Kanisa na matatizo yake: Sehemu ya 1

Kanisa Na Matatizo Yake Na Namna Ya Kuyashughulikia.

Kanisa kama Biblia inavyoeleza ni watu walioitwa na kristo Yesu na kumkubali yeye kama Bwana na mwokozi wa maisha yao. Hivyo kanisa sio jengo au dhehebu. Watu hawa wanaomwamini Yesu katika Biblia wanawekwa katika makundi mawili, kundi la kwanza ni wale waliomwamini Kristo na wanaonana katika mahali pa kijografia inaweza kuwa katika mtaa, kijijii au mji mfano wanaomwamini Yesu walioko wilaya ya Kinondoni wanaweza kuitwa Kanisa la Kinondoni. Kundi la Pili ni watu wanaomwamini Yesu walioko ulimwenguni kote kwa ujumla. Hivyo Biblia anapotaja neno kanisa inakuwa na maana mbili tu, moja watu wanaomwamini Yesu walioko mahali Fulani pa kijografia (mtaa,Wilaya au mji) na mbili ni watu wote wanaomwamini Yesu ulimenguni kote.

NOTE. Kumwamini Yesu kama Biblia inavyoeleza na sio vinginevyo.

Je kanisa linaweza kuwa na matatizo? Jibu ni ndio. Kwa kutumia barua ya mtume Paulo kwa kanisa lililokuwa korintho(Mahali halisi pa kijografia) tutajifunza matatizo yaliyokuwako katikati yao na namna Mungu alivyosema nao namna ya kushughulikia matatizo yao. Katika kujifunza matatizo yao tutaona kuwa matatizo ya kanisa kwa Ujumla (Kanisa la mahali husika pa kijografia na kanisa la Ulimenguni kote) hayajatofautiana na matatizo yaliyokuwepo katika kanisa la Korintho. Unaweza kujiuliza mwandishi wa somo hili anajuaje matatizo ya kanisa la Ulimwengu kwa ujumla? Jibu ni kwamba tunaishi katika karne ya teknologia na sayansi, vinavyotokea upande mwingine wa dunia vinafahamika haraka sana upande mwingine wa dunia, Hivyo sio kazi kujua angalau kwa picha kubwa matatizo ya kanisa katika ulimwengu na katika kanisa la mahali pamoja kijografia. Nakiri siwezi kujua taarifa za ndani za waamini katika ulimwengu wote lakini picha kubwa ya matatizo ya kanisa inaweza kufahamika na mtu yeyote bila ufunuo maalumu.

Nitaanza na kueleza utangulizi kidogo wa barua ya mtume Paulo kwa wakorintho, nitaeleza ni nini wakorintho walielewa kutoka kwenye ujumbe wa Paulo na mwisho nitaeleza leo tunajifunza nini pamoja na kuhusisha mifano halisi ya hali yetu ya sasa ya kanisa.

1. Utangulizi wa barua ya kwanza ya Mtume Paulo kwa Wakorintho.

a. Historia ya kanisa la Korintho.

(Matendo ya mitume 18:1-18).

Kanisa la koritho lilianzishwa na mtume Paulo alipokaa katika mji huo wa Korintho kwa muda wa mwaka mmoja na nusu akiwa fundi wa kushona mahema. Baada ya kukaa mwaka mmoja na nusu Paulo aliondoka korintho na kuliacha kanisa likiendelea. Kanisa lilikuwa la mchanganyiko wa wayahudi na watu wa mataifa mengine mengi kwa kuwa mji huu wa korintho ulikuwa mji wa kibiashara.

b. Sababu za kuandika.

i) Kutoa majibu ya yale aliyoyasikia yakiendelea katika kanisa (1 Wakorintho 1:11).

ii). Kujibu mambo yale ambayo kanisa lilimuandikia kumuuliza (1 Wakoritho 7:1).

c. Matatizo yenyewe.

