MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA MTUME PAULO KWA WAFILIPI
MAELEKEZO
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako; usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI
Barua ya mtume Paulo kwa Wafilipi ni barua ambayo Mtume Paulo aliiandika akiwa Rumi katika kifungo chake cha ndani; akiwa anasubiri hukumu ya kesi yake. Hii ilikuwa ni baada ya kusafirishwa kutoka Kaisaria kwa sababu yeye mwenyewe aliamua kukata rufaa ili kwamba kesi yake ikasikilizwe makao makuu ya dola ya Rumi (Matendo 21:5-28:31). Katika kifungo hichi, Mtume Paulo aliandika barua nyingine kama vile barua kwa waefeso, wakolosai na barua kwa Filemoni. Hii ilikuwa katikati ya miaka ya 59 na 61 BK, hivyo barua hii inakadiliwa kuwa iliandikwa mwaka wa 61 BK.
Utofauti wa barua hii na barua nyingine unaweza kuwekwa katika muhtasari huu; waraka huu ni waraka uliojaa furaha ya mahusiano mazuri na ya karibu yaliyoundwa na ushirika wa pamoja katika injili kati ya mtume Paulo na Wafilipi.
Kuhusu furaha, Waraka huu ndio waraka ambao mtume Paulo ametaja neno furaha/furahini kwa mara nyingi zaidi kwa asilimia kuliko nyaraka nyingine. Hii ni kwa sababu ya furaha yake kubwa aliyokuwa nayo kwa sababu ya maisha ya Wafilipi.
Kuhusu uhusiano mzuri na wa karibu, huu ndio waraka wenye lugha ya kifamilia iliyojaa hisia za ukaribu zaidi kuliko nyaraka nyingine za Paulo. Paulo anaeleza kwa hisia kabisa kwamba Wafilipi wako ndani ya moyo wake (1:7–8; 4:1) na anaonyesha hilo kwa kutumia lugha za kifamilia kama “wapendwa wangu,” “ndugu zangu,” “furaha yangu,” na “taji yangu,” mara nyingi zaidi. Lakini pia, Paulo anazungumza kwa wazi hali yake binafsi, matarajio yake, na shauku yake ya kuwaona Wafilipi wakisimama imara katika Injili (1:12–27; 2:19–20; 3:1; 4:10–20).
Kuhusu ushirika wa pamoja katika injili, Mtume Paulo ameweka wazi mara kadha katika waraka huu kwamba anamshukuru Mungu na anawashukuru wafilipi kwa moyo wao wa kushiriki pamoja naye katika injili toka mwanzo mpaka wakati huu akiwa kifungoni . Wafilipi washirikiana na mtume Paulo katika kuhubiri, kuitetea injili (4:2-3) na katika kutoa mara kadhaa kwa ajili ya mahitaji ya Mtume Paulo akiwa katika kuhubiri injili (1:3–5, 7; 4:10-20).
Kwa hiyo, waraka huu ni waraka uliojaa furaha ya mahusiano mazuri na ya karibu yaliyoundwa na ushirika wa pamoja katika injili kati ya mtume Paulo na Wafilipi.
MJI WA FILIPI
Mji wa Filipi ambao mtume Paulo aliutembelea na kufanya umisheni ulikuwa ni mji mdogo, koloni la Kirumi lililokuwa katika jimbo la Kirumi la Makedonia. Pamoja na udogo wake, Filipi ulikuwa ni kati ya miji michache sana nje ya Italia ambayo ilipewa hadhi ya kuwa “Rumi ndogo.” Hii ina maana kwamba Filipi uliongozwa kwa kufuata sheria za Kirumi kama zilivyotumika Italia. Hii ilipelekea raia wa Kirumi waliokuwa wanaishi Filipi kupata haki na upendeleo sawa na raia wa Kirumi waliokuwa katika mji wa Rumi; makao makuu ya dola nzima. Haki hizi zilijumuisha kununua, kumiliki, na kuuza ardhi. Aidha, kama ilivyokuwa kwa raia wa Kirumi walioishi maeneo mengine, walipata msamaha wa kodi ya ardhi na kodi ya kichwa. Kutokana na sababu hizi, mji wa Filipi ulikuwa na watu wa kutosha wenye uraia wa Kirumi (Matendo 16:12, 21). Pia, kwa miaka kadhaa ya nyuma, wanajeshi wengi wastaafu walikwenda kuishi huko, jambo lililosababisha pia mji huu kuwa na idadi ya kutosha ya raia wa Kirumi.
