SHUGHULI ZA KANISA
Kwa kuwa tumeshajifunza maana ya kanisa, lengo la kanisa, na njia za kutimiza lengo hilo, ni vizuri pia kujifunza kuhusu shughuli za kanisa. Shughuli, katika muktadha huu, inamaanisha mambo yale ambayo kanisa linatakiwa kufanya ili kutimiza lengo lake. Shughuli za kanisa zinahusisha mambo ambayo kanisa linapaswa kufanya linapokutana mahali pamoja—kwa ajili yake lenyewe (yaani, shughuli kwa ajili ya walio ndani) na kwa ajili ya watu wasioamini (shughuli kwa ajili ya walio nje).
Katika namna ya kwanza (shughuli za kanisa kwa ajili ya kanisa lenyewe), mtu anaweza kusema kwamba hakuna haja ya kujifunza hilo kwa sababu kanisa limekuwa likikusanyika kwa miaka mingi, hivyo linafahamu kinachopaswa kufanyika linapokusanyika. Hata hivyo, kwa uzoefu wangu kama mwamini, nimeona kwamba sababu za kanisa kukusanyika zimekuwa tofauti tofauti na hivyo kupelekea kufanya shughuli tofauti tofauti. Hii ndiyo sababu ni muhimu kujifunza ni nini tunapaswa kufanya tunapokusanyika, kwa mujibu wa mafundisho ya Biblia.
Lakini pia unaweza kujiuliza kwa nini mwandishi amekuwa anaeleza kuhusu shughuli za kufanya katika kusanyiko na sio shughuli katika ibada. Kwa kawaida waamini wamezoea kusema “nakwenda ibadani” au “nakwenda kuabudu”. Na wakati mwingi tunaulizana “Wewe una abudu wapi?” au “kwa nini sijakuona kwenye ibada leo?” Yote haya yanaonyesha kwamba neno ibada ni maarufu zaidi kuliko neno kusanyiko. Jambo hili unaweza kujifunza zaidi kwenye ukurasa huu.
Shughuli za Kanisa kama zilivyoripotiwa na Luka.
Luka, mtumishi wa Mungu na mwandishi ambaye anasimulia kwa urefu zaidi kuliko waandishi wengine wote kuhusu maisha ya kanisa la karne ya kwanza, katika kueleza muhtasari wa maisha ya kanisa anatuonyesha kanisa la kwanza lilidumu katika mambo makuu manne. Mambo haya ni yale kanisa lilikuwa linafanya kwa ajili yake lenyewe. Mambo haya ni:
a. Mafundisho
b. Ushirika
c. Kuumega mkate (Meza ya Bwana na Chakula cha pamoja)
d. Maombi
Matendo 2:42-47
“Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume. Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.
MAFUNDISHO.
Jambo la kwanza kabisa ambalo kanisa linatakiwa kufanya pale linapokutana ni kufundishana. Mafundisho ni njia muhimu sana katika kuhakikisha waamini wanaielewa imani yao na kumjua Mungu waliyemwamini. Kwa kuwa watu wanaokolewa wakiwa wametoka katika aina tofauti tofauti za maisha, hivyo ili wabadilishwe wanahitaji kufundishwa. Katika kanisa la kwanza, mitume walifanya kazi hii ya kuwafundisha wote walioamini kwa kuwa ndivyo Bwana wetu Yesu Kristo alivyowaagiza.
Mathayo 28:19-20
“Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Kwa hiyo, kanisa kufundishana si jambo ambalo tunaweza kuchagua kufanya au la, bali ni agizo la Bwana wetu Yesu Kristo. Ni agizo ambalo tunatakiwa kulitii bila wasi wasi wa aina yeyote. Bila mafundisho, kanisa haliwezi kukua hata kufikia kimo cha utimilifu wa Kristo; ndio maana kila tunapokusanyika, ni muhimu kuendelea kufundishana. Waamini wanatakiwa kufundishwa mafundisho yote ya Kristo ili waweze kumfanania Kristo katika yote.
