MWONGOZO WA KUSOMA UJUMBE WA NABII HABAKUKI.
MAELEKEZO
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI
Umewahi kuwa kwenye hali ambayo unaona uovu umeenea kiasi kwamba unajiuliza, “Je, Mungu kweli anaona haya?” Unajiuliza, kama anaona, mbona yuko kimya? Mbona hakomeshi uovu huu? Pale unapoona wabaya wanawafanyia mambo mabaya watu wema, na bado Mungu anaonekana hafanyi chochote. Na mbaya zaidi, inaonekana wazi kuwa wabaya wanazidi kufanikiwa katika uovu wao wa kuwaonea wema, lakini bado Mungu anaonekana yuko kimya. Kama umewahi kuwa kwenye hali hiyo, wewe si wa kwanza; takribani miaka elfu mbili na mia sita iliyopita, nabii Habakuki alipitia hali hiyo hiyo. Hivyo, ujumbe wa kitabu chake unatuhusu sana, kwa kuwa hata sisi huwa tunapitia nyakati kama hizo.
Tofauti na vitabu vingine vya kinabii, kitabu cha Habakuki kina ujumbe wa majibizano kati nabii na Mungu, na si ujumbe wa Mungu kwenda kwa Israeli/Yuda moja kwa moja kama ilivyo kawaida ya vitabu vingine vya kinabii.
MUKTADHA WA KIHISTORIA
Tofauti na manabii wengine, nabii Habakuki hajaweka kalenda katika ujumbe wake ya kutuonyesha moja kwa moja ni wakati gani aliandika ujumbe huu. Hajataja mfalme yeyote ambaye angebainisha ni kipindi gani alifanya kazi yake ya kinabii. Pamoja na hayo, ujumbe wake unatupa picha ya wakati wa utumishi wake.
Baada ya kifo cha Yosia, mfalme wa Yuda aliyeleta uamsho mkubwa wa kiroho, mtoto wake, aitwaye Yehoahazi akafanywa kuwa mfalme. Yehoahazi, kwa muda mfupi, akalirudisha taifa katika kufanya mabaya, na ndani ya miezi mitatu akatolewa madarakani na Farao Neko wa Misri (2 Wafalme 23). Farao akamweka Eliakimu (akamwita Yehoyakimu), mtoto mwingine wa Yosia, kuwa mfalme. Hii ina maana Yuda, kwa wakati huu pamoja na kuwa na mfalme, ilikuwa chini ya Misri. Hii ndio maana walikuwa na wajibu wa kulipa kodi Misri. Mfalme Yehoyakimu pia alifanya mabaya mbele za Mungu, na sifa zake zinafanana kabisa na sifa za taifa ambazo Habakuki anazielezea katika malalamiko yake mbele za Mungu.
Yeremia anamuelezea Yehoyakimu kwa sifa hizi: “Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu! Na vyumba vyake kwa udhalimu! Atumiaye utumishi wa mwenzake bila ujira, Wala hampi mshahara wake; Asemaye, Nitajijengea nyumba pana na vyumba vipana; Naye hujikatia madirisha; Na kuta zake zimefunikwa kwa mierezi, Na kupakwa rangi nyekundu. Je! Utatawala kwa sababu unashindana na watu kwa mierezi? Baba yako, je! Hakula na kunywa, na kufanya hukumu na haki? Hapo ndipo alipofanikiwa. Alihukumu maneno ya maskini na mhitaji; hapo ndipo alipofanikiwa. Je! Huku siko kunijua, asema Bwana? Bali macho yako na moyo wako hauna utakalo ila kutamani, na kumwaga damu isiyo na hatia, na kudhulumu, na kutenda jeuri.Basi, Bwana asema hivi, katika habari ya Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu; au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa! Utukufu wake” (Yeremia 22:13-18). Sifa hizi ni sifa zinazofanana na sifa za maisha ndani ya taifa ambazo Habakuki anazitaja akielezea malalamiko yake (Habakuki 1:1-4). Mfanano huu, ndio sababu ya kwanza ya kutuonyesha kwamba Habakuki alipata ujumbe wa kitabu hiki katika kipindi cha mfalme Yehoyakimu au muda mfupi baada yake.
