MWONGOZO WA KUSOMA UJUMBE WA NABII AMOSI.
MAELEKEZO.
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.
UTANGULIZI.
Amosi ni mmoja kati ya manabii wengi katika historia ya Taifa la Israeli. Manabii hawa wako katika makundi mawili, kundi la kwanza ni manabii wale ambao tuna ujumbe wao au usimulizi wa maisha yao katika vitabu vinavyobeba majina yao (Mfano ni Amosi) na kundi la Pili ni manabii ambao hatuna vitabu vyenye majina yao vinavyobeba ujumbe wao au usimulizi wa maisha yao (Mfano ni Elisha). Mwongozo huu utakusidia kuweza kusoma ujumbe wa Nabii Amosi kama vile ulivyoeleweka na wasikilizaji wa awali. Kabla ya kukuongoza namna ya kusoma unabii wa Amosi tutakueleza kwa ufupi historia ya unabii wa Biblia.
UTANGULIZI WA UNABII.
Pamoja na kwamba Mtu wa kwanza kuitwa nabii katika maandiko ni Ibrahim (Mwanzo 20:6-7), maandiko hayajaonyesha namna gani alifanya kazi hii ya kinabii. Hivyo tunaweza kujifunza vizuri kuhusu unabii baada ya taifa la Israeli kuzaliwa. Baada ya wana wa Israeli kuwa wengi kama ambavyo Mungu alimuahidi Ibrahim[1], Mungu alimtuma Musa na Haruni kumwambia Pharao awaruhusu wana wa Israeli waende kwenye nchi yao. Mungu alimwambia Musa “nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake” Kutoka 7:1-2. Kwa hiyo kutoka hapo tunajifunza kwamba nabii alikuwa ni msemaji kwa niaba ya mtu mwingine (Haruni alikuwa ni msemaji kwa niaba ya Musa). Kwa usahihi kabisa Nabii ni mwanadamu anayesema na wanadamu wengine kwa niaba ya Mungu (Msemaji wa Mungu). Mambo aliyoyanena Nabii hayakuwa maneno yake bali maneno ya aliyemtuma kunena (Mungu). Hii ndio maana Musa anaitwa Nabii kwa kuwa alifanya kazi hii ya kunena na wana wa Israeli kwa niaba ya Mungu[2]. Mungu alikuwa anampa Musa mambo ya kuwaambia wana wa Israeli na Mungu pia akaahidi baada ya Musa atawainulia Israeli Nabii mwingine (Torati 18:15-19). Katika kuahidi Nabii mwingine Mungu pia akawapa Israeli namna ya kutambua Nabii wa kweli na wa Uongo (Torati 18:20-22)[3].
Unabii wa Musa ulioko katika vitabu vitano tunavyoviita vitabu vya sheria ndio msingi wa unabii wote ulioendelea katika Israeli. Msingi huu uko kwenye kile tunakiita “Ahadi za laana na baraka” katika vitabu vya sheria. Ahadi hizi za laana na baraka ndio mambo ambayo manabii waliofuata waliyanena kwa Israeli. Pamoja na kwamba Ahadi hizi za laana na baraka ziko kwenye maeneo mengi katika vitabu vya Torati lakini asilimia kubwa ziko kwenye sura zifuatazo: Mambo ya walawi 26; Kumbukumbu la Torati 28-30. Kwa kuwa Mungu alikuwa amekwisha kuwabariki Israeli (Mwanzo 12:1-3) hivyo ahadi hizi zilikuwa zinaelezea matokeo yatakayotokea (Mungu atakachofanya) kama Israeli watachagua kuiacha sheria ya Mungu (Ahadi za Laana). Kama Israeli baada ya kupata laana hizo watatubu na kumrudia Mungu basi Mungu ataondoa laana na kurejesha baraka (Ahadi za baraka)[4].