Kutokana na ukweli kwamba suala la uraia lilikuwa na maana kubwa sana katika mji huu, ndiyo maana mtume Paulo aliwafundisha Wafilipi kwamba wao ni raia wa mbinguni (Wafilipi 3:20), wala si raia wa dunia hii. Vilevile, ndiyo maana aliwahimiza Wafilipi kuishi kama raia wa mbinguni (Wafilipi 1:27).[1] Lugha ya uraia ilikuwa ni lugha ambayo Wafilipi waliielewa vizuri. Lakini pia, hii ndiyo sababu mtume Paulo alikataa kuachiwa huru kimya kimya baada ya kufungwa gerezani alipokuwa hapa, kwa sababu yeye, kama raia wa Rumi, alipaswa kuhukumiwa kwanza kabla ya kutiwa gerezani (Matendo 16:35–40). Hivyo, alieleza uraia wake kwa makusudi, kwa kuwa alijua vyema thamani ya uraia wake katika mji wa Filipi (pamoja na ukweli kwamba uraia wa Kirumi ulikuwa na thamani mahali popote katika Dola ya Rumi, lakini katika mji wa Rumi na katika miji iliyokuwa na hadhi ya kuwa “Rumi ndogo,” uraia huo ulikuwa na faida zaidi).
Kutokana na kuwepo kwa idadi ya kutosha ya raia wa Kirumi, pamoja na watu kuendelea kuabudu miungu mingi kama ilivyokuwa kawaida katika dunia ya karne ya kwanza, dini ya kumuabudu Kaisari katika mji wa Filipi ilikuwa na nguvu zaidi. Kama ilivyokuwa kawaida ya dini katika ulimwengu wa kale, mahekalu yalijengwa kwa ajili ya kumuabudu Kaisari, makuhani walichaguliwa kuongoza ibada hizo, sikukuu za kidini zilianzishwa, na dhabihu zilifanywa kwa ajili ya Kaisari. Zaidi ya yote, Kaisari, katika kuabudiwa na kuheshimiwa, alipewa majina kama vile Bwana, Mwokozi, na Mleta amani.
Hivyo, Paulo anaposema kwamba Mungu amemkirimia Yesu jina lililo kuu kuliko yote, “ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” (Wafilipi 2:10–11), alikuwa anamaanisha kwamba Kaisari si Bwana, bali Yesu ndiye. Lugha hii ililenga kuonyesha upinzani wa moja kwa moja kwa Kaisari.
Aidha, jambo hili linaeleza pia ni kwa nini mafundisho ya Paulo na Sila yalilalamikiwa pale walipopelekwa mbele ya makadhi baada ya kukamatwa. Kutangaza kwamba Yesu ni Bwana katika mji ambao ulihifadhi na kuendeleza sana ibada za Kaisari kwa sababu ya manufaa uliyoyapata kutokana nazo, ilikuwa ni kwenda kinyume kabisa na desturi ambazo raia wa Kirumi walitarajia ziendelee kuenezwa (Matendo 16:19–21). Vilevile, hii ndiyo sababu Kanisa la Filipi liliendelea kukumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa raia hawa wa Kirumi baada ya mtume Paulo kuondoka (Wafilipi 1:28–30).
Kukosekana kwa sinagogi la Kiyahudi ni moja ya ushahidi kwamba mji wa Filipi ulikuwa na idadi ndogo ya Wayahudi. Lakini pia, waamini wote ambao Paulo anawataja katika barua hii wana majina ya Kiyunani (Euodia, Sintike, na Epafrodito) na ya Kirumi (Klementi), wala si ya Kiyahudi. Yote haya yanaonyesha kwamba mji huu ulikuwa na idadi ndogo ya Wayahudi, na hivyo Kanisa la Filipi lilikuwa na waamini wengi zaidi kutoka kwa watu wa mataifa. Vilevile, kwa mtume Paulo kunukuu Maandiko ya Agano la Kale kwa nadra sana katika barua hii ni ishara kwamba waamini wengi wa Filipi walikuwa wamataifa, jambo linaloendana na hali ya mji kuwa na Wayahudi wachache.
Kiuchumi, mji wa Filipi ulikuwa ni mji wenye utajiri unaotokana na kilimo (tofauti na miji kama Korintho na Efeso, ambapo utajiri ulitokana na biashara), lakini utajiri huu ulikuwa kwa watu wachache ambao kwa sehemu kubwa walikuwa raia wa Kirumi. Hivyo, kiuchumi bado kulikuwa na watu wenye uutajiri mkubwa na watu wenye umaskini mkubwa.
