MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA MTUME PAULO KWA WAEFESO
MAELEKEZO
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako; usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI
Barua ya mtume Paulo kwa Waefeso ni barua iliyopewa sifa za kipekee sana na wanataaluma wa Biblia. Ni barua ambayo wanataaluma wa Biblia wameipa majina mengi ya kuonyesha ubora wake. Wengine wameiita taji ya theolojia ya mtume Paulo, wengine kiini cha theolojia ya mtume Paulo, wengine kilele au kilima cha juu cha Agano Jipya, na wengine muhtasari tukufu wa Agano Jipya. Pamoja na hivyo, Waefeso sio barua iliyopewa kipaumbele sana na waamini wengi ,ukiacha nukuu zake chache ambazo ni maarufu. Lakini barua hii ni muhimu sana hasa kwa ajili ya kuelewa mpango wa Mungu wa milele juu ya kanisa lake. Huwezi kuelewa vizuri mpango wa Mungu wa milele juu ya kanisa bila kusoma barua hii na pia huwezi kusoma barua kwa makini ukabaki katika imani ya kibinafsi, kama Mwandishi John Stott alivyowahi kusema kwamba “Hakuna mtu anayeweza kusoma kwa makini barua ya Paulo kwa Waefeso akabaki na injili ya kibinafsi. Kwa sababu Waefeso ni injili ya Kanisa. Inafafanua kusudi la milele la Mungu la kuumba kupitia Yesu Kristo jamii mpya...” ambayo ndiyo inaitwa Kanisa.
BARUA KWA KANISA LA EFESO?
Ukiwa unasoma waraka huu katika baadhi ya tafsiri za Biblia, utaona kwamba neno Efeso katika sura ya kwanza, mstari wa kwanza, limewekwa ndani ya mabano. Mfano, katika tafsiri ya Swahili Revised Union Version, Waefeso 1:1 inasema: “Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu walioko [Efeso] wanaomwamini Kristo Yesu.” Kuwekwa kwa neno Efeso ndani ya mabano kunatokana na sababu kadhaa. Kwanza, baadhi ya nakala za kale zilizoandikwa kwa mkono, na ambazo ni muhimu katika kutunza maneno ya Agano Jipya, zinakosa neno Efeso. Pili, mazungumzo ya Paulo katika barua hii yanaleta mashaka kuamini kwamba aliandika barua hii kwa watu aliowahubiria na kuwalea yeye mwenyewe kwa muda mrefu. Anaposema “tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu” (Waefeso 1:15) au “ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu” (Waefeso 3:2), inaonyesha kwamba aliwaandikia watu ambao hakukaa nao. Hii ni tofauti na habari tunayoipata katika kitabu cha Matendo ya Mitume; kwa mujibu wa Matendo, Paulo alikaa Efeso kwa zaidi ya miaka miwili (Matendo 19). Tatu, Paulo hatoi salamu kwa kutaja jina la mtu yeyote, jambo ambalo ingekuwa sio rahisi kufanya kama angekuwa ameandika kwa ajili ya kanisa la Efeso, kanisa ambalo alitumia muda mrefu na juhudi nyingi kulipanda.
Kutokana na sababu hizo na nyingine kadhaa, ndiyo maana neno Efeso liko kwenye mabano katika baadhi ya tafsiri. Pia, kutokana na sababu hizo, baadhi ya wataalamu wa maandishi ya kale na wanataaluma wa Biblia wanadhani kwamba barua hii iliandikwa na Paulo kwa ajili ya kwenda kwenye makanisa yaliyokuwa katika eneo zima la Asia Ndogo, na Efeso ikiwa moja ya makanisa hayo.
