Ezekieli – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA UJUMBE WA NABII EZEKIELI

MAELEKEZO

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe, mwamini mwenzangu, unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako; usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa kila mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa mambo yanayoweza kukuongoza kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayotajwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno, tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo. Utaona maelekezo ya ziada yatakayokusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba hiyo.

e. Mpangilio wa mwongozo huu si mpangilio wa mwandishi. Mpangilio wa mwongozo unakusaidia tu kuona mabadiliko ya mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huu wala kwa mpangilio wa sura na mistari.

UTANGULIZI

Kitabu cha nabii Ezekieli ni moja ya vitabu vinavyoitwa vitabu vya manabii wakubwa. Manabii hawa wanaitwa wakubwa kwa sababu vitabu vyao ni virefu katika maandishi ya ujumbe kuliko vitabu vya manabii wanaoitwa manabii wadogo. Manabii hawa ni Isaya, Yeremia, Danieli, na Ezekieli mwenyewe. Kati ya manabii hawa wote, basi kitabu cha Ezekieli ni kitabu chenye umaarufu mdogo katika imani ya Kikristo kuliko vitabu vya manabii hao wengine. Ni mara chache sana kuona kitabu hiki kinasomwa katika makusanyiko ya waamini na ni mara chache pia kuona kitabu hiki kinanukuliwa. Sababu za umaarufu wake mdogo zinaweza kuwa nyingi, lakini chache ni kama zifuatazo: kutokuwepo kwa nukuu fupi fupi za kutoa faraja au motisha kwenye maisha ya kila siku kama vile kitabu cha Yeremia; kutokuwepo kwa simulizi za kutosha za faraja na motisha kama vile kitabu cha Danieli; kutokuwepo kwa unabii wa moja kwa moja kumhusu Masihi kama kitabu cha Isaya; na, mwisho, matumizi makubwa ya lugha ya picha, ambayo yanafanya usomaji wake kuwa mgumu.

Kwa kuwa waamini wengi wanaamini juu ya mamlaka ya Neno la Mungu kama ilivyo katika vitabu 66 vya Biblia, kitabu hiki hakipaswi kupuuzwa kwa sababu ni Neno la Mungu, na kina ujumbe muhimu kwa dunia yetu ya sasa. Zaidi ya hayo, kitabu hiki ni msingi mzuri wa kuelewa kitabu cha Ufunuo wa Yohana. Pamoja na kwamba hakuna nukuu ya moja kwa moja kutoka katika kitabu hiki ndani ya vitabu vya Agano Jipya, kitabu cha ufunuo kina muundo, matukio na jumbe zinazofanana sana na kitabu hiki.[1]

MUKTADHA WA KIHISTORIA WA UJUMBE WA NABII EZEKIELI

Nabii Ezekieli alizaliwa katika taifa la Yuda, kipindi cha utawala wa Mfalme Yosia. Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho kulikuwa na mageuzi ya kidini yaliyoongozwa na Mfalme Yosia; mageuzi hayo yalilenga kuondoa ibada za sanamu na kuimarisha ibada ya kweli Yerusalemu (2 Wafalme 22-23). Kabla ya Mfalme Yosia, taifa la Yuda lilikuwa limezama katika ibada za sanamu zilizoshamiri kiasi kwamba sanamu zilisimamishwa hadi katika hekalu takatifu la Mungu. Mfalme Manase (Babu wa Mfalme Yosia), ambaye alitawala kwa miaka hamsini na tano, ndiye aliyesababisha ibada hizi za sanamu kuota mizizi mikubwa katika taifa la Mungu. Tofauti na baba yake na babu yake, Yosia alijitahidi kuondoa sanamu ambazo watu walizifanyia ibada na kurudisha ibada ya kweli hekaluni.

Kwa kuwa Ezekieli alizaliwa katika kipindi hiki cha uamsho na alikuwa mzaliwa wa familia ya Walawi, aliandaliwa kufanya kazi ya kikuhani hekaluni pale atakapofikia umri wa miaka thelathini. Hata hivyo, ndoto hii ya kufanya kazi yake ya kikuhani hekaluni haikutimia kwa sababu, kabla ya kufikisha umri wa kuruhusiwa kufanya kazi hiyo, baadhi ya watu wa Yuda, akiwemo yeye mwenyewe Ezekieli, walichukuliwa mateka na Mfalme Nebukadneza (2 Wafalme 24:10-16). Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa watu wa Yuda kuchukuliwa mateka na kupelekwa utumwani. Katika awamu ya kwanza, tukio hili lilihusisha watu kama Danieli, Meshaki, na Abednego (2 Wafalme 24:1-4).

Kwa hiyo, kabla Ezekieli hajaanza kazi yake rasmi ya kinabii, tayari taifa lilikuwa limepitia awamu mbili za watu kuchukuliwa na kupelekwa uhamishoni. Haya yote yalikuwa ni utimilifu wa unabii ambao Mungu aliutoa kupitia vinywa vya manabii wake, akiwemo Yeremia. Kwa sababu ya dhambi zao za ibada ya sanamu, Mungu aliahidi kuwapeleka Yuda utumwani. Kabla ya Yosia na baada yake taifa liliendelea na ibada ya sanamu na hivyo Mungu akawaadhibu kwa kuwapeleka utumwani Babeli.

Pamoja na watu kupelekwa utumwani kutokana na dhambi zao, hasa dhambi ya kuabudu miungu mingine na sanamu, watu wa Yuda bado walikuwa na imani thabiti kwamba Mungu ana wajibu wa kuwaokoa kutoka uhamishoni, na hata uhamisho huu waliuona kama jambo la muda mfupi tu. Imani yao ya usalama wa milele ilitokana na imani ya uwepo wa uhusiano usioweza kutenganishwa kati ya Mungu (Yahweh), eneo (nchi ya Kanaani), na watu wake (taifa la Israeli/Yuda). Kwa ufafanuzi, watu wa Yuda waliamini kwamba Mungu ambaye ameweka uwepo wake Yerusalemu kwa njia ya hekalu hawezi kuruhusu uwepo wake kutolewa Yerusalemu. Pili, Mungu ambaye amefanya agano la milele na watu wake katika mlima Sinai hawezi kuwaacha watu wake waonewe na maadui zao. Zaidi, Mungu ambaye amefanya agano la milele na Daudi hawezi kupindua ahadi yake kwa Daudi; Daudi kuwa na mfalme katika taifa la Yuda siku zote milele na milele.

Imani hii ya usalama wa milele kwa sababu ya Agano la Mungu juu yao ilipewa nguvu zaidi na manabii waliokuwa wanatabiri kinyume na manabii wa kweli wa Mungu (Yeremia 6:14; 8:11; 14:13-14; 23:16-17). Mfano wa manabii hawa ni kama nabii Hanania (Yeremia 28). Sasa Ezekieli alikuwa uhamishoni pamoja na watu wengine wa Yuda ambao walikuwa na imani kwamba kwa sababu ya agano lao na Mungu, Mungu lazima atawaokoa na kuwarejesha katika ardhi yao. Waliamini uhamisho huu ni wa muda mfupi tu, na kwa sababu bado Mji wa Yerusalemu ulikuwa umesimama, pamoja na kwamba watu wake walikuwa wamechukuliwa mateka, waliamini watarudi na wataendelea na maisha yao. Katika wakati huo, ndipo Mungu alimtuma Ezekieli kwenda kutoa unabii kwa wenzake walioko huko utumwani. Mungu alimtuma kuwaambia kwamba mji mzima wa Yerusalemu utabomolewa, Mungu ataondoa uwepo wake katika hekalu, sehemu aliyoichagua mwenyewe kuwa maskani yake, hekalu litabomolewa, watu watauawa na mabaki yote ya watu wa Yuda watachukuliwa mateka.

Baada ya mambo hayo kutokea, yaani mji wa Yerusalemu kuvamiwa na Babeli, kubomolewa, na kila kitu kilichokuwa ndani yake, likiwemo hekalu, ujumbe wa Ezekieli ukabadilika. Ujumbe wake baada ya kutimia kwa hayo ukawa ni wa utabiri wa matumaini ya urejesho. Ujumbe huu wote aliutoa ndani ya kipindi cha miaka ishirini na miwili akiwa uhamishoni, akiwalenga watu waliokuwa uhamishoni.

UJUMBE MKUU WA NABII EZEKIELI

Ujumbe mkuu wa Ezekieli kwa watu wa Yuda/Israeli waliopo uhamishoni Babeli na waliobaki Yerusalemu ni kuwa hukumu ya Mungu juu ya Yerusalemu inakuja na haiepukiki. Mji wa Yerusalemu utazingirwa na Babeli, watu wake watapigwa na kuuawa, wengine watachukuliwa mateka, na hatimaye mji wa Yerusalemu na hekalu vitabomolewa. Haya yote yatatokea kwa sababu ya maovu na dhambi za watu wake za muda mrefu (1:1-24:27). Si Yerusalemu pekee itakayohukumiwa, bali pia majirani wa Israeli na Yuda watahukumiwa (26:1-32:32). Hata hivyo, habari ya Yuda/Israeli haitaishia kwenye hukumu, bali kwenye urejesho Mungu atakaoufanya. Watu wake watarudi nyumbani kutoka utumwani, utukufu wa Mungu utarejea katika hekalu lake, haki na utawala bora utarejea, na mji mpya wa Yerusalemu utajengwa (33-48). Mambo haya yote Mungu atayatekeleza kwa sababu anataka Yuda/Israeli wajue kuwa yeye ni Bwana, na mataifa mengine pia yajue kuwa yeye ni Bwana.

