Ujio wa Yesu duniani unafungua Agano Jipya. MATHAYO, MARKO, LUKA, na YOHANA wanaandika maisha ya Yesu Kristo kwa mitazamo tofauti kwa sababu vitabu hivi vililenga watu tofauti. Maisha ya Yesu, kazi zake, mafundisho yake, kifo chake na kufufuka kwake vinarekodiwa katika vitabu hivi kuonyesha kutimia kwa ahadi ya ukombozi. Hii haina maana kwamba vitabu hivi ndio vilikuwa vitabu vya kwanza kuandikwa katika Agano jipya. Vitabu hivi tumevitanguliza kwa sababu vinaunganisha vizuri ahadi za Agano ya kale na utimilifu wa ahadi ya ujio wa Yesu. Kitabu cha MATENDO YA MITUME kinaeleza maisha ya wafuasi wa Yesu na utimizaji wa agizo alilowapa la kupeleka Injili mpaka mwisho wa dunia. Kinaanza kwa kuonyesha jinsi Injili ilivyoenezwa katika Yerusalemu, Uyahudi, Samaria na miji mingine ya mataifa mengine, na kinaishia Injili ikiwa imefika katika mji wa Rumi, makao makuu ya dola ya Rumi, dola iliyotawala wakati huo.
Kwa kuwa kanisa lilizaliwa Yerusalemu siku ya Pentekosti, waamini wengi wa mwanzoni walikuwa ni wayahudi. Na kwa kuwa wayahudi wengi waliishi nje ya Israeli, baada ya tukio la pentekosti walirudi kwenye nchi walizokuwa wanaishi, na hivyo kurudi wakiwa wameamini. Kwa sababu hiyo imani ikaenea nje ya taifa la israeli. Kutokana na mateso waliyokuwa wanayapata wayahudi hawa walioamini kutoka kwa wasioamini, mtumwa wa Mungu na kristo YAKOBO akaamua kuwaandikia barua kwa ajili ya kuwatia moyo na kuwakumbusha mafundisho ya Bwana Yesu.
Baada ya kanisa kuendelea kukua nje ya Israeli, Kanisa la mji wa Antiokia ndio likawa kama kanisa mama kwa makanisa ya wamataifa. Mtume Paulo alikuwa Antiokia baada ya kuchukuliwa na Barnaba. Barnaba na Paulo kutoka Antiokia wakaanza safari yao ya kwanza ya kimishenari. Safari yao ilikuwa kutoka Antiokia kwenda Kipro (Salami na Pafo), kutoka Kipro kwenda Galatia (Perge, antiokia ya pisidia, Ikonio, Listra na Derbe). Baada ya safari hii wakarudi Antiokia walipoanzia kazi. Huko kote walifanya kazi ya kuhubiri na kupanda makanisa. Kutoka Antiokia mtume Paulo akaandika waraka kwa WAGALATIA baada ya kupata habari kwamba kuna waamini wa kiyahudi wanawafundisha Wagalatia injili nyingine. Waalimu hao waliofundisha injili nyingine walifika mpaka Antiokia na hatimaye wakashindana sana na Paulo na Barnaba. Kutokana na mashindano hayo kanisa likawatuma Paulo na Barnaba kwenda Yerusalemu, kuonana na mitume wengine ili kujadili injili sahihi ni ipi. Mkutano huo ukakubali kwamba injili iliyokuwa inahubiriwa na Paulo na Barnaba ndio injili sahihi.
Baada ya muda kupita, Paulo akaamua kurudi kuwaangalia waamini walioamini kipindi cha safari yao ya kwanza ya kimishenari. Safari hii akawa na Sila na Timotheo, ambaye aliungana nao walipotembelea Derbe na Listra kutokea Antiokia. Walitaka kuendelea na safari ya kurudia makanisa yaliyozaliwa katika safari ya ya kwanza ya mtume Paulo lakini Roho wa Mungu akawazua na hivyo akawapeleka mpaka Troa. Kutoka Troa, Paulo akapata maono ya kwenda jimbo la Makedonia. Makedonia waliingia katika mji wa Filipi na kuhubiri hapo na kanisa likazaliwa. Kutoka Filipi wakaenda Thessalonike na huko kanisa likazaliwa. Kutoka Thessalonike Paulo akaenda Athene akiwaacha Timotheo na Sila huko Makedonia. Kutoka Athene Paulo akaenda kwenye mji wa Korintho katika jimbo la Akaya. Sila na Timotheo wakaungana na Paulo huko Korintho ambako walikaa kwa muda wa miaka miwili na kutoka huko ndio wakaandika WARAKA WA KWANZA NA WA PILI KWA WATHESALONIKE. Baada ya hapo Paulo akarudi Antiokia alipoanzia safari ikipitia maeneo machache wakati akirudi.
Baada ya siku kadhaa, mtume Paulo akaanza tena safari yake ya tatu ya kimishenari. Kutoka Antiokia akaenda mpaka Efeso kupitia Galatia. Huko Efeso akakaa muda wa miaka mitatu na kutoka huko ndio akaandika WARAKA WA KWANZA NA WA PILI KWA WAKORINTHO. Hii ni baada ya kupokea taarifa ya changamoto zilizopo katika kanisa hilo. Kutoka Efeso akaenda Thesalonike na Korintho na kurudi tena Efeso. Katika wakati huu ndio akaandika waraka wake kwa WARUMI. Paulo aliandika waraka huu akitarajia kwenda na kuwaandaa kanisa ili akitoka kwao wamsafirishe aende Uhispania. Kutoka Efeso safari yake ikaishia Yerusalemu, na sio Antiokia kama ilivyokuwa kawaida yake. Huko Yerusalemu Paulo akakamatwa na kupelekwa Kaisaria, ambako alitumikia miaka miwili ya kukaa gerezani akisubiri hukumu yake. Baada ya muda huo, Paulo alikata rufaa ili kesi yake ikasikilizwe na Kaisari huko Rumi. Hivyo Paulo akasafirishwa mpaka Rumi, makao makuu ya dola, kwa ajili ya kesi yake kusikilizwa. Huko Rumi alikaa katika kifungo cha ndani, akisubiri hukumu yake. Katika kifungo hicho cha kusubiri kesi yake kusikilizwa, Paulo akaandika nyaraka nne ambazo ni WAEFESO, WAFILIPI, WAKOLOSAI na FILEMONI.
