Tito – Mwongozo na Ufafanuzi


MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA MTUME PAULO KWA TITO.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.

UTANGULIZI.

Paulo aliandika waraka huu kwenda kwa Tito mwanae katika Imani. Paulo aliandika waraka huu muda mfupi baada ya kumuacha Tito huko krete (1:5) na wakati anatarajia kuonana naye tena huko Nikopoli (3:12). Kwa kuwa hakuna maelezo ya Mtume Paulo kuhubiri huko Krete katika kitabu cha matendo ya mitume isipokuwa alipita tu (Matendo 27:7-8)[1] ni dhahiri kwamba huu umisheni Paulo alioufanya na Tito ulifanyika baada ya kutoka kwenye kifungo chake cha nje huko Rumi. Hivyo waraka huu uliandikwa wakati wa karibu na waraka wa kwanza kwa Timotheo.

TITO.

Tito alikuwa ni myunani ambaye hakutahiriwa (Wagalatia 2:3) na mfanyakazi pamoja na Paulo katika Injili (2 Wakorintho 8:23). Hakuna habari nyingi zinazomhusu Tito katika Agano jipya isipokuwa tunamuona anatajwa sana katika waraka wa pili wa mtume Paulo kwa Wakorintho. Na hii ni kwa sababu Paulo alimtuma Tito huko Korintho kupeleka “waraka wa huzuni”[[2]] baada ya ushirika wa Paulo na kanisa la korintho kuingia dosari. Baada ya Tito kupeleka waraka huo kanisa lilitubu na Tito akaonana na Paulo huko makedonia na akampa taarifa njema kwamba waraka umefanya kazi kusudiwa (2 Wakorintho 7:5-16). Baada ya kupokea taarifa hiyo nzuri Paulo akaandika waraka mwingine ambao tunauita kuwa ni waraka wa pili kwa wakorintho na akampa Tito aupeleke. Hivyo Tito alihusika sana katika dosari iliyojitokeza kati ya Mtume Paulo na kanisa la Korintho.

KANISA LA KRETE.

Hakuna maelezo katika kitabu cha matendo ya mitume kuhusu kanisa la huko krete, hivyo kanisa hili linaonekana lilizaliwa baada ya Paulo kutoka kifungoni huko Rumi (Matendo 28:30). Baada ya kifungo hicho Paulo alikwenda krete na Tito na wakahubiri na baada ya makanisa kuzaliwa kisiwani hapo yeye alimuacha Tito huko ili kukamilisha mambo na kuchagua viongozi katika kila mji. Wakati huu wa uhuru wa Paulo baada ya kifungo cha kwanza cha huko Rumi ndio wakati pia alimuacha Timotheo huko Efeso kuwakataza watu wasihubiri elimu nyingine na baadae akamuandikia waraka wa kwanza. Hivyo waraka wa kwanza kwa Timotheo na Tito ziliandikwa wakati huo, ndio maana nyaraka hizi mbili zinafanana sana. Tofauti yao ni kwamba Kanisa la Efeso lilikuwa ni kanisa la muda mrefu na kanisa la Krete lilikuwa kanisa lilitoka kuzaliwa hivi karibuni. Pamoja na kanisa kutokuwa na muda mrefu inaonekana waalimu wa uongo walikuwa tayari wametokea (1:10-16) ambao kwa kiasi wanafanana na waalimu wa uongo waliokuwa Efeso wakati wa Timotheo.

KUSUDI LA WARAKA.

Paulo aliandika waraka huu kwa Tito kwa ajili ya kumkumbusha na kumuelekeza Tito kufanya majukumu aliyomuachia kufanya huko kisiwani krete. Paulo alimuacha Tito kisiwani krete ili ayatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee/viongozi wa kanisa katika kila mji (1:5). Hivyo waraka huu unaeleza kuhusu mambo hayo mawili. Moja, unaeleza sifa za watu wanaotakiwa kuwa viongozi/wazee/askofu (1:6-9) na pili unaeleza mambo yaliyopungua na namna Tito anavyotakiwa kufanya ili kuyatengeneza (1:10-3:15).

MPANGILIO.

NambaMaandikoMaelezo
11:1-4Utangulizi
21:5Makusudi ya Barua
31:6-9Kusudi la Kwanza. Sifa za Wazee/Maaskofu
41:10-3:11Kusudi la Pili. Tengeneza yaliyopungua
 A1:10-16Vinywa vya Waalimu wa Uongo vizibwe
B2:1-15Fundisha kweli kwenye makundi katika kanisa.
C3:1-8Wakumbushe waamini mwenendo mwema kwa ajili ya wasioamini
D3:9-11Jiepushe na mashindano ila shughulika na anayesababisha mgawanyiko.
53:12-15Mwisho wa Barua
 A3:12-14Maagizo ya Mwisho
B3:15Salamu za Mwisho

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.

Waraka huu una muundo kama nyaraka zilivyotakiwa kuwa yaani una utangulizi wa waraka (1:1-4), ujumbe mkuu (1:5-3:11) na Mwisho wa waraka (3:12-15). Utangulizi una utambulisho/anuani ya mwandishi (1:1-3), anuani ya mwandikiwa (1:4a) na salamu (1:4b). Huu ni waraka ambao mtume Paulo amejieleza kwa maneno mengi zaidi katika utambulisho wake ukilinganisha na nyaraka nyingine.

Sehemu ya ujumbe mkuu (1:5-3:11) inaweza kugawanywa kwenye sehemu tatu kama ifuatavyo.

