MWONGOZO WA KUSOMA INJILI YA MATHAYO MTAKATIFU.
MAELEKEZO
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe, mwamini mwenzangu, unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako; usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa kila mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa mambo yanayoweza kukuongoza kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayotajwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno, tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo. Utaona maelekezo ya ziada yatakayokusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba hiyo.
e. Mpangilio wa mwongozo huu si mpangilio wa mwandishi. Mpangilio wa mwongozo unakusaidia tu kuona mabadiliko ya mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huu wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI
Kitabu cha Injili ya Mathayo kimekubaliwa na Kanisa tangu karne ya pili kuwa kiliandikwa na Mtume Mathayo, ingawa mwandishi mwenyewe hajatoa taarifa yoyote ndani ya kitabu hiki inayoonyesha moja kwa moja kuwa yeye ndiye mwandishi.
Ni kitabu muhimu sana kinachounganisha ujumbe wa vitabu vya Agano la Kale na utimilifu wa jumbe zake katika maisha ya Yesu. Wapokeaji wa awali wa kitabu hiki walikuwa waamini wa Kiyahudi[1] ambao hatujui kwa hakika walikuwa wanaishi eneo gani la Kijografia.
Upekee wa Injili ya Mathayo, ukilinganisha na Injili nyingine, unajidhihirisha katika msisitizo wake juu ya utimilifu wa Maandiko ya Kiyahudi (Agano la kale) kwenye maisha ya Yesu na mpangilio mzuri wa mafundisho yake.
KUSUDI LA KITABU
Mwandishi hajasema moja kwa moja kwa nini aliandika kitabu hiki, lakini kwa kusoma vizuri jumbe zake kuu ukilinganisha na vitabu vingine vya Injili, inaonyesha wazi kuwa Mathayo aliandika kitabu hiki kwa lengo la kuwasaidia waamini wa Kiyahudi kuelewa imani yao mpya. Alionyesha kwamba imani hii ni mwendelezo wa imani ya mababa zao, yaani maisha ya Yesu waliyemwamini ni utimilifu wa Maandiko Matakatifu (Mathayo 1:22; 2:15, 17, 23; 4:14; 8:17; 12:17; 13:35; 21:4; 27:9), na mwanzo wa kutimizwa kwa tumaini la Israeli (Mathayo 1:1, 2:6).
Kwa kuwa Wayahudi walikuwa wakisubiri ujio wa Masihi, Mathayo anaonyesha kwamba Yesu ndiye Masihi aliyefanikisha matakwa ya kimaandiko yahusuyo Umasihi (Mathayo 1:22-23, 2:15, 21:4-5). Pamoja na kuwa yeye ni Masihi, hakuja kama mfalme anayekuja kutumikiwa bali kama mtumwa, ili aweze kutolewa kwa ajili ya faida ya wengi (Mathayo 20:28), wakiwemo watu wa mataifa (Mathayo 8:11, 28:19-20).
MPANGILIO WA KITABU
Namba | Maandiko | Maelezo |
1 | 1:1-4:11 | Utangulizi wa Yesu |
A | 1:1-17 | Yesu katika Historia ya Israeli |
B | 1:18-2:23 | Kuzaliwa na Utoto wa Yesu |
C | 3:1-3:17 | Kubatizwa kwa Yesu |
D | 4:1-4:11 | Kujaribiwa kwa Yesu |
2 | 4:12-16:20 | Huduma ya Yesu Galilaya |
A | 4:12-4:17 | Mwanzo wa Huduma ya Yesu Galilaya |
B | 4:18-4:22 | Kuitwa kwa Wanafunzi |
C | 4:23-4:25 | Muhtasari wa Huduma ya Yesu |
D | 5:1-7:29 | Mafundisho ya Yesu (Semina ya Mlimani) |
E | 8:1-9:38 | Uponyaji na miujiza ya Yesu |
F | 10:1-11:1 | Kutumwa kwa wanafunzi (Semina ya kimisheni) |
G | 11:2-11:19 | Mwitikio wa Yohana mbatizaji |
H | 11:20-11:30 | Mwitikio wa miji ya Korazini na Bethsaida |
I | 12:1-12:50 | Mwitikio wa Mafarisayo |
J | 13:1-13:53 | Mafundisho ya Yesu kando ya Bahari (Semina kwa Mifano) |
K | 13:53-13:58 | Mwitikio wa watu wa mji wa nyumbani wa Yesu |
L | 14:1-14:13 | Mwitikio wa Herode |
M | 14:14-14:36 | Miujiza ya Yesu na Uponyaji |
N | 15:1-16:12 | Upinzani wa Mafarisayo dhidi ya mwitikio Chanya wa mataifa |
I | 16:13-16:20 | Yesu ndiye masihi |
3 | 16:21-28:20 | Huduma ya Yesu kuelekea na ndani ya Yerusalemu |
A | 16:21-17:13 | Utabiri wa mateso na utukufu wa Masihi |
B | 17:14-17:27 | Uponyaji na miujiza |
C | 18:1-18:35 | Mafundisho kuhusu mahusiano kati ya wanafunzi (Semina ya mahusiano) |
D | 19:1-20:34 | Mwanzo wa Safari ya kuelekea Yerusalemu |
E | 21:1-22:46 | Yesu awasili Yerusalemu |
F | 23:1-23:39 | Ole kwa Yerusalemu |
G | 24:1-25:46 | Mafundisho kuhusu ujio wake mara ya pili (Semina ya ujio wake mara ya pili) |
H | 26:47-27:66 | Kukatatwa, Kuhukumiwa na kusulubiwa kwa Yesu |
I | 28:1-28:20 | Kufufuka kwa Yesu |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI
Kitabu hiki kinaweza kugawanywa katika sehemu kuu tatu, yaani Utangulizi (1:1-4:16), Huduma ya Yesu Galilaya (4:17-16:20), na Huduma ya Yesu kuelekea na ndani ya Yerusalemu (16:21-28:20).
