MWONGOZO WA KUSOMA KITABU CHA MAMBO YA WALAWI.
MAELEKEZO
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI
Biblia ya Kiyahudi, au Tanaki kama inavyoitwa na Wayahudi wenyewe, ina mpangilio wa makundi matatu ya vitabu vyake. Kundi la kwanza ni vitabu vya Sheria, kundi la pili ni vitabu vya Manabii, na kundi la tatu ni vitabu vya Maandishi. Katika makundi hayo matatu, kundi la vitabu vya Sheria ndilo kundi la awali, ndilo msingi wa Biblia nzima, na ndilo kundi lenye mamlaka zaidi ya makundi mengine. Kundi hili, ambalo ndilo lina mamlaka zaidi kuliko makundi hayo mengine, lina jumla ya vitabu vitano. Katikati ya vitabu hivi kuna kitabu kinachoitwa Mambo ya Walawi. Kama jina linavyojieleza, kitabu hiki ni mahususi kwa ajili ya kuelekeza yafuatayo: Nini Waisraeli wanatakiwa kufanya katika shughuli zote za kiibada. Nini ni wajibu na kazi za makuhani katika ibada (ambapo makuhani hao walitoka katika kabila la Lawi). Zaidi ya hayo, kitabu hiki kinaelekeza ni aina gani ya maisha waisraeli wanatakiwa kuyaishi kila siku katika maeneo yote.
MUKTADHA WA UJUMBE WA KITABU HIKI
Kitabu cha Kutoka kinafikia mwisho baada ya kukamilika kwa ujenzi wa hema ya kukutania; siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, mwaka wa pili tangu Israeli watoke Misri (Kutoka 40:17). Baada ya hema ya kukutania kufunikwa na utukufu wa Mungu, kiasi kwamba hata Musa hakuweza kuingia ndani yake (Kutoka 40:34-35), ndipo Mungu akaanza kuzungumza na Musa ujumbe uliopo kwenye kitabu hiki. Kwa kuwa kitabu cha Hesabu kinaanza na maagizo ya Mungu kwa Musa, yaliyotolewa siku ya kwanza ya mwezi wa pili, mwaka wa pili (Hesabu 1:1), ni dhahiri kwamba ujumbe wa Mungu ulioko kwenye kitabu cha Mambo ya Walawi ulitolewa kwa muda wa mwezi mmoja. Muda wote huu, hema ya kukutania ilikuwa imefunikwa na utukufu wa Mungu: mchana kulikuwa na wingu na usiku kulikuwa na wingu lenye mfano wa moto (Kutoka 40:38; Hesabu 9:15-23). Baada ya ujumbe huu kuisha, siku ya ishirini wingu liliinuka kutoka kwenye hema la kukutania na hivyo kuruhusu Waisraeli kuendelea mbele na safari (Hesabu 10:11).
Ujumbe wa Mungu uliopo kwenye kitabu hiki ni ujumbe wenye kusudi la kuwatenga waisraeli ili wawe taifa teule kwa Mungu: Taifa lisiloishi kwa kufuata taratibu na aina ya maisha ambayo ilikuwa ni kawaida kwa mataifa yaliyokuwa mashariki ya kati ya kale kama vile mataifa ya Kanaani na Misri (Walawi 18:3). Hivyo, maelekezo mengi Mungu anayoyatoa katika kitabu hiki yako kinyume na kawaida ya maisha ya mataifa mengine yaliyokuwa mashariki ya kati ya kale. Mfano wa mambo hayo ni kama ifuatavyo:
- Maisha ya ibada.
Mashariki ya Kati ya Kale ilikuwa jamii ya watu waliokuwa waabudu miungu mingi. Mtu mmoja angeweza kushiriki ibada kwa miungu mbalimbali kulingana na eneo alilopo na mahitaji ya maisha. Kwa mfano, mtu angeweza kumwabudu Ashera (mungu mke wa uzazi), kisha akafanya ibada kwa Anat (mungu mke wa vita na mawindo), na pia akamwabudu Baali (mungu mume wa ardhi na mbingu – ardhini akihusishwa na mazao na mbinguni na mvua, dhoruba, radi na upepo). Zaidi ya hayo, mungu mmoja angeweza kuabudiwa kwa namna tofauti kulingana na mazingira na maeneo. Hali hii ilisababisha kuwepo kwa maeneo mengi ya ibada: madhabahu nyingi, mahekalu mengi, na maeneo mengi yaliyoinuka kama vile milima na vilima maalumu kwa ajili ya ibada. Ibada hizi kwa kawaida zilihusisha kuchinja wanyama na kutoa sadaka kwa miungu. Kwa hiyo, watu walikuwa na uhuru wa kuchinja na kutoa sadaka katika maeneo mbalimbali.
Kinyume na hali hiyo, Mungu aliwaagiza Waisraeli kwamba ibada zao zote zifanyike katika hema la kukutania pekee (yaani, sehemu moja tu kwa watu wote). Kuchinja kwao kulipaswa kufanyika katika mlango wa hema la kukutania (hata kuchinja wanyama kwa ajili ya kula, japo hili lilikoma walipofika kaanani), na sadaka zao zote zilitakiwa kutolewa katika hema ya kukutania. Zaidi ya hapo, waliagizwa kumwabudu Yahweh peke yake bila kumchanganya na miungu mingine (Walawi 17:1–9). Kwa hivyo, maagizo haya yalikuwa ni kinzani dhidi ya ibada za kiasili za mataifa mengine ya Mashariki ya Kati ya Kale, kwa kuwa yaliweka msisitizo katika: Umoja wa ibada (mahali pamoja, si popote) na Umoja wa Mungu (Yahweh peke yake).
- Mahusiano ya kimapenzi.
Sura ya kumi na nane ya kitabu hiki inatoa sheria za Mungu zinazokataza aina fulani za mapenzi, kama vile mapenzi ya jinsia moja (ushoga), mapenzi kati ya ndugu wa karibu, na mapenzi kati ya binadamu na wanyama. Mambo haya yanakatazwa yakitanguliwa na utangulizi unaowataka Waisraeli wasiishi kama Wamisri na Wakanaani walivyokuwa wakiishi (18:1-5). Tena, sura hii inahitimishwa kwa msisitizo kwamba kwa sababu Wakanaani waliishi maisha hayo, nchi ikawatapika, na hiyo ndiyo sababu Waisraeli watapata nafasi katika nchi hiyo. Vivyo hivyo, ikiwa Waisraeli nao wataishi kwa namna hiyo, basi nchi itawatapika pia. Kwa ujumla, ni kwa mara saba Mungu anasisitiza kwamba Waisraeli wasiishi kama Wamisri na Wakanaani katika suala la mapenzi katika sura hii (18:3 [mara mbili], 24, 26, 27, 29, na 30). Zaidi ya hapo, sura ya ishirini inaweka wazi adhabu zitakazompata mtu atakayefuata maisha hayo ya kimapenzi. Adhabu kuu kati ya zote ni kuuawa kwa mtu husika.
Kwa hiyo, Biblia inaonyesha wazi kwamba Mungu aliwakataza Waisraeli wasiishi kama Wakanaani na Wamisri walivyokuwa wanaishi.
Pamoja na kwamba maandishi nje ya Biblia yanaonyesha kuwa kwa sehemu kubwa jamii za wakati huo zilizuia mapenzi kati ya ndugu wa karibu, kuna maandishi mengine yanaonyesha kwamba maisha ya ndoa kati ya dada na kaka yalikuwa ni sehemu katika familia za kifalme za kifarao huko Misri. Mbali na hilo kuna ushahidi wa mapenzi ya jinsia moja katika maandishi ya Mesopotamia na Kanaani. Tena, kuna ushahidi wa mapenzi kati ya binadamu na wanyama unaotoka Misri, Kanaani, na kwa Wahiti. Yote haya yanathibitisha kwamba sheria za Mungu zilikuwa na kusudi la kuwatenga Waisraeli mbali na maisha ya mataifa mengine.
- Desturi za maombolezo.
Katika sura ya ishirini na moja, Mungu anaagiza kwamba makuhani wasihusike katika mazishi isipokuwa kwa ndugu zao wa karibu tu (21:1-4). Hii ni kwa sababu kugusa mwili wa mtu aliyekufa kulihesabiwa kuwa ni kujinajisi. Hivyo, Mungu aliruhusu makuhani kujinajisi kwa ajili ya ndugu zao wa karibu tu. Baada ya agizo hilo, Mungu anasema makuhani “Wasijifanyie upaa kichwani, wala wasinyoe pembe za ndevu zao, wala wasichanje chale katika miili yao” (Walawi 21:5). Unaweza kujiuliza: kwanini amri hii imetolewa katika muktadha wa kuzungumzia mazishi? Jibu ni kwa sababu mambo haya ndiyo makuhani wa Kimisri walikuwa wanafanya kwa ajili ya wafu. Sio tu makuhani wa Misri walifanya hivyo, bali pia waombolezaji Wakanaani na Wamesopotamia walinyoa nywele za kichwa, walipunguza kingo za ndevu, au walichanja mashavu ili kuwaheshimu wafu au miungu ya ulimwengu wa chini, kama inavyoripotiwa na maandishi ya Kiugariti.
