MWONGOZO WA KUSOMA UJUMBE WA NABII HAGAI.
MAELEKEZO.
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI.
Ujumbe wa Nabii Hagai uliopo kwenye kitabu hiki ulitolewa kwa kipindi cha wiki kumi na tano tu, yaani miezi mitatu na wiki tatu. Ujumbe huu, uliotolewa katika semina nne tofauti, ulianza tarehe mosi ya mwezi wa sita (Hagai 1:1) na kumalizika tarehe ishirini na nne ya mwezi wa tisa (Hagai 2:10, 20), katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario katika Dola ya Uajemi.[1] Ujumbe wa nabii ulikuwa kwanza kwa viongozi wawili, yaani Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu. Pili, ujumbe huo ulikuwa kwa ajili ya Waisraeli waliorudi nyumbani kutoka utumwani. Baada ya kazi hii ya muda mfupi ya nabii Hagai, nabii Zekaria aliendeleza kazi ya kuwasukuma na kuwatia moyo viongozi hawa wawili na Waisraeli ili kujenga tena Hekalu (Ezra 5:1, 6:14).
MUKTADHA WA KIHISTORIA WA UJUMBE WA NABII HAGAI.
Baada ya utawala wa Suleimani kuisha, taifa la Israeli liligawanyika na kuwa mataifa mawili: Israeli na Yuda (1 Wafalme 12:1-22). Israeli walianza kuabudu sanamu mara tu baada ya kutengana na Hekalu la Jerusalem (1 Wafalme 12:23-33). Hivyo, Mungu akawatuma manabii kuwaonya kwa mabaya waliyoyafanya. Kati ya manabii wengi Mungu aliowatuma, wapo Hosea na Amosi. Kwa kuwa Israeli haikusikia sauti ya Bwana kupitia manabii hao, Mungu aliruhusu Israeli kupigwa na kuchukuliwa mateka na Dola ya Ashuru. Dola ya Ashuru iliwatawanya Waisraeli kwenye maeneo mbalimbali na kuwachukua watu wengine kutoka maeneo mengine na kuwaleta kwenye ardhi ya Israeli, na hivyo Israeli ikapoteza utaifa wake (1 Wafalme 17).
Pamoja na hayo, taifa la Yuda halikujifunza kutoka kwa ndugu zao; nao walifanya mabaya mbele za Mungu (1 Wafalme 17:19). Mungu pia aliwatuma manabii kwa taifa la Yuda kuwaonya kutokana na dhambi zao, hasa ibada ya sanamu na udhalimu wa kijamii/ukiukaji wa haki katika jamii (1 Wafalme 17:13). Kati ya manabii wengi Mungu aliowatuma, wapo Mika, Isaya, na Yeremia. Kwa kukosa kutubu, Mungu aliruhusu taifa la Yuda kupigwa na watu wake kupelekwa utumwani Babeli kwa awamu mbili: awamu ya kwanza chini ya ufalme wa Yehoyakimu (2 Wafalme 23:34-24:1-7) na awamu ya pili wakati wa ufalme wa Yehoyakini (2 Wafalme 24:8-20). Pamoja na watu wengine kubaki Yuda na mfalme Nebukadneza kuweka mfalme juu ya Yuda, Israeli waliobaki hawakumrudia Mungu, na hivyo Nebukadneza akarudi tena na kuupiga mji wa Jerusalemu na kuuchoma moto (2 Wafalme 25). Hili lilitokea baada ya nabii Ezekieli kutabiri hivyo kwa wale waliokuwa utumwani tayari wakati na yeye akiwa utumwani. Mpaka hapa, Israeli na mataifa mengine mengi yalikuwa yanatawaliwa na Dola ya Babeli.
Kama Mungu alivyotabiri kupitia kinywa cha nabii Danieli (na Isaya pia) kwamba atainua ufalme mwingine baada ya Babeli, basi Mungu akainua Dola ya Umedi na Uajemi (Danieli 2, 7, na 8). Umedi na Uajemi walipiga Dola ya Babeli na hivyo mateka wote na makoloni yote ya Babeli yakawa chini ya utawala wa Umedi na Uajemi. Mungu akatumia utawala huu kuwaruhusu taifa la Yuda kurudi nyumbani kwao na kuwa na shughuli zao za ibada kama ilivyokuwa mwanzo (2 Nyakati 36, Ezra 1:1-4). Hii ni baada ya taifa la Yuda kuwa utumwani Babeli kwa muda wa miaka sabini kama ilivyotabiriwa na nabii Yeremia (Yeremia 25:1). Sera ya utawala wa Umedi na Uajemi iliwaruhusu mateka kurudi kwenye mataifa yao na kuendelea na shughuli zao za kuabudu pamoja na kwamba waliendelea kuwa chini ya utawala huu.
Waliporuhusiwa kurudi, watu wa Yuda hawakurudi wote kwa wakati mmoja; walirudi kwa makundi matatu tofauti. Kundi la kwanza lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Sheshbaza na Zerubabeli, na kusudi lao lilikuwa ni kujenga Hekalu kwanza (Ezra 1-6). Baada ya hatua za kwanza za ujenzi, yaani ujenzi wa msingi (Ezra 3:8-13), upinzani kutoka nje na ndani ulisimamisha kazi kwa muda wa miaka 14. Kwa kusimamishwa kwa kazi ya Hekalu, watu walianza kufuata maslahi yao ya kibinafsi na kujijengea wenyewe majumba mazuri ya kuishi, wakisahau kabisa ujenzi wa Hekalu waliouachia njiani. Hapo ndipo Mungu alipomtuma nabii Hagai kuwarudisha Yuda katika ujenzi wa Hekalu. Baada ya nabii Hagai, nabii Zekaria aliendeleza kazi, na mwishowe Hekalu likajengwa na kukamilika miaka minne baadaye (Ezra 6:14-15).
Kundi la pili la Waisraeli lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Ezra, ambaye alirudisha usomaji na ufuataji wa torati ya Musa (Ezra 7-10). Kundi la tatu lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Nehemia, ambaye alirudi kwa lengo la kujenga tena ukuta wa Yerusalemu uliobomolewa (Nehemia 1-13).
.
UJUMBE MKUU WA NABII HAGAI.
Ujumbe wa Nabii Hagai unasisitiza umuhimu wa kutanguliza ujenzi wa Hekalu la Mungu kule Yerusalemu baada ya Waisraeli kurudi kutoka utumwani/uhamishoni. Hagai anawataka watu wazingatie njia zao na kutanguliza nyumba ya Mungu kuliko mambo yao wenyewe (1:1-15). Licha ya kufikiri kwamba Hekalu hili jipya halitakuwa na utukufu kama lile la kwanza, Hagai anawahakikishia watu kwamba Mungu yuko pamoja nao na hivyo Hekalu hili litakuwa na utukufu kuliko lile la kwanza (2:1-9). Pia Mungu anawaonyesha watu wake kwamba dhambi ya kukataa kujenga Hekalu lake iliwafanya kila wanachokifanya kuwa najisi mbele zake, lakini sasa kwa kuwa wamekubali kujenga Hekalu, atawabariki (2:10-19). Hatimaye, Hagai anahitimisha kwa ahadi kwa Zerubabeli, akithibitisha jukumu lake na hatima yake kama kiongozi aliyechaguliwa (2:20-23). Kwa ujumla, kuna mambo matatu ya msingi katika ujumbe wa nabii Hagai: kujengwa kwa Hekalu la pili lenye utukufu kuliko lile la kwanza (2:6-9), falme kupinduliwa na kupigwa (2:20-22), na kurejeshwa kwa uongozi wa ukoo wa Daudi katika Israeli (2:23).
MPANGILIO WA KITABU.
Namba | Maandiko | Maelezo |
1 | 1:1-15 | Hotuba ya Kwanza |
2 | 2:1-9 | Hotuba ya Pili |
3 | 2:10-19 | Hotuba ya Tatu |
4 | 2:20-23 | Hotuba ya nne |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.
Hotuba ya kwanza ya nabii Hagai ilitolewa siku ya kwanza ya mwezi wa sita mwaka wa pili wa mfalme Dario juu ya Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki (1:1). [2] Hotuba hii inaanza na kukosoa mtazamo mbaya wa waisraeli uliowafanya wasijenge nyumba ya Mungu (1:2), na badala yake wakajenga nyumba zao wenyewe na kutelekeza nyumba ya Mungu (1:3-4). Hivyo, Bwana anawaita kutafakari chaguo hili walilolifanya (1:5). Baada ya hilo, Bwana anawaonyesha madhara waliyoyapata tayari kwa sababu tu waliacha kujenga nyumba yake (1:6-11). Madhara haya ni pamoja na kukosa utoshelevu katika maeneo mbalimbali (1:6). Kabla ya kuendelea kuwaonyesha madhara yaliyowapata, Mungu anawaita kutafakari na kuwataka wamjenge yeye nyumba (1:7-8). Madhara mengine yaliyowapata ni kupata matokeo wasiyoyapenda (1:9), kukosa mvua na mazao (1:10), na kupata ukame katika hali na kazi zote za mikono (1:11). Baada ya hotuba hii ya kwanza, Viongozi hawa wawili pamoja na waisraeli walitii sauti ya Mungu wakaanza kujenga tena Hekalu siku ya ishirini na tatu toka siku ya kutolewa ujumbe huu (1:12-15).
