SEHEMU YA KWANZA
Kanisa lilizaliwa mwaka wa 30 B.K. huko Yerusalemu baada ya Yesu kufa, kufufuka na kupaa mbinguni.[1] Wakati Yesu anapaa kwenda mbinguni, Kanisa lilikuwa na watu wengi tayari, yaani zaidi ya watu mia tano (1 Wakorintho 15:5–6). Baada ya Roho Mtakatifu kuwashukia watu mia moja na ishirini waliokuwa wamekusanyika pamoja Yerusalemu (Matendo 1:15) siku ya Pentekoste, kanisa likazaliwa rasmi. Kutokana na kazi ya Injili, miezi kadhaa tu baada ya Yesu kupaa, Wakristo waliongezeka Yerusalemu na kufikia idadi inayokadiriwa kuwa sawa na elfu kumi (Matendo 2:41; 4:4; 5:14; 6:1). Idadi hii ni asilimia kumi ya wakazi wote wa Yerusalemu, hivyo huu ulikuwa ni ukuaji mkubwa sana kwa muda mfupi.
Pamoja na hayo, ni dhahiri kwamba waamini wakati huu hawakujitambulisha tofauti na Wayahudi. Waamini waliitambua imani yao kama tawi la imani ya Kiyahudi (kama dhehebu kwa lugha ya leo). Hii ndiyo maana hawakuacha kwenda hekaluni kwa ajili ya ibada na mafundisho, pamoja na kupata upinzani mkubwa (Matendo 2:26; 3:1). Pia, waliendelea kwenda kwenye masinagogi na pamoja na kwamba walikusanyika nyumba kwa nyumba (Matendo 5:42).
Kwa muda huu, Kanisa liliongozwa na mitume kumi na wawili, huku Petro akiwa kiongozi wao. Lakini kutokana na waamini kuwa wengi na kutokana na kazi ya mgawanyo wa chakula kuingia dosari, viongozi wengine walichaguliwa. Mmoja wa viongozi hao alikuwa Stefano. Kwa sababu ya ujasiri wake wa kuhubiri Injili, Stefano anakuwa kiongozi wa kwanza kuuawa na Wayahudi waliopinga mafundisho ya imani ya “dhehebu” hili jipya. Kifo cha Stefano kinakadiriwa kutokea mwaka wa 33 BK. Hivyo, toka Yesu apae, miaka mitatu ilipita, Kanisa likiwa halijafanya bidii kubwa ya kwenda nje ya mipaka ya Yerusalemu. Kifo cha Stefano kinasababisha waamini kutawanyika na kwenda nje ya Yerusalemu, isipokuwa mitume (Matendo 8).
Mmoja wa watu walioondoka Yerusalemu ni Filipo. Kama mwenzie Stefano, Filipo alipofika Samaria aliendeleza kazi ya kuhubiri Injili. Wasamaria wakaamini, na mitume Petro na Yohana wakaenda huko kwa ajili ya kuwaombea kupokea Roho Mtakatifu. Filipo, kwa kuongozwa na Roho, pia akamhubiria Towashi kutoka Ethiopia, aliyekuwa mkuu wa hazina chini ya utawala wa malkia Kandake.[2] Towashi akaamini, akabatizwa, na akarudi kwao Ethiopia (Matendo 8).
Mwaka wa 34 BK, wakati akitimiza majukumu yake ya kulitesa Kanisa, Sauli (aitwaye pia Paulo) anakutana na Yesu katika safari yake ya kuelekea Dameski, anaamini na kubatizwa (Matendo 9). Tukio hili lilitokea, Paulo alipokuwa na umri wa takribani miaka 30 (kati ya miaka 28–33). Baada ya hapo, Paulo akaenda kukaa Arabia (Wagalatia 1:17–20). Baada ya miaka mitatu, yaani mwaka 37 BK, Paulo akaenda Yerusalemu kukutana na waamini huko, hasa mitume, na akaonana na Petro, kiongozi kati ya mitume (Matendo 9:26–30 na Wagalatia 1:18–20). Baada ya kukaa Yerusalemu kwa muda mfupi, Paulo akaenda Tarso, mji uliokuwa Kilikia, mji ambao alizaliwa (Matendo 9:30 na Wagalatia 1:21). Wakati Paulo yuko huko, Petro alikuwa anafanya huduma kwenye Pwani ya Bahari ya Mediterania kwa uhuru kwa sababu hakukuwa na mateso tena. Maeneo haya ni kama vile Lida, Yafa, na Kaisaria. Katika huduma hii, ndipo alipofikisha Injili kwa mtu wa mataifa kabisa kwa mara ya kwanza, na hapo ndipo mwanzo wa mgogoro wa kitheolojia ulioendelea kwenye Kanisa kwa muda mrefu. Mgogoro huu ulihusu wamataifa wafanye nini ili waokoke? Wanatakiwa kugeuka na kuwa Wayahudi, au wanaweza kuokoka bila kugeuka na kufuata sheria ya Musa? (Matendo 9–10).
Kutokana na kanisa kutawanyika baada ya kifo cha Stefano Injili ilifika mpaka Antiokia, ya Siria (Kuna Antiokia ya Pisidia). Antiokia ndio mji wa kwanza kuwa na kanisa lenye idadi kubwa ya watu wa mataifa. Kwa nini Antiokia ilikuwa muhimu kwa Kanisa? Antiokia ulikuwa ni mji muhimu sana katika Dola nzima ya kirumi. Mwanahistoria Josephus anasema Antiokia “ni mji mkuu wa Siria, na bila shaka unastahili nafasi ya kuwa mji mkuu wa tatu katika ulimwengu unaokaliwa na watu, ulioko chini ya Dola ya Rumi, kwa ukubwa wake na kwa viashiria vyake vingine vya ustawi.”[3] Josephus anamaanisha kwamba ukitoka mji wa Rumi kwa ukuu, basi unafuata mji wa Aleksandria uliokuwa Misri, na baada ya huo ndio Antiokia wa Siria.
Mwaka wa 40 BK Kanisa la Yerusalemu likamtuma Barnaba kwenda Antiokia kuangalia nini kinaendelea huko. Barnaba alivyoona neema ya Mungu inavyofanya kazi huko akaamua aende kumchukua Paulo Tarso, baada ya hapo akarudi naye Antiokia. Mwaka mzima walikuwa huko wakifundisha pamoja na huko ndiko waamini wakaitwa Wakristo kwa mara ya kwanza (Matendo 11).
Mambo yakiwa yanaendelea hivyo Antiokia, Yerusalemu mwaka wa 43-44 BK mateso yakaanza tena kwa Kanisa chini ya uongozi wa Herode Agrippa wa kwanza (Tazama Jedwali namba 1 hapo chini). Kwa wakati huu, mtume Yakobo, ndugu wa Yohana, akauawa na Petro akawekwa gerezani (Matendo 12). Baada ya kutolewa gerezani na malaika, Petro akaondoka Yerusalemu. Kwa wakati huu, Kanisa lilikuwa linaongozwa na wazee na mitume, na Yakobo, ndugu wa Yesu, anaonekana kuwa kiongozi wa kundi hili kwa sasa kama mbadala wa Petro.
| Mtawala | Uhusiano na Herode Mkuu | Eneo Alilotawala | Muda wa Utawala | Matukio yake katika Agano Jipya |
| Herode Mkuu | Mwanzilishi | Israeli yote (Uyahudi wote) | 37–4 KK | Muuaji wa watoto wachanga wakati wa kuzaliwa kwa Yesu (Mathayo 2:1-20). Baada ya kifo chake, ufalme wake uligawanywa kwa watoto wake watatu. |
| Herode Arkelao | Mtoto | Yudea, Samaria na Idumea | 4 KK–6 BK | Yusufu alimwogopa, ndiyo sababu familia ilienda Galilaya (Nazareti) baada ya kutoka Misri badala ya kurudi Bethlehemu (Mathayo 2:21-23). Baada ya yeye kutolewa katika utawala kutokana na ukatili wake, Dola ya Rumi ikamuweka Pontio Pilato kama mbadala wake. |
| Herode Antipa | Mtoto | Mikoa ya Galilaya na Perea | 4 KK–39 BK | Anatajwa sana katika huduma ya Yesu; Yeye ndiye aliyemwua Yohana Mbatizaji (Mathayo 14:1-12) na ndiye Herode ambaye Pontio Pilato alimpelekea Yesu kwake wakati wa hukumu (Luka 23:1-12). |
| Filipo Tetrarki | Mtoto | Iturea na Trakoniti. | 4 KK–34 BK | Anatajwa katika Luka kama mfalme pamoja na Antipa (Luka 3:1). Mke wake wa kwanza alikuwa ni Herodia; ambaye baadaye ndugu yake Antipa akamuoa na hivyo kusababisha Yohana kumkemea (Mathayo 14:3). |
| Herode Agripa I | Mjukuu | Uyahudi, Galilaya na Perea. | 37–44 BK | Yeye ndiye aliyelitesa kanisa, na hata kumuua mtume Yakobo, na kumfunga Mtume Petro gerezani. Alikufa ghafla kama hukumu ya Mungu (Matendo 12). |
| Herode Agripa II | Kitukuu (Mtoto wa Agripa I) | Kalkisi na maeneo mengine | 48–takribani 100 BK | Mtawala wa mwisho wa ukoo huu; Huyu ndiye alimtembelea Liwali Festo akiwa na dada yake Bernike, na Paulo akajitetea mbele yake (Matendo 25-26). Aliunga mkono Rumi wakati wa vita na Wayahudi na alikufa bila watoto. |
Jedwali namba 1. Ukoo wa Herode na nafasi yao katika huduma na maisha ya Yesu na Kanisa.
