Wagalatia – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA MTUME PAULO KWA WAGALATIA


MAELEKEZO

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe, mwamini mwenzangu, unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako; usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa kila mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa mambo yanayoweza kukuongoza kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayotajwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno, tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo. Utaona maelekezo ya ziada yatakayokusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba hiyo.

e. Mpangilio wa mwongozo huu si mpangilio wa mwandishi. Mpangilio wa mwongozo unakusaidia tu kuona mabadiliko ya mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huu wala kwa mpangilio wa sura na mistari.

UTANGULIZI

Barua ya Mtume Paulo kwa Wagalatia ni waraka wa kipekee sana katika Agano Jipya. Ni waraka wa kwanza kabisa kuandikwa na Mtume Paulo. Ni barua ambayo lugha yake inaonyesha uharaka wa kuandikwa kwake. Yaani, inaonyesha kwamba Mtume Paulo aliuandika waraka huu kwa uharaka zaidi kuliko nyaraka nyingine. ia, ni waraka wenye lugha za ukali zaidi kuliko barua nyingine za Mtume Paulo. Kutokuwepo kwa shukrani, maombi, au ripoti ya maombi, kama ilivyo kawaida katika nyaraka nyingine za Mtume Paulo, ni ushahidi unaoonyesha uharaka wake. Lugha kama “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe,” (1:8) au “Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao!” (5:12) na “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga” (3:1) zinaonyesha jinsi ambavyo Mtume aliandika barua hii kwa ukali zaidi. Kubwa katika yote, waraka huu ni waraka wenye umaarufu mkubwa miongoni mwa waprotestanti kuanzia karne ya kumi na sita mpaka leo.

GALATIA

Galatia, wakati wa maisha ya Mtume Paulo, lilikuwa ni jimbo kubwa la Kirumi lililogusa Bahari Nyeusi upande wa kaskazini na Bahari ya Mediterania upande wa kusini (Tazama ramani 1 hapo chini). Pamoja na eneo hilo kuwa kubwa kiasi hicho, taarifa za kazi ya kimisheni za Mtume Paulo na Barnaba katika eneo la Galatia ya kusini, katika safari yao ya kwanza ya kimisheni (Matendo 13:13–14:23), zinaashiria kwamba makanisa ambayo Mtume Paulo aliyandikia barua hii yalikuwa makanisa ya Galatia ya kusini. Galatia ya kusini ilihusisha maeneo ya Antiokia ya Pisidia, Ikonio, Listra, na Derbe, kama yalivyotajwa na Luka. Kwa hiyo, Mtume Paulo aliandika barua hii kwa makanisa ambaye alihusika moja kwa moja katika kuyapanda.

Ramani 1. Safari ya kwanza ya kimisheni ya mtume Paulo

KWA NINI PAULO ALIANDIKA WARAKA HUU?

Paulo na Barnaba baada ya kuhubiri na kupanda makanisa Antiokia ya Pisidia, Ikonio, Listra, na Derbe, miji ya jimbo la kiutawala la Galatia walimua kurudi Antiokia ya Siria, kule walikoombewa neema na Kanisa kwa kazi Roho mtakatifu aliyowaitia (Tazama Matendo 13:1-3 na 14:26). Katika kurudi waliyarudia makanisa hayo wakiwatia moyo waamini (kwa maana ya kuwahamasisha kukua katika imani) na kuwaweka wazee katika kila kanisa (Matendo 13:13–14:28). Walipofika Antiokia ya Siria waliendelea na utumishi wao hapo kwa muda (Matendo 14:28). Paulo akiwa hapo akapata habari kwamba kuna watu wameenda Galatia na wakahubiri “injili ya namna nyingine” au injili iliyogeuzwa (Wagalatia 1:6-7). Kutokana na taarifa hizo, Mtume Paulo akaamua kuandika waraka huu. Injili yao ilikuaje?

Pamoja na kwamba Paulo hajaweka wazi moja kwa moja kwamba injili hiyo ilihubiriwaje, lakini kwa kusoma waraka wake inaonekana injili hii ilikuwa inawalazimisha Wagalatia, ambao ni waamini wa mataifa, kutahiriwa (wazo la moja kwa moja kutoka 5:2; 6:12–13, na kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutoka 2:3–9; 5:11–12). Injili hii haikuishia katika kulazimisha kutahiriwa tu, bali pia ilitaka Wagalatia wafuate torati/sheria (2:14–16), kama ambavyo ilitakiwa kwa wale waliotahiriwa (5:2–6). Kwa kufanya hivyo, yaani kutahiriwa na kufuata torati, ndipo Wagalatia wangehesabiwa haki mbele za Mungu (Tazama tena 2:14–16; 5:2–6). Si hivyo tu, bali pia wangepata nafasi ya kuwa katika familia ya Ibrahimu, yaani ukoo wa ahadi (3:6–29). Vilevile, wangeweza kushinda nguvu za mwili wa dhambi (kwa njia isiyo ya moja kwa moja, 5:13–6:10).[1] Kutokana na mafundisho haya na ushawishi wa waalimu hawa wa injili nyingine, pamoja na kwamba inaonekana Wagalatia hawakufikia hatua ya kutahiriwa (5:2, 7), walikuwa tayari wameanza kushika sikukuu za Kiyahudi (4:10). Kwa nini waalimu hawa walifundisha hivyo?

Msukumo wa waalimu hawa wa injili nyingine ulikuwa ni kutaka waonekane wazuri mbele ya Wayahudi wenzao na hivyo kuepuka mateso kwa sababu ya imani yao katika Kristo (6:12). Zaidi ya hayo, kwa kuwatahiri watu wa mataifa, walitaka kupata sifa kutoka kwa Wayahudi wenzao (6:13). Lakini pia, walifanya hivyo ili kuwatenganisha Wagalatia na Mtume Paulo, kusudi Wagalatia wawe wafuasi wao (4:17). Hili lina maana gani?

Wakati Waraka wa Wagalatia unandikwa ilikuwa ni kipindi ambacho baadhi ya Wayahudi, hasa “Wazeloti” au makundi yenye msimamo mkali wa kulinda usafi wa dini ya Kiyahudi, walikuwa na harakati za kuimarisha uaminifu kwa Torati na utambulisho wa Kiyahudi. Walikuwa wanapambana kulinda usafi wa dini ya Kiyahudi, yaani kuhakikisha imani inafuatwa vilivyo.

