Ipi Ilikuwa Njozi ya Habakuki?

Kwa miaka kadhaa nilikuwa nimefundishwa kwamba, ukiwa na maono au ndoto za kile unachotaka kufanya au kuwa hapo mbeleni katika maisha haya basi andika na uwaambie watu ili ijulikane. Kwa sababu ya kuwa na imani kwamba kila tunachokifanya kinatakiwa kiwe na mstari wa kusimamia, waalimu walionifundisha hili walitumia maneno ya Mungu kutoka Habakuki 2:2-3. Katika mistari hii Biblia inasema “Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia” (Habakuki 2:2-3).

Pamoja na kwamba nimekuwa nikitumia maandiko haya kwa miaka mingi, sikuwahi kufundishwa kujua hasa njozi ya Habakuki ilikuwa ni ipi. Hata hivyo, leo natambua kuwa ni muhimu kufahamu njozi ya Habakuki ilikuwa ni ipi ili mtu uweze kutumia maandiko haya kwa usahihi. Hivyo basi, fuatana nami tangu mwanzo hadi mwisho ili tuweze kuelewa njozi ya Habakuki ilikuwa ipi, na baada ya hapo tutaona ni kwa namna gani sisi leo tunaweza kuyatumia maandiko haya matakatifu.

Katika mpangilio wake wa kiushairi maandiko haya yanasema hivi:

Bwana akanijibu, akasema,

Iandike njozi

     ukaifanye iwe wazi sana katika vibao,

     ili aisomaye apate kuisoma kama maji.

Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa,

inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo;

 ijapokawia, ingojee;

kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.

Katika sehemu ya kwanza ya maandiko haya, Bwana anamwagiza Habakuki kuandika njozi (maono) kwa kumwelekeza kwamba aiandike juu ya vibao ili iwe wazi. Lengo la kuandika juu ya vibao ni ili mtu asomaye aisome kwa haraka, kama vile maji yanavyotiririka kwa kasi katika mto. Katika sehemu ya pili, Mungu anasema kuwa njozi hii ni ya wakati ujao aliouamua Yeye mwenyewe, na hakika itatimia. Mwishoni, anamsisitiza Habakuki kuwa mvumilivu katika kusubiri utimilifu wa ndoto hii.

Mpaka hapa ni hakika kwamba Mungu hajaweka wazi kwamba ndoto hii ni ipi. Kabla ya kuchambua na kujifunza ndoto hii, basi tuangalie muktadha wa maandiko haya. Mpaka Habakuki anaambiwa aandike maono, alikuwa amekwisha kulalamika mbele za Mungu mara mbili, na ndoto ambayo anaambiwa aindike ilikuwa ni majibu ya malalamiko yake, hasa malalamiko yake ya pili.

Kwa mara ya kwanza Habakuki anapeleka malalamiko yake kwa Mungu akisema, ni kwa muda gani Mungu atakaa kimya wakati ukiukwaji wa haki (udhalimu) unaendelea katika jamii ya Yuda? Habakuki anasema, Mungu, utakuwa kimya hata lini wakati watu wanyonge wanaonewa? wakati watu wana magomvi? wakati hukumu inapotoshwa? wakati sheria yako (yaani torati) inatupiliwa mbali? Na zaidi, wakati watu wabaya wanawazunguka wenye haki na kuwadhuru? (Habakuki 1:1-4).

Majibu ya Mungu kutokana na malalamiko haya ya Habakuki yalikuwa ni tangazo kwamba Yeye Mungu atawaleta Wakaldayo kwa ajili ya kuwahukumu watu wa Yuda. Wakaldayo, au taifa la Babeli, ni taifa lenye sifa mbalimbali za ukatili na uimara wa jeshi, hivyo Mungu anasema atawatumia wao kuwapiga Yuda ili kushughulika na udhalimu unaoendelea katika taifa hilo (Habakuki 2:5–11).

Baada ya majibu hayo ya Mungu, Habakuki akachanganyikiwa zaidi, na mwishowe akaanza kulalamika kwa mara ya pili. Habakuki anasema, kweli Mungu, Yeye ambaye ni wa milele na mtakatifu, amewachagua Wakaldayo kutekeleza hukumu na adhabu kwa watu wake wa Yuda? Mungu, Yeye ambaye hawezi kuangalia uovu, anaamua kutumia taifa ovu kuliko mengine kuwaadhibu watu wengine (wakiwemo Yuda)?

Kwa kutumia lugha ya picha ya uvuvi, Habakuki analalamika kwamba Mungu, kwa kuwatumia Wakaldayo, amewafanya wanadamu wengine kuwa kama samaki na Wakaldayo kuwa wavuvi. Kwa kutumia lugha hiyo hiyo ya picha, Habakuki anaelezea sifa za ukatili wa Wakaldayo: hukusanya mateka kutoka maeneo mengine na kuwaleta chini yao, na katika hao mateka hutoa kafara.

Mwisho, Habakuki anamwuliza Mungu, je, kuna siku Wakaldayo wataacha kuua watu kwa kuwatoa kafara? Yaani, kama Mungu amewatoa Yuda kuhukumiwa na Wakaldayo, watu wenye dhambi zaidi kuliko wao, je, ni nani atakayepona? (Habakuki 1:12–17).

Baada ya hapo, Habakuki akakaa kusubiri majibu ya Mungu, ndipo Mungu akamuagiza kuandika maono (njozi) na kuyaweka wazi ili kila mtu aweze kuyasoma kwa urahisi (Habakuki 2:1–4). Kinachofuata baada ya agizo la kuandika maono hayo katika kitabu hiki ni mambo mawili. Kwanza, ni maonyo (ole) juu ya matendo mabaya yaliyokuwa yakifanywa na Wakaldayo, pamoja na maelezo ya jinsi watakavyohukumiwa (Habakuki 2:4–20). Pili, ni maono ya ujio wa Bwana kwa ajili ya hukumu kwa waovu na wokovu kwa watu wake (Habakuki 3:3–19). Haya mambo mawili ndiyo yanahusisha maono Mungu aliyomuagiza Habakuki kuandika.

