MAANA YA KANISA
Ukipita kwenye barabara kubwa au ukiwa ndani ya miji mikubwa ndani ya taifa letu, basi ni lazima utakutana na majengo yenye ubora na ukubwa tofauti tofauti lakini yakiwa yameandikwa maneno haya “Kanisa la……” Mwendelezo au utangulizi wa neno hili unaweza kutofautiana kwa namna mbalimbali lakini neno “Kanisa” likabaki. Na kwa kuwa lugha ya Kiingereza ni lugha iliyoenea zaidi duniani, basi usipokuta neno “Kanisa” utaona neno “Church”, ambalo tafsiri yake ni Kanisa katika Kiswahili. Hii inaonyesha kwamba angalau asilimia tisini (Makadirio ya kufikirika) ya jamii ina ufahamu wa neno Kanisa na pia ina ufahamu juu ya Kanisa ni nini. Kwa kuwa Kanisa ni maarufu kwa kiasi hiki, unaweza kujiuliza kwa nini tunahitaji kujifunza maana ya neno Kanisa, wakati asilimia tisini ya jamii ina ufahamu wa kuhusu Kanisa? Lakini kwa kuwa maneno yana maana tofauti tofauti kutokana na mazingira na nyakati, ni vizuri kujifunza maana ya Kanisa kama neno hili lilivyotumika katika Biblia.
Kwenye jamii tunayoishi, neno Kanisa linaweza kuwa na maana zaidi ya moja. Kanisa linaweza kuwa ni mahali ambapo wakristo wanakutana kwa ajili ya kufanya “ibada” zao. Mahali hapa panaweza kuwa jengo rasmi au eneo tu lisilo na jengo. Hii ni moja kati ya maana maarufu sana kwenye nyakati na majira ya sasa katika jamii yetu. Maana ya pili ambayo pia ina umaarufu mkubwa ni; Kanisa ni dhehebu au taasisi husika katika dini ya kikristo. Kwa hiyo, mara nyingi watu wanaposema makanisa yanaongezeka huwa wanamaanisha taasisi au madhehebu ya kikristo yanaongezeka au majengo yanaongezeka. Jambo la kushangaza ni kwamba, maana hizi mbili ni tofauti kabisa na maana ya neno Kanisa kama lilivyokusudiwa na waandishi wa Biblia, hasa waandishi wa Agano jipya.
Kutokana na ukweli kwamba neno “Kanisa” linatumika visivyo katika jamii yetu leo, ni muhimu kuchukua muda kuangalia maana halisi ya neno “Kanisa” kama lilivyotumika katika Agano jipya ili kupata uelewa sahihi wa kibiblia. Lakini pia, ili kupata uelewa mpana zaidi tutajifunza maana ya neno “Kanisa” kabla waandishi wa Agano jipya hawajaanza kulitumia neno hili katika maandishi yao. Tuna uhakika kabisa neno kanisa kama lilivyotumika katika Agano jipya katika lugha yake ya asili (Kiyunani εκκλησια, unukuzi katika Kiswahili ekklesia), ni neno ambalo waandishi wa Agano jipya walilikuta likitumika. Kwa maneno mengine, neno kanisa halikuzaliwa baada ya kuzaliwa kwa ukristo. Neno kanisa lilikuwepo na lilikuwa linatumika kabla ya ukristo kuzaliwa.
Neno kanisa (Kiyunani ἐκκλησία, unukuzi katika Kiswahili ekklesia) kabla ya kuzaliwa Ukristo lilikuwa na maana ya kundi la raia waliokusanyika kwa lengo maalumu la kujadili na kufanya maamuzi kwa ajili ya jamii yao. Katika mfumo wa kidemokrasia uliokuwa umezaliwa katika nyakati za Kiyunani, kanisa (ekklesia) ilikuwa ni kusanyiko la raia wote wanaume wenye umri wa miaka kumi na nane au zaidi, ambao walikusanyika kwa ajili ya kujadili na kufanya maamuzi kwa ajili ya jamii yao. Kwa mfano mwepesi tunaoweza kuuelewa katika majira yetu, kanisa ni kundi la wananchi wa mtaa (au mji) waliokusanyika ili kujadili mambo yahusuyo mtaa (au mji) wao.