Sehemu hii tutajifunza tu matatizo yaliyo katika sura ya kwanza hadi ya sita. (Mambo ambayo Paulo aliambiwa yanaendelea katika kanisa). Matatizo haya ni kama ifuatavyo

i) Mgawanyiko katika kanisa (Sura ya 1:9-4:21).

ii) Mtu anayeishi na mke wa Baba yake. (Sura ya 5:1-13).

iii) Waamini kupelekana mahakamani. (Sura ya 6:1-11).

iv) Wanaume kufanya zinaa na makahaba . (Sura ya 6:12-25).

i) Mgawanyiko Katika Kanisa. (Sura ya 1:9-4:21).

Katika sura hizo Paulo anakiri kuwa amepewa taarifa kwamba kuna mgawanyiko katika kanisa. Na anaeleza moja ya sababu ya mgawanyiko ni Watumishi na utumishi wao. Kuna waamini walikuwa wanajitambulisha na Paulo, kuna waaminni walikuwa wanajitambulisha na Apollo na kuna waamini walikuwa wanajitambulisha na Petro (I wakorintho 1:12). Kwa nini walijitambulisha na watumishi hao? Jibu ni kwamba kila mmoja alijitambulisha na mtumishi anayefanya utumishi wake kama wao walivyokuwa wanataka (1 Wakorintho 1:22), kwa waamini wayahudi walitaka Ishara (Hivyo hawa walimpenda Petro) na kwa waamini wayunani walitaka Hekima ya uzungumzaji (Hawa walimpenda Apollo) na wengine walimpenda mwanzilishi wa kanisa (Hawa walimpenda Paulo).

Majibu ya Paulo kwa sababu hii anasema hamtakiwi kujitambulisha na watumishi kwa kuwa utambulisho wao ni KRISTO YESU ambaye ndiye Nguvu ya Mungu, Hekima ya Mungu na Msingi na mkuzaji wa kanisa(I wakorintho 1:23-24, 3:5-11) ambaye wayahudi na wayunani wasio mwamini kwao ni Kikwazo na upuuzi.

Kwa nini Kwa wahayudi Yesu kristo ni kikwazo? Wayahudi walitegemea Kristo kuwa na nguvu za kisiasa na kijeshi kuwatoa kwenye kutawaliwa na warumi sasa kristo anayekufa msalabani kwa aibu kwao alikuwa ni kikwazo.

NOTE. Neno masihi kutoka kiebrania na neno Kristo kutoka kiyunani yana maana moja. Ukiweka neno kristo kwenye masihi au masihi kwenye kristo ni sawa.

Kwa nini kwa wayunani Yesu kristo ni Upuuzi? Wayunani walikuwa wanavutiwa na maneno mazuri na upangiliaji wa hotuba ambazo zinaleta maana katika akili za kibinadamu, sasa Yesu anayeokoa kwa kufa kwao ilikuwa ni upuuzi ikimaanisha ilikuwa aiingii akilini “Huwezi kuokoa kwa kufa” Zaidi huyu Yesu alifufuka, kwao mambo ya kufufuka ilikuwa ni vitu visivyoingia akilini.

Hivyo Paulo amalizia jibu lake kwa kusema “3.21  Basi, mtu ye yote na asijisifie wanadamu. Kwa maana vyote ni vyenu; 3.22  kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; 3.23  nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu. 4.1  Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu.”

Paulo anamalizia kwa kusema wasijisifie mwanadamu bali wawahesabu watumishi kuwa ni mawakili ambao siku moja watahukumiwa na Mungu, akipima kazi zao kama zilikuwa na nia njema (I wakorintho 4:5) na anawaonyesha kwamba utambulisho wao uwe ni KRISTO YESU. Na anasema ametumia mfano wa Yeye na apolo kuwafundisha kwamba wasijivunie binadamu na kusababisha mgawanyiko katika kanisa (1 Wakorintho 4:6).

Mbali na mgwanyiko kutokana na watumishi na utumishi wao, mgawanyiko ulisababishwa pia na baadhi ya waamini kumchukia au kumhukumu Mtume Paulo, Hili analieleza sana sura ya nne.Na hii ni kwa kumlinganisha na mitume Wengine yaani Apolo na Petro. Kwa nini walimhukumu Paulo kwamba hana sifa za utume kwa kumlinganisha na watumishi wengine? Paulo hakuwa mtoa hotuba mzuri kama Apolo, Paulo hakupokea sadaka za kitumishi kama wengine, Paulo alifanya kazi za mahema na mitume wengine walifanya utume tu bila kazi zingine na mengine ambayo Paulo anaeleza pia katika barua yake ya Pili kwa wakorintho.