Baada ya Musa, Mungu alimuinua Nabii Joshua ambaye kupitia yeye Mungu aliwapa Israeli nchi ya kanaani. Wana wa Israeli walipokuwa kanaani kwa muda wa miaka kadhaa hawakuwa wameungana; yaani makabila yalijiongoza yenyewe[5] na hapo pia kanuni ya “ahadi ya laana na baraka” iliendelea kufanya kazi. Israeli walipokosea laana ziliwafuata na walipotubu baraka zilirejeshwa. Urejesho huu wa baraka hasa ya kujitawala (laana yake ilikuwa ni kutekwa na kufanywa watumwa) uliletwa na Mungu kwa kumtumia mtu aliyeitwa Mwamuzi. Mmoja wapo wa waamuzi hawa alikuwa ni Nabii (Waamuzi 4:4). Mwisho wa kipindi cha waamuzi Mungu alimuinua Nabii Samweli (1 Samweli 3:20-21), mwamuzi wa mwisho (1 Samweli 7:15-17) ambaye kupitia yeye Mungu aliwakubalia Israeli shinikizo lao la kutaka kuwa chini ya mfalme. Kipindi hiki ndio wana wa Israeli (makabila yote 12) waliungana na kuwa taifa moja. Tangu agano la mlima Horebu Israeli ilikuwa na taasisi moja tu ambayo ilikuwa imara, taasisi hiyo ilikuwa ni ukuhani. Hivyo katika wakati huu taasisi nyingine imara ikainuka ambayo ni Ufalme. Taasisi ya unabii ilipata nguvu (Kumbuka ilikuwepo tangu mwanzo) baada ya taasisi ya ufalme kuanza. Taasisi ya ufalme ilisababisha taifa la Mungu kwenda kinyume na agano kwa sehemu kubwa, na kwa kuwa taasisi hii ilikuwa na nguvu ilisababisha mpaka taasisi ya ukuhani kwenda kinyume na sheria ya Mungu. Hivyo taifa zima lilienda kinyume na agano kwa sababu ya ushawishi na nguvu ya taasisi ya ufalme. Kabla ya Taifa la israeli kugawanyika Mungu aliwatumia manabii wengi ikiwemo Samweli na Nathani kulionya Taifa (Au mfalme) kwa habari ya kuacha kwenda kinyume na agano lake. Katika kuonya hayo walitabiri ujio wa “laana” kama watashupaza shingo na walitabiri urejesho wa “baraka” kama watakubali kugeuka kama Musa alivyotabiri katika sura tulizozitaja hapo juu. Baada ya kugawanyika taifa la Israeli na kuzaa mataifa mawili yaani Israeli na Yuda Mungu aliwatumia manabii wengi ikiwepo Shemaya, Ahiya Mshiloni, Eliya na Elisha kabla ya manabii ambao tuna vitabu vyenye majina yao[6]. Manabii wote hao walifanya kazi ile ile ya kuonya Taifa na kutabiri ujio wa “laana” kama hawatasikia sauti ya Bwana lakini pia walitabiri urejesho wa “baraka” Mungu atakaoufanya watakapotubu. Manabii ambao tuna vitabu vyenye majina yao walifanya kazi wakati taifa la Israeli limegawanyika na kuzaa Israeli na Yuda. Nabii wa kwanza alikuwa ni Amosi (Ambaye alitumwa na Mungu kwenda kwenye taifa la Israeli yeye akiwa ni mwenyeji wa taifa la Yuda) na nabii wa mwisho ni Malaki ambaye alitumwa na Mungu kwa ajili ya Taifa la Yuda baada ya kurudi utumwani babeli. Katikati ya hapo ndio tunapata manabii wengine[7].
Jedwali hapo chini litakusaidia kupata taarifa muhimu za manabii hawa ili upate kuelewa ujumbe wao vizuri.
Jina la Nabii | Alitumwa kwa ajili ya Taifa gani? |
Amosi | Israeli |
Hosea | Israeli |
Yona | Ashuru (Mji wa Ninawi) |
Isaya | Yuda |
Mika | Yuda |
Baada ya manabii hao juu Israeli (Makabila kumi) walichukuliwa mateka na dola ya Ashuru na kutawanywa na hapo ndio ulikuwa mwisho wa Taifa | |
Habakuki | Yuda |
Nahumu | Ashuru (Mji wa Ninawi) |
Zefania | Yuda |
Jeremia | Yuda |
Baada ya manabii hao (Wakati wa jeremia) Taifa la Yuda lilipelekwa utumwani Babeli | |
Daniel | Yuda |
Obadia | Edomu |
Ezekiel | Yuda |
Manabii hao juu walifanya kazi wakati Taifa la Yuda likiwa utumwani Babeli | |
Hagai | Yuda |
Zekaria | Yuda |
Joeli | Yuda |
Malaki | Yuda |
Manabii hao juu walifanya kazi baada ya Taifa la Yuda kurudi toka utumwani |
MUKTADHA WA KIHISTORIA WA UJUMBE WA NABII AMOSI.