Kwa hiyo, waandishi wa Agano Jipya pia walitumia neno hili kumaanisha kundi la watu waliokusanyika kwa lengo maalumu. Hata hivyo, wao walikwenda mbali zaidi na kupanua matumizi yake, ingawa msingi wa neno uliendelea kubaki uleule (Msingi ni kwamba Kanisa ni kundi la watu). Waandishi hawa waliongeza maana ya neno hilo kwa namna mbili zifuatazo:
- Kwanza, kwao kanisa lilikuwa ni kundi la watu waliomwamini Yesu au walioitikia mwito wa Yesu, Kiongozi, au Mamlaka iliyo juu yao, ambao wanakusanyika katika eneo fulani la kijiografia kwa ajili ya kuishiriki imani yao kwa pamoja. Kundi lile la watu waliomwamini Yesu na walioitikia mwito wake na wanakusanyika katika eneo moja, kwa mfano wale waliokuwa wanakusanyika katika nyumba ya mtu mmoja, ndio walikuwa wanaitwa Kanisa. Hii ndio maana Mtume Paulo analisalimu Kanisa lililo kuwa linakutana katika nyumba ya Prisca na Akila (Warumi 16:4).
- Pili, Kanisa kwao lilikuwa ni kundi la watu wote duniani/au katika eneo fulani la kijiografia kama mji au jiji ambao wanamwamini Yesu/walioitikia mwito wa Yesu, hata kama walikuwa hawakutani pamoja au hawawezi kukutana pamoja. Kwa mfano, watu wote waliomwamini Yesu waliokuwa wanaishi Rumi waliitwa Kanisa la Rumi (Warumi 1:7). Lakini pia, wote waliomwamini Yesu duniani pamoja na kutokuwezekana kwa wao kuonana au kukutana waliitwa kanisa. Yesu aliposema atalijenga kanisa na milango ya kuzimu haitalishinda, alikuwa anamaanisha atajenga kundi la watu watakaomwamini yeye duniani kote ambao kwa ujumla wao milango ya kuzimu haitawashinda, pamoja na kutokuonana kwao au kukutana uso kwa uso (Mathayo 16:18).
Jambo la msingi katika maana hizi zote mbili ni kwamba waandishi wa Biblia walitumia neno Kanisa kumaanisha kundi la watu waliomwamini Yesu. Hivyo, maana ya kanisa ni kundi la watu wanaomwamini Yesu na sio vinginevyo.
Mbali na kundi hili la watu wanaomwamini Yesu kuitwa Kanisa, waandishi wa Agano jipya pia walilipa kundi hili majina mengine yenye lugha ya picha. Majina haya ni kama vile:
- Hekalu la Mungu
1 Wakorintho 3:16-17 na 2 Wakorintho 6:16-18
- Mwili wa Kristo
Waefeso 1:22-23; 4:11-16
- Mke wa mwanakondoo
Ufunuo 19:7-9
Mbali na majina hayo, kanisa pia limefananishwa na vitu mbalimbali kwa lugha ya picha ili kusisitiza mambo mbalimbali kama vile ushirika kati yetu na umiliki wa Mungu wa Kanisa. Baadhi ya picha zinazofanishwa na kanisa ni kama vile: kanisa ni shamba la Mungu (1 Wakorintho 3:9), kanisa ni jeshi (Wafilipi 2:25; Filemoni 2; 2 Timotheo 2:3-4), kanisa ni nyumba ya Mungu (1 Timotheo 3:15; Waebrania 3:6; 1 Petro 4:17) na kanisa ni familia ya Mungu (Waefeso 2:19). Lugha hizi zote hazingumzii kitu kingine isipokuwa zinazungumzia kundi la watu waliomwamini Yesu/kuitikia mwito wa Yesu.