Hii ndiyo maana agizo hili ndani ya Israeli haliishii kwa makuhani pekee, bali linaenda kwa watu wote pia. Katika Walawi 19:27-28 Mungu anasema: “Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu. Msichanje chale yoyote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana.” Bado utaona amri hii ipo katika muktadha wa mazishi au kutoa heshima kwa wafu. Hivyo, sheria ya Mungu kupinga kunyoa kipara, kunyoa pembe za ndevu, kuchanja chale, na kujiandikia alama mwilini iko katika muktadha wa kupinga tamaduni za watu wa mataifa waliokuwa wakifanya hivyo kuwaheshimu wafu au miungu iliyohusishwa na maisha ya ulimwengu wa chini baada ya mtu kufa.
Mambo haya matatu ni mifano ya kuonyesha kwamba sheria ambazo Mungu anatoa katika kitabu hiki ziko katika muktadha wa kuwatenga Waisraeli na maisha yaliyokuwa ya kawaida kwa mataifa mengine. Hivyo, kila unaposoma kitabu hiki, jua kilichokuwa kinaendelea nyuma ya kila sheria na taratibu ambazo Mungu aliweka.
MPANGILIO WA KITABU
| MAELEZO | WALAWI |
| Namna ya kutoa dhabihu | 1:1-7:38 |
| Kutiwa mafuta kwa ukuhani | 8:1-10:20 |
| Unajisi na usafi | 11:1-16:34 |
| Maelekezo ya kuishi utakatifu wa vitendo | 17:1-26:1-46 |
| Sheria za kuhusu kuchinja na umwagaji wa damu | 17:1-16 |
| Sheria kuhusu mahusiano ya kimapenzi | 18:1-30 |
| Sheria kuhusu mambo mbalimbali | 19:1-36 |
| Adhabu kwa wavunja Sheria | 20:1-27 |
| Maelekezo kwa Makuhani | 21:1-22:33 |
| Sikukuu katika taifa | 23:1-44 |
| Kinara cha taa na mikate ya wonyesho | 24:1-9 |
| Ujira wa kulaani na kukufuru jina la Bwana | 24:10-23 |
| Sabato ya ardhi na mwaka wa Yubile | 25:1-55 |
| Ahadi za Baraka na Laana | 26:1-46 |
| Nadhiri, kuweka wakfu na Zaka | 27:1-34 |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI
Kitabu cha Kutoka kinahitimishwa kwa ujenzi wa hema la kukutania na kufunikwa kwake na utukufu wa Mungu, kiasi kwamba hata Musa hakuweza kuingia ndani yake (Kutoka 40:34-35). Kuanzia hapo, kitabu cha Mambo ya Walawi kinaanza kwa Mungu kumuita Musa kutoka katika hema hiyo na kumpa maelekezo kuhusu utoaji wa sadaka. Mungu anamwagiza Musa awapatie Waisraeli mwongozo wa namna wanavyopaswa kumtolea sadaka (au dhabihu) katika hema ya kukutania (1:1-2).
Katika Sehemu ya kwanza ya kitabu hiki (1:3–7:38) Mungu anaelezea aina tano za sadaka ambazo Waisraeli wote walitakiwa kutoa. Katika kila sadaka, Mungu anaelekeza kuhusu nini kitolewe na namna ya kukitoa. Vilevile, Mungu anatoa maelekezo ya kazi na wajibu wa mtoaji na kuhani katika sadaka husika.
Sadaka ya kwanza ambayo Waisraeli wote walitakiwa kutoa ni sadaka ya kuteketezwa (1:3–17). Sadaka hii, Mungu aliruhusu kutolewa kwa namna moja kati ya namna tatu tofauti alizoziweka. Kwanza, mnyama dume asiye na dosari kutoka katika jamii ya wanyama wa kufugwa wenye maumbile makubwa kama vile ng’ombe (1:3–9). Pili, mnyama dume asiye na dosari kutoka katika jamii ya wanyama wa kufugwa wadogo kama kondoo au mbuzi (1:10–13). Tatu, kwa wale wasio na uwezo mkubwa kifedha, ndege wa aina ya njiwa au hua (1:14–17).[1]
Sadaka ya pili ambayo waisraeli wote walitakiwa kutoa ni sadaka ya unga (Nafaka). Sadaka hii pia, Mungu aliruhusu kutolewa kwa namna moja kati ya namna nne tofauti alizoziweka. Kwanza, ingeweza kutolewa kama unga safi usiopikwa lakini umetiwa mafuta na ubani (2:1-3). Pili, ingeweza kutolewa kama unga uliopikwa kwa namna tatu tofauti, yaani uliopikwa tanuuni, kikaangoni au chunguni (2:4-10). Tofauti ya sadaka hii na ile ya kuteketezwa ni kwamba sadaka hii haikuteketezwa yote; masalia yake yalikuwa kwa ajili ya chakula cha makuhani. Baada ya hayo, Mungu anatoa maelekezo kwamba sadaka yoyote ya unga isiwekwe asali wala chachu (hamira), bali iwekwe chumvi (2:11-13). Mwisho, Mungu anatoa maelekezo ni kwa namna gani sadaka hii ya unga/nafaka itolewe kama kinachotolewa ni malimbuko, yaani sehemu ya kwanza ya mavuno mapya (2:14-16).[2]
Sadaka ya tatu ambayo waisraeli wote walitakiwa kutoa ni sadaka ya amani. Sadaka hii pia, Mungu aliruhusu kutolewa kwa namna moja kati ya namna mbili tofauti alizoziweka. Kwanza, mnyama mkubwa wa kufungwa kama ng’ombe angeweza kutolewa (3:1-5). Pili, mnyama mdogo wa kufungwa kama Kondoo (3:6-11) au mbuzi angeweza kutolewa (3:11-17). Tofauti kubwa kati ya sadaka hii na sadaka ya kuteketezwa ni mbili; kwanza, sadaka hii haikuteketezwa yote, sehemu iliyobaki ililiwa na mtoaji na kuhani. Pili, katika sadaka hii mnyama wa jinsia yeyote aliruhusiwa, wakati katika sadaka ya kuteketezwa mnyama dume tu ndio aliruhusiwa.[3]
Sadaka ya nne ambayo Waisraeli wote walitakiwa kutoa ni sadaka ya dhambi. Katika sadaka hii, Mungu anatoa maelekezo kuhusu jinsi ya kuitoa kulingana na kundi husika katika jamii. Kundi la kwanza ni kuhani mkuu (4:1–12). Kundi la pili ni Israeli wote kwa pamoja (4:13–21). Kundi la tatu ni mtawala au kiongozi wa watu (4:22–26). Kundi la nne linahusu kila mtu mmoja mmoja katika jamii ya Israeli. Wao walipaswa kutoa mbuzi jike (4:27–31) au kondoo jike (4:32–35), kulingana na uwezo wao.[4] Mwisho wa maelekezo kuhusu sadaka hii unafikiwa kwa kuelezea mambo mawili ya msingi. Moja, kutolewa kwa mifano minne ya dhambi ambazo zinahitaji kutolewa kwa sadaka hii (5:1-6). Pili, maelekezo ya mbadala wa vitu vinavyoweza kutolewa kama mtu hawezi kutoa mbuzi au kondoo (5:7-13).
Sadaka ya tano ambayo Waisraeli wote walitakiwa kutoa ni sadaka ya hatia (sadaka ya fidia). Hii ni sadaka iliyotakiwa kutolewa kama mtu amefanya dhambi ya kutokukusudia inayohusiana na kuasi mambo matakatifu ya Bwana (mambo haya ni kama vile zaka, sabato, malimbuko, au mali yeyote ya Hema la Kukutania). Mungu anatoa maelekezo ya nini kitolewe ikiwa mtu anajua kwamba kile alichokifanya ni dhambi (5:14–16), au hata kama hajui (5:17–19). Mwisho, Bwana anatoa maelekezo pia kuhusu utoaji wa sadaka hii pale ambapo dhambi iliyofanyika ilihusisha kumkosea mtu mwingine (6:1–7). Sadaka hii inatofautiana sana na sadaka nyingine; ni sadaka ambayo kondoo dume tu ndiye aliyetakiwa kutolewa. Ni sadaka pekee ambayo fidia pamoja na ongezeko la asilimia ishirini (sehemu ya tano) ya kile kilichoharibiwa ilitakiwa kutolewa.
Baada ya maelekezo hayo kuhusu sadaka kwa watu wote, Mungu anawageukia makuhani kuwapa maelekezo kuhusu namna ya kuhudumia katika utoaji wa sadaka hizo. Anaanza na kutoa maelekezo kuhusu sadaka ya kwanza, yaani sadaka ya kuteketezwa (6:8–13). Baada ya hapo, maelekezo kuhusu sadaka ya nafaka yanafuata (6:14–18). Kabla ya kuendelea na sadaka tatu zilizobaki, Mungu anatoa maelekezo kuhusu wao makuhani watoe nini kwenye sadaka ya nafaka (6:19–23). Baada ya maelekezo hayo, anaendelea na maelekezo ya namna gani wao watahudumia katika utoaji wa sadaka wa watu. Anaendelea na maelekezo kuhusu sadaka ya dhambi (6:24–30), sadaka ya hatia (7:1–10), na sadaka ya amani ikiwa kwa ajili ya shukrani (7:11–15) au kwa ajili ya nadhiri/hiari (7:16–21).