Sehemu ya kwanza ya Ujumbe mkuu (1:5), ni sehemu ambayo Paulo anataja kusudi la kumuacha Tito huko kisiwani krete na hilo ndilo kusudi la kuandika waraka huu. Paulo alimuacha Tito huko Krete ili ayatengeneze yaliyopunguka na ili kuchagua viongozi wa kanisa katika kila mji. Hivyo Paulo aliandika waraka huu kumkumbusha Tito kufanya kazi hiyo na kumuelekeza namna ya kufanya kazi hiyo.

Sehemu ya pili ya Ujumbe mkuu (1:6-9), Paulo anampa Tito sifa ambazo ndio zinatakiwa kuwa vigezo vya kumpa mtu nafasi ya uongozi katika kanisa. Sifa hizi ziko kwenye makundi mawili, kundi la kwanza ni sifa za kimwenendo/kimaadili (1:6-8) na kundi la Pili ni sifa za usahihi katika fundisho (1:9). Sifa ya usahihi wa fundisho ilikuwa muhimu kwa sababu tayari waalimu wa uongo walikuwa wameshakuwepo katika kanisa.

Sehemu ya Tatu ya Ujumbe mkuu (1:10-3:11), Paulo anamuonyesha Tito mambo yanayotaka matengenezo na anamueleza namna ya kufanya matengenezo. Mambo yanayohitaji matengenezo ni kama yafuatayo

A. Vinywa vya waalimu wa uongo vizibwe (1:10-16)

B. Makundi katika kanisa yafundishwe maneno yenye Uzima (2:1-15)

C. Waamini wote kwa ujumla wakumbushwe mwenendo mwema waliotiwa kwa ajili ya wasioamini (3:1-8)

D. Jiepushe na mashindano ila shughulika na anayesababisha mgawanyiko (3:9-11).

Fuatilia taratibu

A. Vinywa vya waalimu wa uongo vizibwe (1:10-16).

Paulo anamtaka Tito uwakemee kwa ukali wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara ambao wanafundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu. Waalimu hao wa uongo Paulo anasema wazibwe vinywa na Tito lakini na wazee ambao atawachagua ambao wanaijua kweli (1:9, 1:10-16).

B. Makundi katika kanisa yafundishwe maneno yenye Uzima (2:1-15).

Baada ya hapo Paulo anamuagiza Tito afundishe mafundisho yenye Uzima (2:1) katika makundi yafuatayo.

a. Wanaume wazee (2:2)

b. Wanawake wazee (2:3)

c. Wanawake vijana (2:4-5). Hawa watafundishwa na wanawake wazee

d. Wanaume vijana (2:6)

Yeye mwenyewe awe kielelezo katika kufundisha kwa usahihi na ustahivu na awe kielelezo katika matendo mema (2:7-8.)

e. Watumwa (2:9-10)

Makundi hayo yote yafundishwe hivyo kwa kuwa ndivyo neema ya Mungu iokoayo iliyofunuliwa anavyotufundisha kuishi hapa duniani sasa (2:11-12) huku tukitarajia ujio wa Yesu kristo mara ya Pili, Mungu mkuu na mwokozi wetu (2:13-14).

Paulo anamalizia sehemu hii kwa kusisitiza kwamba mambo hayo (2:2-14) ayafundishe kwa kunena/kusema, kuonya na kukaripia kwa mamlaka yote (2:15) kama alivyoanza kumwambia mwanzoni (2:1).

C. Waamini wote kwa ujumla wakumbushwe mwenendo mwema waliotiwa kwa ajili ya wasioamini (3:1-8).

Paulo sasa anarudi kumuelekeza Tito kwa ajili ya kanisa zima, kwa ujumla bila kuzingatia makundi yao. Paulo anamtaka Tito awakumbushe/awasisitize waamini waishi maisha mapya Mungu aliyowaitia mbele za watu (3:1-2), tofauti na mwenendo wao wa kwanza kabla hawajaokolewa (3:3). Katika kusisitiza hilo Paulo anamuonyesha Tito msingi wa waamini kuishi hivyo, msingi huu ni kwamba Mungu kwa upendo wake alituokoa si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda bali kwa rehema yake. Na hivyo alituzaa mara ya pili na akatufanya upya kwa Roho Mtakatifu na zaidi alituhesabia haki na kutufanya warithi wa uzima wa milele (3:4-7). Maneno hayo Paulo anamuagiza Tito ayanene kwa waamini, ili wadumu katika matendo mema maana yanafaa kwa wanadamu (3:8).

D. Jiepushe na mashindano ila shughulika na anayesababisha mgawanyiko (3:9-11).

Mambo ambayo Paulo alimtaka Tito afundishe ni yale kuanzia 2:1 mpaka 3:8, na hivyo anamuagiza ajiepushe na maswali ya upuzi, nasaba, magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa maana mambo hayo hayana faida, tena hayana maana (3:9). Tena anamuagiza Tito kwamba mtu anayefundisha vitu vinavyoligawa kanisa (mzushi) amuonye mara mbili na kama hajakubali kuacha basi mtoe katika ushirika wa kanisa. Kwa kufanya hivyo Tito anatakiwa kujua kwamba mtu huyo amejihukumu yeye mwenyewe (3:10-11). Kwa muktadha huu mzushi ni mtu anayefundisha kinyume na mafundisho ambayo mtume Paulo anamuagiza Tito kufundisha.

Paulo mwisho wa Waraka wake (3:12-15) anampa Tito maelekezo kadhaa (3:12-14) na salamu za Mwisho (3:15).



FOOTNOTES


[1] Bandari nzuri ya mji wa lasea ilikuwa katika kisiwa cha Krete

[2] Waraka huu wa huzuni hatunao katika Agano jipya ila unatajwa katika waraka wa Pili wa mtume kwa Wakorintho (2 Wakorintho 7:5-16 hasa mstari wa 8)

UFAFANUZI WA WARAKA WA MTUME PAULO KWA TITO.

Unakuja hivi karibuni…….