MPANGILIO WA KITABU

SEHEMU YA MAANDIKOMAELEZO
1:1-3:27Kuitwa kwa Ezekieli katika kazi ya kinabii
 
4:1-24:27HUKUMU INAKUJA JUU YA YUDA/ISRAELI
4:1-5:17Matendo ya Ishara I
6:1-7:27Hukumu inakuja
8:1-11:25Kuondoka kwa uwepo wa Bwana Yerusalemu
12:1-12:28Matendo ya Ishara II
13:1-14:22Hukumu isiyoepukika kwa watu na manabii wa uongo
15:1-19:14Mifano/Mithali tano.
20:1-24:27Hukumu juu ya mji umwagao Damu
  
25:1-32:32HUKUMU JUU YA MATAIFA
25:1-17Unabii juu ya Amoni, Moabu, Edomu na Wafilisti
26:1-28:26Unabii juu ya Tiro na Sidoni
29:1-32:32Unabii juu ya Misri
  
33:1-48:17UREJESHO BAADA YA HUKUMU
33:1-33Kuanguka kwa Yerusalemu na mwitikio wa watu
34:1-31Urejesho wa uongozi bora wa milele
35:1-36:15Urejesho wa Ardhi
36:16-38Urejesho wa heshima ya jina la Bwana
37:1-14Urejesho wa watu/Ufufuo wa watu
37:15-28Urejesho wa taifa moja la Bwana
38:1-39:29Maadui wote wa Bwana na Israeli watapigwa
40:1-43:17Urejesho wa hekalu na uwepo wa Bwana
43:18-46:24Sheria za maisha mapya
47:1-48:30Nchi mpya na mji mpya

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI

Ezekieli anapata mwito wa kazi yake ya kinabii akiwa uhamishoni Babeli, miaka mitano baada ya kuchukuliwa mateka pamoja na mfalme Yehoyakini (2 Wafalme 24:8-17).[2] Mwito huu unaanza kwa maono Mungu aliyomfunulia Ezekieli alipokuwa amefikisha miaka thelathini (1:1-3). Ezekieli aliona wingu la upepo mkali lenye moto uliozungukwa na mwanga mkali. Ndani ya wingu hilo, aliona viumbe vinne vya ajabu. Maajabu yao yalikuwa kwamba walikuwa na miguu, mabawa, mikono, na nyuso za kipekee. Kila kiumbe alikuwa na nyuso nne—uso wa binadamu, simba, ng’ombe, na tai. Viumbe hawa walikuwa na muonekano wa kung’aa sana na uwezo wa kutembea kwa kasi kama umeme (1:4-14).

Kila kiumbe kilibebwa na gurudumu moja. Magurudumu haya yalikuwa na sifa zifuatazo: Kwanza, muonekano wake ulikuwa kama gurudumu ndani ya gurudumu lingine, na hivyo yaliweza kutembea pande zote bila kugeuka. Pili, yalikuwa na mng’ao kama wa vito vya thamani viitwavyo zabarajadi. Tatu, yalikuwa na macho pande zote. Viumbe vilipotembea, magurudumu yalitembea; viumbe viliposimama, magurudumu yalisimama pia. Mwendo wao wote uliongozwa na Roho (1:15-21).Juu ya viumbe hawa kulikuwa na kitu kama anga, ambacho kilikuwa na kiti cha enzi. Katika kiti hicho cha enzi kinachong’aa sana, kulikuwa na mfano wa mwanadamu juu yake. Hivi ndivyo Mungu alivyojidhihirisha kwa Ezekieli, na alipoona maono hayo, alianguka kifudifudi. (1:22-28).[3]

Baada ya kuanguka, Ezekieli anapewa nguvu na Roho kusikiliza mwito wake. Mungu anamwambia kwamba anamtuma kwa nyumba ya Israeli/Yuda, watu waliomwasi yeye. Pamoja na uasi wao, Ezekieli anatakiwa kufikisha ujumbe wa Mungu kwao bila woga (2:1-7). Mwito huu uliambatana na Ezekieli kulishwa gombo (kitabu chenye maandishi) ambalo lilikuwa limeandikwa maombolezo, na vilio, na ole (2:8-3:3). Mungu anatoa msisitizo kwa Ezekieli kwamba anamtuma kwa watu waasi, watu ambao hawatasikiliza ujumbe wake pamoja na kuwa ni watu wa lugha moja na yeye. Zaidi, Mungu anamjulisha Ezekieli kwamba atampa uwezo wa kukabiliana na kupuuzwa (3:4-11).[4] Baada ya hayo, Roho akamuinua Ezekieli, akamsafirisha na mwishowe akawafikia wenzake, na akakaa kati yao ndani ya siku saba akiwa katika mshangao mkubwa wa maono aliyoyaona na wa kazi aliyopewa (3:12-15).

Baada ya siku saba, Mungu akamfafanulia zaidi Ezekieli wito wake. Wito wake ni kuwa mlinzi wa Mnara[5] wa Israeli, yaani roho za watu wabaya na mwenye haki ziko juu yake. Hivyo, anatakiwa kufanya kama Bwana atakavyomtuma afanye kwa kila mtu, yaani mtu mbaya na mwenye haki (3:16-21).

Mwisho wa habari ya mwito wa Ezekieli unafungwa na maono ya mwisho aliyoyaona kabla hajaanza sasa kupokea ujumbe wa kusema na watu wa uhamishoni. Ezekieli aliambiwa aende sehemu tambarare, na huko akaona maono kama yale aliyoyaona mwanzoni, na mwishowe akaanguka tena kifudifudi. Roho akampa nguvu tena na akasikia masharti matatu aliyopewa na Mungu: kujifungia ndani, kufungwa mwilini ili asiweze kujumuika na wenzake, na kuwa bubu mpaka Bwana atakapompa ujumbe wa kunena. (3:22-27).

Baada ya wito wake kukamilika, Ezekieli sasa anapewa ujumbe wa kunena kwa watu wa Yuda waliokuwa uhamishoni. Hata hivyo, ujumbe wake unawasilishwa kupitia matendo ya ishara, ambayo Mungu alimpa kufanya, na kila tendo lilikuwa ishara ya kile alichokuwa anakitabiri. Mfululizo wa kwanza wa matendo ya ishara una matendo manne. Katika tendo la kwanza, Mungu anamwambia Ezekieli achore picha ya mji wa Yerusalemu kwenye ubao wa udongo, na mchoro huo uonyeshe kwamba mji huo umezingirwa na maadui.[6] Kinyume na imani ya Waisraeli wengi wa wakati huo kwamba Yerusalemu ni mji ambao Bwana ameuchagua kuweka uwepo wake, hivyo hauwezi kupigwa, tendo hili la ishara lilitabiri kwamba Yerusalemu itazingirwa na maadui na hatimaye kupigwa (4:1-3). Katika tendo la pili, Ezekieli anaambiwa alale kwa ubavu wa kushoto kwa siku 390 huku akiwa amebeba mzigo wa dhambi wa nyumba ya Israeli. Baada ya siku hizo, ageukie ubavu wa kulia na alale upande huo kwa siku 40, akiwa amebeba mzigo wa dhambi wa nyumba ya Yuda. Afanye hivyo huku akigeukia ubao wenye mchoro wa Yerusalemu uliozingirwa. Ishara hii ilionyesha miaka ya maisha ya dhambi ya nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda (4:4-8). Katika tendo la tatu, Ezekieli anaambiwa atengeneze mkate unaotokana na mchanganyiko wa mazao sita. Mkate huo uwe chakula chake kwa siku 390 atakazolala kwa ubavu. Aliambiwa ale mkate huo kwa vipimo na aupike kwa kutumia mavi makavu ya binadamu kama kuni. Hata hivyo, Ezekieli alimwomba Mungu aruhusiwe kutumia mavi makavu ya ng’ombe badala ya mavi ya binadamu, na Mungu akamruhusu. Tendo hili lilikuwa ishara ya taabu ya chakula ambayo watu wa Mungu wataipata wakati Yerusalemu utakapozingirwa (4:9-17). Tendo la ishara la mwisho katika mfululizo wa huu wa kwanza, lilikuwa ni Ezekieli kunyoa nywele na ndevu zake kwa kutumia upanga kama wembe wa kinyozi. Kama vile upanga ulivyoondoa nywele na ndevu zake, ndivyo upanga wa wavamizi utakavyowaondoa watu wa Yuda kutoka katika ardhi yao. Baada ya kunyolewa, nywele hizo zilipimwa na kugawanywa katika sehemu tatu zilizo sawa. Kitendo cha kupima kilikuwa ishara ya tathmini na hukumu inayokuja. Baada ya kupima, Ezekieli alizitupa nywele hizo kwa namna tatu tofauti. Theluthi moja aliichoma kwa moto ili kuonyesha wale ambao wataangamia ndani ya mji kwa magojwa na njaa. Theluthi nyingine aliikata kwa upanga ili kuwakilisha wale ambao watakaokufa vitani. Theluthi ya mwisho ilitawanyishwa kwa upepo ili kuwakilisha wale ambao watatawanyishwa katika mataifa. Sehemu ndogo ya nywele iliwekwa kwenye upindo wa vazi kuwakilisha masalia ya watu wa Yuda (5:1-17).

Baada ya matendo hayo ya ishara, Mungu anampa Ezekieli ujumbe wa maneno sasa. Ujumbe wa Mungu ni tangazo la hukumu yake juu ya milima, vilima, vijito na mabonde ya Israeli. Sehemu hizi ndizo ibada za sanamu zilikuwa zinafanyika. Mungu anatangaza hukumu juu ya sehemu hizi na juu ya wanaotumia sehemu hizi kuabudu miungu. Sawa na ahadi za laana za Mungu zilizopo katika Walawi 26, Mungu anatangaza upanga kwa watu wake, kuwatawanya wale watakaopona upanga, kufanya ukiwa kwenye maeneo yao ya ibada za sanamu, na mwishowe kujisazia wachache kama mabaki. Haya yote, Bwana atayafanya ili Israeli wajue kwamba yeye ni Bwana na hakusema bure alipoahidi kwamba atawahukumu kama watamwasi yeye (6:1-10). Kwa kutumia matendo ya ishara (kupiga makofi na kupiga kishindo kwa miguu), Mungu anasema na Ezekieli asisitize kuhusu hukumu itakayokuja juu ya Israeli kama alivyosema katika hotuba ya kwanza (6:11-14).

