Yesu Kristo Mzaliwa wa Kwanza, Nini Maana Yake?

YESU KRISTO MZALIWA WA KWANZA, NINI MAANA YAKE?

Biblia katika maeneo mbalimbali ya vitabu vya Agano Jipya inamtaja Yesu Kristo Bwana wetu kuwa ni “mzaliwa wa kwanza”, Maeneo haya ni kama yafuatayo;

WARUMI

8.28  Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

8.29  Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

8.30  Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.

WAKOLOSAI

1.13  Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;

1.14  ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;

1.15  naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.

1.16  Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.

1.17  Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.

1.18  Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.

WAEBRANIA

1.5  Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana?

1.6  Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.

UFUNUO

1.4  Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi;

1.5  tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,

1.6  na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.

Baada ya kusoma maeneo hayo, swali linalowajia waamini wengi ni: Je, nini maana ya Yesu kuwa “mzaliwa wa kwanza“? Yesu kutajwa kama “mzaliwa wa kwanza” kuna maana tofauti tofauti kulingana na muktadha wa kifungu husika. Hebu fuatilia maana hizo kama tutakavyojifunza hapo chini.

WAKOLOSAI 1:18 NA UFUNUO 1:5

Katika maeneo hayo matano yanayomtaja Yesu kuwa ni mzaliwa wa kwanza, maeneo mawili yanaunganisha uzaliwa wa kwanza wa Yesu na kifo, yaani yanaonyesha uzaliwa huu wa kwanza ni cheo baada ya kifo. Wakolosai 1:18 inamuita Yesu “Mzaliwa wa kwanza katika wafu” ili awe mtangulizi katika yote. Ufunuo 1:5 inamuita “Mzaliwa wa kwanza wa waliokufa”. Hivyo ni dhahiri kwamba Yesu anaitwa mzaliwa wa kwanza ikimaanisha ndiye mwanadamu wa kwanza kufufuka (baada ya kufa) na kuwa mtangulizi wa kuishi maisha mapya ya ulimwengu mpya, ambayo waliokufa katika Yesu watakapofufuliwa watayaishi.

Unaweza kujiuliza: Inakuwaje Yesu anakuwa mtangulizi wakati kuna watu walifufuka kabla yake? Mfano ni Lazaro ambaye alifufuliwa na Yesu mwenyewe. Jibu ni kwamba waliofufuliwa kabla ya Yesu walirudi katika miili yao ya kawaida na siyo katika miili ya utukufu. Lakini pia walirudi kuishi maisha yao hapa duniani, na mwisho wakafa tena. Lazaro alifufuliwa na Yesu lakini hakufufuka na mwili wa utukufu, na alikufa tena baadaye.

Lakini Yesu alifufuka na mwili wa utukufu na hafi tena, hivyo yeye ndiye mwanadamu wa kwanza kufa na kufufuka katika mwili wa utukufu ambao watakatifu wote wataupata siku yeye atakaporudi mara ya pili. Kuhusu mwili wa utukufu watakatifu watakaoupata, Paulo anaandika akisema;

1 WAKORINTHO

15.51 Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,

15.52  kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.

15.53  Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.

15.54 Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda.

Hii ndiyo maana maeneo mengine ya Biblia inamuita Yesu Limbuko la waliolala, ikimaanisha yeye ni mtangulizi katika kufufuka. Limbuko ni mazao ya kwanza yanayopatikana katika kilimo na kutolewa kwa Mungu kama uhakikisho kwamba mavuno mengine yatapatikana. Hivyo, Yesu ndiye mwanadamu wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu na kuingia katika maisha ndani ya mwili wa utukufu, na yeye ndiye uhakikisho kwamba jambo hilo litatokea kwa waamini wote.

1 WAKORINTHO

15.20  Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.

15.21  Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu.

15.22  Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.

15.23  Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja.

Hivyo, Yesu anapoitwa Mzaliwa wa kwanza katika wafu/kwa waliokufa katika Wakolosai 1:18 na Ufunuo 1:5, ni sawa na kumwita Limbuko la waliolala. Hii yote ikiwa na maana kwamba Yeye ndiye mwanadamu wa kwanza kufufuka (baada ya kufa) na kuwa mtangulizi wa kuishi maisha mapya ya ulimwengu mpya, ambayo waliokufa katika Yesu watakapofufuliwa watayaishi / waamini wote watayaishi baada ya Yesu kurudi tena.

WAKOLOSAI 1:15

Pamoja na kwamba Wakolosai 1:15 iko kwenye aya moja na 1:18, lakini matumizi ya neno mzaliwa wa kwanza yanatofautiana kidogo. Katika 1:15, Yesu anatajwa kwa sifa zake mbili: ya kwanza, yeye ni mfano/picha ya Mungu asiyeonekana (sawa na Yohana 1:1, 18 na Waebrania 1:3), na sifa ya pili, yeye ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Yeye ni mzaliwa wa kwanza kwa maana ya kwamba yeye ni Mkuu (au ana nafasi ya kipekee) juu ya viumbe vyote. Kwa nini yeye ni Mkuu juu ya viumbe vyote? Ni kwa sababu katika yeye vitu vyote viliumbwa (1:16), yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote (1:17a), na yeye ndiye anayevishikilia vitu vyote (1:17b).

