MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA KWA WAEBRANIA.
MAELEKEZO
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI
Waraka kwa Waebrania ni waraka wa muhimu sana kwa Kanisa kwa sababu mbalimbali. Moja ya sababu hizo ni jinsi ambavyo kitabu hiki kinamtukuza Kristo kwa kiwango cha juu, kwa kumlinganisha na ufunuo wa awali wa Mungu.
Pamoja na kuitwa waraka/barua kwa sababu ya kuwa na sifa kadhaa za waraka (mfano: kuwepo kwa maelezo ya kibinafsi, salamu, na baraka mwishoni; tazama 13:23–25), kitabu hiki kina sifa zaidi za hotuba/semina. Sifa hizi ni pamoja na kukosekana kwa anuani mwanzoni (jambo ambalo lilikuwa kawaida kwa kila waraka), na maandishi kuwa na mpangilio wa semina zaidi. Pia, mwandishi anaita maandishi yake “neno hili lenye maonyo” (13:22), utambulisho ambao umetumika kukaribisha hotuba/semina baada ya maandiko kusomwa katika sinagogi kwa mujibu wa Matendo 13:15.
Kwa hiyo, pamoja na kusomwa kama barua, kitabu hiki kinatakiwa kusomwa au kusikilizwa kama semina/hotuba.
MWANDISHI
Waraka kwa Waebrania ni kitabu ambacho kwa muda mrefu kimekuwa kikitambulika na wengi kama mojawapo ya nyaraka za Mtume Paulo. Ushahidi wa mapema sana unaonyesha kwamba waraka huu uliwekwa kwenye kundi moja na nyaraka nyingine za Mtume Paulo.
Pamoja na hilo, waamini wengi na wasomi wa Biblia pia tangu mwanzoni walionyesha wasiwasi wao kuhusu uandishi wa Mtume Paulo. Hii ni kwa sababu mbalimbali. Kwanza, hakuna utambulisho wa mwandishi — Paulo amejitambulisha katika nyaraka zake zote kumi na tatu. Pili, kuna utofauti mkubwa wa mtindo wa uandishi kati ya waraka huu na nyaraka za Mtume Paulo. Tatu, Paulo asingeweza kujieleza kwamba yeye ni kizazi cha pili cha wapokeaji wa injili. Akiwa anajieleza kwa Wagalatia, Paulo alisisitiza kwamba hakuhubiriwa wala kufundishwa injili na mitume wa Yerusalemu (Wagalatia 1:11–24), lakini mwandishi wa Waebrania anasema alipokea injili kutoka kwa wale waliomsikia Yesu (Waebrania 2:3–4).
Kutokana na sababu hizo, wasomi wengi wa Biblia wamependekeza watu mbalimbali kama waandishi wa kitabu hiki. Baadhi ya wale wanaopendekezwa ni kama vile Luka, Barnaba, Apolo, Prisila, Sila, au Klementi wa Rumi. Kati ya mapendekezo haya, Barnaba na Apolo wanaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi. Kwa sababu kitabu hiki kimejikita sana kwenye imani ya Kiyahudi na hasa kuhusu ukuhani na kazi zake, Barnaba, ambaye alikuwa Mlawi, ana nafasi kubwa ya kuwa mwandishi. Lakini pia, kwa sababu kitabu hiki kina mtindo wa hali ya juu kiufasaha, Apolo, ambaye alikuwa na sifa ya kuwa na ufasaha wa hali ya juu katika uwasilishaji na alikuwa na uelewa mkubwa wa Maandiko ya Agano la Kale (Matendo 18:24–28), ana nafasi kubwa ya kuwa mwandishi.
Pamoja na mapendekezo hayo, majibu ya uhakika ni kwamba hatujui kwa hakika ni nani aliyeandika kitabu hiki. Hitimisho hili linaendana kabisa na maneno ya Origeni wa Iskanderia, msomi wa maandiko kutoka karne ya tatu. Yeye alisema: “Lakini ni nani aliyeandika waraka huu, kwa kweli, Mungu peke yake ndiye anayejua.”
WAPOKEAJI WA AWALI WA WARAKA
Kwa kuwa hatujui kwa hakika mwandishi aliandika waraka huu kwenda kwa waamini waliokuwa katika eneo gani la kijografia, ni vigumu kupata taarifa za watu hawa nje ya maandishi ya waraka huu. Kupitia waraka huu tunajua kwamba mwandishi alifahamiana vizuri na wapokeaji wa ujumbe wake wa waraka huu, na wakati anaandika alikuwa anatamani kuwaona tena (Waebrania 13:18–19, 23). Zaidi ya kujuana, mwandishi anajua jinsi waamini hawa walivyokuja katika imani (yeye mwenyewe akiwemo). Waamini hawa (Waebrania 3:1,6, 14 inathbitisha kwamba watu hawa ni waamini) walihubiriwa na wale waliomsikia Yesu, na injili hiyo ilithibitishwa na Mungu kwa ishara, maajabu, na kwa kupokea zawadi za Roho Mtakatifu (Waebrania 2:3–4).[1] Wale waliowahubiria Injili walikuwa viongozi wao kwa muda (Waebrania 13:7), jambo ambalo lilikuwa kawaida katika upandaji wa kanisa wa karne ya kwanza. Kupitia viongozi hawa, wapokeaji wa ujumbe walifundishwa mafundisho ya msingi ya imani (“mafundisho ya kwanza ya Kristo” au “mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu”) kwa muda mrefu kiasi kwamba mwandishi anasema, kwa wakati anaandika waraka huu, wao wote walitakiwa kuwa wamekomaa na kuwa waalimu wa wengine (Waebrania 5:11–6:3). Zingatia mwandishi anayoyasema “Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu…6:1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, 2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele.” Waebrania 5:12-6:2.
Mwandishi anatuambia pia kwamba baada tu ya kuamini, waamini hawa walipata mateso mbalimbali lakini walistahimili. Waamini hawa walipata dhiki na shutuma kwa wazi (yaani, walifanyiwa aibu hadharani, labda kwa matusi, kudharauliwa, au hata kupigwa/kufungwa mbele ya watu). Walishiriki mateso ya wengine na kuwahurumia waliofungwa, na zaidi, walikubali kupokonywa hata mali zao (Waebrania 10:32–34).