Mwaka wa 44 BK, nabii aitwaye Agabo akiwa Antiokia alitabiri ujio wa njaa katika Yudea, na miaka miwili baadaye njaa ikaikumba Yudea. Njaa hii ilidumu kwa muda wa miaka miwili. Wanahistoria kama Josephus, Suetonius, na Tacitus wanasimulia pia kuhusu njaa hii. Josephus yeye anasema “Sasa kuja kwake kulikuwa na faida kubwa sana kwa watu wa Yerusalemu. Kwa kuwa wakati huo kulikuwa na njaa kali iliyokuwa ikiwasumbua, na watu wengi walikufa kwa kukosa mahitaji ya kupata chakula; Malkia Helena alituma baadhi ya watumishi wake kwenda Alexandria na fedha ili kununua kiasi kikubwa cha nafaka, na wengine aliwatuma kwenda Kipro kuleta mzigo wa tini kavu.” [4]
Kutokana na njaa hii, Kanisa la Antiokia lilitoa fedha kwa ajili ya kuwasaidia waamini wenzao na likawatuma Paulo na Barnaba kupeleka sadaka zao. Baada ya kuwasilisha matoleo hayo, Barnaba na Paulo wakarudi Antiokia wakiwa na Marko (Matendo 11:27-30; 12:24-25). Hii ilikuwa ni mara ya pili, Paulo kwenda Yerusalemu kwa mujibu wa historia iliyoandikwa na Luka.
Mwaka wa 48-49 BK, Barnaba na Paulo wakiwa na Marko (ambaye pia aliitwa Yohana) walianza safari ya kimisheni. Safari hii kwa umaarufu inatambulika kama safari ya kwanza ya kimisheni ya Mtume Paulo. Safari hii ilianza takribani miaka zaidi ya kumi toka Paulo alipoamini. Katika safari yao hii ya kimisheni, Mtume Paulo pamoja na Barnaba walitoka Antiokia ya Siria, kisha wakashuka hadi bandari ya Seleukia. Kutoka hapo, walielekea kwenye kisiwa cha Kipro, wakihubiri kwanza katika mji wa Salami na baadaye katika mji wa Pafo. Kutoka kwenye kisiwa cha Kipro, walielekea bara na kufika Perga katika eneo la Pamfilia, ambapo Yohana Marko akawacha na akarudi Yerusalemu. Paulo na Barnaba wakaendelea hadi Antiokia ya Pisidia, kisha wakaenda Ikonio, Listra, na Derbe (Miji hii yote ilikuwa ndani ya jimbo la kiutawala la Galatia). Baada ya Derbe, walianza kurudi Antiokia ya Siria, lakini walirudi kwa kuyarudia maeneo waliyoyapitia wakati wa kupanda makanisa. Walirudi kupitia miji ya Listra, Ikonio, na Antiokia ya Pisidia, wakiwatia moyo waamini na kuwaweka wazee katika makanisa ya maeneo hayo yote. Kutoka hapo walirudi Perga, wakateremka hadi bandari ya Atalia, na hatimaye wakasafiri kwa meli kurudi Antiokia ya Siria. Walipofika Antiokia wakatoa habari ya yale Mungu amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa (Matendo 13 na 14). Kumbuka: Kuna Antiokia ya Pisidia na Antiokia ya Siria; Antiokia ya Pisidia ilikuwa ni mji ndani ya jimbo la Galatia na Antiokia ya Siria ndiko lilikuwepo kanisa lililomtuma Paulo na Barnaba kwenye kazi ya umisheni (Tazama ramani namba 1 hapo chini).

Ramani 1. Safari ya kwanza ya kimisheni ya mtume Paulo
Katika kipindi hiki cha kukaa Antiokia, Mtume Paulo alipata habari kwamba kuna watu wanawafundisha waamini wa eneo la Galatia kwamba wasipofuata sheria ya Musa, hasa kwenye mambo kama tohara na kuadhimisha sikukuu, hawawezi kuokoka. Baada ya taarifa hizo, Mtume Paulo akaandika waraka wake kwa WAGALATIA kwa ajili ya kupinga fundisho hilo. Mbali na kupinga fundisho hilo, Paulo aliandika pia waraka huu kwa ajili ya kutetea utume wake ambao ulishambuliwa na wapinzani wa Injili yake. Zaidi, mtume Paulo aliandika waraka huu kuwahakikishia wokovu waamini wa Galatia; kwamba wao ni sehemu ya watu wa Mungu bila ya kubadilika na kuwa wayahudi.
Kupitia waamini walioamini siku ya Pentekoste, katika mwaka wa 49 BK Injili ilikuwa imeshafika Rumi, mji mkuu wa dola. Kama ilivyokuwa Yerusalemu na maeneo mengine, waamini walioishi Rumi walikuwa bado ni sehemu ya imani ya Kiyahudi. Tena, kama ambavyo Wayahudi walivyokuwa wanabishana na mitume kule Yerusalemu na hata kwenye miji ambayo Paulo na Barnaba walipita, ndivyo hivyo hivyo kulikuwa na mabishano kati ya Wayahudi wa imani ya Kiyahudi ya asili na Wayahudi wanaomwamini Yesu kama Kristo. Kutokana na mabishano haya kuwa makubwa, taarifa zikamfika Kaisari Claudio. Kwa kuwa dola ya Rumi ilikuwa inatunza sana amani, Kaisari Claudio akawafukuza Wayahudi wote kutoka kwenye mji wa Rumi mwaka huu wa 49 BK ili kuepusha kutokea kwa machafuko ya aina yeyote. Katika Wayahudi waliofukuzwa Rumi walikuwemo Akila na Prisila, ambao baada ya kufukuzwa wakaenda kuishi Korintho (Matendo 18:2). Kufukuzwa huku kwa wayahudi kunaelezwa na mwanahistoria Suetonius. Suetonius anasema “Kwa kuwa Wayahudi walikuwa wakisababisha fujo mara kwa mara kwa kuchochewa na Chrestus, yeye [Kaisari Klaudio] aliwafukuza kutoka Roma.”[5] Wanahistoria na wasomi wengi wanakubali kwamba jina “Chrestus” lililoandikwa na mwanahistoria Suetonius ni sawa na cheo “Christus” (yaani, Kristo), hivyo Seutonius alikuwa anamuelezea Kristo ambaye alikuwa ndiye mada ya mabishano ya wayahudi.
Wakati hayo yakiwa yanaendelea Rumi, Antiokia wakaja watu kutoka Uyahudi (Yerusalemu) na wakaanza kufundisha kwamba “Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka” (Matendo 15:1). Kutokana na mafundisho hayo, Paulo na Barnaba wakashindana nao lakini hawakuweza kufikia muafaka. Kutokana na hilo, kanisa likawatuma Paulo na Barnaba kwenda Yerusalemu ili kupata suluhisho. Kikao cha kanisa kule Yerusalemu kikaamua kwamba watu wa mataifa hawaitajiki kufuata sheria za kiyahudi ili wapate wokovu. Maamuzi haya ya kanisa yaliandikiwa barua kwa ajili ya kusambazwa kwenye makanisa mengine, zaidi ya kanisa la Antiokia. Kanisa la Yerusalemu likawatuma Yuda na Sila kuwasindikiza Paulo na Barnaba ili kufikisha majibu ya kikao katika kanisa la Antiokia (Matendo 15). Baada ya kukaa huko kwa muda, Paulo akaanza safari yake ya pili ya kimisheni, lakini akiwa na Sila na sio Barnaba tena.
Mwaka wa 50 BK ndio wakati ambao Paulo alianza safari hii ya kimisheni. Kutoka Antiokia wakasafiri kwenda kwenda Derbe huku. Walipofika Derbe wakaenda Listra, ambako Paulo akamchukua Timotheo kuwa miongoni wa watu wa timu hii ya Kimishenari (Matendo 16:1-5). Baada ya hapo, walipitia Frigia na Galatia lakini wakazuiliwa na Roho Mtakatifu kuhubiri Asia, hivyo wakapitia Misia na kufika Troa. Huko, Troa daktari Luka akaungana na timu hii katika kazi hii ya kimisheni. Hapo Troa Paulo alipata maono ya mtu wa Makedonia akimwomba avuke kwenda kuwasaidia; Timu ikasafiri kutoka Troa kuelekea Makedonia kwa kupita Samothrake wakafika Neapoli (bandari iliyokuwa karibu na mji wa Filipi). Makedonia (Ulaya ya sasa) ilikuwa ni jimbo ambalo ndani yake kulikuwa na miji ya Filipi, Beroya, Thesalonike na mingine. Hivyo, walipofika jimbo la Makedonia, walianza kazi yao ya injili katika mji wa Filipi. Kwa kuwa katika mji huu hakukuwa na sinagogi la Wayahudi, walienda kando ya mto, ambako walijua kungekuwa na eneo la kukusanyika Wayahudi. Walipofika eneo hilo, Injili ikahubiriwa hapo na kanisa likazaliwa. Baada ya mateso, kufungwa gerezani na kufunguliwa, Paulo na Sila wakasafiri kutoka Filipi mpaka Thesalonike (Timotheo alikuwepo kwenye msafara japo hakuwepo gerezani). Luka hakufika Thesalonike kama anavyotuambia, “Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi” (Matendo 17:1). Hapo Thesalonike, walihubiri Injili (kuhojiana nao kutoka kwenye maandiko) kwenye sinagogi la Wayahudi kwa zaidi ya Jumamosi tatu na baadhi ya Wayahudi, wamataifa waliomcha Mungu kwa dini ya Kiyahudi na wanawake wenye vyeo wakaamini. Pamoja na watu kuamini, kulitokea upinzani mkali juu ya timu ya kimisheni kutoka kwa wayahudi, na hivyo wakasafiri na kwenda Beroya.
