MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA MTUME PAULO KWA FILEMONI.
MAELEKEZO
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI
Waraka wa Mtume Paulo kwa Filemoni ni waraka mfupi kuliko nyaraka zote za Mtume Paulo katika Biblia. Waraka huu Mtume Paulo aliuandika kwa ajili ya Filemoni, mwamini tajiri aliyekuwa akiishi Kolosai. Waraka huu unaeleza juu ya mtumwa wa Filemoni aitwaye Onesimo. Onesimo inaonekana alikimbia kwa bwana wake Filemoni, na baadaye akakutana na Paulo gerezani, ambapo akamwamini Kristo. Kutokana na kuamini kwa Onesmo na historia yake, Paulo akaamua kumwandikia barua Filemoni, mwamini aliyekuwa anamfahamu kumsihi ampokee Onesimo tena, si kama mtumwa tu, bali kama ndugu katika Kristo. Pamoja na barua kumlenga Filemoni, barua hii ilikusudiwa kusomwa/kusikilizwa na kanisa zima.
FILEMONI
Filemoni alikuwa mwamini tajiri anayeishi Kolosai, mtenda kazi pamoja na Paulo, na mwenyeji wa kanisa lililokutana nyumbani kwake (Filemoni 1:1-2).[1]Kwa kanisa kukutana nyumbani kwake na kwa Paulo kumwandikia barua kuna uwezekano mkubwa Filemoni alikuwa kiongozi katika kanisa lililokuwa linakutana nyumbani mwake.
ONESIMO
Onesimo alikuwa mtumwa wa Filemoni ambaye alikimbia kutoka kwa bwana wake, huenda akiwa ameiba kitu au akiwa amefanya kosa lingine lolote ambalo lilisababisha uhusiano wao kuwa na doa. Katika hali hiyo, alikutana na Paulo akiwa kifungoni, na Paulo akamhubiria na hatimaye akaamini. Baada ya kuamini, Paulo anamuona Onesimo ndugu yake katika Kristo na anamrudisha kwa Filemoni si kama mtumwa tena, bali akiwa ndugu mpendwa (Filemoni 1:16).
SABABU YA KUANDIKWA KWA WARAKA HUU
Sababu ya Mtume Paulo kuandika barua hii kwa Filemoni ni kumsihi Filemoni ampokee mtumwa wake Onesimo ambaye alimkosea. Paulo anataka Filemoni ampokee Onesimo si tu kama mtumwa bali kama ndugu katika Kristo. Mtume Paulo anamtetea Onesimo ambaye alikuwa amemkimbia bwana wake Filemoni, lakini sasa amebadilika na kuwa Mkristo, na Paulo anamsihi Filemoni amsamehe na ampokee tena kwa upendo (Filemoni 1:16-17). Pamoja na barua hii kumlenga Filemoni, barua hii mtume Paulo alikuwa amekusudia usomwe/kusikilizwa na kanisa zima, hivyo haikuwa barua kwa ajili ya Filemoni peke yake bali ilikuwa ni kwa ajili ya kanisa zima. Kwa sababu hiyo, barua hii pia ina lengo la kutoa mfano halisi wa namna ambavyo waamini wanatakiwa kusamehe kama Kristo Yesu alivyofanya.
Barua hii iliandikwa na Mtume Paulo akiwa katika kifungo chake cha kwanza huko Rumi. Barua ilipelekwa Kolosai na Tikiko akiwa pamoja na Onesimo. Kwa pamoja, walibeba pia barua ya Wakolosai na Waefeso (Wakolosai 4:7–9; Waefeso 6:21–22).