Taifa la Israeli kwa ujumla wake likihusisha makabila kumi na mbili lilitawaliwa na wafalme watatu yaani Sauli, Daudi na Suleimani. Baada ya Suleimani kufa Taifa liligawanyika katika makundi mawili na kuzaa mataifa mawili yaani Israeli na Yuda. Israeli likiwa ni Taifa lenye watu kutoka katika makabila kumi kati ya yale kumi na mawili na Yuda likiwa ni Taifa lenye watu toka kwenye makabila mawili kati ya yale kumi na mbili yaani kabila la Yuda na Benjamini. Chanzo cha Taifa kugawanyika ni kugeuka moyo kwa mfalme Suleimani (1 Wafalme 11:1-13). Kwa Sababu mfalme Suleimani aligeukia miungu mingine Mungu akaahidi kuugawanya ufalme wake lakini si katika wakati wa kutawala kwake bali wakati wa utawala wa mwanae (1 Wafalme 11:28-43). Ahadi hii ya Mungu ilitimia baada ya Mfalme Suleimani kufa, Israeli ikagawanyika, Taifa la kaskazini (Makabila kumi) likaitwa Israeli na Taifa la kusini (Makabila mawili) likaitwa Yuda. Mtoto wa Suleimani, yaani Rehoboamu akawa ndiye mfalme wa Yuda na mtumishi wa Suleimani, yaani Yeroboamu mwana wa Nebati akawa mfalme wa Israeli (1 Wafalme 12:1-25). Kwa kuwa Hekalu lilikuwa Yerusalemu peke yake (Jerusalem ilikuwa ndani ya Yuda) ilitakiwa waisraeli waende huko kufanya ibada na sikukuu kama Mungu alivyoagiza, lakini Mfalme Yeroboamu akaona kwamba watu wa Israeli wakiwa wanaenda kufanya Ibada huko Yerusalemu mioyo yao itarudi kwa mfalme Rehoboamu wa Yuda hivyo akaamua kuwatengenezea mbadala. Mfalme Yeroboamu akawatengenezea Israeli Sanamu katika miji miwili, moja katika mji wa Betheli na nyingine katika mji wa Dani (1 Wafalme 12:26-33). Mfalme Yeroboamu akatengeneza mfumo mzima wa Ibada kwa kuiga kile Mungu aliachoagiza katika Torati lakini akafanya kinyume na kanuni na masharti ya Mungu. Hivyo Taifa la Israeli likaingia kwenye ibada za sanamu lakini walawi, makuhani na baadhi ya watu wenye imani thabiti walifuata ibada ya kweli Jerusalem iliyoko Yuda (2 Mambo ya Nyakati 11:13-17). Toka wakati huu wa Mfalme Yeroboamu, mwana wa Nebati mpaka wakati wa Mfalme Yeroboamu, mwana wa Yoashi[8] (wakati wa unabii wa Amosi, Amosi 1:1) Taifa la Israeli lilikuwa bado linaendelea kuabudu sanamu pamoja na kwamba Mungu alikuwa anatuma manabii wake kuwaonya na kuwakataza ibada hizo za sanamu. Manabii hao ni kama Eliya (wakati wa mfalme Ahabu na Ahazi) na Elisha (wakati wa mfalme Joramu, Yehu, Yehoahazi na Yoashi). Kwa hiyo Mungu anamtuma Amosi kupeleka ujumbe wakati Taifa likiwa katika hali hiyo kiimani.
Kwa kuwa hili ni Taifa ni vizuri kujifunza pia kuhusu mazingira ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kabla na wakati wa huduma ya Nabii Amosi.
Muktadha wa kisiasa na kiuchumi.