Hotuba ya pili ya nabii Hagai ilitolewa mwezi mmoja baadaye, yaani siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba wa mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario (2:1-2). Katika Hotuba hii, Mungu anawaonyesha kwamba kwa mtazamo Hekalu hili wanalojenga sasa halina viwango ukilinganisha na Hekalu la mwanzo lililojenga na Suleiman (2:3). Lakini pamoja na muonekano huo, Mungu anawatia moyo kwamba yeye yuko pamoja nao (2:4-5). Kwa kuwa yuko pamoja nao, yeye atalifanya Hekalu hili kuwa bora zaidi ya lile lililojengwa na Suleimani kwa kuwafanya mataifa walete vitu vya thamani katika hekalu hili, kwa kuwa vitu hivyo ni mali yake yeye. Vitu hivyo ni kama fedha na dhahabu (2:6-9).
Hotuba ya tatu ilitolewa siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa ya mwaka huo huo, yaani miezi mitatu baada ya kuanza kulijenga tena Hekalu la Bwana (2:10). Katika Hotuba hii Mungu anawauliza makuhani maswali mawili ili kupitia majibu yao awajulishe Israeli hali yao (2:11). Swali la kwanza, Je, kitu kitakatifu kikigusa vyakula , vyakula hivyo vinatakasika? Jibu ni hapana (2:12). Swali la pili, Je, ikiwa kitu najisi kikigusa vyakula, vyakula vinakuwa najisi? Jibu ni ndio (2:13). Kwa kanuni hii, ni dhahiri utakatifu hauji kwa kugusana ( hauwezi kuhamishwa), lakini unajisi unaletwa kwa kugusana (unahamishika). Kupitia kanuni hii Mungu anawaonyesha Israeli hali yao. Kwa sababu ya kukataa kujenga nyumba yake (Unajisi) hivyo kazi zote wanazozinfanya ni najisi (2:14). Hivyo Bwana anawaambia watafakari yaliyowapata wakati ambao hawakuwa watiifu, Mungu aliwazuia wasifanikiwe (2:15-16), na akawapiga kwa upepo, ukungu na mvua ya mawe (2:17). Bwana anawaita tena kutafakari jinsi ilivyo tangu walivyoanza kujenga nyumba yake, kwamba yeye ameanza kuwabariki ndio maana wameweza kupanda na hivyo sasa wanasubiria mavuno ambayo yatakuwa ni ya baraka (2:18-19).
Siku hiyo hiyo ambayo Hagai ilitoa hotuba yake ya tatu, akatoa hotuba ya nne (2:20). Hotuba hii ni fupi kuliko zote zilizopita na ni utabiri kwa Zerubabeli, liwali wa Yuda. Mungu anasema kwamba, kupitia Zerubabeli, liwali wa Yuda Mungu atapindua na kuzipiga falme zingine (2:21-22). Na baada ya hilo Mungu anaahidi kumfanya Zerubabeli kuwa mtawala teule mwenye mamlaka yake (2:23).
FOOTNOTES
[1] Kwa kalenda huu ulikuwa ni mwaka 520 K.K.
[2] Kwa kalenda ilikuwa ni tarehe 29 mwezi wa nane mwaka 520 K.K.
UFAFANUZI UJUMBE WA NABII HAGAI
UTANGULIZI
Baada ya kitabu cha Sefania katika Biblia zetu za Kiprotestanti, tunakutana na kitabu cha nabii Hagai. Baada ya kitabu hiki, kuna vitabu viwili mbele yake, yaani kitabu cha Zekaria na Malaki. Vitabu hivi vyote vitatu vinafuatana na jumbe zake zilitolewa baada ya Israeli/Yuda kuruhusiwa kurudi katika ardhi yao ya nyumbani baada ya kipindi cha miaka sabini ya utumwa kule Babeli. Kitabu cha Hagai ni moja ya vitabu ambavyo havisomwi mara kwa mara katika kanisa, isipokuwa kwa nukuu zake chache ambazo waamini wanazipenda. Nukuu hizi ni kama vile, “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi” (2:8). Ukiacha nukuu kama hizo, ujumbe wa nabii Hagai haujafuatiliwa kwa ukaribu na waamini wengi. Pamoja na kutokufuatiliwa na waamini wengi, ujumbe wa nabii Hagai ni muhimu sana kwa kanisa la karne ya ishirini na moja kama ulivyokuwa muhimu kwa watu wa Israeli/Yuda.
MWANDISHI WA KITABU
Baada ya kitabu cha Sefania katika Biblia zetu za Kiprotestanti, tunakutana na kitabu cha nabii Hagai. Baada ya kitabu hiki, kuna vitabu viwili mbele yake, yaani kitabu cha Zekaria na Malaki. Vitabu hivi vyote vitatu vinafuatana na jumbe zake zilitolewa baada ya Israeli/Yuda kuruhusiwa kurudi katika ardhi yao ya nyumbani baada ya kipindi cha miaka sabini ya utumwa kule Babeli. Kitabu cha Hagai ni moja ya vitabu ambavyo havisomwi mara kwa mara katika kanisa, isipokuwa kwa nukuu zake chache ambazo waamini wanazipenda. Nukuu hizi ni kama vile, “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi” (2:8). Ukiacha nukuu kama hizo, ujumbe wa nabii Hagai haujafuatiliwa kwa ukaribu na waamini wengi. Pamoja na kutokufuatiliwa na waamini wengi, ujumbe wa nabii Hagai ni muhimu sana kwa kanisa la karne ya ishirini na moja kama ulivyokuwa muhimu kwa watu wa Israeli/Yuda.
AINA YA KITABU/UANDISHI
Kitabu hiki kinarekodi hotuba za nabii Hagai, ambapo baadhi ya hotuba hizi zilitolewa kwa kufuata kanuni za kiushairi kama zilivyo hotuba nyingine za manabii. Hotuba hizi za nabii Hagai zinasindikizwa na simulizi ya matukio kabla au (na) baada ya hotuba husika. Hotuba ya kwanza (1:2-11) inatanguliwa na usimulizi (1:1) na inafungwa na usimulizi (1:12-15). Hotuba ya pili (2:3-9) inatanguliwa na usimulizi (2:1-2). Hotuba ya tatu (2:12-19) inatanguliwa na usimulizi (2:10-11) na hotuba ya mwisho (2:21-23) pia inatanguliwa na usimulizi (2:20).
MUKTADHA WA KIHISTORIA WA KUTOLEWA UJUMBE
Baada ya utawala wa Suleimani kuisha, taifa la Israeli liligawanyika na kuwa mataifa mawili: Israeli na Yuda (1 Wafalme 12:1-22). Israeli walianza kuabudu sanamu mara tu baada ya kutengana na Hekalu la Jerusalem (1 Wafalme 12:23-33). Hivyo, Mungu akawatuma manabii kuwaonya kwa mabaya waliyoyafanya. Kati ya manabii wengi Mungu aliowatuma, wapo Hosea na Amosi. Kwa kuwa Israeli haikusikia sauti ya Bwana kupitia manabii hao, Mungu aliruhusu Israeli kupigwa na kuchukuliwa mateka na Dola ya Ashuru. Dola ya Ashuru iliwatawanya Waisraeli kwenye maeneo mbalimbali na kuwachukua watu wengine kutoka maeneo mengine na kuwaleta kwenye ardhi ya Israeli, na hivyo Israeli ikapoteza utaifa wake (1 Wafalme 17).
Pamoja na hayo, taifa la Yuda halikujifunza kutoka kwa ndugu zao; nao walifanya mabaya mbele za Mungu (1 Wafalme 17:19). Mungu pia aliwatuma manabii kwa taifa la Yuda kuwaonya kutokana na dhambi zao, hasa ibada ya sanamu na udhalimu wa kijamii/ukiukaji wa haki katika jamii (1 Wafalme 17:13). Kati ya manabii wengi Mungu aliowatuma, wapo Mika, Isaya, na Yeremia. Kwa kukosa kutubu, Mungu aliruhusu taifa la Yuda kupigwa na watu wake kupelekwa utumwani Babeli kwa awamu mbili: awamu ya kwanza chini ya ufalme wa Yehoyakimu (2 Wafalme 23:34-24:1-7) na awamu ya pili wakati wa ufalme wa Yehoyakini (2 Wafalme 24:8-20). Pamoja na watu wengine kubaki Yuda na mfalme Nebukadneza kuweka mfalme juu ya Yuda, Israeli waliobaki hawakumrudia Mungu, na hivyo Nebukadneza akarudi tena na kuupiga mji wa Jerusalemu na kuuchoma moto (2 Wafalme 25). Hili lilitokea baada ya nabii Ezekieli kutabiri hivyo kwa wale waliokuwa utumwani tayari wakati na yeye akiwa utumwani. Mpaka hapa, Israeli na mataifa mengine mengi yalikuwa yanatawaliwa na Dola ya Babeli.
Kama Mungu alivyotabiri kupitia kinywa cha nabii Danieli (na Isaya pia) kwamba atainua ufalme mwingine baada ya Babeli, basi Mungu akainua Dola ya Umedi na Uajemi (Danieli 2, 7, na 8). Umedi na Uajemi walipiga Dola ya Babeli na hivyo mateka wote na makoloni yote ya Babeli yakawa chini ya utawala wa Umedi na Uajemi. Mungu akatumia utawala huu kuwaruhusu taifa la Yuda kurudi nyumbani kwao na kuwa na shughuli zao za ibada kama ilivyokuwa mwanzo (2 Nyakati 36, Ezra 1:1-4). Hii ni baada ya taifa la Yuda kuwa utumwani Babeli kwa muda wa miaka sabini kama ilivyotabiriwa na nabii Yeremia (Yeremia 25:1). Sera ya utawala wa Umedi na Uajemi iliwaruhusu mateka kurudi kwenye mataifa yao na kuendelea na shughuli zao za kuabudu pamoja na kwamba waliendelea kuwa chini ya utawala huu.