UMUHIMU WA KUZINGATIA MAANA SAHIHI
Unaweza kufikiri kwamba maana ya neno haiathiri namna watu wanavyohusiana na kitu husika, lakini si kweli. Watu wanahusiana na vitu kutokana na maana wanayoifahamu kuhusu vitu hivyo. Ndio maana ni muhimu kuelewa na kuhusiana na kanisa sawa sawa na Biblia inavyofundisha.
Unajua kwa nini gharama kubwa za fedha zinatumika kujenga majengo yanayoitwa kanisa, ukilinganisha na kiasi kinachotumika kuwasaidia waamini kuboresha maisha yao ya kila siku? Hii ni kwa sababu watu wengi wanajua na wanaamini kuwa kanisa ni jengo. Ndiyo maana wako tayari kutoa kwa ajili ya ujenzi wa majengo, lakini si kusaidia moja kwa moja kundi la waamini.
Umewahi kusikia kuna mnada au changizo la kusaidia waamini walioko kwenye umasikini? Na ni mara ngapi umesikia kuna changizo maalumu la kuchangia kujenga jengo linaloitwa Kanisa? Kwa uzoefu wangu mdogo, nimepata barua na kadi maalum mara nyingi zinazonitaka kuchangia ujenzi wa jengo linaloitwa Kanisa, lakini sijawahi kupata kadi wala barua maalum ya kuchangia kundi la waamini wanaoishi kwenye maisha yanayohitaji kuboreshwa. Lakini ukisoma vizuri Agano jipya, utaona makanisa yalikuwa yanafanya changizo kwa ajili ya kundi lingine la waamini ambao wako kwenye hali ya maisha inayohitaji kuboreshwa (Angalia, 1 Wakorintho 16:1–4; 2 Wakorintho 8 na 9; Warumi 15:26–28). Katika kizazi chetu tunafanya tofauti na Kanisa la kwanza kwa kuwa maana ya Kanisa tuliyoielewa na kuiamini sio sahihi. Unataka kufanya jambo linalogusa moyo wa Mungu kwa fedha na mali zako? Basi fanya jambo litakaloboresha maisha ya kundi la waamini kiroho na kimwili, ukianza na wale mnaokutana mahali pamoja. Kwa kufanya hivyo utakuwa umeelewa nini maana ya Kanisa.
Katika maisha yako ya kiimani, ni kitu gani kimekuwa kinakupa kujisikia fahari? Ubora wa maisha ya kundi la waamini (hasa ubora wao katika kumfanania Kristo) au ubora wa jengo mnalokutania? Je, viongozi wako katika kusanyiko lenu wanajivunia nini? Wanajivunia jengo kubwa na zuri mlilofanikiwa kulijenga? Au wanajivunia ubora wa maisha ya kundi la waamini? Majibu ya maswali haya yatakusaidia kukuonyesha wewe au viongozi wako wanatafsiri gani ya Kanisa ndani ya fahamu na mioyo yao. Kama fahari iko kwenye jengo zuri na kubwa, basi ni dhahiri mtu huyu anaamini Kanisa ni jengo. Kama fahari iko kwenye ukubwa na ubora wa dhehebu alilopo, basi ni dhahiri mtu huyu anaamini kwamba kanisa ni dhehebu. Kama fahari iko kwenye ukubwa na ubora wa taasisi aliyopo, basi ni dhahiri kwamba mtu huyu anaamini kwamba kanisa ni taasisi. Wenzetu walioelewa vizuri maana ya Kanisa waliona fahari katika ubora wa maisha ya waamini ambao ndio kanisa (1 Wathesalonike 2:19-20). Na sisi tukielewa vizuri maana ya kanisa katika fahamu zetu na mioyo yetu ikakubali kweli hii, basi tutaona fahari pale tunapoona ubora wa maisha ya kundi la waamini na sio vinginevyo.