Israeli kabla ya kugawanyika wakati wa Suleimani ilikuwa na utajiri mkubwa wa mali, nguvu ya utawala juu ya mataifa mengine, amani katika Taifa na ilikuwa na eneo kubwa la ardhi/mipaka. Wakati wa utawala wa Suleimani ndio kilele cha ahadi ya Mungu kwa Israeli kilitimia, yaani Israeli walikuwa wengi kama mchanga mchanga wa pwani[9] , wakila na kunywa kwa furaha[10] (1 Wafalme 4:20-21) na walikuwa juu ya mataifa yote kama Mungu alivyoahidi kupitia kinywa cha Musa (Torati 28:1-14). Lakini kwa kuwa Suleimani hakuitii sheria ya Mungu[11] hivyo moyo wake akageukia miungu mingine. Kwa kuwa Mungu alishaweka wazi “laana” zitakazofuata kama Taifa litaacha kushika sheria yake basi laana zikaanza kutokea wakati huo huo wa Suleimani; Moja Bwana akainua maadui juu ya Suleiman. Maadui hawa walikuwa ni Hadadi Mwedomi (Uzao wa mfalme wa Edomu) na Rezoni mwana wa Eliada (Aliyeujenga mji wa Dameski katika shamu) na Jeroboam, mwana wa Nebati (Mtumwa wa Suleimani). Kuanzia hapo na kuendelea Israeli ikawa katika vita vya mara kwa mara na maadui, hali hiyo ikapelekea kupotea kwa utajiri wake. Vita hizi vilihusisha maadui wa nje wa Israeli na vita vya waisraeli wao wenyewe baada ya kugawanyika (yaani vita kati ya Yuda na Israeli, 1 Wafalme 14:30).
Kwa kuwa Israeli (Taifa la kaskazini) iliendelea kuabudu sanamu pamoja na Mungu kutuma manabii wake kama Eliya na Elisha, Mungu akaanza kupunguza mipaka ya Israeli. Kuanzia wakati wa mfalmeYehu mpaka wakati wa mtoto wake (mfalme Yehoahazi) Mungu aliruhusu Israeli wanyang’anywe ardhi (2 Wafalme 10:32-33) na wawe chini ya utawala wa Hazaeli mfalme wa shamu. Hazaeli mfalme wa Shamu aliwatesa Israeli kwa muda mrefu wakati wa mfalme Yehoahazi kiasi cha jeshi la Israeli kubaki na wapanda farasi hamsini, na magari kumi, na askari elfu kumi waendao kwa miguu (2 Wafalme 13:7). Pamoja na kwamba Mungu akawatoa Israeli chini ya utawala huu wa Shamu lakini bado Israeli hawakumrudia Mungu, Hivyo Mungu akawaacha waendelee kuteswa na mfalme wa Shamu. Kupitia mjukuu wa mfalme Yehu yaani Yehoashi Israeli ikaanza kurudisha mipaka/ardhi iliyonyang’anywa (2 Wafalme 13:24-25) na ikashinda vita dhidi ya Yuda (2 Wafalme 14:8-16). Na jambo hili la kurudisha ardhi lilifanikiwa sana wakati wa utawala wa Jeroboamu, mwana wa Yehoashi (2 Wafalme 14:21-29). Wakati huu wa utawala wa Jeroboamu mwana wa Yehoashi ndio wakati Nabii Amosi alifanya unabii wake na ndio wakati pia Nabii Yona alifanya kazi yake ya unabii, na tukio la Israeli kurudisha ardhi yake lilikuwa ni utimilifu wa unabii wa nabii Yona. Hivyo wakati huu wa utawala wa Jeroboamu, mwana wa Yehoashi ulikuwa ni wakati wa utajiri mkubwa (Ambao ulianza kupatikana wakati wa baba yake Yehoashi) na wakati wa kujitawala katika ardhi yao walioirejesha.
Muktadha wa kijamii.
Kama tulivyoona hapo juu katika muktadha wa kisiasa na kiuchumi kwamba wakati huu wa Nabii Amosi ndio wakati Israeli chini ya mfalme Jeroboam, mwana wa Yehoashi ilikuwa na utajiri uliorejeshwa, ardhi iliyorejeshwa na utulivu mbali na vita pamoja na kuwa na jeshi imara. Haya yalipelekea utajiri kuwa kwa watu wachache hasa watawala na wengine kuendelea kuwa chini ya umaskini. Hii ni kwa sababu kulikuwa na udhalimu mwingi wa kijamii kama vile rushwa na kunyimwa haki wenye haki na wahitaji (Amosi 2:7 na 5:12), kuwanyonya wanyonge na kuwakandamiza wahitaji (Amosi 4:1), kuwatoza maskini kodi zisizo za haki (Amosi 5: 11), na udanganyifu mkubwa katika biashara (Amosi 8:5). Hivyo Nabii Amosi anapeleka ujumbe wa Mungu kwenye taifa ambalo lina udhalimu mkubwa katika jamii.