Wayahudi wa Beroya walikuwa waungwana, walijifunza na wengine wakaamini, lakini Wayahudi wa Thesalonike waliposikia habari hizo wakaifuata timu ya kimisheni huko Beroya na wakafanyia ghasia huko pia, kiasi cha kusababisha Paulo kuondoka Beroya kwenda mpaka Athene (Matendo 17:11-14). Timotheo na Sila wakabaki Beroya, lakini wale waliomsindikiza Paulo mpaka Athene walipokuwa wanarudi, Paulo akawaagiza kuwaambia Sila na Timotheo kwamba wasikawie wamfuate Athene. Baada ya muda mfupi, Timotheo na Sila walifika Athene wakaonana na Paulo kwa muda mfupi (1 Wathesalonike 3:1-5). Kutoka Athene Paulo alimtuma Timotheo kurudi Thesalonike, Sila kurudi Filipi kwa ajili ya kuwaimarisha waamini huko.
Kutoka Athene Paulo akasafiri peke yake kuelekea mji wa Korintho. Huko Korintho akakutana na Akila na Prisila, ambao walikuwa hapo kwa miezi kadhaa toka walipofukuzwa Rumi. Wakakaa na wakafanya kazi pamoja huku mtume Paulo akiendelea kuhubiri injili katika sinagogi kila sabato. Timotheo na Sila walipofika Korintho walirudi na matoleo kutoka kwenye makanisa waliyokuwa (2 Wakorintho 11:8-9; Wafilipi 4:14-16), hivyo Paulo akaacha kazi ya mikono na akageukia kuhubiri injili tu (Matendo 18:5). Baada ya Wayahudi kukataa injili, Paulo akaacha kwenda kwenye sinagogi akaamua kuhubiria kwenye nyumba ya Tito Yusto, mmataifa aliyekuwa na imani ya Kiyahudi. Nyumba ya Tito ilikuwa karibu kabisa na sinagogi ambalo Injili ya Paulo ilikataliwa (Matendo 18:1-7). Baada ya mkuu wa sinagogi aitwaye Krispo na nyumba yake yote kuamini, Wakoritho wengi wakaamini, wakabatizwa na kanisa likazaliwa (Matendo 18:8 na 1 Wakorintho 1:14-16). Hii ilikuwa ni kati ya mwaka 50-51 BK.
Pamoja na upinzani mkubwa, Paulo na timu ya kimisheni walikaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu katika kulielea kanisa. Uamuzi huu ulifikiwa baada ya Paulo kuambiwa na Bwana aendelee kukaa huko kwa kuwa yeye Bwana ana watu wengi katika mji huo. Katika wakati huu wa kukaa Korintho, Mtume Paulo, Timotheo na Sila waliandika WARAKA WA KWANZA KWA WATHESALONIKE, ambao ulikuwa unaeleza shukrani zao kwa Mungu kwa ajili ya ukuaji wa Kanisa la Thessalonike katika imani, upendo, na tumaini, pamoja na kuwepo kwa mateso kutoka kwa Wayahudi. Taarifa hizi za ukuaji wa Kanisa walizipata baada ya Timotheo kuleta habari pale alipokuwa ametoka huko. Baada ya muda mfupi toka waraka wa kwanza umeandikwa, Paulo akaandika WARAKA WAKE WA PILI KWA WATHESALONIKE kwa ajili ya kurekebisha fundisho la uongo lililofundishwa ndani ya kanisa. Fundisho hili lilikuwa linasema kwamba siku ya kurudi Bwana imeshapita. Na kuna uwezekano mkubwa waalimu hawa wa uongo waliandika barua kwa jina la Paulo katika kufundisha jambo hilo, ndio maana Paulo anawaambia Wathesalonike kwamba “msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.” (2 Wathesalonike 2:2)
Kutoka Korintho, timu ikaelekea Kenkrea, na kisha wakasafiri baharini hadi Efeso. Efeso, Paulo akakaa kwa muda mfupi na mwishoe akaondoka kwenda Yerusalemu akipitia Kaisaria huku akiwaacha Prisila na Akila huko Efeso. Kutoka Yerusalemu Paulo akarudi Antiokia ya Siria, alipoanzia safari, akiitimiza safari yake ya pili ya kimisheni (Matendo 18:18-22).

Ramani 2. Safari ya pili ya kimisheni ya mtume Paulo.
Katika mwaka huu wa 52 BK inaaminika kwamba Mtume Tomaso alisafiri kutoka Yerusalemu na kwenda India. Huko India alifanya kazi ya injili na akapanda makanisa katika maeneo saba katika jimbo la sasa la Kerala.
Mwaka wa 53–54 BK, Mtume Paulo akaanza safari yake ya tatu ya kimisheni akitoka Antiokia ya Siria na kuelekea kwenye maeneo ambayo alipita kwenye safari zake za nyuma (Matendo 19:23). Akiwa pamoja na Tito wakaanza safari na kufika Galatia[6]. Hapo Galatia kazi ilikuwa ni kuwaimarisha waamini na kutoa maagizo ya kukusanya fedha kwa ajili kupeleka Yerusalemu ambako kulikuwa na watakatifu wenye umaskini (1 wakorintho 16:1-3). Katika kazi ya Galatia Paulo na Tito wakamchukua Gayo kutoka Derbe (Matendo 20:4) na kusafiri pamoja naye mpaka Frigia, huko nako lengo likiwa ni kuwaimarisha waamini katika imani na kuagiza kwamba matoleo yatolewe kwa ajili ya watakatifu wa Yerusalemu.
Kabla Paulo (na timu) hajafika Efeso kutoka Frigia, Apolo, mzaliwa wa mji wa Iskanderia (mji uliokuwa Misri), alifika huko kwa ajili ya kufanya kazi ya injili. Apolo alikuwa hodari wa kuzungumza vizuri na mwenye ufahamu mkubwa wa maandiko. Zaidi ya hayo, alikuwa na msukumo mkubwa wa kumhubiri Kristo. Hii ndiyo maana alipofika tu Efeso, alikwenda kwenye sinagogi na akaanza kumhubiri Yesu. Pamoja na sifa hizo nzuri, Apolo alijua kuhusu ubatizo wa Yohana tu. Hivyo, Priscila na Akila waliokuwepo Efeso tangu walipoachana na Mtume Paulo katika safari yake ya pili, wakamfundisha injili kwa usahihi zaidi. “Injili kwa usahihi zaidi” hapa ina maana kwamba walimweleza kuhusu ubatizo wa Kristo. Baada ya masahihisho haya, Apolo, Priscila na Akila waliendelea kufanya kazi yao ya huduma hapa Efeso. Katika muda huu, inawezakana kuna waamini walitoka Korintho kwa lengo la kuwasalimia Priscila na Akila, na walipofika wakakutana na Apolo na wakavutiwa na uongeaji wake mahiri na hivyo wakamkaribisha Korintho.
Kwa sababu ya sifa nzuri za Apolo, waamini wa Efeso, wakiwepo Priscila na Akila wakamwandikia barua ya kumthibitisha ili aweze kupokelewa huko Akaya (Kanisa la Korintho). Kutokana na uhodari wake wa kujua maandiko na usomi wake, Apolo alipofika Korintho aliweza kuwashinda Wayahudi kwa kuwaonyesha katika maandiko kwamba Yesu ndiye Masihi aliyetabiriwa na maandiko. Huko Korintho, Apolo akapata sifa kubwa ya umahiri wake wa kuwasilisha injili na hivyo kusababisha kuwepo kwa watu waliojitambulisha naye (1 Wakorintho 3:4).
Wakati Apolo akiwa Korintho, Mtume Paulo (pamoja na Tito na Gayo) alifika Efeso. Huko Efeso alikutana na wanafunzi ambao hawakuwa wamepokea Roho Mtakatifu wala kumsikia, lakini walikuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana. Baada ya watu hao kuamini, wakabatizwa na wakajazwa Roho Mtakatifu, na wakaanza kunena kwa lugha mpya na kutabiri. Huko Efeso, kama kawaida yake, Paulo alianza kuhubiri kwenye sinagogi. Baada ya “njia ile” kutukanwa, yeye pamoja na wale walioamini wakajitenga na sinagogi. Kutoka kwenye sinagogi, wakaanza kukusanyika katika ukumbi wa mwanafalsafa aitwaye Tirano. Kupitia Injili iliyohubiriwa kutoka kwenye kusanyiko hilo, kwa muda wa zaidi ya miaka miwili, Mungu akafanya miujiza mikubwa kwa mikono ya Paulo, na watu wengi wakaacha uchawi wao na kusalimisha vitu vyao vya kichawi (Matendo 19:1–20).
