Kwa kawaida, mwamini anapokutana na mwamini mwingine, katika mazungumzo yao kila mmoja anaweza kumuuliza mwenzake, “Wewe unaabudu wapi?” au “Wewe unaabudu kanisa gani?” Majibu yanaweza kuwa, “Mimi naabudu katika kanisa fulani lililoko eneo fulani.” Kadhalika, siku ya Jumapili, asilimia kubwa ya Wakristo duniani ukiwauliza, “Unaenda wapi na kufanya nini?” majibu yao yatakuwa, “Naenda kanisani kumuabudu Mungu.” Mazungumzo haya ya kila siku yanaonyesha kwamba waamini wanajua wanachoenda kufanya kwenye majengo yanayoitwa “kanisa”—yaani, wanaenda kumwabudu Mungu au kufanya ibada kwa Mungu. Hii ndiyo maana hata tumekuwa na majina kama “ibada ya kwanza,” “ibada kuu,” au “ibada ya Jumapili.”
Sasa, kama mazungumzo yetu ya kila siku ni hayo, swali letu tunalojiuliza kwamba, “Huwa tunakusanyika au tunaenda kufanya ibada?” linaweza kuonekana kama halina maana kabisa, kwa kuwa majibu tunayo. Hata hivyo, swali hili linajaribu kuchunguza kwa kina usahihi wa jambo lenyewe: Je, kusudi la waamini kutoka kwenye makazi yao au kutoka katika shughuli zao mbalimbali na kwenda kwenye jengo au mahali panapoitwa “kanisa” ni kwenda kumuabudu Mungu au ni kukusanyika kwa ajili ya kufaidiana waamini wao wenyewe? Kwa ufafanuzi zaidi; swali hili linataka kuchunguza chanzo sahihi kinachotakiwa kuwatoa waamini katika makazi yao na katika shughuli zao na kuwaleta pamoja:
- Je, kusudi kuu ni kumuabudu Mungu au kufanya ibada kwa Mungu?
- Au je, kusudi kuu ni kukusanyika au kukutana waamini wao kwa wao kwa ajili ya kufaidiana?
Na zaidi Je, utofauti wa maneno hayo unatija yeyote kwa maisha ya mwamini na Kanisa.
UFAFANUZI WA LUGHA NA MANENO
Kwa kawaida, waamini wanaposema, “Naenda kanisani kumwabudu Mungu,” huwa wanamaanisha wanakwenda mahali fulani ambako shughuli zao zote (au kwa asilimia kubwa) watakazozifanya zitaelekezwa kwa Mungu, na si kwa waamini wengine. Au kwa namna nyingine, kwenda kuabudu ni kwenda kufanya mambo mbalimbali ambayo muelekeo wake ni kwa Mungu na sio kwa mwanadamu mwingine. Na kwa maana ya neno kuabudu, ni sahihi kabisa kwamba ibada inaelekezwa kwa Mungu tu, na si kwa mwanadamu mwingine.
Kwenye lugha ya kiyunani, lugha iliyotumika kuandika agano jipya, kuna maneno kama matano tofauti tofauti ambayo mara nyingi kwenye kiswahili hutafsiriwa kuabudu au kufanya ibada (au wakati mwingine kusujudu). Maneno haya mara nyingi yanatafsiriwa kuabudu lakini kwa undani wake yana maana tofauti tofauti. Maana ya maneno hayo kwa maelezo ni kama ifuatavyo; Moja, kuanguka na kuinama chini ya Mungu au miungu (Hili ni neno Proskyneō ). Pili, huduma inayotolewa kwa ajili ya Mungu au miungu na hasa inayohusisha kutoa dhabihu (Hili ni neno Latreuō). Tatu, huduma ya kikuhani kwa Mungu au miungu au huduma ya umma (leitourgeō). Nne, kuwa na heshima ya juu na ya ndani kwa Mungu au miungu ambayo huonekana kwa kufanya maagizo ya mungu husika (Hili ni neno Sebō).Tano, taratibu za kidini zinazoonekana kwa nje (Hili ni neno Thrēskeía). Maneno haya yamepangwa kulingana na kiwango cha matumizi yake; la kwanza limetumika mara nyingi zaidi, na la mwisho mara chache zaidi.