Pamoja na sababu hizo, kuna ushahidi mwingi zaidi unaothibitisha kwamba barua hii iliandikwa kwa ajili ya kanisa la Efeso. Moja, ni ushahidi wa nakala za kale. Ni nakala chache tu ambazo hazina neno Efeso[1], nakala nyingine nyingi zina neno Efeso, na zaidi hakuna nakala ya kale yenye jina tofauti na Efeso. Pili, idadi kubwa ya mababa wa imani yetu wa kuanzia karne ya pili na kuendelea waliitambua barua hii kuwa iliandikwa kwa ajili ya Kanisa la Efeso. Tatu, toka Paulo atoke Efeso mpaka anaandika barua hii kuna kipindi cha takribani miaka saba, hivyo kauli zinazoonyesha kutofahamiana na wapokeaji wa barua hii zinatokana na kupita kwa kipindi hicho kirefu. Katika kipindi hiki cha miaka takribani saba, kuna mabadiliko makubwa yaliyotokea ambayo mtume Paulo alipata habari zake (Waefeso 1:15). Pia, kulikuwa na watu wengine walioamini baada ya Paulo kuondoka, hivyo walisikia kuhusu habari zake (Waefeso 3:2 na 4:21) kutoka kwa wengine. Pamoja na hayo yote, bado ni sahihi kwamba barua hii ililenga kufika mbali zaidi ya kanisa la Efeso tu; ndiyo maana ujumbe wake haukuwa na mwelekeo wa kushughulika na tatizo lolote maalumu.
MJI WA EFESO
Mji wa Efeso ambao mtume Paulo aliukuta katika kipindi cha utumishi wake ulikuwa ni mji mama wa jimbo la Kirumi la Asia kwa sababu ya ushawishi wake katika siasa, biashara, na dini. Kisiasa, mji wa Efeso ulikuwa mji mkuu wa jimbo la Asia (Asia Ndogo), jimbo lililokuwa chini ya usimamizi wa Baraza la Seneti la Kirumi.[2] Kwa kawaida, jimbo la kiseneti liliongozwa na liwali ambaye ndiye aliyekuwa na mamlaka makubwa katika jimbo husika. Kwa Asia, liwali huyu aliishi Efeso (Matendo 19:38), hivyo kuufanya mji huu kuwa muhimu kiutawala.
Kutokana na kuwepo kwa bandari na barabara za kimkakati zinazounganisha mji huu na maeneo mengine, Efeso ulikuwa mji mkubwa wa kibiashara. Kwa sababu ya biashara nzuri, Efeso ulikuwa mji wenye uchumi unaokua, hivyo kuvutia watu wengi kutoka maeneo mbalimbali. Katika kipindi hiki, ni Rumi na Aleksandria tu ndio iliyokuwa miji mikubwa na yenye umaarufu kuliko Efeso. Hivyo, mji huu ulikuwa miongoni mwa miji muhimu sana kwa wakati huu.
Kidini, Efeso ilikuwa kama miji mingine ya dola ya Kirumi: kulikuwa na miungu mingi inayoabudiwa kwa wingi wake. Kwa sehemu kubwa, hakukuwa na kuabudu mungu mmoja tu; jamii nzima ilikuwa na ufahamu wa kuabudu miungu mingi kadri inavyowezekana. Moja ya mahekalu yaliyokuwepo Efeso ni pamoja na mahekalu ya mungu Zeu na Apolo, hekalu kwa ajili ya kumwabudu Kaisari, na hekalu kwa ajili ya mungu-mke Artemi (au Diana). Pamoja na kuwepo kwa miungu mingi, mungu-mke Artemi ndiye aliyekuwa na uhusiano maalumu na mji wa Efeso. Ingawa alibudiwa pia na wafuasi wa maeneo mengine, Efeso ndio mahali ambapo mungu huyu alikuwa na mvuto mkubwa sana, ndio maana aliitwa “Artemi wa Waefeso” (Matendo 19:34). Hapa Efeso kulikuwa na hekalu kubwa lililokuwa na utukufu kwa ajili ya wafuasi wake kufanyia ibada. Hekalu hili la mungu-mke Artemi lilikuwa kubwa na lenye utukufu kiasi kwamba likapata sifa ya kuwa moja ya maajabu saba ya dunia ya kale.
Artemi aliaminiwa kuwa ni bikira, mungu anayejihusisha na uwindaji na mambo ya uzazi. Aliaminiwa kuwa ana nguvu isiyo ya kawaida ambayo alikuwa anaitumia kuwakinga wafuasi wake dhidi ya roho za nyota, anga, roho za ulimwengu wa chini/kuzimu, na roho za hapa duniani. Hivyo, yeye aliaminiwa ndiye mwenye kuwakinga watu dhidi ya roho zote zenye kuleta laana, magonjwa, tauni, na uharibifu mbalimbali. Hii ndio maana Artemi aliitwa mtunzaji wa mji wa Efeso. Na kwa sababu hiyo, alitukuzwa na wafuasi wake kwa majina kama “Malkia wa Mbinguni,” “Bwana,” au “Mwokozi.”
