Kula Mkate Na Kukinywea Kikombe Isivyostahili?

Biblia inasema katika 1 Wakorintho 11:27 kwamba”….kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana.” Je kula mkate wa Bwana na kukinywea kikombe cha Bwana isivyostahili ina maanisha nini?

Majibu ya swali hili yanapatikana katika sura hii hii ya 11 ya kitabu cha wakorintho wa Kwanza.

UTANGULIZI.

Tutasoma 1 wakorintho 11 kuanzia mstari wa 17 mpaka wa 34. Kwa nini maandiko haya? Ni kwa sababu mstari wetu unatoka kwenye maelezo ya jambo moja ambalo Mtume Paulo alikuwa analielezea kutoka mstari wa 17 na kumalizia mstari wa 34. Ni muhimu kujua mstari unaojiuliza swali kwenye Biblia uko sehemu gani ya maelezo ya maada husika. Paulo katika mistari hii ilikuwa anashughulika na tatizo moja ambalo ni MGAWANYIKO (FARAKA) KATIKA MEZA YA BWANA.

KUKUMBUKA Paulo amezungumza sana na kanisa la korintho kuhusu mgawanyiko(Fitina) tangu sura ya kwanza mstari wa tisa mpaka sura ya nne mstari wa ishirini na moja (Maelezo kuhusu mgawanyiko huu nimeyaandika katika somo la KANISA NA MATATIZO YAKE NA NAMNA YA KUYASHUGHULIKIA Unaweza kupata somo hili pia kusoma).Hii inatuonyesha kuwa mgawanyiko lilikuwa tatizo kubwa katika kanisa la korintho kama mgawanyiko ulivyotatizo kubwa kwenye kanisa la karne ya 21. Hivyo na hapa Paulo anaongea kushughulikia mgawanyiko lakini sasa ni mgawanyiko katika tukio la Meza ya Bwana.

TUJIFUNZE.

1. TATIZO NI NINI?

11.17  Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara.

11.18  Kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki;

11.19  kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu.

MAELEZO.

Moja Paulo anasema kwa haya anayoyaagiza hana la KUWASIFU kwa kuwa AMESIKIA Kuna faraka (MGAWANYIKO) katikati yao.

Pili Paulo anasema wanapokusanyika kama kanisa wanakusanyika kwa HASARA SI KWA FAIDA kwa sababu ya mgawanyiko.

Hivyo tunaona tatizo ni mgawanyiko wanapokusanyika kama kanisa.

2. TATIZO LILIKUWA LINATOKEAJE?

11.20  Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana;

11.21  kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa.

11.22  Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo.

MAELEZO.

Sehemu hii ya Pili Paulo anaeleza sasa mgawanyiko huu ulikuwa unatokeaje.

Moja kuna waliokuwa wanatangulia kula chakula, wakati huo huo kuna walikuwa wana njaa na upande mwingine kuna waliokuwa wamelewa. Kumbuka haya yalikuwa yanatokea wakati wakiwa wamekusanyika.

Anawauliza Je hawana nyumba za kula na kunywea? Au wanafanya hivyo kwa kudharau kanisa la Bwana? Au wanafanya hivyo kuwataharisha masikini (wasio na kitu).

Ili kuelewa vizuri maelezo ya Paulo hapa naomba tujifunze mambo mawili.

a. Kanisa la Bwana.

Kwa wakati wa sasa waamini wengi wakisikia neno kanisa la Bwana wanatasfiri kanisa kama Jengo lile wanalokutania. Hii inadhihirishwa na namna waamini wanavyoheshimu Zaidi majengo yao ya kukutania. Lakini Paulo anaposema kudharau Kanisa la Bwana anamaanisha kudharau waamini wanaokusanyika pamoja. Kumbuka karne ya kwanza mikusanyiko yao ilifanyika katika nyumba za watu hasa wale wenye nyumba au eneo la kuweza kuchukua watu wengi (Hii ina maana hasa wenye uwezo wa kifedha ndio waliweza kuwa na nyumba za kuweza kuruhusu kanisa kukusanyika).

b. Meza ya Bwana.