Kipindi hiki cha huduma katika mji wa Efeso ndio kipindi ambacho mtume aliandika barua kwa kanisa la Korintho iitwayo WARAKA WA KWANZA KWA WAKORINTHO (Kwa mujibu wa 1 Wakorintho 5:9-10, hii haikuwa barua yake ya kwanza kabisa). Barua hiyo aliandika kushughulika na matatizo mbalimbali katika kanisa hilo, ikiwemo swala la mgawanyiko kutokana na mapenzi kwa watumishi waliowahudumia. Pamoja na barua hiyo, hali ya Kanisa la Korintho haikurekebika bali ilikuwa mbaya zaidi. Kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya mtume Paulo akasafiri mpaka Korintho kwa muda mfupi; safari hii inafahamika kama safari ya huzuni ( 2 Wakorintho 2:1; 12:14; 13:1). Kuna viashiria kwamba safari hii haikuzaa matunda na hivyo Paulo akaamua kurudi Efeso kuendelea na huduma yake. Pamoja na safari hii kutokusababisha kanisa kurejea katika toba, Paulo akaandika waraka mwingine kwenda kwa Wakorintho, waraka ambao hatuna kwenye Biblia zetu lakini unaitwa waraka wa Huzuni (2 Wakorintho 2:3–4 na 7:8–12). Katika huduma hii ya Efeso, Paulo hakuwa tu na Tito na Gayo bali na watu wengine wengi, akiwemo Timotheo, Aristarko na Erasto (Matendo 19:22,29). Na kazi ya kupeleka waraka huu wa huzuni iliwekwa kwa Tito.
Baada ya utumishi wa takribani miaka mitatu Efeso, Paulo akapanga kuondoka na hivyo akawatuma Timotheo na Erasto kwenda Makedonia huku yeye akipanga kuwafuata (Matendo 19:22). Kabla ya kuondoka Efeso Paulo akakumbana na ghasia zilizosababishwa na mmoja wa mafundi wa kutengeneza sanamu za mungu mke aitwaye Artemi (au Diana) kwa kutumia madini fedha, fundi huyo aliitwa Demetrio. Mji wa Efeso ulikuwa ni mji maarufu sana katika himaya ya Rumi, ukiwa kituo kikuu cha biashara, dini, na utamaduni. Ndani ya Efeso ndimo palipokuwako na hekalu kubwa la mungu mke Artemi (au Diana). Kutokana na hilo, watu wengi kutoka sehemu mbalimbali walifika Efeso kwa ajili ya ibada ya Artemi, na hivyo biashara ya kutengeneza sanamu za mungu mke Artemi na vitu vingine vya kiibada ilikuwa ikileta faida kubwa kwa mafundi kama Demetrio. Kwa hiyo, Demetrio alipogundua kwamba mahubiri ya Paulo dhidi ya ibada ya sanamu yalikuwa yakiathiri biashara yao, aliwakusanya wafanyakazi wenzake na kuanza kuchochea ghasia. Watu hawa walikuwa wanadai kwamba Paulo anapotosha watu kwa kufundisha kwamba miungu inayotengenezwa kwa mikono si miungu kamili (Matendo 19:26). Watu wengi wa mji wakachukizwa, wakapiga kelele wakisema, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!”
Ghasia hizo zilienea haraka katika jiji lote, watu wakamiminika katika ukumbi wa michezo wa Efeso, na kukawa na vurugu kubwa. Watu wawili katika timu ya injili ambao ni Gayo na Aristarko walikamatwa na kupelekwa mbele ya umati. Paulo alitaka kuingia kuzungumza nao, lakini waamini , pamoja na maafisa wa mji (waliokuwa marafiki wa Paulo), walimzuia kwa hofu kwamba angeweza kuuawa.
Mwishowe, katibu wa mji aliwatuliza watu akisema kwamba ikiwa Demetrio ana malalamiko, kuna njia za kisheria za kuyawasilisha. Baada ya hayo, ghasia zikapoa, na Paulo akaamua kukutana na waamini sehemu nyingine (sio katika ukumbi waliokuwa wanakutana) na kuwaaga kisha kuondoka Efeso kuelekea Makedonia, akipitia Troa (Matendo 20:1). Huko Troa Paulo akapata nafasi ya kuhubiri injili, akahubiri lakini hakuwa na furaha sana kwa kuwa bado alikuwa hajapata majibu ya nini ulikuwa mwitikio wa wakorintho baada ya kuwatumia barua ya huzuni kupitia Tito. Hivyo, alikuwa anamsubiri Tito kwa hamu ili ajue nini kimetokea baada ya wakorintho kupokea waraka huu wa huzuni (2 Wakorintho 2:12-13).
Hata hivyo, alipogundua kuwa kurejea kwa Tito kulichelewa, akaamua kuondoka Troa na kuendelea hadi Makedonia kumtafuta Tito. Akiwa makedonia Paulo, alisafiri katika miji mbalimbali ya Makedonia (kama Filipi, Thessalonike, Berea na mingine) akitembelea makanisa na rafiki zake, akiwaimarisha na kuwahimiza waamini katika imani yao bila kusahau kazi yake ya kukusanya fedha kwa ajili ya waamini maskini wa Yerusalemu; Katika hili alitumia Wakorintho kama mfano mzuri kwa jinsi walivyokuwa tayari kutoa toka mwaka uliopita (2 Wakorintho 9:1-4) na matokeo yake wamakedonia wakatoa mpaka wakawa mfano mzuri kwa wakorintho (2 Wakorintho 8:1-6).
Baadaye, akiwa bado Makedonia, Tito akarudi kutoka Korintho na kukutana na Paulo, ambapo akamletea habari njema kwamba wengi katika kanisa la Korintho walikuwa wametubu baada ya kupokea barua ya huzuni (2 Wakorintho 2:5–11; 7:5–16). Habari hizo zilimletea Paulo furaha na faraja kubwa sana baada ya kuwa na wasi wasi kwa muda wote wa kumsubiri Tito.
Hata hivyo, Tito pia alimweleza kuwa bado kulikuwa na kundi la watu lililompinga yeye, wakiwa wameathiriwa na watu waliotia shaka mamlaka na uhalali wa utume wake. Ili kujibu changamoto hiyo, Paulo akaandika barua nyingine, akiwakemea wapinzani wake na kulithibitishia tena kanisa utume wake. Barua hiyo ndiyo tunayoijua kama WARAKA WA PILI KWA WAKORINTHO. Huu ulikuwa mwaka wa 56 BK na Paulo kwa wakati huu anakadiriwa kuwa na umri wa miaka hamsini (kati ya miaka arobaini na sita hadi hamsini na moja). Hivyo, huu ulikuwa ni wakati wa zaidi ya miaka ishirini toka mtume Paulo alipoamini.
Baada ya kuandika barua hiyo akiwa Makedonia (kuna uwezekano mkubwa akiwa Filipi), Paulo akaamua kwenda Korintho kwa mara ya tatu (Matendo 20:2). Safari hii akakaa hapo kwa muda wa miezi mitatu na katika muda huu ndio akaandika waraka wake kwa WARUMI. Baada ya miezi mitatu kuisha Paulo akadhimilia kwenda Shamu kwa kutumia bahari kutoka hapo Korintho. Lakini kwa sababu ya changamoto zilizosababishwa na wayahudi akaghairi kutumia njia ya baharini badala yake akatumia njia ya ardhini na hivyo akalazimika kupitia Makedonia tena (Matendo 20:3). Paulo alipofika Makedonia, katika mji wa Filipi akaonana na Luka tena (Kumbuka Luka aliachana na Paulo hapa Filipi kwenye safari yake ya pili, Matendo 16:10-17). Kutoka Filipi (iliyopo ndani ya jimbo la Makedonia), Paulo, Luka na watu wengine wachache wakasafiri mpaka Troa, ambako waliungana na watenda kazi wengine kama Sopatro Mberoya, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia (Matendo 20:4). Hii ilikuwa baada ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu. Baada ya kufika Troa Paulo alikuwa amedhamilia kufika Yerusalemu kabla ya sikukuu ya Pentekoste, ili kufikisha matoleo aliyoyakusanya kutoka katika makanisa mbalimbali, hivyo alikuwa na muda mchache sana kwenye vituo alivyopitia akiwa njiani.
Hapa Troa, Paulo na timu nzima ya injili wakakaa kwa muda wa wiki moja. Katika kukaa kwa siku hizo ndani ya Troa, Siku ya Bwana au siku ya kwanza ya juma waamini wakakutana pamoja. Katika kusanyiko hilo Paulo akafundisha kwa muda mrefu hadi usiku wa manane (Matendo 20:7-8). Kijana mmoja aitwaye Eutiko alikuwa akisikiliza mahubiri, lakini akapatwa na usingizi na hatimaye kuanguka dirishani kutoka kwenye ghorofa ya tatu hadi chini. Walipomkuta alikuwa amekufa, lakini Mungu akamrejeshea uhai kwa mkono wa Paulo (Matendo 20:6-10). Baada ya hapo Paulo alishiriki Meza ya Bwana na akaendelea kufundisha hadi kulipokucha (Matendo 20:10-12). Baada ya hapo, Paulo akawaambia wenzake wapite baharini kwenda katika mji wa Aso huku yeye akaamua kupitia ardhini. Wenzake walipofika Aso, wakamsubiri mpaka alipowafikia. Baada ya kukutana na wenzake huko Aso, wakaendelea na safari yao ya kuelekea Yerusalemu. Walifanya mapumziko mafupi huko Mitilene, wakapita Kio, wakavuka hadi kisiwa cha Samos, na hatimaye wakafika Mileto (Matendo 20:14-15).
