Vitabu vya Biblia katika Biblia zetu vimepangwa kwa vigezo tofauti tofauti. Agano la Kale kwa sehemu kubwa limepangwa kwa kuzingatia aina ya uandishi wa vitabu. Kwa mfano, vitabu vya manabii (Isaya hadi Malaki) vimepangwa kwa kufuatana kwa sababu vyote ni vitabu vya unabii. Vitabu vya historia vimepangwa kwa kufuatana kwa sababu vyote ni vitabu vya simulizi (Joshua hadi Esta). Kwa upande wa Agano Jipya, vitabu vimepangwa kwa kufuata mfululizo wa matukio, ingawa ndani yake kuna vitabu vimepangwa kulingana na mwandishi; vitabu vya mwandishi mmoja vimepangwa pamoja. Pamoja na upangaji huo mzuri, vitabu vya Biblia pia vinaweza kupangwa kwa kuzingatia mfululizo wa matukio katika historia. Hivyo, utangulizi huu utakuonyesha mpangilio wa vitabu vya Biblia kwa kufuata mfululizo wa matukio ya kihistoria.
Historia inaanzia katika kitabu cha MWANZO. Kitabu cha Mwanzo kinaonyesha uumbaji wa Mungu wa Mbingu na Nchi, kuingia kwa dhambi duniani, kutabiriwa kwa kuja mkombozi, na maisha ya vizazi mbalimbali baada ya mwanadamu kufukuzwa bustani ya Edeni. Katika vizazi mbalimbali baada ya maisha nje ya bustani tunakutana na mchaji Mungu ambaye maisha yake yanazungumzwa katika kitabu cha AYUBU. Pamoja na wanadamu kuwa mbali na Mungu, Ayubu alikuwa mkamilifu mbele za Mungu.
Baada ya vizazi vingi kupita, Mungu akaamua kujifunua kwa Ibrahim. Kutoka kwa Ibrahim Mungu akatengeneza taifa la Israeli, taifa ambalo lilikuwa na jumla ya makabila kumi na mbili. Kitabu cha Mwanzo kinaisha na taifa hili lenye makabila kumi na mawili liko nchini Misri kama sehemu ya makimbilio baada ya njaa kwenye nchi yao waliyopewa na Bwana.
KUTOKA ni kitabu kinachoeleza mateso ya taifa la Israeli kule nchini Misri, ukombozi wao na kuanza kwa safari yao ya kurudi katika nchi yao ya ahadi. Katika kuelekea nchi ya ahadi, Mungu anafanya Agano na hili taifa katika mlima SINAI. Katika Agano, Mungu anawapa taifa hili sheria na taratibu zake ili waendelee kudumu katika agano hilo. Muda mfupi baada ya Agano, Israeli wakamkosea Mungu kwa kufanya sanamu na kuiabudu. Kwa sababu ya mioyo yao ya dhambi, Mungu anawapa waisraeli taratibu za kukaa na uwepo wake. Taratibu hizi zinarekodiwa katika kitabu cha MAMBO YA WALAWI, Walawi wakiwa wawakilishi wa taifa katika uwepo wa Mungu. Uwepo wa Mungu ukiwa unawakilishwa na SANDUKU LA AGANO ambalo lilikuwa linawekwa kwenye HEMA LA KUKUTANIA.
Kutoka SINAI ambako walikaa kwa mwaka mmoja, safari yao inaendelea ili kuifikia nchi ya ahadi. Muendelezo wa safari unarekodiwa katika kitabu cha HESABU. Kitabu hiki pia kinaonyesha sensa ya makabila yote kumi na mawili ya taifa la Israeli, mgawanyo wao, pamoja na mpangilio wao wakati wa kusafiri na wakati wa kupumzika.
KUMBUKUMBU LA TORATI ni mjumuisho wa sheria zote Mungu alizowapa Israeli ili wawe taifa teule na taifa tengwa kwa ajili yake. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa semina za Musa kwa kizazi kipya kilichozaliwa njiani kabla ya wao kuvuka mto Jordani.
Safari ya kumiliki nchi ya ahadi na kugawana maeneo sawa na makabila yao inaelezewa katika kitabu cha JOSHUA. Maisha ya makabila ya taifa la Israeli katika nchi ya ahadi yanaelezwa katika kitabu cha WAAMUZI. Maisha yao yalikuwa na kawaida ya kumuuzi Mungu; waliingia kila wakati katika kuabudu sanamu. Walipoingia katika kuabudu sanamu, Mungu aliruhusu wapate mateso kutoka kwa majirani zao. Katikati ya mateso waisraeli walimkumbuka Mungu na hivyo, Mungu akawa akiwatuma Waamuzi kwa ajili ya ukombozi. Katikati ya kipindi hiki cha Waamuzi kunatokea njaa katika nchi ya ahadi na familia moja (familia ya Elimeleki) inakwenda nchi jirani ya Moabu kwa ajili ya kukimbia njaa, na hapo tunapata kitabu cha RUTHU. Kitabu hiki kinaelezea nini kilitokea huko Moabu na yaliyofuata baada ya familia kurudi na idadi pungufu ya wanafamilia.
