Wakolosai – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA MTUME PAULO KWA WAKOLOSAI


MAELEKEZO

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako; usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.

UTANGULIZI

Barua ya Mtume Paulo kwa Wakolosai ni barua yenye upekee sana. Upekee wake unaonekana katika mambo kadhaa. Kwanza, ni waraka pekee wa Paulo unaotoa picha tukufu zaidi ya Bwana wetu Kristo. Yesu Kristo katika waraka huu anatajwa kama mfano (picha) wa Mungu asiyeonekana. Yeye ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, Muumbaji wa vitu vyote kwa ajili yake mwenyewe, mshikiriaji wa viumbe vyote, na ndiye kichwa cha kanisa. Yeye ni utimilifu na mpatanishi wa nafsi ya Mungu na uumbaji wote (Wakolosai 1:15–20).

Pili, maneno maarufu ya Mtume Paulo katika barua zingine kama kuhesabiwa haki, sheria, mwili, au Roho Mtakatifu hayapo au yako kwa mbali sana katika barua hii. Hili lote ni kuthibitisha upekee wake.

Pamoja na upekee wake, barua hii ni barua yenye mfanano mkubwa sana na barua ya Mtume Paulo kwa Waefeso katika muundo, lugha, na maada zinazozungumziwa.

MJI WA KOLOSAI

Mji wa Kolosai, mji ambao kanisa lililoandikiwa barua hii na Mtume Paulo lilikuwemo, haukuwa mji muhimu sana katika karne ya kwanza. Mji huu ulizidiwa umuhimu na miji jirani kama vile Laodikia na Hierapoli. Kijiografia, mji huu ulikuwa katika eneo la Frigia, ambalo lilikuwa ndani ya jimbo la Kirumi la Asia Ndogo (leo ni Uturuki).

Pamoja na kutokuwa na umuhimu mkubwa kiuchumi wala kiutawala katika karne ya kwanza, Kolosai, zaidi ya miaka mia mbili kabla ya kuja kwa Yesu, ulikuwa mji muhimu sana kibiashara. Hii ilitokana na kuwa na uzalishaji mkubwa wa nguo. Hali hii ilipelekea hata aina fulani ya sufu ya kifahari yenye rangi nyekundu kuitwa “sufu ya Kikolosai.”

Lakini pia, pamoja na kutokuwa na umuhimu mkubwa sana katika karne ya kwanza, Kolosai ulikuwa na mchanganyiko mkubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali. Hii ilipelekea kuwepo kwa imani mbalimbali za kidini, na hasa miseto ya imani hizo. Moja ya imani za kidini zilizoletwa na watu katika mji huu ilikuwa imani ya Kiyahudi. Hivyo, mji huu pia ulikuwa na idadi fulani ya Wayahudi.

Ukiacha Uyahudi, ushahidi unaopatikana kutoka kwa sarafu za kale zilizopatikana katika eneo hilo unaonyesha kuwa ibada za miungu mbalimbali kama vile Artemisi wa Efeso, Zeus, miungu ya Frigia, Athena, pamoja na miungu ya Misri kama Isisi na Serapi, zilikuwa sehemu ya maisha ya kidini ya jamii ya watu wa mji huu.

KANISA LA KOLOSAI NA MTUME PAULO

Kwa taarifa zilizopo kwenye vitabu vya Agano Jipya na hata nje ya Biblia, hakuna ushahidi kwamba Mtume Paulo aliwahi kutembelea Kolosai, na hivyo yeye hakuwa mpandaji wa Kanisa hili aliloliandikia barua hii (Wakolosai 2:1). Kanisa hili lilipandwa na Epafra, ambaye Paulo anaeleza juhudi yake (Wakolosai 1:7–8; 4:12–13). Na inaonekana pia Epafra ndiye aliyepanda na kanisa la Laodokia na alikuwa kwenye juhudi la kupanda kanisa la Hierapoli muda mchache kabla hajamfuata mtume Paulo ( Wakolosai 4:15-16).[1]