Kwa kuwa maneno haya yana maana tofauti tofauti pamoja na kukabiliana maana, hivyo ni vizuri unaposoma eneo lolote ambalo neno kuabudu limetumika kuzingatia muktadha ili uweze kuelewa nini kinafundishwa na eneo husika la maandiko. Kumbuka, maneno yana maana kutokana na muktadha yalipotumika na sio tu maana ya kwenye kamusi.
Pamoja na maana hizo, ni dhahiri kwamba waamini wanaposema nakwenda kuabudu huwa wana maana ya kwenda kukutana na Mungu na kumfanyia huduma ambayo inaambatana na kutoa dhabihu. Hii ndio maana nukuu za mistari kama Torati 16:16 “……..wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu.” Na Walawi 23:15 “….wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu;” vimesisitizwa kuonyesha kwamba “pasipo sadaka ibada haijakamilika”.
Kwa upande mwingine, kuna maneno kama matatu hivi yanayotumika na waandishi wa Agano jipya kuelezea kusanyiko la waamini au kukutana kwa waamini. Maneno haya yote yana maana ya kuja pamoja au kukusanyika pamoja. Maneno haya ni kama vile synérchomai, ekklēsía (Hili ndio neno linalotafsiriwa Kanisa), synagōgḗ ( Hili ndio neno ambalo wakati mwingine lina maana ya Sinagogi la kiyahudi). Kama tulivyosema awali, maneno yana maana kutokana na muktadha hivyo pia maneno haya huwa yanatafsiriwa kutokana na muktadha lakini maana yake ya awali ubaki pale pale kwamba maneno haya yana maana ya kuja pamoja au kukutanika.
Swali, Je, kinachotakiwa kututoa kwenye shughuli zetu au makazi yetu na kwenda kwenye majengo tunayoyaita makanisa ni kwenda kukutana na Mungu na kumfanyia huduma ambayo inaambatana na kutoa dhabihu au ni kukutana na waamini wengine? Au Je, sehemu tunazotumia kukutana zinatakiwa kuitwa nyumba za ibada au majengo ya kukutania?
MAJIBU YA SWALI NA UTETEZI WA HOJA
Majibu ya moja kwa moja kwenye swali letu ni kwamba waamini hawatakiwi kuacha shughuli zao na makazi yao kwa ajili ya kwenda kumuabudu Mungu au kumfanyia ibada. Badala yake waamini wanatakiwa kuacha shughuli zao na makazi yao kwa ajili ya kukutana na waamini wengine au kwa ajili ya kukusanyika na waamini wengine. Na lengo la kukusanyika kwao sio kumwabudu au kumfanyia ibada Mungu bali lengo ni kujengana wao kwa wao.
Kama umeshitushwa na majibu na ukadhani haya ni mafundisho potofu nikutie moyo ufuatilie mpaka mwisho ili uweze kuchunguza kwa kina kwamba fundisho hili ni potofu au la kweli.
Utetezi wa hoja hii unaweza kufanywa kwa namna mbalimbali, lakini tutatumia namna mbili tu; Moja, kuonyesha kwamba kwenye Agano jipya maneno yaliyotumika kuelezea ibada (kuabudu) yametumiwa kuelezea ujumla wa maisha ya kila siku ya mwamini na sio tukio linalofanyika mara kadhaa kwa wiki. Pili, mitume na waamini wenzetu walipokuwa wanaeleza kuhusu kuja kwao pamoja walitumia maneno kukusanyika au kukutana na sio kufanya ibada.
- Kuabudu ni ujumla wa maisha ya kila wakati ya mwamini.
Katika maisha ya Agano la kale, kuabudu kulihusisha maana nyingi zaidi kuliko hata maneno yale matano kutoka Agano jipya tuliyoyainisha pale juu, lakini kitivo cha mambo yote ilikuwa ni kutoa dhabihu katika eneo maalumu Mungu alilolichangua. Eneo hili mwanzoni lilikuwa ni madhabahu zilizojengwa mahali mahali lakini baadaye eneo hili likawa ni hekaluni. Kama mtu asingetoa dhabihu kwenye madhabahu au hekalu asingeweza kusema kwamba amefanya ibada au amemwabudu Mungu. Kwa mfano, Ibrahimu Baba wa imani, mara baada ya kuitwa na Mungu, maisha yake yakawa yamejaa na kujenga madhahabu kwa ajili ya ibada kwa Mungu (Mwanzo 12:6-7; 12:8; 13:18). Na hata pale alipowaambia vijana wake “Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena.” (Mwanzo 22:5) alisema hivyo kwa kuwa alijua anaenda kujenga madhabahu na kumtoa Isaka mwanae kama dhabihu (Mwanzo 22:6-9).