Pamoja na historia hii nzuri na ya kishujaa—yaani, kuhubiriwa Injili na waliomsikia Yesu, kuamini Injili iliyothibitishwa na Mungu kwa ishara, maajabu, na mgawanyo wa zawadi za Roho Mtakatifu, na zaidi, uvumilivu na ustahimilivu wao juu ya mateso yote na aibu kwa ajili ya imani yao—hali ya baadhi ya waamini hawa ilikuwa imebadilika wakati mwandishi anaandika waraka huu. Baadhi ya waamini hawa walikuwa wameacha kuzingatia neno la Mungu lile lililonenwa na Bwana Yesu na kuthitibishwa na Mungu kwao (Waebrania 2:1-4). Katika hili mwandishi anasema “Kwa hiyo, imetupasa kuwa waangalifu sana kuhusu kile tulichosikia, ili tusije tukakiacha” Waebrania 2:1 NEN.
Pia, wengine hawakujali tena wokovu (Waebrania 2:3); walikuwa katika hatari ya kuacha kuamini na kujitenga na Mungu aliye hai kwa sababu ya udanganyifu wa dhambi, ambao huufanya moyo kuwa mgumu, kama jinsi ilivyokuwa kwa kizazi cha Israeli cha jangwani (Waebrania 3:12–13). Sifa nyingine za waamini hawa zilikuwa ni uvivu katika kusikia neno la Mungu na katika ufuasi (Waebrania 5:11; 6:11–12). Walikuwa wameacha kuangaliana, kuonyana, kuhimizana, na hata kukusanyika kwa pamoja (Waebrania 10:23–25). Na mbaya zaidi, walikuwa wameanza kuvutiwa na mafundisho tofauti na mafundisho ya kristo, mafundisho haya ni mafundisho ya dini ya kiyahudi (Waebrania 13:9).
Sababu ya Mabadiliko
Mabadiliko siku zote huja kwa sababu maalum; hivyo, hata mabadiliko ya wapokeaji wa ujumbe huu yalikuwa na sababu. Mwandishi hajatuweka wazi kwa nini kulikuwa na tofauti kati ya hali ya zamani ya wapokeaji wa ujumbe wake na hali yao wakati anawaandikia ujumbe huu, lakini tunaweza kujua sababu kwa kusoma vizuri waraka wake.
Sababu za mabadiliko ni mchanganyiko wa kufifia kwa picha ya Yesu kwenye maisha yao ya imani na kuchoka kuvumilia mateso ya muda mrefu yaliyoambatana na aibu. Hii ndio maana baada ya kuelezea jinsi walivyovumilia mateso makubwa hapo nyuma (Waebrania 10:32-34), mwandishi anawaambia “Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi. Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia” (Waebrania 10:35-37). Kwa kutaka kuwasisitiza kuvumilia anawaambia wamtazame Yesu, yeye ambaye alivumilia mateso makubwa kuliko wao; wao mateso yao hayajafika hata katika kiwango cha kumwaga damu zao (yaani hawajafikia kufa kwa ajili ya imani). Katika hili, Mwandishi anasema “mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi;” (Waebrania 12:3-4).
KUSUDI LA WARAKA
Kwa sababu hali ya awali ya waamini waliokuwa wapokeaji wa awali wa waraka huu ilikuwa imebadilika na mabadiliko haya yalikuwa na hatari ya kuleta matokeo mabaya kuhusu hatima yao ya umilele, mwandishi akaandika waraka huu ili kuwasisitiza waendelee mbele na wasirudi nyuma. Mwandishi anawaonya na kuwatia moyo waamini hawa ili wasiache kumwamini Yesu, ndio maana waraka wake anauita “ujumbe huu wa kuwatieni moyo” 13:22 BHN au “neno hili lenye maonyo“ 13:22 SUV.
Katika kutimiza hilo, mwandishi anaugawa ujumbe wake katika sehemu kuu tano. Katika kila sehemu anafanya mambo mawili makubwa. Kwanza, kwa kufafanua maandiko, anamwinua Yesu juu ya mtu au kitu chochote ili kuonyesha kwamba anastahili kuaminiwa kabisa na kupokea kujitoa kikamilifu kwa wale wanaomwamini. Pili, kwa sababu ya ukuu wa Yesu anawahimiza waamini wabaki kwa Yesu licha ya kuwepo kwa sababu zenye kulenga kuwatoa (kwa mfano mateso). Katika jambo hili la pili, mwandishi anaweka onyo kali kwenye sehemu zote tano kwa yeyote anayetaka kumwacha Yesu. Kwa hiyo katika sehemu hizo zote tano kuna ufafanuzi wa maandiko na kuna kuhimiza kutendea kazi ujumbe uliofafanuliwa kunakoambatana na onyo.
MPANGILIO WA KITABU
| MAELEZO | WAEBRANIA |
| Utangulizi | 1:1-4 |
| Ukuu wa Yesu juu ya Malaika | 1:5-2:18 |
| Ukuu wa Yesu juu ya Musa | 3:1-4:13 |
| Ukuu wa ukuhani wa Yesu kuliko wa Haruni | 4:14-7:28 |
| Ubora wa Agano jipya la Yesu | 8:1-10:39 |
| Ukuu wa Yesu juu ya mashaidi wote wa Imani | 11:1-12:29 |
| Hitimisho | 13:1-25 |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI
Kama tulivyosema hapo juu, kitabu hiki kinaanza bila anuani, jambo ambalo lilikuwa ni kawaida ya barua za karne ya kwanza. Badala yake, mwandishi anaanza na utangulizi unaonyesha kwamba Mungu katika nyakati za mwisho ameamua kuongea kupitia njia moja tu; kupitia Mwanae Kristo Yesu. Hii ni tofauti na hapo awali; Hapo awali Mungu aliongea kupitia manabii mbalimbali, kwa njia mbalimbali na kwa nyakati tofauti tofauti. Kwa nini Mungu anaongea kupitia Mwanae pekee? Yeye ndiye mrithi wa yote, kupitia yeye Mungu aliumba ulimwengu, Yeye ni mnga’o wa utukufu wa Mungu na ndiye picha halisi ya Mungu. Zaidi ya hayo, kwa sasa Mwana anaushikilia ulimwengu kwa nguvu za neno lake na yuko kwenye kiti cha mamlaka huko mbinguni baada ya kuwatakasa wanadamu dhambi zao. Na kwa sababu hiyo yeye ni bora kuliko malaika (1:1-4).