Utangulizi una sehemu nne ambazo ni: Ukoo wa Yesu/Yesu katika historia ya Israeli (1:1-1:17), Kuzaliwa na utoto wa Yesu (1:18-2:23), Kubatizwa kwa Yesu (3:1-3:17), na Kujaribiwa kwa Yesu (4:1-4:11).
Mwandishi anaanza kitabu chake kwa kuonyesha kwamba Yesu ni mtoto wa Daudi na pia ni mtoto wa Ibrahim (1:1-17). Hii ni kuthibitisha kwamba Yesu ni Kristo/Masihi, kwa sababu maandiko yalitabiri kwamba Kristo/Masihi lazima atoke kwenye ukoo wa Daudi.[2] Baada ya hilo, Mwandishi anasimulia matukio ya wakati wa kuzaliwa kwa Yesu na ya wakati wa utoto wake, akiwa na kusudi la kuonyesha kwamba matukio haya yalikuwa ni utimilifu wa maandiko matakatifu (1:18-2:23). Jambo la kwanza ambalo mwandishi aliloanza nalo ni kuonyesha kwamba mimba ya Yesu ni ya muujiza, yaani ni muujiza wa mwanamke asiyemjua mwanaume kupata ujauzito. Jambo hili, anasema mwandishi, lilitokea kama lilivyotabiriwa na nabii Isaya (1:18-25).[3] Jambo la pili, mwandishi anasimulia jinsi Yesu alivyozaliwa Bethlehemu ya Uyahudi, mji wa Daudi, kama ambavyo maandiko yalitabiri kwamba Masihi atazaliwa huko. Hivyo, kuzaliwa kwake Bethlehemu ya Uyahudi, mji wa Daudi, ni utimilifu wa maandiko (2:1-12).[4] Jambo la tatu, mwandishi anaonyesha kwamba, kama ambavyo taifa la Israeli lilivyokimbilia Misri na kutoka Misri Mungu aliliita kurudi kwenye Nchi ya Ahadi, vivyo hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Yesu (2:13-15).[5] Jambo la nne, mwandishi anaonyesha hata mauaji yaliyotokea huko Bethlehemu katika juhudi za kutaka kutoa uhai wa Yesu yalikuwa ni utimilifu wa maandiko (2:16-18).[6] Na jambo la mwisho, mwandishi anaonyesha kwamba hata baada ya kurudi kutoka Misri, Yesu na familia yake walirudi Israeli, lakini hawakuenda kuishi Bethlehemu ya Uyahudi. Badala yake, walienda Nazareti ya Galilaya (2:19-23), na tukio hili pia lilikuwa ni utimilifu wa maandiko.[7] Baada ya hayo mwandishi anatusimulia kubatizwa kwa Yesu huko Jordani (3:1-17) na kujaribiwa kwake siku arobaini (4:1-11). Bado mfuatano wa matukio haya unaonyesha Yesu anavyoyaishi maisha ya Israeli. Israeli walipopita katika bahari ya shamu (Ubatizo) wakaingia jagwani kujaribiwa miaka arobaini ndivyo ilivyotokea kwa Yesu. Tofauti ni kwamba, Israeli walishindwa lakini Yesu alishinda.
Baada ya utangulizi huo mrefu wa maisha ya Yesu, mwandishi sasa anahamia kutuonyesha huduma ya Yesu katika jimbo la Galilaya (4:12-16:20). Huduma ya Yesu huko Galilaya ilianza kwa Yesu kubadilisha kituo chake kutoka Nazareti kwenda Kapernaumu. Na jambo hili pia, mwandishi anasema, lilikuwa ni utimilifu wa maandiko (4:12-17).[8] Kama sehemu ya maandalizi ya huduma yake, mwandishi anatusimulia jinsi Yesu alivyoita wanafunzi wake (4:18-22). Kabla ya kuelezea huduma ya Yesu kwa kirefu mwandishi anatoa muhtasari wa huduma ya Yesu katika jimbo la Galilaya (4:23-25). Kuna mambo mawili ya msingi katika muhtasari wa mwandishi kuhusu huduma ya Yesu Galilaya. Mwandishi anasema, Yesu alikuwa akifundisha (na kuhubiri) pamoja na kuponya (na kufanya miujiza). Kwa hiyo, hayo ndio mambo makubwa Yesu aliyoyafanya katika huduma yake Galilaya na ndio mwandishi atatuonyesha kwa kirefu.
Kwa kuzingatia mambo hayo mawili, Mwandishi anaanza kwa kuripoti mafundisho ya Yesu katika semina ya mlimani (5:1-7:29). Baada ya semina, mwandishi anaripoti kwa kirefu matukio ya uponyaji na miujiza yaliyofanywa na Yesu (8:1-9:38). Baada ya hapo, mwandishi anatuonyesha jinsi Yesu alivyowatuma wanafunzi wake kumi na wawili kwenda kwa jamii ya Israeli kufanya yale yale mambo mawili ambayo yeye alikuwa akiyafanya, yaani kuhubiri na kuponya (10:1-11:1).