Waliporuhusiwa kurudi, watu wa Yuda hawakurudi wote kwa wakati mmoja; walirudi kwa makundi matatu tofauti. Kundi la kwanza lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Sheshbaza na Zerubabeli, na kusudi lao lilikuwa ni kujenga Hekalu kwanza (Ezra 1-6). Baada ya hatua za kwanza za ujenzi, yaani ujenzi wa msingi (Ezra 3:8-13), upinzani kutoka nje na ndani ulisimamisha kazi kwa muda wa miaka 14. Kwa kusimamishwa kwa kazi ya Hekalu, watu walianza kufuata maslahi yao ya kibinafsi na kujijengea wenyewe majumba mazuri ya kuishi, wakisahau kabisa ujenzi wa Hekalu waliouachia njiani. Hapo ndipo Mungu alipomtuma nabii Hagai kuwarudisha Yuda katika ujenzi wa Hekalu. Baada ya nabii Hagai, nabii Zekaria aliendeleza kazi, na mwishowe Hekalu likajengwa na kukamilika miaka minne baadaye (Ezra 6:14-15).
Kundi la pili la Waisraeli lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Ezra, ambaye alirudisha usomaji na ufuataji wa torati ya Musa (Ezra 7-10). Kundi la tatu lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Nehemia, ambaye alirudi kwa lengo la kujenga tena ukuta wa Yerusalemu uliobomolewa (Nehemia 1-13).
WAPOKEAJI WA AWALI WA UJUMBE
Hotuba ya kwanza na ya pili za nabii Hagai zimeelekezwa kwa viongozi wawili; Yoshua, kuhani mkuu na liwali Zerubabeli (1:1; 2:2). Hotuba ya pili pia inajumuisha “mabaki ya watu” (2:2), ikiwa na maana ya watu wote waliorudi kutoka utumwani. Hotuba ya tatu imeelekezwa kwa makuhani (Hagai 2:11), ikimjumuisha kuhani mkuu Yoshua. Hotuba ya nne ilitolewa siku hiyo hiyo ya hotuba ya tatu, na ilikuwa imeelekezwa kwa liwali Zerubabeli (Hagai 2:20). Hivyo, ujumbe huu ulikuwa maalum kwa viongozi hawa wawili na kwa watu wote waliorejea kutoka utumwani.
Kwa kuwa Dola ya Uajemi iliendelea kutawala juu ya makoloni yake pamoja na kwamba iliwapa uhuru watu kurudi katika ardhi za mababu zao, dola hii ilichagua viongozi katika majimbo iliyoyatengeneza. Kiongozi wa jimbo husika aliitwa Liwali. Hivyo, Zerubabeli alikuwa ni mmoja wa maliwali katika Jimbo la Yehudi (Jimbo la Kiyahudi lililojumuisha Yerusalemu). Maliwali wengine walikuwa ni Sheshbaza (Ezra 1:8) na Nehemia (Nehemia 5:14). Kwa ujumla, liwali alikuwa ni kiongozi wa kiserikali ambaye alitawala watu wake kwa niaba ya mfalme wa Dola ya Uajemi.
Kama ilivyokuwa kabla ya kwenda utumwani, Mungu aliamuru taifa kuwa na kuhani mkuu ambaye alikuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa sheria za Mungu na taratibu za ibada zinatekelezwa ipasavyo. Hivyo, kwa wakati huu, Mungu alimchagua Yoshua mwana wa Yehosadaki (Ezra 3:2) kuwa kuhani mkuu kwa watu wake.
Hivyo, jumbe za kitabu hiki zilikuwa kwa ajili ya kiongozi wa kiserikali na kiongozi wa kiimani, na hatimaye kwa watu wote.
MPANGILIO WA KITABU
Namba | Maandiko | Maelezo |
1 | 1:1-15 | Hotuba ya Kwanza (Hotuba ya Maonyo) |
2 | 2:1-9 | Hotuba ya Pili (Hotuba ya kutia moyo) |
3 | 2:10-19 | Hotuba ya Tatu (Hotuba ya kufundisha) |
4 | 2:20-23 | Hotuba ya nne (Hotuba ya urejesho) |
HAGAI 1:1-11
MAANDIKO
1 Katika mwaka wa pili wa Dario mfalme, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake Hagai nabii, kusema,
2 Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya Bwana.
3 Ndipo neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,
4 Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika?
5 Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.
6 Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.
7 Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.
8 Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema Bwana.
9 Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema Bwana wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake.
10 Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake.
11 Nami nikaita wakati wa joto uje juu ya nchi, na juu ya milima, na juu ya nafaka, na juu ya divai mpya, na juu ya mafuta, na juu ya kila kitu itoacho nchi, na juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya kazi zote za mikono.
UFAFANUZI.
Sura ya kwanza ya kitabu hiki inaweza kugawanywa katika sehemu kuu tatu; Sehemu ya kwanza ni utangulizi wa hotuba ya kwanza ya nabii Hagai (1:1), sehemu ya pili ni hotuba ya nabii Hagai (1:2-11) na sehemu ya tatu ni mwitikio wa wapokeaji wa awali wa ujumbe wa nabii Hagai (1:12-15).
Katika utangulizi, Mwandishi anaanza kitabu chake kwa kutujulisha ni wakati gani tukio analotaka kujulisha lilitokea. Mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario, mwezi wa sita na siku ya kwanza ndio siku ujumbe wa Mungu uliwafikia viongozi wawili ambao ni; Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu. Ujumbe huu uliwafikia kupitia kinywa cha nabii Hagai (1:1). Kabla ya Israeli/Yuda kwenda utumwani Manabii walikuwa wanataja Wafalme wao katika kutaja kalenda za jumbe zao (Mfano Isaya 1:1 na Yeremia 1:1-3), lakini kwa sasa kwa sababu Israeli/Yuda ilikuwa haina mfalme na ilikuwa chini ya utawala wa dola ya Uajemi ndio maana mfalme Dario wa Uajemi anatajwa. Mfalme Dario alikuwa ni mfalme wa nne kutoka kwa mfalme Koreshi, mfalme aliyetoa ruhusa watu wa Yuda kurudi nchini kwao na kuwaruhusu kujenga hekalu lao.
Ujumbe wa Bwana kwa viongozi hawa ulikuwa kuhusu maisha ya watu wa Yuda. Watu wa Yuda wanasema, huu sio wakati sahihi wa kujenga nyumba ya Bwana. Nyumba ya Bwana ilikuwa ni hekalu lililojengwa na mfalme Suleimani (1 Wafalme 6) na kubomolewa na mfalme Nebukadreza (2 Wafalme 25:1-26). Hekalu hili lilianza kujengwa tena upya mara tu baada ya kundi la kwanza la watu kurudi kutoka utumwani, lakini kazi hii iliishia kwenye msingi kwa sababu ya upinzani (Ezra 4:7-24). Kwa muda mrefu watu walikuwa wanasema kwamba “muda huu sio sahihi kujenga nyumba ya Bwana”(1:2). Kwa kuwa watu wa Yuda walikuwa wanasema hivyo, Mungu anatoa ujumbe kwao (1:3) unaoanza na kuwauliza swali la balagha; Swali ambalo jibu lake wasikilizaji wanalo. Mungu anawauliza, Je, huu ndio wakati wa wao kuendelea na maisha yao ya kibinafsi ya kujenga nyumba zao wenyewe na kuacha nyumba yake/hekalu lake likiwa katika hali ya kutelekezwa? Swali hili linawataka wapokeaji wa ujumbe kuelewa Mungu anataka nini kutoka kwao. Lakini pia swali hili linatupa maelezo zaidi ya kuhusu nini kiliendea wakati watu wanasema huu sio wakati sahihi wa kujenga nyumba ya Bwana. Watu walijenga nyumba zao na kuendelea na maisha yao ya kibinafsi wakati wakisema huu sio wakati sahihi wa kujenga nyumba ya Bwana (1:4). Kinyume na mfalme Daudi, ambaye kwa kukaa katika nyumba yake kwa starehe kulimfanya atake kujenga hekalu la Bwana lakini nabii Nathani akamwambia asubiri (2 Wafalme 7), watu hawa hawataki kujenga nyumba ya Mungu wanataka kuendelea kukaa kwenye nyumba zao za starehe. Kutokana na hilo, Mungu anawaita watu wa Yuda kupitia nabii Hagai wainuke na kujenga nyumba yake.