Ezekieli anapata ujumbe kwa mara nyingine tena, ujumbe unaotangaza kwamba mwisho wa Israeli umefika. Hasira ya Mungu iko juu yao, na hivyo watapata hukumu wanayostahili. Hukumu hii ni kwa sababu ya maovu yao, yaani ibada za sanamu (7:20) na udhalimu katika jamii (7:23). Kwa sababu hukumu hii inatoka kwa Mungu, hakuna kitakachozuia wao kuadhibiwa, sio mali wala vito vya thamani (7:1-27).

Mwaka mmoja na miezi miwili ilipita bila Ezekieli kupata ujumbe mwingine kutoka kwa Bwana. Baada ya hapo, Ezekieli akachukuliwa katika roho na mfano wa binadamu anayeng’aa kama moto chini na kama mwanga juu, akapelekwa Yerusalemu. Huko Yerusalemu, akaona sanamu imewekwa mlangoni pa kuingilia sehemu ya patakatifu pa hekalu. Na huko hekaluni, akaona utukufu wa Mungu kama alivyokuwa ameona katika maono yake ya kwanza (8:1-4). Huko Yerusalemu Mungu akamuonyesha Ezekieli machukizo manne yanayofanywa na watu wake. Kwanza, kuwekwa kwa sanamu katika mlango wa kuingilia ua wa ndani wa hekalu (8:5-6). Pili, vinyago na picha za kila aina ya wadudu na wanyama kufanyiwa ibada katika chumba cha siri kilichokuwa kwenye ukuta wa ua wa ndani (8:7-13). Tatu, kufanyika kwa ibada kwa sanamu ya mungu wa Kibabeli aitwaye Tamuzi (8:14-15). Nne, kuabudiwa kwa jua (8:16-17). Kutokana na watu wa Yuda kufanya hayo yote kwenye hekalu, sehemu ambayo Mungu aliichagua kuweka uwepo wake, Mungu anamwambia Ezekieli kwamba hakika atawaadhibu watu wake bila huruma. (8:18).

Baada ya kuonyeshwa maovu hayo, Ezekieli akaonyeshwa hukumu ya Mungu kwa sababu ya maovu hayo. Mungu aliwaita wasimamizi sita wa mji wa Yerusalemu, na akawaamuru wabebe silaha za kuua watu kwa ajili ya kutimiza hukumu yake. Miongoni mwao kulikuwa na mmoja ambaye kazi yake ilikuwa kuwawekea alama wenye haki ili wasiangamizwe pamoja na waovu (9:1-11). Kumbuka kwamba tangu mwanzoni, Ezekieli alipofika Yerusalemu, aliuona uwepo wa Mungu katika hekalu kama alivyouona katika maono yake ya kwanza (1:4-28). Katika uwepo huo, Mungu akamwambia yule aliyekuwa na kazi ya kuwawekea alama wenye haki achukue moto katikati ya makerubi na akaumwage katika mji wa Yerusalemu. Moto huo unatabiri hukumu ya Mungu juu ya mji, ikiwa ni pamoja na kuchomwa kwa mji baada ya wakazi wake kuuawa. Jambo baya zaidi, Ezekieli anaona kuanza kuondoka kwa uwepo/utukufu wa Mungu kutoka katika hekalu (10:1-9). Katika maono yake ya awali, Ezekieli hakufafanua viumbe wale wanne walikuwa ni viumbe gani, wala hakuweka wazi kwamba yule mwenye mfano wa mwanadamu aliyebebwa na viumbe hao alikuwa ni nani. Katika maono haya, Ezekieli anaweka wazi kwamba wale viumbe wanne ni makerubi, na yule mwenye mfano wa mwanadamu ni Mungu wa Israeli (10:20). Huku akirudia kuelezea muonekano wa makerubi, Ezekieli anaona tena uwepo/utukufu wa Mungu ukiendelea kusogea mbali na hekalu (10:10-22).

Katika muendelezo wa ziara yake ya kiroho, Ezekieli akaonyeshwa maono mengine. Akawaona watu ishirini na tano na kati yao aliwatambua viongozi wawili. Viongozi hawa ndio walikuwa wanawapotosha watu katika Yerusalemu. Waliwapotosha kwa kuwaambia kwamba wako salama hawana haja ya kuhofu (11:3).[7] Kwa sababu ya upotoshaji huo, Mungu anamwambia Ezekieli atabiri hukumu itakayokuja juu ya Yerusalemu. Mungu anasema, watu walio hai wanaodhani wako salama ndani ya mji wa Yerusalemu watauwawa na wengine watachukuliwa mateka na mataifa mageni na wafu pekee ndio watakaokuwa salama ndani ya mji. Maono haya yakakamilika kwa Ezekieli kushuhudia kifo cha mmoja wa viongozi aliowatambua (11:1-13). Toka mwanzo wa huduma, Ezekieli amekuwa akipokea utabiri wa hukumu tu, lakini Mungu sasa anatangaza tumaini la urejesho. Mungu anasema baada ya hukumu utakuja wakati ambao atarejesha watu wake katika nchi yao na atawafanya upya mioyo yao nao watayatenda mambo yote sawa sawa na maagizo yake (11:14-21). Habari hizi ya urejesho, Mungu atazielezea kwa urefu katika miaka ya mbele ya utumishi wa Ezekieli. Ziara ya Ezekieli Yerusalemu inafikia mwisho kwa Ezekieli kushuhudia uwepo/utukufu wa Mungu anaondoka kabisa katika mji wa Yerusalemu (11:22-23). Baada kushuhudia tukio hili baya, tukio la uwepo/utukufu wa Mungu kuondoka kabisa Yerusalemu, Ezekieli anarudishwa Babeli kule alikokuwa. Huko uhamishoni Babeli, Ezekieli akawajulisha wenzake maono yote aliyoyaona aliposafiri katika roho mpaka Yerusalemu (11:24-25).

Kwa mara nyingine tena, Mungu anamuagiza Ezekieli kufanya matendo ya ishara. Tendo la kwanza lilikuwa kuwaonyesha Waisraeli kwamba wataenda utumwani. Ezekieli alitoa vyombo vyake nje wakati wa mchana, na jioni akafanya kuhama kutoka kwake kwenda sehemu nyingine kupitia tundu la ukutani huku watu wakimtazama. Tendo hili lilitabiri kwamba Waisraeli wataenda utumwani (12:1-16). Katika tendo la pili, Ezekieli aliambiwa ale chakula na kunywa maji kwa kutetemeka kuonyesha kwamba Waisraeli watakula na kunywa kwa hofu sana kutokana na mabaya yatakayowapata (12:17-20). Kutokana na kuwepo na maneno ya watu wakisema kwamba unabii wa Ezekieli ni wa miaka ya baadaye sana na, isitoshe, toka alivyoanza kutabiri hakuna kilichotokea, Mungu anamwambia Ezekieli mara mbili awahakikishie watu kwamba aliyoyatabiri yatatimia hakika, tena siku si nyingi (12:21-28).

Baada ya kuwahakikishia watu kwamba unabii wa Ezekieli utatimia, Bwana anawageukia sasa manabii wa uongo. Manabii wanaosema Bwana amewatuma lakini hakuwatuma, manabii wanaotabiri amani kwa Yerusalemu (kinyume na Ezekieli anayetabiri hukumu). Mungu anasema atawahukumu, na maneno yao hayataandikwa katika maandiko ya Israeli (13:1-16).

Pia, Mungu anatangaza hukumu juu ya manabii wa uongo wa kike. Manabii wanaotumia hirizi na vitambaa vya kufunga kichwani kuwatega watu wa Mungu. Manabii hao Bwana atawaangamiza ili wasiendelee kuwatesa watu (13:17-23). Baada ya muda, wazee wa israeli wakamjia Ezekieli ili waliulize kutoka kwa Bwana. Bwana akasema, kwa kuwa wazee hawa wanaabudu sanamu toka mioyoni mwao watajibiwa kutokana na hali za mioyo yao. Na sio wazee tu bali Israeli wote wanaoabudu sanamu toka mioyoni mwao. Majibu hayo yatatolewa hivyo (majibu yatakuwa yakuwapotosha) ili wahukumiwe sawa sawa na uovu wao. Pamoja na kuahidi hivyo, Mungu anatoa mwito Waisraeli watubu ili hayo yasitokee (14:1-11). Kwa sababu ya maovu ya Israeli, Mungu anamwambia Ezekieli kwamba hukumu yake juu ya taifa litakalomwasi ni jambo ambalo halizuiliki hata kama Nuhu, Ayubu au Danieli angeomba msamaha kwa niaba yao. Wao wengekuwepo wangejiokoa wenyewe lakini sio kuzuia hukumu yake. Katika hukumu hii kwa Israeli, Mungu atawapiga kwa upanga, na njaa, na wanyama wakali, na tauni. Pamoja na hukumu hiyo ya kutisha bado masalia wachache watabaki (14:12-23).

Baada ya ujumbe huo, Mungu anatumia mifano mitano tofauti kuelezea hali ya uasi wa Israeli, hukumu iliyopita na inayokuja. Katika mfano wa kwanza, Mungu anawafananisha wakazi wa Yerusalemu na mzabibu usiozaa matunda. Ukitoa kuzaa matunda, mzabibu huu haufai hata kutengenezea kigingi cha kutundikia vitu. Mzabibu wa namna hii, ukichomwa moto ndio haufai kabisa. Vivyo hivyo, kwa sababu wakazi wa Yerusalemu hawazai matunda yeyote, hawafai kabisa (hawana tofauti na mataifa), na hivyo wanastahili hukumu (15:1-8). Katika mfano wa pili, Mungu anamtumia mwanamke kuwakilisha watu wake Israeli. Mwanamke huyu alizaliwa katika mazingira yasiyopendeza, na hata yeye hakuwa wa kuvutia. Hata hivyo, Mungu alimchukua, akampamba na kumvika vizuri, na baadaye akaoana naye. Lakini, kwa sababu ya uzuri na umaarufu wake, mwanamke huyu baadaye akawa kahaba. Kwa sababu ya ukahaba wake, Bwana anasema atamhukumu. Pamoja na hukumu hiyo, Mungu anasema agano lake na mwanamke huyu halitaishia katika hukumu; badala yake, tamati yake itakuwa ni urejesho katika ndoa hii (16:1-63).