USHIRIKA.
Jambo jingine lililokuwa likifanyika wakati kanisa linapokutana, Luka anatuonyesha lilikuwa ni ushirika. Ushirika Luka anaoutolea ripoti ulihusu waamini kukutana na mahitaji ya kimwili ya waamini wengine. Waamini waliokuwa na vitu vya ziada, waliwapa wale wasio kuwa navyo. Waamini wakafikia mpaka kuuza walivyokuwa navyo ili kukutana na uhitaji wa waamini wengine. Huu ndio ushirika Luka anaoutolea ripoti katika kitabu hiki cha matendo ya mitume toka mwanzo mpaka mwisho (Matendo 2:44-45; 4:32, 35, 36-37; 5:1-11).
Hivyo, waamini hawakuwa wanakusanyika kwa ajili ya kujifunza tu, bali pia kwa ajili ya kuishi maisha ya kifamilia kweli kweli. Kanisa halikuishi hivyo kwa sababu walijisikia kufanya hivyo, bali waliishi hivyo kwa sababu walikuwa wanatii maagizo ya Bwana Yesu. Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuishi kinyume na kujilimbikizia mali (Luka 12:13-31) na akahimiza wanafunzi kutoa kwa ajili ya wengine (Luka 12:32-34). Pamoja na hilo, Bwana alifundisha kwamba ndugu au jirani wa mtu ni yule anayemsaidia mwenzake wakati anahitaji msaada na sio yule aliyezaliwa pamoja naye katika kabila/taifa au familia moja (Luka 10:25-37). Kwa mafundisho ya aina hii ya Bwana Yesu, kanisa liliweza kuishi kwa ushirika ili kila mwenye mahitaji katikati yao upatiwe suruhisho.
Kanisa la sasa linatakiwa kufanya vivyo hivyo—sio tu tukutane kwa ajili ya kuimba na kufundishana, bali pia tukutane kwa ajili ya kuhakikisha tunakutana na mahitaji ya waamini wenzetu. Hili sio jambo kila mwamini anatakiwa kufanya kwa wakati wake anaojisikia, hili ni jambo ambalo kanisa kwa pamoja linatakiwa kufanya.
KUUMEGA MKATE.
Jambo la tatu, ambalo kanisa lilikuwa linafanya katika orodha ya Luka, lilikuwa ni kuumega mkate. Luka anatuambia waamini walitembea nyumba kwa nyumba kuumega mkate na kula chakula chao kwa pamoja kwa furaha na kwa moyo mweupe (Matendo 2:46). Katika orodha yake (2:42) na katika maelezo ya ziada (2:46) Luka anaeleza matukio mawili yalikuwa yanaenda kwa pamoja.Tukio la kula chakula kwa pamoja liliunganishwa na tukio la kula mkate na divai kwa ajili ya kukumbuka kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo (Meza ya Bwana).
Kanisa liliunganisha tukio la chakula cha upendo na meza ya Bwana, hivyo hata sisi leo tunaweza kufanya hivyo. Kutokana na mapokeo (hasa yaliyoanza karne ya pili), kanisa kwa muda limefundishwa kwamba meza ya Bwana inatakiwa kuandaliwa na kiongozi maalumu katika kanisa na kama haijafanyika hivyo, basi tukio hilo likifanyika linakuwa sio tukio halisi. Lakini hakuna fundisho wala tukio lililopo kwenye Biblia linaloonyesha au kuashiria kwamba Meza ya Bwana inatakiwa kuandaliwa na kiongozi maalumu katika kanisa.