Baada ya maelekezo hayo kwa makuhani, Mungu anarejea kutoa maelekezo mawili ya mwisho kwa jamii yote ya Israeli. Kwanza, Bwana anatoa amri kwamba mafuta na damu ya wanyama visitumiwe na mtu yeyote katika Israeli. Hukumu ya kula vitu hivi ni kukatwa mbali na jamii ya watu wa Mungu (7:22-27). Pili, Bwana anatoa maelekezo ya sehemu ya sadaka ya amani ambayo inatakiwa kuwa ni chakula cha makuhani wote kwa ujumla (yaani, kidari) na ambayo ni kwa ajili ya kuhani aliyehusika katika sadaka ya mtu husika, yaani mguu wa nyuma wa kulia (7:28-36). Sehemu hii ya kwanza ya kitabu hiki inaisha kwa hitimisho (7:37-38).

Mchoro namba 1. Hema ya kukutania, mahali pekee ambapo sadaka zote zilitakiwa kutolewa kabla ya kujengwa kwa hekalu.
Sehemu ya pili ya kitabu hiki (8:1–10:20) inaelezea kuhusu kuwekwa wakfu kwa makuhani, kuanza kwa huduma ya makuhani, na kwa upande mwingine kushindwa kwa makuhani kutii maagizo ya Bwana. Mungu alikuwa tayari ametoa maelekezo ya namna makuhani wawekwe wakfu (Kutoka 28–29), lakini tendo hili lilicheleweshwa na Israeli kuangukia katika ibada ya sanamu (Kutoka 32). Baada ya kufanywa upya kwa Agano (Kutoka 34) na kujengwa kwa Hema ya Kukutania (Kutoka 35–40), ndipo tukio la kuwekwa wakfu kwa makuhani likafanyika.
Tukio linaanza na Musa kutii maagizo kutoka kwa Bwana ya kuwatwaa Haruni na wanawe na kuwakusanya mkutano wote wa Israeli (8:1–5). Baada ya hapo, Musa akamvalisha Haruni mavazi kama alivyoagizwa na Bwana (8:6–9), akampaka mafuta (8:10–12), na mwishowe akawavalisha wanawe (wana wa Haruni) kama Bwana alivyomwagiza (8:13). Baada ya hayo, Musa akiwa kama kuhani akatoa sadaka za aina tatu kwa ajili ya kuwekwa wakfu kwa Haruni na wanawe, kama Mungu alivyoagiza kabla ya tukio la ibada ya sanamu (Kutoka 29). Sadaka ya kwanza iliyotolewa ni sadaka ya dhambi (8:14–17). Sadaka ya pili ni sadaka ya kuteketezwa (8:18–21), na sadaka ya tatu ni sadaka maalumu ya kuwekwa wakfu, inayofanana na sadaka ya amani (8:22–30). Tukio hili la kuwekwa wakfu linafikia kilele kwa Haruni na wanawe kusisitizwa kwamba wakae mlangoni mwa Hema ya Kukutania mpaka siku saba zitakapofika mwisho (8:31–36).
Baada ya siku saba za kuwekwa wakfu, Haruni na wanawe sasa wako tayari kwa ajili ya kazi ya ukuhani. Kazi yao ya kwanza inaanza kwa maagizo ya Mungu kupitia Musa kuhusu sadaka gani ziletwe siku hiyo na kutolewa (9:1–7). Haruni alianza kutoa sadaka kwa ajili yake mwenyewe: akatoa sadaka ya dhambi (9:8–11) na sadaka ya kuteketezwa (9:12–14). Baada ya sadaka kwa ajili yake mwenyewe, Haruni akatoa sadaka kwa ajili ya mkutano wa Israeli: akatoa sadaka ya dhambi (9:15), sadaka ya kuteketezwa (9:16), sadaka ya unga/nafaka (9:17), na sadaka ya amani (9:18–21). Baada ya kutolewa kwa sadaka hizo, Mungu akashusha moto kuteketeza sadaka ya kuteketezwa kama uthibitisho kwamba sadaka imepokelewa (9:22–24).
Jambo la muhimu katika sura hizi mbili ni kurudiwa-rudiwa kwa maneno yanayoeleza kwamba kila kitu kilifanyika kama Bwana alivyoagiza (8:4, 5, 9, 13, 17, 21, 29, 34, 36; 9:6, 7, 10, 21). Kwa kuwa wana wa Haruni walifanya kazi ya ukuhani kwa namna ambayo hawakuagizwa na Bwana, wakafa (10:1–3). Musa akaagiza watoto wa Haruni waliokufa wachukuliwe kutoka katika hema ya kukutania na wana wa mjomba wa Haruni, nao wakafanya kama walivyoagizwa (10:4–5). Tena, Musa akawaagiza Haruni na wanawe wasihusike na mazishi, nao pia wakafanya kama walivyoagizwa (10:6–7).[5] Baada ya maagizo ya Musa kutekelezwa, Mungu anazungumza na Haruni moja kwa moja kwa mara ya kwanza na anampa maagizo makuu matatu: Kutokunywa kileo wakati wa utumishi wao, kupambanua kati ya mambo matakatifu na ya kawaida na mwisho kuwafundisha Israeli wote amri zake (10:8-11).
Baada ya maagizo ya Bwana, Musa anawakumbusha Haruni na wanae kula sehemu ya sadaka ambazo walitakiwa kula baada ya kutolewa, yaani sehemu ya sadaka ya unga (10:12-13) na sadaka ya amani (10:14-15).[6] Uzinduzi wa ukuhani unafikia mwisho kwa mazungumzo makali kati ya Musa na Haruni kuhusu kushindwa kwa makuhani kula sehemu yao ya dhabihu ya dhambi kama ilivyoagizwa (rejea Walawi 6:22–30); badala yake wakaichoma moto.[7] Haruni anakiri kukosea na kumpa Musa sababu kwamba, kutokana na kifo cha watoto wake, aliogopa kula nyama hii takatifu. Musa anakubaliana na maelezo yake (10:16–20).
Miongoni mwa maagizo ambayo Mungu alimpa Haruni moja kwa moja hapo nyuma, ilikuwa ni kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi. Sehemu ya tatu ya kitabu hiki (11:1–16:34) ina kusudi la kupambanua haya.
Mungu anaanza kwa kuwapambanulia Musa, Haruni na Israeli wote, wanyama ambao ni najisi na wanyama ambao ni safi kwa kuliwa. Katika kundi la kwanza: kundi la wanyama wanaotembea juu ya nchi, Mungu anataja sifa za wanyama watakaoliwa na anataja wanyama ambao hawataliwa kwa sababu wanakosa baadhi ya sifa alizozitaja (11:1–8). Katika kundi la pili: kundi la samaki, Mungu anataja sifa za samaki watakaoliwa na wale ambao hawataliwa (11:9–12). Kundi la tatu: kundi la ndege, Mungu anataja ndege ambao hawataliwa na hivyo kumaanisha kwamba ndege wengine wote wataliwa (11:13–19). Kundi la nne: kundi la wadudu warukao, Mungu anakataza kuliwa kabisa isipokuwa wadudu wachache aliowataja (11:20–23).
Baada ya hapo, Mungu anaeleza jinsi mtu anavyokuwa najisi kama akigusa mizoga ya wanyama waliotajwa hapo juu; na zaidi anaeleza namna ya kujitakasa kutokana na unajisi huo. Anafafanua jinsi mizoga ya wadudu warukao (11:24–25) na mizoga ya wanyama wanaotembea juu ya nchi inavyoleta unajisi (11:26–28). Katika muendelezo huo wa kueleza kwamba kugusa mizoga ya wanyama najisi kunaleta unajisi, Mungu anataja kundi jingine la wanyama—wanyama wanaotambaa—ambao pia ni najisi (11:29–30). Mizoga ya wanyama hawa pia ikiguswa inaleta unajisi kwa watu (11:31), na hata yenyewe ikiangukia kitu, kitu hicho kinakuwa najisi (11:32–38).
Si tu kwamba kugusa mzoga wa mnyama najisi kunamfanya mtu kuwa najisi, bali pia kugusa mzoga wa mnyama msafi kunaleta unajisi vilevile (11:39–40). Baada ya maelezo hayo marefu, Mungu anatoa muhtasari wa yote aliyoyasema (11:41–45), na anahitimisha kwa kuthibitisha kwamba haya yote aliyoyasema ndiyo sheria yake (11:46–47).
Baada ya kushughulika na unajisi unaohusiana na wanyama, Mungu anaendelea kuwaeleza Israeli kuhusu unajisi unaotokana na mwili wa mwanadamu yeye mwenyewe. Unajisi wa kwanza unaosababishwa na mwili ni unajisi wa mwanamke baada ya kujifungua. Mwanamke akijifungua anakuwa najisi kwa muda wa siku saba (hatakiwi kugusa kitu kitakatifu na hatakiwi kuguswa au atakaye mgusa anakuja najisi pia) na baada ya hapo anaingia kwenye siku thelathini na tatu za utakaso kama mtoto aliyezaa ni wa kiume (12:1-4). Kama mtoto aliyezaliwa ni wa kike, siku za unajisi na siku za utakaso za mwanamke zinakuwa mara mbili (12:5). Baada ya siku za utakaso kuisha, mwanamke alitakiwa kuleta sadaka mbili mbele ya hema ya kukutania: sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya dhambi, kulingana na kipato cha mwanamke husika (12:6-8).