Jambo hili liliendelea mpaka pale Mungu alipowapa watu wake eneo maalumu la kujenga hekalu ili wamfanyie ibada. Hivyo, pamoja na mambo yote yaliyokuwa yanafanyika hekaluni kitivo cha mambo yote ilikuwa ni kutoa dhabihu kwa Mungu kwa ajili ya dhambi za mtu binafsi na kwa ajili ya dhambi za jamii nzima ya watu wa Mungu. Hii ndio maana kila siku wana kondoo wawili walitolewa dhabihu kwa ajili ya taifa; Mmoja asubuhi na wa pili jioni (Kutoka 29:38-42). Hapo ukiacha ongezekezo la wanyawa waliotakiwa kutolewa na kila mtu kutokana na dhambi zake binafsi (Walawi 4:27-35). Tena ukiacha ungezeko la wanyama kutokana na siku maalumu kama vile sabato (Hesabu 28:9-10), Mwezi mpya (Hesabu 28:11-15), Pasaka (Hesabu 28:16-25) na nyingine nyingi. Wingi za dhabihu hizi, unaonyesha kwamba dhabihu haikuwa kwa ajili ya upatanisho wa dhambi tu, japo upatanisho ndio msingi mkuu.
Hivyo, watu walipokuwa wanatoka maeneo mbalimbali na kwenda hekaluni kuabudu, jambo kubwa walilokuwa wanaenda kufanya ni kutoa dhabihu kwa Mungu. Hichi ndicho kilichomtoa tohashi kutoka Ethiopia kwenda Yerusalemu (Matendo 8:27), hichi ndicho kilichowatoa wayahudi na waongofu wa kiyahudi kutoka Uajemi, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponti, Asia, Frigia, Pamfilia, Misri, Libya karibu na Kirene, Roma, Krete na Arabia na kwenda Yerusalemu (Matendo 2:9-10).
Sasa, kwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa kawaida ya taifa la Israeli, Yesu kupitia mazungumzo yake na Mwanamke msamaria anatuletea jambo jipya. Baada ya mwanamke kusema “ Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.” (Yohana 4:20), Yesu akamjibu akisema “…saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.” (Yohana 4:21). Sasa kumbuka nini kilikuwa kinafanyika Yerusalemu hekaluni ambacho hakikuwa na uwezekano wa kufanya kwenye maeneo mengine, hicho ndicho Yesu anasema hakitafanyika tena Yerusalemu wala katika mlima Gerizimu, mlima ambao wasamaria waliamini ndio mahali Mungu alipopachagua kwa ajili ya ibada (Jambo hilo lilikuwa ni kutoa dhabihu).
Kabla Yesu hajatoa jibu kwamba badala ya Yerusalemu na Mlima Gerizimu ibada itafanyika wapi, alianza kwa kukosoa imani ya Kisamaria na kuthibitisha imani ya Kiyahudi (Yohana 4:22). Imani hii ya Kisamaria ilikuwa na utofauti mkubwa na imani ya kiyahudi kiasi kwamba hata maandiko ya Torati (vitabu vitano vya Musa), ambavyo Wasamaria waliyahesabu kuwa ndiyo neno pekee la Mungu, yalikuwa yametofautiana na Torati ya Kiyahudi kwa sehemu kadhaa. Mfano, kwa nini wao waliamini kwamba Mlima Gerizimu ndio mahali Mungu alipopachagua kwa ajili ya kujenga hekalu na kufanya ibada? Ni kwa sababu kwenye kitabu chao cha Kutoka tofauti na Kutoka ya kiyahudi, baada ya Amri Kumi, neno linasema “Na itakuwa Shema, Mungu wako, atakapokuleta katika nchi ya Kanaani, unayoingia kuimiliki, utaweka mawe makubwa, na kuyapaka chokaa. Na utaandika juu ya mawe hayo maneno yote ya sheria hii. Na baada ya kuvuka Mto Yordani, utaweka mawe hayo juu ya Mlima Gerizimu kama ninavyokuamuru leo. Na hapo utamjengea Shema, Mungu wako, madhabahu ya mawe; usitumie chuma kuikata. Utajenga madhabahu ya mawe yasiyochongwa kwa ajili ya Shema, Mungu wako, na juu yake utatoa sadaka za kuteketezwa kwa ajili ya Shema, Mungu wako. Na utatoa sadaka za amani, na kula hapo, na kufurahi mbele za uso wa Shema, Mungu wako” (Kutoka 20).