 Kwa hili Paulo anatoa majibu mawili anasema moja wakorintho hawastahili kumhukumu kwa kuwa atakaye mhukumu Paulo ni Mungu (1 Wakorintho 4:3-5) na anasema hata kama kuna waalimu wengi wanaowafundisha yeye ndiye aliyeanzisha kanisa hilo hivyo wamsikilize kama baba yao kwa kuwa anawapenda kama watoto wake aliowahubiria injili (1 Wakorintho 4:14-15).

SISI LEO TUNAJIFUNZA NINI?

Tatizo hili la mgawanyiko katika kanisa halijaisha hata leo na sababu za mgawanyiko ni zile zile, kujitambulisha na watumishi makundi makundi kwa kuwa kila mtu kuna kitu anataka kukisikia au kukiona na pia kukosoa au kuhukumu utumishi wa Mtumishi mwingine kwa kumlinganisha na mtumishi mwingine. Kuna wanaopenda miujiza wao huambatana na watumishi wenye karama za miujiza, kuna wenye kupenda hotuba zilizopangiliwa hao pia hujitambulisha na watumishi wenye hotuba nzuri. Kuna wenye kupenda mafunuo na unabii nao pia hujitambulisha na watumishi wa namna hiyo.

Umewahi kukaribishwa kwa mtumishi Fulani? Umewahi kuona uwepo wa mtumishi Fulani unatangazwa na kupambwa Zaidi wa uwepo wa Yesu ? Umewahi kusika Mungu wa mtumishi Fulani? Umewahi kusikia watoto wa mtumishi Fulani? Umewahi kusikia madhabahu ya mtumishi Fulani? Umewahi kusikia upako wa mtumishi Fulani? Umewahi kusikia mtumishi Fulani ana upako kuliko mtumishi Fulani? Umewahi kusikia mtumishi Fulani ni ngazi/level za juu na mwingine ni ngazi/level za chini? Umewahi kusikia utambulisho wa makundi ya theologia (Calvin and Arminian) ? Umewahi kusikia mgawanyiko unaotokana na theologia za mitume (Pauline, Johannine or Petrine theology) ? Kama jibu ni ndio kwenye maswali yote hapo juu au machahe ya hayo hiyo ni dalili kwamba kanisa lina shida ile ile iliyokuwa korintho na jawabu lake ni lile la miaka elfu mbili iliyopita YESU KRISTO NDIYE KILA KITU na ndiye UTAMBULISHO WETU watumishi wote ni sawa kwa uthamani tofauti yao iko katika utendaji kazi kama vile viungo katika mwili vinavyotofautiana  (Paulo anaeleza kwa ureu hili katika 1 wakorintho 12) na hatutakiwi kujitambulisha kwa majina ya watumishi wala hatutakiwi kijisifia mwanadamu yeyote bali muhesabu mtumishi yeyote kuwa mfanya kazi wa Kristo ambaye siku moja atahukumiwa kwa kile alichokifanya kama alikifanya kwa nia njema au la.

Paulo anaeleza vizuri katika sura ya 12 ya barua hii ya wakorintho wa kwanza kwamba waamini wote ni viungo ndani ya kanisa na kristo pekee ndiye kichwa cha kanisa. Hakuna anayestahili kulitambulisha kanisa nje isipokuwa sisi wote kwa pamoja tumtambulishe kristo kwa umoja wetu. Mataifa wanapotazama kanisa wamuone kristo kwa umoja wa waamini. Je umewahi kujiuliza mataifa wanalitambuaje kanisa leo? Karibu wote wanatambua majina na vyeo vya baadhi ya watu katika kanisa au majina ya madhehebu yetu. Kwa nini? Moja waamini wakitoka nje wanatambulisha watumishi wao hasa wachungaji na mitume au waalimu wao, Pili wachungaji au mitume wamepewa mamlaka anayostahili kristo kwa mafundisho yasiyoendana na Biblia hivyo wao wamekuwa ndiyo Picha watu wa mataifa wanayoiona. Tatu waamini wanatambulisha sana madhehebu yao nje kuliko kristo Mwanzilishi na kichwa cha kanisa.