Lakini pia, majibu ya Mungu kwa Habakuki kuhusu malalamiko yake yanatusaidia kuelewa kipindi ambacho nabii huyu alipokea ujumbe wake. Inaonekana kwamba Habakuki alipata ufunuo huu muda mfupi kabla ya Yuda kwenda utumwani Babeli — kipindi ambacho dola ya Babeli ilikuwa imeanza kupata nguvu na kuwa tishio kwa mataifa mengine, ikiwemo Yuda.
Katika majibu yake, Mungu anamwambia Habakuki kwamba atawaleta Wakaldayo — jamii ya watu kutoka katika dola ya Babeli, ambao wakati wa Habakuki walikuwa wameshaanza kupata nguvu za kiutawala — kama chombo cha hukumu dhidi ya watu wa Yuda (Habakuki 1:6).[1] Baadaye, jambo hili lilitokea kama Mungu alivyosema, na likasababisha Yuda kwenda utumwani Babeli (2 Wafalme 24). Hii pia inaonyesha kwamba, nabii Hakakuki alipata ujumbe wake, muda mfupi kabla ya Yuda kuvamiwa na kupelekwa utumwani Babeli.
Hivyo, ujumbe huu ni ujumbe ambao Habakuki aliupata katika kipindi ambacho kulikuwa na ukosefu wa haki katika taifa la Yuda; kipindi kifupi kabla ya dola ya Babeli kuja na kulipigia taifa hili la Mungu na kulipeleka utumwani.

Picha 1. Hili ni jumba lililojengwa katika eneo lililokuwa kaburi la nabii Habakuki; liko katika mji wa Tuyserkan, katika mkoa wa Hamadan, nchini Iran (Picha imetolewa commons.wikimedia.org).
MPANGILIO WA WARAKA
| NAMBA | MAANDIKO | MAELEZO |
| 1 | 1:1-4 | Malalamiko ya kwanza |
| 2 | 1:5-10 | Majibu ya Mungu |
| 3 | 1:11-17 | Malamiko ya pili |
| 4 | 2:1-4 | Majibu ya pili ya Mungu |
| 5 | 2:5-20 | Ole kwa Babeli |
| 6 | 3:1-15 | Ujio wa Bwana kwa hukumu na wokovu |
| 7 | 3:16-19 | Hitimisho |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI
Baada ya utangulizi mfupi (1:1), Habakuki anapeleka malalamiko yake kwa Mungu. Malalamiko yake yanahusu ni kwa muda gani Mungu atakaa kimya wakati ukiukwaji wa haki (udhalimu) unaendelea katika jamii ya Yuda. Habakuki anasema, Mungu, utakuwa kimya hata lini katikati ya ukatili, ugomvi, kupotoshwa kwa hukumu, kuachwa kwa sheria yako, na kuzungukwa kwa mwenye haki na watu wabaya? (1:2–4). Majibu ya Mungu kutokana na malalamiko ya Habakuki ni tangazo kwamba atawaleta Wakaldayo kwa ajili ya kuwahukumu Yuda. Wakaldayo, au taifa la Babeli, ni taifa lenye sifa zifuatazo: Moja, ni taifa linalopita katikati ya dunia ili kuyamiliki maeneo yasiyo yao. Pili, Wakaldayo ni watu wenye kutisha na kuogopwa kwa kuwa sheria zao ni tofauti kabisa. Tatu, ni taifa lenye “vifaa vya kijeshi” vilivyo na uharaka wa kutekeleza utekaji wa mateka kwa wingi. Nne, ni taifa ambalo kwa historia yake, wafalme , wakuu wengine, na ngome za watu wengine ni vitu vya kudharauliwa (2:5–11).
Baada ya majibu hayo ya Mungu, Habakuki analalamika tena kwa mara ya pili. Habakuki anasema, kweli Mungu, yeye ambaye ni wa milele na mtakatifu, amewachagua Wakaldayo kutekeleza hukumu na adhabu?[2] Mungu, yeye ambaye hawezi kuangalia uovu, anaamua kutumia taifa ovu kuliko mengine kuwaadhibu wengine (wakiwemo Yuda)? Kwa kutumia lugha ya picha ya uvuvi, Habakuki analalamika kwamba Mungu, kwa kuwatumia Wakaldayo, amewafanya wanadamu wengine kuwa kama samaki na Wakaldayo kuwa wavuvi. Kwa kutumia lugha hiyo ya picha, Habakuki anaelezea sifa za ukatili wa Wakaldayo: hukusanya mateka kutoka maeneo mengine na kuwaleta chini yao, na katika hao mateka hutoa kafara. Mwisho, anamwuliza Mungu, je, kuna siku Wakaldayo wataacha kuua watu? (1:12–17).
