake kutokana na hofu. Alijua hii inaweza kugharimu maisha yake lakini aliona aibu kukataa ikiwa wenzake wote walikubali, hivyo akainua mkono huku akiwa na hofu kiasi cha tumbo kuvuruga.

Baadaye wakaendelea na michakato mingine iliyoendelea ikiwa ni pamoja na kujiunga na wenzao wengine waliojitolea na kugawanywa katika makundi makundi pasipo kujua bado ni misheni gani iliyo mbele yao. Wakapewa ndege ambazo zitatumika na Jacob na wanzake walipewa ndege aina ya Mitchell B-25.

Baada ya maandalizi yote kukamilika marubani wote wakapewa nasaha kabla ya kuingia katika meli kubwa ya jeshi na safari kuanza pasipo  kujua ni wapi wanaelekea. Ilichukua siku kadhaa ndani ya meli huku kukiwa na minong’ono ya hapa na pale kwa makamanda hao juu ya wapi wanaoelekea. Baadaye kamanda akawaeleza ukweli wote wa misheni yao ikiwa ni mwishoni kabisa wa safari yao na tukio linaloanza ni utekelezaji.  Usiku ule ulikuwa usiku mrefu sana kwa marubani wote ndani ya meli wakitiana moyo na kujiweka tayari.

Siku ilipofika Jacob alijiweka tayari kwa ajili ya misheni hiyo ikiwa ni pamoja na kuvalia mavazi maalum, na kuanza kupakia vifaa maalumu ikiwa ni pamoja na maski ya hewa, kisu kikubwa cha kuwindia, bastola, jaketi la kuogelea, boksi la huduma ya kwanza, tochi kubwa n.k na hapo akawa tayari kwa vita.

KUIVAMIA JAPAN

Walipewa maelekezo maalumu kuwa wakiingia katika anga la Japani waanze kulipua maeneo maalumu kama walivyoelekezwa na kwa muda maalumu, baada ya hapo walitakiwa kutua katika ardhi ya China katika sehemu ambazo walipewa maelekezo kwa ajili ya kujaza mafuta. Safari ikaanza na kweli wakaanza kuilipua Japani katika maeneo mbalimbali kama walivyoelekezwa. Na hili lilikuwa ni shambulizi la kushtukiza.

Wakiwa hewani ile hofu ya vita ikazidi toweka na kujikuta hawana presha tena na hapo wakanogewa kuendelea kulipua. Akiwa angani Jacob DeShazer anasema alijikuta ni mwenye roho mbaya na ngumu, moyo wa hasira na chuki kwa wajapani na alikuwa na shauku ya kuona maangamizi yao makubwa kwa kile walichokifanya huko katika bandari ya Lulu.  Hivyo hiyo ilipelekea kutokuwa na huruma kwa watu wote ambao mabomu yangewapata iwe ni watoto, wakina mama, au raia yeyote asiyehusika, ila kwa kuwa ni mjapani hakujali chochote.

Wakiwa katikati ya vita wakajisahau kabisa kuwa ilitakiwa watue China kwa ajili ya kujaza mafuta ndege zao, wao waliendelea kuachia mabomu sehemu mbalimbali na walikuja kushtuka ndege zinakaribia kuisha mafuta kabisa. Jacob alijaribu kupiga mahesabu kama anaweza kufika kwenye kituo lakini ilikuwa haiwezekani, akaona hali imekuwa tete kwa upande wake. Alijaribu kuwaza kama anaweza kufanya jambo lolote litakalomfanya atoke hai lakini hakukuwa na lolote angefanya zaidi ya kuruka. Muda mfupi ujao ndege inaenda chini na ikifika ni lazima angepotea.

