3 Yohana- Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA TATU WA MTUME YOHANA.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.

UTANGULIZI.

Waraka wa tatu wa Mtume Yohana ni kitabu kinachokubaliwa na waamini kwamba kiliandikwa na Mtume Yohana kwenda kwenye makanisa yaliyokuwa eneo la Asia Ndogo, japo mwandishi hajataja jina lake katika maandishi ya kitabu hiki. Pamoja na kwamba ni kweli mwandishi hajataja jina lake katika maandishi ya kitabu hiki zaidi ya kujiita “Mzee,” kuna viashiria kwamba waraka huu uliandikwa na yeye. Moja ya kiashiria ni ufanano mkubwa wa ujumbe na matumizi ya lugha na vitabu vingine vinavyoaminiwa kuandikwa na yeye. Vitabu hivi ni Injili ya Yohana, Waraka wa Kwanza wa Yohana, na Waraka wa Pili wa Yohana. Mfanano wa vitabu hivi ni ishara tosha kwamba viliandikwa na mwandishi mmoja.

Mtume Yohana

Yohana alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Yesu, mtoto wa Zebedayo, na kaka wa Yakobo Mtume (Mathayo 4:21-22). Yakobo huyu ni Yakobo Mtume wa kwanza kabisa kufa na sio Yakobo mwandishi wa Waraka wa Yakobo (Matendo 12:1-2). Yohana, kabla ya kukutana na Yesu, alikuwa mvuvi wa samaki, kazi ambayo ilikuwa ni kazi ya familia.

Yohana anafahamika kama mwanafunzi aliyekuwa karibu sana na Yesu na anajitaja kama mwanafunzi aliyependwa sana na Bwana Yesu (Yohana 13:23). Ni kweli kwamba Yohana alikuwa karibu sana na Yesu, sababu yeye, Petro, na Yakobo ndio wanafunzi pekee waliona matukio muhimu ya Bwana Yesu ambayo wanafunzi wengine hawakuyaona. Matukio haya ni kama kubadilika kwa Yesu kule mlimani (Luka 9:28-36) na maombi yake katika bustani ya Gethsemane (Mathayo 26:36-46).

Baada ya Kristo kufufuka, Yohana alikuwa huko Yerusalemu kama mmoja wa Mitume waliotambulika kama Nguzo za Kanisa (Wagalatia 2:9-10). Kwa mujibu wa mapokeo ya kihistoria kutoka kwa Mababa wa Kanisa wa kuanzia karne ya pili, Yohana, baada ya kufanya kazi huko Yerusalemu pamoja na Mitume wengine, alisafiri na kwenda Efeso ambako alifanya huduma yake kwa muda wa kutosha (kati ya mwaka 70-100 B.K.). Nyaraka zake tatu ni matokeo ya huduma yake kwa kanisa lililokuwako huko Efeso. Baada ya muda, kama njia ya mateso, Yohana alipelekwa katika kisiwa cha Patmo na huko aliandika Kitabu cha Ufunuo. Inaaminika kuwa Yohana ndiye mtume pekee kufa kifo cha kawaida bila kuuawa kama mitume wengine.

Wapokeaji wa Awali wa Waraka.

Kitabu hiki, tofauti na Waraka wa Kwanza, kinataja mpokeaji wa ujumbe huu. Mpokeaji ni Gayo, mpendwa wa Yohana. Ingawa ni vigumu kujua huyu Gayo ni nani hasa, barua hii inaonyesha kwamba Gayo alikuwa kiongozi katika kanisa. Kazi anayosifiwa nayo na jukumu analopewa vinashiria kwamba alikuwa kiongozi katika kanisa hilo. Katika kanisa hili, kulikuwa na kiongozi mwingine aliyekuwa kinyume na Mzee Yohana. Kiongozi huyu aliwakataa watumishi wa Mungu waliotoka na barua kutoka kwa Mzee Yohana yenye ujumbe kwa ajili ya kanisa. Kiongozi huyu hakuishia tu kutokuwakarimu watumishi hawa, bali aliwazuia waamini wengine kuwapokea. Wale waliojaribu kuwapokea aliwatoa katika kanisa. Hivyo, kanisa hili lilikuwa na mgogoro mkubwa.

KUSUDI LA WARAKA.