Je, ukuu wake unaweza kumaanisha kwamba Yesu ni kiumbe wa kwanza?
Jibu la moja kwa moja ni hapana, Biblia haijasema yeye ni kiumbe wa kwanza. Biblia inapotumia neno hili mzaliwa wa kwanza katika lugha ya picha huwa inazungumzia ubora na siyo kutangulia. Mfano, Mungu anamwambia Farao kwamba Israeli ni mzaliwa wake wa kwanza (Kutoka 4:22) hamaanishi kusema Israeli ndio waliotangulia kuumbwa. Katika muktadha huo Israeli wanatambulishwa kwamba wao ni bora (kwa maana ya kuwa na nafasi ya kipekee) kuliko mataifa mengine katika mpango wa Mungu wa wokovu.

Vivyo hivyo, Yesu anapotajwa kuwa mzaliwa wa kwanza kwa muktadha wa uumbaji, anatambulishwa kwa nafasi yake ya kipekee na siyo kwa maana ya kutangulia kwake.

WARUMI 8:29

Warumi 8:29 inaelezea uzaliwa wa kwanza wa Yesu katika kuhusiana na kufa na kufufuka, japo haijasema moja kwa moja kama Wakolosai 1:18 na Ufunuo 1:5. Swali ni: kwa namna gani?
Warumi inasema Mungu aliwachagua tangu asili waamini ili wafananishwe na mfano/picha ya Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Kwa muktadha huu, Paulo anamtaja Yesu kama ndiye picha halisi ya waamini watakavyokuwa baada ya ukamilisho wa kazi ya ukombozi.

Kwa maelezo zaidi, uhalisia wa Yesu kuwa mzaliwa wa kwanza utatimia pale ambapo waamini watafananishwa na yeye. Kwa lugha nyingine, waamini wasipofananishwa na yeye, hatakuwa mzaliwa wa kwanza (japo hili haliwezi kutokea).

Na kwa kusoma maeneo mengine ya Biblia, tunatambua kwamba waamini watakuwa kama Yesu baada ya wao kufufuliwa/kubadilishwa wakati wa ujio wa Yesu mara ya pili. Hivyo, wakati huo ndipo waamini watafananishwa na Yesu kikamilifu. Kwa sasa, waamini wanabadilishwa kila siku hatua kwa hatua (utukufu hadi utukufu), lakini wakati utakapowadia, watafikia utukufu kamilifu. Paulo anaeleza kuhusu kuchukua picha hii katika muktadha wa ufufuo katika waraka wake kwa Wakorintho.

1 WAKORINTHO 15

15.48  Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.

15.49  Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.

Hivyo, maana ya uzaliwa wa kwanza wa Yesu katika Warumi 8:29 ni sawa na ile katika Wakolosai 1:18 na Ufunuo 1:5.

WAEBRANIA 1:5-6

Kwa Waebrania, uzaliwa wa kwanza wa Yesu ni cheo ambacho Masihi alitabiriwa atakuwa nacho. Cheo hiki ni cheo cha kimahusiano. Hivyo, Yesu kwa waebrania inaitwa mzaliwa wa kwanza kuonyesha kwamba yeye ndiye masihi aliyetabiriwa. Kuelewa maana hii, fuatilia kwa mtiririko jinsi mwandishi anavyotumia unabii wa kumhusu Masihi unaotoka katika kitabu cha Zaburi kumuelezea Yesu.

Muktadha: Yesu Kristo ni bora zaidi ya malaika.


Mwandishi anaanza kwa kuuliza swali:

“Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, ‘Ndiwe Mwanangu, Mimi leo nimekuzaa?’ Na tena, ‘Mimi nitakuwa kwake Baba, naye atakuwa kwangu Mwana?’” (1:5)

Jibu ni kwamba hakuna malaika yeyote ambaye Mungu alimwambia maneno haya: “Ndiwe Mwanangu, Mimi leo nimekuzaa” na “Mimi nitakuwa kwake Baba, naye atakuwa kwangu Mwana.”

Lakini maneno haya Mungu aliyasema kumhusu Masihi miaka mingi kabla ya Yesu kuja na yanapatikana katika Zaburi ya pili.

ZABURI 2:2,7

2 Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.

7 Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.