Akiwa Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso kuwaita wazee wa kanisa, ili azungumze nao. Yeye alighairi kupita Efeso kwa kuwa alijua akienda huko atatumia muda mrefu na hivyo angeshindwa kufika Yerusalemu kabla ya Pentekoste. Paulo alipoonana na wazee wa kanisa la Efeso akawaonya kwamba “mbwa mwitu” watatokea kutoka ndani na nje ya kanisa. Mbwa mwitu hao wataleta mafundisho potovu kwa nia ya kuwavuta wanafunzi wawafuate wao wenyewe. Katika maonyo hayo , Paulo aliwatia moyo wazee hao walilishe na kulilinda kundi la Mungu, na wafanye kazi kwa mikono yao wenyewe—kwa kuwa ni heri kutoa kuliko kupokea, kama Yesu alivyofundisha. Katika kumaliza hotuba yake mtume Paulo akawaambia wazee kwamba hawatamwona tena uso wake, taarifa ambayo ilikuwa ni ya huzuni sana kwa wazee wa kanisa la Efeso. Kisha akapiga magoti na kuomba pamoja nao, nao wote wakalia kwa uchungu huku wakimkumbatia na kumbusu, kisha wakamsindikiza kupanda meli kwa ajili ya kuendelea na safari (Matendo 20:16-38).
Kutoka Melito, mtume Paulo pamoja na wenzake wakasafiri kwa meli kuelekea Siria. Wakapita Kosi, Rodo na Patara, na kutua katika mji wa Tiro (Matendo 21:1-3). Paulo na wenzake walikaa siku saba pamoja na waamini hapo Tiro. Kupitia “Roho Mtakatifu,” waamini hao wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu, lakini Paulo aliamini bila shaka kwamba Yerusalemu ndilo mahali sahihi pa kwenda kwa wakati huu. Baada ya hapo, Paulo na wenzake wakasafiri mpaka Tolemai, ambako walikaa siku moja pamoja na waamini walioko huko, kisha wakaelekea Kaisaria. Walipowasili Kaisaria, walikaribishwa na waamini wa huko na wakakaa nyumbani kwa Filipo, mwinjilisti. Walipokuwa huko, nabii mmoja aitwaye Agabo alishuka kutoka Yudea na kumtabiria Paulo mateso yaliyokuwa yakimsubiri huko Yerusalemu. Licha ya watu wengi kumshauri tena kwamba asiende Yerusalemu, Paulo hakugeuza mawazo yake na akawaambia kuwa anajua mambo yanayomngojea, na kwamba alikuwa tayari hata kufa kwa ajili ya jina la Bwana Yesu (Matendo 21:4-14). Kutoka Kaisaria, Paulo na timu nzima wakasafiri mpaka kufika Yerusalemu na hapo ndipo safari ya tatu ya kimisheni ikafikia tamati. Safari hii ilifikia tamati mwaka wa 57 BK mwezi wa tano au sita mwanzoni (Matendo 21:15-17).

Ramani 3. Ramani ya safari ya tatu ya kimisheni ya mtume Paulo. Chanzo cha ramani ni biblemapper.com
Paulo na timu ya injili, baada ya kufika Yerusalemu, siku ya pili yake wakawa na kikao na Yakobo pamoja na wazee wengine wote wa Kanisa. Katika kikao hicho, Paulo aliwashuhudia yale Mungu aliyoyafanya katika kazi yake nje ya Israeli, yaani kwa mataifa. Yakobo na wazee wengine wakamtukuza Mungu, na pia wakamweleza Paulo jinsi ambavyo Kanisa, ambalo kwa sehemu kubwa lilikuwa limejawa na Wayahudi, lilivyokuwa limepewa taarifa kwamba yeye anawafundisha Wayahudi walioko nje ya Israeli kutokufuata sheria ya Musa. Hivyo, kwa wakati huo, yeye alionekana kuwa adui wa Wayahudi, walioamini na wasioamini.
Yakobo na wazee wengine wakamwomba Paulo afanye ibada ya utakaso pamoja na waamini wengine wanne, ili Wayahudi wajue kwamba yeye bado anafuata sheria ya Musa. Katika kutimiza hilo ndani ya siku saba, siku moja Wayahudi walipomuona hekaluni, wakaanza kumshtaki kwa kuasi Mungu wa kweli wa Israeli, kwa kunena mabaya juu ya sheria ya Musa, na kwa kuwahimiza watu wasitii sheria za Kiyahudi. Mvutano huo ulisababisha ghasia hekaluni, na Paulo akatolewa nje ya hekalu na umati wa watu wenye hasira kali. Askari wa Kirumi wakaingilia kati na kumtia Paulo kizuizini (Matendo 21:27–36).
Baadaye, Paulo akapewa nafasi ya kulihutubia lile kundi la watu, lakini hotuba yake ikaibua ghasia nyingine tena. Warumi wakamchukua Paulo hadi kambini mwao. Walitaka kumpiga mijeledi, lakini Paulo akaweka wazi hadhi yake ya uraia wa Kirumi, na hivyo wakashindwa kumpiga mijeledi kwa sababu ya uraia wake (Matendo 21:37–22:29).
Kesho yake, askari wa Kirumi wakamleta Paulo mbele ya baraza la Kiyahudi ili wajue ni kwa nini ghasia ziliibuka kwa ajili yake hekaluni. Paulo akiwa mbele ya baraza akagundua kwamba baraza hilo lilikuwa na mchanganyiko wa Mafarisayo na Masadukayo, akaeleza kwamba yeye ni Farisayo na kwamba anachukiwa na kuhukumiwa na Wayahudi kwa sababu ya tumaini lake kuhusu ufufuo wa wafu. Kwa kuwa hili lilikuwa ni jambo la kiimani linalowatofautisha Mafarisayo na Masadukayo, mabishano yakatokea, huku Mafarisayo wakisema hawaoni jambo baya alilotenda. Mkutano huo ukaharibika, na Paulo akachukuliwa na askari wa Kirumi ili asije akazuliwa.
Baada ya hapo wahayudi wakapanga mpango wa kuumua Paulo, lakini baada ya mpango huo kujulikana kwa kamanda Klaudio Lisia, Kamanda akampeleka Paulo Kaisaria kwa liwali/gavana Feliki. Paulo alipelekwa Kaisaria, Maritima kwa kuwa huko ndiko kulikuwa ndio makao makuu ya jimbo la kirumi la Yudea. Paulo akapokelewa huko Kaisaria kwa barua kutoka kwa kamanda wa askari na akawekwa katika ulinzi kusubiri wanaomshitaki kufika. Siku tano baadaye, kesi ya Paulo ikaanza rasmi wakati Anania, kuhani mkuu, pamoja na baadhi ya wazee wa Kiyahudi walipowasili Kaisaria kutoka Yerusalemu. Kundi hilo likamleta msemaji aitwaye Tertulo ili kumshtaki Paulo mbele ya Feliki. Tertulo alipoanza mashtaka yake, alianza kwa kumsifia Liwali Feliki. Kisha akamshtaki Paulo kuwa ni mtu mchokozi anayesababisha ghasia kati ya Wayahudi kote katika Dola ya Kirumi. Tertulo alidai kwamba Paulo ni kiongozi wa dhehebu la Wanazareti, na hata alijaribu kulichafua hekalu la Kiyahudi. Wayahudi waliokuwepo wakathibitisha mashtaka hayo.
Kisha Feliki akampa Paulo ishara ya kujibu mashtaka yanayomkabiri. Paulo akajitetea kwa kueleza kwamba hakuna mashahidi waliopo kwenye kikao hicho wanaoweza kuthibitisha tuhuma wanazomtuhumu nazo. Paulo akajieleza kwamba anamwabudu Mungu wa Israeli kama mfuasi wa njia ile, yaani imani juu ya Yesu kama Masihi na akaeleza kuwa alikuja Yerusalemu kwa ajili ya kuwaletea watu wake matoleo kwa ajili ya maskini aliyoyatoa kwa mataifa. Feliki akaahirisha uamuzi wake hadi wakati ambapo Klaudio Lisia (Kamanda wa Kirumi) atakapofika kutoka Yerusalemu. Akaamuru Paulo aendelee kushikiliwa chini ya ulinzi katika jumba la kigavana, huku akiruhusu marafiki wake kumhudumia mahitaji yake.
Mara kwa mara, Liwali Feliki alimwita Paulo na kuzungumza naye,huku akiwa na tumaini kwamba Paulo angempa rushwa ili amwachilie huru. Kila alipomwita, Paulo yeye alimzungumzia imani katika Yesu, haki, kiasi, na hukumu ijayo. Paulo alipoongelea kuhusu hukumu ya Mungu, Feliki akiwa na mkewe wa tatu aliingiwa na hofu na akamwacha Paulo. Hata hivyo, hakumwachilia huru, kwa kuwa alitaka kujipatia sifa kwa Wayahudi. Kwa sababu hiyo, Paulo alikaa gerezani kwa miaka miwili katika moja ya vyumba vya jumba la liwali huko Kaisaria. Kwa hiyo, mpaka mwaka wa 59 BK, Paulo alikuwa huko Kaisaria Maritima kifungoni.
