MWONGOZO WA KUSOMA UJUMBE WA NABII OBADIA.
MAELEKEZO.
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI.
Kitabu cha Nabii Obadia ni kitabu cha pekee kidogo katika vitabu vya agano la kale; Kwanza, ni kitabu kifupi kuliko vyote katika vitabu vya agano la kale. Pili, ni moja ya vitabu vichache ambavyo ujumbe wake si kwa ajili ya taifa la Israeli. Tatu, ni moja kati ya vitabu vichache ambavyo nabii amejitambulisha kwa jina moja tu bila kueleza ukoo wake kama manabii wengine (Mfano Yeremia 1:1, Zefania 1:1 na Yoeli 1:1) na pia bila kutaja ni wakati gani alitoa unabii huo kama manabii wengine walivyofanya (mfano Hosea 1:1, Mika 1:1 na Isaya 1:1). Kwa kuwa kuna watu kumi na wawili wenye jina Obadia[1] katika Vitabu vya agano la kale, ni vigumu kujua Obadia mtoa ujumbe huu ni yupi. Jina Obadia maana yake ni “mtumishi wa Jehovah” ndio maana lilikuwa ni jina maarufu katika Israeli. Ujumbe wa Nabii Obadia ulikuwa ni kwa ajili ya Edomu, taifa Jirani na Israeli ambalo lilikuwa ni taifa lililoanzishwa na Esau kaka wa Yakobo (Mwanzo 36:9).
MUKTADHA WA KIHISTORIA WA UJUMBE WA NABII OBADIA.
Uadui kati ya Edomu na Israeli ulianza kabla hata mababa wa mataifa haya mawili hawajazaliwa, yaani uadui wa Esau na Yakobo ulianza tangu wakiwa tumboni mwa mama yao (Mwanzo 25: 21-26). Mataifa haya yaliendelea kuwa na uadui (Hesabu 20:17-21; 1 Samweli 14:47-48; 2 Samweli 8:12-14 na 1 Wafalme 11:14-25), ingawa Mungu aliwaagiza Waisraeli kutowachukia Waedomu kwa kuwa ni ndugu zao (Kumbukumbu la Torati 23:7). Nabii Obadia alitoa unabii wake juu ya Edomu baada ya tukio la uamisho wa Babeli wa taifa la Yuda. Wakati Babeli walipovamia Yuda, Edomu ilisaidia Babeli kushambulia mji wa Yerusalemu na kufurahia anguko la mji huo (Obadia 1:10-14; Ezekieli 35:15; Maombolezo 2:15-17; 4:21-22). Edomu ilipaswa kuwa mshirika wa Yuda (Yerusalemu), lakini badala yake waliwatia moyo Babeli kushambulia Yerusalemu. Obadia anatoa ujumbe wake ili kuonyesha kwamba Mungu ataihukumu Edomu kwa yale ambayo amefanya juu ya Taifa lake Israeli/Yuda (Obadia 1:10-16). Hivyo ujumbe huu ulitolewa baada ya taifa la Yuda (Taifa la kusini) kuchukuliwa mateka na mfalme Nebukadreza wa Babeli, tukio ambalo limeelezwa na manabii wengi. Pia ni baada ya sehemu ya eneo la Taifa la Israeli (Eneo la kaskazini) liliyokuwa chini ya dola ya ashuru kuchukuliwa na kuwa chini ya utawala wa mfalme Nebukadreza (Obadia 1:19).
UJUMBE MKUU WA NABII OBADIA.
Ujumbe mkuu wa Nabii Obadia ni tangazo la hukumu kali dhidi ya Taifa la Edomu kwa sababu ya ukatili na usaliti wao dhidi ya taifa la ndugu zao yaani Israeli (Obadia 1:10-14). Katika kutangaza hukumu hiyo, Obadia anasisitiza haki ya kimungu kwa kueleza kwamba Bwana ataleta hukumu juu ya Edomu kwa sababu ya matendo yao mabaya (Obadia 1:15-16). Licha ya nguvu na usalama wa Taifa la Edomu, vitu ambavyo vimeleta kiburi na majivuno, watashushwa na kulemewa na mkono wa Mungu (Obadia 1:2-4, 8-9). Nabii Obadia haishii kutangaza hukumu tu bali anatangaza pia tumaini la urejesho. Urejesho huu Obadia anaoutangaza sio wa Edomu bali ni wa taifa lake teule yaani Taifa la Israeli (Obadia 1:17-21). Kwa kuwa Israeli walikuwa utumwani wakati huu, basi Mungu anawatangazia tumaini la Urejesho wa taifa lao yaani watu watarejea, ardhi itarejeshwa na mali zao pia.