Kwa kuwa bado wako kwenye hali ya kukataa kujenga nyumba yake, Mungu anawaita kutafakari maisha yao (1:5). Mungu anawatafakarisha mambo yaliyowapata kwa sababu ya kukataa kwao kujenga hekalu lake. Mambo matano Mungu anayataja yaliyowapata kwa sababu ya kukataa kwao kujenga hekalu lake. Mambo hayo ni kupanda mbegu nyingi lakini kuvuna kidogo; kula bila kushiba; kunywa bila kutosheka; kujivika nguo bila kupata moto (kuendelea kupata baridi); na kupata mshahara unaopotea (1:6). Kabla ya kuendelea kuwaonyesha watu wa Yuda madhara yaliyowapata kwa kukataa kwao kujenga nyumba yake, Mungu anawataka tena watafakari ili mwisho wa siku wajenga nyumba yake (1:7). Mungu anawataka waende milimani kupata malighafi za kujengea nyumba yake, ambapo ujenzi ukikamilika, Mungu atafurahia hekalu hilo na atatukuzwa kupitia hekalu hilo (1:8). Baada ya mwito huo, Mungu anaendelea kuwaonyesha mabaya yaliyowapata kwa sababu ya kukataa kwao kujenga nyumba yake. Madhara haya ni, kupata mavuno chini ya matarajio na hata yale mavuno machache yaliyopatikana kupukutika yakiwa yamepelekwa majumbani (1:9). Kupata ukame wa mvua na ardhi kutokutoa mazao yake (1:10). Ukame Bwana aliouleta uriathiri milima na mashamba ya nafaka, mashamba ya mizabibu na mashamba ya mizeituni na ya kila mmea. Lakini pia ukame huu uriathiri watu, wanyama, na kila kazi ya mikono (1:10). Madhara yote yaliyowapata watu wa Yuda hayakuwa mambo mapya, bali yalikuwa ni mambo yale yale Mungu aliwaambia Israeli yatawapata kama hawatasikia sauti yake katika Agano lake katika mlima Sinai. Laana hizi zilizotajwa mistari ya 6, 9-11 na 2:16-17 ahadi zake zilitolewa katika vitabu vya Mambo ya walawi 26:19–20, 26 na Kumbukumbu la torati 28:16, 18-19, 23–24, 30, 38–40, 48).
TUNAJIFUNZA NINI LEO?
- Kuweka vipaumbele sawa.
Ujumbe wa nabii Hagai kwa watu wa Yuda/Israeli ulikuwa ni kuwataka waache kujiweka mbele zaidi ya kazi ya kujenga hekalu. Kwa lugha rahisi, waache sababu walizokuwa nazo zilizowafanya waone kuwa muda wa kujenga hekalu la Bwana bado haujafika, ila muda wa kujenga nyumba zao na kuishi maisha yao uko tayari. Kwetu sisi katika kanisa, ujumbe huu unatuhusu kabisa. Tofauti na watu wa Yuda, sisi leo hekalu la Mungu/nyumba ya Mungu sio tena jengo lililokuwa limejengwa kule Yerusalemu, bali kwetu leo hekalu la Mungu/nyumba ya Mungu ni kundi la waamini (1 Wakorintho 3:16). Ujenzi wa hekalu la Mungu kwetu sio ujenzi wa majengo, bali ni ujenzi wa waamini (1 Wakorintho 3:10-15; Waefeso 4:7-16). Hivyo, kupitia ujumbe wa Hagai, Mungu anatutaka tuache ubinafsi wa kujenga nyumba zetu (hizi zinaweza kuwa familia zetu, uchumi wetu, majina yetu, vyeo vyetu, na kadhalika) na kuweka kipaumbele katika kuboresha maisha ya waamini sawasawa na Mungu anavyotaka.
Je, kuna jambo gani ninafanya sasa linalochangia ukuaji wa waamini wengine? Kama sina, basi Mungu ananiita kupitia ujumbe wa nabii Hagai kutafakari njia zangu na kuelekea kwenye kufanya mambo yatakayochangia ukuaji wa waamini wengine. Kila nikitaka kufanya jambo kwa ajili ya waamini wengine au kwa ajili ya kuwaleta watu kwa Kristo, napata sababu nyingi zinazoniambia wakati wa sasa sio sahihi. Nasubiri mwakani, nasubiri nipate ndoa, au nasubiri waniteue/wanichague? Kama ninazuiliwa na sababu ya “huu sio wakati sahihi” kufanya mambo yatakayoimarisha maisha ya waamini au kuwaleta wasioamini katika imani, basi ujumbe wa Mungu kupitia nabii Hagai unanihusu. Mungu ananiita kuepuka sababu zote na niingie katika ujenzi wa kanisa.
Je, ulianza maisha yako ya wokovu kwa kasi ya kumtumikia Mungu kupitia kuwatumikia watu wake, lakini sasa hivi unasema una majukumu mengi hivyo huwezi kufanya kama zamani? Mungu anakuita urudi kwenye ujenzi wa kanisa lake. Watu wa Yuda waliporudi kutoka utumwani walianza mara moja ujenzi wa hekalu, lakini walipopata upinzani waliacha kazi hiyo na wakageukia mambo yao. Hata leo inawezekana ulianza kwa bidii kutumika lakini ukakutana na aina mbalimbali za upinzani ukaamua kuacha kabisa kuwatumikia watu wa Mungu na ukaamua kufanya mambo yanayokufaidisha wewe binafsi. Basi, Mungu anakuita kupitia ujumbe wa nabii Hagai rudi kwenye ujenzi wa hekalu lake.
Pale ambapo Yesu anapotuambia, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6:33), Hagai anatuonyesha ni jinsi gani tunatakiwa kuweka ufalme wa Mungu kipaumbele cha kwanza.
- Kuadhibiwa na Bwana.
Mungu kwa kuwa aliwachagua Israeli kuwa taifa lake teule, na akafanya nao Agano pale sinai, aliahidi kuwa atakuwa anawaadhibu kama watakuwa wanaenda kinyume na maagizo yake. Kwa kuwa tumefundishwa swala la wokovu ni swala la kibinafsi , swala hili tunapolisoma (la kuadhibiwa) katika Biblia hasa Agano la kale linatengeneza picha mbaya ya Mungu. Mungu alipokuwa anawaadhibu Israeli kwa sababu ya kwenda kwao kinyume na Agano, ilikuwa ni kwa sababu anawapenda wao kuliko mataifa mengine yote. Hivyo, Mungu anapowaita watu wa Yuda kujenga hekalu anawatazamisha adhabu alizowapa lakini hawakutaka kusikia. Adhabu zilikuwa na lengo la kutaka kuwarejesha kwenye makusudi yake. Vivyo hivyo, kwa watu wa Mungu wa sasa, yaani kanisa, Mungu hutumia adhabu kuturejesha kwenye makusudi yake. Mwandishi wa Waebrania anatuonyesha kwamba Mungu huwaadhibu wanae. Na ikiwa tunaendelea kufanya mambo kinyume na mapenzi yake na hakuna adhabu basi ni ushahidi tosha kuwa sisi si wanae (Waebrania 12:7-8). Kwa Waisraeli Mungu aliorodhesha adhabu zote atakazozitoa kwao ikiwa wataenda kinyume na mapenzi yake (Walawi 26:Torati 28-30), lakini kwa kanisa hajatoa orodha ya nini itakuwa adhabu kwa waamini wakiendelea kufanya mambo kinyume na mapenzi yake. Pamoja na kwamba hakuna orodha ya adhabu Mungu atakazozitoa kwa waamini kama wataendelea kuishi kinyume na mapenzi yake, tuna mfano wa waamini wenzetu walioadhibiwa na Mungu kwa sababu waliendelea kubomoa hekalu la Mungu badala la kulijenga (1 Wakorintho 11:17-34). Waamini hawa, wengine walipata udhaifu, wengine magonjwa na wengine walikufa katika mwili. Haya yote yalitokea kwa kuwa walikuwa wanalibomoa hekalu la Mungu (1 Wakorintho 11:17-18, 22) badala ya kulijenga.
Ujumbe wa nabii Hagai sawa na ule wa mtume Paulo kwa wakorintho ni kwamba, kama tunafanya jambo la kukwamisha ukuaji wa maisha ya kanisa na tukiwa ni mtoto wa Baba, basi Baba atatuadhibu. Adhabu hii sio hukumu kama ya wale wasioamini (1 Wakorintho 11:32), bali ni matumizi ya maumivu (Waebrania 12:11) katika kuturudisha katika mapenzi yake. Kwa ujumbe wa Hagai mwamini unaitwa kujenga maisha ya waamini wengine na sio kudumaza/kukwamisha ukuaji wao, maana ukifanya hivyo adhabu ya Mungu haitazuilika (1 Wakorintho 3:16-17). Pia, ujumbe wa Hagai unatuita kutafakari mabaya tunayoyapitia. Je, mabaya tunayoyapitia yanatokana na adhabu ya Mungu kwa sababu tumeitupa mbali kazi yake ya kujenga kanisa lake au ni matokeo ya imani yetu kwake? Mateso/maumivu kwa waamini yanaweza kusababishwa na utii wao kwa Bwana (Warumi 5:3-5 ;8:18-25) au kutokana na kutokutii kwao (1 Wakorintho 11:17-34). Hivyo, Mungu anatuita kutafakari. Baada ya kutafakari, kama maumivu hayo yanasababishwa na kutokutii Mungu anatuita katika utii. Kutafakari ni muhimu kwa kuwa watu wa Yuda kwa kukosa kutafakari hawakuzingatia/hawakujua kwamba Mungu anawaadhibu ili warudi katika ujenzi wa nyumba yake (Hagai 2:17-18). Lakini pia, wakorintho kwa kukosa kutafakari hawakujua kama Mungu anawaadhibu kutokana na kazi yao ya kubomoa hekalu lake, mpaka pale walipojulishwa na mtume Paulo kupitia barua yake (1 Wakorintho 11:29-32). Mungu anatuita kutafakari.
- Furaha ya Mungu na kutukuzwa kwake.