Akili ya Jacob iliendelea kuchakata mambo upesi sana, ilikuwa ni usiku wa giza nene na mvua kali ikiendelea kunyesha. Baadaye akaamua kuruka lakini ni hatari sana maana asilimia za kusalimika ni ndogo, alisikia sauti ndani yake ikimuambia utakufa, huwezi, huwezi utakufa,  akafuata maelekezo yote aliyopitia mafunzo kwa umakini mkubwa. Wakati akiendelea na taratibu za kunusuru uhai wake alishuhudia ndege za wenzake zikianguka na kulipuka. Ilikuwa ni mstari mwembamba wa uhai na kifo uliosimama mbele yao. Baadaye Jacob akachukua bastola yake, kisu na vitu vichache ambavyo vingemsaidia.

Akakagua parachuti lake kisha akakata mkanda alafu akarudi nyuma kutafuta nafasi ya kuruka,  akajifungua parachuti lake na kuhakikisha halibaki kwenye ndege kisha akajiachia na upepo ukamrudisha juu mpaka pale parachuti lilipoweza kukabiliana na upepo. Akiwa juu ya parachuti akasikia kishindo kikubwa chini, na kushuhudia ndege ikilipuka hapo akavuta pumzi kwa faraja.  Lakini ghafla akakumbuka sehemu anayokwenda kutua ni China upande ambao unamilikiwa na wajapani, akaanza kuwaza nitatulia wapi? Katikati ya kundi kubwa la maadui? Au juu ya mti? Katika pori la wanyama wakali au nitatua wapi?

Usiku wa kiza na mvua kali ikiendelea kulindima Jacob akashukia katika ardhi ya China akiwa hoi, akachukua bunduki yake haraka tu baada ya kutua na kulipua juu ili kama kuna mtu aliyenusulika na ajali ile ya ndege amsaidie, kabla ya wajapani hawajaja na kumkamata maana kishindo kilikuwa kikubwa. Lakini hakusikia majibu yeyote kulikuwa kimya bali  mvua kubwa tu. Ardhi ya eneo alilotua ilikuwa ni tope, hii ilikuwa ni sehemu ya mashamba ya mpunga. Akaamua kuendelea mbele bila kujua anakokwenda wala anapotoka, baada ya muda akafikia katika kibanda Fulani, akajiegesha hapo na akajikuta amelala mpaka asubuhi.

Asubuhi Jacob aliendelea na safari asiyoijua na kukutana na wenyeji mbalimbali ambao hawakumpa msaada wowote zaidi ya kumuogopa. Bila shaka walikuwa wachina maana wakitoa msaada wanaweza kamatwa na wajapani. Jacob alishindwa kutofautisha muonekano wa mchina na mjapani alichokumbuka tu kambini aliambaiwa utofauti ni kwamba mjapani ana kidole gumba kinene na kipo peke yake mguuni. Kiufupi alikuwa ni mtu mwenye hofu pia maana hakujua wa kumuamini, lakini wenyeji walishindwa kumuelewa lugha yake naye akashindwa kuilewa ya kwao.

Mgeni ni mgeni muda mfupi baadaye akakamatwa na askari waliomuelekezea silaha usoni. Baada ya kufikishwa kituoni Jacob akaanza kupoteza muda ili ajue nini cha kufanya akiwa hapo. Hivyo akadai aletewe mtafsiri wakati huo huo alitafakari majina ya hao jamaa wanaokuja kumhoji kama ni majina ya kichina au ya Kijapani ili ajue yupo katika mikono hipi? Lakini hakuweza kutofautisha.

Baadaye akaanza kuhojiwa wewe ni nani? Je umeshuka na hiyo ndege? Mlikuwa wangapi? Na kwanini mnalipua Japani? Wengine wapo wapi? N.k. Jacob majibu yake karibia yote yalikuwa sijui, sitalijibu hilo swali, sijui. Wakamletea chakula ambacho anasema kilikuwa kizuri zaidi katika vitu alivyowai kula,  maswali yaliendelea yalikuwa ni kwa namna ile ile na majibu yale yale. Baadaye kabisa akagundua kuwa alikuwa yupo mikononi mwa wajapani.