Kwa sababu mwisho wa utangulizi hapo juu, Mwandishi amesema Mwana amefanyika bora kuliko malaika, hivyo anaamua kufafanua maneno Mungu aliyoyasema kwenye maandiko kuthibitisha hilo. Kwanza, hakuna malaika aliyeambiwa na Mungu “Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa”[2] au “Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana.”[3] Badala yake malaika waliambiwa wamwabudu Mwana[4] (1:5-6). Pili, wakati malaika wao watajwa na Mungu kuwa ni watumishi,[5] mwana anatajwa na Mungu kuwa ni Mungu wenye mamlaka ya milele, lakini pia ni mfalme mpakwa mafuta (1:7-9).[6] Mbali na sifa hizo ni muumbaji na mtunzaji wa ulimwengu ambaye adumu milele (1:10-12).[7] Tatu na mwisho, hakuna malaika Mungu alimwambia “Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako”[8] kwa kuwa hao ni watumishi wanaowatumikia wale watakourithi wokovu[9] (1:13-14). Kwa maelezo hayo yote matatu mwandishi amethibitisha kutoka kwenye maneno ya Mungu kwamba Mwana ni bora kuliko malaika.
Katika utangulizi, Mwana ni bora kuliko manabii (1:1-4), sehemu ya kwanza, Mwana ni bora kuliko Malaika (1:5-14). Manabii walitumiwa na Mungu kufikisha ujumbe na malaika walitumiwa na Mungu kufikisha ujumbe. Na zaidi, Torati ya Musa ilitolewa kwa mkono wa Malaika (Wagalatia 3:19-20). Sasa kama neno la Mungu (sheria) lililofikishwa kwa njia ya malaika lilisimamiwa na Mungu kwa kiwango ambacho kila kosa lilipata malipo husika, itakuaje kwetu kama tusipozingatia neno la Mungu (Injili ya wokovu) lililonenwa na Mungu kupitia Mwanae na kuthibitishwa na Mungu kwa ishara, maajabu na mgawanyo wa zawadi za Roho mtakatifu? Hatuna chaguo, bali kuzingatia zaidi (2:1-4). Hili ni onyo la kwanza kwa wapokeaji wa ujumbe wa kitabu hiki; Hakuna kupona kama hatutazingatia neno lililonenwa na Mungu kupitia Mwanae ambaye ni mkuu kuliko malaika na manabii.
Baada ya onyo hilo, Mwandishi anajibu swali, kwa nini waamini hawatapona kama hawatazingatia neno la Mungu kupitia Mwana? Jibu ni kwa sababu, ulimwengu ujao haujawekwa chini ya malaika. Kama haujawekwa chini ya malaika maana yake uko chini ya Mwana. Kwa kunukuu Zaburi ya 8:4-6, na kwa kufafanua, mwandishi anaonyesha kwamba ulimwengu ujao na huu wa sasa uko chini ya Mwana. Pamoja na ukweli huo, mwandishi anakubali kwamba kwa sasa bado hatuoni uhalisi wa ulimwengu mzima kuwa chini ya mwana. Pamoja na hivyo, hilo aliondoi ukweli kwamba ulimwengu ujao uko chini ya mwana na ndio maana sasa tunamuona Yesu amekwishavikwa utukufu na heshima baada ya kuwa mdogo kuliko malaika kwa muda na baada ya kufa kwa ajili ya kila mtu (2:5-9).
Mwandishi anamalizia ulinganifu wa Mwana na malaika kwa kueleza uhalali, sababu na manufaa ya Mwana kufanyika mdogo kuliko malaika kwa kitambo (yaani, kufanyika mwanadamu na kupata mateso). Uhalali; Ni haki kwa Mungu kuchagua kumkamilisha[10] Yesu kwa njia ya mateso (mateso inahusisha kufanyika mwili na kufa msalabani) ili awalete watoto wengi katika utukufu (2:10). Sababu; Njia ya mateso ilichaguliwa na Mungu ili Yesu afanane na watoto atakaowaleta katika utukufu na hivyo haoni aibu kuwaita ndugu zake (2:11-13).[11] Manufaa ya Yesu kufanana na watoto ni mawili. Kwanza, kuamharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi ili awaache huru waliokuwa watumwa wa hofu ya mauti. Pili, kufanyika kuhani mkuu mwenye rehema na mwaminifu kwa Mungu kwa sababu anajua hali halisi wanayopitia watoto na hivyo aweza kuwasaidia (2:14-18).
Baada ya kuonyesha ubora wa Yesu kupita manabii katika utangulizi (1:1-4) na ubora wa Yesu kupita malaika katika sehemu ya kwanza (1:5-2:18), mwandishi katika sehemu ya pili anaingia kueleza ubora wa Yesu kupita Musa (3:1-4:13). Mwandishi anaanza kwa kuwaita waamini kumtafakari sana Yesu, aliyekuwa mwaminifu kama Musa katika kazi aliyokabidhiwa. Ingawa anaufananisha uaminifu wa Yesu na wa Musa, mwandishi anasisitiza kuwa Yesu ni bora kuliko Musa kwa sababu, ingawa Musa alikuwa mwaminifu, alikuwa mwaminifu katika hadhi ya mtumishi; lakini Yesu alikuwa mwaminifu katika hadhi ya Mwana. Msisitizo huu wa ubora wa Yesu kuliko Musa unalenga kuwatia moyo waamini washikamane na Yesu hadi mwisho (3:1-6).
Kwenye aya hapo juu, mwandishi amewataka waamini kuwa waaminifu kwa Yesu kama Yesu na Musa walivyokuwa waaminifu. Aya inayofuata, mwandishi anatumia mfano hasi kusisitiza waamini kuwa waaminifu kwa Yesu mpaka mwisho. Mwandishi anatumia mfano wa kizazi cha jangwani. Kwa kunukuu na kufafanua Zaburi 95:7–11, ambayo inaonyesha kwamba kizazi cha jangwani hakikurithi nchi kwa sababu ya kutokuamini kwao, mwandishi anawaonya wapokeaji wa ujumbe wake kwamba waangalie usiwepo kati yao hata mmoja mwenye moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai — kama kile kizazi kilichotolewa Misri na Mungu na kuongozwa na Musa jangwani miaka arobaini, lakini kikakosa kuingia nchi ya ahadi (3:7-19).