Kwa kuwa dini katika ulimwengu wa kale haikuwa jambo la kibinafsi bali jambo la jamii kwa manufaa ya jamii nzima, Artemi aliathiri maeneo mengi ya maisha ya watu wa mji wa Efeso. Hekalu lake lilikuwa kitovu kikuu cha shughuli za benki za mji, sura yake iliwekwa katika sarafu, visanamu mbalimbali vilichongwa kwa ajili ya wafuasi wake, mwezi mmoja wa mwaka uliitwa kwa jina lake, na michezo ya mtindo wa Olimpiki iliandaliwa kwa heshima yake; michezo hiyo ikijulikana kama Artemisia. Kubwa zaidi, mara mbili kila wiki, maandamano ya kidini yalifanyika, ambapo wafuasi wake waliibeba sanamu zake, wakitembea kutoka hekaluni kwenda katikati ya mji, kisha kurejea hekaluni tena.
Kwa kuwa mungu Artemi alikuwa anahusika na maeneo mengi ya maisha ya jamii nzima, hivyo kuingilia dini hii kwa namna yeyote ile ilikuwa ni jambo ambalo lilitakiwa kupingwa kwa nguvu. Hii ndio maana watengeneza visanamu wakati wa injili ya Mtume Paulo walisababisha ghasia katika mji mzima pale walipoona injili imeanza kudhorotesha biashara inayohusika na dini hii moja kwa moja (Matendo 19:23-41).

Picha 1. Artemi Waefeso (Picha na commons.wikimedia.org)
Mbali na hivyo, Efeso pia ulikuwa ni mji wenye sifa kubwa ya uchawi, hasa uchawi unaohusisha matumizi ya maneno fulani fulani kwa ajili ya kutaka ushindi, uponyaji, na ulinzi. Hii ndio maana Efeso pekee ndiyo mji ambao mtumishi wa Mungu Luka katika kitabu cha Matendo anatuambia vitabu vya uchawi vilichomwa baada ya watu kuona miujiza Mungu aliyoifanya kwa mikono ya Paulo. (Matendo 19)[3]. Vitabu hivi vilikuwa na thamani ya fedha hamsini elfu (sawa na malipo ya kazi ya mtu ya siku hamsini elfu ). Hali hii ndio sababu, kwenye barua hii mtume Paulo anasisitiza ukuu wa Yesu juu ya ufalme zote, na mamlaka, na nguvu, na usultani wote. Kwa kuwa watu walitoka kwenye mazingira ambayo walikuwa wanategemea uchawi kuishi ilikuwa ni hitaji la lazima kuwasisitiza kuhusu ukuu wa Yesu waliyemwamini. Zaidi, barua hii ndio barua pekee inayozungumzia vita vya kiroho kwa msisitizo zaidi kuliko barua zote za mtume Paulo (Waefeso 6:10-18).
Kwa sababu ya hayo yote, yaani siasa, biashara na dini, mji wa Efeso ulikuwa ni mji uliojengeka wenye uwanja mkubwa wa maonyesho (wenye uwezo wa kubeba watu 24,000), mifereji ya maji, kumbi za mazoezi, viwanja wa michezo ya wapiganaji, masoko ya kibiashara, malango ya kuvutia, mahekalu ya miungu mbaimbali na majengo mengine makubwa na ya kuvutia ya ulimwengu wa kale.
KANISA LA EFESO NA UTUMISHI WA PAULO
Mtume Paulo alifika kwa mara ya kwanza Efeso mwishoni mwa safari yake ya pili ya kimisheni, akakaa muda mfupi sana na kisha kuondoka (Matendo 18:19–22). Katika safari yake ya tatu akarejea na kuweka kambi hapo kwa takribani miaka mitatu (Matendo 19). Katika muda huo, kwa kushirikiana na waamini wengine wengi, walipanda kanisa na kulilea.