Unajisi wa pili unaosababishwa na mwili ni unajisi unaotokana na magonjwa mbalimbali hatari ya ngozi.[8] Katika sehemu hii, Mungu anatoa kesi saba muhimu za uchunguzi wa magonjwa ya ngozi kwa Haruni na Musa ili waweze kupambanua kati ya mtu najisi na safi. Kesi ya kwanza: Mtu akiwa na kivimbe, kikoko, au kipaku king’aacho anatakiwa aende kwa kuhani akaguliwe. Ikiwa kivimbe, kikoko, au kipaku kina sifa ya kubadilisha nywele na kuzifanya nyeupe, na pia kinaingia ndani ya ngozi, basi huo ni ugonjwa unaomfanya mtu kuwa najisi. Lakini kama sifa hizo mbili hazipo, mtu huyo atawekwa karantini hadi siku kumi na nne. Endapo ndani ya siku kumi na nne hakutakuwa na mabadiliko, mtu huyo atahesabiwa safi. Hata hivyo, ikiwa katika siku hizo mabadiliko yakatokea, yaani ugonjwa ukaingia ndani ya ngozi, basi mtu huyu atakuwa najisi (13:1–8). Kesi ya pili: Mtu akiwa na ugonjwa wa ngozi unaoshukiwa kuwa najisi, apelekwe kwa kuhani kwa ajili ya kuangaliwa. Mtu huyu, kama atakuwa na sifa hizi tatu: kivimbe cheupe katika ngozi yake, nywele katika ngozi kugeuzwa kuwa nyeupe, na pia akiwa na vidonda (nyama mbichi), atakuwa najisi. Kama hana sifa hizi tatu, hata kama ugonjwa huo umeenea mwili mzima, yeye atahesabiwa safi. Lakini pia, akiwa na kidonda tu ni najisi, isipokuwa kidonda kikipona ndipo atakapohesabiwa safi tena (13:9-17).
Kesi ya tatu: Mtu akiwa na kivimbe cheupe, au kipaku king’aacho, cheupe lakini chekundu kidogo katika sehemu ambayo kulikuwa na jipu lililopona, anatakiwa kwenda kwa kuhani kwa ajili ya kuangaliwa. Ikiwa kivimbe hicho au kipaku kimeingia ndani ya ngozi na kubadilisha nywele katika ngozi kuwa nyeupe, basi mtu huyo ni najisi. Akikosa sifa hizo, atawekwa karantini kwa muda wa siku saba. Baada ya siku saba, kama kivimbe au kipaku kimeenea, basi mtu huyo ni najisi; lakini kama kimebaki pale pale bila kuenea, basi mtu huyo ni safi (13:18–23). Kesi ya nne: Ikiwa mtu ameungua katika ngozi yake na pale alipoungua pakawa na kipaku chekundu kidogo au cheupe, atakwenda kwa kuhani kuangaliwa. Kama kipaku kimeingia ndani ya ngozi na kubadilisha nywele katika ngozi kuwa nyeupe, basi mtu huyo ni najisi. Akikosa sifa hizo, atawekwa karantini kwa muda wa siku saba. Baada ya siku saba, kama kipaku kimeenea basi mtu huyo ni najisi; lakini kama kimebaki pale pale bila kuenea, basi mtu huyo ni safi (13:24–28).
Kesi ya tano: Mtu akiwa na kidonda kichwani au kwenye kidevu anatakiwa kwenda kwa kuhani kuangaliwa. Kama hicho kidonda kimeingia ndani na kimebadilisha nywele kuwa za njano na nyembamba, basi mtu huyo ni najisi. Kama kidonda hicho kinakosa hizo sifa, basi mtu huyo atawekwa karantini hadi siku kumi na nne. Kama hicho kidonda hakijaenea na wala hakijaingia ndani ya ngozi, basi mtu huyo ni safi. Lakini ikiwa kimeenea, basi mtu huyo ni najisi. Tena, ikiwa kidonda hicho hakijaenea na nywele nyeusi zimeota, basi mtu huyo ni safi (13:29-37). Kesi ya sita: Ikiwa mwanamke au mwanaume ana vidoti vyeupe kwenye ngozi, atangaliwa na kuhani. Ikiwa vidoti hivyo ni vyeupe kiasi, basi mtu huyo ni safi (13:38-39). Kesi ya saba: Mwanaume akiwa na upara kichwa kizima au kwenye upande wa mbele wa kichwa, huyo ni safi. Lakini ikiwa kwenye upara kuna kivimbe cheupe-chekundu, kuhani atamwangalia. Kama kivimbe kina sifa hiyo ya rangi, basi mtu huyo ni najisi (13:40-44).
Baada ya maelezo hayo marefu ya namna ya kutambua mtu safi na najisi, Bwana anaagiza kwamba mtu akiwa katika unajisi anatakiwa kuvaa nguo zilizolaluliwa (Kama mtu anayekuwa katika maombolezo) na kutengwa na jamii (13:45-46).
Kwa kuwa unajisi hauishii kwa watu tu, Bwana pia anaelekeza namna ya kutambua vazi safi na najisi. Ikiwa vazi linaonekana na mabaka au madoa ya kijani kibichi au mekundu, lazima lipelekwe kwa kuhani ili akague. Kuhani ataliweka vazi hilo karantini kwa siku saba, kisha kulikagua tena kuona kama mabaka hayo yameenea. Ikiwa madoa hayo yameenea, vazi linatangazwa kuwa najisi na lazima lichomwe. Ikiwa hayajaenea, vazi linaoshwa na kukaguliwa tena baada ya siku nyingine saba. Ikiwa vazi hilo baada ya siku kumi na nne halijapoteza rangi ile ya kijani au nyekundu, hata kama haijaenea, vazi hilo ni najisi na lazima lichomwe moto. Tena, kama doa limepungua, sehemu iliyoathirika inakatwa; lakini rangi ikijitokeza tena kwenye vazi lilokatwa, vazi lote lazima lichomwe moto. Lakini baada ya siku kumi na nne, kama lile doa limeondoka katika vazi, vazi litafuliwa tena na kuwa safi (13:47-59).
Baada ya kuelezea namna ya kumtambua mtu na vazi safi au najisi, Bwana anamueleza Musa peke yake kuhusu namna ya kutakaswa kwa mtu aliyepona ukoma. Mtu akipona ukoma, kuna hatua mbili mbele yake ili aweze kuwa safi na kurudi katika jamii (kumbuka, mtu mwenye ukoma alikuwa anatolewa kwenye jamii/kwenye kambi; rejea 13:45–46). Hatua ya kwanza: Kuhani atamuangalia mtu huyo akiwa nje ya kambi ya Waisraeli. Kama amepona, ataagiziwa ndege safi wawili, mti wa mwerezi, sufu nyekundu, na hisopo.[9] Ndege mmoja atachinjwa, na vitu vingine vitachovywa katika damu ya huyo ndege. Kisha atanyunyiziwa yule anayetakaswa mara saba. Baada ya hapo, mtu huyo ataoga na kuondoa nywele zote, na hivyo atakuwa safi na kuruhusiwa kuingia katika kambi ya Waisraeli, lakini hataingia nyumbani kwake kwa muda wa siku saba (14:1–9).
Siku saba zikiisha, mtu ataingia kwenye hatua ya pili ya utakaso. Katika hatua ya pili kuna namna mbili: moja ni kwa ajili ya watu wote, na ya pili ni kwa ajili ya maskini. Kwa watu wengine wote: Siku ya nane, mtu alitakiwa kuleta wana-kondoo wawili waume wakamilifu, na mwana-kondoo mmoja wa kike wa mwaka wa kwanza mkamilifu, pamoja na sehemu tatu za kumi za efa moja ya unga mwembamba na logi moja (takriban theluthi ya lita moja) ya mafuta kwa ajili ya kutakaswa kwake. Mwana-kondoo mume mmoja atakuwa kwa ajili ya sadaka ya hatia. Atachinjiwa ndani ya hema ya kukutania, na damu yake pamoja na mafuta yaliyoletwa yatatumika kwa ajili ya utakaso wake. Utakaso utafanyika hivi: damu ya mwana-kondoo huyu itatiwa katika ncha ya sikio la kuume, katika kidole gumba cha mkono wa kuume wa yule atakaswaye, na tena yale mafuta kuhani atamnyunyizia mara saba. Baadhi ya yale mafuta pia yatatiwa katika ncha ya sikio la kuume, katika kidole gumba cha mkono wa kuume, na mengine yaliyobaki atampaka kichwani. Wana-kondoo wawili waliobaki: mmoja utatumika kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na mwingine kwa sadaka ya kuteketezwa (14:10–20). Kwa maskini: Siku ya nane alitakwa kuleta kama watu wengine isipokuwa hua wawili, au makinda mawili ya njiwa waliletwa kama mbadala wa wana kondoo wawili. Utakaso wake ulifanyika kama wengine isipokuwa hua au makinda ndio walitumika kwa ajili ya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa (14:21-32).