Vitabu vya SAMWELI WA KWANZA NA WA PILI vinaonyesha maisha ya taifa la Israeli chini ya mwamuzi na nabii wa Mungu aitwaye Samweli. Katika kipindi chake Samweli taifa likadai mfalme kama mataifa mengine, na Mungu akawapa wafalme. Hapo ndipo tunapata WAFALME WA KWANZA NA WA PILI. Vitabu hivi vinaeleza maisha ya taifa wakati wafalme wakitawala. Katika kipindi cha wafalme tunampata mfalme Daudi, mfalme ambaye katika ufalme wake alitumiwa na Mungu kuandika kitabu cha ZABURI, kikiwa ni jumla ya mashairi ya taifa kwa ajili ya kumshukuru, kumlilia, kumwabudu, kumtukuza, na kumwomba Mungu tangu ukombozi kutoka Misri mpaka wakati wa utawala wake. Daudi anazaa watoto wengi lakini mwanae Suleimani anakuwa mfalme wa taifa la Israeli. Sulemani anajenga HEKALU kwa ajili ya taifa kumwabudu Mungu na kutunza sanduku la Agano ambalo lilikuwa ndani ya hema la kukutania. Sulemani anakuwa mfalme mwenye hekima kuliko wafalme wote wa taifa la Israeli na hekima zake zinaandikwa katika kitabu cha MITHALI na kitabu cha MHUBIRI. Sulemani pia anahusishwa katika mashairi yenye hekima kuhusu mapenzi katika kitabu cha WIMBO ULIO BORA.
Baada ya kifo cha Mfalme Sulemani taifa la Israeli linagawanyika na kuzaa mataifa mawili; taifa la kaskazini likiwa na jumla ya makabila kumi likiitwa ISRAELI, chini ya Mfalme JEROBOAMU. Jeroboamu alikuwa ni kiongozi aliyeasi katika ufalme wa Sulemani. Taifa la kusini lilikuwa na makabila mawili (Benjamini na Yuda) chini ya mfalme REHOBOAMU, mtoto mrithi wa Sulemani. Taifa hili la kusini liliitwa YUDA.
Mataifa yote mawili, YUDA NA ISRAELI, walifanya mabaya mbele za Mungu kwa kuabudu sanamu na kufanya udhalimu katika jamii. Kwa sababu ya dhambi hizo Mungu alituma manabii wake kuwaonya na kutangaza kwamba, atawapeleka utumwani/uhamishoni kama hawatatubu. Manabii wengi wapo katika vitabu vya Wafalme na vya Mambo ya nyakati. Ujumbe wa maonyo juu ya ufalme wa kaskazini, yaani Israeli ulipelekwa na manabii HOSEA na AMOSI. Manabii hawa walitabiri taifa/dola ya Ashuru itakuja kuwapiga na kuwatawanya, kama adhabu ya Mungu juu ya makosa yao. Hili lilitokea kwa kuwa Israeli hawakuacha dhambi zao na hapo ndipo makabila haya kumi ya kaskazini yanapotea kabisa katika historia ya Biblia.
Mungu pia aliwaonya taifa la kusini kuacha kutenda mabaya kama ndugu zao wa taifa la kaskazini. Katika maonyo hayo, Mungu aliwatumia manabii kutabiri ujio wa dola ya Babeli kama watu wa Yuda hawataghairi mabaya yao. Mungu anafikisha ujumbe huu kupitia vinywa vya YOELI, ISAYA, MIKA , ZEFANIA na JEREMIA. Nabii HABAKUKI yeye katika kipindi hikihiki analalamika kuona Mungu yuko kimya katikati ya maovu makubwa katikati ya taifa la Yuda. Pamoja na Mungu kumjibu kwamba taifa la Yuda litahukumiwa, Habakuki analalamika tena kuona kwamba Mungu anatangaza kuangamizwa kwa taifa alilolitoa Misri kwa kutumia taifa ovu kuliko wao. Unabii wa watu wa Yuda kuchukuliwa mateka na dola ya Babeli unatimia wakati Jeremia akiwa hai, yeye anakimbilia Misri wakati wengine wakipelekwa utumwani Babeli. Unabii huu ulitimia kwa sababu watu wa Yuda hawakusikiliza sauti ya Bwana kupitita manabii wake. Jeremia anaulilia Yerusalemu ulioanguka na kupigwa na taifa la Babeli katika mashairi ya kitabu cha MAOMBOLEZO. Hatua ya mwisho ya kupigwa kwa mji wa Yerusalemu inatabiriwa na nabii EZEKIELI wakati yeye mwenyewe akiwa utumwani Babeli. Mungu pia anamuonyesha Ezekieli matumaini ya urejesho yatakayotokea baada ya miaka sabini ya utumwani kuishi.