Kesho yake akapakiwa kwenye gari lingine wakaanza safari ndefu na ndipo akijisemea tayari nimekuwa mfungwa wa vita (war prisoner). Akiwa njiani alikumbuka usiku wa siku chache tu walipokuwa wakiongelea kuhusu stori za wajapani jinsi walivyo wakatili kwa wafungwa.  Wakasema ni heri ujiue kuliko kutiwa mikononi mwa wajapani ukiwa hai, hawanaga huruma, utu, wala ubinadamu. Leo yeye kukamatwa akiwa hai katika mikono ya wajapani akajiona amekwisha, ukizingatia kwa jinsi walivyoifanya Japani ilikuwa ni hatari sana.

MFUNGWA WA WAJAPANI

Walipofika asubuhi akapelekwa kwenye chumba kimoja kikubwa cha mahojiano na katika hali isiyokuwa ya kawaida aliwaona rafiki zake wawili aliokuwa nao kwenye misheni moja. Marafiki hawa walikuwa ni George Barr na Boby Hite.

Alipofika George Barr alimuangalia sana kwa kumshangaa kitu ambacho Jacob hakukipenda kwa sababu hakutaka wajapani watambue kuwa walikuwa pamoja. Baada ya mahojiano marefu walirudishwa kwenye selo zao na hapo Jacob akakumbuka familia yake, akamkumbuka mama yake kama angekuwepo angemwambia tubu dhambi zako Yesu ni mwenye rehema atakusamehe, alitamani walau kusikia hayo tu.

Wakahamishwa mpaka mji wa Tokyo na hapo mahojiano yakaanza upya, na safari hii ilikuwa ni pamoja na mateso makubwa. Kiukweli Jacob alikuwa ni askari wa kawaida kabisa hakuwa anajua chochote juu ya misheni yeye kazi yake ilikuwa ni kupokea amri tu. Hivyo mateso yakaongezeka kwa kiasi kikubwa,

Baada ya muda wa miezi kadhaa kupita tangu kukamatwa kwao wakiwa katika mateso mwenzao mmoja anayeitwa Bobby Medder.

Ambaye kabla ya kifo chake alikuwa ni mtu mwenye kuwatia moyo sana wenzake kama muda tu wataachwa huru na kurudi nyumbani kwao, alikuwa ni mtu wa imani. Wiki moja kabla ya kifo chake aliomba mbele ya Jacob akisema naamini katika Kristo Yesu na ya kwamba Yesu ni Bwana na Mfalme ajaye, naye ni mwana wa Mungu. Mungu anataka kila mmoja amuamini yeye kama ni Bwana na Mwokozi, na vita ya haiwezi kuisha mpaka yeye atakapotaka iishe (kumbuka ilikua kipindi cha vita ya pili ya Dunia). Bobby alikuwa kama ni mtu aliyejua hana muda mwingi sana wa kuishi.

Maneno yale yalimgusa sana Jacob ingawa bado moyoni mwake alikuwa na maelfu ya maswali ya kutokuamini moyoni mwake, maneno hayo aliyasikia mara nyingi sana alipokuwa kwao. Waliutoa mwili wa Bobby aliyekuwa amejifia kutokana na mateso yaliyoambatana na njaa kali maana kuna kipindi hawakupewa chakula. Baadaye walinzi wakapunguza baadhi ya adhabu kutokana na kifo cha Bobby, wakapata chai ya moto, supu, na baadhi ya vyakula ambayo ilikuwa adimu kwao.

Licha ya vyakula pia walipewa vitabu wasome na miongoni mwa vitabu walivyopewa ni pamoja na SON OF GOD, na SPIRIT OF CATHOLICISM vilivyoandikwa na KARL ADAMS, na vitabu vingine ni THE UNKNOWN GOD chake ALFRED NOYES, kingine kilikuwa ni HAND OF GOD cha WILLIAMS SCOTT, pamoja na toleo la Biblia ya American Standard version (ASV) ambapo unaposoma kitabu kimoja ukimaliza unampa na mwenzako.

