Niende Kanisa Gani?

Kama umewahi kujiuliza wakati wowote kwamba, “Niende kanisa gani?” basi chukua muda wako kusoma na kutafakari kwa kina ujumbe wa makala hii. Pamoja na kwamba swali hilo si sahihi sana, kwa kuwa kanisa si mahali (au jengo) ambako watu wanatakiwa kwenda, bali ni jamii ya waamini ambayo mwamini anatakiwa kuwa sehemu, Lakini kwa sababu hivi ndivyo watu wengi huwa wanajiuliza, basi tutajifunza kwa kujiuliza swali kwa namna hiyo.

Lengo la makala hii ni kumsaidia mwamini kufanya maamuzi sahihi pale anapotaka kuchagua ushirika katika jamii fulani ya waamini. Kwa mtu ambaye hajamwamini Yesu Kristo makala hii haitakuwa na msaada kwake. Wito wetu kwake ni yeye kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu.

Tunaishi katika nyakati ambazo kumekuwa na utitiri wa madhehebu katika imani ya Kikristo ambayo yamekuwa na utofauti mkubwa kabisa katika mambo ya imani. Ukiacha utofauti wa dhehebu moja na jingine, hata ndani ya dhehebu moja, jamii ya waamini waa eneo moja inaweza kuwa tofauti kabisa kiimani na jamiii nyingine ya waamini ya sehemu nyingine. Pamoja na mababa wa Kanisa kutupa ukiri wa imani ya Nikea usemao kwamba Kanisa ni moja, takatifu, katoliki, na la kitume, ambao tunauamini mpaka sasa, lakini katika “damu na nyama” kanisa limekuwa na mgawanyiko mkubwa.

Kanisa ni moja, maana yake ni kwamba kanisa ni mwili mmoja wa Kristo usiogawanyika. Kanisa ni takatifu kwa kuwa limetakaswa kwa damu ya Kristo. Kanisa ni katoliki, maana yake linawahusisha watu wote duniani walioamini (Neno Katoliki lina maana ya ulimwengu wote). Nalo ni la kitume kwa kuwa limejengwa juu ya msingi wa mitume.

Lakini pia pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo kutuombea kwa Baba kwamba tuwe na umoja (Yohana 17:21-23), uhalisia unatuonyesha kwamba kanisa limegawanyika sana. Jambo hili halijaanza leo wala baada ya kuzaliwa kwa Uprotestanti; lilikuwepo tangu karne za awali za ukuaji wa imani yetu, lakini ni ukweli usiopingika kwamba katika nyakati hizi changamoto imekuwa kubwa zaidi.

Kutokana na changamoto kuwa kubwa, waamini (au wale wanaojiita waamini) wamekuwa wakichagua kuwa sehemu ya jamii ya waamini bila kuwa na mwongozo mzuri. Wengi wamekuwa wakichagua kutokana na jina la dhehebu, jambo ambalo si baya kabisa, lakini kama tulivyosema hapo juu, utofauti wa imani umekuwa dhahiri hata ndani ya dhehebu moja. Hivyo, njia hii kwa sasa haiwezi kuwa salama kabisa. Wengine wamekuwa wakichagua jamii ya waamini kwa kuangalia idadi ya watu wanaokusanyika katika makusanyiko ya kanisa husika, jambo ambalo ni hatari. Wengine wamekuwa wakichagua kwa sababu mahitaji yao ya kimwili yanaahidiwa kupatiwa suluhisho na “wahubiri wa kanisa” husika, jambo ambalo ni hatari pia. Na wengiwe wamekuwa wakichagua jamii ya waamini kwa sababu ya kurithi kutoka kwa wazazi, jambo ambalo sio sawa pia. Na mwisho, wengine wamekuwa wakichagua jamii ya waamini kutoka na ukaribu wa sehemu kanisa linapokusanyika, hili nalo sio salama kabisa.

