Kuhusu Sisi
Biblianakanisa.org ni tovuti maalumu iliyoundwa kwa ajili ya kuwasaidia waamini wanaozungumza Kiswahili kupata nyenzo mbalimbali zitakazowawezesha katika usomaji wao wa Biblia. Tunaamini kwamba kila mwamini anapoamua kusoma Biblia anatakiwa kulenga kuelewa vizuri ufunuo wa Mungu ulipo katika Biblia, na baada ya kuelewa vizuri, anatakiwa kulenga kuishi sawa sawa na uelewa huo. Hivyo, tupo kwa ajili ya kumsaidia kila mwamini kukamilisha lengo hilo. Katika kutimiza wajibu huo, tovuti hii inakuletea mwongozo na ufafanuzi wa kila kitabu katika vitabu vyote sitini na sita vya Biblia.
Zaidi ya usomaji wa Biblia, tunalenga pia kuwasaidia waamini kujifunza kuhusu kanisa. Tunaamini kwamba kanisa na Biblia vina mahusiano yasiyoweza kutenganishwa. Mungu alilitumia kanisa kulitambua na kulihifadhi neno lake, ndio maana ni ukweli usiopingika kwamba Biblia tunayoisoma leo ilizaliwa katika maisha ya kanisa. Wakati huohuo, Mungu amelitia kanisa chini ya mamlaka ya neno lake, yaani Biblia. Kwa hiyo, uelewa sahihi wa maandiko hupatikana ndani ya kanisa, na vivyo hivyo, kanisa hueleweka kwa usahihi kadiri linavyoelezewa na Biblia.
DIRA
Ni kulipeleka Kanisa katika lengo sahihi la usomaji wa Biblia na kulipa Kanisa kila nyenzo itakayosaidia usomaji huo.
DHAMIRA
Kuandaa nyenzo mbalimbali zitakazosaidia Kanisa katika usomaji wa Biblia wenye lengo sahihi
Imani Yetu
Kwa kuwa imani yetu ya Kikristo imegawanyika katika taasisi na madhehebu tofauti tofauti, tovuti yetu haifungamani na upande wa taasisi au dhehebu lolote. Hii ni kwa sababu lengo la tovuti hii, halihitaji kufungamana na upande wowote. Pamoja na kusema hivyo, kwa ujumla imani yetu ni imani yenye mlengo wa Kiprotestanti (mlengo unaofuata dhamira ya wanamageuzi wa Kanisa wa karne ya kumi na sita). Hivyo, tunaamini kwamba Biblia yenye vitabu sitini na sita ndiyo yenye mamlaka ya juu kabisa kuliko vitu vingine vyote. Biblia hii ndio mwongozo wenye kauli ya mwisho juu ya mambo yanayohusu imani na mafundisho. Imani yetu hii haimaanishi kwamba tunayakataa mapokeo yote ya Kanisa, bali tunaamini kwamba mapokeo yoyote ya Kanisa yako chini ya Biblia, hivyo yanatakiwa kufuatwa kadri yanavyofuatana na ujumbe wa Biblia. Kutokana na imani hii ya msingi, tunaamini kila fundisho linalofundishwa na Biblia yenye vitabu sitini na sita tu.
Timu Yetu
Kazi ya tovuti hii inafanywa na timu ya watu wachache wakiongozwa na Mwalimu Assa S. Jotham, mhitimu wa shahada ya Biblia na Theolojia kutoka Chuo cha Global Harvest Bible College kilichokuwa Ubungo, Dar es Salaam, kabla ya kuhamia Kibaha, Mkoa wa Pwani. Matarajio yetu ni kuongeza idadi ya watu ili kuyatimiza maono yetu kwa muda muafaka. Hivyo, tunakaribisha kila mtu mwenye sifa zifuatazo kujiunga nasi katika utumishi huu.
- Awe mtu aliyemwamini Yesu si chini ya muda wa miaka mitatu na amekuwa mshirika wa kanisa la mahali pamoja si chini ya muda wa miaka miwili.
- Awe mwamini anayejua kusoma na kuandika Kiswahili fasaha.
- Awe mwamini anayekubali kufanya kazi ya utumishi huu bila malipo.
Mwamini yeyote mwenye sifa hizo anaweza kuwasiliana nasi kwa ajili ya kuwa sehemu ya utumishi huu.
Ushirikiano Wetu
Kwa kuwa lengo letu ni kuwasaidia waamini kusoma Biblia na kufikia kilele cha kuishi sawa sawa na ufunuo wa Mungu uliopo ndani ya Biblia, timu yetu ipo tayari kushirikiana na kanisa lolote la mahali pamoja katika kufundisha au kusoma kitabu chochote cha Biblia kwa pamoja kupitia makundi madogo madogo. Zaidi ya usomaji wa Biblia, timu yetu ipo tayari pia kufundisha na kujifunza kwa pamoja historia ya Kanisa, kwa lengo la kuboresha uelewa wa Biblia. Kwa ushirikiano huu, unaweza kuwasiliana nasi kwa mawasiliano yetu hapo chini.
Wasilana Nasi
Tutafurahi Kusikia kwako. Tutumie ujumbe wako