Sababu ya Mungu kuwaita watu wa Yuda kujenga nyumba yake ilikuwa ni ili atape furaha na kutukuzwa kwa sababu ya Hekalu hilo. Kutukuzwa inaweza kuwa na maana mbili hapa, yaani kuweka utukufu wake au kupata sifa kwa sababu nyumba yake imejengwa. Hata leo, Mungu anafurahishwa na anatukuzwa kama waamini wanajengwa na wanafanyika imara katika imani yao. Kwa kuwa hii ndio sababu Mungu aliwapa watu wa Yuda wakati anawahimiza kujenga hekalu lake, sababu hii ndio inatakiwa pia kuwa sababu itakayo turudisha sisi leo katika kujenga hekalu la Mungu. Utukufu na furaha ya Mungu ndio iwe msukumo wa sisi kufanya kwa bidii kazi ya ujenzi wa maisha ya waamini.
Katika miaka ya hivi karibuni kumtumikia Mungu imekuwa ni kitu cha kuleta manufaa kwa “mtumishi” na hivyo imepelekea hata watu kuingia kwenye kile kinaitwa “utumishi” ili malengo yao ya maisha yatimie. Wakati mwingine mpaka watu wametiana moyo kuingia kwenye “utumishi” kwa kuambiana kwamba utumishi unalipa. Ujumbe wa Mungu kwetu kupitia nabii Hagai ni kwamba, tunatakiwa kufanya bidii ya kujenga maisha ya waamini ili Mungu apate furaha (kwa kuwa anafurahishwa na ubora wa maisha ya waamini) na kupitia ukuaji wa maisha ya waamini apate kutukuzwa. Nia yako na yangu ya kufanya utumishi iwe ni kuleta furaha kwa Mungu na utukufu kwake na sio kuleta furaha, manufaa au utukufu kwetu sisi.
HAGAI 1:12-15
MAANDIKO
12 Ndipo Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, pamoja na hayo mabaki yote ya watu, wakaitii sauti ya Bwana, Mungu wao, na maneno ya Hagai nabii, kama Bwana, Mungu wao, alivyomtuma; nao watu wakaogopa mbele za Bwana.
13 Ndipo Hagai mjumbe wa Bwana, katika ujumbe wa Bwana, akawaambia watu, akisema, Mimi nipo pamoja nanyi, asema Bwana.
14 Bwana akaiamsha roho ya Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na roho ya Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na roho zao mabaki ya watu; wakaenda, wakafanya kazi katika nyumba ya Bwana wa majeshi, Mungu wao;
15 katika siku ya ishirini na nne ya mwezi, katika mwezi wa sita, katika mwaka wa pili wa Dario mfalme.
UFAFANUZI
Baada ya unabii wa Hagai mwandishi anatupa taarifa ya nini kilitokea. Viongozi wawili ambao ndio walikuwa walengwa wa awali wa ujumbe huu, na watu waliorudi toka utumwani ambao walikuwa walengwa wanaofuata, walitii mwito wa Bwana wa kuacha kuishi kwenye maisha ya ubinafsi na kuingia kwenye kazi ya kujenga hekalu lake. Utii huu uliambatana na hofu ya watu kwa Mungu (1:12). Kwa sababu ya hofu hii Mungu anawatia moyo kwa kuwajulishwa kwamba yuko pamoja nao (1:13). Mwandishi anatuambia kwamba hatua za kwenda kujenga Hekalu baada ya ujumbe wa Hagai haikuwa ni maamuzi ya watu tu, bali nyuma yao kulikuwa na Mungu aliyewaamsha kutoka katika usingizi wa muda mrefu, ili waingie katika ujenzi wa nyumba yake (1:14). Kazi hii ya ujenzi ilianza siku ishirini na tatu tangu siku ambayo nabii Hagai alitoa ujumbe wake wa kwanza (1:15).
TUNAJIFUNZA NINI LEO?
- Utii ni kutenda sawa sawa na ujumbe wa Bwana.
Tunajifunza kutoka kwa wenzetu kwamba baada ya kuambiwa na Bwana watafakari na mwisho wa siku warudi kujenga hekalu, utii wao ulionekana mara kwa kurudi kujenga hekalu. Kama ambavyo tumejifunza hapo mwanzo kwamba, Mungu anatutaka tuingie kwenye ujenzi wa maisha ya waamini, hivyo utii kwa ujumbe wa nabii Hagai ni kuingia kwenye kufanya jitahada za kila namna zitakazosababisha maisha ya waamini yanakuwa bora zaidi kila inapoitwa leo. Mara nyingi baada ya kusikia ujumbe wa Mungu, pale tunapotaka kufanya yale tuliyoambiwa shetani huwa anatutengeneza mbadala. Kwa watu wa Yuda Mungu aliwaita kujenga hekalu lake Yerusalemu na wala sio sehemu nyingine na hekalu lilikuwa na vipimo vyake tayari vinavyotakiwa. Utii kwao ulikuwa ni kwenda kujenga hekalu Yerusalemu na sio kwingineko. Kama wangeamua kuchagua eneo jingine na kujenga jengo la hekalu bado kitendo hiki kingekuwa sio utii. Vivyo hivyo, Mungu anatuita sisi leo kujenga maisha ya waamini ambao ndio hekalu lake, usifanye tofauti na hilo kwa kuwa ukifanya hivyo hata kama utatumia nguvu na rasilimali kubwa kiasi gani bado utakuwa hujawa mtii. Shetani anaweza kukupa mbadala wa kujenga programu yenye sura kama ya utumishi kumbe programu hio haichangii chochote katika kuboresha maisha ya waamini au kuwaleta wasioamini katika imani. Shetani anaweza kukupa mbadala wa kujenga jina lako katika sura ya “utumishi”. Shetani anaweza kukupa mbadala wa kujenga taasisi ambayo haina mchango chanya katika kujenga maisha ya waamini au kawaleta wasioamini katika imani. Hayo yote yanaweza kuonekana kama ni utii kwenye “utumishi” lakini kama hayana mchango chanya katika kujenga maisha ya waamini au kuwaleta waliogiza katika nuru ya wokovu basi ni wito wa Mungu kwamba uyape kigosi na uingie katika ujenzi wa kweli wa kuboresha maisha ya watu wa Mungu.
- Ujumbe wa Bwana ni wa watu wake.
Tunaishi kwenye kipindi cha ubinafsi, kiasi ambacho mpaka ujumbe wa Biblia umepewa muelekeo wa kibinafsi kabisa. Popote neno la Mungu linapokuja kwa kanisa mara nyingi matarajio ni kwamba kila mmoja atachukua kinachomhusu na kuwaachia wengine mambo mengine. Lakini tunaona picha tofauti tunaposoma maandiko, ujumbe wa Hagai walengwa wake wa awali walikuwa ni viongozi wawili na watu wote walikuwa ni walengwa wanaofuata, lakini mwandishi anatuambia watu wa Yuda na viongozi wao walimtii Mungu kupitia ujumbe wa nabii Hagai. Mwitikio katika ujumbe haukuachwa kwenye “maamuzi ya moyoni” ya watu, mwitikio ulikuwa ni wa kundi la watu na ulikuwa ni wa vitendo. Mungu anatufundisha kanisa leo kwamba, ujumbe wake unapoletwa kwa ajili ya kanisa husika basi utii Mungu anaoutarajia sio wa mtu mmoja mmoja (sio wa ubinafsi), bali anatarajia utii wa kanisa kwa ujumla. Baba anapotuambia tumetanguliza “masumbufu ya maisha haya” na kutuelekeza ujenzi wa hekalu lake, anatarajia sisi wote kama kanisa kuitikia ujumbe huu kwa utii. Kila mwamini awe sehemu ya kundi lenye mwitikio chanya katika ujumbe wa Mungu. Kila mwamini ambidishe mwamini mwenzie kuitikia ujumbe wa Mungu kwa utii.
- Uhakika wa uwepo wa Mungu.
Mara nyingi tunapopata ujumbe wa Mungu unaotuita tutoke katika maisha fulani yasiyompendeza yeye au pale ambapo tunapoadhibiwa na Mungu, huwa tunadhani yeye ametuacha. Lakini kama tulivyojifunza mwanzo kwamba, Mungu analeta ujumbe wa kutuita kwenye maisha yaliyobebwa na kusudi lake au Mungu anatuadhibu kama tunaenda kinyume na mapenzi yake, kwa sababu yuko pamoja na sisi na anataka kuendelea kuhusiana na sisi. Israeli pamoja na maisha yao ya uovu na ukengeufu, Mungu bado yuko pamoja nao. Pamoja na uadui wao juu ya injili hata sasa, Mungu bado hajawatupa watu wake, taifa la israeli (Warumi 11:25-32). Mungu pia hajaliacha kanisa pamoja na changamoto zake zote. Mungu anapoleta ujumbe wake wa kututoa kwenye maisha kinyume na mapenzi yake na pale anapotuadhibu kwa kuishi kinyume na mapenzi yake, ni ushahidi tosha kwamba yeye yuko pamoja nasi. Watu wa Yuda baada ya ujumbe walikubali kutii, lakini waliogopa pia, ndio maana Mungu aliamua kuwaambia kupitia nabii Hagai kwamba yeye yuko pamoja nao. Hata sisi tunapoonywa na Bwana basi tujue yeye yuko pamoja nasi. Tusiwe na mashaka na uwepo wa Mungu kwetu kwa sababu ya ujumbe wa maonyo kutoka kwa Bwana au kwa sababu ya adhabu kutoka kwake.