Sasa kwa kuwa utawala wa liwali Feliki ulikuwa na sifa ya rushwa, usimamizi mbovu na ukatili, jimbo la Yudea lilikuwa na machafuko na vurugu nyingi katika kipindi chake. Moja ya machafuko yaliyotokea wakati wa utawala ni vurugu kati ya wayahudi na Wasyriani waliokuwa wakikaa Kaisaria. Tukio hili linasimuliwa na Mwanahistoria Josephus akisema “Na sasa palitokea mgogoro mkubwa kati ya Wayahudi waliokuwa wakazi wa Kaisaria na Wasyriani waliokuwa wakikaa hapo pia, kuhusu haki zao sawa za kufurahia fadhila zinazotokana na uraia wao; kwani Wayahudi walidai kuwa wao wanastahili hadhi ya juu, kwa sababu Herode mfalme wao ndiye aliyeujenga mji wa Kaisaria, na kwa kuwa alikuwa Myahudi kwa asili. Wasyriani hawakukataa yale yaliyoelezwa kuhusu Herode; lakini walisema kuwa Kaisaria hapo awali iliitwa Mnara wa Strato, na kwamba wakati huo hakukuwa na Mnyahudi hata mmoja aliyeishi hapo.”[7]
Kutokana na kushughulikia vibaya mgogoro huu na migogoro mingine, Wayahudi na Wasyriani walitoa ripoti kwa Kaisari Nero kuhusu uongozi mbovu wa liwali Feliki, na hivyo Feliki akaitwa Rumi na Porkio Festo akiwekwa kuwa mbadala wake. Josephus anasema kwamba wakati Feliki amerudi Rumi, Wayahudi walienda huko kumshitaki, lakini kwa sababu Feliki alikuwa na kaka yake aitwaye Pallas, mtu ambaye alikuwa anaheshimiwa na Kaisari Nero, akapona kuhukumiwa.
Mwishoni mwa mwaka 59 BK au mwanzoni mwa 60 BK ndio mwaka ambao Festo akafika Yudea kuanza kazi yake ya uliwali. Kumbuka kuwa kazi kubwa ya Festo ilikuwa ni kushughulika na machafuko na vurugu ambazo mtangulizi wake hakuzishughulikia vema. Hivyo, Festo alipofika tu Kaisaria, siku ya tatu akapanda kwenda Yerusalemu. Huko Yerusalemu, akaombwa na Wayahudi amlete Paulo Yerusalemu kuhukumiwa, huku Wayahudi wakiwa wamepanga kuvamia msafara huo na kumuua Paulo. Festo hakukubali ombi hilo; badala yake, akawataka waende Kaisaria yeye atakapokuwa amerejea.
Siku nane hadi kumi baadaye, Festo akarudi Kaisaria na akaagiza Paulo aletwe mbele yake. Wajumbe kutoka kwenye baraza la Kiyahudi (Sanhedrini) walifika Kaisaria na wakamshutumu Paulo mbele ya Liwali Festo—shutuma ambazo hakuna hata moja aliyeweza kuzithibitisha. Paulo akapinga shutuma zote alizoshutumiwa. Hata hivyo, kwa kuwa Festo alitaka kuwafanyia Wayahudi fadhila, akamuuliza Paulo kama yuko tayari kwenda Yerusalemu na kushtakiwa mbele ya baraza la wazee wa Kiyahudi. Kwa kuwa Paulo alijua Wayahudi wanampango wa kumuua, akatumia haki yake kama raia wa Kirumi na kuomba rufaa ili akashtakiwe mbele ya Kaisari huko Rumi. Kisheria, Festo alikuwa analazimika kukubali ombi la Paulo la kupelekwa Rumi na kushitakiwa huko. Lakini ili Festo ampeleke Paulo Rumi, ilibidi aandike barua ya kuambatana naye ambayo inaeleza chanzo cha kesi hiyo na hatua zilizochukuliwa mpaka mfungwa anapotumwa. Kwa kuwa Festo hakujua vizuri mambo ya dini ya Kiyahudi, na kutokana na kusikiliza kwake kesi, aliona kesi ya Paulo inahusisha mambo ya imani ya Kiyahudi, basi akaendelea kumweka Paulo ndani huku akipanga kumpeleka Rumi atakapopata namna nzuri ya kuandika barua yake (Matendo 25:1-12).
Bahati nzuri, Liwali Festo akatembelewa na Mfalme Agripa wa Pili (Tazama Jedwali namba 1 hapo juu) na dada yake aitwaye Bernike. Kwa kuwa Mfalme Agripa alikuwa na ujuzi wa imani ya Kiyahudi, Festo akamshirikisha kuhusu kesi ya Paulo. Mfalme Agripa akaomba kumsikiliza Paulo yeye mwenyewe, na kesho yake Paulo akaletwa mbele yake (Matendo 25:13–27). Paulo akajieleza mbele ya Mfalme Agripa na dada yake hadi kufikia kumhubiri Mfalme Agripa ili yamkini amwamini Yesu. Bado na Injili hiyo ya Paulo, Mfalme Agripa akamwambia Paulo asidhani kwamba anaweza kumfanya yeye kuwa Mkristo kwa maneno hayo machache. Paulo akajibu kuwa anatamani si yeye tu, bali wote wanaomsikia wamwamini Yesu, iwe kwa maneno machache au mengi. Mwisho, Mfalme Agripa anakubali kwamba Paulo alipaswa kuachiwa huru kama asingekuwa ameomba mwenyewe kwenda Rumi kusikilizwa (Matendo 26). Hivyo, Liwali Festo akaandaa kila kitu kwa ajili ya Paulo kupelekwa Rumi kwa msafara wa kiserikali.
MAELEZO YA CHINI
[1] Wasomi mbalimbali wa Biblia na historia wanakubaliana kwamba Yesu alisulubiwa tarehe 7 mwezi wa nne, mwaka wa 30 BK.
[2] Kandake halikuwa jina binafsi la malkia, bali ni jina la kurithi la kiutawala lililochotumiwa na malkia au mama wa kifalme katika ufalme wa Nubia.
[3] Josephus, War 3.29.
[4] Josephus, Antiquities of the Jews, Book 20, chapter 5.
[5] The Lives of the Twelve Caesars – The Life of Claudius, Chapter 25, section 4.
[6] Luka hajamtaja kabisa Tito katika kuelezea safari ya tatu ya kimishenari ya mtume Paulo, lakini kwa kusoma barua za Wakorintho wa kwanza na wa pili tunapata kujua kwamba kwenye safari hii, Tito alikuwa mshirika wa muhimu sana wa mtume Paulo. Barua hizo, ziliandikwa kwenye kipindi hiki.
[7] Josephus, Antiquities of the Jews, Book 20, chapter 8.
SEHEMU YA PILI
Mnamo mwaka wa 60 BK, Paulo akaanza kusafirishwa kutoka Kaisaria Maritima kwenda Rumi/Italia. Paulo na wafungwa wengine wakawekwa chini ya ulinzi wa Akida aliyeitwa Yulio. Mbali na Paulo kuwa mfungwa, wenzake wawili, ambao ni Luka na Aristako, waliweza kusafiri pamoja naye. Kutoka Kaisaria wakapanda merikebu (ambayo ilikuwa na umiliki kutoka Adramatio) na kuelekea Sidoni. Hapo Sidoni, kwa kuwa meli ilikuwa na muda wa kushusha mizigo, Paulo akapewa nafasi ya kwenda kwa rafiki zake ili wamhudumie katika mahitaji yake (Matendo 27:1–3). Kutoka Sidoni wakasafiri mpaka Mira. Hapo Mira wakapanda merikebu nyingine ya kwenda Italia, ambapo jumla walikuwa abiria mia mbili sabini na sita. Kutoka Mira, wakafika Nido, kisha wakasafiri chini ya Krete mpaka kufika mahali palipoitwa Bandari nzuri. Kwa kuwa walifika Bandari nzuri kwa shida, Paulo alishauri kuepuka kuendelea na safari ili wasihatarishe merikebu, mizigo na maisha yao wao wenyewe. Pamoja na ushauri huo, Akida akaruhusu merikebu iendelee na safari kama manahodha walivyoshauri.
Wakiwa wanasafiri pwani kwa pwani chini ya Krete, upepo mkali uitwao Eurakilo ukaikumba merikebu. Kwa wiki mbili merikebu ikasukumwa huku na kule na dhoruba kali. Wakati huo, malaika akamtokea Paulo na kumwambia asiogope kwa kuwa ni lazima afike kwa Kaisari. Pia akamweleza kuwa Mungu amemkirimia uhai wake yeye pamoja na wale wote waliokuwa merikebuni. Kwa shida na kwa kupoteza shehena na merikebu yenyewe hatimaye watu wote mia mbili sabini na sita wakafika kisiwa cha Melita/Malta salama kama Paulo alivyotabiri (Matendo 27).