Katika kazi hii kulikuwa na mambo waliyokutana nayo ambayo mwandishi Luka anayatolea ripoti. Moja, walikutana na matumizi ya maneno ya “uchawi” kwa ajili ya kutoa pepo; ndio maana watoto wa Skewa waliiga matumizi ya jina la Yesu wakidhani kuwa hii ilikuwa aina nyingine ya maneno yanayoweza kutumika kutoa pepo (Matendo 19:13–16). Na kwa kuwa maneno haya mengi walikuwa wanajifunza katika vitabu vya kujifunza kunuia, ndio maana waamini walisalimisha vitabu hivyo vya kichawi baada ya kuona miujiza mikubwa iliyofanywa na Mungu kupitia Paulo (Matendo 19:19). Pili, walikutana na ibada kwa mungu mke Artemi ambayo ilikuwa imejishikiza kwenye kila eneo la maisha, pamoja na eneo la uchumi. Mungu huyu aliaminika kuleta amani na kutunza mji wa Efeso (Matendo 19:23–41). Pia, wafuasi wake walikuwa nao wanatumia maneno maalumu kwa ajili ya kupunga pepo kama ambavyo Plutarch mwandishi alivyoripoti kwamba “waganga waliwaagiza wale waliokuwa wamepagawa na mapepo kutamka kwa kurudia maneno ya Kiefeso (Ephesia Grammata).”[4] Haya, yalikuwa ni maneno maalumu ambayo yakitamkwa vizuri basi uponyaji ungepatikana. Tatu, kanisa lilizaliwa kwa kutokea mgawanyiko katika sinagogi la Wayahudi (Matendo 19:8–10).
Kwa hiyo, Kanisa la Efeso lilizaliwa katika mazingira yaliyojawa ibada za miungu, na hasa ibada ya mungu mke Artemi. Tena lilizaliwa katika mazingira ambayo watu walitegemea uchawi ili kupata usalama, uponyaji, na hata ulinzi. Zaidi ya hayo, lilizaliwa katika mazingira ya uadui wa Wayahudi wasioamini dhidi ya waamini (Wayahudi na Wamataifa). Haya mambo utaona yakijitokeza sana katika barua hii kwa Waefeso.
KUSUDI LA WARAKA
Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso ni waraka ambao hauonyeshi kwamba kulikuwa na jambo maalumu lililosababisha (lazimisha) kuandikwa kwake. Ni waraka ulioandikwa na Mtume Paulo akiwa kifungoni Rumi, akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake; kesi iliyoanzia kule Yerusalemu. Pamoja na kwamba waraka huu ulitumwa pamoja na waraka kwa Wakolosai na waraka kwa Filemoni, nyaraka ambazo ziliandikwa kwa sababu maalumu (sababu zilizochochea kuandikwa), waraka wa Waefeso hauonyeshi kwamba uliandikwa kwa sababu maalumu.
Pamoja na hivyo, kutokana na ujumla wa ujumbe wake, ni sahihi kusema kwamba Paulo aliandika ujumbe huu ili kulithibitishia kanisa utambulisho wake mpya. Kwamba kanisa ni moja, kutoka kwenye mkusanyiko wa Wayahudi na Wamataifa walioitwa na Mungu. Tena, kuthibitisha kwamba kanisa liko juu ya nguvu zote na mamlaka zote za giza kwa sababu ya Yesu aliye kichwa cha vitu vyote. Na zaidi, kutokana na utambulisho huo, kulihamasisha kanisa kuendelea kuishi sawa na utambulisho wao wa utakatifu katika mwenendo wa maisha yao ya kila siku.
MPANGILIO WA KITABU
| MAELEZO | WAEFESO |
| Utangulizi | 1:1-2 |
| MUNGU ALICHOFANYA | |
| Sifa kwa Mungu Baba | 1:3-14 |
| Shukrani na maombi | 1:15-23 |
| Kutoka mautini mpaka kutukuzwa | 2:1-10 |
| Kutoka kwenye ugeni mpaka wenyeji | 2:11-22 |
| Uwakili wa Mtume Paulo | 3:1-13 |
| Maombi kwa Baba | 3:14-21 |
| MWENENDO MPYA WA MWAMINI | |
| Umoja kwa ajili ya ukuaji wa Kanisa | 4:1-16 |
| Kuvua mwenendo za zamani na kuvaa mpya | 4:17-32 |
| Kuenenda katika upendo na katika nuru | 5:1-14 |
| Kuenenda katika hekima, ufahamu na Roho | 5:15-21 |
| Mwenendo katika familia | 5:22-6:9 |
| Kuvaa silaha za upinzani | 6:10-20 |
| HITIMISHO | |
| Hitimisho la Barua | 6:21-24 |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI
Barua hii, kama barua nyingine, inaanza na utangulizi unaotaja mtumaji wa ujumbe, wapokeaji wa ujumbe, na salamu (1:1-2).