KANISA LA FILIPI NA MTUME PAULO.
Kanisa la Filipi lilizaliwa katika safari ya pili ya kimishenari ya mtume Paulo. Safari hii ilianza mwaka wa 50 BK, Paulo akiwa na Sila. Kutoka Antiokia wakasafiri kwenda Derbe, na walipofika Derbe wakaenda Listra, ambako Paulo akamchukua Timotheo kuwa miongoni mwa watu wa timu hii ya kimishenari (Matendo 16:1–5). Baada ya hapo, walipitia Frigia na Galatia, lakini wakazuiliwa na Roho Mtakatifu kuhubiri Asia; hivyo wakapitia Misia na kufika Troa. Huko Troa, daktari Luka akaungana na timu hii katika kazi hii ya kimisheni.
Hapo Troa, Paulo akapata maono ya mtu wa Makedonia akimwomba avuke kwenda kuwasaidia. Baada ya maono hayo, timu ikasafiri kutoka Troa kuelekea Makedonia kwa kupitia Samothrake na kufika Neapoli (bandari iliyokuwa karibu na mji wa Filipi). Makedonia (Ulaya ya sasa) ilikuwa ni jimbo ambalo ndani yake kulikuwa na miji ya Filipi, Beroya, Thesalonike, na mingine. Hivyo basi, walipofika jimbo la Makedonia, walianza kazi yao ya injili katika mji wa Filipi.
Kwa kuwa katika mji huu hakukuwa na sinagogi la Wayahudi, walienda kando ya mto, ambako walijua kungekuwa na eneo la kukusanyika Wayahudi. Walipofika eneo hilo, Injili ikahubiriwa hapo, na kanisa likazaliwa. Miongoni mwa waamini wa kwanza katika mji huu, na ambao baada ya kuamini walifanya kazi ya Injili pamoja na Paulo, Sila, Timotheo, na Luka, walikuwa ni—Lydia, Euodia, na Sintike, pamoja na Klementi (Wafilipi 4:2–3).
Baada ya kufungwa gerezani na kutoka kwa muujiza, Paulo na Sila wakasafiri kutoka Filipi hadi Thesalonike (Timotheo alikuwepo kwenye msafara, japo hakuwepo gerezani). Luka akabaki Filipi, kama anavyotuonyesha kwa kusema, “Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi” (Matendo 17:1). Huko Thesalonike, walihubiri Injili—wakijadiliana nao kutoka katika Maandiko—kwenye sinagogi la Wayahudi kwa zaidi ya Jumamosi tatu, na baadhi ya Wayahudi, watu wa mataifa waliomcha Mungu kwa dini ya Kiyahudi, pamoja na wanawake wenye vyeo wakaamini. Katika kipindi hiki cha kufanya kazi Thesalonike, Paulo na timu ya Injili walipokea sadaka kwa ajili ya mahitaji yao kutoka kwa kanisa la Filipi (Wafilipi 4:15–16).
Pamoja na watu kadhaa wa Thesalonike kuamini, kulitokea upinzani mkali dhidi ya timu ya kimisheni kutoka kwa Wayahudi; hivyo wakasafiri na kwenda Beroya. Wayahudi wa Beroya walikuwa waungwana; walijifunza, na wengine wakaamini. Hata hivyo, Wayahudi wa Thesalonike waliposikia habari hizo, wakaifuata timu ya kimisheni hadi Beroya na wakafanya ghasia huko pia, kiasi cha kumsababisha Paulo kuondoka Beroya na kwenda mpaka Athene (Matendo 17:11–14), huku Timotheo na Sila wakibaki Beroya. Baada ya muda mfupi, Timotheo na Sila wakamfuata Paulo huko Athene na wakaonana naye kwa muda mfupi (1 Wathesalonike 3:1–5). Kutoka Athene, Paulo alimtuma Timotheo kurudi Thesalonike, na Sila kurudi Filipi kwa ajili ya kuwaimarisha waamini huko.
Kutoka Athene, Paulo akasafiri mpaka Korintho. Baada ya muda, Timotheo na Sila walimfuata Paulo huko Korintho, na muhimu zaidi, wakarudi na sadaka kutoka kwenye makanisa hayo (2 Wakorintho 11:8–9). Hivyo basi, mpaka wakati huu Paulo alikuwa amepokea mara kadhaa sadaka kwa ajili ya mahitaji yake kutoka kwa kanisa la Filipi.