Pamoja na vitabu vyote hivyo Jacob alikuwa anasubiri zaidi Biblia na alitamani aanze nayo, lakini Biblia ilikuwa moja na masharti ni kwamba ukiwa na Biblia unaruhusiwa kukaa nayo mpaka wiki tatu ndipo umpe na mwingine hivyo Jacob ilimpasa asubiri wiki tatu kupata Biblia.

Alipoipata Biblia Jacob alishusha chini na kuilengesha sehemu inayopitisha mwanga ingawa kulikuwa na giza na maandishi ya Biblia yalikuwa madogo lakini haikumsumbua kutokana na shauku ya moyo aliyokuwa nayo. Tofauti na wengi Jacob alianza kusoma maandiko ya Agano la Kale, kisha akasoma katika Agano jipya na kupata Ufunuo juu ya Kristo Yesu aliyekataliwa na Wayahudi na kuhukumiwa kwa sheria za Kirumi. Akaanza kupata nuru mpya ya neno la Mungu na pamoja na kusoma kwa vipande vipande (kuunga-unga) Lakini alipata kuelewa. Alijikuta ni mtu mwenye kujawa na upendo na Kristo na kuona uchungu juu ya kifo chake msalabani.

Na hatimaye katika pita pita zake katika maandiko siku moja akajikuta anafungua Warumi 10:9 ambayo inasema,

 “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.”

Jacob aliwahi kuusoma mstari huu zaidi hata ya mara saba miaka ya nyuma kipindi anasoma Biblia lakini safari hii ilikuwa ni tofauti, alihisi maneno yale yana mwanga unaopenya moja kwa moja moyoni mwake na anahitaji kuwajibika kwa maneno hayo kwa kuchukua hatua. Akapiga magoti gerezani (kipindi hicho alikuwa amehamishiwa gereza la China na si Japani tena lakini bado ni mfungwa wa wajapani) Akiwa katika hali ya magoti akafungua kinywa na kusema BWANA, pamoja na kuwa mbali na nyumbani na katika hali ya kufungwa lakini naomba unisamehe. Na hapo ukawa mwanzo mpya wa maisha ya Jacob DeShazer.

MAISHA YA WOKOVU GEREZANI

Tangu hapo Jacob alijikuta ni mtu wa tofauti kabisa na alivyowahi kuwa katika maisha yake, alijawa na furaha na amani ya moyo. Muda wa wiki tatu ulipoisha alirejesha Biblia lakini akibaki na kumbukumbu nzuri za maandiko aliyoyakalili Kichwani.  Hakuhofia tena ufungwa alijiona kuwa na Yesu kumemfanya awe huru, hakuogopa tena kifo aliona kuwa na Yesu kumempa maisha. Alionekana tofauti mpaka kwa walinzi na watu wengine.

Siku moja alipata nafasi ya kutoroka lakini hakufanya hivyo ingawa mlinzi alianguka miguuni pake, ilikuwa ni nafasi nzuri ya kumjeruhi na kukimbia gerezani lakini alikumbuka maneno ya Kristo kwamba wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, na wasalimuni hata wasiowasalimu, alipokumbuka hayo akaamua kuwa mpole. Tangu wakati huo akawa ni mwenye kujidhibiti tabia zake na mwenye kutengeneza mahusiano mazuri kati yake na walinzi ingawaje wanawatenda jeuri. Na akabahatika kuwa na mahusiano mazuri na mmoja wa walinzi waliomsimamia.