Na kwa sababu kwa wakati huu Ukristo bado haukutofautishwa kikamilifu na Uyahudi, hivyo kuruhusu waongofu wa Mataifa kudai kuwa wao ni watu wa Mungu na kwamba wanashiriki baraka zilizoahidiwa kwa Ibrahimu na uzao wake bila wao kutahiriwa lilikuwa ni chukizo kubwa kwa Wayahudi wengi (Kumbuka kwamba Mataifa kabla ya Ukristo, walipomwamini Mungu wa Israeli kwa njia ya Uyahudi, walitahiriwa na walitakiwa kushika Sheria; hivyo si Ukristo tu ulioruhusu Mataifa kumwamini Mungu wa Ibrahimu).

Hivyo, waalimu hawa, ambao ni wakristo kutoka katika jamii ya Wayahudi, waliona ni vema kuwatahiri Mataifa ili wasipate upinzani kutoka kwa Wayahudi wenzao. Kwa hiyo, tunaweza kuelewa kwa urahisi kwa nini baadhi ya Wakristo wa Kiyahudi walitafuta kupunguza mateso kwa kusisitiza kwamba waongofu wa Mataifa wanapaswa kutahiriwa na kushika Sheria ili waweze kukubalika kikamilifu kama watu wa Mungu.

Paulo, yeye, tofauti na waalimu hawa alikubali mateso (5:11) na akawa akifundisha kwamba imani kwa Yesu inatosha kwa watu wa mataifa kuwa watu kamili wa Mungu, warithi wa ahadi za Mungu kwa Ibrahimu na uzao wake.[2]  Kutokana na injili hii, na kutokana na Paulo kutetea utume wake kwa kirefu katika barua hii (Wagalatia 1 na 2), inaonekana waalimu hawa hawakuishia tu kufundisha injili nyingine bali pia waliushambulia utume wa Paulo. Kwa kusoma jinsi Paulo anavyotetea utume wake, inaonekana waalimu hawa walikuwa wanasema yafuatayo kuhusu Paulo na utume wake.

Moja, Paulo si mtume wa kweli kama walivyo mitume walioko Yerusalemu (1:1). Pili, Paulo alifundishwa injili kamili na mitume wa Yerusalemu inayohusisha ulazima wa Tohara (1:11–12, 16–17, 22; 2:6), lakini amebadilisha ujumbe ili kuwashawishi na kuwapendeza watu wa Mataifa (1:10). Hivyo, anachokihubiri hakijakubaliwa na mitume wa Yerusalemu (2:6–10). Na mwisho, inawezekana walimtolea Petro mfano kama Mtume anayehubiri injili kamili inayolazimisha tohara (2:11–21).[3]

Hivyo, kutokana na waalimu hawa waliolisumbua kanisa (1:7) na kuushambulia utume wa Mtume Paulo, Paulo alipopata habari akaandika waraka huu kwa haraka na kwa sauti ya ukali.

MPANGILIO

MAELEZOMAELEZOWAKOLOSAI
UTANGULIZI                          Anuani1:1-5
USIMULIZIMuhtasari wa ujumbe mkuu1:6-10
Chanzo cha Injili iliyohibiriwa na Paulo1:11-24
Kukubalika kwa Injili hiyo na mitume wenye sifa2:1-10
Kefa kupingwa uso kwa uso2:11-14
HOJA KUUKuhesabiwa haki na kuungana na Kristo2:15-21
UTHIBITISHO WA HOJA KUUMaisha ya Wagalatia3:1-5
 Maandiko3:6-4:7
MWITO WA KUTOJITIA CHINI YA TORATIWagalatia4:8-11
 Paulo na wagalatia4:12-20
 Torati yenyewe4:21-31
 Kutokatiza mbio za imani5:1-12
MAISHA YA ROHOMaisha ya Roho, mbadala wa sheria5:13-6:10
HITIMISHOHitimisho la waraka6:11-18

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI

Barua hii, kama barua nyingine, inaanza na utangulizi unaotaja mwandishi wa barua, wapokeaji wa barua, na salamu (1:1-5). Upekee wa utangulizi huu ukilinganisha na barua nyingine za Mtume Paulo ni kwamba, katika utangulizi huu mtume Paulo anafafanua kwa utetezi wito wake wa kitume; kwamba haujatokana na wanadamu bali na Yesu na Mungu Baba. Pili, utangulizi unaweka wazi kwamba waraka huu ni kwa ajili ya “makanisa” na sio kanisa moja.[4] Tatu, salamu zake zina maelezo zaidi.

Bila shukrani wala maombi au taarifa za maombi yake kama ilivyo kawaida yake, Paulo anaingia moja kwa moja kwenye ujumbe mkuu wa barua yake. Anaanza kwa kutangaza mshtuko na mshangao wake (badala ya shukrani) kwa sababu Wagalatia wanataka kutoka kwa Kristo na kugeukia Injili iliyogeuzwa, iliyoletwa na watu kutoka nje. Kwa kurudia mara mbili, anatangaza laana (badala ya maombi) kwa yeyote atakaye kuigeuza Injili, Wagalatia walioipokea; hii ni kusisitiza kwamba Injili waliyoipokea Wagalatia ni Injili ya kweli. Mwisho, kinyume na tuhuma alizopewa na waalimu wa injili nyingine, Paulo, kwa kutumia maswali ya balagha, anathibitisha kwamba yeye hana lengo la kuwapendeza wanadamu; ndiyo maana ni mtumwa wa Kristo (1:6-10).