Baada ya kuonyesha huduma ya Yesu, mwandishi sasa anaonyesha mwitikio wa watu kutokana na kazi ya Yesu na pia mwitikio wa Yesu baada ya kujua mtazamo wa watu juu yake. Mwandishi anaanza na mwitikio wa Yohana Mbatizaji (11:2-19), anafuata na mwitikio wa miji ya Korazini na Bethsaida (11:20-30), na mwisho mwitikio wa Mafarisayo (12:1-50). Pamoja na kuwepo kwa makutano waliokuwa wakiamini kazi yake (12:23), Yesu alipata mwitikio hasi kwa sehemu kubwa katika huduma yake kutoka kwa viongozi wa dini.
Baada ya hayo, mwandishi anaturudisha tena kwenye mambo mawili Yesu aliyokuwa akiyafanya, yaani kufundisha na kuponya. Mwandishi anaanza na mafundisho Yesu aliyoyafanya. Tofauti na semina ya kwanza ya mlimani, semina hii imejaa mifano inayohusu ufalme wa Mungu (13:1-53). Kawaida ya mwandishi ni kuripoti mafundisho, na baada ya hapo ni uponyaji na miujiza, na mwisho ni mwitikio wa watu. Lakini sasa hivi, kabla hajaenda kwenye uponyaji na miujiza, anasimulia mwitikio wa watu kwanza. Anaanza na mwitikio wa mji wa nyumbani wa Yesu (13:54-58) na kisha anamalizia na mwitikio wa Herode (14:1-13).[9] Baada ya hapo, Mwandishi anarudi tena kutusimulia kuhusu miujiza na uponyaji aliyoifanya Yesu. Moja ya miujiza katika habari hii ni ule wa kutembea juu ya maji (14:14-36).
Baada ya hayo, mwandishi sasa anaonyesha utofauti wa mwitikio wa watu tofauti tofauti kuhusu huduma ya Yesu. Mwandishi analinganisha kati ya kundi la viongozi wa dini ya Kiyahudi, yaani Mafarisayo, Masadukayo na waandishi, dhidi ya watu wa mataifa (watu ambao si Wayahudi). Kwa upande wa kwanza, Mafarisayo na waandishi waliosafiri kutoka Yerusalemu kwenda Galilaya, kwa sababu ya kukosa imani, walimkosoa Yesu na wanafunzi wake. Yesu aliwajibu na kutumia wakati huo kuwasahihisha tabia yao ya kutangua Neno la Mungu kwa kutumia mapokeo yao (15:1-20). Kwa upande wa pili, tofauti na viongozi wa Kiyahudi, mwanamke mmoja wa mataifa kutoka pande za Tiro na Sidoni alimwamini Yesu. Kwa sababu ya Imani yake aling’ang’ania sana na hatimaye akapata muujiza (15:21-28). Huyu mwanamke hakuwa ndiye pekee aliyekuwa na imani kwa Yesu; pia maelfu ya watu wa mataifa waliokuwa wakiishi upande wa mashariki mwa Bahari ya Galilaya, eneo linaloitwa Dekapoli (angalia Marko 7:31), walimwamini Yesu. Kwa sababu ya imani yao, walifanyiwa miujiza mingi, ikiwemo kulishwa mikate na Samaki kama wayahudi (Angalia 14:13-21). Kupitia miujiza hiyo, watu wa mataifa walimtukuza Mungu wa Israeli (15:29-39). Pamoja na kwamba watu wa mataifa walimwamini Yesu, Mafarisayo na Masadukayo hawakumwamini. Badala yake, walimjaribu kwa kumwomba ishara. Yesu alikataa kuwapa ishara na, kwa wakati huo huo, akawaonya wanafunzi wake kujiepusha na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo (16:1-12). Baada ya kazi hiyo kubwa Yesu aliyofanya, alichukua wakati kuwauliza wanafunzi wake jinsi watu walivyomtambua na pia jinsi wao walivyomtambua. Katika tukio hilo, Yesu alitambuliwa kama Masihi, Mwana wa Mungu aliye hai (16:13-20).
Baada ya wanafunzi kutambua kwamba Yesu ndiye masihi, huduma ya Yesu sasa inapata mabadiliko makubwa mawili; Moja, Kuanzia wakati huo Yesu anaanza kuwaweka wazi wanafunzi wake kwamba atapata mateso mengi, atauwawa na mwishoe atafufuka. Pili, huduma ya Yesu inahama kutoka Galilaya na kwenda Yudea (Kilele kikiwa ni Yerusalemu). Pamoja na Petro kupata ufunuo ya kuwa Yesu ndiye Masihi (Kristo) lakini hakukubaliana na ukweli kwamba masihi atapata mateso na hata kuawa. Yesu akamsahihisha Petro na kuwafundisha wanafunzi wake kwamba ili wamfuate wanatakiwa kuwa tayari kupitia mateso kama yeye atakavyopitia (16:21-28). Baada ya taarifa hizi za masikitiko kwa wanafunzi, baadhi ya wanafunzi wakapata bahati ya kumuona Yesu, mwana wa Adamu katika utukufu wake kama ambavyo atakuwa akaporudi mara ya pili (17:1-13). Matukio haya mawili ni ishara ya kwamba Masihi atapata mateso kabla ya utukufu.