Leo ukisema tu nimeokaka swali la kwanza utaulizwa, unasali dhehebu gani? Au uko chini ya mtumishi nani? Haya yote yanaonyesha mgawanyiko mkubwa ndani ya kanisa. Leo ukiandaa mkutano/kongamano/tamasha swali la kwanza kila mmoja anataka kujua ni mtumishi nani atahudumu. Majina na vyeo vya watumishi vina sauti kubwa kuliko Yesu wenyewe. Hili ni tatizo la kanisa katika ulimwengu wetu wa karne ya 21 kama ilivyokuwa karne ya kwanza kule korintho.

Tatizo hili sio tu la kanisa katika muktadha wa kanisa katika ulimwengu bali hata kanisa la mahali pamoja. Kwenye ushirika wa waamini tunaoonana kila jumapili bado waamini wanagawanyika kutoka na mtumishi wanayempenda. Hii imepelekea hata waamini wa eneo moja kugawanyika kabisa katika mahali pa kukutana ndio maana makanisa ya mahali pamoja yanaongezeka. Makanisa yamekuwa yakiongezeka sio kwa sababu za ongezeko la mavuno kwa bwana bali kwa sababu za ongezeko la migawanyiko. Wapenda miujiza wameondoka na mwenye karama ya miujiza na wenye kumpenda mwanzilishi wamebaki na mwanzilishi, wenye kupenda fedha na mali wamekwenda na mwenye fedha na mali, wenye kupenda umaarufu wamekwenda na mtumishi maarufu kwa kifupi kila mwamini anajichagulia mtumishi wa kwenda nae.

Hitimisho la tatizo hili na jawabu lake.

Kanisa leo linagawanyika kwa kujitambulisha na watumishi kama wakorintho kwa kuwafuata watumishi wenye utumishi unaoendana na mambo wanayoyataka kuyasikia au kuyaona ambayo hasa yanahusiana na maisha yao kabla ya kuamini, kwa wakorintho ilikuwa ni ishara (Kwa wayahudi) na hekima (Kwa wayunani) leo inaweza kuwa Ishara na miujiza (Kwa wale waliotoka kwenye uvivu, uchawi, uganga, mashindano na magonjwa) , fedha na mali (Kwa waliotoka kwenye umaskini), Umaarufu (Kwa walitoka kwenye kukataliwa, kudharauliwa) au Hekima/hotuba zilizopangiliwa (Kwa walitoka kwenye utajiri na elimu). Na jawabu la kuvunja huu mgawanyiko ni kujua kwamba tunayemhitaji na aliye jawabu la mambo yote ni YESU KRISTO TU bila kujitaambatanisha na mtumishi yeyote maalumu kwa kuwa watumishi wote ni wafanya kazi wa YESU KRISTO. Kifupi YESU KRISTO ndiye tunayemhitaji ambaye hajashikamanishwa na mtumishi yeyote.

Ukimtambua Yesu kisto kama ndiye jawabu utawaheshimu waamini wote kwa utumishi wao kwako na nafasi ya Yesu itabaki kwake. 

Kuwa sehemu ya jawabu na usiwe sehemu ya tatizo, usijitambulishe au kujifisia utumishi wa mtumishi yeyote, usilitambulishe kanisa kwa jina lako au kwa utumishi wako, usidhalau/kuhukumu utumishi wa Mtumishi mwenzio (Hii haimaanishi usisahihishe upotofu, usahihisho uwe katika upendo), usilinganishe watumishi kwa utumishi wao,  Tambua sisi sote tu viungo na watenda kazi tu kama vile ambavyo Paulo au Petro au Apollo hawakufa kwa ajili ya wakorintho wala kwa ajili yetu  ndivyo  ilivyo  Hakuna Mchungaji, askofu, nabii, mtume, mwimbaji, mwalimu na wengine wote  aliyekufa kwa ajili yako. Wewe ni wa KRISTO Utambulisho wako ni KRISTO jisifie KRISTO Jiungamanishe na KRISTO, Jipendekeze kwa KRISTO………….KRISTO.