Mika – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA UJUMBE WA NABII MIKA

MAELEKEZO

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.

UTANGULIZI

Ndipo watu kadha wa kadha miongoni mwa wazee wa nchi wakaondoka, wakanena na mkutano wa watu, wakisema, Mikaya Mmorashti, alitabiri katika siku za Hezekia, mfalme wa Yuda; akasema na watu wote wa Yuda, ya kwamba, Bwana wa majeshi asema hivi, Sayuni utalimwa kama shamba lilimwavyo, na Yerusalemu utakuwa magofu, na mlima wa nyumba utakuwa kama mahali palipoinuka msituni. Je! Hezekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa Yuda, walimwua Mikaya? Je! Hakumcha Bwana, na kumwomba Bwana awafadhili; naye Bwana akaghairi, asiyatende mabaya yale aliyoyatamka juu yao? Na sisi tungetenda mabaya makuu juu ya roho zetu.” (Yeremia 26:17-19)

Umewahi kushangaa au kuumia pale uliposikia au kuona mtu anachukua mali ya mtu mwingine kwa nguvu, na mwisho wa siku aliyenyang’anywa mali kwa nguvu hapati haki yake mahali popote? Siyo hivyo tu, umewahi kusikia mtu akipanga kufanya uonevu na akaufanya kwa kuwa uko kwenye uwezo wake? Au umewahi kuona viongozi wa kiserikali ambao wao ndiyo wanatakiwa kusimamia haki katika jamii lakini wanaipotosha?  Na hawaishii kuipotosha tu, bali wao wenyewe wanafanya unyonyaji mkubwa wa watu wanaowatawala?

Au umewahi kuona manabii wakitabiri mambo mazuri kwa wale wanaowapa fedha na wakitabiri mabaya kwa wale wasiowapa kitu chochote? Siyo manabii tu, umewahi kuona viongozi wengine wa kiimani wakifundisha ili kupata fedha? Basi, Mika aliishi katika vipindi hivyo, vipindi vilivyojawa na udhalimu mkubwa katika jamii uliozalishwa na watu wa Mungu kumuacha Mungu na kugeukia kuabudu sanamu kama mataifa mengine.  Katika vipindi hivyo, ndiyo Nabii Mika alitoa jumbe za unabii wake.

Kwa upande mwingine, Mika alitoa jumbe zake wakati Samaria, mji mkuu wa Ufalme wa Israeli, na miji mingi ya ufalme wa Yuda imepigwa kivita, na Yerusalemu imezingirwa na taifa lenye nguvu la Ashuru. Kipindi hiki kilikuwa ni kipindi cha wasiwasi mkubwa ndani ya mji wa Yerusalemu.

Kutokana na miktadha tofauti tofauti, ndiyo maana kitabu hiki kina jumbe za hukumu kwa upande mmoja, na pia kina jumbe za matumaini ya urejesho kwa upande mwingine.

Jumbe za Nabii Mika hazikupotelea hewani, zingine zilitimia na zingine zilifanya kazi yake ya kuwarudisha watu katika njia sahihi za Bwana na ndiyo maana zilikumbukwa hata na watu wa Yuda wakati wa kipindi cha kazi ya kinabii ya nabii Yeremia (Yeremia 26:17-19). Sio hivyo tu, ujumbe wake ulitumiwa na makuhani na waandishi kumjulisha Herode kuhusu sehemu ambayo Masihi alitakiwa kuzaliwa (Mathayo 2:1-11). Kubwa zaidi, ujumbe huu uliandikwa kwa ajili yetu sisi ili tuweze kujifunza kuhusu hukumu za Mungu kwa upande mmoja na kuhusu rehema za Mungu kwa upande mwingine.

MUKTADHA WA KIHISTORIA

Kitabu cha Nabii Mika ni mkusanyiko wa sehemu ya unabii ambao Nabii Mika (au Mikaya) aliutoa kwa ajili ya Samaria (mji mkuu wa ufalme wa Israeli) na Yerusalemu (mji mkuu wa ufalme wa Yuda) katika kipindi ambacho Yothamu, Ahazi, na Hezekia walikuwa wafalme wa Yuda. Hiki ni kipindi kisichopungua muda wa miaka thelathini na mitano, hivyo unabii huu ni sehemu tu ya kile Mika alichokisema juu ya Samaria na Yerusalemu. Kipindi cha kutoka Yothamu, Ahazi hadi Hezekia kinasimuliwa kwa kirefu katika 2 Wafalme 15:32–20:21 na 2 Mambo ya Nyakati 27–32. Na ni katika kipindi hiki ambacho pia Nabii Isaya alifanya kazi yake ya kinabii (tazama Isaya 1:1; 7 na 20).