Hivyo, kama wewe ni mwamini na unataka kuchagua uwe sehemu ya ushirika gani wa mahali pamoja, kwa sababu unataka kukua katika imani basi maeneo yafuatayo yatakusaidia kufanya maamuzi;

  1. Biblia ndio msingi mkuu wa imani.
  2. Ubatizo na meza ya Bwana.
  3. Uongozi wa Kanisa.
  4. Kusanyiko la waamini
  5. Ushirika wa waamini

1. Biblia ndio msingi mkuu wa imani.

Kabla hujaamua kuwa mshirika wa kanisa lolote la mahali pamoja, basi jihakikishie kwamba kanisa hilo linaamini kwamba Biblia ndiyo msingi mkuu wa imani. Ni ukweli usiopingika kwamba makusanyiko mengi hukiri kwamba Biblia ndiyo msingi mkuu wa imani yao, lakini katika uhalisia ukiri wao hupingana na mwenendo wao. Utajuaje kama ukiri huo ni wa kweli?

Moja, angalia kama katika makusanyiko Biblia inafundishwa kwa uchambuzi. Yaani, katika jumla ya makusanyiko yote ya wiki, je Biblia inafundishwa kwa uchambuzi au la? Kwa ufafanuzi zaidi, kama umehudhuria makusanyiko kadhaa ya “kanisa” husika lakini hakuna hata wakati mmoja sura nzima ya kitabu chochote cha Biblia inasomwa na kuchambuliwa, basi hiyo ni dalili kwamba Biblia siyo msingi wa imani wa “kanisa” husika, hata kama kusanyiko hilo linadai vinginevyo.

Pamoja na hilo, kama kila kusanyiko uliloenda mada mpya ilifundishwa, yaani hakuna mfululizo wowote wa mafundisho, basi hiyo ni dalili kwamba kanisa husika halijaweka Biblia kuwa ndiyo msingi mkuu wa imani. Zaidi ya hapo, ukienda kwenye makusanyiko kadhaa ukaona “mhubiri” au “wahubiri” wanaongea tu uzoefu wao, au hekima zao, au wanatabiri tu muda wote, basi hiyo ni dalili kwamba Biblia siyo msingi wa imani katika kusanyiko hilo.

Pili, mbali na kufundishwa, sikiliza kwa makini jinsi waamini wa kanisa husika, hasa viongozi wa kanisa, wanavyozungumza kuhusu Biblia. Ukiona waamini wa kusanyiko husika wanaizungumzia Biblia kama kitabu ambacho hakijitoshelezi, au kina maneno yaliyopitwa na wakati, au kina makosa mengi, au kina matatizo fulani; lakini mapokeo ya kanisa, au neno la nabii, au la mtume linaonekana kuwa ndilo neno hai la kufuatwa na kuaminiwa kwa nguvu zote, basi hiyo ni dalili kwamba Biblia siyo msingi mkuu wa imani katika kusanyiko hilo.

Hii haina maana kwamba kanisa haliwezi kujifunza kutoka katika vyanzo vingine kama vile mapokeo ya kanisa au taaluma mbalimbali. Badala yake, ina maana kwamba pamoja na kujifunza kutoka katika vyanzo vingine, Biblia inapaswa kuwa ndiyo kipaumbele cha kanisa husika. Kama kanisa halijaweka msisitizo kwamba Biblia ndiyo msingi mkuu wa imani, ambao kwa huo vyanzo vingine vyote hupimwa, basi hiyo ni dalili kwamba kanisa hilo halitakusaidia kukua kiimani.

2. Ubatizo wa maji na meza ya Bwana.

Imani yetu ya Kikristo, kama anavyosema Yuda ilikabidhiwa mara moja tu (Yuda 1:3). Kutoka ilipokabidhiwa kwa kanisa la kwanza, kila kizazi kimepewa wajibu wa kukabidhi imani hiyo hiyo kwenye kizazi kinachofuata (2 Timotheo 2:1-2). Mbali na kupokea imani hiyo, kila kizazi kina wajibu wa kuhakikisha kinailinda imani hiyo na hakiibadilishi (1 Timotheo 6:20-21). Hii ndio maana mtume Paulo anaweza kusema: “…imani nimeilinda” (2 Timotheo 4:7) baada ya kujua wakati wake wa kubaki duniani umeshaisha, kwa sababu kweli aliitunza imani aliyoipokea.