Kinyume chake, tunaona tukio hili lilikuwa linafanywa na waamini nyumba kwa nyumba baada ya kupata chakula chao cha upendo. Nyumba kwa nyumba Luka hamaanishi tukio hili lilikuwa la familia, bali anamaanisha waamini walikusanyika katika nyumba zao. Ni vizuri kuelewa kwamba tukio la meza ya Bwana lina kusudi ya kukumbuka na kutangaza kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo na kuonyesha kwamba waamini walio wengi wamefanyika kuwa mwili mmoja katika Kristo. Mtu yeyote aliyeamini anatakiwa kushiriki na anaweza kuongoza tukio hili.
Pia, kanisa halikufanya jambo hili kwa sababu lilijisikia kufanya hivyo. Kanisa lilifanya tukio hili la kushiriki mkate na divai kama ishara na tangazo la kukumbuka mateso ya Yesu kwa ajili yao, kama ambavyo liliamuriwa na Bwana Yesu mwenyewe. Maandiko yanasema, “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]” (Luka 22:19-20). Hivyo, kanisa lazima lifanye tukio hili la kula mkate na divai kwa makusudi ya kukumbuka mateso ya Yesu yaliyotupatia ukombozi, kwa kuwa tukio hili ni agizo la Bwana.
KUSALI.
Jambo la nne ambalo kanisa lilikuwa linafanya katika orodha ya Luka ni Kusali. Hili ni jambo la muhimu pia kwa kanisa kufanya pale linapokutana. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume, tunaona mifano mingi ya kanisa kukutana na kufanya maombi na sala, na hatimaye Mungu akajibu maombi yao. Moja ya mfano huo ni pale kanisa lilipoomba kwa juhudi kwa ajili ya mtume Petro alipokuwa amefungwa gerezani. Mungu akasikia maombi ya kanisa na mwishowe akamtoa Petro gerezani kwa mkono wa Malaika (Matendo 12:5-12).
Huo ni mfano mmoja tu katika maandiko, lakini kuna mifano mingi sana. Hivyo, kanisa linatakiwa pia kukutana kwa ajili ya kumuomba Mungu. Hili ni moja ya jambo ambalo mara nyingi halijapewa kipaumbele kama inavyotakiwa katika makusanyiko yetu, na wakati mwingine limepangwa kufanyika siku ambazo waamini wachache wanakusanyika. Lakini tunaona kanisa la kwanza lilifanya jambo hili mara kwa mara pale walipokuwa wanakusanyika. Hivyo, na sisi kanisa la leo tunatakiwa kulipa kipaumbele jambo hili.
Bwana Yesu alionesha mfano wa kuwakusanya wanafunzi wake na kuwataka kufanya maombi pamoja nao (Mathayo 26:36-44). Hakuishia hapo tu bali aliwaagiza wanafunzi wake kuomba, akisema, “Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” (Mathayo 26:41). Maagizo ya Yesu kuhusu kuomba na mfano wa maisha yake ndio vilikuwa vichocheo kwa kanisa la kwanza kuwa katika maombi kila wakati. Kwa kuwa tunatakiwa kumfuata Bwana Yesu Kristo katika mwenendo, kanisa la leo pia linatakiwa kujihusisha na jambo hili la muhimu.
