Katika Agano Jipya kuna maandiko mawili yanayofundisha kuhusu kujipamba kwa wanawake. Moja ni kutoka kwa Mtume Petro na la pili ni kutoka kwa Mtume Paulo. Mtume Paulo anasema: “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri pamoja na adabu nzuri na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele wala kwa dhahabu na lulu wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.” 1 Timotheo 2:9-10 (SUV).
Maagizo haya ni sehemu ya maagizo ya Mtume Paulo kwa Timotheo kuhusu namna gani makanisa yanapokutana katika maombi yanatakiwa kuenenda. Mtume alianza kutoa maelekezo kwa kanisa lote (2:1-7), akaenda kwa wanaume (2:8), na akamalizia na wanawake (2:9-15). Maelekezo kwa wanaume ni mafupi sana na yanalenga kukataza wanaume kuwa na hasira na magomvi ya hoja (mabishano/majadiliano ya kubishana) wakati wa maombi. Hili katazo lilikuwa la lazima kwa kuwa kanisa la Efeso lilikuwa na changamoto ya mashindano ya maneno (6:4-5).
Maelekezo kwa wanawake ni marefu ukilinganisha na maelekezo kwa wanaume. Kama ilivyokuwa kwa wanaume, maelekezo kwa wanawake yanaendana na matatizo yaliyokuwa katika kanisa la Efeso. Katika kanisa la Efeso kulikuwa na wanawake walioathiriwa na mafundisho ya waalimu wa uongo (2 Timotheo 3:5-6), wanawake wasioweza kujizuia/hawana kiasi (1 Timotheo 5:6), na wengine walikuwa wamemgeukia Shetani tayari (1 Timotheo 5:15). Kutokana na changamoto hizo, ndio maana maelekezo ya Mtume Paulo kwa wanawake ni marefu na yanahusiana na matatizo hayo. Sehemu ya kwanza ya maelekezo kwa wanawake (2:9-10) ndipo tunapata mafundisho ya Mtume Paulo kuhusu kujipamba.
Mtume Paulo anasema wanawake wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri kwa adabu na kwa kiasi. Wasijipambe kwa kusuka nywele kwa dhahabu na lulu na wala kwa mavazi ya thamani (mavazi ya bei kubwa). Wajipambe kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kumcha Mungu (2:9-10). Katika Kiyunani, mstari wa tisa na wa kumi una neno moja tu la kujipamba, lakini nimeweka maneno matatu kwa ajili ya ufafanuzi kama ilivyo katika tafsiri nyingine za Biblia. Kwa ujumla, maana ya mistari hii sio kukataza kabisa kujipamba. Mistari hii inazungumza kuhusu vipaumbele. Wanawake wanaruhusiwa kujipamba, lakini watatakiwa kufanya hivyo kwa kujisitiri. Kujipamba kwao kuwe kwa mavazi ya adabu. Na wafanye hivyo kwa kiasi (wasizidishe). Ufafanuzi wa kanuni hio unakuja kwa namna mbili: namna ya kwanza ni ya zuio na namna ya pili ni ya hamasa. Zuio ni kuhusu kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu na lulu, na kuvaa mavazi ya bei kubwa. Hamasa ni kuhusu kujipamba kwa matendo mema.
Zuio la kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu/lulu na mavazi ya bei ghali sio zuio la kutokufanya kabisa, bali ni zuio la kipaumbele. Paulo anachosema ni kwamba mapambo ya mwanamke yawe zaidi kwenye matendo mema, na ikiwa ni katika mavazi basi wafanye hivyo kwa kujisitiri, kwa adabu na kwa moyo wa kiasi. Mtindo huu wa zuio la kipaumbele umetumika katika maeneo mengi katika Biblia na mara zote hauna maana ya zuio la kutokufanya kabisa.
Mfano, ukisoma Mathayo 6:19-20, Bwana Yesu anasema: “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi.” Maelekezo haya ya Bwana Yesu pia yana pande mbili: upande wa zuio na upande wa hamasa. Zuio ni kujiwekea hazina/akiba duniani. Hamasa ni kujiwekea hazina/akiba mbinguni. Ni dhahiri kwamba hapa napo Bwana Yesu anafundisha kuhusu vipaumbele. Bwana Yesu hafundishi kwamba tusiweke akiba kabisa duniani, bali anafundisha kwamba kuweka akiba mbinguni ni kipaumbele kuliko kuweka akiba duniani. Mtindo huu uko kwenye maeneo mengi ya Biblia. Mifano michache ni kama vile Luka 14:26, Wakolosai 3:2, na Yohana 6:27.