Tena, miaka kadhaa baadaye, Paulo akiwa katika safari yake ya tatu ya kimisheni, ambayo kwa sehemu ilihusisha kukusanya fedha katika makanisa ya mataifa kwa ajili ya kupeleka kwa kanisa la Yerusalemu, alifika Filipi. Kwa kuwa Wafilipi walikuwa katika hali ngumu ya kifedha, na kwa kuwa tayari walikuwa wameonyesha ukarimu mkubwa mara kadhaa, Paulo hakuwa na nia ya kuwahusisha katika utoaji huu. Hata hivyo, mara tu waliposikia habari zake, Wafilipi walisisitiza kushiriki katika utoaji huo, pamoja na changamoto zao kubwa za kifedha walizokuwa nazo, na hivyo wakatoa kwa ajili ya kanisa la Yerusalemu (2 Wakorintho 8:1–5).
Paulo, baada ya kukusanya fedha hizo na za makanisa mengine, alizipeleka Yerusalemu (Matendo 21:17–19; Warumi 15:25–32), na huko ndiko alikamatwa na kufungwa kule Kaisaria kwa miaka miwili. Baada ya miaka miwili, alikata rufaa ili kesi yake ikasikilizwe Rumi, na hivyo akasafirishwa mpaka Rumi. Huko Rumi, akiwa anasubiri hukumu yake, Paulo alipata nafasi ya kuhubiri Injili kwa watu wengi kwa kuwa alikuwa katika kifungo cha ndani. Pamoja na nafasi hiyo ya kuhubiri na kutembelewa na watu, kipindi hiki kilikuwa ni kipindi cha dhiki kwa Paulo, kipindi kilichojaa hali za kutokuwa na uhakika wa hatima yake, na kipindi kilichojaa mahitaji.
Baada ya kupata taarifa za Paulo, Wafilipi, kama kawaida yao, wakatoa fedha kwa ajili ya Paulo na wakamtuma Epafrodito kupeleka fedha hizo Rumi (Wafilipi 4:18). Pamoja na hilo, walitaka Epafrodito abaki Rumi kumsaidia Paulo, na badala yake Timotheo aende kwao. Wakati Epafrodito akiwa njiani kwenda Rumi, aliugua sana, na Wafilipi walipopata habari hizo wakawa na huzuni kubwa. Epafrodito akafikisha sadaka ya wafilipi na Paulo alipokaa pamoja naye kwa muda na baada ya Epafrodito kupona akaamua kuandika barua na kumtuma Epafrodito kurudi nayo Filipi. Paulo aliandika barua hii kwa makusudi yaliyoelezwa hapo chini.
KUSUDI LA WARAKA.
Paulo hajaweka wazi kwa nini aliandika waraka huu, lakini kwa kusoma vizuri waraka huu tunagundua kusudi lake la kuandika. Waraka huu uliandikwa kwa sababu zilizopo katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni sababu za kindugu/kirafiki. Kundi la pili ni sababu za kushughulika na changamoto walizokuwa nazo Wafilipi.
Kama tulivyoona hapo juu katika “Kanisa la Filipi na mtume Paulo”, mtume Paulo na kanisa la Filipi walikuwa na ushirikiano mkubwa, hali iliyosababisha kuwa na mahusiano mazuri. Hivyo, kutokana na uhusiano wao huu, baada ya kupokea sadaka kutoka kwao, Paulo aliandika waraka huu ili kutambua zawadi yao kwake/kutoa shukrani kwa sadaka yao. Lakini pia, kama ndugu yao, Paulo aliandika barua hii ili kuwaelezea hali yake akiwa kifungoni. Tena, Paulo aliandika barua hii ili kuambatana na Epafrodito anaporudi, yaani kumtetea na kuwaomba wamuheshimu kwa sababu ya sifa zake njema katika Bwana. Aidha, katika waraka huu Paulo alitaka pia kuelezea mpango wake wa kumtuma Timotheo baada ya kujua kesi yake itaendaje, na nia yake ya yeye mwenyewe kwenda ikiwa atapata uhuru tena (Wafilipi 2:19–26). Sababu zote hizi zinatokana na uhusiano wao mzuri wa kindugu katika Kristo.