Je, huwa unafanya jitihadi zote kuhakikisha umeingia tu kwenye lile jengo na kusikiliza kitakachoendelea lakini hutaki kujihusisha na chochote? Au huwa unafanya jitihada kuhakikisha unachangia kwenye ustawi wa maisha ya kundi la waamini? Una uwezo gani mkubwa kati ya kutetea kundi la watu waliomwamini Kristo au kutetea taasisi/dhehebu ulilopo? Kipi kimejaa kichwani mwako kati ya taarifa za maendeleo ya kundi la watu unaokutana nao waliomwamini Yesu, au historia ya taasisi/dhehebu ulilopo? Majibu ya maswali haya pia kama ukiyajibu kwa ukweli yatakusaidia kukuonyesha maana ya neno Kanisa iliyoko kwenye ufahamu na moyo wako.
Majengo, madhehebu au taasisi kwa ujumla wake sio vitu vibaya kabisa, ni vyema sana, lakini hivyo vyote ni nyenzo na sio kitu halisi. Kundi la waamini ndio kitu halisi, kama tunaamini Kanisa ni kundi la watu, basi mioyo yetu ijawe na kundi la watu kiasi ambacho matendo yetu yataonyesha kwamba ni kweli tumejawa na kundi la watu walioamini. Rasilimali zetu, vipaumbele vyetu, fahari yetu na furaha yetu inatakiwa iwe imeelekezwa kwenye kundi la watu walioamini na sio kwenye nyenzo, kama kweli tunaelewa kanisa ni kundi la watu walioamini.
LENGO LA KANISA
Je, ni nini makusudi ya Mungu kuanzisha Kanisa? Kwa nini baada ya kumuokoa mtu mmoja mmoja, Mungu asituache kila mtu aendelee na maisha yake kwa kujitegemea? Kwa upande mwingine, kwa nini Mungu anataka waamini kukutana mahali pamoja? Mungu alianzisha Kanisa kwa kuwa kuna jambo alitaka Kanisa lifanye, na jambo hilo ndilo lengo la Kanisa.
Lengo la Kanisa ni moja, lakini linaweza kutazamwa kwa namna mbili: lengo la ndani na lengo la nje.
Lengo la kanisa ni kumfanya kila mwanadamu amfananie Bwana Yesu Kristo katika mawazo, nia, fikra, tabia, mwenendo na ujumla wote wa maisha yake. Kwa kuligawa lengo hili tunapata lengo la ndani la kanisa na lengo la nje la kanisa.
Lengo la Ndani.
Lengo la ndani la kanisa ni kumfanya kila mwamini awe kama Kristo alivyo katika nia, mawazo, tabia, mwenendo na ujumla wa maisha yake (Awe mwaamini anayemfanania Kristo). Hili ni lengo la kanisa kwa ajili yake lenyewe. Kwa lugha nyingine, lengo la kundi la waamini ni kumfanya kila mwamini aliye katika kundi hilo awe kama Kristo Yesu alivyo katika nia, mawazo, tabia, mwenendo na katika ujumla wote wa maisha yake.
Lengo la Nje.
Lengo la nje la kanisa ni kuwa nuru kwa wasioamini ili waitikie mwito huu mkuu wa wokovu. Hili ni lengo la kanisa kwa ajili ya watu ambao bado hawajafikia kumwamini Bwana Yesu Kristo. Kwa ufafanuzi zaidi, lengo la kundi la watu walioamini ni kumfanya kila ambaye hajamwamini Yesu afikie kwenye maamuzi ya kumwamini yeye na hivyo kupata wokovu.