Kwa kuwa Zaburi aliyonukuu mwandishi inatoa mwaliko wa kuingia raha ya Mungu kwa watu watakaosikia sauti ya Mungu LEO, mwandishi anawasisitiza waamini kwamba wajitazame kwa tahadhari (“tuogope”), ili kwamba asiwepo miongoni mwao atakayekosa raha hiyo — ambayo kizazi cha jangwani, kilichosikia neno kama wao, kilikosa kuingia (4:1–5). Mwisho, mwandishi anasisitiza tena waamini kujitahidi kuingia raha hii ya Mungu, ili asiwepo atakayekosa, kwa sababu nafasi bado ipo. Mwandishi anatoa ufafanuzi kwa kusema, raha ya Mungu bado ipo kwa sababu kama Waisraeli waliingia kwenye raha ya Mungu wakati wa Joshua, Mungu asingetoa wito wa kuingia kwenye raha hiyo miaka mingi baadaye kupitia kinywa cha Daudi. Kutolewa kwa wito kwa kinywa cha Daudi ni ushahidi bado nafasi ya kuingia kwenye raha hii ipo hata LEO (4:6–13). Aya nzima ya kuanzia 3:1–4:13 ina onyo la pili la kitabu hiki: Msifanye migumu mioyo yenu. Tuogope, mmoja wetu asije akaonekana ameikosa raha ya Mungu; na hivyo, tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kama kizazi cha jangwani.
Baada ya kuonyesha kwamba Yesu ni bora kuliko Musa na kusisitiza waamini kutokuiga mfano wa kizazi cha jangwani, mwandishi anaingia sehemu ya tatu kuonyesha kwamba ukuhani wa Yesu ni mkuu kuliko ule wa Haruni. Kumbuka kwamba mwandishi anatumia theolojia (ufafanuzi) kuwaita (kuwahimiza) wapokeaji wake kumwamini Yesu mpaka mwisho na kuwaonya juu ya madhara ya kutokufanya hivyo.
Katika sehemu hii, mwandishi anaanza kwa kuwasisitiza waamini kuyashika sana maungamo yetu (yaani, ukiri wetu wa imani ndani ya Yesu), kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu, Yesu, ambaye anajua jinsi majaribu yalivyo, kwa kuwa naye alijaribiwa, lakini bila kufanya dhambi. Kwa sifa hizi za Kuhani Mkuu Yesu, mwandishi anawaita waamini kukikaribia kiti cha neema kwa ujasiri wakati wowote wa uhitaji (4:14-16).
Kwa kuwa mwandishi amesema zaidi ya mara moja sasa kwamba Yesu ni Kuhani Mkuu (2:17; 4:14), anaamua kuelezea imekuwaje Yesu kuwa Kuhani Mkuu wakati yeye hakutoka kwenye ukoo wa Lawi, ukoo ambao ulitoa makuhani. Kujibu swali hilo, anaanza kwa kutaja sifa tatu za makuhani. Kwanza, makuhani walikuwa wakiwawakilisha watu wote katika kutoa dhabihu zilizofanya upatanisho wa dhambi. Pili, walikuwa wanawawakilisha watu wenye udhaifu kama wao. Tatu, Walikuwa hawajichagui wenyewe, bali walikuwa wanachaguliwa na Mungu (5:1-4). Mwandishi anasema, Yesu pia ana sifa hizo zote lakini kwa ubora zaidi (anaelezea sifa hizo akianzia mwishoni, yaani 3,2,1). Tatu, Yesu pia amechaguliwa na Mungu, lakini amechaguliwa kutoka kwenye ukuhani wa Melkizedeki na sio kwa Haruni.[12]Pili, Yesu pia alikubali udhaifu wa kuwa mwanadamu na alijifunza kutii kwa Mungu kwa uzoefu wa kibinadamu kabisa ingawa hakutenda dhambi, hivyo anawawakilisha watu aliokuwa kama wao. Moja, Yesu alitolewa kama dhabihu kwa ajili ya wokovu wa milele kwa watu wote (5:5-10).
Mwandishi baada ya kuthibitisha ukuhani wa Yesu na kuonyesha kwamba Yesu anatoka kwenye ukuhani wa ukoo wa Melkizedeki na sio wa Haruni, anasitisha kwa muda nia yake ya kuelezea kwa kina ukuhani wa Yesu kutoka kwenye ukoo wa Melkizedeki na anaamua kuelezea matumizi ya theolojia yake; anaingia kuhimiza. Mwandishi anaanza kwa kutoa tathmini ya moja kwa moja kuhusu hali ya wasikilizaji wake kwa wakati huo. Anaonyesha kuwa wamekuwa wavivu katika kusikia neno la Mungu (kusikia kunahusisha kuzingatia na kutendea kazi), ingawa wamekuwa katika imani kwa muda wa kutosha kiasi ambacho walitakiwa kuwa waalimu wa wengine. Katika hali hiyo mwandishi anawafananisha na watoto wachanga wanaonyonya maziwa , ambao hawawezi kuhimili chakula kigumu (5:11-14). Baada ya tathimini hiyo, Mwandishi anawaita kukua; sio kuendelea kurudia rudia mafundisho ya awali katika imani (6:1-3).
Kwa nini waamini wanatakiwa kukua katika imani na wasibaki katika utoto? Mwandishi anajibu swali hilo kwa kutoa onyo namba tatu. Mwandishi anasema ni kwa sababu, kama watu waliopata baraka kubwa za wokovu wataanguka, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu. Hii ni kwa sababu kuanguka baada ya baraka zote hizo kubwa za wokovu ni kumsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili na kumfedhehi kwa wazi kabisa (6:4-6). Kufikisha ujumbe wake vizuri, mwandishi anatoa mfano wa ardhi inayokunywa maji kwa mvua inayoinyeshea. Ikiwa ardhi hiyo huzaa matunda, hupewa baraka na Mungu. Lakini ikiwa huzalisha miiba na magugu, basi hukataliwa na huwa karibu kulaaniwa. Mwishowe, itachomwa moto. Vivyo hivyo, ikiwa wasomaji hawataendelea kuelekea kwenye ukuaji kiimani, bali wakaanguka, basi nao pia, kama ile nchi, watakataliwa na kulaaniwa na Mungu (6:7-8).