Katika kisiwa cha Melita, Paulo na wafungwa wengine wakakaa kwa muda wa miezi mitatu. Katika muda huo, Mungu alifanya uponyaji na miujiza mingi kwa mikono ya Paulo. Kutoka hapo, wakasafiri kwa merikebu mpaka Sirakusa. Kupitia Regio na Puteoli, hatimaye wakafika Rumi. Paulo alifika Rumi mwanzoni mwa mwaka 61 BK (Matendo 28:1–14). Huu ulikuwa mwaka wa saba wa utawala wa Kaisari Nero katika Dola ya Rumi, wakati ambao Kaisari Nero alikuwa tayari ameonyesha matendo ya ukatili, mojawapo ikiwa ni kumuua mama yake aliyeitwa Agripina, mwaka mmoja kabla ya Paulo kufika Rumi.[1]
Huko Rumi, Paulo hakuwekwa Gerezani bali alikuwa chini ya kifungo cha ndani, akisubiri hukumu ya kesi yake.Katika muda huo, watu wengi walimtembelea na yeye akatumia muda huo kuhubiri injili (Matendo 28:16-31). Ndani ya miaka miwili ya kukaa katika kifungo hichi, Paulo aliandika barua nne, ambazo ni WAKOLOSAI, WAEFESO, WAFILIPI NA FILEMONI.
| Kaisari | Miaka ya Utawala | Kutajwa kwake katika Biblia |
| Augusto | 27 KK – 14 BK | Luka 2:1 |
| Tiberio | 14 BK – 37 BK | Luka 3:1 |
| Kaligula | 37 BK – 41 BK | Hakuna |
| Klaudio | 41 BK – 54 BK | Matendo 11:28; 18:2 |
| Nero | 54 BK– 68 BK | Hajatajwa kwa jina lakini Matendo 25;10-12; 27:24; 28:19 na Wafilipi 4:22 zinamhusu yeye. |
Jedwali 2. Majina ya makaisari na miaka ya utawala wao kuanzia wakati wa kuzaliwa kwa Yesu hadi kufika kwa Paulo katika mji wa Rumi, makao makuu ya Dola ya Rumi.
Wakati Paulo akiwa Rumi, huko Yudea/Uyahudi mwaka wa 62 BK, Liwali Festo aliyemsafirisha Paulo alikufa. Baada ya kifo cha Festo, Kaisari Nero akamteua Albinusi kuwa liwali wa Yudea. Wakati wa kipindi cha mpito kabla ya Liwali Albinusi kufika Yudea, Mfalme Agripa wa Pili, aliyekuwa na mamlaka ya kumteua kuhani mkuu, akamwondoa Yusufu bin Simoni na kumchagua Anania wa Pili (Anania mwana wa Anania) kuwa kuhani mkuu.
Anania, baada ya kupata ukuhani mkuu, akaitisha baraza la Kiyahudi (lililoitwa Sanihedrini) ili kuwashitaki Wayahudi kadhaa, akiwepo Yakobo, mdogo wa Yesu. Yakobo akahukumiwa pamoja na Wayahudi wengine kwa kuvunja Torati ya Musa; hivyo akaletwa juu ya kilele cha hekalu, akatupwa chini, akapigwa kwa mawe, na hatimaye akauawa. Kutokana na mauaji hayo ya Yakobo na Wayahudi wengine, Wayahudi wengine walikasirishwa na jambo hili. Baadhi walitoa taarifa kwa Mfalme Agripa wa Pili, na wengine wakatoa taarifa kwa Liwali Albinusi akiwa njiani kuja Yudea. Kutokana na malalamiko hayo, Mfalme Agripa wa Pili akamwondoa Anania katika ukuhani mkuu na akamchagua Yesu, mwana wa Damneusi, kuwa kuhani mkuu.[2]
| Jina la Liwali | Miaka ya Utawala (BK) | Eneo alilotawala |
| Pontio Pilato | 26–36 | Yudea, Samaria, na Idumea |
| Marcellus | 36–37 | Yudea |
| Marullus | 37–41 | Yudea |
| Cuspio Fado | 44–46 | Yudea |
| Tiberio Julio Aleksanda | 46–48 | Yudea |
| Ventidio Kumano | 48–52 | Yudea |
| Feliki | 52–59 | Yudea |
| Festo | 59–62 | Yudea |
| Albino/Albinusi | 62–64 | Yudea |
| Florus | 64–66 | Yudea |
Jedwali 3. Majina ya maliwali toka wakati wa kuhukumiwa kwa Yesu mpaka wakati wa uasi wa wayahudi wa mwaka 66 BK.
Mwaka wa 62 BK mwishoni au mwanzoni mwa mwaka 63 BK, Paulo alishinda kesi iliyomleta Rumi na hivyo akaachiwa huru. Kutoka Rumi alisafiri mpaka Uhispania kwa ajili ya injili. Paulo hakuishia Uhispania, bali alirudi Mashariki na kwenda hadi Efeso ambako alikutana na Timotheo. Baada ya muda alimwacha Timotheo kuweka mambo sawa yaliyoanza kuharibiwa na waalimu wa uongo, naye akaendelea na safari ya kimishenari. Paulo alisafiri tena na Tito hadi Krete na kupanda makanisa huko. Baadaye alimwacha Tito huko Krete ili kuchagua wazee katika kila kanisa na kukamilisha mambo yaliyopungua. Wakati Paulo alipokuwa akisafiri tena katika eneo la Makedonia, aliandika barua ya KWANZA KWA TIMOTHEO na barua kwa TITO ili kuwahimiza na kuwaelekeza kufanya kazi alizowaachia kufanya.[3]
Mwaka wa 64 BK Mwezi wa saba, moto ulizuka katika mji wa Rumi. Moto huu ulienea na kuunguza kama asilimia sabini ya mji huo, ndani ya kipindi cha juma moja. Mwanahistoria Tacitus katika kuelezea madhala anasema “Kwa hakika, Rumi imegawanyika katika maeneo kumi na manne, manne kati ya hayo yalibaki salama, matatu yakiungua kabisa ; na saba yaliyosalia, hakuna kilichobaki isipokuwa mabaki machache ya nyumba zilizokuwa zimeharibika na kuungua nusu.”[4]
Baadhi ya raia walimshutumu Kaisari Nero kuwa ndiye aliyewasha moto huu. Raia walirusha tuhuma hizo kwa Nero kwa kuwa kabla ya tukio hili alionekana kuwa na maono ya kuujenga mji wa Rumi kwa upya. Hivyo, kuunguza mji ilionekana kama njia ya kuusafisha ili aujenge kwa upya. Kwa lengo la kukwepa lawama Nero akawasingizia Wakristo kuwa ndiyo wahusika (yani wao ndio chanzo cha moto). Kwa sababu hiyo, mateso yakaanza juu ya wakristo waliokuwa katika mji wa Rumi. Mateso yalikuwa makali na yalisababisha wakristo wengi kuuawa kwa kutupwa katikati ya wanyama wakali huku wakiwa wamevalishwa ngozi za wanyama. Wengine walisulubiwa na wengine walichomwa moto na kufanywa kama taa wakati wa usiku. Mateso haya yanasimuliwa na mwanahistoria Tacitus akisema “Lakini wala msaada wa kibinadamu, wala ukarimu wa kifalme, wala njia zote za kuituliza Mbingu, hazikuweza kuizima tuhuma wala kuondoa imani iliyokuwa imeenea kwamba moto ule uliwashwa kwa amri maalumu. Kwa hiyo, ili kukomesha uvumi huo, Nero aliwasingizia wengine kuwa wahalifu badala yake na akawaadhibu kwa ukatili wa kiwango cha juu kabisa, kundi la watu waliodharauliwa kwa maovu yao, ambao umati uliwaita Wakristo. Kristo, mwanzilishi wa jina hilo, alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo katika utawala wa Tiberio, kwa hukumu ya msaidizi mkuu Pontio Pilato, na ushirikina huo mbaya ulikuwa umedhibitiwa kwa muda mfupi tu, lakini baadaye ukazuka tena, si tu huko Uyahudi—mahali chimbuko la “ugonjwa” huo—bali hata katika mji mkuu wenyewe, ambamo mambo yote ya kutisha au ya aibu duniani hukusanyika na kupata umaarufu. Kwanza, basi, wale waliokuwa wamekiri kuwa sehemu ya kundi hilo walikamatwa; kisha, kutokana na maelezo yao, idadi kubwa ilitiwa hatiani, si hasa kwa mashtaka ya kuwasha moto, bali kwa ‘chuki dhidi ya jamii ya wanadamu’. Na dhihaka iliandamana na mwisho wao: walivalishwa ngozi za wanyama na kuwekwa kwenye mbwa wakali, wakang’atwa hadi kufa; au walisulubiwa, na mwanga wa mchana ulipokoma, walichomwa moto ili kuwa kama taa za usiku. Nero alikuwa ametoa Bustani zake kwa ajili ya tamasha hilo, na akatoa maonyesho katika Uwanja wake wa Circus, akichangamana na umati akiwa na mavazi ya mwendesha gari wa mashindano, au akiwa amepanda gari lake la farasi.”[5]
Mateso haya kwa Kanisa ndani ya mji wa Rumi yaliendelea kwa muda wa miaka mitatu hadi minne. Katika kipindi hiki, ndipo mtume Petro aliuawa kwa kusulubiwa kichwa chini miguu juu. Katika kipindi hiki hiki, Paulo alikatwa tena mara ya pili akiwa Troa na akasafirishwa mpaka Rumi. Huko Rumi, akafungwa gerezani, na sio kifungo cha ndani kama ilivyokuwa mwanzo. Kutoka kifungoni, mtume Paulo akaandika WARAKA WA PILI KWA TIMOTHEO, Timotheo akiwa bado Efeso. Muda mrefu haukupita, mtume Paulo aliuawa; inakadiriwa kuwa hili lilitokea mwaka 67 BK. Mateso katika kanisa yalifikia mwisho baada ya kifo cha Kaisari Nero, kilichotokea baada ya kupinduliwa na kutangazwa kuwa adui wa serikali ya Rumi na baraza la Seneti. Kifo cha Kaisari Nero kilitokea mwaka wa 68 BK.