Hivyo kwa ujumla wakati wa utawala wa mfalme Jeroboamu, mwana wa Yehoashi ambao ndio wakati wa Nabii Amosi Taifa la Israeli lilikuwa na sifa zifuatazo;
- Taifa lilikuwa linafanya ibada za samanu katika Dani na Betheli kama zilivyotengenezwa na mfalme Jeroboamu, mwana wa nebati.
- Taifa lilikuwa na utajiri mkubwa uliorejeshwa (japo haukuwa kama ule wa wakati wa Suleimani).
- Taifa lilikuwa huru mbali na maadui na lilikuwa na jeshi imara
- Taifa lilikuwa na udhalimu mkubwa katika jamii kama vile rushwa, kukosekana kwa haki, unyonyaji na udanganyifu katika biashara.
UJUMBE MKUU WA AMOSI.
Ujumbe mkuu wa Nabii Amosi ulikuwa ni kutangaza hukumu inayokuja kwa taifa la Israeli kwa sababu ya dhambi zao. Dhambi kubwa nabii anazozitaja ni ibada ya sanamu/miungu mingine na udhalimu katika jamii/ukikwaji wa haki katika jamii. Kwa sababu ya mambo haya mawili Mungu anatangaza kuachilia laana kama alivyoahidi kupitia nabii wake Musa, na kilele cha laana hizo ni taifa kuvamiwa, kupigwa na kupelekwa utumwani. Pamoja na hukumu hio, ujumbe wa Mungu ni kwamba baada ya hukumu atarejesha taifa na kurejesha baraka.
Ukiacha taifa la Israeli Mungu pia anatangaza hukumu kwa matifa mengine yaliyozunguka Israeli. Wao wanatangaziwa hukumu kwa sababu ya mauaji waliyofanya katika vita mbalimbali.
MPANGILIO WA KITABU.
Namba | Maandiko | Maelezo |
1 | 1:1-2 | Utangulizi |
2 | 1:3-2:16 | Maneno ya Bwana kwa Mataifa. |
3 | 3:1-6:14 | Maneno ya Bwana kwa Israeli |
a. | 3:1-15 | Kwa kuwa ni taifa teuli ndio maana utahukumiwa |
b. | 4:1-13 | Pamoja na hukumu Israeli hawakumrudia Mungu |
c. | 5:1-6:14 | Maombolezo ya Israeli |
4 | 7:1-9:10 | Maono juu ya hukumu ya Israeli |
a. | 7:1-3 | Nzige waharibuo |
b. | 7:4-6 | Moto ulao |
c. | 7:7-17 | Timazi |
d. | 8:1-14 | Kapu lenye matunda yaliyoiva |
e. | 9:1-10 | Hukumu ya Mungu karibu na madhabahu |
5 | 9:11-15 | Ahadi ya urejesho |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.
Mwandishi wa kitabu ameanza na utangulizi kabla ya kwenda kwenye ujumbe mkuu, Utangulizi uko kwenye sehemu mbili yaani utangulizi wa kitabu na ujumla wa ujumbe wa kitabu. Katika Utangulizi wa kitabu, mwandishi anatoa utangulizi unaoeleza ujumbe huu aliouandika ulitolewa na nani, kwa ajili ya Taifa gani na kwa wakati gani (1:1). Na baada ya hapo anatoa ujumla wa ujumbe wake wote (1:2).