Jambo kubwa la kujua kuhusu hali ya mataifa haya mawili katika nyakati hizi ni kwamba, kulikuwa na ibada nyingi za sanamu (ibada kwa miungu mingine) zikiendelea, ambazo zilisababisha udhalimu mkubwa/ukwaji wa haki katika jamii. Udhalimu huu ni kama vile rushwa, umwagaji wa damu na watawaliwa kunyimwa haki zao (Mika 3:9-12).

Mfalme wa kwanza wa Yuda katika siku za utumishi wa Nabii Mika alikuwa ni Yothamu. Yothamu alitawala kwa miaka kumi na sita katika ufalme wa Yuda. Yothamu alikuwa mfalme mwema, ingawa chini ya utawala wake watu waliendelea kufanya ibada kwa miungu mingine (2 Wafalme 15:32–38). Katika utawala wake, Bwana alianza kuwatuma Shamu (chini ya uongozi wa Mfalme Resini) na Israeli (chini ya uongozi wa Peka), wakiwa wameungana dhidi ya Yuda katika vita.

Baada ya Yothamu kufa, Ahazi akawa mfalme wa Yuda. Yeye ndiye mfalme wa pili katika siku za Nabii Mika. Kwa kuwa Ahazi alikuwa mfalme aliyetenda mabaya mbele za Bwana, katika utawala wake (2 Mambo ya Nyakati 28:1–4), Yuda ilishambuliwa vikali na muungano wa Israeli (ukiongozwa na Peka) na Shamu (ukiongozwa na Resini). Mataifa haya yalitaka Yuda ijiunge nayo ili kuunda umoja wa kupambana na nguvu kubwa ya ufalme wa Ashuru, ufalme uliokuwa unakua kwa kasi. Mfalme Ahazi wa Yuda alikataa kujiunga nao, jambo lililosababisha Israeli na Shamu kuivamia Yuda vikali (2 Wafalme 16:1–5).

Kutokana na Yuda kupigwa na ushirikiano huu wa Israeli na Shamu kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kupigwa na Waedomu kutoka upande wa kusini-mashariki na Wafilisti kutoka upande wa magharibi, Mfalme Ahazi wa Yuda akaomba msaada kutoka kwa Mfalme Tiglath-pileseri, mfalme wa Ashuru, badala ya kumtumaini Mungu, kama Nabii Isaya alivyokuwa amemsihi (Isaya 7:1–17).

Ashuru iliisaidia Yuda kwa kuwaokoa kutoka kwa maadui zao (hasa kwa kuuangusha kabisa ufalme wa Shamu, uliokuwa na makao makuu yake Dameski[1]), lakini kwa gharama kubwa. Mfalme Ahazi alilazimika kuanza kulipa kodi kubwa kwa mfalme wa Ashuru; akitumia hazina ya Hekalu na ya jumba lake la kifalme, jambo lililoifanya Yuda kuwa chini ya Ashuru (2 Mambo ya Nyakati 28:5–21).

Urafiki wa Mfalme Ahazi na Mfalme Tiglath-pileseri wa Ashuru, aliyemsaidia, ukamfanya aendelee kupotea zaidi katika ibada za sanamu (2 Mambo ya Nyakati 28:22–27; 2 Wafalme 16:10–20) na kufikia kiwango cha kulifunga kabisa Hekalu (2 Mambo ya Nyakati 28: 24-27). Hii ikaifanya watu wa Yuda kuendelea katika ibada za miungu mingi kwa kasi zaidi.

Ufalme/TaifaMakao makuuWafalme wake wakati wa Nabii Mika
IsraeliSamariaPeka >Hoshea >Kuanguka kwa Israeli
YudaYerusalemuYothamu >Ahazi >Hezekia
Shamu (Aramu)DameskiResini >Kuanguka kwa Shamu
AshuruNinawiTiglath-pileseri >Shalmanesa >Sagoni >Senakeribu

Jedwali 1. Majina ya falme na miji yao mikuu na wafalme wake katika kipindi cha kazi ya kinabii ya Nabii Mika.