Baada ya maelekezo hayo ya namna gani mtu mwenye ukoma atatakaswa, Bwana anaendelea kuelekeza ni kwa namna gani Musa na Haruni watatambua kati ya najisi na safi. Katika hatua hii, Mungu anawaelekeza Musa na Haruni namna ya kutambua unajisi katika nyumba, ambazo wataishi pale watakapokuwa wameingia kwenye nchi yao ya ahadi. Bwana anasema, nyumba ikiwa na ukungu, mwenye nyumba atamwita kuhani kuja kuangalia, akiwa ametoa vitu vyote nje. Kama ukungu huo wa nyumba uko kwenye ukuta na una rangi ya kijani au nyekundu, na unaonekana umeingia ndani ya ukuta, nyumba itafungwa kwa siku saba (14:33-38). Baada ya siku saba, kuhani atarudi tena kutazama. Kama ukungu huo umeenea kwenye kuta za nyumba, kuhani ataagiza mawe yaliyoathirika yatolewe na chokaa yote ya nyumba ikwanguliwe. Baada ya hapo, mawe mapya yawekwe pale palipotolewa mawe yaliyoathirika, na chokaa mpya ipakwe katika nyumba (14:39-42). Kama baada ya kufanya hivyo, ukungu ukarudi tena, basi nyumba hiyo ni najisi, na hivyo itabomolewa na vitu vyote vitatupwa nje ya mji (14:43-45). Katika kipindi cha kufungwa kwake, mtu yeyote atakayeingia ndani ya nyumba hiyo atakuwa najisi (14:46-47). Lakini ikiwa ukungu haukurudi baada ya mawe na chokaa kubadilishwa, basi nyumba hiyo ni safi (14:48). Nyumba hii nayo itafanyiwa utakaso, vile vile kama hatua ya kwanza ya utakaso wa mtu aliyepona ukoma (14:49-53). Mwisho, Mungu anatoa muhtasari, akisisitiza kwamba maelekezo haya ndio sheria ya ukoma (14:54-57).
Maelekezo haya yote tangu 13:1 mpaka 14:57 yalikuwa ni kuhusu unajisi unaosababishwa na magonjwa mbalimbali ya ngozi. Baada ya hapo, Mungu anaendelea kuwaelekeza Musa na Haruni kuhusu Unajisi wa tatu unaosababishwa na mwili wa mwanadamu wenyewe. Unajisi huu ni ule unaosababishwa na usaha. Mungu anasema, mtu yeyote atakapokuwa na usaha atakuwa najisi, na hivyo chochote atakachokigusa kitakuwa najisi, na yeyote atakayegusa vitu vyake atakuwa najisi kwa siku nzima (15:1-12). Mtu huyu, akipona usaha wake, atahesabu siku saba, na baada ya hapo atapeleka hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa kuhani, katika hema ya kukutania, kwa ajili ya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya upatanisho wake (15:13-15).
Unajisi wa nne unaosababishwa na mwili ni unajisi wa kutokwa na shahawa. Bwana anasema, mwanaume akitokwa na shahawa anakuwa najisi kwa siku moja na anatakiwa kuoga. Nguo zake zote na chochote kitakachoguswa na shahawa kitakuwa najisi. Zaidi, kama mwanamke ndiye sababu ya mwanaume kutokwa na shahawa, basi wote watakuwa najisi kwa siku moja na watatakiwa kuoga (15:16-18).
Unajisi wa tano unaosababishwa na mwili ni unajisi wa damu ya hedhi ya mwanamke. Bwana anasema, mwanamke akitokwa na damu ya hedhi atatengwa na atakuwa najisi kwa muda wa siku saba. Chochote atakacholalia na kukalia kitakuwa najisi, na yeyote atakayekigusa atakuwa najisi kwa siku moja. Na mwanaume atakayelala naye akiwa katika unajisi, atakuwa najisi kwa siku saba (15:19-24). Tena, kama mwanamke anatokwa na damu kwa muda wa siku nyingi kuliko ilivyo kawaida au anatokwa damu wakati usio wa majira yake ya kutokwa damu, basi ataendelea kuwa najisi muda wote damu inapomtoka (15:25-27). Na baada ya damu kuisha, mwanamke atatakiwa kuhesabu siku saba, na baada ya hapo, siku ya nane atapeleka hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa kuhani katika hema ya kukutania, kwa ajili ya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya upatanisho wake (15:28-30). Mwisho, Mungu anatoa muhtasari akionyesha kwamba kwa maelekezo hayo ndivyo watu watajijua kuwa ni najisi au safi, ili wasije wakaingia kwenye hema ya kukutania wakiwa katika unajisi (15:31-33).
| MAELEZO YA ZIADA |
| UNAJISI NI DHAMBI? Katika Walawi, kuwa najisi ni kuwa katika hali ya uchafu ambayo inamzuia mtu kuja karibu na uwepo wa Mungu, yaani kuja kwenda kwenye hema la kukutania. Kwa lugha nyepesi ni kuwa kwenye hali ambayo hauruhusiwi kushiriki katika ibada katika hema la kukutania na baadae katika Hekalu. Sababu ya unajisi ni pamoja na kugusa mabaki ya wanyama waliokufa (Walawi 11:24–28, 39–40), uzazi (Walawi 12:1–8), magonjwa ya ngozi (Walawi 13–14), na kutokwa na damu au maji ya mwili (Walawi 15:1–33). Hali hizi za uchafu mara nyingi ni za kawaida, zisizoweza kuepukika, na za muda; ili kutakasika zinahitaji mtu kuosha au kuoga, kusubiri hadi jioni, au kutoa sadaka au vyote kwa pamoja. Kuwa mchafu kwa namna hii sio kuwa mdhambi. Kwa maneno mengine, kuwa najisi sio kuwa na dhambi. Badala yake mtu alikuwa mdhambi kama angeamua kutokufuata maelekezo ya kujitakasa baada ya kuwa najisi au kwenda kwenye hema la kukutania wakati ukiwa katika hali ya unajisi. Pamoja na hilo, kula wanyama wasio safi ni tofauti: kula wanyama najisi kunafanya mtu kuwa najisi (Walawi 11:24–28, 39–40), na pia ni kinyume na agizo la Mungu la wazi (Walawi 11:43–45). Hivyo basi, kula wanyama hao kwa makusudi ni dhambi na kunamfanya mtu kuwa najisi. Kwa muhtasari, Kuwa najisi haina maana ya kutenda dhambi bali kutofuata maelekezo ya kujitaka au kwenda kwenye hema la kukutania katika kipindi hicho ndio dhambi. Lakini kula wanyama najisi kwa makusudi ni dhambi na kunamfanya mtu kuwa najisi. |
Sehemu ya tatu ya ujumbe huu inafikia kilele na kuanzishwa kwa siku maalumu sana katika taifa la Israeli: siku ya utakaso wa kuhani mkuu, utakaso wa taifa zima, na utakaso wa Hema ya Kukutania. Siku hii ni maarufu kwa jina la Sikukuu ya Upatanisho au Yom Kippur. Maelekezo ya Mungu kuhusu siku hii yako katika maeneo kadhaa. Moja, kazato la kuhani mkuu kuingia Patakatifu pa Patakatifu isipokuwa mara moja tu kwa mwaka: katika Sikukuu hii ya Upatanisho (16:1-2). Pili, maelekezo ya nini kuhani anatakiwa kuleta katika siku hii (mbuzi wawili, kondoo wawili na ng’ombe mmoja) na ni mavazi gani anatakiwa kuvaa katika siku hii (16:3-5). Tatu, kwa kuwa Haruni alitakiwa kuleta ng’ombe mmoja kwa ajili ya sadaka yake ya dhambi na mbuzi wawili kwa ajili ya sadaka ya dhambi ya taifa, Mungu anatoa maelekezo ya matumizi ya wanyama hawa wote watatu (16:6-10).
Baada ya maelekezo hayo ya utangulizi, Mungu anatoa maelekezo ya namna ya kufanya upatanisho katika siku hii. Upatanisho huu utafanyika katika hatua mbili. Katika hatua ya kwanza, Haruni atafanya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na familia yake kwa kuchinja ng’ombe kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Damu ya ng’ombe ataipeleka Patakatifu pa Patakatifu huku akiwa na chetezo chenye uvumba ili moshi husitiri kiti cha rehema, na kwa kutumia kidole atanyunyiza damu hiyo mara saba kwenye kiti cha rehema (16:11-14).