Baada ya hapo, mtume Paulo anamtukuza (au anambariki) Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa yale aliyoyafanya kwa waamini ndani ya Yesu.[5] Paulo anambariki Baba kwa sababu zifuatazo: Moja, alituchagua kabla ya kuumbwa ulimwengu tuwe watakatifu na tuwe watoto wake kupitia Yesu Kristo (1:3-6). Pili, alitukomboa kupitia kifo cha Yesu na akatujulisha mpango wake kwamba, wakati ukitimia, ataviunganisha vitu vyote chini ya Kristo / kuviweka vitu vyote chini ya kichwa kimoja, ambacho ni Kristo (1:7-10). Ambapo, ndani ya Kristo kwa sasa sisi tumefanywa kuwa urithi wa Mungu na sifa ya utukufu wake (1:11-12). Tatu, baada ya kumwamini Yesu, Waefeso wakawekwa muhuri ambao ni Roho Mtakatifu. Huyu Roho ndiye malipo ya awali yanayothibitisha kwamba malipo yatamaliziwa (1:13-14).
Kutokana na hayo yote Mungu aliyoyafanya, na kutokana na taarifa ya imani ya Waefeso kwa Yesu na upendo wao kwa watakatifu wote, Paulo anaripoti kwamba amekuwa haachi kumshukuru Mungu kwa ajili yao katika maombi (1:15–16). Katika maombi hayo, pia Paulo amekuwa anawaombea kwamba wapate kumjua sana Mungu kupitia ufahamu na hekima inayoletwa na Roho. Matokeo yake ni macho ya mioyo yao kutiwa nuru na hatimaye wajue yafuatayo. Moja, wajue tumaini la mwito ambao Mungu aliwaitia; pili, wajue utajiri wa urithi wa Mungu uliotukuka katika watakatifu; na mwisho, wajue ubora wa nguvu yake itendayo kazi ndani yetu (1:17–19). Ubora wa nguvu ya Mungu ulionekana katika ufufuo wa Yesu na katika kutukuzwa kwake, yaani kuwekwa juu ya kila kitu, kwa ajili ya Kanisa, ambalo ni ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote (1:20–23).
Baada ya kumbariki Mungu kwa mpango wake wa tangu awali na baada ya kuwaombea waamini ili waelewe tumaini la mwito wao, utajiri wa urithi wa Mungu na ubora wa nguvu inayofanya kazi ndani yao, Mtume Paulo anaingia kuelezea kwa kirefu jinsi Mungu alivyotekeleza mpango wake wa milele wa wokovu; jinsi anavyowabadilisha wenye dhambi kuwa watakatifu na kuwajenga pamoja kuwa Kanisa, yaani Mwili wa Kristo. Katika 2:1-10, Paulo anaeleza tatizo lililokuwepo, Mungu akafanya nini, na mwisho anatoa mjumuisho wa kile Mungu alichofanya katika kuwafanya wamataifa na wayahudi kupatana na Mungu.
Tatizo: Waamini wa mataifa kabla ya kuamini walikuwa wamekufa kwa sababu ya dhambi zao, walizofanya kwa kumfuata shetani. Wayahudi kwa upande wao nao wakaishi katika dhambi hizo na hivyo kutokana na mwenendo wao wakahesabika kama wana wa kuasi (2:1-3). Mungu akafanya nini? Mungu, kwa rehema yake na upendo, akatuhuisha pamoja na Kristo sisi sote (wamataifa na Wayahudi). Baada ya kutuhuisha/kutufufua/kutuokoa, akatutukuza pamoja na Kristo. Sababu ya kuhuisha, kufufua, na kutukuza waamini pamoja na Kristo ni ili Mungu aonyeshe wingi wa neema yake katika enzi zinazokuja (2:4-7). Ujumuisho: Kwa kuwa watu walikuwa wamekufa, Mungu ndiye aliyewafufua na kuwatukuza pamoja na Kristo; hivyo, wokovu ni zawadi ya Mungu inayopokelewa kwa njia ya imani na sio matokeo ya matendo ya mwanadamu. Hata hivyo, wokovu toka awali ulikuwa na kusudi la kuwaleta wanadamu kuishi katika matendo mema (2:8-10).