Wakati Kaisari Nero akiwatesa waamini katika mji wa Rumi katika kipindi hichi cha mwaka 64 BK hadi 67 BK, mwaka 66 BK wayahudi wa Yudea waliasi utawala wa Warumi na kujitangazia uhuru. Jambo hili lilisababishwa na sababu nyingi zilizokuwa zimekusanyika kwa muda mrefu. Katika sababu nyingi zilizosababisha jambo hili, moja kubwa ilikuwa ni tamaa ya muda mrefu ya wayahudi ya kuuondoa utawala wa Kirumi na kurejesha taifa lao katika uhuru. Tamaa hii iliongezeka zaidi baada ya kifo cha Herode Agripa wa kwanza, ambapo kuanzia hapo Yudea yote ilikuwa chini ya Liwali wa kirumi moja kwa moja.
Pamoja na hivyo, kisa kilichosababisha uasi huu kutokea kilikuwa ni ugomvi wa ardhi uliotokea katika mji wa Kaisaria, ambako ndiko kulikuwa makao makuu ya Yudea. Hapo Kaisaria, Wayahudi kwa mara kadhaa walitaka kununua ardhi iliyokuwa karibu na sinagogi ambayo ilikuwa inamilikiwa na Myunani/mgiriki mmoja. Pamoja na kukataa kuuza ardhi hiyo, Myunani huyu akaanza kujenga jengo la kufanyia kazi katika eneo hilo, na hivyo kupelekea Wayahudi kuwa na nafasi finyu sana ya kuelekea katika sinagogi. Vijana wa Kiyahudi walijaribu kutumia nguvu kuzuia ujenzi huo, lakini walizuiliwa na Liwali Florus. Kwa namna nyingine, Wayahudi walijaribu kumhonga Florus kiasi kikubwa cha fedha ili azuie ujenzi huo, lakini Florus hakufanya chochote pamoja na kupokea fedha hizo. Jambo hili likawa limechochea Wayahudi kutaka kufanya vurugu, lakini vurugu hazikuzuka muda huo.
Siku moja ya Sabato, Myunani mmoja wa Kaisaria aliweka chungu cha udongo kikiwa kimegeuzwa chini juu kwenye mlango wa sinagogi na kutoa dhabihu ya ndege—kitendo ambacho kilikuwa ni kufuru na uchochezi kwa Wayahudi, hivyo Wayahudi vijana wakaanzisha ghasia kubwa ambazo kamanda wa kikosi na jeshi lake walishindwa kuzizima. Wakati vijana wanafanya ghasia, Wayahudi wengine wenye busara wakachukua vitabu vyao vya Sheria na kwenda kwa Liwali Florus ili kulalamika kuhusu tukio hilo na pia kumkumbusha kuhusu talanta nane walizompa ili azuie ujenzi karibu na sinagogi. Lakini Liwali Florus akawatia chini ya ulinzi na akawashtaki kwa kuvitoa vitabu vya Sheria nje ya Kaisaria.
Wayahudi wa Yerusalemu, pamoja na kuumizwa na habari hizi za kile kilichotokea Kaisaria, walijizuia kuanzisha machafuko. Lakini baada ya Liwali Florus kwenda Yerusalemu, na kuchukua fedha katika hazina ya Hekalu na kudai kwamba Kaisari Nero amemtuma kufanya hivyo, ghasia zikaanza, na Wayahudi wakafanya dhihaka kubwa juu ya Florus.
Liwali Florus, ili kuwaadhibu waliofanyia dhihaka, akalitaka baraza la Kiyahudi liwalete waliofanyia dhihaka hiyo, lakini baraza likakataa kufanya hivyo. Kwa hasira, Liwali akaagiza jeshi kushughulika na kitendo hicho. Jeshi likavamia maeneo ya Yerusalemu na hatimaye kuua watu elfu tatu na mia sita. Kuanzia hapo, mgogoro ukaendelea kukua hatua kwa hatua. Pamoja na juhudi za Mfalme Agripa wa pili kuzuia kuanza kwa vita (na kupindua utawala wa Liwali Florus), Yudea ikaingia kwenye machafuko na vita. Kwa sababu Yudea ilikuwa chini ya Siria, gavana wa Siria akavamia Yudea ili kukomesha machafuko hayo. Jeshi la gavana wa Siria likashindwa vita, na Yudea ikajitangazia uhuru kwa kuanzisha serikali yake ya muda huko Yerusalemu chini ya uongozi wa Ananasi ben Ananasi.
Mnamo mwaka 67 BK, Kamanda Vespasiani alitumwa na Kaisari Nero kwenda Yudea kushughulika na uasi huo. Kamanda Vespasiani akawasili Galilaya akiwa na vikosi vyake kwa ajili ya mapambano. Vita vikaanza, na kwa muda warumi waliendelea kusonga kusini kuelekea Yerusalemu hatua kwa hatua, huku ngome za Wayahudi zikianguka moja baada ya nyingine njiani. Mwaka wa 68 BK, Vespasiani akiwa ameshikiria eneo kubwa la Yudea na akiwa amekaribia kuta za Yerusalemu, alipata habari za machafuko yaliyotokea Rumi kufuatia kifo cha Kaisari Nero. Vespasiani akaacha vita hivyo na akamkabidhi mwanae Tito kumaliza kazi hiyo huku yeye akienda kutetea kiti cha Ukaisaria ambacho mwishoni alikipata.
Mwaka wa 70 BK, Kamanda Tito aliuzingira (kuufunga kivita ili walioko ndani wasiweze kutoka wala walioko nje wasiweze kuingia) mji wa Yerusalemu na kusababisha njaa kali ndani yake, njaa iliyoua watu wengi. Baada ya njaa hiyo, majeshi ya Rumi yalivamia mji wa Yerusalemu, yakaunguza na zaidi kubomoa Hekalu, ambalo hadi leo halijajengwa tena. Kipigo hiki kilisababisha madhara makubwa kwa Waisraeli, kwa kuwa mbali na wengi kufa na kuuawa, wengine walitawanywa.Jambo hili lilikuwa na athari kubwa kuhusu imani ya kiyahudi, kwa kuwa imani hii ilikuwa imeegemea Hekalu; hivyo kubomolewa kwa Hekalu na kuhamishwa kwa watu kulikuwa ni changamoto kubwa sana kwao.[6]
Kwa maandishi ya mababa wa kanisa wa karne ya nne (kama Eusebio na Epifaniusi wa Salamisi), inasemekana Wakristo walikimbia mji wa Yerusalemu na kukimbilia Pella katika eneo la Dekapoli ng’ambo ya Mto Yordani kabla ya mji kuangushwa na Warumi. Hili lilifanyika kutokana na mwitikio wao juu ya utabiri wa Yesu kama ulivyoripotiwa na waandishi wa Injili (Marko 13 na Mathayo 24). Pamoja na kwamba ni ngumu kuthibitisha kihistoria kwamba Wakristo walikimbia kabla ya tukio hili kutokea, lakini ni kweli kwamba Bwana wetu Yesu Kristo alitabiri tukio hili takribani miaka thelathini na saba kabla. Baada ya Hekalu kubomolewa ndipo wakati ambao, kwa sehemu kubwa, Ukristo ulijitenga kabisa na Uyahudi. Kumbuka, kwa muda mrefu imani ya kikristo ilionekana kama “dhehebu” ndani ya dini ya kiyahudi.

Picha 1. Mwaka 71 BK, sherehe ya ushindi ilifanyika huko Rumi kuadhimisha ushindi Rumi dhidi ya wayahudi wa Yudea. Tukio hilo linakumbukwa katika Lango la Tito, ambalo linaonyesha askari wa Kirumi wakibeba nyara zilizochukuliwa kutoka Hekaluni, ikiwemo kinara cha taa (Menora). Picha na commons.wikimedia.org.
Itaendelea…
MAELEZO YA CHINI
[1] Taticus, The annals 14.1-14.13.
[2] Habari hii inasimuliwa na mwanahistoria Josephus katika kitabu chake Antiquities of the Jews, 20.9.1, na pia taarifa zingine zinapatikana katika kitabu cha Eusebius, The History of the Church, 2.23.
[3] Maelezo haya ya maisha ya mtume Paulo baada ya kifungo cha Rumi ni vigumu kuyathibitisha mpangilio wake kihistoria kwa sababu taarifa zake zinapatikana kwa uchache-uchache kutoka katika vyanzo vichache kama vile barua zake yeye mwenyewe Paulo kwa Timotheo na Tito, Kipande cha Muratoria, na barua ya kwanza ya Klementi wa Rumi.
[4] Taticus, The annals 15.40
[5] Taticus, The annals 15.44
[6] Tukio hili la kuanguka kwa Yerusalemu linasimuliwa na Josephus, katika kitabu chake cha The Wars of the Jews.