Lengo hili na katika mgawanyo wake ndio mwongozo wa nini kanisa linatakiwa kufanya likiwa hapa duniani. Hivyo, sisi kama waamini wa mahali pamoja tunapotaka kuamua nini cha kufanya, tutatakiwa kuongozwa na lengo hili. Tuna uhuru wa kufanya jambo lolote lile ikiwa jambo hilo mwisho wa siku litatimiza lengo hili. Kwa lugha nyingine, hata kama tunafikiria jambo tunaloweza kulifanya ni zuri kiasi gani, lakini kama halilengi kumfanya mwanadamu amfananie Bwana Yesu Kristo katika mawazo, nia, fikra, tabia, mwenendo na ujumla wa maisha yake, basi jambo hilo sio la kwetu kulifanya. Na kwa upande mwingine, tunaweza kuona jambo fulani ni gumu au halina mvuto, lakini kama jambo hilo likifanyika linalenga kutimiza lengo basi tunatakiwa kufanya jambo hilo kwa moyo wote.
Kweli hii pia inatuita kutathimini yale tunayoyafanya; Je, mambo tunayoyafanya sisi kama kanisa yanatuwezesha kufikia lengo hili? Kama jibu ni ndio, basi tunatakiwa kufanya kwa bidii zaidi. Kama jibu ni hapana, basi tunatakiwa kuacha kufanya jambo hilo na kutafuta kufanya jambo litakaloweza kutimiza lengo.
Lengo hili la kanisa linafundishwa na sehemu nyingi katika Biblia, lakini tutaangalia maandiko mawili tu kutoka katika barua mbili za mtume Paulo ambazo kwa ujumla jumbe zake zinafanana sana. Kwa kuwa tutafafanua kwa kirefu Waefeso 4:1-16 katika sura inayofuata, katika sura hii tutaangalia kutoka kwa Wakolosai 1:24-29.
Wakolosai 1:24-29
Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake;ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo. Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu.
Katika kifungu hiki cha maandiko hasa mstari wa ishirini na nane (28), Paulo anaonyesha wazi kwamba anamwonya kila mtu na anafundisha kwa hekima yote ili kuhakikisha anamleta kila mtu kuwa mtimilifu ndani ya Kristo. Lugha hii ni sawa na kusema; Paulo anafanya yote hayo kuhakikisha anamfanya kila mtu anamfanania Yesu Kristo. Tafsiri nyingine za Biblia kama ile ya Biblia Habari njema kwenye neno mtimilifu inatumia neno KUKOMAA lugha ambayo ni sawa na kusema kumfanania Yesu.
Wakolosai 1:28
‘‘Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo.’’BHN
Kwa nini lengo la Mungu ni kila mwanadamu amfananie Bwana wetu Yesu Kristo? Hii ni kwa sababu Bwana wetu Yesu Kristo ndiye sura/mfano halisi wa Mungu (Wakolosai 1:15; 3:10 na 2 Wakorintho 4:4). Katika kuelezea jambo hilo hilo kwa lugha nyingine, Biblia inasema Yesu ni mng’ao wa utukufu wa Mungu na chapa yake halisi. Zaidi ya hayo, Yesu pekee ndiye anayemfunua Mungu kikamilifu katika mwili (Yohana 1:18). Hivyo, misheni ya Mungu, ambayo inapaswa kuwa lengo la kanisa, ni kumfanya kila mwanadamu amfananie Kristo Yesu, aliye sura halisi ya Mungu. Misheni hii ya Mungu kuwafanya watu wamfananie mwanae Yesu kristo sio jambo lililojitokeza kama mpango wa kando au wa pili wa Mungu. Mungu alikusudia hilo tangu awali kama maandiko yanavyosema “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.” Warumi 8:28-29
NJIA YA KUTIMIZA LENGO
Baada ya kujua nini ni lengo la kanisa, ni muhimu kujua ni kwa njia gani kanisa linaweza kutimiza lengo hili. Kwa kukumbusha, lengo la kanisa ni kumfanya kila mwanadamu amfananie Bwana Yesu Kristo katika mawazo, matendo, nia, fikra, mtazamo na ujumla wote wa maisha yake. Tutajifunza njia za kanisa kutimiza lengo kupitia ujumbe ulioko kwenye barua ya mtume Paulo kwenda kwa Kanisa lililokuwa kule Efeso.