Mbali na Yuda na Israeli, Mungu aliwatumia manabii wake kuwaonya mataifa mengine; alimtumia NAHUMU na YONA kuwaonya watu wa mji wa Ninawi, mji ambao ulikuwa mkuu wa taifa/dola ya Ashuru. Mungu anamtumia OBADIA kuwatangazia Edomu kuangamizwa kwao kwa ajili ya dhambi yao ya kutokumsaidia ndugu yao (Yuda) wakati wa kuvamiwa kwake.
Maisha ya watu wa Yuda utumwani/uhamishoni Babeli yanarekodiwa na DANIELI katika kitabu chake. Katika kitabu chake pia Mungu anamuonyesha dola zitakazotawala dunia baada ya Babeli. MAMBO YA NYAKATI WA KWANZA NA WA PILI ni vitabu vinavyotoa muhtasari wa sehemu kubwa ya Maandiko ya Agano la kale. Muhtasari wake unaanza na Adamu na kumalizia na tangazo la kurudi kwa Israeli kutoka uhamishoni.
Wakati unatimia, Mungu anawapa dola ya Umedi na Uajemi utawala juu ya dunia na watu wa taifa la Yuda/Israeli wanaruhusiwa kurudi nyumbani kwao. Waliporuhusiwa kurudi, watu wa Yuda hawakurudi wote kwa wakati mmoja; walirudi kwa makundi matatu tofauti kama inavyoelezwa katika vitabu vya EZRA NA NEHEMIA. Kundi la kwanza na la pili linaelezwa katika kitabu cha Ezra na kundi la tatu katika kitabu cha Nehemia. Kundi la kwanza lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Sheshbaza na Zerubabeli. Kusudi la kundi hili lilikuwa ni kujenga Hekalu kwanza. Baada ya hatua za kwanza za ujenzi, yaani ujenzi wa msingi , upinzani kutoka nje na ndani ulisimamisha kazi kwa muda wa zaidi ya miaka kumi na nne . Baada ya kusimamishwa kwa kazi ya Hekalu, watu walianza kufuata maslahi yao ya kibinafsi na kujijengea wenyewe majumba mazuri ya kuishi, huku wakisahau kabisa ujenzi wa Hekalu waliouachia njiani. Hapo ndipo Mungu alipomtuma nabii HAGAI kuwarudisha watu wa Yuda katika ujenzi wa Hekalu. Baada ya nabii Hagai, nabii ZEKARIA aliendeleza kazi hiyo, na mwishowe Hekalu likajengwa na kukamilika miaka kadhaa baadaye. Kundi la pili la Waisraeli lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Ezra, ambaye alirudisha usomaji na ufuataji wa torati ya Musa katika taifa. Kundi la tatu lilirudi likiwa chini ya uongozi wa Nehemia, ambaye alirudi kwa lengo la kujenga tena ukuta wa Yerusalemu uliobomolewa.
Pamoja na watu wengi wa Yuda kurudi nyumbani kwao,bado kuna baadhi yao walibaki katika miji ya dola ya Uajemi. Katika kipindi hicho tunakutana na kitabu cha ESTA kikieleza maisha ya watu wa Yuda katika mji mkuu wa dola ya Uajemi. Kitabu kinaeleza jinsi walivyopata kibali na kupata malkia katika nchi isiyo yao. Pamoja na watu wa Yuda kwenda uhamishoni/utumwani kwa muda wa miaka sabini, maisha yao hayakubadilika. Baada ya kurudi katika nchi yao na baada ya kujenga hekalu na mji wao, maisha yao yalirudi kuwa kama yalivyokuwa kabla ya kwenda utumwani. Hapo ndipo Mungu anamtuma nabii MALAKI kuwataka watu wa Yuda kutubu na kumrudia yeye. Mwisho, Malaki anatabiri ujio wa mjumbe atakayemtayarishia Bwana njia, kabla ya siku ya hukumu yake. Hapo ndiyo tamati ya ujumbe wa Agano la kale.