Mambo haya manne ambayo Luka anayataja kwamba yalikuwa yanafanyika katika kanisa la Yerusalemu karne ya kwanza, tunaona pia ndiyo yanayotolewa ripoti na Yustino Mfiaimani (Justin Martyr) kwamba yalikuwa yanafanyika na Wakristo kwa ujumla, hasa Wakristo wa Rumi katika karne ya pili. Yustino Mfiaimani, katika maandishi yake yaitwayo “Utetezi wa Kwanza wa Wakristo” (First Apology), aliandika akisema:
“Na katika siku iitwayo Jumapili, wote wakaao mijini au vijijini hukusanyika mahali pamoja, na kumbukumbu za mitume au maandiko ya manabii husomwa kwa kadri muda unavyoruhusu; kisha msomaji anapomaliza, kiongozi (rais) hutoa mafundisho kwa maneno na kuhimiza kuiga mambo hayo mema. Kisha sisi sote husimama pamoja na kuomba, na, kama tulivyosema awali, sala inapomalizika, mkate, divai na maji huletwa, na kiongozi hutoa sala na shukrani kwa kadri ya uwezo wake, na watu hukubaliana kwa kusema Amina; na kuna mgao kwa kila mmoja, na ushiriki wa kile ambacho shukrani imetolewa juu yake, na kwa wale ambao hawapo hutumiwa sehemu yao na mashemasi. Na wale walio na uwezo mzuri wa maisha, na walio radhi, hutoa kile ambacho kila mmoja anaona kinafaa; na kile kilichokusanywa huwekwa kwa kiongozi, ambaye huwasaidia yatima na wajane na wale ambao, kwa sababu ya ugonjwa au sababu nyingine yoyote, wana mahitaji, na wale walio kifungoni, pamoja na wageni wanaotutembelea, na kwa ujumla huwajali wote walio na uhitaji.”
Kutoka kipindi cha maisha ya kanisa kinachoripotiwa na Luka hadi kipindi cha maisha ya kanisa kinachoripotiwa na Yustino, kuna tofauti ya takriban miaka tisini hadi mia moja. Aidha, kutoka Yerusalemu hadi Rumi ilikuwa ni safari ya zaidi ya wiki nne mpaka sita kwa kutumia njia ya nchi kavu pamoja bahari. Pamoja na utofauti huu mkubwa wa muda na umbali, bado tunaona kwamba kanisa lilikuwa linafanya mambo haya manne mara kwa mara kila walipokutana.
Katika maandishi yake, Yustino kwanza anaonyesha kuwa mafundisho katika kusanyiko la kanisa yalikuwa na msingi wa kumbukumbu za mitume (sawa na maandishi ya mitume) au maandiko ya manabii (sawa na vitabu vya Agano la Kale). Pili, Yustino anaeleza kuwa kanisa lote lilishiriki katika maombi—kwa lugha nyingine, waamini wote waliokusanyika walifanya maombi kwa pamoja. Tatu, Yustino anaonyesha jinsi Meza ya Bwana ilivyokuwa ikichukuliwa kwa uzito mkubwa kiasi kwamba waamini ambao hawakuweza kufika katika kusanyiko walitumiwa kwa mikono ya mashemasi. Na mwisho, kama vile Luka alivyosema, waamini wenye uwezo walitoa kwa hiari ili kusaidia kukidhi mahitaji ya waamini wengine—tendo ambalo Luka analitaja kama ushirika.
Kwa ushahidi huu kutoka kwenye maandiko na nje ya maandiko, ni dhahiri kwamba Mungu analitegemea kanisa lifanye mambo haya kila linapokutana. Kanisa linapaswa kufundishwa kutoka kwenye maandiko yote—yaani, Agano la Kale na Agano Jipya—na si kutoka kwenye uzoefu wa maisha ya wahubiri au kutoka kwenye elimu nyingine inayopingana na maandiko katika ujumla wake. Kanisa linapaswa kuomba kwa pamoja, si wachache kuwaombea wengine tu. Kanisa linapaswa kushiriki Meza ya Bwana mara nyingi iwezekanavyo, na waamini wote wahimizwe kushiriki badala ya kujiepusha. Zaidi ya hayo, kanisa linapokutana linapaswa kuangalia mahitaji ya waamini na kuyatatua, badala ya kulenga tu mahitaji ya taasisi au majengo.
Mambo zaidi kutoka kwa Luka.