Inawezekana kwamba Epafra alikuwa mmoja wa watu waliomwamini Kristo kupitia huduma ya Mtume Paulo wakati wa huduma yake ya karibu miaka mitatu huko Efeso, katika safari yake ya tatu ya kimisheni (Matendo 19 na kuendelea). Kwa kuwa mji wa Efeso ulikuwa kituo kikubwa cha biashara, watu kutoka sehemu mbalimbali za Asia ndogo walifika huko. Kwa njia hii, kupitia huduma ya Paulo huko Efeso, “Wayahudi na Wagiriki wote walioishi katika jimbo la Asia waliisikia neno la Bwana” (Matendo 19:10). Na hivyo kumfanya Epafra kuwa mmoja wa wale waliolisikia neno la Bwana kutoka kwa Paulo na kuliamini. Na kwa yeye mwenyewe alikuwa mwenyeji wa Kolosai (Wakolosai 4:12), hivyo baada ya kuamini alirudi Kolosai na akahubiri injili huko na kupanda kanisa katika mji huo (Hii haimaanishi Kolosai kulikuwa na jamii moja tu ya waamini , kumbuka kuna kanisa lilokuwa linakutana nyumbani kwa Filemoni, Filemoni 1:1-2; Wakolosai 4:9 na nyumbani kwa Nimfa, Wakolosai 4:15).

Baadaye Epafra akasafiri mpaka Rumi ambako Paulo alikuwa amefungwa kwa ajili ya Injili, na inaonekana hata alishiriki kifungo hicho pamoja na Paulo, kwa kuwa katika Filemoni 1:23 Paulo anamwita “mfungwa mwenzangu.” Kwa sababu hiyo, hakuweza kurudi Kolosai akiwa na waraka huu ambao Paulo aliandika, hivyo Paulo akamtuma Tikiko pamoja na Onesmo kutekeleza jukumu hilo (Wakolosai 4:7–8).

Sababu ya Epafra kwenda kumtembelea Paulo inaonekana ilikuwa hasa ni kutafuta msaada katika kushughulikia mafundisho yasiyokuwa sahihi yaliyokuwa yameanza kujitokeza katika Kanisa na ambayo yalikuwa yanapotosha Injili ya Kristo. Pamoja na hivyo, Epafra pia alifikisha taarifa njema za maendeleo mazuri ya Kanisa (Wakolosai 1:4-5; 2:5). Kwa hiyo, Paulo anaandika waraka huu kwa kanisa ambalo, amelilea kwa njia isiyo ya moja kwa moja yaani, alihusika nalo kupitia huduma ya Epafra, aliyekuwa mwanafunzi na mtumishi mweza katika Injili.

SABABU YA KUANDIKWA KWA WARAKA HUU

Paulo hajaweka wazi kwa nini aliandika waraka huu kama ilivyo katika nyaraka nyingine, lakini kuwepo kwa maangalizo kama vile “mtu asije akawadanganya kwa maneno ya kuwashawishi” (Wakolosai 2:4), “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu” (Wakolosai 2:8), “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;” (Wakolosai 2:16) na “Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili;” (Wakolosai 2:18) ni ushahidi tosha kuwa kusudi kubwa la kuandika waraka huu ni kukinzana na mafundisho yasiyokuwa sawa na injili ya Kristo.

Mafundisho haya yanaonekana yalikuwa ni matokeo ya mseto wa imani, ukihusisha imani ya dini ya uyahudi na falsafa za kijadi zilizokuwa katika mji wa Kolosai. Wafundishaji wa mafundisho haya inaonekana walikuwa wakijisifu kwa uwezo wao wa kufikia utimilifu wa mwisho wa kiroho kwa sababu ya kuwa na hekima, ufahamu na maarifa (2:1-4), maono yao ya kiroho, ibada kwa malaika na maisha yao ya kujinyima au kuutawala mwili kwa ukali (Wakolosai 2:8-23). Kwa upande mwingi inaonekana walikuwa wanajisifu na kuwataka Wakolosai kufuata sheria ya Musa hasa kuhusu vyakula na ufuataji wa sikukuu, mwandamo wa mwezi, na sabato.

Kwa sababu, kwa kufanya hivyo walikuwa wanapingana na utimilifu unaopatikana kwa Kristo, Mtume Paulo anatumia muda wa kutosha kuelezea kwamba utimilifu unapatikana kwa Kristo (Wakolosai 1:19; 2:19) na Wakolosai hawana wanachopungukiwa ndani ya Kristo na hivyo Waendelee katika imani kwa Kristo kama walivyofundishwa (2:6-7). Kwa hiyo, ujumbe mkuu wa Mtume Paulo kwa Wakolosai ni waendelee katika imani ndani ya Kristo kama walivyofundishwa kwa kuwa ndani yake ndiyo kuna utimilifu.