Baada ya kesi yake kusikilizwa, Paulo alishinda kesi na akaachiwa huru. Kutoka Rumi alisafiri hadi Efeso na kukutana na Timotheo huko. Baada ya muda alimwacha Timotheo kuweka mambo sawa yaliyoanza kuharibiwa na waalimu wa uongo na yeye kuendelea na safari ya kimishenari. Paulo alisafiri tena na Tito hadi Krete na kupanda makanisa huko. Baadaye, akimwacha Tito huko Krete ili kuchangua wazee katika kila kanisa na kukamilisha mambo yaliyopungua. Wakati Paulo alipokuwa akisafiri tena katika eneo la Makedonia, aliandika barua ya KWANZA KWA TIMOTHEO na barua kwa TITO ili kuwahimiza na kuwaelekeza kufanya kazi alizowaachia kufanya.
Baada ya muda katika mji wa Rumi moto mkubwa alizuka ambao uliteketeza makazi ya watu na mali kwa muda wa siku tisa. Kutokana na uharibifu wa moto huo, watu walirusha lawama zao kwa Kaisari Nero. Kama mtawala ili kujiepusha na lawama hizo, yeye akawasingizia wakristo. Kwa sababu ya hilo, wakristo wakaanza kupitia mateso makali katika mji wa Rumi. Kutokana na mateso hayo, Wakristo wengine wakawa wanarudi kwenye imani ya kiyahudi kwa kuhudhuria kwenye masinagogi. Hii ni kwa sababu dini ya kiyahudi ilikuwa ni dini inayotambulika na serikali ya Rumi na iliruhusiwa kufanya shughuri zake za kiibada. Kutokana na hali hio ya mateso na wengine kutaka kurudi kwenye uyahudi kwa sababu kuna usalama, mwandishi akaandika waraka kwa WAEBRANIA. Waraka uliandikwa kuwaonya waamini wanaotaka kurudi kwenye uyahudi kutokana na mateso, huku mwandishi akiwaonyesha ubora wa Yesu na ubora wa imani yao katika yeye.
Baadaye Katika kipindi cha mateso makali kwenye dola nzima ya Rumi yaliyoratibiwa na Kaisari Nero, Paulo alikamatwa tena na kuwekwa katika gereza la kirumi ambako huko aliandika barua yake ya mwisho, WARAKA WA PILI KWA TIMOTHEO. Wakati mtume Paulo yuko gerezani mtume Yohana alienda Efeso. Mtume Yohana aliishi huko na kufanya huduma yake katika eneo la Asia ndogo. Kutokana na mahusiano yake na makanisa yaliyokuwa Asia ndogo, na kwa sababu tofauti tofauti akaandika nyaraka zake tatu, yaani WARAKA WA KWANZA WA YOHANA, WARAKA WA PILI WA YOHANA na WARAKA WA TATU WA YOHANA.
Katika kipindi hicho hicho cha mateso makali ya kanisa, Mtume Petro akiwa Rumi aliamua kuwaandikia barua waamini waliokuwa wanaishi Asia ya katikati na ya kaskazini. Aliandika barua hii kuwatia moyo kutokana na mateso wanayoyapitia. Barua hii ndio inaitwa WARAKA WA KWANZA WA MTUME PETRO. Na kutokana na mateso kuendelea Rumi, Mtume Petro alijua amebakiwa na muda mchache wa kuishi hivyo akaandika barua yake ya pili kwa makanisa ya mataifa ambao walipokea barua yake ya kwanza na ambao walipokea pia barua za mtume Paulo. Barua hii ndio inaitwa WARAKA WA PILI WA MTUME PETRO. Baada ya hapo mtume Paulo alitangulia kuawa na baadaye akafuata mtume Petro. Katika kipindi hiki wakristo wengi waliuawa kwa mateso makali yaliyosimamiwa na Kaisari Nero. Kutokana na ukatili wake Kaisari Nero alipinduliwa, na baraza la seneti likamtangaza kama adui wa Rumi na hatimaye akajinyonga akiwa mafichoni.
Pamoja na jitahada za mtume Paulo, Timotheo, Tito, Mtume Petro na wengine kupingana na mafundisho ya uongo bado mafundisho ya uongo yaliendelea kuenea kwa kasi. Kuendelea kwa mafundisho ya uongo ndio kulimsababisha mdogo wa Yesu kuandika barua yake kuwaelezea kanisa kuhusu uhakika wa hukumu juu ya waalimu wa uongo. Barua hii ndio inaitwa WARAKA WA YUDA kwa watu wote.
Baada ya miaka kupita katika utawala wa Kaisaria Domitiani, Mtume Yohana akakamatwa, akateswa na kupelekwa kisiwani Patmo. Kutoka huko mtume Yohana akapata maono na kuandika kitabu cha UFUNUO kwa ajili ya kwenda kwenye makanisa yaliyokuwa Asia ndogo. Katika kitabu hiki Yohana analieleza kanisa kwamba, mwisho Mungu wetu atashinda na hatimaye ataweka utawala wake wa milele katika nchi.