Mfano wa tatu, Mungu anasema kulikuwa na tai mkubwa ambaye alienda mpaka Lebanoni, akatua juu ya mti aina ya mwerezi na akaondoka na tawi la juu na kulipeleka nchi ya biashara. Katika sehemu ya mwerezi akapanda mzabibu, na akaupa kila kinachohitajika ili ukue. Baada ya kukua, mzabibu huo ukapindisha mizizi yake kutoka kwa tai aliyeupanda na kuelekeza mizizi yake kwa tai mwingine mkubwa. Bwana anauliza, Je, mzabibu huu utafanikiwa? Je, hauta ng‘olewa na tai aliyeupanda? (17:1-10). Baada ya mfano huo, Bwana anatoa ufafanuzi. Tai wa kwanza ni mfalme wa Babeli, aliyekuja Israeli na kumuondoa mfalme Yekonia/Yehoyakini na badala yake akamfanya Sedekia/Matania kuwa mfalme. Lakini Sedekia akaamua kumwasi mfalme wa Babeli na kugeukia Misri ili wamsaidie atoke chini ya utawala wa Babeli. Bwana anasema kwa kufanya hivyo, mfalme Sedekia hatafanikiwa na Misri haitakuwa na uwezo wa kumsaidia (17:11-18). Kwa sababu ya kuasi maagizo na sheria ya Mungu, mfalme Sedekia atapigwa na kupelekwa uhamishoni (17:19-21)[8]. Kwa kutumia lugha ya picha (mfano) Mungu anatabiri kwamba yeye mwenyewe atafanya urejesho baada ya hukumu hii kupita (17:22-24).

Kabla ya kuendelea na mfano wa nne, Mungu anakanusha usemi wa watu wake unaoonyesha kwamba watoto wamekuwa wanahukumiwa kwa sababu ya makosa ya baba zao. Bwana anasema kwamba kila mtu atahukumiwa kutokana na matendo yake. Watendao haki bila kugeuka wataishi na watendao uovu bila kugeuka watahukumiwa. Pamoja na ukweli huo, Mungu bado anawaita Israeli kutubu ili waepuke hukumu (18:1-32). Mfano wa nne na wa tano uko katika ushairi mmoja wa maombolezo, Mungu aliomwagiza Ezekieli aliimbe. Mfano wa nne unaeleza kuhusu simba jike aliyezaa watoto kadhaa. Kati yao, akachagua mmoja kuwa kiongozi wa kundi. Simba huyu akajifunza kuwinda na hatimaye akararua mawindo na watu. Kwa sababu ya hayo, simba huyu akawindwa na mataifa, akakamatwa, na kupelekwa Misri. Badala yake, simba jike akamteua mwana mwingine kuwa kiongozi, ambaye akatenda kwa uharibifu mkubwa zaidi ya yule wa kwanza. Simba huyu naye akawindwa na mataifa, akakamatwa, na kupelekwa Babeli (19:1-9). Simba jike anawakilisha ukoo wa kifalme wa Daudi katika kabila la Yuda. Simba mdogo wa kwanza anamwakilisha Mfalme Yehoahazi. Yehoahazi alirithi ufalme kutoka kwa baba yake Yosia, akatawala kwa miezi mitatu tu kisha akakamatwa na kupelekwa Misri (2 Wafalme 23:31-34). Simba mdogo wa pili anawakilisha mfalme Yehoyakini (Yekonia), mfalme aliyetawala miezi mitatu pia na akakamatwa na kupelekwa uhamishoni Babeli (2 Wafalme 24:8-17).

Katika mfano wa tano, Mungu anasema mama wa mfano wa nne alikuwa kama mzabibu uliopandwa karibu na maji na hivyo ukastawi vizuri na kuwa na matawi mengi. Mzabibu huu ukakuwa na kuwa mrefu sana pamoja na matawi yake. Lakini mzabibu huu uling’olewa na kuangushwa chini kwa ghadhabu. Matawi ya mzabibu huu yakateketezwa kwa moto na wenyewe ukapandwa katika nchi ya ukame (19:10-14). Mfano huu unaonyesha jinsi Yuda/Israeli ilivyokuwa na ustawi na jinsi ilivyohukumiwa na Bwana na hatimaye watu wake wakapelekwa uhamishoni.

Baada ya mwaka mmoja kupita, Ezekieli akapata ujumbe mwingine kutoka kwa Bwana. Ujumbe huu ulikuja baada ya wazee wa Israeli kumjia Ezekieli ili kuuliza kutoka kwa Bwana. Bwana akakataa kuuliza na wazee wa Israeli (20:1-4). Bwana anakataa kuulizwa na wao kwa sababu Israeli kwa ujumla wamekuwa na historia ya kumuasi yeye miaka yote. Bwana alipowatoa utumwani Misri, muda mfupi tu walimuasi na wakashikilia ibada za sanamu (20:5-9). Walipokuwa jangwani pia walimwasi, pamoja na Bwana kuwapa sheria zake (20:10-17). Kizazi kipya kilichozaliwa jangwani pia kiliagizwa na Bwana kutoasi kama baba zao walivyofanya, lakini hakikusikia (20:18-26). Miaka yote hii katika historia Mungu hakuwaangamiza Israeli kabisa pamoja na kuamuasi kwao kwa sababu ya kulitunza jina lake (Kulitunzia heshima jina lake). Kwa hiyo, kwa sababu Israeli ya sasa inafanya ibada za sanamu kama Baba zao walivyofanya katika milima mirefu au miti, basi Bwana anasisitiza kwamba yeye hataulizwa na watu waasi kama wao (20:27-31).

Pamoja na maasi hayo ya Israeli tangu kuanzishwa kwake na pamoja na Bwana kukataa kuulizwa na wazee wa Israeli bado Bwana hajawaacha watu wake. Bwana anasema nia ya Israeli kuishi kama mataifa mengine kwa kuabudu sanamu haitafanikiwa. Baada ya hukumu kupita Bwana atawatawala yeye mwenyewe. Ataanza na kuwarudisha kutoka atakakowafukuzia, atawaleta jangwani, atafanya nao agano na mwisho atalisafisha taifa ili waasi wasikae Israeli tena (20:32-38). Katika kuendelea kutangaza urejesho/uhamsho utakaokuja baada ya hukumu, Bwana anawaambia Israeli waendelee tu kuabudu sanamu ikiwa ndivyo wanavyotaka, lakini wakati unakuja ambapo hawatalichafua tena jina lake. Katika wakati huo, Israeli watamuabudu Mungu katika mlima mtakatifu na watakubaliwa na Mungu watakapomtumikia. Baada ya urejesho huo, Israeli watakumbuka uovu wao uliowafanya waadhibiwe na Bwana na wataichukia historia hiyo. Zaidi ya hayo, maisha haya ya urejesho yatawafundisha Israeli kwamba Bwana amewatendea haya (kuwageuza mioyo) si kwa sababu ya matendo yao, bali kwa sababu ya kutunza heshima yake (20:39-44).

Baada ya unabii huo, Ezekieli anapata unabii mwingine ambao unaelezea kwa kirefu kuhusu hukumu inayokuja. Kwa kutumia lugha ya picha/mithali mbili Mungu anatangaza ujio wa hukumu kwa Israeli/Yuda. Katika mithali ya kwanza, Mungu anatangaza ujio wa moto utakaoteketeza mti mbichi na mti mkavu. Moto huu utateketeza kutoka kusini mpaka kaskazini na hautazimika. Kutokana na madhara ya moto huo, watu wote watajua kwamba Bwana ndiye aliyeuwasha (20:44-48). Baada ya mithali hii mwitikio wa watu ukawa ni kudhihaki ujumbe wa Ezekieli kwa sababu ya kutumia mithali katika uwasilishaji wake (20:49). Pamoja na mwitikio huo, Mungu anasema tena kwa mithali ya pili. Katika mithali hii, Bwana anasema atautoa upanga alani mwake na utafanya kazi ya kuangamiza kutoka kusini mpaka kaskazini na hautarudi tena alani. Upanga huu utakuwa juu ya watu wote, wenye haki na waovu. Na kwa sababu ya madhara yake, watu wote watajua kwamba upanga huu ulitoka kwa Bwana (21:1-5). Kusisitiza ujumbe ulioko kwenye mithali hizi mbili, Mungu anamwagiza Ezekieli kufanya tendo la ishara. Mungu anamwagiza Ezekieli afanye maombolezo mbele ya watu ili wamuulize sababu ya maombolezo yake.  Ndipo atakapowajibu kwamba anaomboleza kwa sababu ya taarifa watakazozipokea, taarifa zitakazo sababisha kila moyo kuyeyuka, mikono kuwa dhaifu, roho kuzimia, na magoti yote kulegea kama maji (21:6-7).[9]

Baada ya kutumia mithali hizo mbili, Mungu sasa anatumia mashairi mawili kutangaza ujio wa upanga juu ya watu wake. Katika shairi la kwanza, Mungu anamwambia Ezekieli atangaze kwamba upanga umeshanolewa na kusuguliwa kwa ajili ya machinjo na uko tayari kuwekwa mkononi mwa mtumiaji (21:8-11). Ezekieli anaambiwa alie kwa uchungu, kwa sababu upanga huu ni kwa ajili ya watu wa Israeli na viongozi wao na upanga huu hautaogopa hata ukoo wa kifalme/fimbo (21:12-13). Katika shairi la pili, Mungu anamuagiza Ezekieli kupiga makofi kuashiria uhakika wa ujio wa upanga. Upanga huu utawapiga watu mara mbili hata mara tatu. Upanga huu utawaangamiza watu katika pande zote, kushoto na kulia na mwisho Bwana atapiga makofi pale hukumu yake itakapokuwa imetoshelezwa (21:14-17).