Taifa la Edomu lilivyosimama upande wakati wa maangamizi ya Jerusalem (Obadia 1:10-11).
MPANGILIO WA KITABU.
Namba | Maandiko | Maelezo |
1 | 1:1a | Utangulizi |
2 | 1:1b-9 | Hukumu juu ya Edomu |
a. | 1:1b-4 | Tangazo la kwanza |
b. | 1:5-7 | Tangazo la Pili |
c. | 1:8-9 | Tangazo la Tatu |
3 | 1:10-14 | Sababu ya Hukumu |
4 | 1:15-16 | Hukumu ni ya Haki |
5 | 1:17-21 | Urejesho wa Israeli |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.
Kitabu kinaanza kama maono ya Obadia (1:1a).
Sehemu ya kwanza ya maono haya yanaanza na tangazo la kuhumu juu ya taifa la Edomu (1:1b-9). Maono yanaanza na taarifa kwamba mataifa mengine yametumiwa mjumbe na Mungu kuwakusanya ili wapigane na Edomu (1:1b). Na Bwana anaahidi kuifanya Edomu kuwa ndogo kati ya mataifa (1:2a). Kwa kuwa mataifa ya kale walikuwa wanapigana kwa ajili ya kupata ardhi, mateka ya watu na mali nyingine hivyo kama mataifa yataungana na kuipiga Edomu ni dhahiri kwamba nchi hii itanyang’anywa ardhi na hivyo kuwa nchi ndogo kwa eneo la ardhi na kuwa ndogo kwa ushawishi kwa sababu ya kupigwa. Bwana anasema matokeo ya nchi hii kufanywa ndogo ni kudharauliwa (1:2b). Katikati ya kutangaza hukumu hii Bwana anaweka wazi sababu ya kuihukumu Edomu. Kwa kuwa Edomu ilikuwa juu ya milima na katikati ya miamba, taifa lilipata kiburi na kujinadi kwamba hakuna atakayeweza kulipiga. Uganyanyifu utokanao na kiburi ndio sababu Bwana anaihukumu Edomu (1:3). Bwana anasisitiza kwamba ataishusha Edomu hata kama itaweka makao yake juu kama vile tai au hata kama itaweka makao yake juu kiasi cha kuwa katikati ya nyota(1:4).
Bwana anasema kupigwa kwa Edomu hakutakuwa kama wezi au wanyang’anyi, kwa maana wao huiba kiasi cha kuwatosha tu hasa kile watakachokiona (1:5a). Lakini pia hakutakuwa kama kuchumwa kwa zabibu na wachumaji, kwa kuwa wao pia huchuma zinazowatosha na zile wanazoziona na kuacha nyingine (1:5b). Kinyume na mifano hiyo Edomu itapigwa kabisa, yaani pamoja na kuwa juu ya milima na katikati ya miamba nchi itakaguliwa kaguliwa na kila mali iliyofichwa itatafutwa tafutwa ili ichukuliwe (1:6). Mataifa washirika wa Edomu watawakataa pale watakapokuja kuomba msaada na watawarudisha mpakani kwao (1:7a). Mataifa yale yaliyoweka amani kati yake na Edomu watamdanganya Edomu na mwisho kuwashinda (1:7b).Na mataifa yanayokula pamoja na Edomu yameweka mtego lakini Edomu hawana habari (1:7c). Kwa kukosa msaada kutoka nje, Bwana ataangamiza pia msaada kutoka ndani (yaani wenye hekima na mashujaa/wanajeshi) ili kila mtu katika Edomu aangamizwe (1:8-9).
Sehemu ya pili ya maono haya inajikita kuelezea sababu, kwa nini Bwana ataiangamiza Edomu. Edomu itaangamizwa kwa sababu ya udhalimu(Matendo mabaya) iliyoyatenda juu ya ndugu zao Israeli wakati wa kupigwa kwao (1:10). Ni mambo gani ya udhalimu Edomu alifanya kwa Israeli? Moja, Edomu haikuisaidia Yuda/Israeli wakati wa kuvamiwa Babeli (1:11).Pili, Edomu walifurahishwa na Uharibifu wa Yuda/Israeli, na wakaingia kwenye lango lake na kupora mali yake (1:12-13). Tatu, Edomu walisimama kando ya barabara ili kuua wakimbizi wa Yuda/Isreali na kuwatia gerezani waokokaji wake Yerusalemu ilipoanguka (1:14).