Waamini wenzetu wa karne ya pili na ya tatu kwa kuwa hawakuwa na Biblia katika namna ya mkusanyiko wa vitabu kama sisi tulivyonayo leo, walipinga imani potofu au mwenedo kinyume na ukristo kwa kulinganisha na imani waliyoipokea kutoka kwa mitume. Askofu Ireneo kwa wakati wake anasema “Kanisa, ingawa limetawanyika ulimwenguni kote, hata hadi miisho ya dunia, limepokea kutoka kwa mitume na wanafunzi wao imani hii” akionyesha kwamba anachofundisha sio jambo jipya bali ni lile lile lililopokelewa kutoka kwa mitume (Irenaeus, Against Heresies 1.10.1).

Kati ya mambo ya msingi ambayo Kanisa lilipokea kutoka kwa Bwana Yesu ni ubatizo wa maji na mlo wake, ambao tunauita Meza ya Bwana.

Bwana Yesu akiwa anajua kwamba wakati wake wa kusulubiwa umefika aliandaa mlo wa pasaka ya kiyahudi ili ale pamoja na wanafunzi wake. Wakiwa wanakula akaanzisha jambo jipya.  Jambo hili lilianza hivi, “Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu” (Mathayo 26:26). Tena, “Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.” (Marko 14:23-24). Katika kuanzisha mlo huu Bwana Yesu akasema “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” (Luka 22:19). Na zaidi akasema mlo huu hautaishia katika ulimwengu wa sasa  (Marko 14:25).

Mitume walivyopokea hili kutoka kwa Bwana walilifanya kila wiki (Matendo 2:42, 46; 20:7, 11) na waliyafundisha makanisa mengine yote kufanya vivyo hivyo. Ndio maana Paulo anawaambia Wakorintho kwamba “Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.” (1 Wakorintho 11:23-26).

Toka hapo, kila karne, waamini walilipokea jambo hili na kulifanya mara nyingi iwezekanavyo. Kwa karne za awali, ilikuwa kila juma, kama inavyoripotiwa na waandishi wengi wa karne ya kwanza na ya pili. Moja ya maandishi hayo yanatoka katika kitabu kiitwacho Fundisho la Mitume Kumi na Wawili (Didache). Maandishi haya katika swala la meza ya Bwana yanasema “Katika Siku ya Bwana, kusanyikeni pamoja mkaumega mkate na kutoa shukrani, baada ya kuungama dhambi zenu, ili sadaka yenu iwe safi” (Didache 14).

Hivyo, ukiwa unatafuta jamii ya waamini, basi hakikisha kanisa hilo linashiriki Meza ya Bwana mara nyingi iwezekanavyo. Kama umehudhuria katika makusanyiko kadhaa ya kanisa husika lakini hakuna ushiriki wa Meza ya Bwana, basi hiyo ni dalili kwamba imani iliyopo katika kanisa hilo sio imani ile ya mitume tuliyoipokea.

Vivyo hivyo, Bwana Yesu baada ya kufufuka akiwa anaondoka duniani aliwaambia mitume “…Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mathayo 28:18-20). Kwa kusema hivyo, Bwana Yesu aliwakabidhi mitume kazi ya kubatiza watakaoamini. Na mitume, kwa utii wa maagizo ya Yesu, kila wakati watu walipokuwa wakiamini, waliwabatiza kwa maji (Matendo 2:37-41; 8:11-15; 8:27-40; 9:17-18; 10:44-48; 16:14-15, 30-33). Kutokana na umuhimu wake, wingi wa watu haukuwazuia mitume kubatiza (Matendo 2:41), wala giza (Matendo 16:30-33).

Kanisa la kwanza la mitume halikuishia kubatiza tu, bali lilipeleka katika kizazi kijacho kazi hii ya kubatiza waamini. Katika maandishi niliyonukuu hapo awali, yaitwayo Fundisho la Mitume Kumi na Wawili (Didache), ubatizo unasisitizwa kufanyika hata kama kuna hali ngumu zinazoweza kusababisha uhairishwe. Didache inasema “Kuhusu ubatizo, ubatize kwa njia hii: Baada ya kwanza kufafanua mambo yote, ubatize kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu, katika maji yanayotiririka. Lakini ikiwa huna maji yanayotiririka, ubatize katika maji mengine; na kama huwezi kutumia maji baridi, basi tumia maji ya joto.Ikiwa ni kidogo sana, mimina maji mara tatu juu ya kichwa kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” (Didache 7). Maelekezo haya yote ni kuhakikisha kwamba mwamini anabatizwa.