Hatua ya pili, ambayo ni hatua ya utakaso wa watu wa Israeli na utakaso wa Hema ya Kukutania, pia imegawanyika katika hatua nyingine mbili. Hatua ya kwanza, Haruni atachinja mbuzi na kuipeleka damu yake Patakatifu pa Patakatifu kama alivyofanya kwa ajili ya upatanisho wake. Baada ya hapo, atatoka Patakatifu pa Patakatifu na kurudi sehemu ya Patakatifu. Hapo, atachukua damu ya mbuzi na ng’ombe, ataipaka kwenye pembe zote za madhabahu, na kisha atanyunyiza baadhi ya damu katika madhabahu hiyo mara saba (16:15-19). Katika hatua ya pili, Haruni ataweka mikono yake juu ya yule mbuzi aliye hai na ataungama dhambi zote za wana wa Israeli, ndipo yule mbuzi atachukuliwa mpaka jangwani na mtu aliyekuwa ameandaliwa. Kupelekwa jangwani kwa mbuzi huyu ni ishara kwamba dhambi zote zimeondolewa katika jamii ya israeli (16:20-22).
Baada ya hatua hizi, Mungu anatoa maelekezo ya kuhitimisha tukio hili muhimu. Katika hitimisho, Haruni atarudi kwenye hema la kukutania na kuvua mavazi aliyoingia nayo katika patakatifu pa patakatifu, na pia ataosha mwili wake. Baada ya hapo atakwenda nje kwenye madhabahu ya kuteketezea na atatoa sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yake na kwa ajili ya watu wa Israeli (kondoo waume ndio watatekekezwa). Kwa upande mwingine, yule aliyemchukua yule mbuzi mpaka jangwani ataosha nguo zake na mwili wake kabla hajarejea kwenye kambi ya watu. Pia, ng’ombe na mbuzi wa sadaka ya dhambi watachukuliwa na kuchomwa nje ya kambi ya watu, na atakayefanya hivyo atafua nguo zake na kuoga kabla ya kurudi kwenye kambi ya Waisraeli (16:23-28). Baada ya maelekezo yote haya kuisha, Mungu sasa anatangaza kurasimisha tukio hili; tukio lifanyike katika mwezi wa saba, siku ya kumi ya mwezi, milele na milele (16:29-34).
Sehemu ya nne ya kitabu hiki (16:1–26:46) ina maelekezo ya namna gani Israeli wanatakiwa kuishi maisha ya utakatifu kwa vitendo. Maelekezo ya kwanza kabisa ni maelekezo kuhusu kuchinja na umwagaji wa damu wa wanyama. Baada ya utangulizi wa hotuba hii (17:1–2), Mungu anaweka sheria tano muhimu kuhusu jambo hili. Sheria ya kwanza inaamuru kwamba wanyama wafugwao wenye miguu minne wanaoruhusiwa kuliwa lazima wachinjwe mlangoni mwa hema la kukutania (17:3–7). Sheria ya pili inakataza Waisraeli na wageni wakaao nao wasitoe dhabihu kwa miungu mingine (17:8–9). Sheria ya tatu inaweka marufuku ya moja kwa moja dhidi ya kula damu, kwa Waisraeli na wageni wote (17:10–12). Sheria ya nne inaamuru kwamba damu ya wanyama wa porini waliouawa na Mwisraeli au mgeni lazima izikwe (17:13–14), na sheria ya tano inasema kwamba Mwisraeli au mgeni atakayekula mnyama aliyekufa mwenyewe lazima ajitakase (17:15–16).
Melekezo ya pili ni maelekezo yahusuyo mahusiano ya kimapenzi. Baada ya utangulizi wa kuwasisitiza Israeli kutokuishi kwa kuiga maisha ya Misri walikotoka wala Kaanani wanakoelekea, bali waishi kwa kufuata sheria za Bwana (18:1-5), Bwana anaweka katazo la mahusiano ya kimapenzi baina ya ndugu wa karibu (18:6-18). Mbali na mapenzi kati ya ndugu wa karibu, Bwana anaweka katazo la: mwanaume kufanya la mapenzi na mwanamke kipindi cha hedhi, kutoa watoto kwa Moleki, kufanya mapenzi na mke wa mtu, mapenzi ya jinsia moja, na mapenzi na wanyama (18:19-23). Mwisho, Bwana anawasisitiza kuishi kwa kufuata maagizo yake na si kuiga maisha ya mataifa, huku akiwaonyesha hatari ya kukiuka amri zake (18:24-30).
Maelekezo ya tatu ni maelekezo yanayohusu sheria mbalimbali zinazotakiwa kufuatwa kwenye maisha ya kila siku. Katika sehemu hii, Mungu anaanza na mwito wa kuwaita Waisraeli kuwa watakatifu kama yeye alivyo (19:1-2). Kuwa mtakatifu ni mtu kufanya kwa usahihi wajibu wake wa kiimani (19:3-8), kuishi kwa usahihi na majirani (19:9-18), na kufuata maelekezo ya Mungu kuhusiana na kilimo, ufugaji, chakula, mavazi, mazishi na kuwatunza wajakazi na watoto wa kike (19:19-29). Kwa namna nyingine, Mungu anasisitiza wajibu wa mtu wa kiimani (19:30-31), anasisitiza kuishi kwa usahihi na majirani (19:32-35), na mwisho anasisitiza kushika sheria hizi (19:36).[10]
Maelekezo ya nne ni maelekezo yanayohusu adhabu za wale watakaokwenda kinyume na sheria za Mungu. Baada ya utangulizi (20:1-2a), Mungu anasema: mtu yeyote atakayefanya ibada kwa miungu mingine atauawa, na atakayewaendea wachawi na wenye pepo atatengwa na jamii ya Israeli(20:2b-6).[11] Kabla ya kuendelea na maelekezo mengine, Mungu anawasisitiza Israeli kuishi kwa kufuata sheria zake (20:7-8). Baada ya msisitizo huo, Mungu anaendelea kusema: mtu yeyote atakayekuwa na mahusiano ya kimapenzi ambayo Mungu ameyakataza atauawa (20:7-21). Baada ya msisitizo mwingine kwa Israeli, akiwataka waishi kwa kufuata sheria zake watakapoingia nchi ya ahadi (20:22-26), Mungu anamalizia kwa kuagiza kuuawa kwa mtu ambaye ni njia ya kuwasiliana na wafu au anayetoa usaidizi wa kuwasiliana nao (20:27).[12]
Maelekezo ya tano ni maelekezo yanayowahusu makuhani. Kwanza, Bwana anaagiza wasiguse maiti za ndugu zao, isipokuwa ndugu wa karibu kabisa (21:1-6). Pili, wasioe kahaba, wala mjane, na hata wasiwe na binti anayeishi katika ukahaba (21:7-9). Kwa makuhani, Mungu aliruhusu kugusa miili ya ndugu zao wa karibu, lakini Kuhani Mkuu Bwana alimzuia kugusa maiti ya mtu yeyote, hata ya mama au baba yake (21:10-12). Zaidi ya hayo, Kuhani Mkuu alitakiwa kuoa bikira tu kutoka katika ndugu zake (21:13-15). Tatu, Mungu anaagiza kwamba, kuhani yeyote mwenye kilema mwilini hataruhusiwa kukaribia madhabahu na kutoa sadaka; yaani hataruhusiwa kufanya huduma za kikuhani. Hata hivyo, pamoja na katazo hilo, kuhani huyo alipewa ruhusa ya kula kila stahiki za kikuhani zinazotokana na sadaka za watu (21:16-24).
Jambo la nne Mungu analoagiza kwa makuhani ni kuhusu kula vyakula vilivyotolewa kama sadaka na wana wa Israeli. Bwana anaagiza kwamba kuhani yeyote aliye katika hali ya unajisi haruhusiwi kula vyakula hivi vitakatifu mpaka amejitakasa kwa kuoga na kwa kusubiri jua kuzama (22:1-9). Si hivyo tu, lakini pia anayestahiri kula vyakula hivi ni watu wa familia ya kuhani tu na si vinginevyo: mgeni, mwajiriwa na hata mtoto wa kike wa kuhani aliyeolewa haruhusiwi kula vyakula hivi vitakatifu (22:10-16). Katika kumalizia maelekezo kwa makuhani, Mungu anawasisitiza kwamba kama ambavyo kuhani mwenye kilema haruhusiwi kufanya huduma ya kikuhani ndivyo hivyo hivyo sadaka yenye kilema hairuhusiwi kutolewa (22:17-25). Mbali na kutokuwa na kilema, sadaka isiwe ya mnyama mwenye umri chini ya siku saba, na zaidi mnyama na mama yake wasitolewe sadaka siku moja (22:26-33).