Baadaye Jacob alianza kuomba Mungu kuhusu amani, aliombea amani kwa ajili ya Taifa la Japani, aliwaombea viongozi wake. Aliomba kuanzia asubuhi mpaka saa nane mchana, ndipo akasikia sauti ikimwambia inatosha sasa, amka, vita Imekwisha. Baada ya hapo Jacob alifurahi na kuwaambia wenzake kuwa vita Imekwisha ingawa katika sura ya nje mapigano makali yaliendelea bila kukoma.

Haukupita muda mrefu sana Jacob alichukuliwa na kikosi maalumu cha wamarekani wakiwa wameshuka kutoka katika parachuti na kumpakia kwenye ndege iliyosafiri mpaka China., Akapelekwa kuoga maji ya moto, akanyolewa ndevu na nywele, akapewa mavazi mapya ingawaje yalikuwa makubwa kwake, kisha yeye na wenzake wakaambiwa mpo huru sasa vita Imekwisha. Ilikuwa ni Agosti 20,1945 na ilipofika tarehe 24 mwezi huo wakaanza safari kurejea Ardhi ya nyumbani. Safari yao ilianzia mji wa Chungking, China na waandishi wa habari walijaa wengi ambapo Jacob hakusita kuwaelezea kuhusu imani yake mpya na akaahidi kurudi tena Japani siku za baadaye.

KUFIKA NYUMBANI AKIWA HURU.

Alipofika Washington Jacob alipokelewa kwa heshima kubwa jeshini na kiti cha kwanza ni kupiga simu nyumbani kwa mama na baba yake aligundua ni wazima wa afya alifurahi sana, wazazi walilia na akawaambia atakuja kuwaona karibuni na wataongea mengi.

Akiwa Marekani Jacob alifanikiwa kuzitazama filamu tatu zilizoelezea kisa cha misheni yao, na jinsi ambavyo wameacha familia wamejitolea maisha yao. Filamu hizo ni Thirty Second over Tokyo, Purple heart,  na Destination Tokyo ambazo filamu hizo ni za kubuniwa na kufikirika haziendani sana na ukweli lakini zilichochea kuinua morali ya watu wa Marekani dhidi yao.

Watu wengi walitamani kusikia historia ya Jacob baada ya kurudi hivyo alilipwa kwa kila nakala ya Gazeti ambalo yeye anaandika dola 2,500 na dola 400 kwa kuhojiwa katika redio, unaweza kugundua kwa miaka hiyo thamani ya hela ilikuwa kiasi gani. Baada ya wiki nane akaruhusiwa kurudi nyumbani kutoka jeshini kilikuwa kipindi cha Chrismass na aliwaza sana juu ya mustakabali wa maisha yake yajayo. Akiwa gerezani aliweza kuwapenda walinzi wa gerezani sasa yupo huru.

USHUHUDA WA MAMA

Baada ya Jacob kurudi nyumbani na kuwaelezea kila kitu kilichotokea mama yake naye akamuelezea hali waliopitia kipindi yeye akiwa mfungwa. Anasema yeye na dada yake Hellen walikuwa na imani kuwa Jacob hajafa, hata kipindi walipopewa taarifa mbaya kuhusu Doolittle raiders (kikosi cha misheni ya siri kilichoenda Japani) Lakini bado wao walishikilia msimamo wao.

Walikuwa wakimwambia Mungu tunaomba umlinde Jacob kwa nguvu zako na malaika zako wamzunguke. Na siku moja Askari akaja kutuambia watatu kati ya wanajeshi wa Doolittle’s wameuawa lakini mama akapinga akasema Jacob ni hai, na anaishi namwamini Mungu. Hivyo pamoja na yote yaliyomtokea Jacob gerezani Japani bado maombi ya ndugu zake yalimbeba.

Jacob alikuwa kuwa maarufu na watu wengi walimwomba saini yake, alianza kuhudhuria vipindi mbalimbali vya kanisani.