Meza ya Bwana kwa waamini wa kanisa la kwanza ilikuwa inafanyika kama sehemu ya mlo wa pamoja wa Upendo. Kwenye mlo huu wa upendo wa pamoja Kila mtu anakuja na chakula chake au mwenye nyumba anawaalisha waamini wengine. Hii ikiwa na maana walikuwa wanakula chakula cha kawaida na kunywa kwa pamoja kama mlo wa upendo, katika mlo huo huo ndio walikuwa wanakula mkate na kunywa kikombe cha divai kukumbuka mauti ya Bwana Yesu. Hivyo meza ya bwana na mlo wa pamoja wa upendo ulikuwa unafanyika pamoja. Bahati mbaya leo haifanyiki hivyo ndio maana inaweza kuwa ngumu kumuelewa Paulo vizuri katika sehemu hii.

Kwa maelezo hayo tatizo lilikuwa watu wengine walikuwa wanakula chakula chao (Wenye uwezo wa kuleta chakula) bila kushiriki (Kuwasubiri) na wengine, hivyo ikapelekea kati yao walikuwepo waliokuwa na njaa (Wale wasiokuwa na uwezo wa kuleta chakula). Si hivyo tu bali maskini ambao ilitakiwa katika mkusanyiko huu nao wale vizuri walikuwa wakifadhahishwa.  Ndio maana Paulo anauliza Je hamna nyumba za kwenu za kula na kushiba? Hii ikimaanisha walichofanya si kizuri kufanyika katika mkusanyiko wa waamini kama walikuwa na njaa wangekula nyumbani mwao maana Lengo la chakula hiki ilikuwa ni USHIRIKA SIO KUSHIBA.

Chakula hiki kililetwa na waamini wenyewe (Kila mtu anakuja na chakula chake katika mlo huu wa upendo au Mwamini mwenyeji aliwalisha waamini waliokusanyika kwake.)

Kwa  ujumla naweza kusema tatizo lilikuwa ni mgawanyiko kati ya walio navyo na wasio navyo katikati ya mkusanyiko uliokusudia KUWAUNGANISHA NA KUKUMBUKA MAUTI YA BWANA.

3. KUSUDI LA MEZA YA BWANA.

11.23  Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate,

11.24  naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.

11.25  Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.

11.26  Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

MAELEZO.

Paulo sasa baada ya kuonyesha tatizo ni nini na lilitokeaje anawakumbusha waamini wa korintho kuhusu Meza ya Bwana. Anasema yeye aliwapa (Aliwafundisha) kama yeye alivyopokea (Alivyofundishwa) kwamba Yesu usiku ule ulitwaa mkate, ukaumega na kuwapa wanafunzi wake wale na pia akakitwa kikombe na kusema hii ndio damu yake ya Agano imwagikayo na wanywe kwa kumkumbuka Yeye. Hii habari Paulo anaisema kwa kufafanana kabisa na kile Luka alichoandika katika Luka 22.

Na Paulo anamalizia kwa kusema kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

KUMBUKA. Yesu anasema tufanye Tukio la Meza ya Bwana kwa kumbukumbu yake (Luka 22:19, Paulo anarudi maneno ya Yesu katika mstari wa 24 wa sura ya 11 ya 1 wakorintho kwamba tukio hili lifanyike kwa ukumbusho. Paulo anaongeza kwa kusema kwa kufanya tukio hili tunaitangaza mauti ya Bwana mpaka atakaporudi. Na Yesu alisema akirudi na ufalme wake atakuwa na meza kama hii na waamini.

Hapa tunajifunza lengo la meza ya Bwana. Kumbukumbu ya Yesu na kutangaza mauti yake katikati ya waamini ndio lengo la meza ya Bwana. Ulimwengu unamkumbuka Yesu kwa kusherekea Pasaka au Christmas lakini Yesu alisema kumbukumbu yake iwe kwenye kula mkate na kunywa kikombe.

Je wewe huwa unashiriki Meza ya Bwana kwa ajili gani????? Je sababu yako ya kushiriki iko kama Biblia inavyofundisha?????

4. KUNYWA NA KULA ISIVYOSTAHILI.

a. Nani ana makosa?

11.27  Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana.

MAELEZO.

Angalia mtiririko wa Paulo, ameanza na kueleza tatizo na jinsi linavyotokea, akaeleza kwa usahihi tukio la meza ya Bwana na sababu ya kufanya, sasa anasema Yeye atakaye kula mkate na kunywa kikombe isivyostahili atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu.

“Isivyostahili” ni kwa namna gani?