Kundi la pili la sababu za kuandikwa kwa barua hii ni kushughulika na changamoto walizokuwa wanazipitia Wafilipi, kama ambavyo huenda alipewa taarifa na Epafrodito. Mafundisho ya Paulo hapa yanatokana na changamoto mbili. Moja, ni upinzani ambao waamini walikuwa wanaupata kutoka katika jamii inayowazunguka, uliokuwa unahusisha mateso (Wafilipi 1:28–30). Pili, ni kuwepo kwa faraka kati yao, yaani kukosekana kwa umoja ndani ya kanisa (Wafilipi 1:27; 2:1–16; 4:1–3).
Hivyo basi, Paulo aliandika barua hii ili kudumisha uhusiano wao mzuri, lakini pia ili kuwasaidia katika changamoto walizokuwa wanazipitia Wafilipi.
MPANGILIO WA KITABU.
| MAELEZO | MAELEZO | WAFILIPI |
| UTANGULIZI | Anuani | 1:1-2 |
| Shukrani | 1:3-8 | |
| Maombi | 1:9-11 | |
| KUFUNGWA KWA MTUME PAULO | 1:12-26 | |
| MAAGIZO YA MTUME PAULO | Kuuishi uraia kama ipasvyo Injili | 1:27-30 |
| Mwito wa Umoja | 2:1-4 | |
| Kuwa na nia kama ya Kristo | 2:5-11 | |
| Kufanyia kazi wokovu | 2:12-18 | |
| MIPANGO YA MTUME PAULO KWA AJILI YA WAFILIPI | Timotheo | 2:19-24 |
| Epafrodito | 2:25-30 | |
| KUJIHADHARI NA MAADUI WA MSALABA | Waalimu wa sheria | 3:1-11 |
| Kukaza mwendo | 3:12-16 | |
| Maadui wa msalaba | 3:17-4:1 | |
| HITIMISHO LA BARUA | Maagizo ya mwisho | 4:2-9 |
| Shukrani kwa sadaka | 4:10-19 | |
| Salamu za mwisho | 4:20-23 |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.
Barua hii, kama barua nyingine, inaanza na utangulizi unaotaja mtumaji wa ujumbe, wapokeaji wa ujumbe, na salamu (1:1-2).[2] Baada ya utangulizi, Paulo anatoa ripoti ya shukrani na maombi yake; huwa anamshukuru Mungu kwa ajili ya Wafilipi kila anapowakumbuka na anapowaombea. Anamshukuru Mungu kwa sababu ya ushiriki wao katika kueneza Injili, kuitetea, na kuithibitisha (1:3-8). Baada ya ripoti hiyo, mtume Paulo anawaombea Wafilipi. Anaomba kwamba upendo kati yao uzidi kuwa mwingi katika hekima na maarifa yote, ili waweze kuyakubali yaliyo bora zaidi. Mwisho wa siku wawe na moyo safi, wasiwe na mawaa/kosa lolote, na wajazwe matunda ya haki hata siku ya Kristo (1:9-11).
Baada ya utangulizi huu (anuani, shukrani, na maombi), mtume Paulo anaingia kuwaeleza Wafilipi kuhusu habari za kufungwa kwake. Paulo anawaambia Wafilipi kwamba kufungwa kwake kumefanya Injili iendelee mbele. Kupitia kufungwa kwake, Injili imeendelea mbele kwa namna mbili. Kwanza, imejulikana kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine kwamba yeye ni mfungwa kwa sababu ya Injili. Pili, waamini wamepata ujasiri wa kuhubiri Injili kwa nguvu; wengine kwa nia njema na wengine kwa nia mbaya (1:12–17). Mwitikio wa Paulo kutokana na hali hii ni upi? Kwanza, Paulo anafurahi kwa kuwa Injili inahubiriwa bila kujali nia ya wahubiri. Pili, ana uhakika kwamba atapata uhuru baada ya kifungo hiki. Paulo anasisitiza kwamba anajua hataaibika, bali Kristo atatukuzwa katika mwili wake, kwa namna yeyote ile—iwe kwa kifo au kwa kuishi kwake. Paulo anamalizia kwa kusema kwamba, pamoja na kutamani kwenda kuwa na Kristo, yaani kufa, anaona kuishi kunahitajika zaidi kwa sasa ili Wafilipi waendelee kukua katika Imani na kuifurahia na hatimaye wapate kuona fahari katika Kristo kwa sababu ya Mtume Paulo kuendelea kuishi (1:18-26).