Kama tulivyosema katika swala la Meza ya Bwana, ni sahihi pia katika ubatizo wa maji. Ukiwa unatafuta jamii ya waamini, basi hakikisha kanisa hilo linabatiza waamini mara baada ya kuamini. Kama umehudhuria katika makusanyiko kadhaa ya kanisa husika, lakini waamini wapya hawabatizwi au ubatizo unakosolewa, basi hiyo ni dalili kwamba imani iliyopo katika kanisa hilo sio imani ile ya mitume tuliyoipokea.

3. Uongozi wa Kanisa

Biblia kutoka Agano la Kale mpaka Jipya inaonyesha umuhimu wa viongozi wazuri katika kuwaelekeza wale wasio viongozi kwa usahihi katika imani. Sio Biblia tu, hata uzoefu wetu wa maisha unaonyesha kuwa watu huwa sawa au hufanana na viongozi wao. Hivyo, katika kuchagua ni kanisa lipi la mahali pamoja ambalo unataka kuwa sehemu yake, basi ni muhimu sana kuangalia uongozi wa kanisa husika ukoje.

Katika swala la uongozi kuna mambo mawili ya msingi. Moja ni kutazama mfumo wa uongozi wa kanisa hilo la mahali pamoja ukoje. Pili ni kutazama kama viongozi waliopo wanabeba sifa ambazo maandiko yamesisitiza kuwa ndizo sifa za viongozi.

Kanisa lolote la mahali pamoja ambalo mfumo wake wa uongozi unaonyesha kwamba kila kiongozi yuko kwenye nafasi ya uwajibikaji, hilo ni kanisa salama. Kwa uwajibikaji tunamaanisha kuwa kiongozi yeyote akikosea au kutenda kinyume na imani, au kufundisha kinyume na imani, anaweza kuwajibishwa kwa kurekebishwa au hata kuondolewa katika uongozi ikibidi. Kanisa ambalo mfumo wake unaonyesha kwamba kiongozi fulani hawezi kusahihishwa, kurekebishwa, au kuwa chini ya uangalizi wa viongozi wengine, kanisa hilo si salama kwa ukuaji wa mwamini.

Bila kujali cheo cha kiongozi, kiongozi yeyote anaweza kukosea katika fundisho au katika mwenendo, na ikitokea hivyo, basi kanisa linatakiwa kumrekebisha au kumsahihisha na kumsaidia kutoka katika makosa hayo. Kanisa ambalo nafasi hiyo haipo ni hatari kwa maisha ya waamini. Petro, kiongozi wa mitume, kiongozi ambaye Yesu alimpa wajibu mkubwa katika kanisa (Luka 22:32; Yohana 21), ambaye hakupungukiwa na Roho Mtakatifu (Matendo 2:1–4; 4:8, 31) wala mafunuo (Matendo 10:9–16), alifanya makosa ya kimwenendo na akasahihishwa na kiongozi mchanga katika imani kuliko yeye (Wagalatia 2:11–14). Jambo hili liliwezekana kwa kuwa kanisa la kwanza lilikuwa na mfumo ambao viongozi wote walikuwa katika nafasi ya uwajibikaji. Hivyo, ni muhimu sana kuchagua jamii ya waamini ambayo kila kiongozi anaweza kusahihishwa au kusaidiwa anapokosea katika mwenendo au fundisho.

Lakini si hivyo tu; ni muhimu pia kutazama viongozi wa kanisa husika kama wanafanana na sifa ambazo maandiko yanatuambia kuwa ndizo sifa stahiki kwa viongozi. Kwa nyakati za leo, sifa zile ambazo maandiko yameainisha kuhusu viongozi zimepewa kisogo, huku sifa za kidunia ndizo zimepewa kipaumbele. Maandiko yanatuambia kuwa viongozi wa kanisa wanatakiwa kuwa na sifa kama zinavyoainishwa katika 1 Timotheo 3:1–7, Tito 1:5–9, Matendo 20:28–35, na 1 Petro 5:1–4. Baadhi ya sifa hizo ni kama ifuatavyo;