Katika Sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu (1:3-2:16), Mungu kupitia Amosi anatangaza hukumu yake inayokuja juu ya mataifa nane kwa maovu waliyoyafanya hapo nyuma. Mataifa sita ambayo sio sehemu ya Israeli wanatangaziwa hukumu kutokana na maovu yao yanayohusiana na mauaji walioyafanya katika vita. Mataifa ya Israeli na Yuda wanatangaziwa hukumu kwa kuiacha sheria ya Mungu wao. Katika kutangaza Hukumu hizo Amosi ametangaza kwa mfululizo ufuatao
- Utangulizi “Haya ndiyo asemayo Bwana”
- Tangazo la hukumu “Kwa makosa matatu ya ……., naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate”
- Kutajwa kwa Makosa yao
- Maelezo ya Hukumu itakavyokuwa
- Hitimisho “……. asema Bwana”
Hukumu inaanza kutangazwa kwa dameski (1:3-5), ikifuatiwa na Gaza (1:6-8), tiro (1:9-10), Edomu (1:11-12), amoni (1:13-15) na Moabu (2:1-3), mataifa yanayozunguka Israeli na Yuda. Tangazo la hukumu kwa mataifa linaishia kwa kutangaza hukumu kwa mataifa yake Mungu, yaani Yuda (2:4-5) na Israeli (2:6:16).
Katika sehemu ya pili ya ujumbe mkuu (3:1-6:14), Mungu anaendelea kutangaza hukumu juu taifa la Israeli tu. Sehemu hii ina hotuba tatu za maelezo ya hukumu kwa Israeli ambazo hotuba moja na nyingine zinatenganisha na maneno “Lisikieni neno hili…” (Angalia 3:1, 4:1 na 5:1). Katika Hotuba ya kwanza ya hukumu, Mungu anaweka wazi kwamba atawapatiliza maovu watu wake Israeli kwa sababu wao ni maalumu kwake (3:1-2). Na kwa kutumia maswali ya balagha[12] mwandishi anawathibitishia ujio wa hukumu ya Mungu juu ya Israeli na kuthibitisha ukweli wa tangazo hilo linalotolewa na manabii kama tahadhari kwao kabla ya hukumu hiyo kuja (1:3-8). Hukumu ya Mungu itahusisha kuvunjwa kwa ngome na majumba ya wana wa Israeli kwa sababu ya dhambi zao ambazo majirani wao wanaalikwa kuzishuhudia (3:9-11). Israeli itapigwa na wachache ndio watasalimika kama vile mchungaji apokonyavyo kinywani mwa simba miguu miwili, au kipande cha sikio (3:12). Pamoja na kwamba Hukumu hii itapiga nyumba za wana wa Israeli pia itapiga madhabahu zilizoko huko betheli (3:13-15).[13]
Hotuba ya pili ya hukumu ya Mungu juu ya Israeli inaanza kwa kutangaza kutolewa kwa watu wa Israeli[14] waliopo kwenye mji mkuu wa taifa, yaani Samaria na kupelekwa utumwani Harmoni (4:1-3). Mungu pia anawaonyesha Israeli kwamba sadaka zao na zaka wanazozitoa huko Betheli na Gilgali ni upotofu na anawaonya kwa kuwataka waendelee kufanya ibada hizo (4:4-5). Baada ya hapo Mungu anawajulisha Israeli mapigo ambayo yeye aliyaachilia kwao ili yamkini wamrudia yeye, lakini hawakumrudia (4:6-11). Mwisho wa hotuba hii Mungu anawahakikishia Israeli kwamba atawatenda zaidi ya yale mapigo ya kwanza kwa kuwa yeye Mungu ni mkuu na wa pekee (4:12-13).
Hotuba ya tatu ya hukumu juu ya Israeli inaanza kwa kutangaza maombolezo juu ya Israeli, ambayo itaanguka kwa kupigwa na kubakiwa na miji yenye watu wachache (5:1-3). Kabla ya hilo kutokea Mungu anawaita wamtafute yeye ili waishi na akiwakataza wasiende kwenye sanamu (5:4-6). Kwenda kwenye sanamu kumewafanya Israeli kugeuza hukumu na kuangusha haki chini (5:7). Huyu Mungu anayetangaza hukumu ni muumbaji mkuu ambaye amefanya makubwa, tofauti na sanamu wanazoziabudu huko Betheli. hivyo hili la kuhukumu Israeli ni dogo ndio maana bado anawaita wamrudie (5:8-9).[15] Baada ya kueleza ukuu wa Mungu Amosi anarudi kuelezea makosa na dhambi zinazoendelea kutokana na kugeukia sanamu na kwa hizo Mungu anatangaza hukumu juu ya Israeli (5:10-13). Kwa kurudia tena Mungu anawaita Israeli kugeuka na kutenda mema ili Mungu aghairi hukumu yake (5:14-15). Kwa msisitizo Mungu anatangaza maombolezo kwa Israeli ambayo yataenda mpaka kwa wakulima (5:16-17) kama alivyotangaza mwanzoni (5:1-3).