Baada ya ufalme wa Shamu kuangushwa kabisa, Israeli pia ikiwa chini ya utawala wa ufalme wa Ashuru, yaani walitakiwa kulipa kodi kama ufalme wa Yuda ulivyokuwa unafanya. Hiki kilikuwa ni kipindi cha mfalme Hoshea (Mfalme aliyefuata baadala ya mfalme Peka). Baada ya kulipa kodi kwa muda, mfalme Hoshea akaacha kulipa kodi kwenye ufalme wa Ashuru na badala yake akataka kutengeneza ushirikiano na Misri ili ajiepushe na ufalme wa Ashuru. Kutokana na uasi huo, ufalme wa Ashuru chini ya mfalme Shalmanesa ukauzingira Samaria kwa miaka mitatu na hatimaye Samaria ukaanguka na watu wakapelekwa utumwani (2 Wafalme 17:1-6) kama nabii Mika alivyotabiri (Mika 1:2-7).[2]

Na kwa kuwa kuhamisha watu ndiyo ulikuwa utamaduni uliofanywa na ufalme wa Ashuru, watu wa mataifa mengine yaliyopigwa wakahamishiwa Samaria, kama waisraeli waliokuwa Samaria walivyohamishiwa katika maeneo mengine. Watu hawa waliohamishwa, walioana na Waisraeli wachache waliokuwa wamebaki katika Samaria. Muunganiko huu ndio ukaja kuzaa Wasamaria.

Mwanzoni, imani ya Wasamaria ilihusisha mchanganyiko wa imani : “Walimcha BWANA, lakini wakati huohuo waliitumikia miungu yao wenyewe” (2 Wafalme 17:33). Hata hivyo, baadaye Wasamaria waliikana ibada ya miungu mingi  na wakafuata mafundisho ya Musa, imani ya kumwabudu Mungu mmoja tu. Hii ndio maana mpaka leo wasamaria wanaamini vitabu vitano vya Musa pekee ndiyo neno la Mungu.

Baada ya Ahazi, mwanawe aitwaye Hezekia ndiye aliyefuata kuwa mfalme katika Yuda. Huyu ndiye mfalme wa tatu katika kipindi cha utumishi wa nabii Mika. Hezekia alikuwa mfalme aliyefanya mema machoni pa Bwana (2 Wafalme 18:3). Hezekia alipoanza kutawala alifanya uamsho mkubwa katika Yuda. Alifungua tena na kulitakasa Hekalu, ambalo milango yake ilikuwa imefungwa na baba yake Ahazi (2 Mambo ya Nyakati 28:24; 29:3–5). Akarejesha ibada kama Mungu alivyoagiza kwa kurejesha utoaji wa dhabihu za kila siku, na hatimaye kuadhimisha Pasaka ya kipekee ambayo watu wa Yuda pamoja na mabaki ya ufalme wa kaskazini (Israeli) walialikwa kuhudhuria (2 Mambo ya Nyakati 29:3–36; 30:1–27). Si hivyo tu,bali alikomesha ibada ya sanamu kwa kuondoa mahali pa juu, kubomoa nguzo za ibada na maashera, na hata kuvunja nyoka wa shaba iliyotengenezwa na Musa, kwa kuwa watu walikuwa wameanza kuitolea uvumba na kuiabudu (2 Wafalme 18:4; 2 Mambo ya Nyakati 31:1).

Kumbuka kwamba, Baba yake Hezekia, yaani Ahazi alikuwa anatoa kodi katika ufalme wa Ashuru kwa kuwa ulimsaidia katika vita. Sasa, Hezekia kwa kuwa alikuwa anamtegemea Mungu, akaacha kulipa kodi kwa mfalme wa Ashuru ambayo Baba yake Ahazi alikuwa anailipa (2 Wafalme 18:7). Kutokana na kufanya hivyo, mfalme Senakeribu, mfalme wa Ashuru akavamia na kuiteka miji mingi ya Yuda iliyokuwa imezungushiwa kuta (2 Wafalme 18:13) na akaweka makao yake katika mji wa Lakishi ili kuukabili mji Yerusalemu. Kwa kuona hivyo, Hezekia akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru ili kukubali kushindwa na akalipa fedha na dhahabu kutoka katika Hekalu na hazina ya jumba lake. Pamoja na kufanya hivyo, mfalme Senakeribu, mfalme wa Ashuru akatuma mjumbe kumtisha Hezekia na watu wa Yerusalemu kwamba atavamia na sio Misri wala Mungu wao atakayeiokoa Yerusalemu dhidi yake (2 Wafalme 18:14-37).