Kwa kuwa Paulo amesisitiza kwamba Injili Wagalatia waliyoipokea ni ya kweli na yeye ndiye aliyewahubiri Injili hiyo, hivyo anaamua kutetea chanzo cha Injili yake huku akikinzana na tuhuma za waalimu wa Injili iliyogeuza dhidi yake. Paulo anaweka wazi kwamba Injili aliyowahubiri Wagalatia hakuipokea kutoka kwa wanadamu bali alipokea kwa njia ya ufunuo wa Yesu Kristo (1:11-12). Mambo haya mawili anayafafanua kwa kusimulia historia yake. Kwanza anasimulia jinsi Mungu alivyomfunua Yesu Kristo kwake ili amhubiri kwa watu wa mataifa.[5] Anasimulia jinsi alivyotolewa kwenye dini ya kiyahudi ambako alikuwa na mafanikio makubwa ya kushika mapokeo ya Baba zake na kufikia kuitetea Imani kwa kiwango cha kufikia kulitesa kanisa (1:13-16a). Pili, baada ya kupata ufunuo huo anasema hakwenda Yerusalemu kule walikokuwa mitume kabla yake. Hii akimaanisha Injili hakuipokea kutoka kwa mitume wa Yerusalemu (1:16b-17). Hii ni hatua ya kwanza ya simulizi ya maisha yake.

Pamoja na ukweli kwamba Paulo hakupokea Injili kutoka kwa mitume wa Yerusalemu anaweka wazi kwamba baada ya miaka mitatu alikwenda Yerusalemu. Yerusalemu alikwenda ili aonane na Petro/Kefa na akakaa naye wiki mbili tu bila kuonana na mitume wengine isipokuwa alionana na Yakobo, ndugu yake Bwana Yesu. Kuonyesha kwamba hakufundishwa Injili hata katika ziara hii ya Yerusalemu, Paulo anasisitiza kwamba hakukaa muda mrefu huko ndio maana makanisa ya Uyahudi hayakumjua bali yalisikia tu habari zake na kumtukuza Mungu (1:18-24). Hii ni hatua ya pili ya simulizi ya maisha yake.

Baada ya hatua hizo mbili za simulizi zinazothibitisha kwamba Paulo hakupokea injili kutoka kwa mwanadamu yeyote, mitume wa Yerusalemu wakiwemo, anaingia kuonyesha usahihi wa injili yake kwa kuwa ilikubalika na wale waliokuwa na sifa ya kutambulika kama nguzo za kanisa huko Yerusalemu. Paulo anasema kwamba baada ya miaka kumi na nne alikwenda Yerusalemu kwa kufunuliwa, na lengo lilikuwa kuthibitisha kama alichokuwa anahubiri kwa mataifa ni sahihi. Paulo anasema katika ziara hiyo, Tito ambaye ni mtu wa mataifa (Myunani), hawakumlazimisha kutahiriwa; huu ni uthibitisho kwamba mitume wenye sifa walikubali kwamba mataifa wanaweza kuwa watu wa familia ya Mungu bila tohara na kufuata Torati. Hii ni pamoja na kuwepo kwa shinikizo la ndugu wa uongo waliotaka Tito atahiriwe.[6] Lakini baada ya kutoa ripoti ya kile alichokuwa anakihubiri kwa mataifa, Paulo anasema mitume wenye sifa walikubaliana na injili hiyo bila kumuongezea chochote. Paulo anamalizia kwa kusema kwamba mkutano huu wa faragha ulimalizika kwa mitume kukubaliana kwamba kila watu waendelee na utumishi waliokabidhiwa, bila kusahau kuwakumbuka maskini (2:1-10). Hii ni hatua ya tatu ya simulizi ya maisha yake.[7]

Mpaka hapa, Paulo amesema Injili yake hakuipokea kutoka kwa wanadamu, bali alipewa kwa njia ya ufunuo wa Yesu Kristo (1:11–12). Kuokoka kwake na mwito wake ni uthibitisho kwamba injili yake alipewa na Mungu mwenyewe, kwa maana maelezo pekee yanayoweza kuelezea mabadiliko yake kutoka kuwa mtesaji wa kanisa hadi kuwa mhubiri wa Injili ni kutokewa kwake na Kristo akiwa njiani kuelekea Dameski (1:11–17). Injili yake hakupokea kutoka kwa Petro, kwa sababu hakukutana naye hadi miaka mitatu baada ya kuokoka kwake, na hata wakati huo alikaa naye kwa muda wa wiki mbili tu (1:18–20). Wala hakuipokea kutoka kwa makanisa ya Uyahudi, kwa kuwa hata hayakumjua uso kwa uso bali walisikia tu habari zake (1:21–24). Zaidi ya hayo, viongozi wa Yerusalemu waliposikia injili ya Paulo miaka kumi na nne baada ya kuokoka wake, hawakumtaka Tito atahiriwe, wala hawakuongeza chochote katika injili yake (2:1–10). Badala yake, walikubaliana kwamba injili yake ilikuwa kweli imetoka kwa Mungu.

Baada ya utetezi huu kwa njia ya simulizi ya maisha yake na uhusiano wake na mitume kabla yake, Paulo anamalizia simulizi ya maisha yake katika hatua ya nne. Katika hatua hii Paulo anaeleza nini kilitokea Antiokia (Inaonekana anasahihisha taarifa ambayo waalimu wa injili iliyogeuza waliwapa Wagalatia kuhusu kilichotokea Antiokia). Paulo anasema kwa kile kilichotokea Antiokia, yeye alimpinga Petro uso kwa uso kwa kuwa Petro alistahiri hukumu. Kabla ya kuja kwa watu kutoka Yerusalemu (kutoka kwa Yakobo) alikula chakula pamoja na watu wa mataifa walioamini (kama alivyofanya nyumbani mwa Kornelio). Lakini walipokuja hao watu alijetenga kwa sababu ya hofu[8] na hivyo kusababisha waamini wengine wa kiyahudi kujitenga na waamini wamataifa na Barnaba akiwafuata. Kutokana na tendo hilo kuwa kinyume na kweli ya Injili, Paulo alimkea Petro kwa kumwambia “Ikiwa wewe uliye Myahudi unaishi kama watu wa mataifa, na huishi kama Myahudi, unawezaje kuwalazimisha watu wa mataifa mengine waishi kama Wayahudi?” (2:11-14).[9]