Wale wanaotamani siku ya Bwana wakidhani itakuwa ni siku njema Mungu anawaonya na kuwaonyesha kwa kutumia lugha ya picha jinsi siku hiyo itakavyokuwa mbaya (5:18-20). Hii ni kwa sababu Mungu anachukia kila jitihada za kidini wanazozifanya (5:21-23) na badala yake anataka haki na hukumu kutawala (5:24). Kuwaonyesha kwamba jitihada za kidini kama kutoa dhabihu na sadaka sio kitu Mungu anachokihitaji kutoka kwao anauliza swali la balagha, je Israeli walimpa Mungu vitu hivyo wakati wakiwa safarini kule jagwani? (5:25) Jibu ni hapana. Na kwa sababu hawataki kumtafuta Mungu kama ambavyo amekuwa akiwataka kufanya hivyo, Mungu anawaambia watakwenda utumwani pamoja na hiyo miungu yao (5:26-27).
Baada ya hayo Mungu anatoa ole kwa kundi maalum, kundi la viongozi ambao wanaishi maisha ya kustarehe katika Samaria. Ole hii inakosoa wanavyoishi na inawatangazia kwamba wao watakuwa wakwanza kwenda utumwani (6:1-7). Watakwenda utumwani kwa sababu watavamiwa na taifa lingine ambalo litapiga majumba na kuuwa watu kiasi ambacho mabaki wachache watakataa kutaja jina la Bwana (6:8-14).
Sehemu ya tatu ya mjumbe mkuu (7:1-9:15), Mungu anamuonyesha Nabii Amosi maono ya hukumu yake juu ya Israeli na kumalizia na tumaini la urejesho. Katika sehemu hii kuna maono ya aina tano Nabii Amosi aliyoyaona. Maono mawili ya awali yanaonyesha Mungu alivyoghairi mabaya kwa sababu ya maombezi ya Nabii Amosi na maono yaliyobaki yanaonyesha hukumu ya Mungu iliyotayali isiyoepukika. Maono ya kwanza yanahusu Mungu alivyoghairi kuleta njaa baada ya maombezi ya Nabii Amosi (7:1-3). Maono ya pili yanahusu Mungu kughairi kuleta ukame baada ya maombezi ya Nabii Amosi (7:4-6). Maono ya tatu yanahusu Mungu kumuonyesha Nabii Amosi jinsi atakavyoipiga Israeli (7:7-9). Baada ya Nabii Amosi kutangaza maono ya hukumu aliyoiona basi kuhani wa ibada za Sanamu zilizokuwa zinafanyika Betheli, Amazia akatoa katazo kwa Nabii Amosi kuendelea kutabiri na pia alitoa taarifa kwa mfalme kuhusu utoaji wa unabii wa Amosi (7:10-17). Maono ya nne yanahusisha Mungu kumuonyesha Nabii Amosi kwamba Israeli wako tayari kwa hukumu kama kapu lenye matunda yaliyoiva ambayo yako tayari kwa kuliwa. Katika maono haya kuna maelezo mengi ya Mungu ya namna gani atawapiga Israeli na kwa nini anaachilia hukumu hiyo (8:1-14). Maono ya tano yanahusu Mungu kumuonyesha Nabii Amosi jinsi atakavyoipiga Israeli kiasi kwamba watu watakuwa hawana pa kukimbilia popote watakapoenda watakufa (9:1-6).
Lakini pamoja na kutangaziwa hukumu Israeli tangu mwanzo wa huduma ya Nabii Amosi, Mungu anatoa ahadi kwamba hukumu yake sio mwisho wa Israeli bali anatangaza na tumaini la urejesho baada ya hukumu yake kupita. Utakuja wakati ambao Israeli watarudi kutoka uhamishoni, watarudishwa kwenye miji yao, wataijenga na kufurahia baraka za Mungu za kuzaa matunda na usalama kwa watu wake (9:7-15). Na hapo ndio mwisho wa ujumbe wa Nabii amosi.
