Kwa muda wa miaka kadhaa ambayo nimekuwa sehemu ya makanisa yenye mwelekeo wa Kipentekoste, sikuwahi kukutana na swali hili, wala kujiuliza, kwa kuwa majibu yake kwangu yalikuwa mepesi tu: “Maria si Mama wa Mungu.” Kumwita Maria Mama wa Mungu ni kufuru kubwa, kwa kuwa Mungu hana mwanzo wala mwisho, hivyo hawezi kuzaliwa. Majibu haya yanaweza kuwa majibu ya baadhi ya Waprotestanti, hasa wale ambao, kwa sababu mbalimbali, hawajapata nafasi ya kujifunza historia ya Kanisa. Kwa ndugu zetu wa Kanisa Katoliki la Roma na waorthodoksi, hili ni swali lenye majibu mepesi kabisa kwamba: “Maria ni Mama wa Mungu.”
Katika karne ya tano, Kanisa lilikumbwa na mashindano ya kitheolojia. Nestori, Askofu Mkuu wa mji wa Konstantinopoli, aliweka tahadhari kubwa katika kumwita Maria “Theotokos,” yaani “Mama wa Mungu” au “Yule anayemzaa Mungu.” Kinyume chake, Nestori alipendekeza Maria aitwe “Christotokos,” yaani “Mama wa Kristo.” Kwa kusema hivyo, Nestori alimaanisha kuwa Maria alizaa tu asili ya kibinadamu ya Yesu, na si Yesu katika munganiko wake kamili wa Uungu na Ubinadamu.
Kinyume na Askofu Mkuu Nestori, Askofu Cyril wa Iskanderia na mkutano wa Kanisa uliofanyika Efeso (Mtaguso wa Efeso, 431 BK) walitangaza kuwa Maria anastahili kuitwa “Theotokos,” yaani “Mama wa Mungu” au “Yule anayemzaa Mungu” kwa kuwa mtoto aliyemzaa na kumbeba tumboni si mwingine bali ni Mwana wa milele wa Mungu, aliyefanyika mwili. Kwa maneno ya ufafanuzi, Mtaguso wa Efeso ulikubali kuwa Maria alimzaa Yesu akiwa na Uungu na Ubinadamu kamili. Hivyo basi, Maria alimzaa mtu mmoja—Yesu Kristo—ambaye ni Mungu kamili na mwanadamu kamili.
UFAFANUZI
Kwa kuwa jina hili limetumiwa vibaya na watu wengi katika historia ya Kanisa, ni vizuri kufafanua mambo yafuatayo;
a. Tunamaanisha nini tunaposema “Mama wa Mungu”?
b. Je, jina hili ni sahihi katika theolojia ya Kibiblia?
c. Je, jina hili linafaa kwa Waamini kulitumia?
a. Tunamaanisha nini tunaposema “Mama wa Mungu” ?
Jina “Mama wa Mungu” halimaanishi Maria ni chanzo cha uungu, bali linaonyesha umoja wa nafsi ya Kristo. Maria hakumuumba Mungu au kusababisha kutokea kwa Mungu—Mungu ni wa milele. Lakini alimzaa Yesu Kristo, ambaye Biblia inamtaja kuwa ni “Emmanueli,” yaani “Mungu pamoja nasi” (Mathayo 1:23), na pia yeye ndiye “Neno aliyefanyika mwili” (Yohana 1:14), ambaye neno huyu “alikuwa Mungu,” (Yohana 1:1).
Hivyo basi, kusema Maria ni Mama wa Mungu ni kukiri kwamba Yesu aliyemzaa ni Mungu katika mwili. Yesu alipokuwa tumboni mwa Maria na alipozaliwa alikuwa ni nafsi moja yenye ukamilifu wa Uungu na Ubinadamu. Hii ni kusema hakuna wakati ambapo Yesu alikuwa mwanadamu bila Uungu.
b. Je, jina hili ni sahihi katika theolojia ya Kibiblia?
Ni ukweli kwamba jina “Mama wa Mungu” halipo katika maandiko kabisa. Jina la karibu kabisa ambalo Maria anapewa katika maandiko ni “mama wa Bwana wangu” (Luka 1:43), ambapo Bwana huyo ni Yesu Kristo, ambaye anaitwa na Tomaso: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yohana 20:28). Ambaye pia Paulo anamwita “Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu” (Tito 2:13).
Kwa hiyo, kukana kwamba Maria ni Mama wa Mungu si kumshusha cheo Maria, bali ni kukana kwamba Yesu Kristo ni Mungu — au ni kusema kwamba kuna wakati ambapo Yesu Kristo hakuwa Mungu.
Kwa hiyo, jina hili lina kazi ya kutunza Uungu wa Kristo, na si njia ya kumpa Maria heshima asiyostahili.
c. Je, jina hili linafaa kwa Waamini kulitumia?
Kuitwa kwa Maria “Mama wa Mungu” kumesababisha, na kumeendelea kusababisha, majina mengine mengi kuzaliwa. Kwa mfano, Maria huitwa “Malkia wa Mbinguni,” “Mkombozi mwenza/Mshiriki wa Ukombozi” (Co-Redemptrix), “Mpatanishi wa Neema” (Mediatrix), au “Mtetezi.” Kutokana na majina hayo na mengine mengi, Maria amekuwa na nafasi kubwa sana katika maisha ya imani ya watu wengi.
Kwa sababu ya kumtukuza Maria—tena kumweka katika hadhi ya karibu au sawa na Kristo Yesu, hasa katika kazi yake ya Ukombozi—ambayo ni kinyume kabisa na maandiko yanayoeleza upekee wa Yesu kwa kila namna, Waprotestanti wengine wameangukia katika kukana kabisa jina la Maria kama “Mama wa Mungu.”
Hata hivyo, matumizi mabaya hayapasi kutufikisha kwenye kuukataa ukweli. Kama tulivyoona hapo juu, kuitwa kwa Maria “Mama wa Mungu” haina maana ya kumtukuza Maria, bali kuna maana ya kukubaliana na Uungu wa Kristo Yesu Bwana wetu. Hivyo basi, waamini wanaweza kulitumia jina hili kwa ajili ya kumtukuza Kristo Bwana wao, na siyo Maria.
Pamoja na kusema hayo yote waamini wengine wanaweza kusema: “Je, jina hili halifungui mlango wa kumwabudu au kumtukuza Maria?” Jibu ni hapana—iwapo litafasiriwa vyema kama tulivyoeleza hapo juu. Kumwita Maria “Mama wa Mungu” sio kumfanya yeye kuwa mwanzo wa maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo au ya Mungu katika utatu wake. Kumwita Maria “Mama wa Mungu” haina maana ya kumtukuza kwenye kiwango cha kumpa heshima asiyostahili bali ni kumpa Kristo Yesu sifa anayostahili.
Tunapaswa kumheshimu Maria kwa nafasi yake ya kipekee katika historia ya wokovu (Luka 1:48), lakini hatupaswi kumuabudu, kumwomba wala kumfanya mwombezi au mpatanishi. Ibada ni kwa Mungu tu na maombi ni kwa Mungu tu kwa njia ya Yesu Kristo pekee.
HITIMISHO
Kwa hiyo, ni sawa kabisa kumwita Maria “Mama wa Mungu,” kwa kuwa kwa kufanya hivyo tunakubali kwamba Bwana Yesu Kristo alikuwa Mungu katika mwili alipokuwa tumboni mwa Maria, alikuwa Mungu katika mwili alipozaliwa, na alibaki kuwa hivyo hivyo katika maisha yake yote.