MPANGILIO WA KITABU

MAELEZOMAELEZOWAKOLOSAI
UTANGULIZI                          Anuani1:1-2
Shukrani1:3-8
Maombi1:9-12
Ukuu wa Yesu1:13-20
Wokovu wa Wakolosai1:21-23
Paulo mhudumu wa injili1:24-2:5
UJUMBE MKUUMsifanywe mateka2:6-15
 Msihukumiwe wala kunyang’anya thawabu yenu2:16-3:4
 Maisha yawapasayo waamini3:5-4:6
HITIMISHOSalamu na maagizo ya mwisho4:7-18

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI

Barua hii, kama barua nyingine, inaanza na utangulizi unaotaja watumaji wa barua, wapokeaji wa barua, na salamu (1:1-2). Baada yautangulizi, Mtume Paulo na Timotheo wanamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa ajili ya Wakolosai. Shukrani hizi wanazifanya sasa, lakini pia kila wakati wanapowaombea. Sababu ya shukrani zao ni habari walizozisikia kuhusu Imani ya Wakolosai kwa Yesu Kristo na upendo walionao kwa watakatifu wote. Sababu ya imani yao na upendo wao ni tumaini walilowekewa mbinguni. Tumaini hilo walilisikia katika neno la kweli la Injili iliyofika kwao na kuzaa matunda kama ilivyokuwa katika ulimwengu wote. Injili hiyo walifundishwa na Epafra, mhudumu mwaminifu wa Kristo na mtumwa mweza wa Paulo na Timotheo (1:3-8).

Baada ya shukrani, Paulo na Timotheo wanatoa ripoti ya maombi yao ambayo wamekuwa wakiomba toka waliposikia habari za Imani na upendo wa Wakolosai. Ombi lao kubwa ni Wakolosai wajazwe na maarifa ya mapenzi ya Mungu katika hekima yote na ufahamu wa rohoni. Maarifa haya yawapelekee Wakolosai kuenenda kama ulivyo wajibu wao kwa Bwana, wakimpendeza kabisa. Maisha ambayo ni wajibu wao na ambayo yanampendeza Bwana ni yapi? Moja, ni maisha ya kuzaa matunda katika kila tendo jema (kazi njema). Pili, ni maisha ya kukua katika maarifa ya Mungu. Tatu ni maisha ya kuwezeshwa kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha. Na mwisho ni maisha ya shukrani kwa Baba aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu (1:9-12).

Huyu Baba, alituokoa kutoka kwenye utawala wa giza kwa kutuhamisha kutoka huko na kutuingiza katika ufalme wa mwana wake. Katika huyo mwana wake tuna ukombozi, yaani msamaha wa dhambi (1:13-14). Huyu Mwana ni nani? Kuhusu uhusiano wake na Mungu, yeye ni picha (au sura) halisi ya Mungu asiyeonekana. Kuhusu uhusiano wake na viumbe, yeye ni mzaliwa wa kwanza juu ya viumbe vyote.[2] Hii ikiwa na maana yeye ni mkuu juu ya viumbe vyote. Kwa nini yeye ni mkuu juu ya viumbe vyote? Ni kwa sababu katika yeye vitu vyote viliumbwa (tena kwa ajili yake), yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, yeye ndiye anayevishikilia vitu vyote na ndiye kichwa cha Kanisa (1:15-18a). Sehemu ya kwanza ya ushairi huu unaomuelezea Yesu imejikita kwenye uumbaji, sehemu inayofuata itajikita kwenye ukombozi/uumbaji mpya. Yeye mwana ni Mwanzo na ni mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu.[3] Yeye ni mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu ili awe mtangulizi katika yote. Hii ni kwa sababu ilimpendeza Mungu utimilifu wake wote ukae ndani yake Kristo na kupitia Kristo avipatanishe vitu vyote na nafsi yake (1:18b-20).

Kwa kuwa ushairi huu unaomtukuza Kristo unahitimishwa kwa kueleza kwamba Kristo ni mpatanishi wa vitu vyote, Paulo anatumia ujumbe huo kama daraja la kuunganisha na mada inayofuata: kwamba Kristo amewapatanisha Wakolosai na Mungu ili awalete mbele zake wakiwa watakatifu, wasio na mawaa wala lawama, ikiwa tu watadumu katika imani na kutokugeuzwa na kuliacha tumaini la Injili, Injili ambayo Paulo amekuwa mhudumu wake. (1:21-23).