NDOA NA UTUMISHI

Mnamo Agosti 16,1946 Jacob DeShazer alifanikiwa kufunga ndoa takatifu na Bi Frolence Matheny, ambaye walibahatika kupata watoto kwa vipindi tofauti tofauti ambao ni Paul, John, Mark, Calor a Lucy DeShazer. Sherehe ya ndoa yao ilikuwa ndogo iliyohudhuriwa wa na watu wachache kutokana na hali ya maisha ya Jacob kwa kipindi hicho ambapo baadhi ya nguo alizovaa kwenye sherehe aliazima.

Baada ya vita vya pili kukoma Generali Daugratius MacAthur wa Marekani alitoa wito kwa wamisionari wa kimarekani kwenda Japani kutangaza Injili. Kwa maelezo yake watu wa Japani wanahitaji matumaini makubwa sana na nguvu hiyo inapatikana katika Kanisa. (Nafikiri hii kauli pia ilitokana na matokeo ya vita kwa watu wa Japani hayakuwa mazuri kabisa kwao)

Bwana na bibi DeShazer wakaweka nia ya kumtumikia Mungu na hapo wakaamua kuingia chuoni kujifunza mambo mbalimbali ya kiutumishi na kimazingira. Walijifunza kuhusu tamaduni mbalimbali za watu wa Japani, maisha yao. Juni ya 1948 Bwana na Bi DeShazer walihitimu masomo yao na hapo wakaanza safari ya kuzungukia miji ya Marekani kwa ajili ya kuomba na kukusanya michango mbalimbali itakayowasaidia katika kipindi cha mwanzo wa huduma yao.

KURUDI JAPANI

Walipofika Japani walianza kazi ya Mungu, na Jacob alianza kumuhubiri Yesu na kuelezea ushuhuda wake jinsi alivyowachukia watu wa Japani, na jinsi walivyomtenda na vile alivyoweza kuwasamehe. Aliona siku zote kisasi hukaa kwa mtu ambaye hana Mungu na kitamtesa. Katika moja ya siku ya ibada alisimama binti mmoja ambaye alitoa ushuhuda kuwa alimchukia Jacob kiasi cha kutaka kumuua. Binti alieleza kuwa alipoteza ndugu zake katika shambulio ambalo Doolittle walilifanya na alimchukia Jacob kiasi cha kutaka kumuua. Ila siku aliposikia ushuhuda wa Jacob na moyo wake kwa watu wa Japan ilimfanya amsamehe. Jacob alimwalika nyumbani kwake binti huyo na kumkaribisha katika ibada na katika ufalme wa Mungu.

Miongoni mwa matokeo ya kazi ya Jacob ni kuokoka kwa kamanda wa Jeshi la Marekani aliyeongoza mashambulio mengi likiwemo lile shambulio la Pearl Harbor huko Marekani lililosababisha vita hii kwa kiasi kikubwa. Kamanda huyu anaitwa MITSUO FUCHIDA, ambaye yeye alisikia habari za Jacob na vile alivyokuwa mfungwa wa vita Japani na yale waliyomtenda na jinsi alivyowasamehe kiasi cha kumtafuta. Na baadaye Fuchida alieleza jinsi anavyoumizwa na mateso ya wafungwa wa kivita katika nchi mbali mbali.

Fuchida alimpokea Yesu na kuungana na Jacob kuhubiri Injili huko Japani, ni ajabu kiasi gani maadui wawili ambao ni wazalendo wa nchi zao Yesu akawaunganisha na kuwa ndugu. Fuchida alihusika na aliongoza mashambulizi yaliyowaua wajapani wengi na Jacob alikuwa mstari wa mbele katika mashambulizi ya kuivamia Japani lakini Yesu akawaweka katika zizi lake.

Ukipenda kuifuatilia historia murua za Fuchida utazipata kwa kina katika kitabu chake cha FROM PEARL HARBOR TO CALVARY, na kitabu cha MIDWAY.

MAFANIKIO YA HUDUMA YA JACOB NA FROLENCE DESHAZER.