Baada ya kueleza jinsi wayahudi na wamataifa walivyopatanishwa na Mungu, katika 2:11-22, Paulo anaeleza jinsi wayahudi na wamataifa waliovyounganishwa katika Kristo na kuunda mwili wa Kristo. Kama katika 2:1-10 hapa pia anaeleza tatizo lilikuwa ni nini, Mungu akafanya nini na mwisho matokeo ya kile Mungu alichokifanya. Tatizo lilikuwa ni nini? Wamataifa kabla ya kuamini walikosa faida zile wayahudi walizokuwa nazo, na hivyo walikuwa wametengwa na taifa la Mungu (2:11-12). Mungu akafanya nini? Kwa Kristo Yesu kuwa amani ya Wayahudi na Waataifa, wamataifa wakawa wamoja na wayahudi na kupata faida walizozikosa hapo awali. Yeye, kwa njia ya msalaba, alibomoa kile kilichowatenga hawa wawili (yaani, sheria ya Musa[6]) na hivyo akawaunganisha hawa wawili kuwa mtu mmoja mpya na akawapatanisha na Mungu kwa njia moja tu (2:14-16). Kisha akawatangazia hiyo amani wamataifa na wayahudi pia, kwa kuwa wote wamepata njia ya kumwendea Baba kwa Roho mmoja (2:17-18). Matokeo ya kazi hii ya Mungu nini? Kutokana na muunganiko huo, Wamataifa walioamini hali yao imebadilika; wao si wageni tena bali ni wenyeji, ni watu wa nyumbani mwa Mungu. Pamoja na Wayahudi walioamini, wamejengwa wawe maskani ya Mungu katika Roho, yaani wawe hekalu la Mungu (2:19-22).
Baada ya kuelezea jinsi ambavyo wamataifa wameunganishwa na wayahudi na kuwa mwili mmoja ndani ya Kristo, Paulo anaelezea nafasi yake na ya mitume wengine na manabii katika utekelezaji wa mpango huu wa Mungu kabla ya kuendeleza maombi. Paulo anasema, yeye amekuwa mfungwa kwa sababu ya uwakili wa neema ya Mungu aliopewa kwa ajili ya wamataifa. Katika uwakili huo, kwa kufunuliwa, yeye pamoja na mitume wengine na manabii wa nyakati zao walijulishwa siri ambayo vizazi vilivyopita havikujulishwa. Siri hiyo ni kwamba watu wa mataifa ni warithi pamoja na wayahudi, waurithio urithi mmoja, na tena wote wawili ni mwili mmoja. Na zaidi, wamataifa ni washiriki pamoja na wayahudi wa ahadi ya Mungu iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili (3:1-7).
Kutokana na kupokea uwakili huo, Paulo alipewa kazi ya kuwahubiri mataifa utajiri wa kristo usiopimika na kuwatangazia watu wote utekelezaji wa siri hiyo ya Mungu iliyofunuliwa sasa. Matokeo ya kazi hiyo ni ili kwa njia ya kanisa hekima ya Mungu ijulikane katika ulimwengu mzima—kwa falme na mamlaka katika ulimwengu wa mbinguni.[7] Kujulikana huku kwa hekima ya Mungu kwa ulimwengu wote, ni sawa sawa na kusudi lake la milele alilolikusidia ndani ya kristo, ambaye anatupa ujasiri waamini kumkaribia Mungu. Kutokana na maelezo haya yote kuhusu uwakili wake, Paulo anawatia moyo Waefeso kutovunjika moyo kutokana na kufungwa kwake (3:8-13).
Baada ya kueleza nafasi yake katika utekelezaji wa mpango wa Mungu wa milele, Paulo anaomba tena. Maombi yake anayapeleka kwa Baba (3:14–15), na maombi yake ni kwamba Baba awafanye imara Waefeso kwa nguvu katika utu wao wa ndani ili Kristo akae mioyoni mwao (aweke makazi katika mioyo yao). Pia anamwomba Baba kwamba Waefeso wawe na shina na msingi katika upendo ili kwa pamoja na watakatifu wote, waufahamu na kuujua upendo wa Kristo katika ukubwa wake. Kilele cha maombi ya Paulo ni kwamba Waefeso watimilike kwa utimilifu wote wa Mungu (3:16–19). Paulo anamalizia maombi yake kwa kumtukuza Mungu anayeweza kufanya zaidi ya maombi aliyoyaomba (3:19–21).