Jibu linapatikana katika maelezo ya tatizo (mstari 17-22) na katika suruhisho Paulo alilolitoa (mstari wa 33-34). Yaani kama Mtu atashiriki meza ya Bwana katikati ya waamini kwa fitina ( kuligawa kanisa) atakuwa na hatia ya mwili na damu ya Yesu. Kwa maelezo Zaidi anawaambia wakorintho kama unakula na kunywa meza ya Bwana kwa MGAWANYIKO basi kila afanyae hivyo anajipatia hatia.

b. Nifanye nini ili nisiwe mwenye makosa?

11.28  Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.

MAELEZO.

Hivyo kila mtu ajihoji mwenyewe kabla hajala mkate au kukinywea kikombe. Kujihoji hapa ni kila mwamini kujitafakari kwamba anashiriki katika kuliunganisha kanisa au kulitengenisha katika tukio hili muhimu la Meza ya Bwana.

c. Matokeo ya kunywa isivyostahili ni nini?

11.29  Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili.

MAELEZO

Kula na kunywa isivyostahiri kunaleta hukumu kwa afanyaye hivyo kwa sababu amefanya hivyo bila kuupambanua mwili. Je Paulo anamaanisha nini kusema kutokuupambanua mwili? Mwili hapa anamaanisha mkate? Au anamaanisha kanisa? Kanisa ni mwili wa kristo na mkate pia ni mwili wa kristo.

Paulo angemaanisha mkate asingeweza kuacha damu/kikombe kwa kuwa popote alipotaka kuzungumzia mkate hakuacha kutaja na kikombe/damu pia maana hivi zinaenda pamoja (Angalia mstari wa 27na 28). Kwa maneno mengine angesema kutokupambanua mwili na damu ya Bwana kama mstari wa 27.

Paulo anamanisha huu upambanuzi ni wa Mwili wa kristo yaani kanisa. Mtu atapata hukumu akishiriki meza ya Bwana bila kufanya maamuzi sahihi kuhusiana na kanisa (Mwili). Kama atashiriki meza ya Bwana na  kusababisha mgawanyiko huyo mwaamini anajipatia hukumu.

Kwa nini Paulo anatumia neno mwili hapa akimaanisha kanisa(Waamini)? Hili analieleza katika barua hii hii sura ya 10 anasema

10.15  Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.

10.16  Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?

10.17  Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.”

Na katika sura ya 12 anaeleza kwa kirefu kuhusu mwili huu. Mwili ambao wakorintho walishindwa kuupambanua.

d. Wapo waliopata tayali matokeo?

11.30  Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala.

11.31  Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa.

11.32  Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia.

MAELEZO.

Sasa kwa kuwa wakorintho walishakula na kunywa isivyostahiri Paulo anasema hukumu imeshapita ndio maana kuna wengine wanaumwa na kuna wengine wamekufa. Anasema kama tungefanya maamuzi sahihi ya kulitambua kanisa tusingehukumiwa na Bwana. Lakini anamalizia kwa kusema hukumu hii walioipata wakorintho kwa kufa na kuugua sio sawa na ile watakayopata wasioamini(Sio hukumu ya kwenda Jehanum). Hukumu hii ni ya kimahusiano yenye lengo la kurekebisha. Neno “twarudiwa na Bwana” ni “God’s chastening” kwenye Lugha ya kiingereza, likiwa na maana ya adhabu Mungu anayoitoa kwa lengo la kumrekebisha mwamini au kurekebisha kanisa. Mwandishi wa waebrania ameeleza kwa uzuri jambo hili katika Waebrania 12:7-13

f. Jawabu la tatizo ni nini?

11.33  Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojaneni;

11.34  mtu akiwa na njaa, na ale nyumbani kwake; msipate kukutanika kwa hukumu. Na hayo yaliyosalia nijapo nitayatengeneza.

Maelezo

Paulo anamaliza kwa suruhu kwamba wakati wa meza ya Bwana ambayo huusisha mlo wa upendo waamini wasubiriane ili kuimarisha ushirika. Kama mtu ana njaa basi ale mapema nyumbani ili ashibe akienda kwenye kukusanyika asubiri wenzake kwa kuwa lengo la chakula cha pamoja ni USHIRIKA na sio KUSHIBA au KUTENGANISHA WAAMINIna mengine alisema atawapa maelekezo akienda.