MAELEZO YA ZIADA: Nini maana ya swali hili la Mtume Paulo kwa Mtume Petro?
Kwa kawaida Wayahudi walikuwa hawatakiwi kula chakula pamoja na watu wa mataifa kwa sababu mbalimbali, ikiwemo utofauti wao kuhusu chakula; watu wa mataifa walikula kila kitu, lakini Wayahudi hawakula kila kitu, na pia kwa sababu watu wa mataifa walikuwa watu nje ya agano na Mungu, hivyo hawakutakiwa kuchangamana nao katika tukio hili muhimu. Lakini pale Wayahudi walipokula katika meza moja na watu wa mataifa, hawakutumia vyombo sawa; bado Wayahudi walitumia vyombo vyao wenyewe bila kuchangamana na vyombo vya wamataifa. Hivyo, suala la chakula lilikuwa ni moja ya vitenganishi kati ya Wayahudi na watu wa mataifa (Matendo 10:28; 11:2–3), ukizingatia kwamba kula pamoja lilikuwa jambo muhimu sana katika ulimwengu wa kale. Kwa hiyo, Petro kula na watu wa mataifa huko Antiokia[10] ilikuwa ni ishara kwamba, pamoja na yeye kuwa Myahudi wa kuzaliwa, aliachana na desturi hii ya Kiyahudi na akaishi kama watu wa mataifa kwa kutokuwa na mipaka ya nani wa kula naye chakula (kama alivyofanya nyumbani kwa Kornelio, Matendo 11:1–3). Lakini pia ilikuwa ni ishara kwamba watu wa mataifa walioamini na yeye ni familia moja ya Mungu na hivyo hawana mipaka tena bali wana ushirika wa pamoja ( 1 Wakorintho 10:16-17). Sasa, kwa Petro kujitenga baada ya watu kutoka Yerusalemu kuwasili, ilikuwa inaonyesha kwamba anawaambia watu wa mataifa walioamini kwa vitendo  kwamba wanatakiwa kufanyika kuwa Wayahudi ili yeye na Wayahudi wengine waweze kula nao tena, yaani ili waweze kuwapokea na kula nao kama watu kamili wa Mungu. Hii ndiyo maana ya swali mtume Paulo alilomuuliza Petro.

Baada ya hapo, Mtume Paulo anatumia maongezi yake kwa Petro, ambayo yanafafanua sababu ya yeye kumpinga Petro, kuelezea hoja yake kuu kwa Wagalatia (Kuelezea injili na namna ya kuishi kwa kufuata kweli ya Injili).[11] Kwanza, anasema yeye na wayahudi walioamini (Petro na Barnaba wakiwepo), ambao ni wayahudi wa kuzaliwa na sio mataifa wenye sifa ya kuwa watenda dhambi, wakijua kwamba mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa imani ya Kristo,[12] walimwamini Kristo ili wahesabiwe haki kwa imani ya Kristo na sio kwa matendo ya sheria. Hii ni kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki kwa matendo ya sheria (2:15-16). Katika pointi hii ya kwanza ya namna gani mwanadamu atahesabiwa haki, Paulo na wayahudi walioamini wanakubaliana. Paulo na waalimu wa injili iliyogeuzwa (Na kwa namna nyingine, Petro na wayahudi wengine walioishi kinyume na injili Antiokia wanahusika)[13] wanatofautiana kwenye pointi ya pili. Pili, Paulo anajibu hoja ya waalimu wa injili iliyogeuzwa, wanayosema kwamba, kama kuhesabiwa haki kwa imani ya Kristo na si kwa matendo ya sheria kunamaanisha kuachana na sheria, je, hiyo haimaanishi kuwaacha waamini kwenye kutenda dhambi kama mataifa, ambao wao kwa kukosa sheria walikuwa ni watenda dhambi? Na kufanya hivyo, je, hakumfanyi Kristo kuwa mhamasishaji wa dhambi? Jibu la Mtume Paulo ni hapana kubwa. Badala yake, Mtume Paulo anajibu akisema kwamba kuirudisha sheria tena baada ya kuhesabiwa haki kwa imani ya Kristo (“Maana nikiyajenga tena yale niliyoyabomoa”) ndiko kutakakowafanya waamini Wayahudi wahesabiwe kuwa wadhambi (2:17-18).[14] Paulo anafikisha kileleni hoja yake kwa kujibu swali; mwamini ataishije sasa kama sheria haipo tena? Paulo anasema lengo la kufa kwenye sheria ni ili kumuishia Mungu. Na kumuishia Mungu kunamaanisha Kristo kuishi ndani yake, yaani ndani ya mwamini. Hii ina maana kwamba katika sheria, mwamini amekufa na badala yake amefufuka katika maisha ambayo Kristo anaishi ndani yake. Mwisho anamaliza kwa kauli nzito kwamba kama haki hupatikana kwa sheria basi Kristo alikufa bure na yeye haibatili neema ya Mungu (2:19-21).

Toka mwanzo mpaka hapa Mtume Paulo alijikita katika kutetea utume wake na ujumbe wa injili aliyoihubiri kwa njia ya simulizi ya maisha yake. Kwa kutumia mazungumzo yake kwa Mtume Petro, Mtume Paulo akaelezea hoja yake kuu, ambayo kuanzia sasa atakuwa anaitolea uthibitisho. Hoja yake ni kwamba mwanadamu haesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa imani ya Kristo na tena mwamini haishi tena chini ya sheria badala yake anaungana na Kristo (yaani Kristo anaishi ndani ya huyo mtu) ili aishi kwa ajili ya Mungu. Kwa hiyo, kuanzia hapa, Paulo anatoa uthibitisho wa pande hizi mbili ya hoja yake kuu.