- Uwezesho wa kimungu katika utii.
Kilichosababisha watu wa Yuda wasijenge hekalu sio kwa sababu walikuwa hawathamini hekalu au hawajui umuhimu wake. Watu wa Yuda hawakujenga hekalu kwa sababu walipoanza walikutana na upinzani. Kutokana na upinzani wakaishi wakisubiri wakati ambao hakutakuwa na upinzani. Hii ndio maana walikuwa wanasema huu sio wakati sahihi wa kujenga hekalu. Baada ya kusikia ujumbe wa Mungu kupitia nabii wake, wakageuza mtazamo wao na wakatii neno la Bwana. Baada ya kugeuza mtazamo wao, Mungu akawaamsha roho zao ili waingie katika ujenzi wa hekalu. Mungu yuko tayari kutusaidia katika kutekeleza kile anachotuita kukitekeleza. Tunapokubali tu maonyo yake, yeye huuisha nia/roho zetu ili tuingie katika utendaji wa kile anachotuitia. Mungu anapotuita kwenye kubadilika hatuachi mbali na kutuangalia tutafanya nini, bali huwa pamoja nasi kutusaidia kufanya yale anayotaka tufanye. Kwa kuwa yeye ni Baba mwema, unapotuonya anatarajia tugeuke na tunapogeuka hutusaidia kuchukua hatua. Unapopata maonyo yoyote kutoka kwa Bwana wala usidhani Mungu amekuacha anakusubiri mbele, Mungu yuko pamoja nawe, anataka ubadilishe mtazamo na yeye yuko tayari kukusiaida kutekeleza kila anachotaka wewe ufanye. Hii ndio maana Petro anasema hatujapungukiwa kitu chochote cha kutuwezesha kuishi maisha yenye tabia ya Uungu (2 Petro 1:3-4).
HAGAI 2:1-9
MAANDIKO
1 Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema,
2 Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hayo mabaki ya watu, ukisema,
3 Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu?
4 Lakini sasa uwe hodari, Ee Zerubabeli, asema Bwana; nawe uwe hodari, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni hodari, enyi watu wote wa nchi hii, asema Bwana; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema Bwana wa majeshi;
5 kama neno lile nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope.
6 Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu;
7 nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema Bwana wa majeshi.
8 Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi.
9 Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema Bwana wa majeshi.
UFAFANUZI.
Baada ya hotuba ya kwanza yenye maonyo ambayo ilileta mwitikio mzuri, Mungu anampa nabii Hagai tena ujumbe kwa ajili ya viongozi wale wale wawili na watu wote pia. Hii ilikuwa mwaka ule ule wa pili wa mfalme Dario,mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja, yaani siku ishirini na sita au na saba baada ya hekalu kuanza kujengwa (2:1-2). Ujumbe wa Mungu ulianza na maswali matatu kwa watu wake. Swali la kwanza, miongoni mwao ni nani aliyeliona hekalu la kwanza katika utukufu wake? Swali la Pili, Je, wanaonaje hekalu wanalojenga sasa? Na swali la Tatu, Je hekalu la sasa wanaliona sio kitu, wakilinganisha na lile la kwanza? Katika watu waliorudi kutoka utumwani walikuwapo wachache walioliona Hekalu la kwanza lilivyojengwa na Suleimani na jinsi lilivyokuwa na utukufu. Pamoja na kwamba utukufu una maana ya uwepo wa Mungu, ambao ni kweli ulikuwepo kwenye Hekalu la kwanza (1 Wafalme 8:10-11), lakini utukufu hapa una msisitizo kwenye muonekano wa Hekalu, yaani hekalu lilikuwa limejengwa kwa fahari ya vito vya thamani. Hivyo, wale walioliona hekalu la kwanza lililojengwa na Suleimani, hekalu la sasa walilokuwa wanalijengwa waliliona si kitu (Ezra 3:8-13). Hii ni kwa sababu lilikuwa linajengwa kipindi ambacho watu wametoka utumwani hivyo hawana malighafi za thamani kwa kiwango kama kile cha wakati wa Suleimani (2:3). Kwa kuwa watu walikuwa wanaona hekalu wanalojenga sasa si kitu ukilinganisha na hekalu la awali, Bwana anawasisitiza kwamba wawe hodari. Ujumbe huu wa kuwa hodari haukutolewa kwa ujumla, bali kila mmoja anaambiwa awe hodari. Zerubabeli anaambiwa awe hodari, Joshua anaambiwa awe hodari na watu wote pia wanaambiwa wawe hodari. Uhodari huu ni wa kuendelea kujenga hekalu la Mungu kwa kuwa yeye yupo pamoja nao (2:4). Maneno haya ya kutia moyo yanafanana na maneno yaliyotolewa na Daudi kwa Sulemani alipokuwa akijenga hekalu la kwanza (1 Mambo ya Nyakati 22:16, 18; 28:10, 20). Mungu anawahimiza kuwa hodari (kutokuogopa) kwa kuwa yeye yuko pamoja nao (Roho yake inakaa kati yao). Hii ni kwa sababu, toka siku ya ukombozi wao kutoka misri yeye alikuwa pamoja nao, kiasi kwamba walishinda kwa utukufu juu ya maadui zao (2:5).
Mungu katika kuendelea kuwatia moyo katika ujenzi wa Hekalu anawaahidi kwamba atatikisa uumbaji wake ili mataifa yote walete vito hivyo vya thamani kwa ajili ya kupendezesha hekalu lake (2:6-7). Mfano wa vito hivyo ni fedha (madini sio pesa) na dhahabu, kwa kuwa hivi vyote ni mali yake (2:8).Kwa kuwa vito hivi vya thamani vilifanya hekalu la Suleimani kwa na fahari kubwa, hivyo Bwana kwa kuvileta katika hekalu la sasa, Hekalu hili litakuwa na utukufu kuliko lile la kwanza. Zaidi ya kuwa na Hekalu lenye vito vya thamani kuliko lile la mwanzo, Bwana pia anawaahidi atafanya amani katika Jerusalem baada ya ujenzi wa hekalu hili kukamilika (2:9). Unabii huu wa mataifa kuleta fedha na dhahabu ulitimia wakati wa utawala wa mfalme Artashasta, wakati kundi lingine la watu wa Yuda walipoamua kurudi nyumbani wakiongozwa na Ezra (Ezra 7:8-28).
TUNAJIFUNZA NINI LEO?
- Historia isiwe kikwazo katika kufanya kazi ya ujenzi wa kanisa.
Kwa miaka mingi tumekuwa tukisikia kwamba kanisa la sasa halina nguvu kabisa ukilinganisha na kanisa la “wazee wetu” na hivyo kupelekea vijana kuona hakuna tumaini katika kazi hii ya ujenzi wa kanisa. Ujumbe wa Hagai ni kwetu kanisa la sasa kwamba, hata kama tunaona kwa macho kwamba kanisa la sasa halina nguvu ya Mungu kama la “wazee wetu”, Mungu yuko pamoja nasi na anatutia moyo kufanya kwa bidii kazi hii ya ujenzi wa watu wake. Wakati wa kuweka msingi wa hekalu hili la pili (Ezra 3:8-13) kulikuwa na mchanganyiko wa kilio na furaha. Wazee walikuwa wanalia kwa kuwa waliona hekalu hili si kitu, ukilinganisha na hekalu la kwanza. Vijana walifurahi kwa kuwa waliona tumaini kubwa baada ya utumwa wa muda mrefu. Jambo hili la wazee kulia pamoja na upinzani wa nje, lilisababisha kazi ya ujenzi wa hekalu kusimama kwa miaka zaidi ya kumi na nne. Hivyo vijana tusikubali historia iturudishe nyuma katika ujenzi wa kanisa. Mungu kwa kujua hilo ndio maana alimtuma Hagai tena kuwatia moyo watu wa Yuda mara baada tu ya kuamua kujenga hekalu ili wasije wakaicha kazi hii njiani. Mungu pia, unakutia moyo wewe unayeona kama kanisa la sasa halina nguvu kama lile ulilowahi kuliona katika historia. Anakutia moyo kwa kukutaka kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa utukufu wa kanisa utaongezeka na sio kupungua.
Wakati mwingine shetani anawazuia watu kufanya kazi ya Mungu ya ujenzi wa kanisa kwa sababu anawaonyesha kwamba wanachokifanya sasa ni kidogo ukilinganisha na walichokuwa wanakifanya hapo nyuma. Basi ujumbe wa Hagai kwako ni kwamba, usiruhu tathmini ya historia kukurudisha nyuma katika kufanya bidii ya ujenzi wa watu wa Mungu.Tathimini ya historia ukipe juhudi ya kuongeza bidii ya kujenga maisha ya waamini na sio kukurudisha nyuma.
- Mungu yupo pamoja nasi kwa sababu ya Agano lake na sisi.
Mungu anawaambia watu wa Yuda wasiogope waendelee kujenga hekalu, kwa sababu yeye yuko pamoja nao. Mungu yuko pamoja nao kwa sababu alifanya Agano na taifa hilo siku alipowatoa utumwani Misri. Hawezi kuwatupa wala kuwaacha kwa sababu ya Agano lake. Mungu pia anatutia moyo sisi leo kwamba yuko na sisi kwa sababu ya Agano lake alilolifanya pale msalabani. Hivyo popote tunapoamua kumtumikia tusiwe na wasi wasi wala tusiogope kwa kuwa yeye yuko pamoja na sisi. Hayuko pamoja na sisi kwa sababu tunamtumikia, bali yuko pamoja na sisi kwa sababu ya Agano alilolifanya pamoja nasi kupitia kifo cha mwanae Yesu kristo.