Baada ya hayo, Yesu anarudi katika kazi yake ile ile ya kufundisha na kufanya miujiza na uponyaji. Yesu kwa sasa anaanza na miujiza na kuponya alafu ndio mafundisho. Yesu anamponya kijana mwenye pepo ambaye wanafunzi wake walishindwa kumponya kwa sababu ya kukosa imani (17:14-21). Kabla ya kuendelea na miujiza anarudia tena kuwakumbusha wanafunzi wake kwamba anakwenda Yerusalemu kuteseka lakini mwisho wake ni ufufuo (17:22-23). Baada ya hilo, Yesu akafanya muujiza mwingine, muujiza wa kulipa kodi ya hekalu kwa shekeli iliyopatikana kinywani mwa samaki, pamoja na ukweli kwamba alikuwa na uwezo wa kukataa kulipa kodi hii (17:24-27).[10] Baada ya miujiza hiyo, Yesu anawafundisha wanafunzi wake kwa kirefu kuhusu maisha ya mahusiano katikati yao. Yesu anawafundisha kuhusu unyenyekevu, kutokufanyika kwazo kwa ndugu na ulazima wa kusameheana (18:1-35).
Baada ya kumaliza semina hii, Yesu akaanza rasmi safari ya kuelekea Yerusalemu. Akaondoka Galilaya na kuelekea Yudea/Uyahudi. Akiwa njiani akaendelea kuponya kama kawaida ya huduma yake (19:1-2). Baada ya miujiza hiyo, Yesu akawafundisha wanafunzi wake pamoja na makundi manne ya watu tofauti waliomuendea ili kutafuta majibu ya masuala yao. Kundi la kwanza lilikuwa la Mafarisayo, waliomjia kwa lengo la kumjaribu ili kujua msimamo wake kuhusu talaka. Yesu akawajibu kwamba Mungu amekusudia mume na mke wasiachane baada ya ndoa, isipokuwa kwa sababu ya zinaa (19:3-12). Kundi la pili lilikuwa la watu waliomletea watoto ili awawekee mikono. Kwa kuwa watoto katika utamaduni wa Kiyahudi hawakupata kipaumbele, wanafunzi wake wakawazuia. Lakini Yesu akawawekea mikono na kuwafundisha wanafunzi wake kwamba wasiwazuie, kwa kuwa watu kama hao Ufalme wa Mungu ni wao (19:13-15). Mtu wa tatu alikuwa kijana tajiri aliyekuja kuuliza Yesu afanye nini ili kujihakikishia uzima wa milele. Yesu, kwa kumpenda, akamwambia auze kila alichonacho kisha amfuate. Kijana huyo hakuweza kumtii Yesu kwa sababu ya mali nyingi alizokuwa nazo. Hivyo, Yesu akaweka wazi kwamba ni vigumu kwa tajiri kuurithi Ufalme wa Mungu. Baada ya fundisho hilo, wanafunzi wake wakataka ufafanuzi, naye akawafafanulia yote (19:16-30). Yesu alipomaliza ufafanuzi wake kwa wanafunzi, akasema, “Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.” Ili wanafunzi waelewe alichomaanisha Yesu akaamua kufafanua maana ya usemi huo kwa kutumia mfano (20:1-16). Kabla ya Yesu kuendewa na kundi la nne, akarudia tena kuwaambia wanafunzi wake kwamba anaenda Yerusalemu, ambako atateswa na kuuawa, lakini baada ya siku tatu atafufuka (20:17-19). Kundi la nne lilikuwa ni mama wa Yohana na Yakobo pamoja na wanawe. Mama huyo akaomba Yohana na Yakobo wawe upande wa kuume na kushoto mwa Yesu katika Ufalme wake. Yesu akatumia nafasi hii kuwafundisha wanafunzi wake kuhusu aina ya utumishi na ukuu anaoutegemea kuona katikati yao, kama ambavyo yeye mwenyewe anawaonyesha kwa mfano wa maisha yake (20:20-28). Mpaka hapa, Yesu alikuwa amefika Yeriko. Baada ya kutoka Yeriko, makutano wakamfuata, naye Yesu akawaponya vipofu wawili waliokuwa kando ya njia (20:29-34).
Baada ya safari ndefu, Yesu sasa akafika Yerusalemu. Yerusalemu hakuingia kama alivyoingia miji mingine, bali aliingia kwa msafara mkubwa uliosababisha mji mzima kutaharuki akiwa amepanda punda.[11] Alipoingia Yerusalemu, akaenda kulitakasa hekalu kwa kuondoa biashara zilizokuwa zikifanyika humo.[12] Baada ya hapo, akafanya kazi yake ya uponyaji kama ilivyokuwa desturi katika huduma yake. Pamoja na kuwa huduma yake ilikuwa inafanyika Yerusalemu, Yesu alichagua mji wa Bethania kama eneo lake la kupumzika usiku. Hivyo, hata siku hiyo ya kwanza, alikwenda kupumzika huko (21:1-17). Asubuhi yake akatoka Bethania na kwenda Yerusalemu kuendelea na huduma yake. Alipokuwa njiani, akafanya muujiza wa kunyauka kwa mtini na akawafundisha wanafunzi wake kuhusu imani (21:18-22).[13] Alipofika Yerusalemu Yesu akajibizana na makundi manne ya viongozi wa Kiyahudi na watu wa madhehebu ya kiyahudi waliokuwa wakimjaribu kwa maswali yao mbalimbali.