Kwa kusoma habari za kanisa kupitia Luka, pia tunaona kanisa lilikuwa linafanya mambo mengine mawili ya msingi, moja kuhubiri injili kwa wasioamini na pili, kubatiza watu waliokuwa wanaamini. Mambo haya katika sura ya mbalimbali za kitabu cha Matendo ya mitume yamesimuliwa kwa sababu yalikuwa yanafanyika, pamoja na kwamba hayakutajwa kwa kuorodheshwa kama mambo yale manne. Sababu ya kutokutajwa katika orodha ile ilikuwa ni kwa sababu mambo haya hayakuwa mahususi kwa ajili ya kundi la waamini. Wasioamini walihubiriwa injili na walipoamini walibatizwa mara moja ili kuonyesha kwamba sasa wameingia kwenye familia ya Mungu licha ya ubatizo kuwa makusudi mengine.
Kabla ya kuorodhesha mambo yale manne, Luka anasimulia kazi ya kuhubiri ambayo mtume Petro aliifanya akiwa amesimama na mitume kumi na moja (Matendo 2:14-40) na baada ya mahubiri hayo, walioamini walibatizwa na wakapokelewa katika familia ya Mungu (Matendo 2:41). Tofauti na miaka ya hivi karibuni, ambapo watu wakiamini wanaambiwa waseme “sala ya toba” kanisa la kwanza liliwapokea watu baada ya kubatizwa, jambo lilofanyika mara baada ya watu kuamini.
Kitabu cha Matendo ya Mitume kwa ujumla kinatuonyesha kwamba kanisa lilikuwa linahubiri injili kwa wasioamini na watu walipokubali, lilikuwa linawabatiza (Matendo 8:5-13, 8:26-38, 9:1-48, 16:13-15, 16:27-34, 18:5-8 na 19:1-5). Hivyo, haya mambo mawili pia ni miongoni mwa mambo ya msingi ambayo kanisa la leo linatakiwa kufanya kama yalivyofanywa na kanisa katika karne ya kwanza.
KUHUBIRI INJILI.
Wakati tunajifunza lengo la kanisa, tuligawanya lengo la kanisa katika ngazi mbili. Ngazi ya pili ilikuwa kuhusu kanisa kuwa nuru kwa wasioamini ili waitikie wito mkuu wa wokovu. Njia ya kuwafanya wasioamini waitikie mwito mkuu wa injili ni kuwahubiria. Hii ndio maana Luka anaonyesha jinsi kanisa lilivyokuwa linafanya jambo hili kwa pamoja na kwa bidii. Kanisa la sasa pia linatakiwa kufanya juhudi zote na kutumia mbinu mbalimbali katika kuhubiri injili kwa wasioamini ili waitikie mwito huu wa wokovu. Bila kuhubiri injili, watu wasioamini hawawezi kupata wokovu.
Bwana Yesu, kabla ya kuondoka, aliwaagiza wanafunzi wake kuhubiri injili, akisema, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa” (Marko 16:15-16). Agizo hili halikuwa kwa ajili ya wanafunzi wake wa karne ya kwanza pekee, bali ni agizo kwa wanafunzi wake wote kwa ujumla. Ikiwa kundi la waamini halihubiri injili, basi linapoteza sifa ya kuitwa kanisa, kwa sababu kanisa linatakiwa kutimiza mwito wa Bwana wake.
UBATIZO.
Baada ya watu kuhubiriwa injili, wale waliofikia hatua ya kuamini, kanisa liliwabatiza mara moja kwa kuwa hivyo ndivyo Bwana Yesu alivyoagiza. Hivyo, kubatiza ni moja ya shughuli ambazo kanisa linatakiwa kufanya ili kuwakaribisha waamini wapya katika imani. Tunaposoma kitabu cha Matendo ya Mitume, tunaona kwamba kanisa liliwabatiza waamini mara moja baada tu ya kuamini (tofauti na maendeleo tunayoyaona kwenye karne za mbele baada ya kipindi cha mitume), kwa kuwa ubatizo ulikuwa ni ishara ya kuzikwa pamoja na Kristo na kufufuka pamoja naye, ikiashiria uhalisi uliotokea kwa mtu mara tu baada ya kuamini. Hakukuwa na muda mrefu wa kusubiri wala hakukuwa na mafundisho ya muda mrefu ya kumfanya mtu awe na kigezo cha kubatizwa (Matendo 2:41; 8:12, 36-38; 9:18; 10:47-48; 16:31-33; 22:16).