Paulo na Timotheo walianza na shukrani na maombi kwa Mungu Baba (1:3-13), kisha wakaelezea ukuu wa Mwana katika uumbaji na katika uumbaji mpya pia (1:14-20). Wakaelezea pia kuhusu wokovu wa Wakolosai ambao ni matokeo ya kazi ya Mwana (1:21-23), na sasa Paulo anajielezea yeye mwenyewe kama mhudumu wa injili (1:24-2:5).

Katika uhudumu wake, Paulo anasema anafurahia mateso anayoyapata kwa ajili ya watu wa mataifa,[4] ambayo yanamjia kwa sababu ya uwakili aliopewa wa kuhubiri neno la Mungu, ambalo lilikuwa ni siri kwa vizazi vya nyuma lakini sasa limefunuliwa, yaani Kristo ndani ya watu wa mataifa. Mwitikio wa mtume Paulo baada ya kufunuliwa kwa siri hii, yaani Kristo ndani ya watu wa mataifa, anafanya bidii (pamoja na wenzake) tena kwa kujitaabisha, kuhubiri kwa njia ya kuonya na kufundisha ili kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo (1:24-29).[5] Baada ya kueleza utumishi wake kwa ujumla, sasa anaeleza utumishi wake kwa kuhusianisha na Wakolosai na majirani zao. Paulo anasema anataka Wakolosai na majirani zao ambao hawajawahi kumuona kwa uso wajue juhudi yake aliyonayo kwa ajili yao ili watiwe nguvu na kuunganishwa katika upendo, ili wapate utajiri wa ufahamu kamili wa kufahamu siri ya Mungu, yaani Kristo, ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimefichwa. Paulo anasema amewaambia Wakolosai kwamba ndani ya Kristo hazina zote za hekima na maarifa zimefichwa ili mtu asije akawadanganya kwa maneno ya kushawishi. Paulo anamaliza aya hii kwa kuwathibitishia tena kwamba anahusika katika maisha yao na anafurahishwa na uthabiti wa imani yao pamoja na kwamba hayuko pamoja nao katika mwili (2:1-5).

Baada ya utangulizi huo mrefu, mtume Paulo anaingia katika ujumbe mkuu wa barua hii. Katika ujumbe mkuu wa barua hii, Paulo anaanza na kuwaamrisha Wakolosai kwamba waendelee kuishi katika Kristo Yesu Bwana wao. Kwa kuwa wamepandwa katika yeye, waendelee kujengwa na kufanywa imara katika imani kama walivyofundishwa (2:6-7). Baada ya kueleza sifa za ukuu wa Yesu na kutoa angalizo wasije wakashawishiwa na maneno, Paulo anatoa amri kwa Wakolosai kwamba wanatakiwa kuendelea katika Kristo. Huu ndiyo ujumbe mkuu wa mtume Paulo kwa Wakolosai. Baada ya amri hiyo chanya, Paulo anaiambatanisha na onyo au amri hasi. Paulo anawaonya Wakolosai kuangalia wasije wakafanywa mateka kwa elimu na madanganyo matupu, ambayo ni mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya awali ya ulimwengu, ambayo si ya jinsi ya Kristo (2:8). Baada ya amri hizo mbili, chanya na hasi, mtume Paulo anatoa sababu. Kwa nini Wakolosai waendelee kuishi katika Kristo na waangalie wasifanywe mateka na elimu iliyo kinyume na Kristo?

Moja, katika Kristo, utimilifu wote wa Mungu unakaa kwa jinsi ya mwili, na hivyo wao wametimilika katika yeye (2:9-10).[6] Pili, katika yeye, Wakolosai wametahiriwa kiroho, kwa kuvuliwa mwili wa nyama. Mwili wa nyama ulivuliwaje? Au Toraha ya kiroho ilifanyikaje? Kwa kuzikwa na kufufuliwa pamoja na kristo kwa njia ya ubatizo (2:11-13a).[7] Kwa kuwa kifo kwa Wakolosai ilikuwa ni kwa sababu ya makosa na kutokutahiriwa kwao, katika kufa na kufufuka pamoja na Kristo sio tu kwamba Wakolosai walitahiriwa, bali pia walisamehewa makosa yote na Mungu. Na ile hati ya mashitaka kutokana na makosa yao ilifutwa kwa kugongomelewa msalabani (2:13b-14). Katika msalaba huo, Mungu hakuishia tu kugongomelea hati ya mashitaka, bali pia ulizivua uwezo “enzi na mamlaka” na akazitangaza hadharani kuonyesha kushindwa kwake (2:15).[8]