Kundi la kwanza lilikuwa ni wakuu wa makuhani na wazee wa watu. Hawa, kwa kukosa kumwamini Yesu, wakamuuliza chanzo cha mamlaka yake. Yesu hakuwajibu, kwa sababu wao pia hawakuweza kumjibu swali lake kwao (21:23-27). Pamoja na kutokujibu swali lao, Yesu akatumia mifano mitatu kuelezea hali yao ya ukaidi kwa Mungu. Katika mfano wa kwanza, wakuu wa makuhani na wazee wa watu ni kama mtoto wa kwanza aliyeambiwa aende, akaitikia lakini asiende. Watoza ushuru na makahaba ni sawa na mtoto aliyeambiwa aende, akakataa lakini baadaye akatubu na akaenda (21:28-32). Katika mfano wa pili, Mungu ndiye yule mtu mwenye shamba la mizabibu. Watumwa waliotumwa na mmiliki wa shamba ni manabii wote waliotangulia kabla ya Yesu, na Yesu ndiye yule mwana aliyetumwa mwishoni. Hivyo, Yesu anasema kwamba kwa Yerusalemu kuwaua manabii na hatimaye kuwa na nia ya kumuua yeye (Mwana wa Mungu), Mungu atawahukumu na shamba hilo atawapa watu wengine (21:33-46).[14] Katika mfano wa tatu, Yerusalemu inafananishwa na watu walioalikwa arusini, lakini kila mmoja akatoa udhuru. Hivyo, Mungu akaamua kuwaalika watu wengine wote (22:1-14). Mifano yote hii inaonyesha jinsi viongozi wa Kiyahudi na Yerusalemu kwa ujumla wanavyomkataa Mungu kwa kumkataa Yesu, na jinsi ambavyo Mungu anafungua mlango kwa kila mtu, hasa wale waliokuwa hawahesabiwi kama wanastahiri uhusiano na Mungu, kama vile makahaba na watu wa mataifa.
Baada ya kundi la kwanza kushindwa kwa hoja, Mafarisayo wakawatuma wanafunzi wao na Maherode kumtega Yesu. Kundi hili la pili wakamtega kwa kumuuliza kama ni halali kulipa kodi kwa Kaisari au la. Yesu akawajibu kwa kielelezo kwamba ni halali kufanya hivyo (22:15-22). Kundi la tatu lililomjia Yesu lilikuwa ni Masadukayo. Kwa kuwa wao walikuwa hawaamini kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, wakamuuliza swali ili kujua kama yeye anaamini kama wao au kama Mafarisayo, ambao waliamini kuwa kuna ufufuo wa wafu. Yesu akawajibu kwamba ufufuo wa wafu upo, lakini watu wakifufuliwa hawaoi wala kuolewa (22:23-34).[15] Kundi la nne na la mwisho lilikuwa ni mtu kutoka kwa wanasheria. Huyu alimuuliza Yesu, kati ya amri za Mungu ipi ni kuu kuliko zote. Yesu akajibu kwamba amri ya kumpenda Mungu ndiyo kuu, ikifuatiwa na amri ya kumpenda jirani. Yesu akasema maandiko —yaani, Torati na manabii—yanazungumzia amri hizi (22:35-40).[16] Baada ya majibizano hayo marefu, Yesu akawauliza Mafarisayo swali kuhusu maneno ya Daudi kwa Masihi. Kwa swali hili, Yesu alilenga kujitambulisha kwao, lakini Mafarisayo hawakuweza kumjibu (22:41-46).[17] Kwa majibu hayo yote kwa makundi hayo yote, Yesu aliweza kuwafunga kinywa wapinzani wake.
Baada ya kuwafunga vinywa wapinzani wake, Yesu akafungua kinywa chake kufundisha makutano na wanafunzi wake. Yesu akawaonya wasifuate mfano wa maisha ya waandishi na Mafarisayo, bali wafanye yale tu wanayofundisha (23:1-12). Kwa nini Yesu anawakataza makutano na wanafunzi wake kufuata mwenendo wa waandishi na Mafarisayo? Ni kwa sababu wao wanafanya mambo kwa unafiki, yaani, wanaonyesha sura ya nje tofauti na ilivyo ndani yao. Katika kuonyesha mwenendo mbaya wa waandishi na Mafarisayo, Yesu anatangaza ole saba (za moja kwa moja au nane kwa ujumla), zinazoelezea tabia zao za kinafiki (23:13-36). Baada ya ole hizo, Yesu anahitimisha na sikitiko lake juu ya mji wa Yerusalemu, ambao umekuwa mkaidi kwa Mungu kila wakati. Mji huu umeua manabii (kumbuka mfano wa shamba la mizabibu), na matokeo yake Mungu ameondoka katika hekalu lake, hivyo hekalu limekuwa ukiwa. Yesu anasisitiza kwamba hatarudi katika hekalu tena mpaka pale watakapomkiri kuwa amekuja kwa jina la Bwana (23:37-39).