Kwanza, anaanza kuthibtitisha kwamba mwanadamu anahesabiwa haki kwa imani na sio kwa matendo ya sheria, kwa kutumia kile kilichotokea kwenye maisha ya Wagalatia wao wenyewe. Kwa kuwauliza maswali ya balagha, anawathibitishia kwamba wao wenyewe walipokea Roho ambaye ni uthibitisho wa kukubaliwa na Mungu, kwa imani na sio kwa matendo ya sheria. Lakini pia walipata mateso kwa ajili ya imani na tena Mungu alifanya miujiza kwao kwa imani na sio kwa matendo ya sheria. Kwa uthibtisho huu wa maisha yao wenyewe Wagalatia, Mtume Paulo anathibitisha kwamba wagalatia walikubaliwa na Mungu kwa imani na sio kwa matendo ya sheria na hivyo wanatakiwa kumaliza kwa Roho kama walivyoanza (3:1-5).[15]

Pili, anathibitisha kutoka kwenye maandiko kwamba mwanadamu anahesabiwa haki kwa imani na sio kwa matendo ya sheria kwa kumtumia Ibrahimu, Baba aliyeagizwa tohara.[16] Mtume Paulo anasema, hata Ibrahimu alihesabiwa haki kwa imani kwa mujibu wa Mwanzo 15:6, hivyo wote walio wa imani ndiyo wana wa Ibrahimu. Si hivyo tu, bali pia mataifa leo wanahesabiwa haki kwa imani kwa sababu Mungu alitoa ahadi kwa Ibrahimu katika Mwanzo 12:3 kwamba kupitia yeye mataifa wote watabarikiwa, yaani watahesabiwa haki kwa imani. Hivyo, wote walio wa imani wamebarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa wa imani (3:6-9). Baada ya uthibitisho huu chanya kutoka kwenye maandiko, Mtume Paulo anaingia kwenye uthibitisho hasi; kwamba kwa sheria hakuna ahesabiwaye haki mbele za Mungu. Kwa kutumia Kumbukumbu la Torati 27:26 Mtume Paulo anaonyesha kwamba mtu anayeishi kwa kutegemea matendo ya torati yuko chini ya laana kwa kuwa hatendi matendo hayo kwa ukamilifu. Kisha ananukuu Habakuki 2:4 na Mambo ya Walawi 18:5 ili kuonyesha njia mbili tofauti za kuishi/kupata uzima—kwa imani na kwa kutimiza torati. Kwa kuwa Paulo anaamini hakuna anayeweza kupata uzima kwa njia ya kuitimiza torati na hivyo wote tuko chini ya laana, anatumia Kumbukumbu la Torati 21:22–23, kuonyesha kwamba Kristo alibeba laana hiyo msalabani ili kutimiza ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu (Mwanzo 12:3; 22:18), ya kuwapa Mataifa baraka ambayo ni Roho wa ahadi, kwa njia ya imani (3:10-14).

MAELEZO YA ZIADA: Nini maana ya kuhesabiwa Haki?
Kuhesabiwa haki, kwa haraka haraka kunaweza kudhaniwa kuwa na maana nyepesi ya moja kwa moja. Lakini katika Wagalatia kuhesabiwa haki kuna maana kubwa inayohusisha mambo mengi kwa wakati mmoja. Kuhesabiwa haki ni tamko la kimahakama la Mungu lenye mtazamo wa siku za mwisho, linalotangazwa katika wakati wa sasa, kwamba mtu yuko katika hali ya haki mbele zake. Tamko hilo pia linamtambulisha mtu huyo kuwa ni mmoja wa watu wa familia yake, yaani mmoja wa watu wa agano lake na warithi wa ahadi alizompa Ibrahimu. Kuna pande mbili katika maana hii. Moja, kutangazwa kuwa na haki mbele za Mungu. Pili, kutangazwa kuwa ni mmoja wa watu wa familia ya kiagano ya Mungu. La kwanza linahusisha mtu na Mungu na la pili linahusisha mtu na watu wengine wa familia ya Mungu. Pande zote mbili zinakwenda pamoja. Kwa hiyo, kwa kuzingatia hoja za Paulo katika Waraka kwa Wagalatia, kuhesabiwa haki ni tangazo la Mungu la kimahakama lenye mtazamo wa siku za mwisho, linalotangazwa katika wakati wa sasa, ambalo kupitia hilo Mungu huwatangaza wale wanaomwamini Kristo kuwa wenye haki na kuwa washirika wa familia yake ya agano. Tangazo hili linategemea kikamilifu kazi ya Kristo ya ukombozi kupitia kifo chake, linatimiza ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu, linapokelewa kwa njia ya imani badala ya matendo ya torati, huwapatia waamini kipawa cha Roho Mtakatifu pamoja na hadhi ya kuwa wana na warithi wa Mungu, na huzaa maisha yaliyobadilishwa na kuongozwa na Roho. Matumizi ya Paulo ya neno “kuhesabia haki” katika Waraka kwa Wagalatia yanaonyesha tamko la kimahakama la Mungu juu ya mtu mmoja. Hili linaonekana katika lugha yake ya kisheria kuhusu mtu “kuhesabiwa haki” mbele za Mungu (2:16–17; 3:11). Wakati huohuo, Wagalatia inaonyesha kwamba kuhesabiwa haki pia kuna upande wa kiagano na wa kimahusiano, kwa sababu hoja kuu ya waraka huu ni kubainisha ni nani hasa wanaounda watu wa Mungu (Je, ni wale wa tohara au wale wa imani? Tazama, Wagalatia 3:6-14). Paulo anasema kwamba wale waliohesabiwa haki ndio watoto wa kweli wa Ibrahimu (3:6–9, 29), wana wa Mungu kwa njia ya imani (3:26), familia moja katika Kristo bila kujali tofauti za kabila, hali ya kijamii, au jinsia (3:28), na warithi wa ahadi ya Mungu (3:29). Hivyo basi, katika Waraka kwa Wagalatia, kuhesabiwa haki ni tangazo la Mungu linalomtangaza mtu kuwa mwenye haki mbele zake, na wakati huohuo ni tamko linalomtambulisha mtu huyo kuwa ni mmoja wa watu wa familia ya Mungu ya kiagano.

Tatu, Paulo anathibitisha kwamba mwanadamu anahesabiwa haki kwa imani na sio kwa matendo ya sheria kwa kuangalizia historia ya wokovu; Katika historia, ahadi ilitangulia sheria. Paulo anasema kama ilivyo katika agano la wanadamu, baada ya kuthibitishwa hakuna kulibadilisha wala kufutwa, vivyo hivyo Mungu alifanya agano na Ibrahimu katika Mwanzo 15:18 na 17:7-8 na kuweka ahadi kwa uzao wake. Ahadi hizo zinatimia kikamilifu kwa mzao wake, ambaye ni Yesu na hivyo haziwezi kubadilishwa na ujio wa Torati iliyokuja miaka mia nne na thelathini baadaye (3:15-18). Kwa kifupi, Paulo anasema kuja kwa Torati hakukuweza kubatilisha ahadi ya Mungu aliyokuwa ameitoa awali kwamba atawabariki mataifa, yaani atawahesabia haki kwa imani, na hivyo kuwa watu wake kamili. Lakini pia hakukuweza kubatilisha ahadi ya Mungu ya kuwapa urithi mataifa kupitia kwa Mzao wa Ibrahimu, yaani Kristo.