Pamoja na onyo kali kiasi hicho, mwandishi anasema ana imani kwamba wapokeaji wa ujumbe hawatakuwa kwenye upande huo mbaya; wao watabaki kwenye upande wa wokovu. Kwa nini mwandishi ana imani hiyo? Ni kwa sababu imani yao imedhihirika katika upendo kwa watakatifu, hapo awali na mpaka sasa. Swali ni kwamba, kama mwandishi anajua waamini hawa hawako kwenye hatari, kwa nini kutoa onyo kali hivyo? Moja, kuwahimiza kila mmoja wao adhihirishe bidii ile ile mpaka mwisho. Pili, ili wasiwe wavivu, bali wawe wafuasi wenye imani na uvumilivu (6:9-12). Kwa sababu mwandishi anakusudi la kuhimiza bidii na uvumilivu kwenye ahadi za Mungu, anaamua kuwaonyesha kwa mfano. Ibrahimu, Baba wa imani, aliipata kwa uvumilivu ahadi ambayo Mungu alimpa kwa kuapa kwa nafsi yake. Mwandishi anaongeza kwa kusema kwamba wanadamu wanaapa kwa mkuu kuliko wao ili kuthibitisha ahadi zao, lakini Mungu, kwa kuwa hana mkubwa kwake, kuapa kwake ni kwa ajili ya kuwaonyesha wale wanaorithi ahadi zake kwamba makusudi yake hayabadiliki. Kwa nini Mungu ameamua kuwaonyesha warithio ahadi uhakika wa ahadi hizo? Ni ili wapate faraja imara, na faraja hiyo wataipata kwa kuwa wanajua Mungu hawezi kusema uongo kwenye ahadi yake na kwenye kiapo chake (hivyo ndiyo vitu viwili visivyoweza kubadilika). Lakini wanaopata faraja hiyo ni wale walioshika matumaini yaliyo mbele yao, matumaini yanayopenya mpaka sehemu ya ndani zaidi ya pazia, yaani, hadi katika uwepo wa Mungu, ambako Yesu, kuhani mkuu wa ukoo wa Melkizedeki, aliingia kwa ajili yetu (6:13-20).
Mwandishi, baada ya kueleza matumizi ya theolojia yake (kuhimiza), anarejea katika kuelezea (ufafanuzi) ukuu wa ukuhani wa Yesu kutoka kwenye ukoo wa Melkizedeki (Kumbuka 5:11). Kumbuka, mwanzoni mwandishi alianza kutetea kwamba Yesu ni Kuhani Mkuu pamoja na kwamba hajatoka kwenye uzao wa Haruni; Yesu yeye ni Kuhani Mkuu kutoka kwenye ukuhani wa Melkizedeki (Rejea 5:1-10). Sasa anataka kuonyesha kwamba ukuhani wa ukoo wa Melkizedeki ni mkuu kuliko wa ukoo wa Haruni; Lengo lake likiwa ni kufikia kuonyesha kwamba Ukuhani Mkuu wa Yesu ni bora kuliko wa Lawi. Lakini kabla hajafika hapo, anaanza kwa kuonyesha uhusiano wa Yesu na Melkizedeki — yaani, Yesu na Melkizedeki wanahusianaje ili tuweze kusema Yesu anatoka kwenye ukoo wa Melkizedeki? (Kumbuka, makuhani wakuu walikuwa na uhusiano na Haruni kwa kufuatilia koo zao).
Melkizedeki ana sifa mbili zinazofanana na sifa za Mwana wa Mungu (Yesu). Moja, Kuhani Melkizedeki ni “Mfalme wa haki” na ni “Mfalme wa amani” (hizi mbili ndizo sifa za Masihi kwa mujibu wa maandiko kama vile Isaya 9:6-7).[13] Pili, Kuhani Melkizedeki hana taarifa zozote za ukoo wake, mwanzo wake wala mwisho wake katika maandiko (hizi ni sifa pia za Mwana wa Mungu asiye na mwanzo wala mwisho) (7:1-3). Baada ya kuonyesha kwamba kwa sababu ya sifa hizo Yesu ni Kuhani Mkuu kutoka kwenye ukuhani wa Melkizedeki, sasa mwandishi anafafanua Mwanzo 14:14-20 kwa kuonyesha kwamba ukuhani wa Melkizedeki ni mkuu kuliko wa Haruni. Ukuu huu unaonekana kwa Lawi—kabila la kikuhani—kutoa fungu la kumi kwa Melkizedeki kupitia Abrahamu, na Abrahamu kubarikiwa na Melkizedeki (7:4-10).
Baada ya kuonyesha kwamba ukuhani wa Melkizedeki ni bora kuliko wa Lawi, sasa mwandishi anaonyesha kwamba ukuhani wa Yesu (kupitia ukuhani wa Melkizedeki) ni bora kuliko ule wa Lawi. Mwandishi anasema, kwa maandiko (Zaburi 110:4) kutabiri ujio wa Kuhani Mkuu kwenye ukoo wa Melkizedeki ni ishara kwamba ukuhani wa Lawi haukuleta ukamilifu. Na kwa sababu hiyo, ukuhani umebadilika. Si hivyo tu, bali hata sheria imebadilika — ndiyo maana Kuhani huyu Mkuu, Yesu, ametoka kwenye kabila la Yuda, kabila ambalo halikuwa na nafasi ya ukuhani kwa mujibu wa sheria ya awali. Zaidi, kwa mabadiliko haya ya sheria, ukuhani wa Yesu haukupatikana kwa sababu ya sifa za kiukoo kama makuhani wa Lawi, bali ulipatikana kwa sababu ya sifa ya umilele wake. Na kwa Yesu kuchukua ukuhani huo, kumeleta matumaini mapya ambayo sheria ya zamani haikuweza kukamilisha, yaani kumkaribia Bwana (7:11-19).
Kufikisha hoja zake kileleni, mwandishi anamfananisha Yesu katika ukuhani wake na makuhani kutoka kwa Lawi moja kwa moja. Moja, wao walifanywa makuhani pasipo kiapo cha Mungu, lakini Yesu alifanywa Kuhani Mkuu kwa kiapo (kiapo toka Zaburi 110:4). Pili, wao walichaguliwa wengi kwa sababu walikuwa wanakufa, lakini yeye ni mmoja kwa kuwa ni wa milele. Na kwa sababu hii, “aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee” (7:20-24). Mwandishi anahitimisha hoja yake ya ukuu wa ukuhani wa Yesu (Aliyoanza nayo 5:1) kwa kurejea sifa bora za Yesu ambazo makuhani wa Lawi hawakuwa nazo (7:25-28).