Baada ya kusema hayo Yesu akaondoka hekaluni na kwenda mpaka mlima wa mizeituni. Mlimani hapo Yesu akaanza kutabiri kuhusu kubomolewa kwa hekalu, kuhusu kuja kwake mara ya pili na kuhusu mwisho wa dunia sawa sawa na alivyoulizwa na wanafunzi wake (24:1-3). Kuhusu mwisho wa dunia, Yesu akataja dalili zitakazotokea ambazo ni ishara za mwanzo kabisa wa siku hizo (24:4-13). Mbali ya dalili hizo nyingi, Yesu akaweka wazi tukio litakaloleta mwisho wa dunia, yaani kuhubiriwa kwa habari za ufalme ulimwenguni kote (24:14). Kuhusu kubomolewa kwa hekalu, Yesu anasema pale watakapoona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli[18], limesimama katika patakatifu walioko uyahudi (Yudea) wakimbie mbali na Yerusalemu ili kujisalimisha kwa maana mji wao utavamiwa na kupigwa na watu wasioweza kukimbia watapata tabu na hata kuawa (24:15-20). Dhiki ambayo Yerusalemu itaipata inafanana na dhiki ile itakayokuwepo kipindi kifupi kabla ya Yesu kurudi mara ya pili.[19] Katika kipindi cha dhiki hio Yesu anatoa onyo watu wasije wakadanganyika na wale watakaokuwa wakisema Kristo yuko huku au yuko kule (24:21-28). Kuhusu kuja kwake, Yesu anasema baada ya dhiki kuu ndipo atashuka pamoja na parapanda ya Malaika na uumbaji utatikisika (24:29-31).
Mwendelezo wa semina hii ya Yesu sasa ni matumizi ya lugha ya picha mbalimbali katika kusisitiza kile ambacho amekwisha kufundisha. Katika picha ya kwanza, anasisitiza kwamba, kama vile watu wanavyoweza kutabiri ujio wa mavuno kwa kuangalia tabia ya mti aina ya mtini, basi watakapoona mambo hayo aliyoyasema, wajue kwamba wakati wa yeye kurudi kuvuna umekaribia (24:32-35). Katika picha ya pili, anasema kwamba kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa siku za ujio wake; watu watakuwa bize na mambo yao, naye atakuja ghafla (24:36-42). Tena, kwa picha ya tatu, anasema kwamba kama ambavyo mwenye nyumba hajui siku ya mwizi kuja, ndivyo ilivyo kwa wanafunzi. Wao hawajui siku ya kurudi kwa Bwana wao, hivyo wanatakiwa kuwa tayari wakati wowote (24:43-44). Katika lugha ya picha ya nne, Yesu anatumia watumwa wawili—yaani, mwaminifu na asiye mwaminifu—kuwasisitiza wanafunzi kutokuchoka kufanya yale aliyowaachia, hata kama itaonekana kwamba anachelewa (24:45-51).
Mazungumzo yote hayo ya Yesu ya kutumia lugha ya picha yanasisitiza kujiweka tayari kwa ujio wake usiojulikana ni lini utatokea na kuendelea kuwa waaminifu katika kipindi cha kumsubiri. Kwa mifano mingine mitatu, Yesu anasisitiza mambo hayo tena. Mfano wa wanawali (mabikira) kumi unasisitiza juu ya kujitayarisha kwa ajili ya ujio wake usiojulikana utatokea lini (25:1-13). Mfano wa talanta unasisitiza uaminifu na ustahimilivu kwa wanafunzi katika kipindi cha kumsubiri Bwana wetu (25:14-30). Na mfano wa kondoo na mbuzi unazungumzia hukumu na thawabu mwishoni baada ya ujio wake (25:31-46).
Baada ya semina hiyo kuisha, kilele cha huduma ya Yesu kinafika. Yale aliyoyasema katika mfano wake wa shamba la mizabibu (Kumbuka 21:33-46) kumhusu yeye sasa yanaingia kwenye utimilifu. Katika kutusimulia habari hizi za mateso ya Yesu, mwandishi anaweka utangulizi kwanza. Kwanza, anatujulisha kwamba kipindi hiki kilikuwa ni kipindi cha Pasaka, kipindi ambacho kinaambatana na sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu (26:1-2). Pili, anatujulisha jinsi mipango ya kumkamata na kumuua Yesu ilivyokuwa inapangwa (26:3-5). Tatu, anatuonyesha jinsi Yesu alivyo pakwa mafuta kwa ajili ya kuandaliwa kwa mazishi yake (26:6-13). Na mwisho, anazungumzia kuhusika kwa mmoja wa wanafunzi wake katika mpango wa kumkamata (26:14-16).
Mfululizo wa matukio kuelekea kuuawa kwake ulianza siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo pia ilikuwa ni siku ya Pasaka. Yesu aliandaliwa chakula kwa ajili ya kula Pasaka, kumbukumbu ya Mungu kuwaokoa Waisraeli kutoka utumwani Misri kupitia damu ya kondoo. Pamoja na kutabiri kwamba msaliti wake yuko pamoja naye katika chakula hiki, Yesu akageuza mlo wa Pasaka kuwa mlo wa kutangaza kifo chake kwa ajili ya wokovu wa wengi (26:17-29). Usiku huo huo, Yesu akawachukua wanafunzi wake na kuwapeleka katika Mlima wa Mizeituni. Huko, akawaweka wazi kwamba wakati wa kutengana nao umefika. Petro akabisha na kuonyesha kwamba hawezi kutengana na Yesu kwa gharama yoyote, lakini Yesu akamweka wazi tena kuwa kabla ya asubuhi kufika, atamkana mara tatu (26:30-35). Tokea hapo, wakasogea wote mpaka kwenye bustani ya Gethsemane, na hapo Yesu akawachukua Petro, Yakobo, na Yohana ili waende kuomba (26:36-46).