Kutoka kwenye utangulizi, Mtume Paulo amekuwa akisisitiza ukuu wa Yesu kwa upande mmoja na upande mwingine amekuwa akitahadharisha dhidi ya mafundisho kinyume na kweli (2:4,8). Sasa mtume Paulo anaweka wazi ni aina gani ya mafundisho kinyume na kweli Wakolosai wanatakiwa kujiepusha nayo. Moja, ni mafundisho yanayotoa hukumu kwa sababu ya vyakula, sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato (2:16-17).[9] Pili, ni mafundisho yenye unyenyekevu wa uongo unaohusisha ibada kwa malaika, ambayo wahubiri wake husimulia maono waliyoyaona kwa kirefu huku wakijisifu katika akili zao za kimwili (2:18-19). Mafundisho haya yanakataliwa na Paulo kwa sababu hayashikamani na Kristo.

Kinyume na mafundisho hayo, Paulo anasisitiza kwamba Wakolosai kama kweli walikufa na Kristo katika ulimwengu wa awali, hivyo hawatakiwa kurudi tena katika mafundisho hayo ya awali, ya kuutesa mwili za ukali (2:20-23). Lakini pia, ikiwa walifufuliwa na Kristo na kuketi naye juu aliko, wanatakiwa kufikiria ya juu Kristo aliko si ya nchi (3:1-4). Kwa lugha nyingine; Kufa pamoja na Yesu kunatutoa kwenye kufuata mafundisho ya ulimwengu wa awali (2:20-23) na kufufuka pamoja na Yesu kunatupa kufikiri mambo ya juu Kristo aliko (3:1-4).

Mafundisho kinyume na kweliMajibu ya Mtume Paulo
Wakolosai 2:16-17 Mnahitaji kufuata sheria za vyakula, sikukuu, mwandamo wa mwezi, na Sabato ili kufikia ukamilifu wa kiroho. Tatizo: Kivuli kinachukuliwa kana kwamba ndiyo kitu halisi.  Wakolosai 2:20-23 Mlikufa pamoja na Kristo katika ulimwengu wa kwanza na mafundisho yake na hivyo hamtakiwa kuwa chini yake.
Wakolosai 2:18-19 Mnahitaji kujinyima (Unyenyekevu wa uongo), kuabudu malaika, na kupata maono maalum ili kufikia kiwango cha juu zaidi cha kiroho. Tatizo: Kutomshikilia Kristo aliye Kichwa.Wakolosai 3:1–4 Mmefufuliwa pamoja na Kristo; yatafuteni yaliyo juu ambako Kristo ameketi mkono wa kuume wa Mungu.

Kutokana na uhalisia huu wa kufa na kufufuka pamoja na Kristo, Mtume Paulo anawaamrisha Wakolosai kuishi iwapasavyo. Kwanza, anaanza na makatazo. Mtume Paulo anawaamrisha “kufisha” matendo ya dhambi zinayohusiana na ngono, na “kuweka mbali” maisha ya dhambi zile yanayohusiana na mahusiano kati ya watu. Dhambi za ngono zifishwe kwa kuwa hizo huleta ghadhabu ya Mungu na ni maisha ya zamani ya Wakolosai. Dhambi za kimahusiano na watu ziwekwe mbali kwa kuwa wao wamevua utu wa zamani na wamevaa utu mpya (3:5-11). Pili, baada ya makatazo hayo, anaingia kwenye maagizo ya mwenendo mpya kama jamii ya waamini. Paulo anawaamrisha kujivika tunda la Roho, ambalo kifungo chake cha ukamilifu ni upendo. Anawaamrisha kwamba amani ya Kristo iwe sababu ya kuamua katikati yao, kwa kuwa wameitiwa katika mwili mmoja. Anawaamrisha kuwa watu wa shukrani. Anawaamrisha kwamba neno la Kristo likae kwa wingi katikati yao, kwa kufundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni. Zaidi, anawasihi kufanya mambo yote kwa jina la Yesu huku wakimshukuru Mungu Baba(3:12-17). Tatu, Mtume Paulo anawaamrisha makundi sita katika familia kuishi iwapasavyo kutokana na nafasi zao katika familia (3:18-17). Mwisho wa sehemu ya ujumbe mkuu, Mtume Paulo, akimhusisha Timotheo (zingatia, lugha ya wingi imerudi tena kama ilivyokuwa katika utangulizi), anawatazamisha Wakolosai nje ya jamii yao (kumbuka, kutoka 2:16–3:17 mambo yaliyozungumziwa yalikuwa yanahusu jamii ya waamini walioko Kolosai). Anawatazamisha kwenye kazi yao ya kimisheni na jamii ya watu wasioamini iliyo karibu nao. Kuhusu wao, Paulo anawaagiza kudumu katika maombi na shukrani, huku wakiwaombea wao wapate nafasi ya kuhubiri neno. Kuhusu watu wasioamini, Paulo anawaamrisha Wakolosai kuishi nao kwa hekima na kuwa na maneno yaliyo na neema yanayofaa pale wanapowajibu (4:2-6).