Mzee Yohana alipata taarifa kuwa Gayo aliwapokea vizuri watumishi wa Mungu ambao walifika katika kanisa ambalo yeye alikuwa ni sehemu (3 Yoh 1:5-6). Lakini kwa upande mwingine, Diotrefe hakuwapokea watumishi wa Mungu ambao Yohana aliwapa na barua kwa ajili ya kanisa. Hakuishia tu kutokuwapokea bali aliwazuia waamini wengine kuwapokea na waliojaribu aliwatoa katika kanisa (3 Yoh 1:9-11). Hivyo, Yohana anaandika waraka huu kumpa moyo Gayo kuendelea kuwapokea na kuwaonyesha ukarimu watumishi wa Mungu. Moja ya njia ya kuwapokea na kuwaonyesha ukarimu ni kuwasafirisha watakapokuwa wanaondoka. [1] Lakini pia anampa Gayo taarifa kwamba jambo hili ambalo Diotrefe amelifanya yeye atalishughulikia akija. Barua hii pia haikuenda pasipo mtu mwingine ambaye Yohana anamtambulisha kuwa ana ushuhuda mzuri na wa uhakika.

MPANGILIO.

SehemuMaelezo
1:1-2Utangulizi
1:3-8Gayo kupongezwa
1:9-11Kuhukumiwa kwa Diotrefe
1:12Ushuhuda wa Demetrio
1:13-15Salamu za mwisho

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.

Waraka huu una muundo kama waraka/barua ya karne ya kwanza ilivyotakiwa kuwa, yaani kuna Utangulizi (3 Yoh 1:1-2), ujumbe mkuu (3 Yoh 1:3-12) na Salamu za Mwisho (3 Yoh 1:13-15). Utanguzili una sehemu tatu yaani una anuani ya mtuma waraka (1:1a), anuani ya mpokeaji (1:1b) na maombi (1:2).

Sehemu ya kwanza ya ujumbe Yohana anatoa pongezi kwa Gayo kwa kuwa alipata taarifa ya jinsi anavyoenenda katika kweli (1:3), kitu ambacho kinamfurahisha sana (1:4). Jambo moja wapo mahususi kabisa ambalo Gayo alilifanya na linaonyesha kuenenda kwake katika kweli, ni kuwakaribisha na kuwatunza watumishi waliofika katika kanisa. Kwa ukarimu huu Mzee Yohana anamsihi Gayo kufanya hivyo zaidi (1:5-8).

Sehemu ya pili ya ujumbe Yohana anatoa taarifa alizozipokea kuhusu mwenendo wa Diotrefe, ambaye anaishi kinyume na kweli na tofauti na mwenendo wa Gayo. Diotrefe hakuwapokea watumishi wa Mungu ambao Yohana aliwatuma kwa kuwapa na barua yenye ujumbe wa kanisa. Hakuishia tu kutokuwapokea bali pia aliwanenea maneno mabaya, aliwazuia waamini wengine kuwapokea na wajiojaribu aliwatoa katika kanisa. Hivyo Yohana anamsisitiza Gayo kutokuiga mfano mbaya ya Diotrefe (1:9-11).

Kwa kuwa hali ilikuwa hivyo katika kanisa, Yohana anamtuma Demetrio pamoja na waraka huu ili Gayo asibebwe na mwenendo wa Diotrefe. Hivyo anamuhakikishia Gayo ushuhuda ambao Demetrio anao kwa kanisa na kwa watu wote (1:12).

Mwisho, anamalizia kwa kueleza kwa nini ameandika waraka mfupi hivi. Waraka ni mfupi sio kwa sababu ana mambo machache ya kusema naye, bali ni kwa sababu anatarajia kwenda kwake hivi karibuni (1:13-14). Mwisho kabisa anamaliza na salamu za mwisho wa barua (1:15).




FOOTNOTES

[1] Kama ilivyo leo katika maeneo mengi kwamba watumishi wa Mungu wanaofanya kazi kwa kusafiri katika maeneo tofauti tofauti hupewa huduma ya chakula na malazi na mwenyeji, ndivyo ilivyokuwa kwa kanisa la kwanza. Tofauti inaweza kuwa hawa walikuwa hawana mawasiliano ya karibu kama  ilivyo kwetu leo kwa hiyo hawakuwa na mialiko. Watumishi walitumwa na kupewa barua za utambulisho kutoka kwa viongozi.

Unakuja hivi karibuni