Baada ya mashairi haya mawili, Bwana anamwagiza Ezekieli kufanya tendo la ishara ambalo lina ujumbe ule ule wa upanga unaokuja kwa watu wake. Katika tendo hili la ishara, Ezekieli anaambiwa aweke alama katika njia mbili, yaani katika sehemu ambapo barabara mbili zinagawanyika, Ezekieli aweka bango linaloonyesha njia zinazoelekea mji wa Raba wa Waamoni na Yerusalemu. Ezekieli anaambiwa aweke hilo bango hili upanga wa mfalme wa Babeli uchague sehemu ya kwenda kuangamiza (21:18-20). Baada ya tendo hilo la ishara, Mungu anamwambia Ezekieli jinsi mfalme wa Babeli atakavyoichagua Yerusalemu badala ya mji wa Raba. Mfalme wa Babeli atakwenda kwenye njia panda, atafanya uganga kwa njia tatu, na mwishowe ataichagua Yerusalemu kwa ajili ya kuiangamiza. Uganga huu ulioichagua Yerusalemu utaonekana na Waisraeli kuwa sio wa kweli hata hivyo, utawakumbusha uovu wao uliosababisha kukamatwa kwao (21:21-23). Tendo hili la ishara linafungwa na tamko la hukumu juu ya watu wa Israeli kwa sababu ya dhambi zao na juu ya mfalme wa Israeli/mkuu wa Israeli (21:24-25). Mkuu wa Israeli anaambiwa avue mavazi ya kifalme na arekebishe matabaka katika jamii kwa kuwa kiti chake kitapinduliwa mpaka atakapokuja yeye aliye haki (21:26-27).[10] Katika kumalizia ujumbe unaohusu upanga, Mungu anamwambia Ezekieli atabiri upanga juu ya wana wa Amoni. Upanga umefutwa na kusuguliwa kwa ajili ya mauaji katika nchi yao. Mungu atawaangamiza wana wa Amoni kwa kuwatia katika mikono ya watu wenye uzoefu wa mauaji na hivyo hawatakumbukwa tena (21:28-32).

Baada ya hayo, Ezekieli anapata jumbe zingine tatu, ambazo bado zinatangaza hukumu ya Yuda kwa sababu ya dhambi zao. Katika ujumbe wa kwanza, Mungu anaanza kwa kutangaza mashikata yake juu ya Jerusalemu kwa kutaja dhambi ambazo viongozi na wakazi wa Jerusalemu wanajihusisha nazo. Baada ya kutaja dhambi hizo, Mungu anawajulisha Yuda kwamba hawatavumilia hukumu yake kabisa (22:1-16). Katika ujumbe wa pili, Mungu anatumia mfano kutangaza hukumu yake inayokuja juu ya nyumba ya Israeli. Kama vile watu wanavyoyeyusha metali (kama vile fedha, shaba, chuma, risasi na bati) katika tanuru ili kupata metali iliyo safi, ndivyo Mungu anaahidi kuwakusanya na kuwayeyusha watu wake kwa ghadhabu yake (22:17-22). Katika ujumbe wa tatu, Mungu atoa mashitaka tena kama alivyofanya kwenye ujumbe wa kwanza, lakini sasa anataja makundi ya viongozi (manabii, makuhani na wakuu) wanaojihusisha na kila aina ya uovu. Na kwa sababu hakuna mtu wa kuongoza watu kutubu (kurekebisha maosa yote), hivyo Mungu ameamua kuachilia ghadhabu yake (22:23-31).

Kwa mara nyingine tena, Mungu anatumia mfano wa mwanamke na ukahaba kuelezea uovu wa watu wake na hukumu inayokuja juu yao (mara ya kwanza ilikuwa katika sura ya 16). Safari hii, Mungu anatumia wanawake wawili kuzungumzia uovu wa mataifa yake yote mawili, yaani Israeli na Yuda. Israeli, ambayo makao yake makuu yalikuwa Samaria, inawakilishwa na Ohola, wakati Yuda, ambayo makao yake makuu yalikuwa Yerusalemu, inawakilishwa na Oholiba. Baada ya utangulizi wa kuwatambulisha wanawake hawa (23:1-4), Mungu anaeleza maovu yaliyofanywa na watu wake wa Israeli kwanza (23:5-8). Na kwa sababu ya maovu hayo, Mungu aliwahukumu Israeli, na hivyo wakapigwa na kupelekwa utumwani na dola ya Ashuru (23:9-10).[11] Pamoja na Israeli kuhukumiwa hivyo, Yuda haikujifunza kutoka kwa ndugu zao na haikuacha kutenda maovu ya kila namna (23:11-21). Kwa sababu ya maovu hayo, Mungu anatangaza ujio wa hukumu juu yao, kama alivyofanya kwa ndugu zao wa Israeli (23:22-35). Ingawa hukumu juu ya Ohola (Samaria) ni historia, yaani ilishatokea, Mungu anahitimisha ujumbe wake kwa kueleza zaidi kuhusu maovu ya wanawake hawa wote wawili (23:36-45) na kutangaza ujio wa hukumu yake (23:46-49).

Mwaka wa tisa tangu Ezekieli kutolewa nyumbani kwao Yerusalemu, ambao pia ni mwaka wa nne toka alipoitwa katika kazi yake ya kinabii, Mungu anampa ujumbe tena. Kabla ya ujumbe, Mungu anamwambia kwamba aweke kumbukumbu ya tarehe ya siku hii anayopokea ujumbe huu, kwa sababu siku hii ndiyo siku dola ya Babeli ilianza kuzingira mji wa Yerusalemu. Baada ya hilo, Mungu anamwambia Ezekieli atoe mithali kwa watu. Mithali inasema: watu watenge sufuria katika moto na ndani yake waweke nyama nzuri na mifupa mizuri kwa ajili ya kupikwa (24:1-5). Baada ya mithali hiyo, Mungu anatoa ole kwa Yerusalemu kwa sababu ya kumwaga damu wazi wazi, na kwa sababu ya uovu wao huo unaofananishwa na sufuria lenye uchafu ndani yake. Kwa sababu ya kumwaga damu wazi wazi, Mungu ataiacha damu wazi ili iwe ushahidi atakapokuwa anawahukumu (24:6-8). Kwa mara nyingine tena, Mungu anatoa ole kwa Yerusalemu huku akisema yeye atachochea moto mwingi kwa ajili ya kuunguza nyama na mifupa ndani ya sufuria hilo (ambalo ni Yerusalemu), na sufuria lenyewe ataliunguza mpaka hasira yake itakapotoshelezwa ili mwisho wa siku litakaswe. (24:9-14).

Ujumbe wa Ezekieli wa kutabiri wa ujio wa hukumu juu ya Israeli kabla ya kugeukia mataifa mengine unafika tamati kwa maisha ya Ezekieli mwenyewe kuwa tendo la ishara. Mungu anamwambia Ezekieli kwamba mke wake atakufa lakini yeye asifanye maombolezo yeyote zaidi ya kuumia kwa ndani tu. Zaidi ya hayo, alitakiwa kuendelea na kazi yake ya kinabii kama kawaida. Mke wa Ezekieli akafa na Ezekieli akatii maelekezo ya Bwana, ndipo watu walipomuuliza ni nini maana ya tendo hili? Tendo la kutokuomboleza baada ya kufiwa na mke wake (24:15-19). Mungu akawajibu kwamba kama ilivyokuwa kwa Ezekieli, ndivyo itakavyokuwa kwa Yerusalemu na wakazi wake. Mahali patakatifu, yaani Yerusalemu na hasa Hekalu, mahali ambapo palikuwa ni fahari ya Israeli, patabolewa na wao hawataomboleza kabisa kama Ezekieli (24:20-24). Na siku tukio hili likitokea, kuna watu watasalimika na hao wataleta habari kwa Ezekieli kumjulisha kuhusu kubomolewa kwa Yerusalemu na Hekalu ndani yake, na hivyo itakuwa uthibitisho wa kile Mungu alichokuwa anakisema kupitia Ezekieli (24:25-27).

Kabla ya kushuhudia tukio la kuanguka kwa mji wa Yerusalemu kama Ezekieli alivyokuwa anatabiri, Mungu anampa Ezekieli ujumbe kwa ajili ya mataifa saba, mataifa jirani na Israeli. Ujumbe wao pia unahusu ujio wa hukumu. Mungu anatangaza ujio wa hukumu juu ya taifa la Amoni (25:1-7), Moabu (25:8-11), Edomu (25:12-14), na Wafilisti (25:15-17). Mataifa haya yanahukumiwa kwa sababu yaliungana na Yuda ili kulipinga taifa la Babeli, lakini Babeli alivyoipiga Yuda, wao wakalitelekeza taifa la Yuda na wakalidhihaki kwa kupigwa kwake.