Katika zaburi hii, Daudi anaandika kwamba Masihi ameambiwa na Bwana kwamba: “Wewe ndiwe Mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.”“Leo nimekuzaa” inaonyesha ni cheo anachokipata Masihi kisheria (kwa njia ya kuasili, au kwa Kiingereza inaitwa Adoption). Lugha hii ya kuasili mtoto ni ngumu kidogo kueleweka katika jamii yetu kwa sababu jambo hili linafanyika kwa uchache. Kuasili ni kumchukua mtoto aliyezaliwa na mtu mwingine na kumfanya kuwa mwanao kwa njia ya kisheria.

Mungu anamwambia Daudi kwamba katika uzao wake kutatokea Masihi ambaye Mungu atamfanya mwanae. Unabii huu ulianzia pale ambapo Daudi alitaka kumjengea Mungu hekalu, hivyo Mungu akamuahidi kumjengea yeye Daudi nyumba ya kifalme milele/nasaba. Unabii huo ulianzia katika kitabu cha Samweli wa pili sura ya saba.

2 SAMWELI 7

14 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu;

15 lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako.

16 Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.

Daudi anaambiwa kwamba kupitia yeye atakuja Masihi (mwanae) ambaye Mungu atakuwa Baba yake naye atakuwa mwanae. Hii ndiyo maana Yesu anaitwa Mwana wa Daudi ili kutimiza unabii mwingi ambao Mungu aliusema kuhusu Masihi ambaye ni Yesu. Lakini pia ndiyo maana Mungu alifungua mbingu na kusema wazi kwamba: Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye (Mathayo 3:17, 17:5; Marko 9:7; na Luka 9:35).

Baada ya maneno haya, wanafunzi wakapata uhakika kwamba Yesu ni Masihi kwa kuwa walijua unabii. Hii ndiyo maana baada ya tukio hili, wanafunzi wakamuuliza Yesu kwamba: “Kwa nini basi waandishi wanasema kuwa Eliya lazima aje kwanza?” Yesu anawajibu kwamba Eliya alishakuja, ambaye ni Yohana Mbatizaji).

SASA TURUDI KWA WAEBRANIA.

Baada ya kuonyesha kwamba Masihi pekee ndiye Mungu alimpa cheo ambacho malaika hawakupewa, yaani kuitwa Mwanae, sasa anaonyesha kwamba wakati Mungu anamleta Masihi (Mzaliwa wa kwanza) ulimwenguni aliwaambia malaika wamsujudu.“Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, ‘Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.’” (1:6)

Hivyo, mwandishi wa Waebrania ametumia cheo cha uzaliwa wa kwanza kikihusiana na umasihi wa Yesu. Kama ambavyo pia Mungu alitoa unabii kwamba Masihi atakuwa kwake mzaliwa wa kwanza katika zaburi nyingine ya 89.

ZABURI 89

26 Yeye ataniita, Wewe baba yangu, Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.

27 Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.

28 Hata milele nitamwekea fadhili zangu, Na agano langu litafanyika amini kwake.

29 Wazao wake nao nitawadumisha milele, Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.

Hivyo, uzaliwa wa kwanza ni cheo ambacho Masihi aliahidiwa kupewa, sio kwamba Masihi atazaliwa wa kwanza katika familia yake, bali cheo hiki kilikuwa kinaelezea mahusiano kati ya Mungu na Masihi. Kwa Wayahudi, mtu kupewa hadhi ya uzaliwa wa kwanza (Mwanzo 25:29-34) ilikuwa ni kupewa mamlaka sawa na ile ya Baba, kwani mzaliwa wa kwanza alikuwa ndiye mrithi wa vitu vyote.
Ndio maana mwandishi wa Waebrania anasema Yesu amechaguliwa kuwa mrithi wa vyote (Waebrania 1:2).

Hitimisho.

Biblia inapomtaja Yesu kuwa ndiye Mzaliwa wa Kwanza, haina maana moja katika kila mstari/aya. Kama tulivyoona, katika Wakolosai 1:18, Ufunuo 1:5, na Warumi 8:29, Yesu ni mzaliwa wa kwanza kwa maana ya kwamba yeye ndiye mwanadamu wa kwanza kufufuka (baada ya kufa) na kuwa mtangulizi wa kuishi maisha mapya ya ulimwengu mpya, ambayo waliokufa katika Yesu watakapofufuliwa watayaishi / waamini wote watayaishi baada ya Yesu kurudi tena.

Kwa Wakolosai 1:15, yeye ni mzaliwa wa kwanza kwa maana ya kwamba yeye ni Mkuu (au mwenye nafasi ya kipekee) juu ya viumbe vyote / uumbaji wote.
Na kwa Waebrania 1:5-6, yeye ni mzaliwa wa kwanza kwa maana ya kwamba yeye ndiye Masihi aliyetabiriwa kuja kupitia ukoo wa Daudi, na kuasiliwa na Mungu (yaani kufanywa Mwana kisheria), na hivyo kuchaguliwa kuwa mrithi wa vitu vyote.