Sifa mbaya ambazo hawatakiwa kuwa nazoSifa njema ambazo wanatakiwa kuwa nazo
Asiwe na lawama (yaani asiwe analaumiwa kwa sababu ya mwenendo wake)Awe mume wa mke mmoja
 Asiwe mleviAwe mwenye kiasi
 Asiwe mgomviAwe na busara
Asiwe mbishi Awe mtaratibu
Asiwe mtu apendaye fedha Awe mkarimu
Asiwe mtu aliyeongoka/aliyeamini hivi karibuniAwe ajuaye kufundisha
 Asiwe na sifa mbaya kwa watu wa nje (yaani asiwe na ushuhuda mbaya wa wasioamini) Awe mpole
 Awezaje kuisimamia nyumba yake vizuri
 Awe na watoto wanyenyekevu na wenye heshima

Ni ukweli usiopingika kwamba viongozi nao ni waamini kama waamini wengine, ambao bado wako katika safari ya kumfanania Bwana wetu Yesu Kristo katika mwenendo na ujumla wa maisha yao. Hivyo, sifa hizi hazimaanishi kwamba viongozi hawawezi kukosea au kufanya dhambi. Maandiko yanapotoa sifa hizi, yanajua kuwa hizi ni sifa tarajiwa kwa kila mwamini, lakini kwa kuwa waamini wanatakiwa kukua kufika huko, inahitajika waongozwe na watu ambao wao wamekua zaidi katika sifa hizo. Hivyo, ni muhimu sana unapofanya maamuzi ya kuwa sehemu ya jamii fulani ya waamini usifanye maamuzi kwa haraka bila kutafakari na kufuatilia mambo haya ya msingi kuhusu uongozi wa kanisa, kama ambavyo huwa unafanya maamuzi mengine ya muhimu kwa uangalifu mkubwa.

4. Kusanyiko la waamini

Katika mambo ya muhimu sana kwa kanisa ni kukusanyika mara kwa mara. Kwa sehemu kubwa, makanisa mengi yanakusanyika siku ya Jumapili, na kwa sehemu ndogo, siku nyingine za wiki. Mwandishi wa Waebrania aliwasisitiza pia waamini kwamba wasiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine, kama Mungu anavyotusisitiza sisi leo kupitia maandiko haya (Waebrania 10:24–25).

Pamoja na kukusanyika, wewe kama mwamini unayetafuta ushirika katika jamii fulani ya waamini, hakikisha kuwa lengo la kukusanyika la kusanyiko husika ni kwa ajili ya kujengana katika imani yetu ndani ya Kristo na si vinginevyo.

Watu wanaweza kukusanyika kwa malengo tofauti tofauti, lakini ili kusanyiko liwe na sifa ya kuwa kanisa, linatakiwa kuwa na lengo la kujengana katika imani ndani ya Kristo Yesu. Lengo likiwa ni kujengana, basi kanisa litafanya mambo mbalimbali, lakini yote yakiwa na kusudi la waamini kujengana katika imani yao. Hivyo, unapohudhuria kusanyiko lolote lile na mambo yanayofanyika hayapelekei wewe kujengwa na kuwajenga wengine, basi kusanyiko hilo halitakufaa wewe kama mwamini.

Mtume Paulo, akiwa anaelezea matumizi sahihi ya karama za kiroho ambazo Mungu amezitoa kwa kila mwamini, alisema: “…Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga” (1 Wakorintho 10:25). Katika muktadha huu, Mtume Paulo anasema ikiwa kuimba zaburi, ikiwa kufundishana, ikiwa kutoa na kupokea ufunuo, au kunena kwa lugha na kutafsiri lugha, vyote vifanyike kwa lengo la kujenga kanisa na si vinginevyo. Hivyo, kusanyiko la waamini linatakiwa liwe na mambo mbalimbali ambayo yote yanafanyika kwa lengo la kujenga kanisa na si vinginevyo.

Ukienda kwenye kusanyiko linaloitwa la kanisa lakini yanayofanyika hayafanyiki kwa lengo la kujengana katika imani, hata kama mambo hayo yanaitwa kwa majina ya kibiblia, basi kusanyiko hilo si sahihi kwako kama mwamini. Makusanyiko yanayofanyika kwa lengo la kukuburudisha tu hayakufai kama mwamini. Makusanyiko yanayofanyika kwa lengo la kutatua changamoto zako za kimwili pekee hayakufai kama mwamini. Makusanyiko yanayowafanya waamini wengi kuwa watazamaji isipokuwa wachache, hayo pia hayakufai.