DeShazer pamoja na mkewe walifanikiwa kudumu Japani miaka 30 kabla kustaafu kwao, wakiwa Japani walifanikiwa kuanzisha makanisa 23 na moja katika mji wa Nagoya ambao Jacob aliulipua. Walirejea nyumbani na Jacob alifariki Machi 15, 2008 akiwa na miaka 95.

Hii ni moja ya chapisho ambalo lilipata umaarufu mkubwa sana miaka hiyo lililoandikwa na Jacob na kuwafungua watu wengi, chapisho hilo lina kichwa kinachosema nilikuwa mtumwa wa Japani (I was prisoner of Japan) Tusome wote.

NILIKUWA MTUMWA WA JAPANI

Nilikuwa mfungwa wa Japani kwa muda wa miezi arobaini, miezi thelathini na nne kati ya hiyo nilikuwa katika kifungo cha upweke. Nilikuwa mshiriki wa kikosi cha Doolittle kwenye shambulio la kwanza la Japani Aprili 18, 1942, moyo wangu ulijaa uchungu mkubwa juu ya taifa hilo. Wakati ndege yangu ilipoisha gesi mimi pamoja na wafanyakazi wenzangu tuliruka kwa parachuti katika maeneo yaliyoshikiliwa na wajapani huko China. Moyo wangu ulijawa uchungu zaidi kwa watekaji kuliko dubu.

Mimi na wenzangu walionusurika tulichukuliwa na kupelekwa Tokyo, huko tulipigwa na kuteswa kwa njaa, na kufungiwa katika vifungo vya upweke kiasi ambacho hakuna mtu hata wa kuongea naye. Mateso haya kutisha yalifanyika katika miji ya Tokyo, Shanghai. Nanking na Peiping. Marafiki zangu watatu, Dean Hallmark, Bill Farrow na Harold Spatz waliuawa na kikosi cha risasi miezi sita baada ya kukamatwa kwetu. Na miezi kumi na nne baadaye mwingine wao Bob Meder alikufa kwa njaa polepole. Chuki dhidi ya watu wa Japani iliniendesha kiasi cha kuchanganyikiwa.

Mara tu baada ya kifo cha Meder nilianza kutafakari sababu ya chuki iliyo katika jamii za wanadamu, nilitafakari kwa nini wajapani wanatuchukia sana wamarekani na kwa nini mimi Mmarekani ninawachukia sana wajapani? Mtazamo wangu ukaangukia kwa Wakristo ambao chuki ya ulimwengu wanaigeuza kuwa upendo wa kweli kwa Mungu, nilishikwa na hamu kubwa ya kuichunguza Biblia ya Mkristo ili niweze kujua siri hiyo. Niliwaomba walioniteka waniletee Biblia na mwezi Mei 1944 walinipa Biblia ila nikae nayo kwa muda wa wiki tatu tu.

Nilianza kusoma kurasa zake kwa hamu, sura baada ya sura, Biblia ilishika moyo wangu. Kwa wakati ufaao nilikuja kwa vitabu vya manabii, na kugundua kwamba kila maandishi yao yalionekana kulenga Mkombozi kutoka kwa dhambi, mmoja ambaye angetumwa kutoka mbinguni ili azaliwe katika umbo ya mtoto wa binadamu. Maandishi yalinivutia sana hivi kwamba nilipata nikazisoma tena na tena hadi nilipozisoma kwa bidii mara sita. Kisha nikaingia kwenye Agano Jipya, na hapo nilisoma juu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. yule ambaye kwa hakika alitimiza unabii hasa wa Isaya, Yeremia, Mika na wale waandishi wengine wa Agano la Kale

Moyo wangu ulifurahi niliposoma Matendo ya Mitume 10:43

Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.

Baada ya hapo nilisoma kwa umakini kitabu ya Matendo, nilendelea mpaka waraka wa Warumi.