Baada ya kusokoa imani ya kisamaria, Yesu anatoa sehemu mbadala ya kufanyia ibada. Yesu anasema “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.” (Yohana 4:23) Na anaongeza kwa kusema “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yohana 4:24). Yesu katika maongezi haya anatoa ibada kwenye maeneo maalumu kwenda kwenye utu wa ndani usioonekana kwa macho. Kama ambavyo Mungu ni Roho, yaani haonekani kwa macho ya damu na nyama, ndio hivyo hivyo watu wanatakiwa kumwabudu (katika utu wao wa ndani). Kumbuka jambo kubwa lililokuwa linafanyika Yerusalemu na mlimani Gerizimu ilikuwa ni kutoka dhabihu (pamoja na Yesu kutumia neno Proskyneō lenye maana ya kuanguka na kuinama chini ya Mungu au miungu ni dhahiri muktadha unahusisha kutoa dhabihu), hivyo ibada hii Yesu anayoisema bado inahusisha zaidi kutoa dhabihu lakini sasa hivi sio zile zinazoonekana kwa macho ya damu na nyama.
Kwa mabadiliko haya ndio maana Petro anaweza kusema “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo” 1 Petro 2:4-5. Pamoja na kutokutaja moja kwa moja dhabihu za roho ni zipi, ni dhahiri Petro anathibitisha mabadiliko. Kutoka kutoa dhabihu zanazoonekana na kushikika, Mungu kwa kumtoa Yesu, dhabihu inayoonekana na kushikika ametupa waamini nafasi ya kutoa dhabihu zisizoshikika wala kuonekana. Kwa muktadha wa Petro, “kuweka mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote” (1 Petro 2:1) na “kuepuka tamaa za mwili zipiganazo na roho.” (1 Petro 2:11), ndio kutoa dhabihu za roho na hiyo ndio ibada kwa muktadha wa Agano jipya.
Paulo pia anazungumza kwenye muelekeo huo huo wa Petro kwamba “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” (Warumi 12:1). Mtume Paulo na yeye anasisitiza kwamba kuishi kinyume na matakwa ya miili yetu ndio dhabihu Mungu anayoitaka na hiyo ndio ibada yenye maana.
Lakini pia mwandishi wa waraka kwa Waebrania na yeye anasema “Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake. Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu” (Waebrania 13:15-16). Ukisoma kwa haraka unaweza kudhani mwandishi wa Waebrania anazungumzia kuimba nyimbo za sifa tu. Lakini ukisoma kwa makini utagundua anazungumzia kuhusu sifa zinazohusisha kukiri jina la Yesu. Sio kukiri tunapoulizwa tu au tunapokuwa tumekutana pamoja,bali anazungumzia kukiri jina lake kila siku, saa na wakati (daima). Kwa muktadha wa Waebrania mwito wa kumkiri Yesu umetumika kuhamasisha waamini kuikubali imani yao kwa Yesu kwa ujasiri hata kama kuna upinzani (Angalia, Waebrania 3:1; 4:14; 10:23).
Lakini pia mwandishi wa Waebrania anasema kutenda matendo mema na kushiriki vitu na watu ndio sadaka zinazompendeza Mungu. Lugha anayoitumia ndio lugha inayotumika kueleza utoaji wa dhabihu kwenye Agano la kale, lakini yeye anatumia lugha hiyo kuelezea ujumla wa maisha ya kila wakati ya mwamini.
Maandiko mengi yanathibitisha kwamba maisha ya waamini kwa ujumla ndiyo sasa yamebeba maana ya lugha zilizokuwa zikitumika kuelezea kuhusu ibada zilizofanyika hekaluni Yerusalemu au mlimani Gerizimu. Lugha kama za “dhabihu” na “ibada” sasa hazihusiani tena na matukio maalum katika maeneo maalum au siku maalumu katika wiki, bali zinahusiana na ujumla wa maisha ya kila siku ya waamini. Ujumla wa maisha ya waamini unahusisha kuitikia mwito wa kuishi kwa kumfuata Roho kila wakati na kila saa.