Baada ya kuelezea jinsi Mungu alivyowatoa Waefeso kutoka katika hali ya ufu mpaka katika hali ya kutukuzwa na jinsi alivyowaunganisha wayahudi na wamataifa ndani ya Kristo ili wawe mwili mmoja, Paulo sasa anaingia kuagiza aina ya mwenendo unaotakiwa kwa waamini kutokana na yale Mungu amefanya kwao (Zingatia; Kila mwanzoni mwa aya kuna neno kuenenda/kutokuenenda).
Kwanza, anawaita kuutunza umoja wao ulioletwa na Roho (4:1-3). Kisha anatoa sababu kwa nini wanatakiwa kuutunza umoja wao; kila wanachokishiriki kiko kimoja (4:4-6). Pamoja na waamini kushiriki vitu hivyo katika umoja, bado kila mmoja wao amepewa kipawa na Kristo tofauti na mwingine kwa kadiri ya kipimo chake Kristo mwenyewe (4:7-10).[8] Kwa kutoa mifano ya vipawa, Kristo alivyovitoa, Paulo anasema lengo la vipawa hivyo ni ili mwili wa Kristo ujengwe na mwili huo uwe mtu mkamilifu. Yote haya ni kwa msaada wa kila kiungo (4:11-16).
Pili, anawaita Waefeso kuishi tofauti na wamataifa ambao hawajaamini wanavyoishi, ambao wao wanaishi katika ubatili wa nia zao na katika kila namna ya uchafu wa kutamani kwa sababu akili zao zimetiwa giza, wametengwa na uzima wa mungu na wamekufa ganzi. Paulo anawaita Waefeso wavue mwenendo huo wa tamaa mbaya wa zamani, wafanywe upya nia zao na wavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli (4:17-24). Baada ya kuagiza hivyo, Paulo anataja maeneo mitano ambayo waamini wanatakiwa kuvua mwenendo wa zamani na kuvaa mwenendo mpya na kwa kila eneo anataja sababu ya kuvaa mwenendo huo. Maeneno hayo ni uongo/ukweli, hasira itendayo dhambi/hasira isiyotenda dhambi, wizi/utoaji, maneno maovu/maneno yenye neema, uchungu, dhadhabu,hasira, kelele na matukano/ fadhili, huruma, kusameheana (4:25-32).
Tatu, Paulo anawaita Waefeso kuenenda katika upendo na katika nuru. Katika upendo, Paulo anawaita Waefeso kuishi katika upendo kwa kufuata kielelezo cha Kristo cha kujitoa kwa ajili yetu (5:1–2). Baada ya hapo, anawaita kuishi katika nuru. Katika hili, anaanza kwa kutaja mambo ya giza ambayo hayatakiwi kuwa sehemu ya waamini. Moja, anataja mambo yanayohusiana na tabia (Uasherati, uchafu na tamaa) na anasema sababu ya kuyaepuka ni kwamba hayastahili kwa watakatifu. Pili, anataja mambo yanayohusiana na usemi, na anataja shukrani kuwa mbadala wa mambo maovu ya kiusemi. Kwa ujumla, sababu ya kuepuka maisha haya ya giza ni kwamba wanaoishi katika hayo hawana nafasi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Na pia, hayo ndiyo yanayoleta ghadhabu ya Mungu kwa wasioamini; hivyo, waamini hawapaswi kushiriki katika hayo (5:3–7). Baada ya sababu hizo mbili, Mtume Paulo anaongeza sababu nyingine kwa nini waamini waepuke maisha ya giza; wao zamani walikuwa giza lakini sasa wamekuwa nuru, hivyo wanatakiwa kuenenda nuruni (5:8-14).
Nne, Paulo anawaita Waefeso kuwa na mwenendo unaokwepa mambo matatu, ambayo kila moja wapo analipa mbadala wake. Moja, badala ya kuenenda kama watu wasio na hekima, waenende kama watu wenye hekima. Pili, badala ya kuwa wajinga, wawe na ufahamu wa mapenzi ya Mungu. Tatu, badala ya kulewa kwa mvinyo, wanatakiwa kujazwa Roho (5:15–18). Kujazwa Roho kuna matokeo matatu, ambayo ni: kusemezana kwa nyimbo na kumwimbia Mungu, maisha ya shukrani kwa Mungu sikuzote, na kunyenyekeana katika Kristo (5:18–21).