Waefeso 4:1-16
“Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa. Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi? Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote. Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.
Katika kipengele hiki cha maandiko, kuna mambo ya msingi ya kujifunza kuhusu namna gani kanisa linaweza kutimiza lengo lake. Na tutajifunza kwa hatua kama ifuatavyo;
- Mstari wa 13-15, unataja lengo la kanisa kama tulivyojifunza. Paulo anataja lengo hili katika muktadha wa kueleza njia gani itafanya kanisa lifikie hapo. Paulo anataja kwamba tunatakiwa sisi wote kwa pamoja tuufikie umoja wa imani, tufikie kumfahamu sana Mwana wa Mungu, kanisa lifike kuwa mtu mkamilifu, tufikie kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo, tufikie mahali ambapo hatuwezi kubebwa na udanganyifu, tufikie kuishika kweli katika upendo na mwishoe “kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.”
Kwa hiyo, Paulo anasema yale yote aliyoyafundisha katika 4:7-12, Mungu ameyafanya yawe hivyo ili kanisa likue hata limfikie Kristo katika yote. Hicho ndicho tulichojifunza kwenye lengo la kanisa.
- Mstari wa 7-12, Paulo anafundisha jinsi Mungu alivyokusudia kanisa kufikia lengo hili. Paulo anasema kila mmoja wetu (Msisitizo “kila mmoja wetu” sio wachache), alipewa neema au kipawa au zawadi kwa kadiri ya kipimo chake Kristo (7). Paulo anathibitisha utoaji wa vipawa wa Yesu kwa kunukuu maandiko kutoka katika Zaburi ya 68 na kuyafafanua kulingana na anachokisema (8-10). Baada ya hapo, anataja sasa zawadi Yesu alizozitoa, anasema Yesu alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu (11). Haya yametolewa ili watakatifu wakamilishwe, kazi ya huduma itendeke na mwili wa Kristo ujengwe. Swali ni kwamba, kama Kristo ametoa zawadi kwa kila mwamini, je, kila mwamini atakuwa na utume, au unabii au uinjilisti au uchungaji au ualimu tu? Kwa kujaribu kujibu swali hili, wengine wakasema kwamba Kristo amewapa zawadi hizi tano watu wachache ili walisaidie kanisa. Lakini wazo hili ni kinyume na muktadha. Muktadha unasisitiza kwamba kila mmoja wetu alipewa zawadi na kristo na sio wachache. Lakini pia hakuna aliyepewa kulisaidia kanisa ambaye yeye si sehemu ya kanisa. Kwa hiyo, kwa kusoma maeneo mengine ya Biblia ambapo mtume Paulo anataja zawadi/neema/vipawa tunagundua kwamba hapa mtume Paulo hakutaja zawadi zote Kristo alizozitoa kwa waamini. Kwa kuwa hakuna namna angeweza kutaja zawadi zote Yesu alizozitoa kwa kila mwamini. Hivyo, mtume Paulo ametaja baadhi ya zawadi kwa ajili ya kueleweka kile alichokuwa anafundisha, kwamba Kristo ametoa zawadi kwa kila mmoja wetu. Zawadi zingine Mtume Paulo alizitaja kwenye waraka wake kwa Wakorintho (I Wakorintho 12). Hebu msikie kidogo anavyosema “Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.” 1 Wakorintho 12:28. Hakuishia hapo, zawadi zingine alizataja katika waraka wake kwa kanisa la Rumi (Warumi 12:5-8).