MPANGILIO WA WARAKA
| NAMBA | MAANDIKO | MAELEZO |
| 1 | 1:1-3 | Anuani ya waraka na salamu |
| 2 | 1:4-7 | Shukrani na maombi |
| 3 | 1:8-16 | Maelezo ya badiliko alilolipokea Onesimo baada ya kuiamini injili |
| 4 | 1:17-22 | Ombi la Paulo kwa Filemoni la kumpokea Onesimo |
| 5 | 1:23-25 | Salamu za mwisho na baraka |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI
Kama ilivyokuwa kawaida ya barua za karne ya kwanza, barua hii inaanza na utangulizi, utangulizi ukiwa na anuani, salamu na shukrani. Paulo anajitambulisha kuwa ndiye mwandishi wa barua hii akiwa na Timotheo. Paulo anajiweka wazi kama mfungwa wa Kristo Yesu kwa sababu wakati huu alikuwa kifungoni. Baada ya kujitambulisha anataja wapokeaji wakusudiwa wa waraka wake (1:1-2). Baada ya anuani hiyo, Mtume anatoa salamu zake kwa kanisa (1:3). Maneno “mpendwa” na “mtenda kazi pamoja nasi,” ni maneno yanayoonyesha uhusiano wa karibu kati ya Mtume Paulo na Filemoni.
Baada ya Anuani na salamu za awali mtume Paulo anatoa taarifa kwa Filemoni kwamba siku zote huwa anamshukuru Mungu katika maombi kwa ajili ya imani yake kwa Kristo na upendo wake kwa watakatifu. Pamoja na taarifa yake ya Maombi, Paulo bado anamuombea Filemoni kwamba imani yake izidi kufanya kazi zaidi. Na maombi haya ni kwa sababu Paulo ana taarifa kwamba Filemoni umeburudisha maisha ya waamini wengine (1:5-7).
Baada ya utangulizi huo, barua hii inaingia katika sehemu kuu ya ujumbe wake. Katika sehemu hii, Paulo anaeleza kwamba anaghairi kutumia mamlaka yake ya kuagiza, bali anamwomba kwa upendo Filemoni amkubali Onesimo. Ni kweli kwamba Onesimo hapo awali hakuwa wa manufaa, lakini baada ya kukutana na Paulo gerezani, amebadilika na sasa ni mtu anayefaa sana kwa sababu ya imani yake kwa Kristo. Paulo anaongeza kuwa alitamani abaki na Onesimo kwa kuwa amekuwa mtu wa karibu sana naye moyoni, lakini hakutaka kufanya hivyo bila ridhaa ya Filemoni (1:8-14).
Baada ya ombi hilo, Paulo anaongeza kwa kusema kwamba tukio la kuharibika kwa uhusiano kati ya Onesimo na Filemoni kwa muda lilikuwa ni tukio lenye manufaa kiroho. Katika tukio hili, Filemoni alitengana na Onesimo kwa muda ili waungane milele katika Kristo. Na wa sababu ya tukio hilo, Onesimo amebadilika kutoka kuwa mtumwa na kuwa ndugu mpendwa (1:15-16).
Paulo anaendelea kumsihi Filemoni ampokee Onesimo kama ambavyo angempokea yeye mwenyewe. Zaidi, Paulo anasema kwamba kama kuna chochote ambacho Onesimo anapaswa kulipa, basi yeye mwenyewe yuko tayari kulipa kwa niaba ya Onesimo. Pamoja na kuonyesha utayari huo, Paulo anaamini kwamba Filemoni atampokea Onesimo bila masharti yoyote. Kutokana na imani hiyo kwa Filemoni, Paulo anamwagiza amuandalie mahali pa kukaa kwa kuwa anatarajia kufika Kolosai (1:17-22).
Baada ya ujumbe huo, barua inafikia mwisho. Mwishoni mwa barua, Paulo anahitimisha kwa kutuma salamu kutoka kwa watu aliokuwa pamoja nao: Epafra, Marko, Aristarko, Demasi, na Luka. Hawa ni washirika wa huduma wa Paulo ambao walikuwa wakishirikiana naye katika kazi ya Injili. Mwisho kabisa, Paulo anamaliza barua yake kwa kutoa baraka ya amani kwa Filemoni, akimwombea neema ya Kristo iwe juu ya roho yake na kanisa kwa ujumla (1:23-25)
FOOTNOTES
[1] Biblia haijasema wazi kwamba Filemoni alikuwa tajiri, lakini kutokana na yeye kuwa na mtumwa na waamini kukusanyika katika nyumba yake, ni dhahiri kwamba alikuwa tajiri. Hii ni kwa sababu sifa hizi mbili zilikuwa ni za waamini wenye uwezo wa kiuchumi.
Unakuja hivi karibuni…