Paulo anaendelea kueleza ni kwa namna gani waamini katika familia wanatakiwa kuenenda kwa hekima, kwa ufahamu wa mapenzi ya Mungu, na kwa kujazwa na Roho. Kwa wake, wao wanatakiwa kuwatii waume zao, kama waamini wanavyomtii Kristo (5:22–24). Kwa wanaume, wao wanatakiwa kuwapenda wake zao kama Kristo anavyolipenda Kanisa (5:25–33). Watoto, wao wanatakiwa kuwatii na kuwaheshimu wazazi wao katika Bwana (6:1–3). Wakina baba, wao wanatakiwa kuwalea watoto wao katika adabu na maonyo ya Bwana na sio kuwalea katika namna itakayowafanya watoto kuwa na hasira nao (6:4). Watumwa, wao wanatakiwa kuwatii mabwana wao wa mwili kama wanavyomtii Kristo (6:5–8). Na mwisho, mabwana wao wanatakiwa kuishi na watumwa wao kwa sifa zile zile walizoagizwa watumwa (6:9).
Mwisho wa ujumbe wake mkuu, Paulo anawaita Waefeso kuzidi kuwa hodari katika Bwana kwa kuvaa silaha zote za Bwana, ili waweze kuzipinga hila za Shetani katika ulimwengu wa roho na, mwisho wa siku, waweze kusimama (6:10–13). Baada ya mwito huo wa msisitizo, Paulo anataja silaha sita ambazo Waefeso wanatakiwa kuvaa (6:14–17)[9]. Mwisho, anawaita Waefeso kuwa katika sala na maombi kila wakati katika Roho; maombi yakihusisha kuwaombea watakatifu wote, yeye akiwa mmoja wao (6:18–20).
Paulo anahitimisha barua hii kwa kumtambulisha Tikiko na kwa kutamka baraka ya mwisho (6:21–24).
FOOTNOTES
[1] Nakala za kale ambazo hazina neno Efeso, tafsiri ya mstari huu inakuwa “Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu walioko na wanaomwamini Kristo Yesu”
[2] Kuna majimbo mengine yalikuwa chini ya usimamizi wa Kaisari moja kwa moja. Mfano, jimbo la Yudea lilikuwa ni jimbo chini ya Kaisari moja kwa moja. Majimbo yaliyokuwa na changamoto za kiusalama yalikuwa chini ya Kaisari, lakini yale yaliyokuwa hayana changamoto za kiusalama basi yalikuwa chini ya baraza la Seneti.
[3] Hakuna uhakika wa moja kwa moja kwamba uchawi ulikuwa unahusiana na mungu Artemi moja kwa moja ua la.
[4] Plutarch, Table Talk, 7.5
[5] Kuanzia mstari wa 3 mpaka wa 14 ni mstari mmoja unaoelezea sifa kwa Mungu.
[6] Kwa ujumbe wa jumla wa vitabu vya Torati, Mungu aliwapa Wayahudi Torati baada ya kuwatenga na mataifa mengine ili wao waishi tofauti na mataifa. Hii ndiyo maana wao tu ndiyo waliotahiriwa, hawakuruhusiwa kula chakula pamoja na Wamataifa, na hawakutakiwa kuoa nje ya jamii yao. Hivyo, Torati ndiyo kiambaza kilichowatenga Wayahudi na Wamataifa, na ndiyo uadui Yesu aliouondoa kwa kifo chake cha msalaba.
[7] Paulo anataja falme na mamlaka mara tatu katika barua hii (1:21; 3:10 na 6:12), akionyesha kuwa falme hizi si za mwili bali ni za kiroho, ambazo makazi yake ni katika mbingu au angani kwa lugha rahisi (2:2).
[8] Paulo anatumia Zaburi 68:18 pamoja na muktasari wa sura hii nzima (Zaburi 68) kuelezea tukio la Yesu kushuka chini, kupaa juu, na kutoa vipawa. Hii ina maana kwamba Mtume Paulo hajatumia Zaburi 68:18 kama nukuu ya moja kwa moja.
[9] Silaha hizi ni silaha za Bwana, kwa kuwa Bwana au Masihi wake ndiye anayeonekana kuzivaa katika Agano la Kale (tazama Isaya 11:5; 59:17) na hivyo sasa anazitoa kwa waamini.
Unakuja hivi karibuni…