FOOTNOTES
[1] Mungu alimuahidi Ibrahim Taifa kubwa (Mwanzo 12:1-3), Taifa lenye watu wengi (Mwanzo 15:1-6) na ahadi hii ilianza kutimia huko Misri (Kutoka 1:7-22)
[2] Kumbuka Mungu alitaka kunena na watu wote wa Israeli lakini Israeli walitaka wasikie kutoka kwa Musa na sio kutoka kwa Mungu kwa kuwa katika mlima Horebo Mungu alishuka na utisho mkubwa (Kutoka 20:19-26)
[3] Petro anasema mambo haya mawili katika waraka wake wapili, kwamba manabii hawakunena mambo yao bali walinena yaliyotoka kwa Mungu na pia kulikuwa na manabii wa uongo (2 Petro 1:19-2:1)
[4] Kwa kuwa huu ni muongozo tu hatutaweza kuchambua ahadi hizo za laana na baraka lakini ni muhimu wewe uzisome ili uweze kuelewa vitabu vya manabii. Manabii walichotabiri/kusema kuhusu Israeli kina utegemezi mkubwa katika sura hizi (Walawi 26 na Torati 28-30)
[5] Inakadiliwa kuwa Israeli hawakuungana kama Taifa moja zaidi ya miaka 180
[6] Kuna Manabii wengine Biblia haitawataja kwa majina. Popote atakaposoma na kuona biblia inasema “Mtu wa Mungu” au “Mwonaji” basi ujue inamuelezea Nabii. (1 Samweli 9:8-14)
[7] Manabii wengine Mungu aliwatuma nje ya Taifa la Israeli, manabii hawa ni kama Yona, Obadia na Nahumu
[8] Kuna Jumla ya wafalme 11 katikati ya kipindi cha ufalme wa Yeroboamu, mwana wa Nebati na Yeroboamu, mwana wa Yoashi. Kipindi hicho kina Zaidi ya miaka 170. Hivyo toka Taifa limeingia kwenye ibada ya sanamu mpaka ujio wa ujumbe wa Mungu kupitia Amosi ni zaidi ya miaka 170 imepita.
[9] Mungu alitoa ahadi hii kwa Ibrahim (Mwanzo 13:14-17)
[10] Kama Mungu alivyowaahidi nchi ya maziwa na Asali (Kutoka 3:8)
[11] Mungu aliwaagiza Waisraeli wasioe nje ya Israeli (Kumbukumbu la Torati 7:1-4). Hata hivyo, Sulemani alifanya hivyo kinyume na agizo hilo (1 Wafalme 11:1-2). Pia, Mungu aliagiza mfalme asioe wanawake wengi na asijikusanyie mali nyingi (Kumbukumbu la Torati 17:14-19), lakini Sulemani alifanya yote hayo kinyume na maagizo ya Mungu (1 Wafalme 10:14, 26-27; 11:3-4).
[12] Swala balagha ni swali ambalo halitolewi kwa lengo la kupata jibu moja kwa moja, bali badala yake kutumika kufanya hoja, kuchochea fikra, au kusisitiza wazo fulani au hoja. Muuliza swali huwa anajua wasikilizaji wake wanajua jibu la swali analouliza.
[13] Kumbuka Madhabahu za Betheli zimetejwa kwa kuwa huu mji ndio moja ya mji ambao mfalme Yeroboamu alijenga madhabahu za waisraeli kufanya ibada kama mbadala wa Hekalu za kule Jerusalem (1 Wafalme 12:26-33). Hivyo ibada za sanamu zilikuwa zinafanyika katika mji huu kama tulivyoeleza katika utangulizi
[14] Lugha ya picha imetumika kuwataja wahusika wa hukumu hii. “Ng’ombe wa bashani” ndio lugha iliyotumika ikimaanisha wanawake wa wakuu wa mji wa Samaria ambao wanawaonea maskini na wahitaji.
[15] Kilimia na Orioni ni makundi nyota ambayo waandishi wa Biblia wamekuwa wakiyataja pale Mungu anapoelezea ukuu wake (Angalia pia Ayubu 9:5-9 na 38:31-32).
Unakuja hivi karibuni….