Yona – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA UJUMBE WA NABII YONA

MAELEKEZO

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.

UTANGULIZI

Kitabu cha Yona ni mojawapo kati ya vitabu kumi na mbili vinavyoitwa na sisi Wakristo kama “vitabu vya manabii wadogo” katika sababu ya ufupi wa ujumbe wake. Kitabu hiki ni cha kipekee sana. Tofauti na vitabu vingine vya kinabii, kitabu hiki hakijajaa maneno ya unabii wa moja kwa moja, bali ni usimulizi kuhusu maisha ya nabii mwenyewe na uhusiano wake na Mungu. Pili, badala ya nabii kuonyeshwa kama mtu mtiifu ambaye watu wengine wanatakiwa kumuiga, kitabu hiki kinamwonyesha nabii kama mtu muasi, ambaye hana tabia za kimungu. Na zaidi, Nabii Yona ni mmoja wa manabii wachache ambao Mungu aliwatuma kupeleka ujumbe wake nje ya taifa la Israeli na Yuda. Yona yeye alitumwa na Mungu kupeleka ujumbe kwa watu wa Ninawi, jiji lililokuwa katika dola ya Ashuru, taifa lililokuwa na uadui na Israeli kwa muda mrefu.

Kitabu hiki kinafundisha wazi kwamba upendo na rehema za Mungu hazina mipaka ya kitaifa au kikabila, bali ni kwa ajili ya mataifa yote. Pia kinaonyesha jinsi Mungu anavyoshughulika na mtumishi wake ili amfunze kutii na kuelewa moyo wake.

MUKTADHA WA KIHISTORIA WA UJUMBE WA NABII YONA

Nabii Yona alikuwa mwana wa Amitai (2 Wafalme 14:25), na alitumika katika kipindi cha awali cha utawala wa mfalme Yeroboamu wa pili (mwana wa Yehoashi, siyo Yeroboamu mwana wa Nebati). Kipindi hicho taifa la Israeli la kaskazini lilikuwa na nguvu ya kijeshi na kimaeneo (ardhi), lakini kimaadili na kiroho lilikuwa katika hali ya uasi kwa Mungu. Katika huduma yake, kwenye kipindi hiki cha utawala wa mfalme Yeroboamu wa pili, Yona alitabiri kwamba Bwana Mungu ataurejesha mpaka wa Israeli uliokuwa umechukuliwa na dola ya Ashuru, na Mungu akafanya hivyo sawasawa na neno lake kwa mkono wa mfalme Yeroboamu. Hii ilikuwa pamoja na kwamba Yeroboamu alikuwa mfalme aliyefanya mabaya mbele za Mungu (2 Wafalme 14:23–29).

Kwa upande mwingine, Ashuru (ambako kulikuwa na jiji la Ninawi) ilikuwa ni dola kubwa yenye nguvu na ukatili mwingi, na kwa muda mrefu ilikuwa adui wa Israeli. Hivyo, agizo la Mungu kwa Yona kuhubiri toba kwa watu wa Ninawi lilikuwa gumu kwake kulikubali — si kwa sababu hakujua sauti ya Mungu, bali kwa sababu hakutaka maadui wa taifa lake wapate rehema ya Mungu.

UJUMBE MKUU WA NABII YONA

Ujumbe wa Yona ni kwamba Mungu ni wa rehema kwa wote na anatamani toba kwa kila mtu, si kwa Israeli pekee. Pia unaonyesha kwamba mtumishi wa Mungu anaweza kushindwa kuelewa upendo wa Mungu, lakini Mungu humfunza kwa njia mbalimbali ili kufikisha kuelewa mapenzi yake.

Kitabu cha Yona kinatufundisha kwamba:

  1. Haiwezekani kumkimbia Mungu (Yona 1).
  2. Mungu husikia maombi hata katika hali ya kukata tamaa (Yona 2).
  3. Toba ya kweli ya mtu yeyote inaleta rehema ya Mungu (Yona 3).
  4. Mungu hufundisha watu wake kwamba upendo na rehema zake ziko hata juu ya maadui wao (Yona 4).