Kwa mji wa Tiro, Mungu anasema kwamba kufikiri kwao kuwa kuanguka kwa Yerusalemu kutawapa wao faida za kibiashara ni ubatili. Mungu ataleta mataifa juu yao, na hivyo mji wa Tiro pia utapigwa na kuanguka (26:1-6). Baada ya kutoa tangazo hilo la hukumu, Mungu anaweka wazi kwamba Babeli ndilo taifa atakalolitumia kuupiga mji wa Tiro (26:7-14). Kwa sababu ya kipigo ambacho mji wa Tiro utapokea kutoka kwa Taifa la Babeli, mataifa na miji iliyoko ukanda wa bahari na baharini itatetemeka na kushangaa (26:15-21). Kwa kutumia ushairi, Mungu anaeleza jinsi mji wa Tiro ulivyokuwa na uzuri na mafanikio ya kibiashara. Mataifa mbalimbali yalifanya biashara na mji huu, na hivyo kuufanya kuwa mji mtukufu katikati ya mataifa mengi (27:1-25). Pamoja na hayo yote, mji huu utaanguka huku ukishuhudiwa na mataifa mengine, ambapo baadhi ya mataifa yatauombolezea na mengine kuuzomea. Kuanguka kwake kumefananishwa na kuzama kwa meli katikati ya maji makuu kwa sababu ya upepo wa mashariki (27:26-33).[12] Baada ya kuzungumza hayo juu ya mji, Bwana anasema na mfalme (mkuu) sasa. Mungu anamwambia mfalme wa Tiro asijiinue na kujiweka nafasi ya Mungu kwa sababu ya utajiri wake, kuwa Bwana atamtumia watu kumuua kwa kuwa yeye ni mwanadamu na sio Mungu (28:1-10). Kwa kutumia Lugha ya picha mfalme wa Tiro anafananishwa na kerubi aliyekuwa Edeni, aliyejaa uzuri na utukufu lakini akaanguka kwa sababu ya kiburi na uovu wake uliotokana na utajiri. Mungu anatangaza kwamba anguko lake litakuwa la aibu mbele ya mataifa, na ataharibiwa kabisa kama adhabu ya dhambi zake (28:11-19).

Jirani na Tiro ni Sidoni, Mungu pia anatangaza ujio wa hukumu juu ya Sidoni (28:20-26). Baada ya mataifa hayo sita, taifa la mwisho kutangaziwa hukumu ni Misri. Katika mwaka wa kumi, Ezekieli anapata maono ya kwanza ya tangazo la hukumu juu ya Misri. Kwa kumfananisha mfalme wa Misri na joka kubwa likaalo ndani ya maji, Mungu anasema atamtoa joka huyo katika maji na kumtupa jagwani ili awe chakula cha wanyama na ndege. Lugha hii ya picha inamtangazia Farao hukumu inayokuja kwa sababu amejitangazia kwamba mto Nile ni mali yake (29:1-16). Baada ya miaka kumi na saba baadaye, Mungu akampa tena Ezekieli neno juu ya Misri. Miaka zaidi ya kumi na saba hapo nyuma, Ezekieli alitabiri Babeli kuupiga mji wa Tiro (sura ya 26-28), lakini Babeli, katika kuupiga mji wa Tiro, hawakufanikiwa kupata mateka na nyara. Hivyo, Mungu anamwambia Ezekieli kuwa kwa kazi mfalme wa Babeli aliyofanya katika kuupiga mji wa Tiro, Mungu atawapa Misri kama mshahara wa kazi hiyo. (29:17-21). Kwa kutumia ushairi Bwana anatangaza kwamba Misri atakapohukumiwa kwa upanga, dhiki, moto, ukame na majanga mengine haitanguka peke yake bali na mataifa mengine washirika wa Misri watanguka pia (30:1-19). Kwa kutumia lugha ya picha, Mungu anasema ataidhoofisha nguvu ya kijeshi ya Misri (kuvunja mikono) na kuiimarisha nguvu ya kijeshi ya Babeli (kuitemegemeza mikono) ili Misri ipigwe na Babeli, na hivyo taifa la Misri lipate kushindwa (30:20-26). Kwa kutumia Ashuru kama mfano, mfano wa kukua na kuufikia ukuu na baadaye kuanguka, Mungu anatangaza hatima ya Farao mfalme wa Misri. Licha ya Ashuru kuwa na urefu na uzuri, ilipigwa na kumalizika, hii ndio itakuwa hatima ya Farao, mfalme wa Misri. Ujumbe huu wote unatolewa kwa kutumia lugha ya picha ya kufananisha dola ya Ashuru na Farao mfalme wa Misri na mti mkubwa (31:1-18). Unabii juu ya Misri unaishia na mashairi mawili ya maombolezo. Moja linahusu maombolezo juu ya Farao, na la pili ni maombolezo juu ya watu wa Misri. Farao, ambaye amejiona kama Mwana Simba katikati ya mataifa na wakati ni joka kubwa, atapigwa, na kipigo chake kitasababisha hofu na wasiwasi kwa mataifa mengine. Hii ndiyo sababu Ezekieli anaambiwa kumuombolezea (32:1-16). Watu wa Misri watapigwa, na Misri itaanguka hadi chini ya nchi (kuzimu au shimoni), sawa na mataifa mengine yaliyopigwa ambayo tayari yako shimoni/kuzimu/chini ya nchi. Mataifa haya ambayo Misri itakutana nayo huko shimoni ni Ashuru, Elamu, Mesheki, Tubalu, Edomu, na Sidoni. Lugha hii inamaanisha kufa na kuzikwa kwa taifa la Misri, sawa na mataifa mengine yaliyotangulia kufa na kuzikwa (32:17-32).

Baada ya ujumbe wa Mungu juu ya mataifa mengine, Mungu anamrudisha Ezekieli kwa taifa lake teule. Ezekieli anaanza kwa kutoa ujumbe kwa Waisraeli kwamba yeye amekuwa mlinzi wa mnara kama Bwana alivyomwita (Angalia 3:16-21). Hivyo, Bwana anataka mwenye dhambi ageuke na mwenye haki abaki katika haki yake (33:1-20). Baada ya ujumbe huo, Ezekieli anapokea ujumbe kutoka kwa mtu mmoja aliyetoroka wakati mji wa Yerusalemu unapigwa. Ujumbe huu ulikuwa kumjulisha Ezekieli kwamba unabii umetimia: mji wa Yerusalemu na hekalu ndani yake vimebomolewa. Tukio hili la mjumbe kuja kuleta taarifa kwa Ezekieli lilikuwa ni tukio ambalo Ezekieli alilitabiri miaka miwili nyuma (angalia 24:25-27) kwamba litatokea (33:21-22). Pamoja na Jerusalemu kubomolewa waisraeli waliobaki katika mji huu uliobomolewa hakuwa na moyo wa toba kabisa. Wakawa wanasema kama Ibrahimu alikuwa mmoja akarithi nchi, basi wao wana haki ya kurithi nchi kwa kuwa wao ni wengi. Mungu anamwambia Ezekieli awaambie kwamba wao pia watauwawa kwa kuwa bado wanaendelea na dhambi zao (33:23-29). Baada ya unabii kutimia na Ezekieli kuwa maarufu katikati ya wenzake walioko utumwani, Bwana anamjulisha kwamba umaarufu wake miongoni mwa watu ni wa juu juu. Watu wanakuja kumsikiliza kwa shauku lakini hawana nia ya kubadilika katika maisha yao. Wanaona maneno yake kuwa ya kufurahisha na hawana nia ya kuweka kanuni hizo katika matendo (33:30-33).

Sura ya 33 ya kitabu cha Ezekieli ni sura ya katikati, ni sura inayogawanya ujumbe wa Ezekieli. Kabla ya sura hii, ujumbe wa Ezekieli ulihusu ujio wa hukumu ya Mungu juu ya Israeli na kwa sehemu juu ya mataifa. Baada ya sura hii, ujumbe wa Ezekieli unabadilika na kuwa ujumbe wa kutangaza tumaini la urejesho.

Ujumbe wa kwanza wa tumaini la urejesho unaanza na tangazo la Mungu kurejea kuwachunga watu wake baada ya kuwaondoa viongozi (wachungaji) wabaya waliosababisha watu kutangatanga na kutawanyika kwa sababu ya uongozi wao mbovu. Kwa sababu Mungu mwenyewe atawarejea watu wake, basi atawakusanya na kuwarejesha nyumbani kwao Israeli, na atamweka mtumishi wake Daudi[13] kuwa mtawala. Katika kipindi hiki cha urejesho, Mungu atarejesha baraka zote waisraeli walizozikosa (34:1-31). Baada ya unabii huu unaohusu uongozi, unabii unaofuata wa tumaini la urejesho unahusu ardhi ya Israeli. Mungu anasema kwa kuwa Mlima Seiri (yaani nchi ya Edomu) umekuwa na uadui wa kudumu juu ya Israeli, kiasi cha kufikia kushiriki kuiharibu Yerusalemu, kufurahia kuanguka kwake na kuwa na nia ya kuchukua ardhi ya Israeli, yeye ataufanya mlima huu kuwa ukiwa kama ilivyo Yerusalemu sasa (35:1-15). Kinyume na kile kitakachotokea Mlima wa Seiri, milima ya Israeli itapata urejesho. Katika urejesho huu, milima ya Israeli, yaani ardhi ya Israeli, itakuwa na sifa kuu nne. Moja, ardhi hii itazaa tena. Pili, Waisraeli wote watarudi na kuongezeka katika ardhi yao. Tatu, kurudi kwa Waisraeli katika ardhi hii kutakuwa kwa kudumu. Nne, watu wa Mungu hawatadhihakiwa na kudharauliwa tena katika ardhi yao (36:1-15).

Baada ya unabii unaohusu urejesho wa uongozi na kuhusu ardhi, unabii unaofuata unahusu kurejea kwa heshima ya jina la Mungu. Mungu anasema kwamba kwa sababu ya maovu ya Israeli, yeye aliwahukumu, na katika hukumu hiyo, Israeli waliangukia katika mataifa mbalimbali. Tendo hilo la Waisraeli kuishia katika mataifa mengine baada ya kupigwa na Babeli likaleta aibu juu ya jina la Bwana[14]. Kwa sababu Mungu hataki aibu, ameamua kuwa atawarudisha Waisraeli wote katika nchi yao, na zaidi, atawapa mioyo mipya—mioyo itakayomtii yeye—ili heshima yake irejee katika mataifa yote. Bwana atarejesha baraka zote na kuondoa laana zote ili Israeli istawi tena. Lengo la kufanya haya ni ili jina lake lipate heshima juu ya mataifa yote (36:16-38).