Waraka huu unafungwa kwa salamu za mwisho, ambapo mbeba waraka, Tikiko, pamoja na Onesimo, ambao ndio watakaowajulisha Wakolosai kuhusu hali ya Mtume Paulo na wafanyakazi wenzake, wanasifiwa (4:7–9). Kisha wafanyakazi wenzake na mtume Paulo katika huduma wanatuma salamu (4:10–14). Mwisho Mtume Paulo mwenyewe anatuma salamu zake na kuagiza Wakolosai na Walaodokia kubadilishana barua, Kanisa la Kolosai kumsisitiza Arkipo kutumia huduma aliyopewa na Bwana na mwisho kukumbuka kufungwa kwake (4:15–18).

MAELEZO YA CHINI


[1] Kutokutajwa kwa kanisa la Hierapoli katika 4:15–16 na kutokuandikwa kwa waraka huko kunaonyesha kuwa kanisa lilikuwa kwenye mchakato wa kupandwa na Epafra kabla hajamfuata mtume Paulo Rumi.

[2] Mzaliwa wa kwanza haina maana ya kiumbe cha kwanza. Mungu katika Kutoka 4:22 analitambulisha taifa la Israeli kama “mzaliwa wa kwanza wangu.“ Lakini pia katika Zaburi 89:27 Mungu anasema atamjalia Daudi kuwa “mzaliwa wangu wa kwanza, kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.“ Sehemu hizi zote hazionyeshi kwamba Israeli wala Daudi ni kiumbe cha kwanza, bali zinaelezea ukuu au nafasi ya upekee juu ya wengine. Hivyo, kuhusu uhusiano wake na viumbe, Yesu ni mkuu juu ya vyote.

[3] Mzaliwa wa kwanza katika watu ina maana ya kwamba Yesu ndiye mwanadamu wa kwanza kufufuka (baada ya kufa) na kuwa mtangulizi wa kuishi maisha mapya ya ulimwengu mpya, ambayo waliokufa katika Yesu watakapofufuliwa watayaishi.

[4] Mateso haya ni kama ambavyo kwa sasa yuko gerezani kwa ajili ya injili kwa watu wa mataifa.

[5] “kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo“ ina maana ya kumfikisha kila mtu katika kilele cha kukomaa ndani ya Kristo siku ile Yesu atakaporudi. Kwa ufafanuzi zaidi, Paulo anafanya bidii kuhakikisha Yesu atakaporudi kila mtu amefikia ukomavu ule unaotakiwa katika Kristo.

[6] Hii ina maana kwamba Wakolosai hawajapungukiwa kitu kwa kuwa Kristo hajapungukiwa kitu.

[7] Tohara ilikuwa ni chapa ya kuthibitisha kwamba mtu husika alikuwa mshirika wa agano la Mungu (Mwanzo 17:10–11), na kutotahiriwa kulikuwa ni kuvunja agano. Hivyo Paulo anawaambia Wakolosai wao ni watu wa agano kwa kuwa wamefanyiwa tohara ya kiroho ambayo hasa Mungu ndiye alikuwa anaitaka (Kumbukumbu la Torati 10:16 na 30:6).

[8] Paulo katika mstari huu anatumia picha ya kijeshi iliyozoeleka wakati wake. “Kuvua enzi na mamlaka” ni kama askari wa adui kupokonywa silaha na kupotezwa uwezo wa kupigana. Kisha “kuzifanya kuwa mkogo” ni kuwapeleka hadharani wakiwa kama wafungwa wa vita katika gwaride la ushindi, wakioneshwa kama wameshindwa wazi mbele ya wote, kuonesha ushindi kamili wa mshindi.

[9] Kumbuka kwamba masharti ya chakula, kushika sikukuu, mwanadamo wa mwezi na sabato ilikuwa ni msingi wa imani ya kiyahudi. Hivyo, mafundisho Paulo aliyokuwa anayapinga yalikuwa yanayohusiana na imani ya kiyahudi

Unakuja hivi karibuni…