Baada ya vitisho hivyo, Hezekia akajinyenyekesha katika maombi huku akimshirikisha Nabii Isaya (2 wafalme 19:1-19). Mungu akajibu maombi yake kwa kuliangamiza jeshi la Waashuru usiku kupitia malaika, jambo lililomlazimu Senakeribu Mfalme wa Ashuru kurudi Ninawi (2 Wafalme 19:20–37). Wakati jeshi la Ashuru limejipanga kuujia Yerusalemu Nabii Mika ndiyo akatoa unabii wa matumani ya urejesho (Mika 4-5).

Baadaye, Hezekia aliugua sana na kupitia nabii Isaya, Mungu alimtangazia kwamba atakufa. Lakini baada ya maombi yake, Mungu akamwongezea miaka kumi na mitano ya kuishi (2 Wafalme 20:1–11). Katika miaka hiyo ya nyongeza, wajumbe kutoka katika ufalme wa Babeli walifika Yerusalemu baada ya kusikia kuhusu kupona kwake. Hezekia aliwaonyesha kwa majivuno hazina zote za jumba lake la kifalme na za Hekalu. Isaya akamkemea na kutabiri kwamba siku moja hazina hizo, pamoja na baadhi ya wazao wake, watakwenda utumwani Babeli, hii ilikuwa ni mara ya kwanza ya utabiri wa uhamisho wa Babeli (2 Wafalme 20:12–21; Isaya 39:1–8).

Hizi ndiyo nyakati ambazo, Nabii Mika alitoa ujumbe wake kwa Samaria na Yerusalemu.

MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOSOMA UJUMBE HUU

Kama ilivyo vitabu vingine vya manabii ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo unaposoma ujumbe wa kitabu hiki.

  1. Vitabu vya manabii kikiwepo kitabu hiki, vimeandikwa kwa mtindo wa ushahiri, ambao unatumia mtindo wa usambamba kufikisha ujumbe. Usambamba kwa upande mmoja maana yake ni kurudia ujumbe ule ule kwa maneno mengine. Mfano “sikiliza, Ee dunia, na vyote vilivyomo” ni marudio ya maneno “Sikilizeni, enyi watu wa kabila zote” (Mika 1:2). Kwa hiyo, siyo kila sentensi katika unabii huu inaelezea ujumbe mpya.
  2. Vitabu vya manabii kwa kuwa vimeandikwa kwa mtindo wa ushahiri, vina matumizi makubwa ya lugha ya picha. Kwa hiyo sio kila kitu kinachosemwa kina maana ya moja kwa moja. Kuelewa lugha ya picha iliyotumika kunasaidia kuelewa ujumbe husika. Mfano Nabii Mika katika 7:1 anaposema;

Ole wangu!

Maana mimi ni kama hapo walipokwisha kuyachuma matunda ya wakati wa hari, kama zabibu zichumwazo baada ya mavuno;

hapana shada la kuliwa;

roho yangu inatamani tini iivayo kwanza,” anatumia lugha ya picha kujilinganisha na mtu ambaye amekwenda shambani baada ya mavuno ya wakati kupita. Mtu akienda wakati huo hapati matunda ya kuliwa hata kama roho yake inatamani. Hivyo, ni muhimu kuelewa lugha ya picha inachoelezea ili uweze kuelewa ujumbe. Usipoelewa maana ya lugha ya picha iliyotumika ni vigumu kuelewa ujumbe husika.

  • Ujumbe wa vitabu vya manabii pamoja na kuwa kwenye kitabu kimoja mara nyingi huusisha jumbe mbalimbali zilizotolewa katika nyakati tofauti tofauti. Mfano Ujumbe wa Nabii Mika katika sura ya kwanza mstari wa pili mpaka wa saba (1:2-7) ulitolewa wakati tofauti na ujumbe wa mstari wa nane mpaka kumi na sita wa sura ya kwanza (1:8-16). Sura ni moja, lakini ujumbe ulitolewa nyakati tofauti tofauti. Hivyo, ni muhimu kuzingati jambo hili unaposoma kitabu hiki.

MPANGILIO WA WARAKA

MAELEZOMAANDIKOMAELEZO
Awamu ya kwanza ya matangazo ya hukumu1:1-7Tangazo la hukumu juu ya Samaria na Yerusalemu
1:8-16Tangazo la hukumu juu ya miji ya Yuda
2:1-11Tangazo la hukumu juu ya wanyonyaji
2:12-13Tumaini la kwanza la urejesho
Awamu ya pili ya matangazo ya hukumu3:1-4Tangazo la hukumu juu ya Viongozi wa kiserikali
3:5-8Tangazo la hukumu juu ya manabii wa uongo
3:9-12Tangazo la hukumu kwa viongozi wote kwa ujumla
Tumaini la pili la urejesho4:1-8Urejesho wa ujumla
4:9-5:9Hali ya hatari ya sasa na ahadi ya urejesho wa baadae
5:10-15Hukumu ya kusafisha taifa
Awamu ya tatu ya matangazo ya hukumu6:1-16Kesi ya Mungu dhidi ya watu wake
7:1-7Malalamiko ya Nabii Mika juu ya Yerusalemu
Hitimisho7:8-20Tumaini la tatu la urejesho