Kwa upande mwingine, Mtume Petro anasema: “Kujipamba kwenu kusiwe kujipamba kwa nje, yaani kusuka nywele na kujitia dhahabu na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani waliomtumaini Mungu na kuwatii waume zao. Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yoyote.”1 Petro 3:3-6
Tofauti na Mtume Paulo, Mtume Petro maelekezo yake yalikuwa yameelekezwa kwa wanawake waliolewa. Mistari yetu ni sehemu ya ujumbe wa maelekezo ya Mtume Petro kwa wake za watu (3:1-6). Ukisoma kwa makini mstari huu, utaona Mtume Petro anawaambia wake kwamba kujipamba kwao kusiwe kwa nje, yaani kusuka nywele, kujitia dhahabu na kuvaa mavazi. Bali kujipamba kwao kuwe kwa utu wa ndani (moyoni). Katika utu wa ndani pia anatoa ufafanuzi kwamba mapambo yawe ni roho ya upole na utulivu. Katika kusoma huko, utagundua kwamba hapa napo Mtume Petro anafundisha vipaumbele. Mtume Petro anawafundisha wake kwamba wafanye jitihada zaidi katika kuupamba utu wao wa ndani usioonekana kuliko wanavyofanya jitihada katika kuupamba utu wa nje. Kama tulivyotoa mifano pale juu kuhusu mtindo huu wa uwasilishaji wa ujumbe. Tuna uhakika kwamba isingewezekana mtume Petro kuwakataza kabisa wake za watu “kuvaa mavazi”, hivyo kwa ujumla wa maandiko yanafundisha kutanguliza mbele mambo ya utu wa ndani usioonekana.
Labda pia unaweza kujiuliza mbona Mtume Petro na Mtume Paulo wanafanana kabisa wanachokisema, pamoja na kwamba walikuwa wanawaandikia makundi tofauti?
Mtume Petro na Mtume Paulo hawakuwa wanaandika jambo jipya kabisa wanapoandika jumbe zao. Msisitizo huu unaonekana pia kwenye maandishi ya watu wengi wa jamii ya Dola ya Rumi (watu nje na Ukristo). Jamii kubwa ya Rumi ilikuwa inasisitiza wanawake kujipamba kwa tabia za ndani na sio katika mwonekano tu. Jamii hii ilisisitiza kujisitiri, kuwa na kiasi pamoja na adabu katika mavazi kwa wanawake. Waandishi kama Seneca, Dio Chrysostom, Juvenal, Plutarch, Epictetus, Pliny, na Tacitus waliandika kuhusu jambo hili. Kwa mfano, Plutarch katika ushairi wake uitwao “Ushauri kwa Bwana Harusi na Bibi Harusi”, anasema: “Sio dhahabu au mawe ya thamani au nguo nyekundu ambayo humfanya kuwa hivyo [yaani kuwa mrembo], lakini chochote kinachoingia ndani kile kinachoonyesha utu, tabia nzuri, na kiasi.”
Kwa nini ni muhimu kujua hili? Utagundua kwamba maana ya kujisitiri, kuwa na adabu, na kuwa na kiasi hayana mstari wa kutofautisha kinyume chake (hakuna mstari Biblia imechora kutenganisha kati ya kujisitiri na kutokujisitiri). Jamii husika ndio inaweza kusema vazi hili sio la kujisitiri, sio la adabu, na mtu huyu aliyevaa vazi husika amekosa kiasi. Jamii ndio inasema kweli maisha ya namna hii ndio maisha ya upole na utulivu au kinyume chake. Hivyo, ni muhimu kwa wanawake waliookoka kuvaa kwa kujisitiri, kwa adabu na kwa kiasi, kama jamii yote kwa ujumla inavyowatarajia. Tusiseme jamii imepitwa na wakati, hawaelewi mambo ya kizungu au wao ni washamba. Sisi kama waamini tunatakiwa kuishi kwenye kiwango bora zaidi kuliko madai ya jamii katika swala la maadili. Hii ndio maana Mtume Petro na Paulo waliwaelekeza wanawake waamini kufanya yale yaliyokuwa mazuri na yanayokubalika na jamii yao nzima.
Jibu la moja kwa moja: Biblia haikatazi wanawake kujipamba kwa mapambo ya aina yoyote ile isipokuwa mapambo hayo yafanyike kwa kujisitiri, kwa adabu, na kiasi. Na muhimu zaidi kuliko yote, wanawake watumie jitihada zaidi katika kupamba utu wao wa ndani usioonekana kuliko wanavyofanya katika utu wao wa nje unaoonekana.
Kwa upande mwingine, kama mapambo ya mwanamke hayasitiri mwili wake, ni mavazi ya aibu na hayaonyeshi kiasi (kiasi ni uwezo wa kujizuia matakwa yako), hayo ni machukizo mbele ya Bwana. Na tena, kama bidii inayotumika kupamba utu wa nje ni kubwa kuliko bidii inayotumika kupamba utu wa ndani, basi kuna changamoto ya kiroho kwa mwanamke huyo, na hivyo anahitaji kubadilika.