- Uumbaji wote ni mali ya Bwana hivyo Mungu ataviamulisha vitu vyote viende katika kazi yake ili vitimize kusudi lake.
Mara nyingi tukiongelea kumtumikia Mungu, swala la rasilimali limekuwa likijitokeza kwa watu wengi. Waamini wengi wamekuwa wanawaza kwamba ladba watafute kwanza pesa alafu baadaye ndio waingie katika kumtumia Mungu. Pamoja na kwamba haya mawazo yanachangiwa na kuwa na ufahamu usio sahihi kuhusu kumtumikia Mungu, lakini pia ukweli ni kwamba Mungu ataviamulisha vitu vyote vifuatane na watu wanaomtumikia ili kusudi lake yeye lipate kutimia. Mungu hawezi kuzuiwa kuwaokoa watu kutoka gizani eti kwa sababu ya kukosekani kwa rasilimali fulani ya kuwezesha injili kuhubiriwa. Mungu hawezi kuzuiwa kukuza maisha ya waamini kwa sababu rasilimali pesa imekosekana. Hilo jambo halipo na halitakuwepo. Kwenye kusudi lolote, na kwenye kazi yeyote inayoleta utukufu kwa Mungu, Mungu huwa anaamrisha kila kitu kiendane na kazi hiyo ili kusudi lake yeye litimie. Changamoto ni kuyahusianisha makusudi yetu na makusudi yake. Tukiyaacha makusudi yake kuwa makusudi yake, basi ataziamrisha rasilimali zote zituate makusudi yake. Na kwa sababu makusudi ni yake basi tutaacha afanye kwa muda wake, kwa viwango vyake na kwa namna yake.
Mawazo yangu na yako yanatakiwa yatawaliwe na nini ninatakiwa kufanya ili maisha ya waamini yawe bora na sio nipate wape rasilimali ili nimtumikie Mungu. Kwa miaka ya nyuma nilikuwa namuomba Mungu anisaidie niwe tajiri mkubwa ili kupitia utajiri huo Mungu atukuzwe. Lakini ukweli ni kwamba hizo pesa, nilikuwa nazitamini tu kama watu wengine. Sasa najua kwa hakika, ukidhamiria kufanya kazi ya Mungu, Mungu ataachia kila rasilimali kufanikisha kazi hiyo ili kanisa lijengwe. Watu wa Yuda hawakuingia hata kuomba fedha na dhahabu kwa Mungu wao, waliingia kufanya kazi ya ujenzi, Mungu mwenyewe ndio akasema nitaziamuru mbingu na nchi, bahari na mataifa yote ili walete fedha na dhahabu ili kufanya hekalu lake kuwa bora zaidi. Vivyo hivyo, tukiingia kufanya kazi yake Baba kwa moyo wa kutaka kuboresha maisha ya waamini Mungu atatupa rasilimali zinazoenda na kazi hiyo. Changamoto ni pale tunapotaka rasilimali hizo ili tuzitumie kwa tamaa zetu wenyewe. Katika biashara hio Mungu kweli hayupo. Kwa kuwa Mungu hayupo katika biashara ya namna hio, imepelekea watu wengine kumwasi Mungu ili wapate rasilimali ambazo baadae wanasema watazitumia katika “kumtumikia Mungu”. Ukifika kwenye kiwango cha kutokutii maagizo ya Baba kwa sababu unataja rasilimali, basi ujue lengo lako sio kuboresha maisha ya waamini wala kuwaleta watu katika imani . Na kama lengo la “Utumishi” wako sio kuboresha maisha ya waaminiau kuwaleta watu katika imani, basi unachokifanya sio utumishi na hivyo sio kusudi la Baba.
- Tuna tumaini la Hekalu lenye utukufu zaidi.
Ujumbe wa manabii pamoja na kwamba ulikuwa ni ujumbe unahusu matukio ya wakati wa taifa la Israeli, ulikuwa pia ni ujumbe unaotabiri mambo yatakayotokea siku za mwisho. Hivyo, Hagai pia anapotabiri ubora wa hekalu la pili ukilinganisha na lile la kwanza, anatabiri pia maskani ya Mungu itakayokuwa bora zaidi katika ulimwengu ujao. Kama tulivyojifunza toka mwanzo kwamba kwa sasa hekalu la Mungu ni kanisa, na kanisa ndio maskani ya Mungu, hivyo Mungu anaishi ndani ya waamii na katikati yao. Lakini kanisa bado liko kwenye ulimwengu unaotawaliwa na dhambi na madhara yake, hivyo bado kuna udhihirisho wa kimungu unapungua kwa sasa. Lakini tunatarajia katika ulimwengu ujao tutakuwa pamoja na Mungu kwa udhihirisho kamili bila ya kuwa na upinzani wowote kutoka kwa adui, kwa kuwa adui atakuwa amehukumiwa tayari. Huu ndio wakati Yohana alipata nafasi ya kuuchungulia na akashangaa kwamba kwenye huo mji hakukuwa na hekalu tena alilolijua, hii ni kwa sababu Mungu mwenyewe katika udhihirisho wake kamili atakuwa na watu wake (Ufunuo 21:22-27). Kwa kujua hili ndio maana Yohana pia aliliambia kanisa kwamba ni kweli sisi ni maskani ya Mungu kwa sasa, lakini bado kuna utukufu mkubwa ujao ambao haujadhihirishwa bado na utadhihirika akirudi Bwana wetu Yesu kristo mara ya pili (1 Yohana 3:1-3). Tuna tumaini la hekalu bora zaidi katika ulimwengu ujao.
HAGAI 2:10-19
MAANDIKO
10 Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa kenda, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema,
11 Bwana wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani katika habari ya sheria, mkisema,
12 Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye akagusa kwa upindo wake mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula cho chote, je! Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La.
13 Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je! Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi.
14 Ndipo Hagai akajibu, akasema, Hivyo ndivyo walivyo watu hawa, na hivyo ndivyo lilivyo taifa hili mbele zangu, asema Bwana; na hivyo ndivyo ilivyo kila kazi ya mikono yao; na kitu hicho wakitoacho sadaka huko ni najisi.
15 Na sasa nawaomba, tafakarini; tangu siku hii na siku zilizopita; kabla halijatiwa bado jiwe juu ya jiwe katika nyumba ya Bwana;
16 katika wakati huo wote, mtu alipofikia chungu ya vipimo ishirini, palikuwa na vipimo kumi tu; na mtu alipofikia shinikizo apate kuteka divai ya vyombo hamsini, palikuwa na divai ya vyombo ishirini tu.
17 Naliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunielekea mimi, asema Bwana.
18 Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kenda, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la Bwana tafakarini haya.
19 Je! Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki.
UFAFANUZI
Hotuba ya tatu ya nabii Hagai ilikuja miezi matatu tangu watu walipoanza kujenga hekalu. Hii ilikuwa ni siku ya ishirini na nne mwezi wa tisa, mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario (2:10). Ujumbe wa hotuba hii unaanza na maswali kwa makuhani. Makuhani wanaulizwa maswali kwa kuwa wao ndio walikuwa wanajua vizuri kuhusu mambo ya utakatifu na unajisi (Walawi 10:8-11) kama ilivyo katika torati ya Musa (2:11). Swali la upande wa kwanza linauliza kwamba, nyama takatifu ikigusa chakula kingine, Je, hicho chakula kilichoguswa kitakuwa kitakatifu? Makuhani kwa kuwa wanajua vizuri mambo haya wakajibu kwamba jibu ni hapana. Kitu hakiwezi kuwa kitakatifu kwa kuwa kimeguswa na kitu kitakatifu (2:12). Swali la upande wa pili ni kwamba, mtu najisi akigusa chakula, Je, chakula hicho kitakuwa najisi? Jibu la makuhani ni ndio. Kitu chochote kikiguswa na kitu najisi basi kitu hicho kitafanyika kuwa najisi (2:13).[1] Kwa lugha nyepesi maswali haya mawili yanaelezea ukweli kwamba utakatifu hausambai kwa kugusa bali unajisi unasambaa kwa kugusa. Hii ni kweli hata katika hali ya kawaida, mtu anaweza kupata magonjwa kwa kumgusa mgojwa lakini mgojwa hawezi kupona ugonjwa kwa kumgusa mtu mzima. Kwa kanuni hiyo (hasa ya swali la pili) Mungu anasema watu wa Yuda kwa sababu ya uovu wao (Unajisi) kila walichokuwa wanakishika kilikuwa najisi, yaani kazi za mikono yao zilikuwa najisi na hata vile walivyovitoa vilikuwa najisi (2:14).