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI

Kitabu cha Nabii Mika kinaanza na utangulizi unaoeleza chanzo cha ujumbe huu, jina la Nabii aliyetoa ujumbe na wakati wa kutolewa kwa jumbe zake (1:1).

Mara tu baada ya utangulizi huo mfupi, kitabu hiki kinafuatiwa na awamu ya kwanza ya matangazo matatu tofauti tofauti ya hukumu. Tangazo la kwanza la hukumu ya Mungu ni ushairi unaotangaza ujio wa Mungu juu ya dunia kwa ajili ya hukumu ya Samaria na Yerusalemu. Ushairi unaanza kwa kuwaita watu wote kusikiliza na kuangalia ujio wa kutisha wa Mungu juu ya dunia kutoka mahali pake (1:2-4). Ujio huu wa kutisha ni kwa ajili ya hukumu ya mji wa Samaria. Mungu anasema utauharibu mji wa Samaria kwa kuvunja misingi yake, kuta zake, sanamu zake na zawadi zilizopatikana katika ibada za sanamu, na mwisho mji huu utakuwa kama shamba lililosafishwa kwa ajili ya kupandwa mizabibu (1:5-7).

Unabii huu ulitimia katika Samaria wakati wa utawala wa Hoshea. Israeli ilipigwa na mji wa Samaria ulizingirwa kijeshi na ufalme wa Ashuru kwa muda wa miaka mitatu. Mwisho wa miaka hiyo mji ukaangamia na wakazi wake wakapelekwa utumwani (tazama, 2 Wafalme 17:1-23). Na huu ndio ukawa mwisho kabisa wa taifa la Israeli.

Baada ya muda tena, Nabii Mika akapata ujumbe kutoka kwa Bwana. Ujumbe huu unaanza na tangazo la maombolezo, ambalo ni tangazo la pili la hukumu ya Mungu katika kitabu hiki. Mika anasema anaomboleza kwa sababu ya kuangamia kwa mji wa Samaria. Kwa nini anaomboleza kwa ajili ya kuanguka kwa mji wa Samaria? Kwa sababu hukumu hiyo ya Mungu (…jeraha zake…) juu ya Samaria haiwezi kutenguka (…haziponyekani…) na inakaribia kufika na Yerusalemu pia (1:8-9). Kwa kucheza na maneno,[3] Mika anaiita miji sita ya Yuda kuomboleza kwa sababu ya hukumu ijayo, huku akiita kila mji kufanya mambo ambayo ni kinyume na maana ya jina la mji husika. Mfano jina Shafiri lina maana ya “kuwa mzuri,” lakini Mika anawaita wakazi wa mji huo kupita katika hali ya uchi na aibu. Jina Saanani lina maana ya “kutoka nje” lakini Mika anasema wakazi wake hawatatoka nje. Hukumu kwa hii mji sita ya Yuda ni uhakikisho wa ujio wa hukumu hii mpaka Yerusalemu, mji mkuu wa ufalme wa Yuda (1:10-12). Tena, Mika anaiita miji mingine mitano ya ufalme wa Yuda kwenye maombolezo, kwa sababu ya hukumu hiyo inayokuja ambayo itafika mpaka Yerusalemu; ambayo kilele chake ni kwenda utumwani (1:13-16).

Unabii uliopo kwenye maombelezo haya ya Nabii Mika yalitimia katika kipindi cha ufalme wa mfalme Hezekia, pale Ashuru ilipovamia miji ya Yuda na kuiteka na hatimaye kuweka kambi yao katika mji wa Lakishi[4] kwa ajili ya kujipanga kuivamia Yerusalemu (2 Wafalme 18:13).[5]