Mnamo Juni 8,1944 maneno ya kitabu cha Warumi 10:9  yalisemwa kwa ujasiri mbele ya macho yangu,

Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.

Wakati huo huo Mungu alinipa neema ya kuungama dhambi zangu kwake, naye akanisamehe dhambi zangu zote na kuniokoa kwa ajili ya Yesu, kama mimi baadaye niligundua kwamba Neno Lake tena linaahidi kwa uwazi sanakatika 1 Yohana 1:9

“Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na atusamehe dhambi zetu, na kutusafisha udhalimu wote.”

Moyo wangu ulifurahi kupata upya wa rohoni ingawa mwili wangu uliendelea kuteswa kwa vipigo na njaa . Mungu alikuwa amenipa macho ya rohoni ambayo ilikuwa tofauti sana kila nilipowatazama walinzi waliotutesa na kutupiga na kutunyima chakula ni kwa sababu hawana Mungu ndani yao, nami niliwachukia sababu sikuwa na Mungu. Nikakumbuka Yesu akiwa msalabani aliwaombea watesi wake akisema Baba wasamehe hawajui walitendalo, tena tunatakiwa kuwaombea adui zetu. Hivyo nilimwomba Mungu afanye jambo hili wajapani nao wamjue Mungu ili wawe kama Wakristo wengine. sura ya 13 ya Wakorintho wa Kwanza ilichukua maana hai: “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo huhusudu; upendo haujivuni, haujivuni, hautafuti mambo yake wenyewe, haukasiriki upesi, haufikirii mabaya. hufurahi si katika udhalimu, bali hufurahi katika kweli; huvumilia yote mambo, huamini yote. hutumaini yote, hustahimili yote. Upendo haushindwi kamwe.

Baada hata ya mwaka kupita bado niliendelea kukumbuka zile wiki nilizokaa na Bibilia yangu, aisee ilikuwa tamu siku baada ya siku. Siku moja nikiwa nipo kifungoni chumba cha upweke nilikuwa nikiugua sana, nakumbuka Meder naye aliniambia anaumwa kabla ya kufa kwa njaa. Nilipiga magoti na kuongea na Mungu, walinzi walinikimbilia na kuanza kunipiga ili niache lakini sikuacha kuomba mpaka pale walipoacha kunipiga bado niliendelea kuomba, Mungu akanitokea kwa katika maono katika kipindi hicho cha mateso.

Hatimaye uhuru ukaja. Mnamo Agosti 20, 1945, wanajeshi wamaparachuti wa Kimarekani walishuka kwenye uwanja wa gereza na walitutoa kutoka kwa seli zetu. Tulirudishwa kwa ndege Marekani na kuwekwa katika hospitali ambapo sisi polepole tulipata nguvu zetu za kimwili.

Kwa Sasa ninafanya mafunzo katika Chuo cha Kikristo, nikijiandaa kwa kazi katika uwanja wa misheni. Mungu ameniamuru waziwazi, “Nenda, ukawafundishe Wajapani njia ya wokovu kwa damu ya Yesu Kristo.” Ninatii Amri yake. Nitakapomaliza mafunzo yangu, nitaenda Japani kama mmisionari, nikiwa na kusudi moja la kuniongoza kumtangaza Kristo. Ninatuma ushuhuda huu kwa watu kila mahali, lakini hasa kwa watu wa Japan na China, na maombi yangu ya dhati ni kwamba jeshi kubwa la Kijapani na Wachina wanaweza kumkiri Yesu Kristo kama mwokozi wao binafsi.

REJEA.

Benge, Janet and Geoff Benge. Jacob Deshazer: Forgive Your Enemies (Christian Heroes: Then and Now): YWAM Publishing, January 1, 2009.

“Jacob DeShazer” accessed through https://en.m.wikipedia.org/wiki/Jacob_DeShazer

Watson, C. Hoyt. The Amazing Story of Sergeant Jacob De Shazer, Light and Life Press. January 1, 1950.