Wakati wa nyuma nilikuwa najiuliza sana bila kupata majibu kwamba Mungu yeye alikuwa wapi wakati anaumba mbingu na Nchi? Swali langu hili lilitokana na uelewa wangu wa jumla kwamba Mungu enzi/makao yake yasioyoonekana kwa macho yako katika Mbingu Kama Biblia inavyosema kweli hii katika vitabu vingi kama Zaburi 103:19, 11:4, Isaya 66:1-2,Mathayo 5:34, Matendo 7:49.
Kwa uelewa wangu huu, nilipokuwa nasoma Mwanzo 1:1 “Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na Nchi” nilikuwa najiuliza kama Mungu ana makazi/enzi katika Mbingu (Mbinguni) wakati anaumba hapo anapokaa (Mbingu) yeye alikuwa anakaa wapi?
Lakini sasa nashukuru Mungu kwa wale walionifundisha namna gani ya kuepuka maswali kama haya na kupata majibu sahihi unapopata swali kama hili. Mmabo mawili hapa chini yatakusaidia kupata majibu ya swali hili..
1. Maneno yana maana kutokana na mahali yametumika. Neno katika lugha linaweza kuwa moja lakini likawa na maana tofauti tofauti kutokana na mahali limetumika. Mfano katika Kiswahili neno “Nyumba ndogo” ni neno moja lakini lina maana tofauti tofauti kutokana na mahali neno hili lilipotumika. Nikisema, “Nimenunua Nyumba ndogo Tanga” na Nikisema, “Nimepata nyumba ndogo Tanga”, hizi sentensi mbili zinamaana tofauti kabisa pamoja na kwamba neno moja “Nyumba ndogo” limetumika katika sentensi zote mbili.
Hivyo hivyo katika Biblia maneno yanaweza kufanana lakini yasiwe na maana sawa. Ukiwa na maana jumuishi kichwani utachanga mambo kama mimi nilivyokuwa nachanganya mambo. Hii ndio maana sio vizuri kuchanganya maandiko, kila sehemu ya maandiko isomwe katika muktadha wake, pia kila sehemu ya maandiko ieleweke vizuri kabla ya kuchanganywa na sehemu nyingine ya maandiko.
Hili lilinipelekea kuelewa kwamba Neno mbingu sio kila wakati linamaanisha enzi ya Mungu/Makazi ya Mungu yasiyoonekana kwa macho wakati Mwingine linamaanisha Anga tunaloliona juu yetu. Mwanzo 1 neno Mbingu linamaana ya “Anga tunaloliona juu” kama Mungu anavyotoa jina yeye mwenyewe katika Mwanzo 1:6-8 “Mungu akasema, “Anga liwe katikati ya maji, liyatenge maji sehemu mbili.” Mungu akalifanya anga, akayatenga maji yaliyo juu ya anga na yale yaliyo chini ya anga hilo. Ikawa hivyo. Mungu akaliita anga “Mbingu.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya pili.”
Hivyo katika Biblia neno Mbingu au Mbinguni linaweza kumaanisha anga linaloonekana juu au enzi/makao ya Mungu yasiyoonekana kwa macho, kutokana na mahali lilipotumika au linaweza kuwa na maana zote mbili kwa wakati mmoja.
Maana zote mbili kwa wakati mmoja limetumika katika Kutoka 16:4 “Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Mimi nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Kila siku watu watatoka na kukusanya chakula cha siku hiyo. Kwa njia hii nitawajaribu nione kama watazifuata sheria zangu au hawatazifuata.”
Hivyo Mwanzo 1 haielezi Uumbaji wa enzi ya Mungu (Makao yasiyoonekana kwa macho) bali inaeleza uumbaji wa anga tunaloliona juu, japo Katika Isaya Mungu anasema hata enzi yake isiyoonekana kwa macho ameiumba (Isaya 66:1-2) na hizo pia hazimtoshi (1 Wafalme 8:27).
Jibu rahisi la swali langu juu ni kwamba Mungu alikuwa katika Mbingu (Mahali pa enzi yake pasipoonekana kwa macho) wakati anaumba Mbingu (Anga tunaloliona juu).
Kanuni hii ni Muhimu sana, itakusaidia kutokuwa na maana Jumuishi ya maneno bali kila neno utataka kulielewa sawa sawa lilivyotumika katika muktadha.
2. Biblia inatoa majibu ya maswali mengi na inaonyesha maswali ya majibu inayoyatoa. Ukijiuliza swali kabla hujaenda kutafuta majibu kwenye Biblia jiulize, Je Biblia inaonyesha swali hilo?. Ukikosea swali jua utakosea jibu. Mimi nilifikiri kuwa kila swali ninalojiuliza basi Biblia imejibu kwa sababu tu Mungu anajua yote na lazima atakuwa ametoa majibu ya maswali yangu yote katika Biblia.
Biblia inajitosheleza lakini haiko kujibu kila swali ninalojiuliza. Biblia inafundisha kwamba kila kitu tunachokiona na tusichokiona kimeumbwa na Mungu lakini haitufundishi namna gani kila kitu kimeumbwa. Biblia inafundisha malaika ni viumbe lakini haijatufundisha Mungu aliwaumba wakati gani na kwa namna gani.
Hivyo Biblia inatufundisha namna ya uumbaji wa Mbingu “Anga tunaloliona juu” lakini haitufundishi namna ya uumbaji wa Mbingu “Mahali pa enzi ya Mungu pasipoonekana kwa macho”.