Katika wakati mwingine[6] Nabii Mika akapata unabii, unabii wa kuwatangazia hukumu wenye nguvu katika jamii, ambalo ndiyo tangazo la tatu la hukumu ya Mungu katika kitabu hiki. Mika anatangaza hukumu kwa wenye nguvu katika jamii kwa kuwa wanapanga uovu vitandani mwao na wanautelekeleza, kwa kuwa uko katika uwezo wao. Wanyafanya shughuli za unyonyaji, kama vile kupokonya nyumba au mashamba kutoka kwa wanyonge. Bwana anasema amepanga jambo baya juu yao ambalo hawatalikwepa na litapelekea maombelezo makubwa katikati yao (2:1-5). Baada ya hapo Mika ananukuu ukinzani wa wenye nguvu (au manabii wao) wakimkataza yeye kutabiri ubaya juu yao kwa kwa kusema ubaya hautawapata (2:6). Bwana anajibu kupitia Mika, uvumilivu wake umefika kikomo na yeye ndiye atakayetenda haya (yaani, hukumu), lakini kwa wale waendao kwa unyoofu maneno yake yanawafaa (2:7). Baada ya hapo, Bwana kupitia nabii Mika anathibitisha unyonyaji wao kwa kutaja mambo wanayofanya kwa wanyonge (2:8-9). Baada ya uthibitisho huo, anatangaza hukumu yao tena (2:10), huku akimaliza kwa kuonyesha kwamba watu hawa wanatabia ya kuwapokea manabii wa uongo, wanaowatabiria kuhusu mvinyo na kileo (2:11).

Baada ya matangazo haya matatu ya hukumu, Mungu akatangaza ahadi ya urejesho wa mabaki wa Israeli. Mabaki ya Yakobo Mungu atawakusanya pamoja na utawaongoza kutoka chini ya utumwa wakiwa na mfalme wao (2:12-13).

Baada ya awamu hiyo ya kwanza ya matangazo matatu ya hukumu yaliyohitimishwa na tangazo la tumaini la urejesho (1:1-2:13), Kitabu hiki kinafuatiwa na awamu ya pili ya matangazo mengine matatu ya hukumu ya Mungu juu ya viongozi wa taifa la Yuda (3:1-12) na kufungwa na matangazo ya matumaini ya urejesho (4:1-5:15).

Katika matangazo haya, kila tangazo lina sehemu mbili. Sehemu moja ni ya kuelezea uovu unaofanywa na viongozi (tuhuma), na sehemu ya pili ni tangazo la aina ya hukumu inayowasubiri viongozi husika. Katika tangazo la kwanza, viongozi wa kiserikali katika ngazi mbalimbali wanatuhumiwa kwa unyonyaji. Kwa kutumia lugha ya picha ya binadamu anayekula binadamu wengine, Mungu anaonyesha jinsi wanavyowatesa watu wake. Hukumu yao viongozi hawa ni kutokusikiwa na Bwana pale watakapomuomba (3:1–4).

Katika tangazo la pili, manabii wanatuhumiwa kuwakosesha watu wa Mungu kwa kutabiri amani kwa yule anayewapa kitu cha kula na kutabiri vita kwa yule asiyewapa kitu. Hukumu yao ni kutokupata ujumbe kutoka kwa Bwana. Tofauti na hao, Mika yeye amepokea ujumbe kutoka kwa Bwana na anautoa kwa Israeli (3:5–8).

Katika tangazo la tatu, viongozi wa kiserikali wa ngazi mbalimbali wanatuhumiwa kujenga mji wa Yerusalemu kwa gharama ya damu. Mbali na hayo, makuhani wenyewe hufundisha ili wapate malipo, na manabii hutoa unabii ili wapate fedha. Kutokana na maovu hayo, hukumu ya Mungu itakuwa ni kuangamiza kabisa mji wa Yerusalemu (3:9–12).

Baada ya awamu hii ya pili ya matangazo ya hukumu ya Mungu, Mungu anatoa ujumbe wa matumaini juu ya Yerusalemu baada ya tangazo la kuangamizwa kwake katika 3:12. Ujumbe huu wa matumaini inawezekana kabisa ulitolewa na Nabii Mika wakati Yerusalemu umezingirwa na Senakeribu Mfalme wa Ashuru wakati wa mfalme Hezekia.[7]

Unabii huu wa urejesho unaanza na tangazo la urejesho utakaotokea katika siku za mwisho. Katika siku hizo, Bwana atauinua kwa umuhimu Mji wa Yerusalemu, kiasi kwamba watu wa mataifa mengine watakwenda huko kutafuta mafundisho/sheria ya Mungu na kujitiisha chini ya haki yake, ambayo itageuza silaha za vita kuwa nyenzo za kilimo na hivyo kusababisha usalama wa hali ya juu (4:1-5). Katika hiyo,Bwanaatawakusanya watu wakealiowatesa na kuwafukuzia katika mataifa mengine na kuwafanya kuwa taifa lenye nguvu, huku yeye akiwa mfalme wao (4:6-8).