Kama tulivyoona katika maandiko yaliyoorodheshwa hapo juu (pamoja na Maandiko kama Marko 16:15-16 na Mathayo 28:19-20), baada ya mtu kuamini (yaani kupata wokovu) ndipo mtu alitakiwa kubatizwa. Hivyo, ubatizo ni kwa watu waliookoka na sio vinginevyo.
Shughuli za kanisa kwa mujibu wa Mtume Paulo.
Kupitia barua ya kwanza ya Mtume Paulo kwa Wakorintho, tunajifunza mambo mengine ambayo kanisa lilikuwa likiyafanya lilipokutana. Mambo haya tofauti na yale ya awali yameandikwa katika muktadha wa masahihisho, lengo likiwa ni kuhakikisha yanafanyika kwa utaratibu unaofaa na kwa lengo kusudiwa. Hivyo, ni wazi kuwa Mtume Paulo alitegemea kwamba mambo haya yafanyike katika makusanyiko ya kanisa.
Kutoka kwa 1 Wakorintho 14:26-33 tunaona kanisa lilikuwa linafanya mambo yafuatayo:
- Kuimba Zaburi
- Kupokea na kutoa ufunuo wa kiroho
- Kunena kwa lugha mpya
- Kutasfiri lugha mpya
KUIMBA ZABURI
Kama ambavyo Mtume Paulo anawasisitiza Wakorintho wafanye mambo yote kwa mpangilio na akihusisha kuwepo kwa wakati wa kuimba nyimbo au zaburi (1 Wakorintho 14:26), ndivyo hivyo hivyo anawaagiza makanisa mengine kufanya jambo hili. Paulo anawaambia Waefeso na Wakolosai pia washiriki pamoja katika kuimba zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni. Kwenye barua yake kwa Waefeso, Paulo anaonyesha makusudi mawili ya kuimba: kusudi la kwanza la kuimba likiwa ni kusemezana waamini, na kusudi la pili likiwa ni kumwimbia Mungu na kumshangilia. Katika barua hii, Mtume Paulo anasema “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu;” (Waefeso 5:18-19).
Kwa Wakolosai vivyo hivyo Mtume Paulo anaonyesha makusudi mawili ya kuimba. Kusudi la kwanza ni kufundishana na kuonyana na kusudi la pili ni kumwimbia Mungu. Katika waraka huu, Paulo anasema “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.” (Wakolosai 3:16). Ushahidi huu wa kutoka kwenye maandiko unaonyesha jinsi ambavyo kanisa lilitarajiwa kushiriki katika kuimba nyimbo au zaburi katika kusanyiko kwa makusudi tajwa hapo juu.
Pia, tuna ushahidi nje ya Biblia unaoonyesha kwamba kanisa lilishiriki katika kuimba nyimbo hata katika kipindi ambacho kukusanyika kwao tu kulihatarisha maisha yao. Kupitia barua ya Pliny Mdogo (Pliny the Younger) kwenda kwa Kaisari Trajan, aliyoiandika kati ya mwaka wa 110-112 BK, tunapata ushahidi huu. Barua hii Pliny Mdogo, Gavana wa Bithinia—mji uliokuwa kaskazini mwa Asia Ndogo (Uturuki ya sasa)—aliandika kwa kusudi la kumuuliza Kaisari Trajan ni kwa namna gani ashughulike na Wakristo. Katika barua hii Pliny mdogo anasema Wakristo “Walikuwa na desturi ya kukutana siku iliyopangwa kabla ya mapambazuko na kuimba kwa zamu wimbo kwa Kristo kana kwamba ni kwa mungu.” Pamoja na kwamba maandishi haya yanatoka kwa mtawala mpagani (asiyeamini) yanaeleza wazi ni mambo gani waamini walikuwa wanafanya pale wanapokutana. Na jambo moja kati ya mengi aliyoyataja ilikuwa ni kuimba kwa Yesu, Bwana wao.