Unabii wa kwanza wa urejesho ulikuwa unahusu uongozi, wa pili ulikuwa unahusu ardhi, na wa tatu ulikuwa unahusu heshima ya jina la Bwana. Sasa Ezekieli anatoa unabii wa urejesho kuhusu watu, yaani Waisraeli wenyewe. Kwa mara nyingine tena, Mungu anamchukua Ezekieli kwenye maono na kumwonyesha bonde lenye mifupa mikavu sana, na anamtaka Ezekieli kutabiria mifupa hiyo kuishi. Ezekieli anatabiri sawa sawa na alivyoamuriwa, na jeshi kubwa linasimama kutoka kwenye mifupa hio mikavu. Maono haya yana maana kwamba Bwana atawafufua Waisraeli na kutia roho yake ndani yao ili waishi[15] (37:1-14). Kwa kutumia tendo la ishara la kuunganisha vijiti viwili vilivyoandikwa majina ya mataifa mawili yaliyozaliwa baada ya Israeli kugawanyika, Mungu anasema ataunganisha mataifa haya mawili ili kuunda taifa moja tu. Taifa hili moja litakaa kwenye ardhi moja ya Israeli (milima ya Israeli) na litaongozwa milele na kiongozi mmoja aitwaye Mtumishi wangu Daudi. Zaidi ya hayo, Mungu atafanya agano la amani na Israeli na atakaa pamoja nao milele (37:15-28).

Baada ya Israeli kupata urejesho wake, wakiwa wanaishi kwa amani na mafanikio kama ahadi za Bwana zilivyo, Bwana atamuinua Gogu, wa nchi ya Magogu, mkuu wa Roshi, Mesheki, na Tubali kuja juu ya Israeli kwa vita. Mkuu huyu ataongoza jeshi lenye muunganiko wa mataifa mengi kama vile Uajemi, Kushi, Putu, Gomeri, na Togarma. Ujio wao juu ya Israeli utakuwa kama ujio wa tufani kubwa (38:1-9). Kwa ufafanuzi zaidi, Gogu ataamua moyoni mwake kwenda kuvamia Israeli ambayo, kwa sababu ya amani yake, haina kuta, maboma, wala malango. Lengo lake ni kuchukua vitu mateka ili kufanya biashara na mataifa mengine kama vile Sheba, Dedani, na Tarshishi (38:10-13). Bwana anasema, pamoja na Gogu kuamua yeye mwenyewe moyoni mwake kuja juu ya Israeli, pamoja na majeshi ya mataifa mengi kuungana naye, nyuma ya pazia Yeye Bwana ndiye anayewaleta kupigana na Israeli ili mataifa wamjue Yeye (38:14-16). Siku hiyo ambayo Gogu na majeshi yake watakuja juu ya Israeli, Bwana ataingilia kati kwa kushusha hasira yake juu ya mataifa hayo. Bwana atayapiga mataifa hayo kwa tetemeko kubwa, upanga (watu kuwana wenyewe), tauni (magonjwa ya mlipuko), mvua kubwa ya mawe, na kwa moto. Kwa kipigo hicho, heshima ya jina la Bwana itarejea (38:17-23).

Kwa msisitizo, Bwana anarudia kueleza jinsi Gogu na washirika wake watakavyopigwa na yeye. Bwana anasema atawapiga maadui hawa wa Israeli kiasi ambacho silaha zao za vita zitatumiwa na Waisraeli kama chanzo cha moto (yaani, kama kuni) kwa muda wa miaka saba. Tena anasema jinsi miili ya wanajeshi waliouawa itakavyokuwa mingi, miezi saba itatumika kuwazika ili kuisafisha Israeli (39:1-16).Katika kipindi ambacho Waisraeli wanahangaika kuzika miili ya wanajeshi waliouawa, Bwana atawaalika ndege wa kila namna na wanyama wa kondeni kuja kula mlo wa sherehe ambao Bwana amewaandalia. Kwa pamoja, watakula mazao yote ya vita, ambayo ni watu na wanyama waliouawa vitani. Kwa kufanya hivi, Israeli na mataifa wote watajua ya kuwa Bwana ndiye Mungu na kwamba hukumu zake ni za haki (39:17-24). Utabiri juu ya Gogu unahitimishwa na msisitizo kwamba Bwana atafanya urejesho kama ambavyo Ezekieli amekuwa akitabiri tangu alipoanza sura ya 34 (39:25-29).

Baada ya miaka kumi na nne tangu Yerusalemu na hekalu ndani yake kubomolewa, Ezekieli anachukuliwa tena katika maono mpaka Yerusalemu. Safari ya kwanza ya Ezekieli (Sura ya 8-11) ilikuwa ni kushuhudia ibada za sanamu zinazoendelea huko na kuondoka kwa uwepo wa Mungu katika hekalu. Safari hii, Mungu anamleta Ezekieli Yerusalemu ili kumuonyesha tumaini la urejesho wa hekalu/nyumba ya Mungu (40:1-4). Ziara ya Ezekieli, ikiongozwa na mtu aliyeng’aa kama shaba, ilianzia nje ya eneo zima la hekalu, eneo likiwa limezungukwa na ukuta. Wakaanza kuingia ndani kwa lango la mashariki. Vipimo vya ukuta wa eneo la hekalu na vya eneo la lango la mashariki vimerekodiwa na Ezekieli (40:5-16). Walipoingia tu ndani ya eneo la hekalu walifika ua wa nje, ambao ulikuwa na vyumba thelathini (40:17-19). Katika eneo hilo la ua wa nje, wakaenda kwenye lango la nje lakini lililoko upande wa kaskazini (40:20-23). Kutoka lango la nje lililoko upande wa kaskazini, wakaenda mpaka kwenye lango la nje lililoko upande wa kusini (40:24-27). Kwa ujumla, mpaka sasa kutoka nje ya eneo la hekalu kuingia ndani, yaani kwenye ua wa nje, kuna malango matatu: lango la mashariki, kaskazini, na kusini. Malango hayo yote Ezekieli aliyatembelea na vipimo vyake akavirekodi.

Kama ilivyo kawaida ya eneo la hekalu, huwa linakuwa na ua wa nje na ua wa ndani. Sasa Ezekieli anaingia ua wa ndani kwa kupitia lango la kusini (40:28-31). Kutoka lango la kusini wakaelekea lango la mashariki (40:32-34). Kutoka lango la mashariki wakaelekea lango la kaskazini (40:35-37). Kama ambavyo ua wa nje ulikuwa na malango matatu, ua wa ndani pia ulikuwa na malango matatu. Katika malango haya kulikuwa pia na chumba cha kusafishia sadaka ya kuteketezwa (40:38) na meza nane za kuchinjia sadaka hizo (40:39-43). Ndani ya ua huu wa ndani Ezekieli aliona vyumba kwa ajili ya makuhani kujiandaa (40:44-47). Baada ya hapo, Ezekieli anafika kwenye hekalu lenyewe sasa. Anaanza kwa kupita sehemu ya kuingilia (40:48-49), anafika patakatifu pa Hekalu (41:1-2), na mwishowe Ezekieli anaachwa nje wakati yule mtu aliyemuongoza anaingia patakatifu pa patakatifu kufanya vipimo (41:3-4). Baada ya kufika patakatifu pa patakatifu, ambapo ndio kilele cha hekalu, Ezekieli anaonyeshwa vipimo vya viambatisho vya hekalu, mapambo yake (41:5-26), na mwishowe anatolewa nje kurudi kwenye ua wa nje.

Katika ua wa nje, upande wa kaskazini, yaani katikati ya ukuta wa hekalu na ukuta wa eneo la hekalu ulioko kaskazini, Ezekieli akaonyeshwa vyumba kwa ajili ya makuhani, vyumba kwa ajili ya kula na kuhifadhi vitu vitakatifu (42:1-14). Baada ya hapo, Ezekieli akatolewa nje, na huko nje yule mtu akapima eneo zima la hekalu lililozungukwa na ukuta pande zote nne (42:15-20).

Mchoro 1. Ziara ya Ezekieli katika eneo la hekalu jipya (Ezekiel’s Temple tour. Block, Daniel (1998). The Book of Ezekiel, Chapters 25-48 (The New International Commentary on the Old Testament). Eerdmans.

Maono haya ya tumaini la urejesho wa hekalu hayaishii kwa Ezekieli kuonyeshwa jengo la hekalu kubwa na bora zaidi kuliko lile lililobomolewa, bali yanafikia kilele kwa Ezekieli kushuhudia kurudi kwa uwepo wa Bwana katika hekalu lake. Wakati Ezekieli anaona maono haya ya kurudi kwa uwepo wa Bwana, akachukuliwa mpaka ua wa ndani na kuambiwa apeleke habari kwa Waisraeli kuhusu matumaini haya ya hekalu kubwa na bora lililorejeshewa uwepo wa Mungu (43:1-12). Na akiwa katika ua wa ndani, Ezekieli anapewa vipimo vya madhabahu ya sadaka za kuteketeza (43:13-17).

Baada ya hayo, maono yanayofuata kwa sehemu kubwa ni maelekezo ya maisha mapya baada ya urejesho. Mungu anaanza kutoa maelekezo ya jinsi ambavyo madhabahu itakavyotakiwa kuwekwa wakfu na makuhani walio uzao wa Sadoki (43:18-27). Pia, Bwana anatoa maelekezo kwamba lango la mashariki linatakiwa kufungwa na lisifunguliwe tena, kwa kuwa lango hilo ndilo Bwana alilopita wakati analirudia hekalu lake (44:1-3). Ezekieli akachukuliwa tena mpaka nje, upande wa lango la kaskazini, na huko akaona uwepo wa Bwana ukiwa umelijaza hekalu, akaanguka kifudifudi na Bwana akampa maelekezo kuhusu makuhani. Bwana akampa utambulisho wa makuhani ambao watafanya kazi katika hekalu lake, akamjulisha majukumu yao, sheria za ufanyaji kazi wao, na mwisho akamjulisha urithi wao (44:4-31). Pia, Bwana akampa maelekezo ya mgawanyo wa ardhi kwa makuhani, Walawi, mkuu na watu (45:1-8). Bwana anaendelea kutoa maelekezo zaidi, anatoa maelekezo kwa wakuu kusimamia haki katika biashara (45:9-12), anatoa maelekezo ya matoleo yanayotakiwa kutolewa na watu kwa mkuu (45:13-16), na wajibu wa mkuu wa kutoa sadaka za kila aina katika mwezi mpya, katika sabato, na katika sikukuu zote za nyumba ya Israeli zilizoamriwa (45:17). Sikukuu ambazo mkuu anatakiwa kutoa sadaka ni kama sikukuu ya kutakasa hekalu, sikukuu ya Pasaka inayoambatana na sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na sikukuu ya vibanda (45:18-25).