Baada ya kuelezea kuhusu habari za kifungo chake, Paulo anahamia kwenye kushughulika na changamoto zilizokuwa katikati ya Wafilipi. Paulo, kwanza, anawaagiza Wafilipi kuishi uraia wao kama ipasavyo Injili ili, akiweza kwenda kuwaona au ikishindikana, apate taarifa ile ile kwamba wanasimama kwa umoja katika kuishindania imani ya Injili bila kuwaogopa wapinzani wao. Kuishindania imani ya Injili katikati ya upinzani ni ishara ya kupotea kwa wapinzani na ni ishara ya wokovu kwa Wafilipi. Kwa nini ushindani wa imani katikati ya upinzani ni ishara ya wokovu? Kwa sababu wamepewa zawadi ya kuteswa kwa ajili ya Kristo, kama walivyopewa zawadi ya kumwamini (1:27–30). Pili, Paulo anawaagiza Wafilipi waitimize furaha yake kwa kuwa na umoja katikati yao. Umoja utapatikanaje? Kwa kutokutenda neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno, bali kwa unyenyekevu; kwa kila mtu kumhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake; na mwisho, kwa kila mtu kutokuangalia mambo yake mwenyewe, bali kuangalia mambo ya wengine (2:1–4).
Kwa kuwa umoja unaletwa na kutokuishi kwa ubinafsi bali kuishi kwa unyenyekevu, agizo la tatu la Mtume Paulo ni kuwaagiza Wafilipi wawe na nia ile ile iliyokuwa ndani ya Kristo. Kristo alionyesha kwa vitendo unyenyekevu na kutokuwa na ubinafsi, na hivyo Mungu Baba akamtukuza kwa utukufu wake (2:5–11). Agizo la nne Mtume Paulo analolitoa kwa Wafilipi ni kuufanyia kazi wokovu wao wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa nini? Kwa sababu Mungu ndiye anayefanya kazi ndani yao, katika kutaka na kutenda kwao kulingana na mapenzi yake. Baada ya hapo, Paulo anaweka wazi namna moja wapo ya wao kuufanyia kazi wokovu wao: kutenda mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano, ili wapate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama wala hila, na ili mwisho wa siku, Yesu atakaporudi, Paulo aone faraja na furaha ya kazi yake (kumbuka, changamoto yao kubwa ilikuwa ni kukosa umoja). Mwisho, Paulo anawaita Wafilipi kufurahi pamoja naye, kwa kuwa yeye anafurahi hata kama maisha yake yanaweza kuishia katika kuuawa, juu ya maisha yao ya Imani (2:12-18).[3]
Baada ya kumaliza maagizo hayo, mtume Paulo anarudi katika kueleza yale yanayoendelea huko Rumi aliko na kuhusu maamuzi yake kuhusu Wafilipi. Hapa Paulo anaanza kwa kuwaeleza Wafilipi kwamba anatumaini kumtuma Timotheo kwao mara tu atakapojua mwelekeo wa kesi yake, ili afarijiwe atakapopata habari za hali yao kupitia Timotheo. Paulo anasema atamtuma Timotheo kwa sababu yeye ana sifa na nia kama yake, yaani nia ya kuwajali Wafilipi kweli kweli, tofauti na wengine ambao hawana nia ya Kristo. Pamoja na hayo, Paulo anatarajia kwenda yeye mwenyewe kwao baada ya kushinda kesi yake (2:19–24). Hata hivyo, pamoja na barua hii, mtume Paulo anawaambia Wafilipi kwamba imemlazimu kumrudisha Epafrodito kwao, kwa kuwa Epafrodito alikuwa na shauku kubwa ya kuwaona Wafilipi baada ya kuugua kwa kiwango cha kukaribia kufa. Mwishoni, mtume anawasisitiza Wafilipi wampokee Epafrodito na kumpa heshima kwa sababu ya moyo wake wa kujitoa katika kumhudumia Paulo (2:25–30).[4] Pamoja na kuwataja Timotheo na Epafrodito katika kuelezea hali yake na mipango yake, Paulo pia anawataja watu hawa kama mifano ya wale wanaoishi kwa vitendo yale maagizo manne aliyokuwa amewaagiza Wafilipi hapo juu.