Baada ya malalamiko haya ya mara ya pili, Habakuki alikaa mkao wa kusubiri majibu ya Mungu juu ya malalamiko yake (2:1). Mungu anajibu malalamiko yake kwa kumuagiza aandike maono. Ayaandike maono hayo kwa uwazi ili kila atakayeyasoma aweze kuyaelewa kwa urahisi. Ni maono ya kuaminika, ushuhuda wake ni wa kweli, na Habakuki anatakiwa kusubiri kwa uvumilivu utimilifu wake, hata kama utaonekana kuchelewa kufika. Kutokana na maono haya, kutakuwa na mwitikio wa aina mbili: mwenye haki ataishi kwa imani yake katika maono haya na asiye na unyoofu ataonyesha kiburi/kujivuna (2:2-4).
Mwenye kiburi hujidanganya na hatulii, kwa kuwa hashibi wala hatosheki kama kuzimu; kila wakati anafanya jitihada kukusanya mataifa ili wawe mateka wake (2:5).[3] Kwa mujibu wa sifa zinazotajwa, kinachozungumziwa hapa ni taifa, na si mtu binafsi, tena ni taifa la Babeli. Kwa sababu ya sifa hizo, watu wote — yaani mataifa mengine — watainuka na kumdhihaki taifa hilo kwa kutoa “ole” tano juu yake. Ole ya kwanza inatoa onyo kwa yule anayejilimbikizia mali kwa njia ya unyang’anyi. Kwa sababu ya tabia hiyo, mataifa yaliyonyang’anywa mali yao watainuka na kumfanya mnyang’anyi wao kuwa mateka wao (2:6–8). Ole ya pili inatoa onyo kwa yule anayejitajirisha kwa kuonea wengine na kujijenga ili kujihakikishia usalama. Huyu naye, kile alichokijenga kitashirikiana kumuangusha (2:9-11).
Ole ya tatu inatoa onyo kwa yule ajengaye mji kwa njia ya mauaji au kumwaga damu. Kwa sababu ya uovu huo, Mungu ameagiza kazi yake yote ya ujenzi wa mji kuwa bure (yaani, kazi yake kuwa hasara), na kila mtu atajua kwamba yeye Mungu amefanya hivyo (2:12-14). Ole ya nne inatoa onyo kwa yule ampaye jirani yake kileo ili kuutazama uchi wake. (Kileo na sumu katika muktadha huu ni lugha ya picha inayomaanisha matumizi mabaya ya nguvu; “uchi” unawakilisha ardhi na mali za mji uliotekwa. Tazama Nahumu 3:5–7 na Yeremia 51:7).[4] Malipo ya tendo hilo ni kunyweshwa kileo kilekile alichowapa jirani zake, kwa mkono wa kuume wa Bwana (2:15-17). Ole ya tano ni onyo kwa watengenezaji wa sanamu, wanaoziomba na kuzungumza nazo. Sanamu hazina pumzi wala uwezo wa kuzungumza, lakini Mungu yuko hai na anakaa katika hekalu lake takatifu; kwa hiyo dunia yote inapaswa kunyamaza kimya mbele zake (2:18-20).
Baada ya ole hizo, kwa mara ya tatu Habakuki anapeleka hoja zake kwa Mungu, lakini sasa hoja yake iko katika maombi na si malalamiko. Maombi yake ni kwamba Mungu afanye mambo katika wakati huu kama alivyofanya katika nyakati za nyuma; mambo hayo ya nyuma ni mambo ambayo Habakuki, kwa kuyasikia, anaogopa (3:1-2). Baada ya maombi hayo, Mungu anamuonyesha Habakuki maono na kwa kutumia ushairi yeye anaelezea alichokiona.[5] Habakuki aliona kushuka kwa Mungu kutoka katika milima akiwa katika utisho wake uliodhihirika kwa mwangaza mkali, moto, utisho mkubwa, pamoja na tetemeko la ardhi (Kushuka kwake kulifanana na kuona majeshi yakielekea vitani). Kutokana na kushuka na kupita kwake katika hali ya kivita, mataifa yaliyokuwa njiani yalipatwa na taabu (3:3-7). Je, Ujio wa Bwana katika utisho huu ulikuwa kwa ajili ya milima, mito, au viumbe vingine? (Kumbuka kwamba ujio wake ulihusisha kupata shida kwa viumbe, kama vile milima kutetemeka na jua na mwezi kusimama). Habakuki anapata jibu kwamba ujio wa Bwana katika hali ya vita haukuwa kwa ajili ya viumbe hao, bali ulikuwa kwa ajili ya kuangamiza mataifa (ikiwepo Babeli) na kuwaokoa watu wake (3:8-15).