Baada ya maombi haya kuisha, Yesu akakamatwa (26:47-56) na kupelekwa mbele ya baraza la wazee wa Kiyahudi kwa ajili ya kushtakiwa (26:57-67). Wakati mashitaka yanaendelea kwa upande wa Yesu, Petro kwa upande wake akamkana Yesu mara tatu na hatimaye jogoo akawika (26:68-75). Kwa kuwa Israeli ilikuwa chini ya utawala wa Rumi, baraza la wazee wa Kiyahudi halikuwa na uwezo wa kutoa hukumu ya kifo, hivyo wakampeleka Yesu kwa Pilato, ambaye ndiye aliyekuwa liwali (kiongozi mwakilishi wa serikali ya Rumi) na mwenye mamlaka ya kutoa hukumu ya kifo. Pamoja na Pilato kutokuona sababu ya hukumu ya kifo, Wayahudi wakamshinikiza atoe hukumu hiyo. Basi, kwa sababu ya shinikizo, Pilato akaamua kama walivyotaka Wayahudi lakini akafanya ishara ya wazi iliyoashiria kwamba yeye hajahusika katika kufanya maamuzi hayo. Wakati hayo yanaendelea kwa upande wa Yesu, upande wa pili Yuda, msaliti wa Yesu, akajuta kwa kile alichofanya na akaamua kujinyonga (27:1-26). Baada ya hukumu kutolewa, Yesu akapigwa, akasulubiwa katikati ya waalifu wawili, akafanyiwa dhihaka mbalimbali na watu mbalimbali, akafa, na jioni yake akazikwa na Yusufu, mtu tajiri wa Arimathaya (27:27-61).
Kesho yake, ambayo ni Jumamosi, wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakamwomba kaburi lilindwe ili ujanja wowote usifanyike wa kumchukua Yesu na kutangazwa kwamba amefufuka. Wakapewa ruhusa na wakafanya hivyo (27:62-66). Kesho yake asubuhi, wanawake wakaenda kaburini alikozikwa Yesu, wakakuta kaburi liko wazi na malaika juu ya jiwe. Malaika akawapasha habari kwamba Yesu aliyesulubiwa amefufuka na hivyo wakawapashe habari wanafunzi wake. Wakiwa njiani, Yesu akawatokea wanawake hao na akawaagiza waende Galilaya (Kumbuka Yesu alianzia huduma Galilaya, lakini alifia Yerusalemu) pamoja na wanafunzi wake, maana huko ndiko watakakomuona (28:1-10).
Taarifa zilipoanza kuenea na wanafunzi walipoanza kuelekea Galilaya, askari wakapewa fedha ili wapotoshe taarifa za kufufuka kwa Yesu (28:11-15). Baada ya kufika Galilaya, Yesu akawapa wanafunzi wake kazi ya kufanya huku akiwajulisha kwamba mamlaka yote mbinguni na duniani amepewa yeye (28:16-20).
FOOTNOTES
[1] Hii ni kwa sababu Mathayo haielezei sana taratibu za kiyahudi kwa kuwa anajua wapokeaji wake wanajua hizo taratibu. Hii ni tofauti na Marko ambaye anaelezea kwa ufafanuzi hizo taratibu kwa kuwa anajua wapokeaji wa ujumbe wake hawazijui taratibu hizo. Linganisha maelezo ya Mathayo na Marko katika Maeneo yafutayo; Mathayo 15:2 // Marko 7:3– 4; Mathayo 26:17 // Marko 14:12; Mathayo 27:62 // Marko 15:42).
[2] Maandiko katika Agano la kale yalitabiri kwamba Kristo/masihi atatoka kwenye ukoo wa mfalme Daudi ambaye Mungu alimuahidi kwamba ufalme wake utakuwa wa Milele (2 Samweli 7:1-14)
[3] Mstari wa 23 sura ya 1 ni nukuu kutoka Isaya 7:14.
[4] Mstari wa 6 sura ya 2 ni nukuu kutoka Mika 5:2,4.
[5] Mstari wa 15 sura ya 2 ni nukuu kutoka Hosea 11:1
[6] Mstari wa 18 sura ya 2 ni nukuu kutoa Jeremia 31:15
[7] Hakuna nukuu ya moja kwa moja kutoka katika Maandiko ambayo inaonyesha Masihi ataitwa mnazarayo ndio maana Mwandishi pia amesema hili lilitokea kama utimilifu wa neno lilonenwa na “manabi” na sio nabii. Hivyo utimilifu huu ni wa ujumbe wa jumla sio wa nukuu moja kama sehemu zingine za juu.
[8] Mstari wa 15 na 16 sura ya 4 ni nukuu kutoka Isaya 9:1,2
[9] Katika kuelezea mwitikio wa Herode kwa Habari alizozisikia kuhusu Yesu, Mwandishi anaelezea kile Herode alichokifanya kwa Yohana kwa kuwa Herode alimfananisha Yesu na Yohana. Hii mbinu iliyotumika hapa inaitwa kisengere nyuma au mbinu rejeshi.