Mpaka hapa, mwandishi amesema kuwa Yesu ni njia bora ya Mungu kuzungumza kuliko manabii (1:1–4), Yeye ni bora kuliko malaika (1:5–2:18), Yeye ni Mwana mwaminifu, mkuu kuliko Musa mtumishi mwaminifu (3:1–4:13), na zaidi, Yesu ni Kuhani Mkuu bora kuliko makuhani wakuu wote kutoka kabila la Lawi (5:1–7:28). Sasa katika sehemu ya nne anakwenda kuongelea ubora wa huduma ya Yesu ya kikuhani katika Agano bora lenye ahadi bora zaidi (8:1–10:39). Sehemu hii inaweza kugawanywa katika sehemu sita.
Sehemu ya Kwanza: Mwandishi anahitimisha aya ya juu kwa kusema kwamba, hoja ya msingi kwa yote aliyokuwa anayasema ni kwamba tunaye Kuhani Mkuu, Yesu, ambaye yuko mbinguni kwenye kiti cha mamlaka. Mbali na kuwa kwenye mamlaka, yeye ni mhudumu bora kwa kuwa anatumika katika hema (madhabahu) isiyojengwa na wanadamu. Hivyo, yeye ni mpatanishi wa agano bora lenye ahadi bora (8:1–6). Sehemu ya Pili: Mwandishi anatoa sababu kwa nini agano la Yesu ni bora. Sababu ni kwamba, kuwepo kwa ahadi ya agano jipya kupitia kinywa cha Yeremia (Yeremia 31:31–34) ni ushahidi tosha kwamba agano la kwanza lilikuwa na mapungufu (8:7–13).
Sehemu ya tatu: Mwandishi anaonyesha udhaifu wa hema ya agano la kwanza na taratibu zake za ibada ili mbeleni aeleze ubora wa huduma ya kikuhani ya Yesu. Mwandishi anafanya hivyo kwa kuelezea mpangilio wa hema hiyo na taratibu zake za ibada (kama vile kuingia kwa Kuhani Mkuu mara moja tu ndani ya Patakatifu pa Patakatifu), ili aonyeshe udhaifu wake. Kuwepo kwa utaratibu wa Kuhani Mkuu kuingia mara moja kwa mwaka Patakatifu pa Patakatifu ni uthibitisho kwamba njia ya kupaingia Patakatifu ilikuwa haijafunguka kwa kila mtu (linganisha na 10:19–20). Lakini pia mpangilio wa hema, ambao ulikuwa unaonyesha utengano kati ya Mungu na watu (kuwa na patakatifu pa patakatifu ndani zaidi watu wengine wasipoweza kufika), ni ishara tosha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zinatolewa zilikuwa haziwezi kumkamilisha mtu aabuduye (yaani, hazikuweza kumfikisha kwenye uwepo wa Mungu). Pamoja na udhaifu wa hema hiyo, hema hiyo ilikuwa ni mfano au ishara ya hema ya sasa anayohudumia Yesu (9:1-10).
Sehemu ya nne: Baada ya kuonyesha udhaifu wa huduma iliyokuwa inafanyika katika hema na ukuhani wa Agano la Kwanza, sasa mwandishi anajikita kuelezea ubora wa huduma ya Yesu ya kikuhani. Anaanza na utangulizi akiainisha mambo matatu bora kwa upande wa huduma ya Yesu: Huduma yake alifanyia kwenye hema iliyoko mbinguni; Dhabihu yake ni damu yake mwenyewe; na Ametoa mara moja tu kwa wokovu wa milele (9:11-12). Haya mambo matatu anayasisitiza kwa maelezo zaidi. Kwanza, Dhabihu ya Yesu ilikuwa ni damu yake mwenyewe tofauti na agano la kwanza ambapo dhabihu ilikuwa ni damu ya mbuzi na mafahali (9:13-22). Pili, Huduma yake alifanyia kwenye hema isiyofanywa na mikono ya wanadamu tofauti na agano la kwanza (9:23-24). Mwisho, dhabihu yake ilitolewa mara moja tu, tofauti na agano la kwanza, ambapo kulikuwa na marudio ya dhabihu (9:25-28). Pamoja na Yesu kufa mara moja tu, mwandishi anasema atakuja mara ya pili kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.[14]
Sehemu ya tano: Mwandishi anarudia tena kusisitiza sifa moja kati ya zile tatu za kuhusu ubora wa huduma ya Yesu ya kikuhani. Anarudia sifa ya kutolewa mara moja tu kwa dhabihu ya Yesu na hivyo kukamilisha waamini kabisa. Mwandishi anatekeleza hilo kwa njia mbili; Moja, anaeleza udhaifu wa sheria, yaani kutolewa kwa dhabihu kwa marudio ni ushahidi kwamba dhabihu hizo zilikuwa haziondoi dhambi. Pili, unanukuu Zaburi 40:6-8 na kufafanua kwamba, Mungu hakuzitaka dhabihu zilizokuwa zinatolewa chini ya Sheria, lakini badala yake Yesu alikubali kuja kufanya mapenzi yake, yaani kuja kufa mara moja kwa ajili ya dhambi (10:1-10).[15] Kwa msisitizo tena, mwandishi anatofautisha dhabihu ya Yesu na dhabihu chini ya Sheria akisisitiza sifa ile ile ya hapo juu. Mwandishi anasema, chini ya sheria dhabihu zilitolewa kila siku, makuhani walisimama, na pamoja na kurudiwa rudiwa dhabihu hizo hazikuondoa dhambi. Kwa upande mwingine, Kristo alitoa dhabihu moja, sasa ameketi mkono wa kuume wa Mungu, na pamoja na kutolewa mara moja aliwakamilisha waliotolewa dhabihu hiyo (10:11-14). Tena kwa kunukuu Yeremia 31:33-34 anaonyesha sifa mbili za ubora wa Agano hili linalohudumiwa na Yesu; Dhambi zimefutwa kabisa na sheria za Mungu zimeandikwa moyoni (10:15-18).[16]
Sehemu ya sita; Kwa nini ufafanuzi wa kina kiasi hiki kuhusu ubora wa huduma ya Yesu ya ukuhani (8:1–10:18), uliotanguliwa na maelezo marefu juu ya ukuu wa ukuhani wa Yesu (5:1–7:28)? Jibu ni hili: kuwaita waamini kwenye mambo matatu. Moja, kukaribia patakatifu pa Mungu kwa ujasiri. Pili, kushika sana ungamo la tumaini letu bila kugeuka. Tatu, kuangaliana, kuhimizana, kuonyana, na kutoacha kukusanyika (10:19–25). Kwa nini mwandishi anawaita waamini katika mambo hayo matatu? Jibu ni onyo la nne la kitabu hiki. Ni kwa sababu, kama wakikengeuka kwa makusudi na kutoka kwa Yesu, basi hawatafaidika na dhabihu ya Yesu. Badala yake, watakabiliwa na hukumu kali ya Mungu, kali kuliko hukumu katika kipindi cha torati ya Musa. Kusisitiza kwamba hukumu hii itatoka kwa Mungu mwenyewe, mwandishi anarejea maneno ya Mungu kutoka Kumbukumbu la Torati 32:35-36 (10:26-31). Pamoja na onyo hilo kali, mwandishi anawatia moyo waamini kuendele kuamini kwa namna mbili. Moja, anawakumbusha jinsi walivyovumilia mateso kipindi cha nyuma (10:32-34). Pili, anawaonyesha mbele kwa kunukuu Habakuki 2:3-4; yaani anatumia maandiko hayo kusema kwamba muda wa kurudi Yesu umebaki mchache, hivyo waendelee kuwa na imani mpaka mwisho (10:35-39). Hapa ndipo Mwandishi amefikia kilele cha ujumbe wake kuhusu ubora wa huduma ya kikuhani ya Yesu.