Kama kweli Torati haikuongeza au kubadilisha kitu katika agano la Mungu kwa Ibrahimu, na Torati ilitolewa na Mungu mwenyewe, kwa hiyo kwa nini torati ilitolewa? Paulo akijua swali hili linaweza kuulizwa kutokana na alichosema anatoa sababu za kutolewa kwa sheria au makusudi ya kutolewa kwa sheria. Jibu la kwanza, ililetwa ili kuifanya dhambi iwe uvunjaji halisi wa sheria. Lakini pia ilikusudiwa kudumu kwa muda hadi Masihi atakapokuja, na kwamba uwepo wa mpatanishi (“mjumbe”) unaonyesha kuwa Sheria ilikuwa na “hadhi” ya chini kuliko ahadi (3:19-20).[17] Jibu hili la kwanza linazalisha swali lingine; je, jibu hili lina maanisha kwamba Sheria inapingana na ahadi za Mungu? Jibu la Pili, hapana, Sheria haipingani na ahadi, kwa sababu Sheria ilitolewa kuwa kama mlinzi wa gereza mpaka imani itakapokuja (3:21-23). Lakini pia ilitolewa kuwa kama mlezi wa nyumbani, ambaye alikuwa anahakikisha mtoto anakuwa salama, mpaka pale wakati wa kuhesabiwa haki kwa imani utakapofika (3:24). Kabla ya kueleza mfano wa tatu unaoelezea kusudi la pili la Torati, Paulo anaonyesha kwamba muda wa kuwa chini ya mlezi wa nyumbani umeshapita, kwa kuwa wao wameshakuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani kwa Yesu na hivyo wao wote wameungana na Kristo na hivyo kuwa watoto wa ibrahimu ambao ni warithi sawa sawa na ahadi bila utofauti wao kitaifa, kijamii wala jinsia (3:25-29). Mwisho, Paulo anasema sheria ilikuwa kama wadhamini/mawakili wanaosimamia mali/urithi wa mtoto ambaye hajafikia umri wa utu uzima. Paulo anasema, wao wayahudi walikuwa chini ya sheria mpaka Mungu alipomtuma mwanae kuja kuwakomboa, yaani kuwafanya kuwa wana wanaoweza kuwa warithi kamili. Lakini Mungu alivyofanya hivyo kwa wayahudi, aliwafanya na wamataifa pia kuwa wana wake, kwa pamoja akawapa Roho wake, na hivyo wote sasa sio watumwa bali warithi (4:1-7).

Baada ya kuthibitisha kwamba mwanadamu anahesabiwa haki kwa imani ya Yesu na si kwa matendo ya sheria kwa hoja tatu hapo juu, na baada ya kumalizia kwa kueleza makusudi ya kutolewa kwa sheria (Makusudi mawili), Mtume Paulo anawageukia Wagalatia na kuwapa mwito wa kutokujitia chini ya sheria.

Wito wa kwanza. Kumbuka kwamba, mtume Paulo alipoelezea kwamba Torati iliwafunga (3:23), na ilikuwa kama mlezi wa nyumbani (3:24), na zaidi kwamba chini yake walikuwa kama watumwa pamoja na kuwa na hadhi ya wana (4:1–7), ametumia lugha ya sisi, akieleza kuhusu wao Wayahudi. Kujitofautisha na Wagalatia, ambao ni watu wa mataifa, amekuwa anatumia neno ninyi (3:26; 4:6). Kwa hiyo, mpaka hapa Wayahudi ndio walikuwa watumwa au wafungwa chini ya Sheria na si watu wa mataifa. Kutokana na hilo, mtume Paulo sasa anasema kwamba wao Wagalatia, kwa kuwa ni watu wa mataifa, walikuwa chini ya utumwa wa kutumikia sanamu ambazo kwa asili si miungu. Sasa, baada ya kuamini, kujitia chini ya sheria ni sawa tu na kubadilisha aina moja ya utumwa na kuingia katika aina nyingine ya utumwa (4:8–11).

Wito wa pili. Paulo anawaita Wagalatia wawe kama yeye (yeye hayuko chini ya sheria 2:19; 3:23–25), kwa kuwa yeye amekuwa kama wao (ambapo hawakuwa chini ya sheria). Baada ya kuwaita wawe kama yeye, anaongeza kwa kuwaita wamsikilize yeye na si waalimu wa injili iliyogeuzwa (ambao wana nia mbaya), kama walivyomsikiliza alipowahubiri injili hapo kwa mara ya kwanza. Paulo, katika hili, anawakumbusha kwamba ingawa alikuwa na udhaifu katika mwili (kwa mtazamo wa watu wa mataifa, ugonjwa au ulemavu wa mwili ungeweza kutafsiriwa kuwa ni ishara ya kutopendelewa na mungu au dosari ya kuaibisha, na hivyo kumfanya adharauliwe), walimtambua kuwa alikuwa mjumbe wa Mungu kwao; ilikuwa kama Kristo Yesu mwenyewe ndiye aliyekuwa akinena nao (4:12-20).