Pamoja na mgawanyiko wa wataalamu wa Biblia kuhusu yapi hasa yalikuwa maono aliyoyaandika Habakuki (wengine wakiona sehemu ya kwanza tu ndiyo jibu, na wengine sehemu ya pili), kwa ujumla ni kwamba maono ya Habakuki yalikuwa ni tangazo la hukumu ya Mungu juu ya watendao maovu (Wakaldayo wakiwa wa kwanza), hasa yanayohusisha ukiukaji wa haki.

Sehemu ya kwanza (Habakuki 2:4–20), inatoa matangazo ya “ole” kwa watu/taifa lifanyalo yafuatayo: kujilimbikizia mali kwa njia ya unyang’anyi, kujitajirisha kwa kuonea wengine huku wakijijenga ili kujihakikishia usalama wao, kujenga mji kwa njia ya mauaji au umwagaji damu, kuwalevya wenzao kwa ajili ya kuchukua mali zao, na mwisho kutengeneza sanamu, kuziomba na kuzungumza nazo. Haya yote Mungu anasema atayakomesha kwa hukumu yake. Mungu anasema udhalimu huu wote Yeye ataukomesha kwa kuwahukumu watendao hayo.

Sehemu ya pili (Habakuki 3:3–19), Habakuki anaona maono ya ujio wa Mungu Yeye mwenyewe kwa ajili ya hukumu. Katika maono haya, Habakuki anaona ujio wa Mungu kwa sura ya kutisha ya vita, na ujio wake huu haukuwa kwa ajili ya viumbe vingine kama milima na wanyama, bali ni kwa ajili ya watu/taifa ovu. Ujio huu ulikuwa ni ujio wa Mungu kwa ajili ya hukumu ya kutisha.

Kwa hiyo, maono ya Habakuki yalihusu hukumu ya Mungu inayokuja juu ya taifa (au mataifa) yanayokiuka haki. Haya hayakuwa maono binafsi ya Habakuki kuhusu maisha yake, mafanikio, au utukufu wake, bali yalikuwa ni ufunuo wa Mungu kuhusu adhabu yake kwa udhalimu unaoendelea. Kwa maneno mengine, maono ya Habakuki yalikuwa ni tangazo la Mungu juu ya hukumu yake kwa ukiukaji wa haki,na wala hayakuwa maono ya mafanikio ya kibinafsi.

MAREJEO

Kumbuka, Habakuki alianza kwa kulalamikia ukimya wa Mungu katikati ya maovu na ukiukwaji mkubwa wa haki katika Yuda. Mungu akamjibu kwamba atatumia taifa la Babeli (wakaldayo) kukomesha maovu hayo. Habakuki akamlalamikia tena Mungu kwa kutangaza kwamba atatumia taifa lenye dhambi kuliko Yuda katika kuwarekebisha Yuda katika dhambi zao. Ili kumuonyesha Habakuki kwamba, kuwatumia Babeli hakumaanishi kukubaliana na maisha yao, Mungu anampa Habakuki onyo tano zinazoelekea taifa la Babeli, onyo hizo zikiwa na maelezo ya namna gani Mungu atawahukumu Babeli kwa udhalimu wao. Mbali na hivyo, Mungu akampa Habakuki maono ya kumuonyesha jinsi ambavyo, mwishoni, Yeye mwenyewe atashuka kuangamiza mataifa maovu na, upande mwingine, kuwaokoa watu wake. Hivyo, Yuda, wakiukaji wa haki, wataadhibiwa na Mungu kupitia Babeli na Babeli wakiukaji wa haki watahukumiwa na Mungu, lakini wenye haki wataishi kwa imani na mwishoe wataokolewa na Mungu mwenyewe.

Baada ya Habakuki kupata maono haya, akajawa na hofu kuu, mpaka mwili wake wote ukatetemeka. Wakati huo hakumjibu tena Mungu, bali alikubali kusubiri udhihirisho wa mambo aliyoyaona. Mwishoni, anamalizia kwa kusema kwamba, hata kama hali za nje zinaonyesha kana kwamba Mungu yuko kimya (kwa mfano, mashamba hayatoi chakula), yeye bado atamshangilia Bwana, kwa kuwa Yeye ndiye Mwokozi wake na nguvu zake.

Ni kweli kwamba Yuda ilipata hukumu yake kwa kupigwa na Babeli, mwaka wa 586 KK na Babeli ilihukumiwa kwa kupigwa na Wamedi na Waajemi mwaka 539 K.K, hivyo maono ya Habakuki yalitimia kama Mungu alivyoahidi.

HITIMISHO

Maono ya Habakuki ni ufunuo wa Kimungu unaoonyesha hukumu yake ya haki juu ya uovu, hasa unaohusisha udhalimu katika jamii na kutetewa kwa watu wake, yaliyoandikwa ili kuhakikishia vizazi vyote kwamba haki ya Mungu, ijapochelewa, hakika itatimia. Popote palipo na ukiukwaji wa haki, Mungu hayupo kimya; Mungu atatoa hukumu kwa wakati wake. Kwa kusema hivyo, maono ya Habakuki hayatakiwi kutumika kuhamasisha ubinafsi, kwa kuwa maono yake hayakuwa ya kumfaidisha yeye binafsi.

Ukipenda kusoma kitabu cha Habakuki kwa kina, tumia mwongozo huu kufanya hivyo.