Mwisho wa aya iliyopita, mwandishi akiwa anawasisitiza wapokeaji wa ujumbe wake kuamini mpaka mwisho, amenukuu Habakuki 2:3-4 ambayo ina maneno“Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye” (10:38). Maneno hayo yanasisitiza imani na kukataza kusisita sita. Na wakati anafunga kabisa aya hiyo akasema “Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu” (10:39). Maneno haya yanaonyesha kuwa mwandishi yuko upande wa wenye imani inayookoa roho, na siyo miongoni mwa wanaopotea. Na kama ambavyo amekuwa akisisitiza waamini hawa kuwa na imani mpaka mwisho na kuwaonya dhidi ya kutokuamini na kukengeuka, mwandishi sasa anataka kuielezea imani hiyo anayoizungumzia. Kwa lugha nyingine, mwandishi anataka kuelezea: Imani inayomfanya mwenye haki kuishi ni ipi? Imani inayookoa roho ni ipi? Hii ndio sehemu ya tano ya kitabu hiki.
Mwandishi anaielezea imani ambayo amekuwa anawataka wapoakeaji wa ujumbe wake kuwa nayo mpaka mwisho, kwa kuwa kwa hiyo wazee walipata kibali mbele za Mungu (11:1-2). Wazee hao waliopata kibali mbele za Mungu kwa imani ni Abeli, Henoko, Nuhu na Ibrahimu pamoja na familia yake (11:3-12). Kabla hajaendelea kuelezea imani ya Ibrahimu na famili yake, mwandishi anawaonyesha waamini kwamba Ibrahimu na familia yake pamoja mashahidi wa imani kabla yao, walikufa katika imani wakiwa hawajapokea zile ahadi kikamilifu. Pamoja na hivyo, hawakuacha kuwa na imani kwa kuwa walijua wao ni wageni na wasafiri katika nchi ya sasa (11:13-16). Baada ya hapo mwandishi anaendelea kuelezea imani ya Ibrahimu, Isaka, Yakobo, Yusufu, Musa, watu waliovuka bahari ya shamu na Rahabu yule kahaba (11:17-31). Kwa kuwa mashahidi walioshi kwa imani mpaka mwisho ni wengi, mwandishi anaamua kutoa muktasari. Muktasari wa kwanza ni wa wale waliopata ushindi wa aina mbalimbali kwa imani (11:32–35a). Muktasari wa pili ni wa wale ambao walifanyiwa mabaya na hata kuuawa, lakini wakiwa na imani bado (11:35b–38). Na anarudia alichokisema kwenye kiingilio kifupi cha mwanzoni (yaani 11:13–16): hawa wote hawakuipokea ahadi. Lengo la Mungu kuwasubirisha ile ahadi ni ili sisi pia tuwepo pamoja katika kupokea ahadi hiyo. Ahadi hiyo ni utimilifu wa mpango wa ukombozi wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, yaani kuingia katika mji mpya wa Yerusalemu (11:39–40).
Baada ya kuonyesha mifano yote hiyo ya mashahidi wa imani, mwandishi anawaita waamini kuweka kando kila kinachowazuia kuendelea mbele na mbio zao (Anatumia picha ya mashindano ya mbio). Tena anawaita kumtazama Yesu kama mfano bora zaidi kuliko hata ile ya mashahidi wa imani, kwa kuwa yeye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, hivyo wakimtazama yeye hawatachoka wala kuzimia moyo (12:1-3). Katika kuwasisitiza kuendelea na imani hata katikati ya mateso, mwandishi anawaonyesha mambo mawili. Moja, Wanatakiwa kuendelea kuamini kwa kuwa pamoja na mateso wanayopata bado hawajafikia kiwango cha kumwaga damu (kama Yesu alivyomwaga damu). Pili, kwa kunukuu na kufafanua Mithali 3:11-12, mwandishi anawakumbusha waamini kwamba kupata mateso ni dalili ya kukubalika na Mungu kama watoto wake. Kama vile mzazi wa dunia anavyotumia hali ambazo mtoto huziona kuwa za kuumiza ili kufikia lengo fulani, vivyo hivyo Mungu — ambaye anastahili heshima zaidi kuliko mzazi wa duniani — hutumia maumivu kwa watoto wake wa kweli ili kuwaletea utakatifu katika mwenendo (12:4-11).[17] Kama hitimisho la msisitizo wa kuendelea kupiga mbio, mwandishi anarudi tena kwenye picha ya mashindano ya mbio kuwataka waimarike katika mbio zao za imani (12:12-13).