Hivyo, tunasema kuabudu Mungu ni jambo la kila wakati kwa mwamini, na si jambo ambalo tunatakiwa kusubiri siku fulani au mahali fulani ili kulifanya kama ambavyo ilikuwa katika Agano la Kale. Sasa, kwa kutaka kuendelee na ufunuo wa awali, waamini leo bado wanang’ang’ania kuwa na mahali maalumu pa kuabudu (pamoja na Yesu kupindua hilo – Yohana 4:20-24), kuwa na siku maalumu ya kuabudu (pamoja na Agano Jipya kupindua hilo – Wagalatia 4:10-11), kuwa na madhabahu zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu (pamoja na ukweli kwamba kwa kuwa dhabihu ni za rohoni na madhabahu ni za rohoni), na kuwa na watu wachache kama makuhani (wakati waamini wote ni makuhani – 1 Petro 2:1-9).
Mwisho, kwa kuwa tumeona kuwa maisha ya waamini—maisha yao ya jumla na ya kila wakati—ndio ibada (yaani, kujitoa dhabihu), swali ni: nini itakuwa sababu ya kunitoa kwenye makazi yangu au kwenye shughuli zangu na kunipeleka kwenye jengo lile tunaloliita Kanisa? Kwa maneno mengine, kama naweza kuabudu Mungu nikiwa nyumbani kwangu, au hata nikiwa kazini au kwenye michezo, je, nini itakuwa sababu ya kunifanya Jumapili, Jumamosi au Jumatano niache mambo mengine yote na niende kuonana na wengine? Kumbuka, kwenye Agano la Kale ibada (yenye kitivo katika kutoa dhabihu) ilikuwa haiwezi kufanyika sehemu nyingine yeyote ile isipokuwa hekaluni. Majibu ya swali hili yapo kwenye sehemu inayofuata…
- Kanisa la kwanza lilitumia Lugha ya “kukutana” au “kukusanyika” badala ya kwenda ibadani.
Kama mitume wangekuwepo leo na ungekutana nao siku ya kwanza katika juma (au siku ya tano au ya sita), na ungewauliza wanaenda wapi, basi jibu lao lingekuwa: “Naenda kwenye kusanyiko,” na siyo: “Naenda ibadani.” Maandiko ni mengi yanayoonyesha lugha yao hii, ambayo imekuwa adimu sana kwetu, lakini tutanukuu maandiko machache na kuelezea andiko moja tu.
Hebu soma maandiko hayo kwa taratibu na uone jinsi wenzetu walivyokuwa wanajieleza.
“Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru…..20 Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.” Mathayo 18:17-20
“Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja,….31 Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.” Matendo 4:23-31
“….25 Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia. Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia. Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio” Matendo 11:22-28
“Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba.” Matendo 12:12
“Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane. Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika.” Matendo 20:7-8
“Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo. Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu…” 1 Wakorintho 5:3-5
“Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara. Kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki;….20 Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana;…22 Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo….33 Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojaneni; mtu akiwa na njaa, na ale nyumbani kwake; msipate kukutanika kwa hukumu. Na hayo yaliyosalia nijapo nitayatengeneza.” 1 Wakorintho 11: 17-34.