Wito wa tatu. Paulo anawaita Wagalatia kutojitia chini ya Torati kwa kuitumia Torati kuonyesha utofauti wa wana wa ahadi, ambao ni wana huru (muungwana), na wana wa mwili, ambao ni wana wa mtumwa (mjakazi). Paulo anasema kutoka kwa Ibrahimu familia mbili zilizaliwa, moja kwa njia ya mwili na nyingine kwa njia ya ahadi. Hiyo ni sawa na maagano mawili, moja ni la Sinai linalohusisha mpaka Yerusalemu ya sasa (ya wakati wake), na jingine ni la Yerusalemu wa juu. Kama ambavyo Isaka ndiye alikuwa mwana wa ahadi, ndivyo hivyo wale walio wa imani ndio wana wa ahadi. Lakini pia, kama vile mwana wa mtumwa Hajiri alivyomwudhi mwana wa mwanamke huru, ndivyo hivyo wana wa utumwa wa Yerusalemu ya sasa wanawaudhi wana wa ahadi, yaani wale walio wa imani ya Yesu. Pamoja na hayo, Paulo anamalizia kwa kuonyesha kwamba mwisho wa siku mwana wa mtumwa ndiye aliyefukuzwa na si mwana wa mwanamke huru. Hivyo, Wagalatia wabaki katika imani ili mwisho wathibitishwe, kwa kuwa wao si wana wa mtumwa bali wa mwanamke huru (4:21-31).

Wito wa nne. Baada ya kuwaonyesha Wagalatia kwamba wao ndio wana wa mwanamke huru, Paulo anawaagiza Wagalatia kusimama imara katika uhuru bila kujitia tena chini ya utumwa, kwa sababu ni kwa uhuru Kristo aliwaweka huru (5:1). Kusisitiza hilo, anaweka wazi matokeo hasi ya kujitia chini ya utumwa wa tohara na sheria, ambayo ni: Kristo kutokuwa na faida kwao, wajibu wa lazima wa kutimiza Torati yote, kutengwa na Kristo, na kuanguka kutoka kwenye neema (5:2–4). Kinyume na hayo, katika Roho kuna kutazamia tumaini la kuhesabiwa haki kwa imani (5:5), kwa kuwa katika Kristo kinachohitajika si tohara wala kutokutahiri, bali imani inayofanya kazi kupitia upendo (5:6). Paulo anamalizia mwito huu kwa kuwaonyesha Wagalatia kwamba msukumo wa wao kutahiriwa hautoki kwa Mungu, na wanaofanya hivyo watahukumiwa. Pamoja na kushangaa kitendo cha kukatisha mwendo wakati walianza vizuri kupiga mbio, mtume Paulo bado ana matumaini kwamba Wagalatia hawatageuzwa na waalimu wa injili iliyogeuzwa (5:7–12).

Baada ya kuwaita Wagalatia kutojitia chini ya Torati, Mtume Paulo anageukia kuelezea namna wanavyotakiwa kuutumia uhuru wao walioitiwa. Uhuru wao unawataka kutumikiana kwa upendo, kwa kuwa hivyo ndiyo namna ya kuitimiza sheria (5:13–15). Pia, uhuru unawataka kuishi kwa kuongozwa na Roho, na si mwili (5:16–18). Kuongozwa na Roho au na mwili ni jambo linaloweza kuonekana, kwa kuwa matendo ya mwili yanaonekana na matunda ya Roho yanaonekana. Wanaotenda matendo ya mwili hawataurithi uzima wa milele, kama Paulo alivyowaambia hapo mwanzo, na wenye tunda la Roho ndiyo waliousulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake (5:19–24).

Baada ya kueleza maisha ya Roho na ya upendo kwa ujumla, Paulo anafafanua namna wanavyotakiwa kuishi maisha yao Wagalatia kwa umahususi. Anazungumzia mambo matatu kwa mahususi kwao. Moja, anataka mwamini mmoja mmoja kuepuka kujisifu kwa wengine, huku akiruhusu mtu kujisifu ndani yake kama kweli kuna sababu ya kujisifu baada ya kujipima mwenyewe. Pili, anawakataza Wagalatia kuchokozana na kuhusudiana; badala yake wasaidiane, walio wa Rohoni wawasaidie wale walio na udhaifu kama maisha ya Roho (5:25–6:5). Tatu, anawahimiza kutenda mema; mwanafunzi kwa mwalimu wake na waamini kwa watu wote, na hasa kwa waamini wenzao. Katika hili Paulo anasisitiza kila kinachofanyika ni mbegu ambayo itatoa mavuno (6:6–10).

Paulo anahitimisha waraka wake kwa kueleza wazi nia ya ndani ya waalimu wa injili iliyogeuzwa ya kusisitiza tohara (6:11–13). Kwa kufanya hivyo, analinganisha na nia yake mwenyewe ya kutetea kweli (6:14–17). Mwisho kabisa, anahitimisha kwa baraka/salamu ya mwisho (6:18).

MAELEZO YA CHINI


[1] Kwa kusoma 5:13–21, inaonekana katika Kanisa kulikuwa na watu wanaoishi maisha yao ya zamani, yaani maisha ya dhambi, na Paulo alikuwa amekwisha waonya hapo mwanzo. Lakini waalimu hawa wa injili nyingine walipokuja, wakawa wakiwafundisha kwamba kushika Torati ndiyo njia ya kuepuka kuishi maisha ya dhambi. Hii ndiyo sababu mtume Paulo anatoa mbadala wa sheria, yaani Roho Mtakatifu. Yeye ndiye anayewezesha kuishi maisha mbali na dhambi. Na kwa sababu hili lilikuwa tatizo katika Kanisa, ambalo waalimu hawa wa injili nyingine walilichukua kama fursa, ndiyo maana Paulo anawaonya tena Wagalatia kutoishi katika maisha ya dhambi.

[2] Injili hii ndiyo iliyomfanya Paulo akamatwe mwishoni mwa safari yake ya tatu ya umisheni alipoenda Yerusalemu (Matendo 21:18 na kuendelea).

[3] Hatuna uhakika kwamba hizi ndizo tuhuma zilizotumiwa na waalimu hawa; haya ni mapendekezo kutokana na majibu ya utetezi wa Mtume Paulo kuhusu utume wake.

[4] Hii ni sawa na tulivyoona katika utangulizi kwamba Galatia ilihusisha makanisa ya Antiokia ya Pisidia, Ikonio, Listra, na Derbe.

[5] Paulo hapa anazungumzia tukio la Yesu kumtokea alipokuwa njiani kuelekea Dameski, kama linavyosimuliwa na Luka katika Matendo 9:1–22.