Baada ya kueleza yale yaliyokuwa yakiendelea kwa upande wake, Paulo anarudi tena kuzungumzia hali ya Wafilipi. Anawaagiza wajihadhari dhidi ya waalimu wa uongo wa Kiyahudi, ambao walisisitiza kwamba ili mtu aokoke lazima atahiriwe. Kinyume na wao, Paulo anawahakikishia Wafilipi kwamba hawahitaji tohara ya mwili, kwa kuwa wao—pamoja na yeye—wanaomwabudu Mungu kwa Roho, wametahiriwa kweli kweli (3:1-3).[5] Kwa kuwa Wayahudi hawa wanaona fahari katika mwili, Paulo anawaonyesha Wafilipi kwamba yeye alikuwa na nafasi bora kuliko wao ya kuona fahari katika mwili; lakini kwa sababu ya kumjua Kristo Yesu, Bwana wake, ameyahesabu mambo yote yaliyompa sababu ya kuona fahari katika mwili kuwa kama takataka. Malengo ya kuyahesabu mambo hayo kama mavi ni mawili: kwanza, kumpata Kristo; na pili, kuonekana mbele zake katika siku ya mwisho akiwa na haki ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, ile itokayo kwa Mungu, kwa imani na siyo haki ipatikanayo kwa sheria. Mwisho, katika uhusiano wake huu mpya, Paulo anataka kumjua Kristo; anataka kujua uweza wa kufufuka kwake na kushiriki mateso yake ili, mwisho wa siku, apate ufufuo/kufufuliwa kutoka kwa wafu (3:4-11).
Kwa msisitizo wa kurudia-rudia maneno, Mtume Paulo anawaambia Wafilipi kwamba bado hajafika, hajakamilika, wala hajashika kile ambacho kwa hicho Kristo alimshikilia. Anasema anakaza mwendo kwa kusahau yaliyo nyuma na kupiga mbio kama wanariadha, ili mwisho wa siku apewe tuzo ya mwito mkuu wa Mungu (3:12–14). Kumbuka 4:11 alisema kwamba, kwa njia yoyote ile, anataka kufikia ufufuo wa wafu; hivyo basi, tuzo hii ni tuzo ya baada ya ufufuo. Mwisho, Paulo, akijijumlisha na Wafilipi waliokomaa, anawaita waishi kwa mtazamo huo wa kutazamia mambo ya mbele ndani ya Kristo. Lakini anasema kwamba kama kuna mtu ana mtazamo tofauti na yeye, Mungu atamwongoza kufika mtazamo huu sahihi. Pamoja katika hilo, anasisitiza kwamba pale walipofika wale waliokomaa wasihame, bali waendelee (3:15–16).
Paulo alianza na kuwasihi Wafilipi kujihadhari dhidi ya waalimu wa uongo wa kiyahudi, huku akionyesha jinsi yeye alivyoacha kuona fahari katika mwili kama wao wanavyofanya sasa, kwa sababu ya uzuri wa kumjua Kristo. Katika Kristo, Paulo anasema anatarajia mwisho wa siku kupata ufufuo, kitu ambacho bado hajafikia; na hivyo anaishi kwa kupiga mbio ili afikie kupewa tuzo ya mwito mkuu wa Mungu. Hivyo, mwisho wa aya hii, anamaliza kwa kuwaita Wafilipi kuiga mfano wa maisha yake na wa maisha ya waamini wanaoishi kama yeye. Anawaita kuiga mfano wa mwenendo wake kwa kuwa wapo wengi wanaoishi kinyume na msalaba wa Kriso. Tofauti na maadui wa msalaba, Paulo na waamini wote uraia wao uko mbinguni, ambako kutoka huko tunamsubiri Kristo aje ili aubadilishe mwili wetu wa unyonge kuwa mwili wa utukufu kama wake, kwa nguvu ambayo kwa hiyo aweza kuvitiisha vitu vyote chini yake. Kutokana na hilo wanalolisubiri, Paulo anawaita Wafilipi kusimama imara katika Bwana (3:17-4:1).
Paulo sasa anahitimisha barua hii kwa mahimizo matatu, neno la shukrani, na salamu za mwisho. Kwanza, kama alivyokwisha kuwasisitiza Wafilipi wote kuwa na umoja (2:2), Mtume anawahimiza Euodia na Sintike wapatanishwe ili wawe na nia moja (4:2–3). Pili, anawahimiza Wafilipi wote kufurahi katika Bwana, upole wao uwe dhahiri, na kutokujisumbua; badala yake wamjulishe Mungu haja zao (4:4–7). Tatu, anawahimiza Wafilipi kuyatafakari yaliyo ya kweli, ya heshima, ya haki, safi, ya kupendeza, yenye sifa njema, wema, na sifa nzuri na kutenda yale waliyojifunza, kuyapokea, kuyasikia na kuyaona kwa mtume Paulo (4:8–9).