“Haya! Ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha, kisha ikawa wameingia watu wajinga au wasioamini, je! Hawatasema ya kwamba mna wazimu?…26 Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga.” 1 Wakorintho 14:23-26
Sasa, pamoja na kunukuu maandiko hayo hapo juu, hayo ni mifano tu ya kuonyesha kwamba wenzetu walikutana au walikusanyika, na hawakwenda ibadani (Angalia pia Yakobo 2:2-4; Waebrania 10:19-25). Unaweza kudhani kwamba kusema “kwenda ibadani” au “kukusanyika” ni kama kucheza na maneno, lakini ukweli ni kwamba waamini wanaokwenda ibadani watakuwa tofauti na waamini wanaokusanyika. Kwenda ibadani kama tulivyosema hapo mwanzo kwamba kunakuwa na mwelekeo wa kufanya mambo kwa ajili ya Mungu tu na sio kwa ajili ya wengine, hivyo hata wenye mtazamo wa kwenda ibadani mwelekeo wao unakuwa kwa Mungu tu na sio kwa waamini wengine. Lakini kukusanyika kunakuwa na mwelekeo wa kufanya mambo mbalimbali kwa ajili ya waamini wengine kwa lengo la kutaka kujengana. Waamini wanaokwenda ibadani hawatataka hata kujua jina la mwamini mwingine, lakini wanaokusanyika watajuana, watashirikiana na watajengana. Kinachotofautisha makundi haya mawili ni mwelekeo wa awali. Wewe unaweza kuwa shahidi, inawezekana umekuwa anaendea kwenye kile kinaitwa “ibada” kwa miaka sasa kwa ajili tu ya kukutana na Mungu na kumtolea dhabihu na ndio maana hata hujui au haujataka kujua hao waamini wenzio wanaendeleaje katika maisha yao ya kiimani, kimaadili, kiuchumi na nyanja nyingine. Hii, ni tofauti na waamini ambao wanamlengo wa kukusanyika, wao mlengo wao wa kwanza ni kwenda kutoa mchango chanya kwenye maisha ya waamini wengine.
Sasa katika maandiko tuliyonukuu hapo juu tulisema tutaelezea andiko moja kwa sehemu. Andiko hili ni kutoka kwenye 1 Wakorintho 14:26. Moja, katika muktadha wake tuna uhakika pasipo shaka andiko hili linazungumzia kuhusu kukutana waamini kwa pamoja kama mstari wa 23 unavyoonyesha, lakini pia kama mstari wa 26 inayothibitisha. Sasa mtume Paulo katika mstari huu anatupa sababu ya kukutana au kukusanyika kwa pamoja. Mtume anasema mambo yote (zingatia yote) yanayofanyika, yafanyike kwa kusudi la kujenga kanisa. Yaani, kila mtu anapokuja na zaburi, na fundisho, ufunuo,lugha au tafsiri hayo yote yafanyike kwa kujenga kanisa (kumbuka kanisa sio jengo wala taasisi kanisa ni kufanyiko la waamini). Pili, sura zote nne kutoka 1 Wakorintho 11 mpaka 14 zinaeleza utaratibu uweje tunapokusanyika. Kwa sura zote hizo nne, Paulo hajatumia neno hata moja linalotumika kueleza ibada. Kwenye meza ya Bwana anatumia neno kukusanyika au kukutana (1 Wakorintho11:17-18, 20, 33), ndio maana anasisitiza kungojeana waamini, na sio kumngoja Mungu. Anasisitiza akisema “Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojaneni;” (1 Wakorintho 11:33). Kwenye kupangilia matumizi ya karama za Roho katika kusanyiko haachi kutumia maneno kukutanika au kukusanyika (1 Wakorintho 14:23, 26) na huku akisisitiza kujenga kanisa.
Kama umeelewa kwamba tunatakiwa “kukusanyika” na siyo “kwenda ibadani,” basi hakikisha kila wakati unapokutana na waamini wengine, unajiuliza: Utachangia jambo gani kwa ajili ya waamini wengine? Na unapoondoka kwenye kusanyiko, jiulize: Umewafaidisha nini waamini wengine? Mungu yuko nawe kila wakati na kila saa, na unamwabudu kila wakati na kila saa. Lakini waamini wenzako hauko nao kila wakati na kila saa; huwezi kuwajenga wala kujengwa nao kila wakati, ndiyo maana tunapaswa kukutana.
VIPI KUHUSU MATENDO 13:2
Katika Utetezi wetu wa hoja kwenye sehemu ya pili, tumenukuu maandiko kadhaa kuonyesha kwamba wenzetu walitumia lugha ya kukusanyika au kukutana wakati wanaelezea kuja kwao kwa pamoja na tumesema hawakujieleza kwa kusema “naenda ibadani” au “naende kumwabudu Mungu.” Sasa ukisoma Matendo 13:2 maandiko yanasema “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.” Kwa andiko hili mtu anaweza kusema; unaona hapo kanisa lilikuwa linafanya ibada na katikati ya ibada Roho akasema nitengeeni Paulo na Barnaba kwa ajili ya kazi ile niliyowaitia. Kwa kusema hivyo, itakuwa kwamba mwandishi Luka alikuwa anaelezea kusanyiko la kanisa liitwalo ibada.