[10] Kodi ya nusu shekeli ilikuwa ni kodi ya hekalu ya kila mwaka iliyotozwa kwa wanaumewote wa Kiyahudi waliokomaa. Hii ilikuwa tofauti na kodi za Kirumi (angalia Mathayo 22:15–22), kodi hii ilitarajiwa kulipwa kama jukumu la kizalendo. Hata hivyo, Masadukayo walipinga kodi hii na wanachama wa jamii ya Qumran kwa misingi ya kanuni zao walilipia kodi hii mara moja tu maisha yao yote. Hii ndio maana hoja kutoka kwa watoza ushuru inaonyesha walihisi kwamba Yesu pia huenda asingeona kodi hii kuwa ni jukumu la lazima.
[11] Mstari wa 5 (21:5) ni nukuu kutoka katika Zekaria 9:9. Hii inamaanisha kwamba Yesu kuingia Yerusalemu akiwa amepanda punda ilikuwa ni utimilifu wa unabii wa Zekaria. Punda katika maandiko amekuwa akiwakilisha utumishi, hivyo unabii wa Zekaria kuhusu ujio wa mfalme ambaye atapanda punda ulikuwa unawakilisha mfalme atakayewatumikia watu na sio kutumikiwa.
[12] Tukio la Yesu kupindua meza ni utimilifu wa unabii wa Malaki 3:1-4. Unabii huu ulitabiri kwamba Bwana atalijilia hekalu lake ghafla na atalisafisha. Lakini wakati Yesu anapindua meza, alisema, “Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi”, akinukuu maneno haya kutoka Isaya 56:7 kwa sehemu ya kwanza na kutoka Yeremia 7:11 katika sehemu ya pili.
[13] Pamoja na ukweli kwamba tendo hili la Yesu kuulani mtini lilikuwa ni tendo la muujiza, lakini lilikuwa tangazo kwa Yerusalemu. Kwamba kwa sababu hawana matunda (matendo mema yatokanayo na toba), hukumu inakuja juu yao. Kufananisha Israeli na mtini au mzabibu ni jambo la kawaida katika maandiko (Yeremia 8:13 na Hosea 9:10).
[14] Picha ya shamba la mizabibu katika mfano huu wa pili inatoka katika Isaya 5:1-7 , ambapo Israeli inafananishwa na shamba la mizabibu ambalo halizai matunda mazuri, na hivyo kusababisha hukumu yake. Nukuu ya Yesu katika mstari wa 42 (21:42) inatoka katika Zaburi ya 118:23-24.
[15] Katika mstari wa 32 (22:32) Yesu ananukuu Kutoka 3:6
[16] Yesu anaunganisha Kumbukumbu la Torati 6:5 (kumpenda Mungu) na Mambo ya Walawi 19:18 (kupenda jirani), akijibu kuhusu ipi ni sheria iliyokuu kuliko zote.
[17] Swali la Yesu liko hivi: Daudi, mwandishi wa Zaburi ya 110, ameandika hivi katika mstari wa kwanza: “Neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.” Katika mstari huo, Daudi anamwita Masihi ajaye Bwana wangu, lakini unabii unasema Masihi atatoka katika ukoo wa Daudi, maana yake Daudi ni baba wa Masihi, na Mafarisayo wanajua hilo. Swali sasa ni: inakuwaje Daudi anamwita mwanawe Bwana wangu? Pamoja na kwamba Yesu hakutoa jibu moja kwa moja, jibu ni kwamba katika Roho, Daudi alijua kwamba Masihi ni mkubwa kuliko yeye.
[18] Chukizo la uharibifu limenenwa na nabii Danieli mara tatu katika unabii wake (Danieli 9:27, 11:31, na 12:11), na katika maeneo yote hayo, chukizo la uharibifu ni kusimamishwa kwa kitu au mtu juu ya madhabahu hekaluni baada ya kusitishwa kwa sadaka ya kuteketezwa. Tukio hili, ambalo Danieli alilitabiri, inawezekana lilitimia kwa mara ya kwanza mwaka 167 KK, wakati mtawala wa Kigiriki kwa jina Antioko IV aliponajisi Hekalu la Yerusalemu. Antioko alimtengenezea mungu Zeu madhabahu juu ya madhabahu ya dhabihu ya kuteketezwa iliyokuwa hekaluni Yerusalemu, na akatoa dhabihu ya nguruwe kwenye madhabahu hiyo. Hivyo, Yesu alikuwa anawaonya wanafunzi kwamba wakiona tukio kama hili linajitokeza, wakimbie wala wasiungane katika kupinga uvamizi huo, maana wakifanya hivyo hawatasalimika. Inawezekana pia kwamba jambo hili ni utabiri wa wakati unaokuja.
[19] Hatuna uhakika wa asilimia 100 kuhusu kipindi hiki cha dhiki kuu Yesu anachokizungumizia ni kipi. Inaweza kuwa kipindi cha dhiki tangu wakati wa kuvamiwa kwa Yerusalemu na kubomolewa kwa hekalu mpaka pale kristo atakaporudi. Pia, inaweza kuwa kipindi cha Hekalu kubomolewa kwa mara ya kwanza na katika kipindi kifupi kabla ya Yesu kurudi mara ya pili.
Unakuja hivi karibuni…