Kwa ushahidi huu wote, ni dhahiri kwamba kanisa la leo pia linatakiwa kuimba nyimbo, tenzi na zaburi pale tunapokutana kwa makusudi tajwa hapo.
KUPOKEA NA KUTOA UFUNUO WA ROHO
Jambo lingine la muhimu sana waamini wa kanisa la karne ya kwanza walikuwa wanafanya walipokutana lilikuwa ni kupokea ufunuo kutoka kwa waamini wenye zawadi/karama/huduma ya unabii. Kwa kuwa Wakorintho walitumia zawadi hizi Mungu alizowapa kwa malengo tofauti tofauti na hivyo kupelekea machafuko, Mtume Paulo anawarekebisha kwa kuwaambia kwamba: “…Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga.” (1 Wakorintho 14:26). Katika kutoa maelekezo ya namna nzuri ya kufanya jambo hili katika kusanyiko, Mtume Paulo anasema: “Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue.” (1 Wakorintho 14:29).
Kwa maelekezo hayo, ni dhahiri kwamba Mtume alitegemea kanisa kupokea ufunuo wa Roho kutoka kwa manabii. Lakini ili mambo mengine pia yafanyike na sio unabii tu, Mtume anatoa maelekezo kwamba wanene manabii wachache—wawili au watatu. Manabii wengine, Mtume Paulo anawapa kazi ya kupambanua ufunuo huo wa Roho kama kweli unatoka kwa Roho au la. Katika barua yake kwa Wathesalonike, Mtume Paulo anasisitiza kwamba ujumbe wa unabii (ufunuo wa Roho) ujaribiwe kabla ya kutekelezwa, lakini pia ujumbe huo usipuuzwe (1 Wathesalonike 5:20).
Zaidi ya kupambanua, Mtume Paulo anatoa maelekezo pia kwamba manabii wapeane nafasi ya kutoa ufunuo wa Roho ili waamini “wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe” (1 Wakorintho 14:31). Mwisho, Paulo anasisitiza utii wa manabii kwa manabii wenzao (1 Wakorintho 14:32).
Maelezo haya marefu ya Mtume Paulo yanaonyesha kwamba alikubaliana na kanisa kupokea ufunuo wa Roho kutoka kwa manabii, na alitaka jambo hilo lifanyike kwa ajili ya kulijenga kanisa—yaani, kwa ajili ya kusababisha kanisa zima likue na kuongezeka katika kumfanania Bwana wetu Yesu Kristo. Sisi pia, waamini wa leo, tunatakiwa kuruhusu manabii wapate nafasi katika makusanyiko yetu ili tupate ufunuo wa Roho ulio na makusudi ya kujenga kanisa.
Matumizi mabaya ya huduma hii kwa baadhi ya watu yamepelekea makusanyiko mengine kutokutoa nafasi kabisa kwa ajili ya manabii, lakini hilo siyo suluhisho. Mtume Paulo, kwa kujua huduma hii inaweza kutumiwa vibaya na kwa kutambua umuhimu wake, ndio maana ametoa maelekezo mengi ili kuhakikisha huduma hii inafanya kazi kwa makusudi husika. Maelekezo haya ni: Uwepo wa utaratibu mzuri wa kupokea ufunuo wa Roho kwa watu wachache katika kusanyiko moja. Uwepo wa manabii na waamini wengine wenye uwezo wa kupambanua usahihi na ukweli wa unabii huo. Uwepo wa utii kati ya manabii kwa manabii wenzao. Hivyo, kila kusanyiko linatakiwa kutoa nafasi kwa ajili ya manabii kutoka unabii kwa ajili ya kanisa kama ambavyo tunaweza kutoa nafasi kwa ajili ya nyimbo na mafundisho.