Baada ya mwanzo huo, ujumbe wa urejesho unaingia kwenye hatua nyingine. Kwa mara tatu Nabii Mika anaeleza hali ya hatari inayoikabili Yerusalemu kwa sasa na anatangaza ukombozi wa Mungu wa wakati ujao. Kwanza, anasema kwa sasa watu wa Yerusalemu wanalia kama mwanamke mwenye uchungu kwa sababu ya hatari iliyoko mbele yao ambayo hakuna mfalme wala mshauri wa kuwasaidia. Ni kweli wanastahiri kulia kiasi hicho kwa kuwa watatolewa katika mji wao wa Yerusalemu na kupelekwa utumwani Babeli, lakini mwisho wa siku Bwana atakwenda kuwakomboa (4:9-10). Pili, anasema kwa sasa pia mataifa mengi wamejikusanya kinyume na Yerusalemu, lakini hawajui mawazo ya Bwana na kusudi lake la kuwakusanya pamoja. Bwana amewakusanya ili baadae Yerusalemu aweze kuwaponda ponda maadui hao na hatimaye Yerusalemu utachukua nyara za vita na kuziweka wakfu kwa Bwana (4:11-13). Tatu, anasema kwa sasa wakazi wa Yerusalemu wajipange vikosi vikosi kupigana na adui zao ambao wamewazingira. Pamoja na kujikusanya vikosi vikosi dhidi ya maadui zao, watapigwa na mfalme wao atapigwa kwa aibu. Pamoja na kupigwa, Mungu anaahidi kwamba baadaye kupitia Bethlehemu Efrata, ambao ni mji mdogo miongoni mwa miji ya Yuda, atatokea mtawala. Mtawala huyu ana asili ya kale, atawachunga Israeli kwa nguvu na mamlaka ya Mungu, na  atakuwa mkuu hadi miisho ya dunia (5:1-4).[8] Yeye atakuwa amani ya Israeli na ikiwa Ashuru itawavamia, viongozi wa kimungu watakwenda dhidi ya Ashuru na kuiharibu, na hivyo ndivyo mtawala huyu atakavyowaokoa (5:5-6). Na wale wa Israeli watakaobaki kwenye mataifa, nje ya nchi yao, watakuwa wengi kama umande wa Mungu na watakuwa na nguvu kama simba katikati ya wanyama wa msituni. Hivyo ndivyo Israeli itakavyowashinda maadui zake na kuwaangamiza kabisa (5:7-9). Mwisho wa sehemu hii ya ujumbe wa urejesho, Mungu anatangaza hukumu ya kusafisha taifa lake, hukumu yenye lengo la kurejesha Israeli katika kumtumaini Mungu tu. Mungu anatangaza kuondoa mambo manne: uwezo wa kufanya vita, miji na ngome zinazotegemewa, uchawi, na kila aina ya miungu/sanamu (5:10-15).

Mara baada ya tangazo la pili la urejesho kuisha, ujumbe wa Nabii Mika unakwenda kwenye awamu ya tatu ya matangazo ya hukumu. Awamu hii, tangazo la hukumu linawasilishwa na Mika kama mlalamikaji kwa niaba ya Mungu katika mahakama. Kwa kuita milima kuwa mashahidi wa kesi hii, Mungu kupitia Nabii Mika analalamika kwa kuwauliza watu wa Israeli kama kuna namna yoyote yeye hajawa mwaminifu katika Agano lake; huku akielezea jinsi alivyowaokoa kutoka Misri (6:1–5). Namna hii ya kulalamika inaonyesha kwamba Israeli hawajawa waaminifu kwa upande wao katika Agano. Kwa kuelewa malalamiko haya, Israeli wanajitetea kwamba wao wamekuwa waaminifu; ndiyo maana wanamuuliza Mungu: Je, watoe dhabihu gani zaidi ili aone kama wamekuwa waaminifu? (6:6–7). Nabii Mika anajibu kwamba Mungu anataka kile ambacho wanakijua tayari; kuishi kwa haki, huruma na kuhusiana na yeye kwa unyenyekevu, na si kuongeza dhabihu yeyote (6:8).