Hivyo, kanisa litafikia lengo kwa kila mwamini kutumia zawadi/kipawa/neema Mungu aliyoweka ndani yake. Mungu anataka tumfikie Kristo katika kumfanania, ndio maana ametoa uwezo tofauti tofauti kwa kila mwamini ili kila mmoja akitumia zawadi yake, kanisa lijengwe na kukua na hatimaye kumfikia Kristo katika yote. Hili ndilo jambo mtume Paulo anasisitiza anapomaliza aya hii tunayoisoma, akisema “Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.” Waefeso 4:16
Njia pekee kanisa litafikia lengo ni kwa kila mwamini (Kiungo) kufanya anachotakiwa kufanya sawa sawa na zawadi aliyopewa.Sisi kama Kanisa tusipoweza kuhakikisha kila kiungo kinafanya kazi yake, basi hatutaweza kutimiza lengo. Na kushindwa kutimiza lengo hakutakuwa kwa sababu Mungu hajatupa rasilimali zinazohitajika, bali itakuwa ni kwa sababu hatujataka kutumia rasilimali zote Mungu alizotupa.
- Mstari wa 1-6 ni msingi wa muhimu sana katika mazingira ambayo kila kiungo kinafanya kazi yake. Kabla Paulo hajaanza kufundisha kwamba kila mwamini ana zawadi ambayo Mungu amempa, na ya kwamba inatakiwa kila mwamini afanye anachotakiwa kufanya ili mwili ujengwe, alianza na kufundisha kuhusu umoja. Kama kila mmoja ana uwezo wa kipekee na anatakiwa kuutumia uwezo huo ni rahisi sana kuwa na mvurugano kama katika mazingira hayo hakuna jitihada za kuwa na umoja. Hii ndio maana mtume Paulo alianza na kusisitiza umoja. Kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu,na kwa kuchukuliana katika upendo, Roho wa Mungu anatutaka tujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Neno la msingi katika aya hii ni JITIHADA. Roho wa Mungu analitaka kanisa litumie jitahada kuuhifadhi UMOJA. Ni rahisi sana kwa watu wenye uwezo tofauti tofauti kutofautiana, ndio maana Roho wa Mungu anatutaka kuweka jitihada katika kuuhifadhi umoja. Kwenye Kiswahili kuna msemo unasema “Mafahali wawili hawakai zizi moja” lakini Roho wa Mungu anatuita waamini tuwe mafahali wengi tunaokaa zizi moja. Kila mmoja atumie zawadi yake kama Mungu alivyompatia lakini akumbuke kwamba anahitaji kufanya bidii katika kuuhifadhi umoja.
Hivyo, kwa njia ya kila mmoja kutumia kipawa chake na kwa umoja kanisa litaweza kufikia lengo lake. Hii ndio maana kila mahali mtume Paulo alipozungumzia utofauti wa zawadi/vipawa Mungu alivyotupa waamini, hakuacha kuzungumzia umoja wetu. Kwa Warumi alianza na umoja ndio akaelezea utofauti wetu (Warumi 12:5-8). Kwa Wakorintho (1 Wakorintho 12) ndio zaidi, ametaja umoja kwa kila namna. Pale tunaposikia kanisa limetawanyika, mara nyingi husababishwa na matumizi ya zawadi hizi Mungu alizozitoa kwa waamini. Lakini kila mwamini anatakiwa kujua kwamba inahitajika jitihada katika kuhakikisha sote tunafanya kazi kutokana na zawadi Mungu ametupa na wakati huo huo tunahakikisha tuna uhifadhi umoja wetu kama kanisa.
Mambo haya mawili ni muhimu sana ili kanisa liweze kutimiza lengo lake; Ufanyaji kazi wa kila mwamini na umoja wa waamini. Jambo moja likipungua, kanisa haliwezi kutimiza lengo lake. Changamoto zote tunazoziona ndani ya kanisa zimesababisha na kukosekana kwa jambo moja kati ya haya mawili au kukosekana kwa yote. Unatiwa moyo kuwa sehemu ya walioelewa ujumbe huu kwa kuanza kutumia zawadi Mungu aliyokupa kwa ajili ya kanisa na jitahidi kuuhifadhi umoja wa kanisa kwa unyenyekevu, upole na uvumilivu wakati unatumia zawadi Mungu aliyokupa kwa ajili ya kanisa.