Lakini kwa kusoma vizuri maandiko hayo, utagundua Luka haielezei kuja kwa pamoja kwa kanisa. Moja, Luka anachokieleza kwenye mstari huu kinawahusu watu watano tu ( Barnaba, Simeoni, Lukio, Manaeni na Paulo) huku akiwatofautisha na Kanisa kwa ujumla (Matendo 13:1). Pili, Luka katika mstari huo hasimulii tukio bali anaelezea kwa ujumla walikuwa katika hali gani kipindi Roho anawaita Paulo na Barnaba kwa ajili ya kazi yake. Kwa mfano, “Nikisema nilipokuwa masikini ndipo nilikutana na mke wangu.” Katika lugha hiyo nakuwa nimeelezea hali na sio tukio, hicho ndicho Luka alikuwa anakielezea. Tatu, katika maneno yetu yale matano, neno liliotafsiriwa kuabudu hapa ndio lile lenye maana ya huduma ya kikuhani kwa Mungu au miungu au huduma ya kijamii. Sasa kwa kuwa maana ya maneno haitegemea tu maana ya kamusi bali huwa inategemea muktadha, swali tunaloweza kujiuliza hapa ili kupata maana na neno hili katika muktadha wake ni kwamba; hawa watu watano walikuwa wanafanya kazi gani ya kikuhani Antiokia? Waraka wa Paulo kwa Warumi unaweza kutusaidia kupata jibu hilo, kwa kuwa unatumia neno hilo hilo katika kiyunani pamoja na kwamba katika kiswahili halijatafsiriwa kama kuabudu, lakini litatupa mwanga wa kazi ya kikuhani waliokuwa wanafanya watu hawa watano. Paulo anassema “Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu.” (Warumi 15:16-17).
Kutokana na mwanga huu, itakuwa sahihi kusema kazi waliokuwa wanafanya wale watano ilikuwa ni kuhudumia Kanisa. Kwa upana wake, Luka anasema wakati wale watu watano wakiwa nalihudumia kanisa na wakati katika kufunga na kuomba ndio wakati huo Mungu aliwaambia wawatenge Barnaba na Paulo kwa ajili ya kazi aliyowaitia. Hii ndio maana tafsiri nyingine za kingereza zimetafsiri kazi hii kama huduma (KJV, ASV, HCSB, NASB, NKJV), kama ambavyo hata tasfiri yetu ya kiswahili imetasfiri neno hilo kama “huduma” kwenye Warumi 15:16-17 na maeneo mengine mengi (Kama vile Luka 1:23), ambako kote huko wazo ni huduma ya kikuhani.
HITIMISHO
Kama makusanyiko yetu tutayaitwa “kusanyiko” badala ya “ibada”, itakuwa tuko karibu zaidi na ujumbe wa Agano Jipya. Kama waamini watakusanyika kwa ajili ya kukutana wao kwa wao ili wajengane, itakuwa tuko karibu zaidi na picha ambayo Mungu aliikusudia kwa ajili ya watu wake. Kama mtazamo wa kila mwamini utaendeshwa na swali hili: Je, nikienda kwenye kusanyiko nitachangia nini katika kuboresha au kuyajenga maisha ya mwamini mwingine?, basi tutakuwa na matokeo makubwa sana katika ulimwengu.
Kama tutafanya mambo yote tunapokutana kwa lengo la kujengana, basi kila mtu atakuwa na sababu ya kumfanya aache kazi zake zote na shughuli zake ili aje kujengwa na kujenga wengine. Kwa kuwa huwezi kujenga wengine na kujengwa kwa kutazama vipindi vya televisheni vinavyoitwa ibada. Wala hilo haliwezekani ukiwa nyumbani kwako peke yako au ukiwa kwenye shughuli zako. Kwa mtazamo huu, kila mwamini atatumia karama, huduma, na vipawa ambavyo Mungu amempa kwa ajili ya kujenga Kanisa, na si kuwategemea watu wachache tu kufanya kazi hiyo. Kwa mtazamo huu pia, waamini watatoa kwa ajili ya kusaidiana wao kwa wao zaidi kuliko kwa ajili ya kufaidisha majengo na nyenzo nyingine.