MPANGILIO WA KITABU

Maandiko                             Maelezo
  1:1-16                     Yona anakimbia agizo la Mungu na safari yake baharini
 1:17–2:10              Yona ndani ya tumbo la samaki na sala yake
 3:1-9       Yona anahubiri Ninawi na watu wanatubu
  3:10-4:1-5             Mungu kughairi kuangamiza mji wa Ninawi na mwitikio wa Yona
4:6-11Mungu anamfundisha Yona rehema

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI

Kitabu cha Yona, kwa kuwa ni usimulizi, kina mpangilio ufuatao: utangulizi, kupanda kwa mgogoro, kilele, kuanguka kwa mgogoro, na suluhisho la migogoro.

Mchoro 1. Huu ni mchoro unaonyesha sehemu tano za usimulizi.

Katika utangulizi, ujumbe wa Yona unaanza kwa Mungu kumtuma Yona kwenda Ninawi. Badala ya kutii, Yona anakimbilia Tarshishi ili akimbie kutimiza maagizo ya Bwana (1:1-3). Safari yake ya Tarshishi inaleta dhoruba baharini, na mabaharia wanatambua kwamba yeye ndiye chanzo cha dhoruba, hivyo wanaamua kumtupa baharini. Baada ya Yona kutupwa baharini, dhoruba inatulia(1:4-16).

Katika tukio linalopandisha mgogoro, Mungu akamwandaa samaki mkubwa ammeze Yona, naye anakaa ndani ya tumbo la samaki kwa muda wa siku tatu, mchana na usiku[1]. Ndani ya tumbo la samaki, Yona anamwomba Mungu kwa maombi ya shukrani. Baada ya Yona kuzungumza na Mungu kwa njia ya maombi, samaki akamtapika pwani(2:1-10).

Katika kilele cha simulizi, Mungu anamrudishia tena Yona agizo lile lile la kwenda Ninawi (3:1-2). Safari hii, Yona anatii; anakwenda Ninawi, anahubiri ujumbe wa Mungu, na watu wa Ninawi — kuanzia mfalme mpaka wananchi wa kawaida — wanatubu (3:3-9).

Katika kuanguka kwa mgogoro, Mungu anakubali toba ya mji wa Ninawi na anaghairi mabaya aliyoyatabiri Yona. Msamaha huu unamkasisisha Yona, na Yona anaomba afe (Hii ni mara ya pili). Katika kuelezea hasira yake, Yona pia anaeleza sababu za yeye kukataa kuja Ninawi katika mwito wake wa kwanza (3:10-4:5).[2]

Katika suluhisho, Mungu anamfundisha Yona kuhusu rehema zake kwa watu wote, hata wale nje ya Israeli, kupitia mti. Mti ulipooteshwa na Bwana, Yona alifurahia kivuli chake, lakini alipokatika, na baada ya Yona kupigwa na jua kali hadi kukaribia kuzimia, alikasirika kiasi cha kutamani kufa (4:6-9). Kupitia tukio hilo, Mungu anamfundisha Yona kwamba, kama ambavyo yeye alihurumia mmea ambao hakuufanyia kazi wala kuuotesha, yeye Mungu ana haki ya kuhurumia mji wenye watu wengi wasio na hatia na wanyama wengi wa kufugwa (4:10-11).

Picha 1. Hili ni jeneza la mawe lililochongwa kutoka karne ya tatu. Bila shaka lilitengenezwa kwa ajili ya maziko ya Mkristo tajiri. Pamoja na kuonyesha matukio mengine, tukio la Yona kutupwa baharini, kumezwa na samaki mkubwa, na kutapikwa ufukweni limepewa nafasi kubwa. Aidha, Yona anaonyeshwa pia akiwa chini ya mmea uliompatia kimvuli. (Chanzo cha picha: Web Gallery of Art)


MAELEZO YA ZIADA


[1] Simulizi ya Yona ndani ya tumbo la samaki imetumika pia na Yesu kama ishara ya siku tatu za kufa na kufufuka kwake (Mathayo 12:39-41).

[2] Maneno ya Yona kwamba Mungu ni mwenye neema, amejaa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, na kwamba anaghairi mabaya, ni maneno yaliyorudiwa mara nyingi zaidi katika Agano la Kale. Maeneo mengine maneno haya yanasemwa ni: Hesabu 14:17-19, Torati 5:9-10, Yoeli 2:13, Nahumu 1:2-3 na Zaburi 86:15; 103:8-10; 111:4; 145:8. Kwa mara ya kwanza, yalizungumza na Mungu katika Kutoka 34:6-7.

Unakuja hivi karibuni……