Baada ya mahimizo hayo, Paulo anafurahia sadaka Wafilipi waliyoweza kuitoa sasa kwa kumtuma Epafrofito. Pamoja na hivyo, Paulo anasema haonyeshi furaha yake kwa sababu tu yuko kwenye uhitaji, kwa kuwa yeye amejifunza kuridhika katika hali zote. Pamoja na kusema hivyo, Paulo anawasifu Wafilipi kwa moyo wao wa utoaji toka mwanzoni wa utumishi wake. Na mwisho, anakiri kupokea sadaka zao kwa mkono wa Epafrodito na anawaombe kwamba Mungu awajaze kila kitu wanachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake (4:10-20).
Baada ya neno la shukrani, Paulo anafunga barua yake kwa salamu za mwisho (4:21-23)
FOOTNOTES
[1] Neno lililotafsiri “mwenendo” katika kiswahili katika kiyunani ni neno politeuesthe lenye maana ya kuishi kama raia.
[2] Paulo, katika nyaraka nne tu, hajitambulishi kama mtume. Nyaraka hizo ni Wathesalonike wa Kwanza na wa Pili, Filemoni, na waraka huu kwa Wafilipi. Katika nyaraka hizi nne, tatu kati yake ni kwa makanisa yaliyokuwa Makedonia. Kwa kusoma vizuri nyaraka hizi, utagundua kwamba makanisa ya Makedonia yalikuwa na uhusiano mzuri sana na mtume Paulo. Hivyo, ni sahihi kusema kwamba hakuona haja ya kutambulisha utume wake kwa makanisa ambayo yalikuwa na uhusiano mzuri naye.
[3] Mstari wa 17 na 18, Mtume Paulo anatumia lugha ya picha ya uendeshaji wa ibada kama ilivyokuwa katika Israeli au hata katika dini za kipagani. Paulo anaona kwamba imani au maisha ya imani ya Wafilipi ndiyo dhabihu kuu katika ibada, na kifo chake yeye, kama kitatokea, ni kama sadaka ya kuambatanishwa na dhabihu hiyo kuu. Sadaka ya kumiminwa ilikuwa ni sadaka inayoongezwa juu ya dhabihu/sadaka kuu kama vile sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya kuchinjwa (Hesabu 15:1–5). Hivyo, Paulo katika mstari wa 17–18 anasema kwamba ikiwa atauawa, yeye bado anafurahi, kwa kuwa kuawa kwake kutakuwa kama kumimina sadaka ya divai juu ya sadaka ya kuteketezwa, ambayo kwa muktadha huu ni maisha ya imani ya Wafilipi.
[4] Pamoja na kutaja sifa nzuri za Epafrodito, ukisoma kwa makini utaona kwamba kuna namna mtume Paulo anamtetea Epafrodito; anaagiza kwamba apokelewe na apewe heshima. Hii ni kwa sababu Wafilipi walikuwa na matarajio kwamba Timotheo angekuja kwao na Epafrodito angebaki na Paulo kifungoni. Hivyo basi, kurejea kwa Epafrodito bila maelezo haya kungeweza kusababisha mwitikio hasi kutoka kwa Wafilipi dhidi ya Epafrodito.
[5] Sifa zote tatu—mbwa, watendao mabaya, na wajikatao—zinawaelezea Wayahudi waliokuwa wakisisitiza kwamba mtu lazima atahiriwe (na kushika sheria) ili apate kuokoka. Hawa ndio waalimu waliobishana na Paulo na Barnaba huko Antiokia (Matendo 15:1–2), na ndio waliohubiri injili nyingine huko Galatia (Wagalatia 1:6–7; 5:2–3, 6; 6:12–13, 15). Kwa kawaida Wayahudi waliwaita wale wasio Wayahudi mbwa (kwa kuwa walikuwa wanakula kila kitu bila masharti), lakini Paulo anageuza kibao na kuwaita Wayahudi hawa mbwa. Tena, kwa kawaida Wayahudi waliwaita Mataifa watendao mabaya, lakini Paulo anageuza kibao na kuwaita Wayahudi hawa watendao mabaya. Mwisho, Paulo, badala ya kutumia lugha ya moja kwa moja—yaani kuwaita watu wa tohara—alitumia lugha ya kejeli kwa kuwaita wajikatao.
Unakuja hivi karibuni…