Maelekezo ya sita ni maelekezo yanayohusu sikukuu ambazo Waisraeli walitakiwa kuzitunza na kufanya kusanyiko. Katika kila sikukuu, Mungu anaelekeza ifanyike katika siku gani na anaagiza Waisraeli wafanye nini katika sikukuu husika. Baada ya utangulizi (23:1-2) na baada ya kutaja sikukuu ya kila wiki (23:3), Bwana anataja sikukuu saba ambazo Israeli walitakiwa kuzitunza. Sikukuu ya kwanza ni sikukuu ya Pasaka, ambayo iliambatana na sikukuu ya pili, yaani sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu (23:4-8). Sikukuu ya tatu ni sikukuu ya Mavuno ya Kwanza (23:9-14). Sikukuu ya nne ni sikukuu ya Majuma (23:15-22). Sikukuu ya tano ni sikukuu ya Baragumu (23:23-25). Sikukuu ya sita ni sikukuu ya Upatanisho, na sikukuu ya mwisho ni sikukuu ya Vibanda (23:33-44).
| MAELEZO YA ZIADA | ||
| Sikukuu | Kalenda ya Kiyahudi | Tarehe Kulingana na Biblia ya Kiswahili |
| Pasaka | 14 Nisan | Siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza |
| Mikate Isiyotiwa Chachu | 15–21 Nisan | Kuanzia siku ya kumi na tano hadi ishirini na moja ya mwezi wa kwanza |
| Sadaka ya Malimbuko | 16 Nisan | Siku ya kumi na sita ya mwezi wa kwanza |
| Pentekoste | 6 Sivan | Siku ya hamsini baada ya sabato ya Pasaka |
| Baragumu | 1 Tishri | Siku ya kwanza ya mwezi wa saba |
| Upatanisho | 10 Tishri | Siku ya kumi ya mwezi wa saba |
| Vibanda | 15–21 Tishri | Kuanzia siku ya kumi na tano hadi ishirini na moja ya mwezi wa saba |
Maelekezo ya saba ni maelekezo kuhusiana na kinara cha taa na mikate ya wonyesho katika hema la kukutania. Kuhusiana na kinara cha taa, Mungu anaagiza kwamba kiwekewe mafuta safi ya mzeituni ili kiweze kuwaka kila siku milele na milele (24:1-4). Kuhusu mikate ya mwonyesho Mungu anaagiza kwamba, mikate kumi na miwili ipikwe na ipangwe kwenye meza yake iliyopo mahali patakatifu pa hema la kukutania na ibadilishwe kila sabato. Mikate inayotolewa, Bwana anaagiza iliwe na makuhani (24:5-9).

Mchoro namba 2. Kinara cha taa kilichokuwa kinakaa kwenye mahali pa takatifu pa hema la kukutania.
Maelekezo ya nane ni maelekezo ya kipekee katika kitabu hiki. Haya ni maelekezo yaliyoambatana na simulizi ya tukio lililotokea katikati ya jamii ya Waisraeli. Simulizi hii inahusu kugombana kwa Mwisraeli mwenye baba Mmisri na Mwisraeli mwenye wazazi wote Waisraeli. Baada ya Mwisraeli mwenye baba Mmisri kulaani na kukufuru jina la Bwana, Waisraeli wakamfunga ili kusubiri maelekezo kutoka kwa Bwana (24:10-11). Bwana akaagiza mtu huyo auwawe na kuelekeza kwamba kila kosa la kuumiza mtu mwingine linastahili ujira unaofanana na kosa husika, yaani, kama mtu ameua anastahili kuuawa (24:12-22). Baada ya maelekezo hayo, wana wa Israeli wakatii maelekezo ya Bwana (24:23).
Maelekezo ya tisa ni maelekezo yanayohusu Sabato ya ardhi na mwaka wa Yubile. Kuhusu Sabato ya ardhi, Bwana alitoa maelekezo kwa Musa kwamba kila baada ya miaka sita ardhi itapumzika, yaani katika mwaka wa saba Waisraeli hawakutakiwa kulima, kuvuna, wala kufanya shughuli zozote za kutunza mazao yao. Zaidi, Bwana alikataza hata kuvuna kile kilichojiotea chenyewe, pamoja na kuruhusu mazao hayo kuliwa kama chakula na watu wote pamoja na wanyama (25:1-7).
Kuhusiana na mwaka wa Yubile, Mungu aliagiza kwamba kila baada ya sabato saba za ardhi, mwaka unaofuata uwe mwaka wa Yubile. Katika mwaka huo, kwenye Sikukuu ya Upatanisho baragumu itapigwa, na kuanzia hapo watumwa wote watatangaziwa uhuru, na wale waliouza mali zao (ardhi) kwa sababu ya umaskini watarudishiwa. Tena, sheria zote za kilimo zilizowekwa na Mungu kwenye mwaka wa Sabato ya ardhi zilitakiwa kutekelezwa katika mwaka huu wa Yubile (25:8-13). Kwa kuwa ardhi iliyouzwa ilitakiwa kurudishwa katika mwaka huu wa Yubile, Mungu alitoa maelekezo kuhusu bei za ardhi ili mtu mmoja asimuonee mwingine. Bwana alisema bei ya ardhi itaamuliwa na muda uliobaki kutoka wakati wa kununua mpaka mwaka wa Yubile. Kama muda ulikuwa mrefu basi bei ingekuwa juu, na kama muda ulikuwa mfupi basi bei ingekuwa ndogo (25:14-17).
Kwa kuwa Mungu anajua watu wana wasiwasi na namna watakavyoishi ikiwa mwaka mzima hawatalima wala kuvuna, Mungu anawahakikishia kwamba kama watafuata maelekezo yake, katika mwaka wa sita atawapa mazao kiasi ambacho kitawatosha mpaka mwaka wa tisa (25:18-22). Tena, kuhusu ardhi, Mungu anasema ardhi haitauzwa kabisa kabisa kwa kuwa ni mali yake yeye. Ikiwa mtu ameingia kwenye umaskini na akauza ardhi yake, basi ndugu yake anatakiwa kuikomboa (kuilipia gharama ili irudi kwa mmiliki) au mtu yule aliyeuza ataikomboa kama atatajirika baadaye. Ikishindikana kukombolewa wakati huu, basi ardhi hiyo itakombolewa katika mwaka wa Yubile (25:23-28). Tofauti na ardhi, nyumba iliyo ndani ya wigo ikiuzwa kutakuwa na muda wa mwaka mmoja tu wa kuikomboa. Mwaka ukipita haitaweza kukombolewa tena. Lakini nyumba ambayo haiko ndani ya wigo itakombolewa tu kama ardhi. Zaidi, nyumba au ardhi za Walawi zote zitakombolewa wakati wowote (25:29-34).
Kwa kuwa Waisraeli wote wana thamani mbele za Mungu, Mungu anaagiza kwamba mtu akiwa maskini asitumike kuwapa faida wengine (25:35-38), wala asifanywe kuwa mtumwa bali awe tu mfanyakazi wa kuajiriwa, na katika mwaka wa Yubile aachwe huru (25:39-43). Kwa kuwa Waisraeli hawakuruhusiwa kuwafanya Waisraeli wenzao kuwa watumwa, Mungu aliwaruhusu kuwa na watumwa kutoka nje ya Israeli (25:44-46). Kwa upande mwingine, Mungu aliwapa Waisraeli wajibu wa kuwakomboa ndugu zao waliyoangukia katika umaskini na kujiuza kwa mtu ambaye si Mwisraeli (25:47-52). Zaidi ya kumkomboa mtu, Mungu pia anaagiza Waisraeli wahakikishe ndugu zao ambao ni watumwa kwa wageni hawatumikishwi kwa nguvu bali wanakuwa kama waajiriwa. Haya yote Mungu aliagiza kwa kuwa Israeli ni watumishi wake aliowakomboa toka utumwani Misri (25:53-55).
Maelekezo ya kumi ni maelekezo yanayohusu ahadi za baraka na laana zitakazotokana na uchaguzi wa Israeli katika kumtii au kutokumtii maagizo haya yaMungu. Mungu anaanza kwa kuwaita Israeli kuishi kwa kumfuata yeye na sheria zake (26:1-2). Baada ya mwito huo, Mungu anataja aina tano za baraka zitakazoambatana nao iwapo watakubali kumtii. Baraka hizo ni: mafanikio katika kilimo, amani katika nchi, ushindi wa kivita juu ya maadui, uzazi bora, na uwepo wake katikati yao (26:3-13).
Lakini kama Israeli watakataa kumtii, Mungu anawajulisha laana zitakazowafuata: ambazo ni kinyume cha zile baraka. Laana hizi zitakuja hatua kwa hatua. Katika hatua ya kwanza, Mungu anaahidi hofu kubwa, magonjwa yanayoharibu mwili, kukosa kula mazao ya kilimo chao na kupigwa na kutawaliwa na maadui zao (26:14-17).Kama baada ya hayo hawatasikia, Mungu anaahidi laana zenye mapigo mara saba zaidi kama hatua ya pili ya laana (26:18-20). Wasiposikia, hatua ya tatu itafuata, ambayo inahusisha watu kuliwa na wanyama wakali ili idadi yao ipungue (26:21-22). Kutoendelea kutii kukiendelea, basi hatua ya nne itafuata; hatua hii inahusisha kufa vitani na pia uwepo wa njaa (26:23-26). Hatua ya tano itakuwa ni ya hatari zaidi iwapo kutokutii kutaendelea pamoja na hatua zote zilizopita. Hatua hii itahusisha njaa kali kiasi kwamba Waisraeli wataanza kulana wao wenyewe. Mwisho wa hatua hii utakuwa ni Israeli kupelekwa utumwani (26:27-33).
Matokeo ya Israeli kwenda utumwani yatakuwa ni kupumzika kwa ardhi (26:34-35), pamoja na kuendelea kwa mateso kwa wale wachache watakaobaki katika nchi yao (26:36-39). Mateso haya yatawapelekea kukubali uovu wao, na wakinyenyekeza, Mungu anaahidi kuwasamehe (26:40-42). Hata wale waliokwenda utumwani kabisa, Mungu anaahidi kwamba hukumu hii haitakuwa kauli yake ya mwisho, bali mwisho wake atalikumbuka agano lake na Yakobo, na hivyo atawasamehe Israeli uovu wao na kuwaondolea laana zote (26:43-46).