Baada ya kuwafundisha ukweli huo Mungu anawataka watu wa Yuda watafakari jinsi ilivyokuwa kabla hawajaanza kujenga tena hekalu lake (2:15). Wakati huo mtu alipoenda kwenye fungu la mazao/nafaka akiwa anatarajia kupata vipimo ishirini alipata kumi tu. Kwa upande mwingine mtu alipoenda kwenye mashine ya kutengenezea divai alitarajia kupata vyombo hamsini, lakini mwisho wa siku alipata vyombo ishirini (2:16). Yote haya yanaonyesha jinsi walivyopata laana katika kilimo kama alivyoleza katika hotuba yake ya kwanza (1:6-9). Pia Mungu anawatafakarisha jinsi alivyoleta hali ya hewa iliyoharibu kazi zao za mikono (hasa kazi za kilimo), lakini hawakuelewa mpaka alipomtuma nabii Hagai (2:17). Baada ya kuwatafakarisha kwa kurudi nyuma, sasa Mungu anawatafakarisha kwa kuangalia mbele, yaani tangu walipoanza kujenga hekalu mpaka siku ya hotuba hii ya tatu (2:18). Ni ukweli kwamba pamoja na kupanda mbegu zao (ndio maana hakuna mbegu ghalani) lakini hawajapata mazao ya matunda mpaka sasa. Lakini kwa kuwa walikubali kurudi kujenga hekalu lake Mungu hivyo Bwana atawabariki na watapata utoshelevu (2:19).
TUNAJIFUNZA NINI LEO?
- Utii ni bora kuliko dhabihu
Bwana anawaambia watu wa Yuda kwamba kwa sababu ya kutokujenga kwao hekalu kuliwafanya kila wanachofanya kuwa ni najisi, pamoja na utoaji wao ulikuwa najisi pia. Mara nyingi tunadhani Mungu anataka vitu vyetu kama vile fedha au mali, lakini ujumbe wa Hagai ni kwamba, Mungu anataka tumtii yeye kwanza ndio tutoe vitu tulivyonavyo kwake. Utii katika muktadha huu ni mwitikio chanya katika kujenga hekalu lake. Mungu anatuita kupitia nabii Hagai kufanya kazi ya kujenga hekalu lake kwanza alafu ndio mengine yanafuata. Kwa wakati tulionao waamini wengi wanapenda kwenda tu kwenye kusanyiko kusikiliza na kuona kinachoendelea au wengine wanasema wanaenda kwenye makusanyiko kukutana na Mungu lakini hawataki kabisa kushiriki katika kujenga maisha ya waamini wengine. Kwa kufanya hivyo wanaacha jambo la msingi Mungu analolitaka na kugeukia mambo mengine. Baba kupitia ujumbe wa Hagai anatuambia kama hatutaki kufanya juhudi katika kushiriki ujenzi wa maisha ya waamini, kuhudhuria kwetu kwenye makusanyiko hakuna maana. Kwa lugha ngumu zaidi, mahudhurio yetu ni unajisi mbele zake. Mwamini anatakiwa kufanya bidii ya kila namna kuhakiksha anachangia kwenye kuboresha maisha ya waamini wengine. Na hili likifanyika Baba ndio anafurahishwa.
Footnotes:
[1] Kinyume na kanuni hii Yesu kwa utakatifu wake aliweza kutakasa watu kwa kuwagusa (Marko 1:40-42)
HAGAI 2:20-23
MAANDIKO.
20 Kisha neno la Bwana likamjia Hagai mara ya pili, siku ya ishirini na nne ya mwezi, kusema,
21 Sema na Zerubabeli, liwali wa Yuda, ukisema, Nitazitikisa mbingu na dunia;
22 nami nitakipindua kiti cha enzi cha falme, nami nitaziharibu nguvu za falme za mataifa; nami nitayapindua magari, na hao wapandao ndani yake; farasi na hao wawapandao wataanguka chini; kila mtu kwa upanga wa ndugu yake.
23 Katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, nitakutwaa wewe, Ee Zerubabeli, mtumishi wangu, mwana wa Shealtieli, asema Bwana, nami nitakufanya kuwa kama pete yenye muhuri; kwa kuwa nimekuchagua, asema Bwana wa majeshi.
UFAFANUZI.
Hotuba ya nne na ya mwisho ya nabii Hagai ilikuja siku ile ile ambayo Mungu alimpa kutoa hotuba ya tatu, yaani siku ya ishirini na nne, mwezi wa tisa, mwaka wa pili wa kutawala kwake Dario (2:20). Ujumbe huu sasa ni maalumu kwa Zerubabeli liwali peke yake. Katika Hotuba hii kwa Zerubabeli Mungu anaahidi kutikisa Uumbaji wake. Ni kwa mara ya pili sasa Mungu anaahidi kutikisa uumbaji wake (2:21). Kwa mara ya kwanza Mungu aliahidi kutikisa uumbaji wake ili mataifa yalete mali na vito vya thamani katika nyumba yake, lakini sasa Mungu atatikisa uumbaji wake ili kupindua falme za mataifa. Mungu atapindua falme za mataifa kupitia vita ambayo mataifa watapigana wao wenyewe (2:22). Na katika siku hiyo, Bwana anaahidi atamfanya Zerubabeli, liwali wa Yuda kutoka katika ukoo wa Daudi (mwana wa Shealtieli) kuwa mfalme mwenye mamlaka (pete yenye muhuri)[1] kwa kuwa amemchagua yeye (2:23). Kwa kuwa wakati huu Israeli wako chini ya utawala wa Dola ya Uajemi na Zerubabeli ni kiongozi wa kisiasa aliyewekwa na mfalme wa Uajemi, hivyo hana mamlaka zaidi ya kumwakilisha mfalme mwingine. Mungu anamuahidi Zerubabeli kwamba jambo hilo litaisha na Zerubabeli atakuwa mtawala mwenye mamlaka.
TUNAJIFUNZA NINI LEO?
- Bwana Mungu Mwenyezi atashinda katika mpango wake wa milele.
Watu wa Yuda katika wakati huu wa utawala wa Dola ya Uajemi walikuwa na uhuru wa kurudi nyumbani na kufanya mambo kadhaa kama kurejesha ibada zao na maisha yao ya kawaida, lakini bado walikuwa chini ya utawala wa dola nyingine. Hivyo, pamoja na kuendelea na ujenzi wa hekalu, mioyo yao ilikuwa inatamani na kukumbuka ahadi ya Mungu ya kulifanya taifa la Israeli kuwa taifa kubwa duniani huku likijitawala lenyewe chini ya mtawala kutoka katika ukoo wa Daudi. Matarajio haya yote yalikuwa ni ndoto kwao kwa maana uhalisi ulikuwa tofauti. Israeli iliendelea kuwa chini ya utawala wa dola mbalimbali.
Hata baada ya kuja Yesu duniani, yaani baada ya maisha yake, kifo chake, na kufufuka kwake, bado Israeli walikuwa na shauku ya utawala. Hii ndiyo maana wanafunzi wake walipoona kwamba Yesu ameshinda mpaka mauti, wakajua wakati wa Israeli kupata ufalme wake umefika. Jibu la Yesu kwenye swali lao lilikuwa, wayaache mambo ya ufalme kwa Baba na waingie kwenye kazi ya ujenzi wa kanisa (Matendo 1:6-8).
Hata sisi waamini leo tunatamani kuona wema ukishinda katika dunia ya sasa, lakini ukweli ni kwamba kwa sasa Mungu ameruhusu ubaya kuushinda wema. Lakini uko wakati Baba aliouweka ambapo yeye mwenyewe atapindua ulimwengu na kumuweka mfalme kutoka katika ukoo wa Daudi ambaye atatawala kwa mamlaka na haki. Mfalme huyu ni Yesu wa Nazareti katika ujio wake wa mara ya pili.
Kwa waamini, maisha ya sasa kuna wakati yanaonyesha kama vile Mungu hana nguvu, kwa kuwa unaweza kuonewa kwa haki na Mungu akawa kama hajaona. Unaweza kuomba kupata haki yako lakini ukakosa. Kuna wakati unaona kanisa linaonewa, na Mungu anakuwa kimya kiasi ambacho unaweza kudhani kwamba yuko mbali. Au kwa jinsi mambo yalivyo sasa, ufalme wa shetani unaonekana kuvutia na ufalme wa nuru unaonekana hauna nguvu. Hii ni kwa sababu mali na fedha ziko kwenye ufalme wa giza zaidi, watu wenye ushawishi mkubwa duniani hawamtaki Mungu, na mataifa yenye maamuzi makubwa yanamtukana Mungu na yeye anaonekana hana la kufanya.
Ujumbe wa Hagai tukiwa kwenye hali hizi ni kwamba, sisi kazi yetu iwe ni kujenga maisha ya waamini na kuwalhubiri walioko gizani; yeye Mungu atajitetea mwenyewe. Kuna wakati ameweka ambao atakipindua kiti cha enzi cha falme, naye ataziharibu nguvu za falme za mataifa; atapindua silaha zao na majeshi yao, na atamweka mtumishi wake Yesu Kristo kuwa mtawala mwenye mamlaka kwa kuwa amemchagua. Huo ndio wakati ambao tutaona haki ikishinda.
Mambo yote aliyoyasema Mungu kwa Zerubabeli amesisitiza atafanya yeye. Kwenye kila jambo alilotaja amesema atafanya yeye, lakini kwa upande mwingine ujenzi wa hekalu aliutaka ufanywe na watu wa Yuda na viongozi wao. Vivyo hivyo, Mungu ametupa wajibu wa kujengana sisi kwa sisi, na suala la utawala katika dunia ameliacha katika mikono yake yeye mwenyewe. Hii haina maana kwamba yeye hausiki katika ujenzi wa kanisa, la hasha, bali anasisitiza watu wake kuwajibika kwenye mambo ambayo Mungu ametushirikisha katika utendaji.
Footnotes:
[1] Pete yenye Muhuri ilikuwa ishara ya mamlaka kwa mfalme na ilitumika kuthibitisha hati za kifalme na matangazo ya kisheria (kwa mfano, Mwanzo 28:18; 1 Wafalme 21:8).