Kumbuka, Habakuki alianza kwa kulalamikia ukimya wa Mungu katikati ya maovu na ukiukwaji mkubwa wa haki katika Yuda. Mungu akamjibu kwamba atatumia taifa la Babeli kukomesha maovu hayo. Habakuki akamlalamikia tena Mungu kwa kutangaza kwamba atatumia taifa lenye dhambi kuliko Yuda katika kuwarekebisha. Ili kumuonyesha Habakuki kwamba, kuwatumia Babeli hakumaanishi kukubaliana na maisha yao, Mungu anampa Habakuki onyo tano zinazomuelekea Babeli. Mbali na hivyo, Mungu akampa Habakuki maono ya kumuonyesha jinsi ambavyo, mwishoni, Yeye mwenyewe atashuka kuangamiza mataifa maovu na, upande mwingine, kuwaokoa watu wake. Baada ya Habakuki kupata maono haya, akajawa na hofu kuu, hofu iliyodhihirika hata katika mwili wake. Wakati huo hakumjibu tena Mungu, bali alikubali kusubiri udhihirisho wa mambo aliyoyaona (3:16). Mwishoni, anamalizia kwa kusema kwamba, hata kama hali za nje zinaonyesha kana kwamba Mungu yuko kimya (kwa mfano, mashamba hayatoi chakula), yeye bado atamshangilia Bwana, kwa kuwa Yeye ndiye Mwokozi wake na nguvu zake (3:17–19).
.
FOOTNOTES
[1] Wakaldayo ilikuwa ni jamii ya watu walioishi kusini wa Babeli, ambao katika wakati wa maisha ya Habakuki walikuwa wameshaanza kupata nguvu za kiutawala katika Babeli, hivyo kwa wakati huu kutaja Wakaldayo ilikuwa ni sawa na kutaja Babeli.
[2] Sio rahisi kujua maana halisi ya mstari wa 12b. Kwa maana nyingine, unaweza kueleweka kama malalamiko ya Habakuki kwamba Mungu amewaweka au amewatunza Yuda kwa ajili ya hukumu na amewahifadhi ili waje kuadhibiwa. Kwa maana hii, kulikuwa hakuna maana ya kuwatunza Yuda miaka yote hii kama mwisho wake ulikuwa ni kuadhibiwa na taifa ovu kuliko wao.
[3] Kwa kuzingatia sifa zinazotajwa katika mstari huu, ni dhahiri kwamba kinachozungumziwa si mtu binafsi bali ni taifa. Tena, katika muktadha wetu, taifa linalorejelewa ni taifa la Babeli, yaani Wakaldayo.
[4] Kwa ujumla, mstari huu unatoa onyo kuhusu matumizi ya nguvu ya Babeli dhidi ya jirani zake, ambayo yalikuwa na lengo la kutumia vibaya ardhi na mali zao.
[5] Sura hii ya tatu inatumia zaidi sifa ya ushairi iitwayo usambamba. Sifa hii maana yake ni kwamba sehemu ya pili ya sentensi hutumia maneno mengine kuelezea jambo lilelile lililotajwa katika sehemu ya kwanza. Mfano, maneno “Naliziona hema za Kushi katika taabu” katika sehemu ya kwanza ya mstari wa saba yanasisitizwa na maneno “Mapazia ya nchi ya Midiani yakatetemeka.” Katika sehemu ya pili. Sehemu hizi zote mbili zina ujumbe mmoja—kupata shida kwa mataifa kutokana na kupita kwa Bwana katika utukufu wake.
Unakuja hivi karibuni……