Sehemu ya tatu ya maono haya inatangaza ujio wa siku ya Bwana. Siku ya Bwana sio tu juu ya Edomu bali juu ya mataifa yote(1:15a). Kama ambavyo Edomu inahukumiwa kwa haki (yaani inapata malipo ya kile ilichofanya dhidi ya Israeli/Yuda) ndivyo mataifa mengine yatahukumiwa kwa haki pia (1:15b). Kama vile mataifa yalivyoshiriki kuiharibu Yerusalemu (pamoja na Edomu), vivyo hivyo (pamoja na Edomu) yataangamizwa milele (1:16).
Sehemu ya nne ya maono haya inatangaza tumaini la urejesho kwa Israeli/Yuda, kinyume na matangazo ya hukumu kwa Edomu na mataifa. Pamoja na hali ya Israeli ya sasa Bwana anasema watakuwepo waliosalimika ndani yake na watamiliki nchi yao tena (1:17). Bwana anasema Israeli/Yuda wataipiga Edomu kama vile moto unavyoteketeza mabua (1:18). Baada ya kipigo hicho Israeli watarejesha ardhi yao na kutanua mipaka (1:19-20). Ushindi Israeli wanakaopata juu ya Edomu utakuwa ni mali ya Bwana yaani Ufalme wa Israeli/Yuda utakuwa Ufalme wa Mungu (1:21).
Utabiri wa urejesho wa Jerusalem (1:17-21). Picha zote na VideoBible.com
MATUMIZI YA LUGHA.
Unabii mara nyingi unasifa za ushairi kwa kiasi kikubwa, hata kitabu hiki cha Obadia kina sifa za kiushahiri kama vifuatavyo:
- Matumizi ya Lugha ya Picha.
Katika kufikisha ujumbe wake Nabii Obadia ametumia lugha ya picha (Taswira) mara kadhaa. Katika Mstari wa 4 makao ya Edomu yanatajwa kwamba yako juu kwa kufananishwa na makao ya tai na nyota pia. Mstari 5-6, unarejea utendaji wa kawaida wa wezi/wanyang’anyi na wavunaji zabibu ili kuweka tofauti na uangamizo kamili ambao Edomu itapata. Mstari wa 10 unalinganisha aibu na vazi litakalofunika Edomu. Mstari wa 11 unaonyesha jinsi mji wa Yerusalemu ulivyochaguliwa kupigwa na adui zake kwa kuwaonyesha kuwa walipiga kura kwa ajili ya jiji hilo. Mstari wa 16 unatumia sitiari ya kikombe cha ghadhabu, ambayo inalinganisha uzoefu wa kuadhibiwa na ghadhabu ya Mungu na kulewa kwa divai. Hatimaye, Mstari wa 18 unalinganisha Israeli na moto unaoteketeza Edomu kama makapi.
- Usambamba
Sifa nyingine ya pili ya ushairi wa kibiblia (tofauti na ule wa kiswahili) ni usambamba. Kwa kifupi Usambamba ni kutumia maneno mengine katika mstari wa pili kusisitiza jambo lile lile linalozungumza mstari wa kwanza wa Ubeti. Obadia pia ametumia usambamba katika ujumbe wake. Mstari wa 8, wazo “je! Sitawaangamiza watu wenye akili katika Edomu” limesisitizwa kwa kutumia lugha tofauti lakini ujumbe ni ule ule “wenye ufahamu katika kilima cha Esau”. Mstari wa 15, wazo “kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa” limesisitizwa kwa maneno tofauti lakini ujumbe ukiwa ni ule ule kwamba “malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe”. Hii ni mifano tu ya usambamba katika ujumbe huu bado kuna maeneo mengi Nabii Obadia ametumia usambamba.
[1] Jina obadia limeonekana katika maeneo haya; 1 Wafalme 18:3-16; l Nyakati 3:21; 7:3; 8;38; 9:16; 12:9; 27;19; 2 Nyakati. 17:7; 34:12.
Unakuja hivi karibuni….