KUNENA KWA LUGHA MPYA NA KUFASIRI.
Jambo jingine la muhimu ambalo Mtume Paulo analitolea maelekezo kwa urefu katika sura hii ya kumi na nne ya barua yake kwa Wakorintho ni kunena kwa lugha mpya na kufasiriwa kwa lugha hiyo. Moja ya mambo ambayo kanisa kwa sehemu kubwa limeyaweka kando ni jambo hili. Wengi wamefundisha kwamba jambo hili lilikuwa kwa ajili ya kanisa la kwanza tu, na muda huo ulipopita, nalo likapita. Pamoja na mafundisho hayo, hatuoni fundisho lolote la Biblia linaloonyesha kwamba kunena kwa lugha mpya kulikuwa kwa ajili ya kanisa la mitume tu. Mtume Paulo anapotoa maelekezo kwa Wakorintho anaonyesha kwamba alitegemea jambo hili kufanyika katika kusanyiko.
Kunena kwa lugha mpya, ambako Mtume Paulo anategemea kufanyike katika kusanyiko, ni kule ambako lugha hiyo itafasiriwa ili kanisa lijengwe na si vinginevyo. Mtume Paulo anaenda mbali zaidi hadi kufikia kunyamazisha kabisa kunena kwa lugha kama lugha hiyo haitapata mtu atakayefasiri (1 Wakorintho 14:27-29). Sisi, kanisa la leo, pia tunatakiwa kutoa nafasi ya kusikia ujumbe wa Mungu kupitia kunena kwa lugha mpya na kufasiriwa kwa lugha hiyo.
Sio mambo tajwa hapo juu tu ndio mambo pekee kanisa linatakiwa kufanya linapokutana, bali kanisa linaweza kufanya mambo mengi zaidi ya hayo. Haya ni msingi tu wa mambo kanisa lilikuwa linafanya, hata hivyo hatujamaliza kutaja mambo yote ambayo kanisa la kwanza lilikuwa linafanya kutokana na mwitikio wao kwa maelekezo ya Bwana Yesu. Muongozo wa nini kanisa lifanye ni LENGO la kanisa. Kwa lugha nyepesi, kanisa linaweza kufanya jambo lolote pale linapokutana kama jambo hilo linasaidia waamini kukua katika kumfanania Kristo Yesu. Lakini pia, kwa pamoja kanisa linaweza kufanya jambo lolote lile ambalo linawaleta wasioamini katika imani. Kama jambo lina matokeo kinyume na LENGO la kanisa basi jambo hilo halitakiwi kufanywa na kanisa.
Mambo haya tajwa hapo juu sio sheria kwamba yafanyike kila wakati kanisa linapokutana na wala haina maana kwamba kanisa lisipofanya jambo moja wapo ya hayo basi linakuwa limekusanyika kwa hasara. Mambo yote yanatakiwa kufanyika kwa utaratibu unaolenga kuhakikisha lengo la kanisa linatimia. Mambo haya yanaweza kufanyika kila wakati kanisa linapokutana kama inawezekana au yanaweza kufanyika kwa nyakati tofauti tofauti kutokana na uhitaji au uongozi wa Roho mtakatifu.
REJEA
Justin Martyr. The First Apology. In The Ante-Nicene Fathers, Vol. 1, edited by Alexander Roberts and James Donaldson, 163–186. Buffalo, NY: Christian Literature Publishing Co., 1885. Reprint, Peabody, MA: Hendrickson Publishers, 2004. Accessed March 13, 2025. https://www.ccel.org/ccel/schaff/anf01.html.
Pliny the Younger. Letters of the Younger Pliny. Translated by John D. Lewis. London: Trübner & Co., 1873. Accessed May 24, 2025. https://ia902807.us.archive.org/34/items/lettersofyounger00plinuoft/lettersofyounger00plinuoft.pdf.