[6] Ndugu wa uongo, maana yake ni waamini wa kiyahudi ambao Mtume Paulo hawapi sifa ya kuwa waamini wa kweli, kutokana na msimamo wake ambao ni kinyume na ukweli wa Injili. Ndugu hawa wa uongo wanafanana na waalimu walioenda Galatia.

[7] Kumbuka katika utangulizi, inaonekana Paulo anasimulia ziara yake hii kwa sababu waalimu wa injili iliyogeuzwa walimtuhumu kubadilisha ujumbe aliofundishwa ili kuwashawishi na kuwapendeza watu wa Mataifa. Hivyo, kwa mujibu wa tuhuma hizo, injili yake haikuwa imekubaliwa na mitume wa Yerusalemu.

[8] Ni vizuri kuelewa sababu ambayo Mtume Paulo anasema ilimfanya Petro kujitenga. Sababu haikuwa kuhusu theolojia yake, sababu ilikuwa ni woga. Paulo anakiri kwamba Petro aliacha desturi za kiyahudi na kufuata desturi za watu wa mataifa (2:14), lakini pia Petro alijua haki inapatikana kwa imani na sio kwa matendo ya sheria (2:15-21), na zaidi hakukuwa na tofauti za kitheolojia katika yao (2:1-10).

 

[10] Inawezekana kabisa chakula hiki ni meza ya Bwana, kwa kuwa kwa karne ya kwanza, meza ya Bwana ilikuwa ni chakula cha pamoja cha kushiba, sio kama inavyofanya leo katika jamii nyingi za waamini.

[11] Kumbuka Paulo anasema hakukubali kuwapa nafasi waliotaka Tito atahiriwe kwa sababu alitaka kweli ya Injili ikae pamoja watu wa mataifa (2:5). Lakini pia alimpinga Petro kwa sababu yeye na wayahudi wengine kwa kujitenga na wamataifa walikuwa hawaendi sawasawa na ile kweli ya Injili (2:14). Hivyo, 2:15-21 ni maelezo ya injili ni nini na inataka waamini waishije ili kweli yake isimame.

[12] Kutoka katika kiyunani, Lugha iliyotumika kuandika Agano jipya, ni vigumu kusema kwa uhakika maana ya msamiati huu “Imani ya Kristo.” Hii ni kwa sababu unaweza kumaanisha uaminifu wa Kristo (kwa kuwa imani na uaminifu hutafsiriwa kutoka kwenye neno moja) au imani ya mtu kwa Kristo. Kwa ufafanuzi zaidi, inaweza kumaanisha wanadamu wanahesabiwa haki kwa sababu ya uaminifu wa Yesu aliouonesha katika kazi yake aliyotumwa na Baba au inaweza kumaanisha wanadamu wanahesabiwa haki kwa sababu ya wao kumwamini Yesu.

[13] Tofauti ya waalimu wa Injili iliyogeuzwa na wayahudi wa Antiokia waliojitenga na waamini wa mataifa ni hii; waalimu wanashida ya kitheologia lakini Petro na wayahudi wengine wanashida ya kuisimamia kweli kwa vitendo.

[14] Hii kwa sababu pamoja na kusisitiza kuifuata sheria, waamini wayahudi wao wenyewe hawaifuata sheria ipasavyo (Angalia 5:3; 6:13).

[15] Kuhubiriwa Injili (3:1), kupokea Roho (3:2–3), kupata mateso baada ya kuamini Injili (3:4), na kutendeka kwa miujiza iliyothibitisha ujumbe wa Injili (3:5), kwa pamoja, vilikuwa uthibitisho wa wokovu wa wale waliopokea mambo hayo. Hivi vitu ndiyo mwandishi wa kitabu cha Waebrania anatumia pia kuonyesha kwamba wapokeaji wa ujumbe wake walipokea wokovu. Kuhubiriwa neno (Waebrania 2:3; 6:4-5), kupokea Roho (Waebrania 2:4; 6:4), kupata mateso (Waebrania 10:32-34) na kutendeka kwa miujiza (Waebrania 2:3-4).

[16] Kumbuka, tohara ndiyo jambo kuu ambalo waalimu wa Injili iliyogeuzwa walikuwa wanalisisitiza, na tohara ilianza kwa Ibrahimu. Hivyo, ilikuwa muhimu kwa Paulo kuonyesha kwamba hata Ibrahimu hakuhesabiwa haki kwa tohara, bali kwa imani, kama Maandiko yasemavyo. Lakini pia, kwa kawaida kwa mujibu wa maandiko watu wa Mungu au familia ya Mungu ilikuwa ni ya wale walio wa familia/ukoo wa Ibrahimu (Mathayo 3:9-10; Luka 3:8; Yohana 8:39–40; Matendo 7:2). Kwa hiyo, Paulo anakwenda kuonyesha kwamba walio katika familia ya Ibrahimu si wale waliotahiriwa na kupewa torati, bali ni wale walio na imani kama Ibrahimu, ambaye Mungu aliahidi tangu zamani kwamba kupitia yeye mataifa yangekuwa watu wake. Zaidi ya hayo, inawezekana kabisa waalimu wa Injili iliyogeuzwa waliwaambia Wagalatia watahiriwe ili wafanyike kuwa watoto wa Ibrahimu na hivyo wawe watu wa Mungu kamili. Kinyume nao, Paulo ataonyesha kutoka katika Maandiko kwamba watoto wa Ibrahimu si wale waliotahiriwa na kushika torati, bali ni wale walio wa imani kama Ibrahimu. Hivyo, Wayahudi na Wamataifa wote wanakuwa watoto wa Ibrahimu kwa njia ya imani.

[17] Mstari wa 19-20 una maanisha kwamba Mungu alipotoa ahadi alitoa yeye mwenyewe moja kwa moja kwa ibrahimu, lakini sheria ilitolewa kwa njia ya malaika na mtu wa kati ambaye alikuwa kati ya malaika na watu waliopokea sheria, huyu anaitwa mjumbe (SUV) au mpatanishi (BHN/NENO). Kwa huu mpangilio tu, ilionyesha kwamba sheria ilikuwa haina hadhi sawa na ahadi ambayo ilitolewa moja kwa moja na Mungu mwenyewe.

Unakuja hivi karibuni…