Bwana pia anatoa maelekezo kuhusu jinsi Mkuu na watu wote watakavyotakiwa kuabudu siku ya sabato na siku ya mwezi mpya. Pia, anatoa maelekezo ya sadaka ambazo Mkuu anatakiwa kutoa katika siku hizi (46:1-8). Maelekezo zaidi na ya jumla yanatolewa kuhusu wakati wa kuabudu na kuhusu kutolewa kwa sadaka katika siku hizi na sikukuu nyingine zilizoamriwa (46:9-15). Maelekezo haya yanafuatiwa na maelekezo yanayohusu umiliki na utoaji wa urithi (hasa ardhi) wa Mkuu (46:16-18). Baada ya hapo, Ezekieli akachukuliwa mpaka kwenye ua wa ndani, sehemu ambayo kulikuwa na vyumba vilivyoangalia kaskazini, na vyumba hivyo vilikuwa na majiko kwa ajili ya makuhani kupikia sadaka zilizotolewa na watu (46:19-20). Pia, akapelekwa kwenye ua wa nje, ambako katika pembe zote nne kulikuwa na vyumba vilivyotumika kama majiko kwa ajili ya wahudumu wa hekalu kupika sadaka zilizotolewa (46:21-24).

Pamoja na mambo yote hayo ya urejesho, ziara ya Ezekieli ilikuwa haijaisha. Ezekieli anachukuliwa tena mpaka mlangoni mwa hekalu, na hapo anaona maji yanayotoka hekaluni na kutoka nje kupitia mlango wa mashariki. Maji haya yakafanyika mto mkubwa uliosababisha uhai katika ardhi ya Israeli (47:1-12). Maono haya yaliashiria kusafishwa (kutakaswa) kwa ardhi ya Israeli. Baada ya kutakaswa kwa ardhi, Mungu anatoa maelekezo ya namna ya kugawanywa kwa ardhi hiyo kwa makabila kumi na mawili ya Israeli, Walawi, makuhani wa ukoo wa Sadoki, na Mkuu (47:13-48:29). Mgawanyo huo umeonyeshwa katika Mchoro namba 2 hapo chini. Maono ya Ezekieli yanafikia mwisho kwa kuonyesha mji mpya wa mraba (Yerusalemu Mpya), ambao utaitwa Bwana Yupo Hapa. (48:30-35).

Mchoro 2. Maono ya Ezekieli kuhusu mgawanyo wa ardhi wa makabila ya Israeli (Adapted from Block, Daniel (1998). The Book of Ezekiel, Chapters 25-48 (The New International Commentary on the Old Testament). Eerdmans

FOOTNOTES


[1] Vyote vinaanza na maono ya utukufu wa Mungu (Ezekieli 1; Ufunuo 1). Vinasisitiza hukumu: Ezekieli anatoa unabii wa kuanguka kwa Yerusalemu kwa sababu ya dhambi (Ezekieli 4–24), wakati Ufunuo unatangaza hukumu ya Mungu kwa ulimwengu kupitia mihuri, tarumbeta/baragumu, na vitasa (Ufunuo 6–16). Vitabu hivi pia vina hukumu dhidi ya mataifa (Ezekieli 25–32; Ufunuo 17–18) na ushindi wa mwisho dhidi ya nguvu za uovu (Ezekieli 38–39; Ufunuo 19–20). Mada za urejesho ni za msingi, ambapo Ezekieli anatoa ahadi ya kufufuliwa kwa Israeli, uamsho wa kiroho (Ezekieli 37), na hekalu jipya (Ezekieli 40–48), huku Ufunuo ukionyesha Yerusalemu Mpya, urejesho wa kiroho, na Mungu kukaa milele na watu wake (Ufunuo 21–22).

[2] Mfalme Yehoyakini kwa jina jingine anatambulika kama Yekonia.

[3] Ni vigumu kujua kwa hakika muonekano sahihi wa kile Ezekieli alikiona katika maono yake. Hii ni kwa sababu anatumia lugha ya mfananisho (kwa kutumia neno “kama”) kuelezea alichokiona. Mambo anayoyaelezea hajawahi kuyaona kabla katika maisha yake, ndiyo maana anatumia vitu alivyowahi kuviona kufananisha na vile alivyoviona katika maono hayo. Kwa ujumla, aliona viumbe wanne waliobeba kiti cha enzi, Mungu akiwa ameketi juu ya enzi hiyo.

[4] Mstari wa 11 unaonyesha wazi kwamba wapokeaji wa awali wa ujumbe wa Ezekieli walikuwa ni watu waliokuwa tayari utumwani Babeli. Ujumbe wake haukuwa moja kwa moja kwa watu waliobaki Yuda/Israeli.

[5] Miji mingi ya kale ilikuwa imezungushiwa ukuta kama njia ya kujilinda na uvamizi. Kwa sababu ya kuwepo kwa kuta, miji ilikuwa na mnara ambao juu yake alikuwapo mlinzi wa mnara, ambaye kazi yake ilikuwa kuangalia nje ya ukuta kama kuna adui yeyote anayekuja na, kama kuna adui, kupiga mbiu kuwajulisha watu waliopo ndani ya mji huo. Hii ndiyo picha ambayo Mungu anamwelekeza Ezekieli kwamba yeye amefanyika mlinzi wa mnara.

[6] Kuzingirwa ni hali ya mji au eneo kufungwa na maadui ili watu walioko ndani ya mji wasitoke nje na walioko nje wasiingie ndani. Mbinu hii mara nyingi inakuwa na lengo la kuwanyima watu wa ndani chakula, maji, au msaada wowote kutoka nje. Kwa miji ya zamani ambayo ilikuwa imezungukwa na kuta pande zote, mbinu hii ilikuwa ni mbinu nzuri ya kushinda vita.

[7] “Wakati wa kujenga nyumba si karibu; mji huu ni sufuria na sisi ni nyama” usemi huu ndio ulitumika na viongozi ukiwa na maana ya kutangaza kwamba watu ndani ya Yerusalemu wako salama na hivyo hawana haja ya kuwa na wasi wasi. Kumbuka ujasiri huu ulitoka na theologia ya watu wa Yuda, ambapo waliamini kwamba kwa sababu Yerusalemu ni mji mteule wa Mungu, hivyo hatuwezi kuangamizwa kabisa.

[8] Matukio haya anayoyaeleza Ezekieli; matukio ya mfalme Yekonia kupigwa na kupelekwa utumwani Babeli na kuwekwa kwa Sedekia kuwa mfalme, na Sedekia kuigeukia Misri ili kujitoa chini ya utawala wa Babeli, yanapatikana katika kitabu cha 2 Wafalme 24. Utimilifu wa unabii kwamba mfalme Sedekia hatafanikiwa katika kuigeukia Misri kwa msaada na hivyo atapigwa na kupelekwa uhamishoni Babeli unarekodiwa pia katika 2 Wafalme 25.

[9] Taarifa hizi ni kuhusu Yerusalemu kupigwa, wakazi wake kuuawa, na wengine kuhamishwa kama unabii unavyosema. Taarifa hizi zitapokelewa na walioko Babeli, ambao ndio wasikilizaji wa ujumbe wa Ezekieli, na zitawamaliza nguvu kabisa. Hawatakuwa na tumaini tena baada ya kusikia kuhusu tukio hilo.

[10] Yeye aliye haki ambaye Mungu atampa ufalme ni Masihi. Maandiko haya yanatabiri kwamba kiti cha kifalme kitapinduliwa mpaka pale Masihi atakapokuja.

[11] Tukio la taifa la Israeli kupigwa na kupelekwa utumwani linaelezwa katika kitabu cha 2 Wafalme 17:1-23. Hili ni tukio lililotokea baada ya Israeli kugawanyika na kuwa mataifa mawili, yaani Yuda na Israeli. Hivyo, kuanguka kwa taifa hili kunakosimuliwa hapa hakuhusishi taifa la Yuda.

[12] Sura hii ya 27 inafanana sana na maono ya Yohana katika Ufunuo 18. Kama ilivyokuwa kwa Mji wa Tiro, kwamba kiburi chake kilichozaliwa kwa sababu ya utajiri wake (Ezek. 28:1-2, 6-9) ndicho kilichosababisha anguko lake, ndivyo Yohana anavyoona juu ya Babeli/Roma. Pia, sura hizi zinafanana na ujumbe wa Isaya kuhusu Babeli yenyewe (Isa. 47:7-11).

[13] Hii ni lugha ya picha ya kutabiri ujio wa Masihi, ambaye atatoka katika uko wa Daudi.

[14] Katika nyakati hizi za kale, Nchi zilifahamika na kujitambulisha na miungu, hivyo kupigwa kwa taifa ilikuwa ni aibu kwa Mungu au miungu ambayo taifa imejitambulisha nayo. Soma 2 Wafalme 18:33-35. Hivyo, kupigwa kwa Yuda na Babeli kulionekana kama kushindwa kwa Yahweh dhidi ya mungu Marduki/Bel. Mungu Marduki ndiye alikuwa mungu mkuu kati ya miungu mbalimbali iliyokuwa inaabudiwa na Babeli.

[15] Ufufuo huu unaozungumza hapa sio ufufuo wa miili, bali ni lugha ya picha inayoashiria kuwa hai katika mahusiano na Mungu.

album-art

00:00