5. Ushirika wa waamini

Pamoja na jambo hili kuwa la mwisho katika makala hii, jambo hili sio la mwisho kwa umuhimu. Kama unatafuta kuwa sehemu ya jamii fulani ya waamini basi tazama jinsi waamini hao wanavyoishi pamoja. Kama tulivyoona hapo juu kwamba Kanisa sio jengo wala mahali watu wanakwenda bali ni jamii ya waamini, jamii hii inatakiwa kutambulika kwa jinsi watu hawa wanavyoishi maisha ya Kristo hapa duniani.

Kristo Yesu katika mafundisho yake ya kusisitiza upendo katikati ya waamini alisema “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” (Yohana 13:35). Hapa alikuwa na maana kwamba ili uweze kuwatambua wanafunzi wa Yesu basi utaona jinsi wanavyopendana, kama yeye alivyowapenda. Hivyo, kanisa sahihi la mahali pamoja lazima ilipimwe kwa jinsi waamini wanavyopendana.

Maisha ya upendo Yesu aliyoyafundisha hayakuwa nadharia, bali yeye mwenyewe alionyesha mfano. Hii ndio maana anaagiza kwa kuonyesha mfano wa namna gani kanisa linatakiwa kuwa na upendo. Anasema “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:12-13). Kwa hiyo, upendo kwa mujibu wa Bwana Yesu unaonekana kwa waamini kujitoa kwa ajili ya waamini wenzao. Ukiona jamii ya waamini ambayo waamini wamejifunza na wanajitoa kwa ajili ya waamini wengine basi hiyo ni dalili ya kuwa hao ni wanafunzi wa Kristo kweli kweli.

Kujitoa kwa waamini kunaweza kuwa kwa namna gani? Yesu aliwahi kufundisha kwamba pale atakaporudi mara ya pili atagawa watu kama mchungaji anavyogawa kondoo na mbuzi. Na kondoo atawaweka mkono wa kuume na kuwaambia “Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;  kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.” (Mathayo 25:34-36). Baada ya kusema hivyo, waamini watamuuliza Yesu ni lini tulikutendea matendo hayo? Ndipo Yesu atajibu “Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” (Mathayo 25:40). Hivyo, Yesu anasema pale mwamini atakapomlisha mwamini mwingine mwenye njaa, basi kwa kufanya hivyo amemlisha yeye. Mwamini atakayemvisha mwamini asiye na nguo basi kwa kufanya hivyo amemvisha yeye.

Kwa hiyo, waamini wanatakiwa kuhudumiana katika maeneo hayo Yesu aliyoyajata na mengine mbalimbali. Kwa kuishi hivyo ndio kanisa linatambulika kuwa ni jamii ya wanafunzi wa Yesu. Kwa hiyo, ni muhimu sana unapotafuta jamii ya waamini basi zingatia kuangalia kama jamii hiyo ni kweli inatambulika kwa upendo katikati yao.

Hii haina maana kwamba utafute kanisa ambalo litakusaidia wewe katika changamoto zako (huo ni ubinafsi), bali ina maana ya kuangalia kanisa ambalo waamini wao kwa wao wanatendeana kwa upendo kama Kristo Yesu alivyotuagiza.

Hitimisho

Tunajua kwamba yako mambo mengi sana ya kuyaangalia katika nyakati zetu ili uweze kuwa sehemu ya jamii ya waamini ambao wana imani ile ile waliyokuwa nao mitume na ambayo ilianzishwa na Bwana wetu Yesu kristo, lakini tunaamini mambo haya yatakuwa muhimu sana kukusaidia kama utangulizi mzuri na wa muhimu kwako. Kama ambavyo ukiwa unataka kuoa au kuolewa unakuwa mwangalifu , basi unatakiwa kuwa mwangalifu sana pale unapoamua kuchagua kanisa. Na mwisho kabisa pamoja na kufuatilia haya yote, kumuomba Mungu ni muhimu ili haya tuliyoyaeleza uweze kuyaona katika uhalisi wake.