Kwa kutumia mangalizo matatu, mwandishi anawasisitiza tena waamini kuendelea kuamini, mpaka pale watakapopata ahadi. Angalizo la kwanza: Hakuna kumwona Mungu pasipo utakatifu, hivyo tafuteni sana kuwa nao huo (Pamoja na amani na kila mtu) Angalizo la pili: Angalieni sana asiwepo mtu atakayepungukiwa neema ya Mungu (yaani mtu atakayegeuka, kama ilivyoonywa katika Torati 29:18). Angalizo la tatu: Asiwepo mtu kama Esau ambaye aliuza uzaliwa wake wa kwanza kwa chakula kimoja, na hakuwa na nafasi ya kuupata tena (12:14-17).
Kwa nini mwandishi ametoa msisitizo kwa kurudia rudia kuwahimiza kwamba waendele kuamini mpaka wapate ile ahadi? Jibu ni kwamba waamini hawajafika kwenye mlima Sinai bali wapo kwenye mlima Sayuni. Sinai—mahali pa moto, giza, mawingu mazito na tufani; mahali pa mlio wa baragumu na sauti ya Mungu ya kutisha. Kinyume chake, Sayuni ni mlima katika mji wa Yerusalemu ya mbinguni. Hapo waamini wapo katika ushirika na maelfu ya malaika wanaosherehekea, pamoja na washirika wa kanisa walio duniani na wale waliokwisha kufa. Zaidi ya yote, wamefika kwa Yesu, mpatanishi wa agano jipya, ambaye damu yake inanena mema kwa ajili yao (12:18-24). Mwisho,mwandishi anamalizia kwa onyo la tano na la mwisho katika barua hii. Waamini wanaonywa wasimkatae anenaye kutoka mbinguni (kutoka Mlima Sayuni), kwa kuwa wakifanya hivyo hukumu yao itakuwa kubwa kuliko ya Waisraeli waliokataa kusikia sauti ya Mungu iliyonena juu ya nchi (katika Mlima Sinai). Hii ni kwa sababu ameahidi kutikisa mbingu na nchi, kama alivyotikisa nchi katika Mlima Sinai. Mungu atakapotikisa mbingu na nchi, ufalme wake pekee ndio utakaobaki. Hivyo, kwa kuwa huo ndio ufalme tutakaoupokea, tunatakiwa kuonyesha shukrani kwa Mungu kwa kumtolea Mungu ibada ya kumpendeza, kwa kuwa yeye ni moto ulao (12:25-29).
Barua hii inafikia mwisho kwa mwandishi kuwasisitiza waamini kuishi maisha ya shukrani kwa Mungu kwa sababu ya mambo mazuri na makubwa waliyoyapokea. Mwandishi anaanza na kuhamasisha upendo, ufadhili, kuhudumia wafungwa, kuheshimu ndoa na kuridhika katika maisha (13:1-6).[18] Mwandishi anawasisitiza waamini kujitambulisha na Kristo katika mateso yake na kutoa dhabihu za sifa na matendo mema, huku akiwataka kuwaiga viongozi wao wa zamani na kuwatii viongozi wa sasa (13:7-17). Baada ya hapo, mwandishi anaomba maombi, anatamka baraka za mwisho na anamalizia kwa salamu za mwisho (13:18-25).
FOOTNOTES
[1] Kile anachokieleza mwandishi kuhusiana na namna walivyopokea neno la Mungu na jinsi Mungu alivyolithibitisha kwa ishara, maajabu, na Roho Mtakatifu ndiyo kawaida tunayoiona kwenye upandaji wa kanisa katika maeneo mengi kama vile Galatia (Wagalatia 3:2–5), Korintho (1 Wakorintho 2:1–5), na Efeso (Matendo 19:10–20).
[2] Nakuu kutoka Zaburi 2:7
[3] Nakuu kutoka 2 Samweli 7:14
[4] Nukuu kutoka Zaburi 97:7
[5] Nukuu kutoka Zaburi 104:4
[6] Nukuu ikitoka Zaburi 45:6-7
[7] Nukuu kutoka Zaburi 102:25-27
[8] Nakuu kutoka Zaburi 110:1
[9] Marudio ya Nukuu ya Zaburi 104:4
[10] Kukamilisha katika muktadha wa waebrania ina maana ya kufikisha kitu katika hali iliyokusudiwa/hali ya mwisho. Kwa maana hiyo, lugha hii ina maana kwamba Mungu aliamua kumfikisha kristo katika heshima na utukufu kwa njia ya mateso.
[11] Mwandishi anaeleza hilo kwa kunukuu Zaburi 22:22 na Isaya 8:17-18
[12] Ukweli huu, mwandishi anaufundisha kwa kunukuu zaburi mbili za kimasihi. Zaburi ya kwanza ni ile ambayo amekwisha kuinukuu hapo awali, yaani Zaburi 2:7, na zaburi ya pili ni Zaburi 110:4.
[13] Kumbuka kwamba Makuhani kutoka katika kabila la Lawi walikuwa hawana sifa ya Ufalme. Watu wenye sifa za kiufalme walitoka katika kabila la Yuda, yaani kwenye ukoo wa Daudi.
[14] Mwandishi na mfafanuzi George H Guthrie, anatusaidia kutuonyesha kwamba ”Waebrania 9:11–28 inazungumza kuhusu “kuonekana” kwa Kristo mara tatu tofauti,…kwa mpangilio wa wakati. Akiashiria dhabihu yake kwa ajili ya dhambi, mwandishi anazungumza kuhusu kuonekana kwa Mwana kwa mara ya kwanza (nyuma ya wakati), ambapo alipata ukombozi wetu (9:11). Katika 9:24, anataja kuwa Kristo, katika nafasi yake ya Kuhani Mkuu, sasa anaonekana mbele za Mungu kwa ajili yetu (9:24). Hatimaye, Kristo ataonekana tena mwisho wa nyakati (mara ya “pili” kuhusiana na uumbaji huu), kuleta wokovu wa mwisho kwa wale wanaomngoja kwa shauku kuja kwake (9:28).
[15] Waebrania 10:5-7 ni nukuu ya Zaburi 40:6-8. Kwa mujibu wa Mwandishi, Yesu ndiye msemaji wa maneno haya ya Zaburi.
[16] Waebrania 10:16-17 ni nukuu ya Yeremia 31:33-34
[17] Waebrania 12:5-6 ni nukuu kutoka Mithali 3:11-12
[18] Katika Waebrania 13:5, mwandishi ananukuu Torati 31:6, na katika 13:6 ananukuu Zaburi 118:6.
Unakuja hivi karibuni…