Baada ya kuwaonyesha kile Mungu anataka, Nabii Mika anawaonyesha kwa mifano halisi wakazi wa Yerusalemu jinsi wanavyoishi kinyume na kile Mungu anataka. Kwa sababu bado hii ni kesi, hivyo haya maovu ndiyo tuhuma husika za Mungu juu ya mji wa Yerusalemu (6:9–12). Kutokana na Israeli kupatikana na hatia ya hayo maovu, Mungu anatangaza hukumu juu ya Yerusalemu (6:13–15). Kesi hii inafikia tamati kwa muhtasari unaoeleza sababu ya hukumu na tangazo la hukumu yenyewe (6:16).

Awamu hii ya tatu ya matangazo ya hukumu inahitimishwa na malalamiko ya Nabii Mika juu ya hali mbaya inayoendelea katikati ya watu wa Mungu. Nabii Mika anatoa maelezo ya hali mbaya inayoendelea katika jamii, hali inayohusisha umwagaji damu, rushwa na uadui katikati ya ndugu wa familia (7:2–6). Malalamiko haya Nabii Mika anayahitimisha kwa kauli ya matumaini yake kwa Bwana (7:7).

Ujumbe wa kitabu cha Nabii Mika unatamatishwa na ujumbe wa matumani ya urejesho baada ya hukumu. Hitimisho hili linaanza na ushairi unaosemwa na mji wa Yerusalemu. Mji wa Yerusalemu unawaambia maadui zake wasifurahi kuanguka kwake, ambako ni hukumu ya Bwana, kwa kuwa Bwana ataurejesha na hivyo maadui wake watapata aibu kwa dhihaka walizofanya juu yake (7:8-10). Baada ya hapo, Nabii Mika anautangazia mji wa Yerusalemu kwamba urejesho unakuja. Kuta zake zitajengwa, mipaka yake itatanuliwa na mabaki ya watu wake watarejeshwa huku sehemu iliyobaki ya dunia itakuwa ukiwa (7:11-13).

Baada ya tangazo hilo, Mika anaomba kwa Mungu. Anamuomba Mungu awe kama mchungaji juu ya kondoo; anaomba Mungu awatawale watu wake na kuwaongoza (7:14). Bwana anajibu kwamba atafanya, na atafanya kama ilivyokuwa wakati anawatoa utumwani Misri (7:15). Kwa kuwa Bwana atafanya kama siku ile aliyowatoa utumwani Misri, Mika anasema mataifa watayaona matendo makuu ya Bwana na kuzionea aibu nguvu zao (7:16-17). Mwisho kabisa Nabii Mika anamtukuza Mungu kwa sababu ya tabia yake ya msamaha, hata baada ya hukumu. Moyo wake wa kuleta urejesho hata baada ya hukumu (7:18-20).

MAELEZO YA CHINI


[1] Kuanguka kwa ufalme wa Shamu (2 Wafalme 16:9), ambao ulikuwa na makao yake makuu Dameski ilikuwa ni utimilifu wa unabii wa nabii Amosi alioutoa miaka iliyopita (Amosi 1:5).

[2] Pamoja na kwamba mfalme Shelmanase ndiye aliyeuzingira mji wa Samaria, mfalme Sagoni aliyekuja baada yake ndiye alimalizia kazi ya kuuangusha mji na kuwapeleka watu utumwani.

[3] Kucheza huku kwa maneno mfano wake ni sawa na kusema , Kwa wakazi wa Dar es salaam (ikiwa na maana ya bandari salama) hawatakuwa salama. Ni kutangaza hukumu kwa kutumia maana ya majina ya miji huku akitaja hukumu kinyume na maana ya jina husika la mji.

[4] Katika ufalme wa Yuda, Mji wa Lakishi ulikuwa mji wa pili kwa umuhimu, Wa kwanza ulikuwa ni Yerusalemu na Lakishi ndio ulifuata. Kutekwa kwa mji wa Lakishi ilikuwa ni tishio kubwa kwa Yerusalemu.

[5] Huu ndio wakati ambao hata mji wa Morashti (Moresheti), mji alikozaliwa na kuishi nabii Mika, ulianguka na watu wake wakafanywa mateka, kama Mika alivyotabiri katika maombolezo yake.

[6] Ni vigumu kujua ni wakati gani unabii huu ulitolewa, lakini wanataaluma wanapendekeza kipindi cha mfalme Ahazi.

[7] Mika 4:9, 11; 5:1 ni dalili kwamba unabii huu ulitololewa kipindi ambacho Yerusalemu umezingirwa.

[8] Unabii wa Mika 5:2 ndiyo unabii uliotumiwa na makuhani na waandishi kumjulisha Herode kuhusu sehemu ambayo Masihi alitakiwa kuzaliwa (Mathayo 2:1-11)

Unakuja hivi karibuni……