Ujumbe wa kitabu hiki unafikia mwisho kwa sehemu ya tano (27:1-34), sehemu ambayo ina maagizo ya Mungu kwa Waisraeli kuhusu nadhiri, kuweka wakfu na Zaka. Kama mtu ataamua kuweka nadhiri (ni hiari) ya kujitoa yeye mwenyewe au mtu mwingine kwa ajili ya kazi ya Mungu kwenye Hema la Kukutania, basi mtu huyo ataiondoa nadhiri hiyo kwa kutoa fedha kama mbadala: kiasi cha fedha za kutolewa kikiwa tofauti tofauti kulingana na umri na jinsia ya mtu huyo (27:1-8).[13] Kama nadhiri inahusisha mnyama na siyo mtu, na tena mnyama ambaye kwa kawaida angeruhusiwa kutolewa kama sadaka mbele za Bwana, basi mnyama huyo atakuwa mtakatifu na hatatafutiwa mbadala (yaani, mnyama husika aliyewekewa nadhiri atatolewa). Lakini ikiwa mnyama wa nadhiri ni mnyama ambaye kwa kawaida asingeruhusiwa kutolewa kama sadaka, basi kuhani atafanya tathmini na kuamua kiasi cha fedha cha kutoa badala ya mnyama huyo. Kiasi hicho kitakuwa ni cha mtu mwingine tofauti na yule aliyetoa; na kama aliyetoa mwenyewe atataka kumkomboa, basi ataongeza asilimia ishirini ya thamani iliyoamuliwa na kuhani (27:9-13).
Ukiacha nadhiri, mtu akiamua kuiweka wakfu nyumba yake (kuitoa kwa ajili ya matumizi maalumu na siyo ya kawaida), basi kuhani ataamua thamani ya nyumba hiyo, na kama aliyeitoa atataka kuikomboa ataongeza asilimia ishirini ya thamani yake (27:14-15). Kama mtu ameamua kuweka wakfu ardhi ambayo ni urithi wake, basi thamani ya ardhi hiyo itaamuliwa kwa mambo mawili: Kwanza, kiasi cha mbegu zitazotumika kulipanda shamba hilo; kwa kila kilo ishirini za mbegu za shayiri thamani yake itakuwa shekeli hamsini za fedha. Pili, idadi ya miaka iliyosalia mpaka mwaka wa Yubile (27:16-21). Lakini kama mtu ameweka wakfu shamba ambalo si mali yake ya urithi (yaani, shamba alilonunua), basi kuhani ataamua thamani yake kulingana na miaka iliyosalia mpaka mwaka wa Yubile; na baada ya Yubile shamba litarudi kwa mmiliki wa asili (27:22-25).
Kwa sababu wazaliwa wa kwanza (wanyama na binadamu) tayari ni mali ya Bwana, hawa hawawezi kuwekwa wakfu tena, isipokuwa mzaliwa wa kwanza wa mnyama asiye safi, huyo atakombolewa (27:26-27). Pamoja na taratibu hizo za nadhiri na kuweka wakfu, vile vilivyowekwa wakfu moja kwa moja havitakombolewa wala kuuzwa, bali vitakuwa vya Bwana moja kwa moja (27:28-29).[14] Mwisho kabisa, Bwana anaagiza zaka ya mazao itolewe, na kama mtu anataka kubaki na mazao yake, basi atatoa fedha yenye thamani ya zaka hiyo huku akiongeza asilimia ishirini ya thamani hiyo. Kwa wanyama, Bwana anaagiza mnyama yeyote atakayehesabiwa kuwa wa kumi na mchungaji atatolewa kama zaka bila kubadilishwa. Na haya yote ndiyo maagizo ya Bwana aliyomwagiza Musa kwa ajili ya Waisraeli huko Sinai (27:30-34).
FOOTNOTES
[1] Lengo la sadaka hii ilikuwa ni upatanisho kati ya Mungu na yule aliyetoa. Upatanisho huu haukuwa kwa sababu ya mtu kufanya dhambi fulani mahususi, bali ilikuwa ni kwa sababu ya hali ya jumla ya dhambi ya mwanadamu na hitaji la kudumisha ushirika sahihi na Mungu katika maisha ya kila siku. Sadaka hii ilionyesha moyo wa kujisalimisha kikamilifu ndio maana mnyama mzima aliteketezwa.
[2] Lengo la sadaka hii ilikuwa ni kutangaza shukrani kwa Mungu, kujitoa kwa atoaye sadaka na kutambua utoaji wa Mungu wa mahitaji hasa chakula kwa watu wake.
[3] Sadaka hii ingeweza kutolewa katika mazingira ya aina tatu. Ingeweza kutolewa kama shukrani (Walawi 7:11-12), au kutimiza nadhiri maalum (Walawi 7:16), au kama sadaka ya hiari (Walawi 7:16).
[4] Lengo la sadaka hii lilikuwa ni upatanisho kati ya Mungu na mtu aliyetenda dhambi maalum (au taifa lilipotenda dhambi fulani). Sadaka hii ilitolewa baada ya mtu kutenda dhambi bila kukusudia. Tofauti na sadaka ya kuteketezwa, iliyotolewa kwa ajili ya dhambi kwa ujumla, sadaka hii ilitolewa kwa ajili ya dhambi maalum ambayo mtu aliitambua.
[5] Kutokuhusika kwenye mazishi kwa kuhani mkuu ilikuwa ni maagizo yatakayotolewa hapo mbele na Mungu (Walawi 21:10-12).
[6] Kumbuka kuwa hizo sadaka mbili zilitolewa kwa ajili ya watu katika sura ya tisa, na hivyo zilitakiwa kuliwa na Haruni na wanae. Mungu aliagiza makuhani wajipatie chakula katika sadaka hizo (sadaka ya unga, rejea Walawi 6:14–16, na sadaka ya amani, rejea Walawi 7:30–36), ndiyo maana Musa anawakumbusha Haruni na wanae kufanya hivyo.
[7] Sadaka ya dhambi ilitakiwa kuliwa na makuhani ikiwa damu yake haikupelekwa ndani ya hema la kukutania (Walawi 6:24–30; hasa mistari ya 26, 29). Lakini kama damu ya sadaka hii ilipelekwa ndani ya hema la kukutania, haikutakiwa kuliwa bali ilipaswa kuchomwa nje kabisa ya marago/kambi ya waisraeli (Walawi 4:12, 21; 6:30).
[8] “Neno Ukoma, linalotumika na tafsiri nyingi, si sahihi sana, kwani ugonjwa tunaoujua leo kama ukoma haujatajwa katika maandiko haya kama mojawapo ya magonjwa ya ngozi yanayochukuliwa kuwa ni najisi. Tena, neno ukoma limetumika hata kwenye mabaka ya kwenye nguo na ukungu wa nyumba, hivyo ukoma unaoelezwa katika sura hii na zijazo sio ugonjwa tunaoujua leo.
[9] Hisopo ni mmea mdogo wenye majani na matawi madogo.
[10] Katika sura hii ya 19, sheria kumi za Mungu zimerudiwa, zimefafanuliwa na kugusiwa.
[11] Uzinzi unaotajwa hapa ni lugha ya picha inayomaanisha kutoka nje ya Agano kwa kuabudu miungu mingine. Biblia imekuwa ikiiita ibada kwa miungu mingine uzinzi au uasherati katika maeneo mengi, yakiwemo Kutoka 34:15-16 na Waamuzi 2:17.
[12] Kuna mfanano mkubwa kati ya sura ya 18 na sura ya 20 ya kitabu hiki. Sura ya 18 ina mwelekeo wa kukataza, wakati sura ya 20 ina mwelekeo wa kueleza adhabu kwa wale watakaoishi kinyume na yale ambayo Mungu ameyakataza katika sura ya 18.
[13] Kwa kuwa watumishi katika Hema la Kukutania walitakiwa kuwa watu wa kabila la Lawi peke yake, hivyo kama mtu mwingine akiamua kujitoa kwa ajili ya kazi katika Hema la Kukutania, ilibidi kuwe na njia mbadala ya kutimiza nadhiri yake. Hivyo Mungu akawapa Waisraeli kiwango cha fedha walichotakiwa kutoa kama njia ya kutimiza nadhiri yao ya kujitoa kwa ajili ya kutumika katika Hema la Kukutania
[14] Pamoja na kwamba katika lugha ya Kiswahili hakuna tofauti ya maneno kati ya kuweka wakfu kunakozungumziwa katika mistari ya 14-27 na kule kunakozungumziwa katika mistari ya 28-29, katika lugha ya Kiebrania wakfu hizi ziko tofauti. Wakfu za kuanzia mistari ya 14-27 zina uwezekano wa kukombolewa na kurudishwa, lakini wakfu ya mistari ya 28-29 ni mali ya Bwana moja kwa moja; hakuna nafasi ya ukombozi au uuzaji.
Unakuja hivi karibuni……

