Warumi – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA PAULO KWA WARUMI

MAELEKEZO

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.

UTANGULIZI

Barua ya mtume Paulo kwenda katika makanisa yaliyokuwa katika mji wa Rumi ni barua pendwa sana katika historia ya kanisa. Ni moja ya barua zinazosomwa sana na waamini hata leo. Ni barua iliyoweza kutoa nukuu nyingi maarufu, mfano ni kama vile “mshahara wa dhambi ni mauti” (6:23), “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” (21:1) na “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu” (8:1).

Barua hii ndiyo barua ndefu kuliko barua zote zilizoandikwa na mtume Paulo. Ni moja katika ya barua mbili tu ambazo Mtume Paulo aliandika kwa makanisa ambayo hakuwahi kuyatembelea kabla. Na zaidi, barua hii ina mafundisho kuhusu wokovu kwa urefu zaidi kuliko barua zake nyingine. Hivyo, barua hii ni muhimu sana na inafaa sana kama itasomwa kwa usahihi.

SABABU ZA KUANDIKWA KWA WARAKA HUU.

 Mtume Paulo aliandika barua hii kwa sababu zilizo kwenye makundi mawili: Moja, aliandika barua hii kwa sababu zake binafsi na Pili, aliandika kwa sababu ya changamoto iliyokuwepo katika kanisa la Rumi.

Sababu Binafsi za kuandika barua hii:

Mtume Paulo aliandika barua hii kwenda kwa kanisa la Rumi kwa sababu alitaka Rumi iwe kituo chake cha muda wakati anatarajia kwenda kuhubiri injili uhispania. Mtume Paulo alikuwa na mpango wa kwenda kuhubiri injili uhispania, mahali ambako injili ilikuwa haijafika, hivyo akaandika barua hii kwa Warumi ili kujitambulisha kwa kanisa hilo; kutambulisha injili yake. Lengo la kujitambulisha ni ili kanisa liweze kumpa rasilimali kwa ajili kazi ya injili ya Uhispania (15:15-24). Kwa kanisa la karne ya kwanza ilikuwa kawaida kwa kanisa kutoa kwa ajili ya kuwezesha kazi ya injili, hivyo mtume Paulo aliandika barua hii ili mwisho wa siku kanisa la Rumi lihusike katika upandaji wa makanisa uhispania.

Changamoto katika kanisa la Rumi:

Kanisa la Rumi wakati mtume Paulo anaandika barua hii lilikuwa na changamoto ya kimahusiano kati ya waamini wayahudi na waamini wamataifa. Hii ndio maana Mtume Paulo anatumia sehemu kubwa ya barua hii kuwapatanisha. Anaanza na kuwaonyesha kwamba wokovu unawahusu wote (1:16) pamoja na wayahudi kupewa kipaumbele. Wote walikuwa chini ya hukumu ya Mungu kwa sababu ya makosa yao (3:9), kwa kuwa Mungu hana upendeleo kwa yeyote (2:9-11). Kwa sababu ya kazi yake Mungu ya ukombozi, wote wanahesabiwa haki bure kwa njia ya imani (3:22-24; 28-30). Wote wanahesabiwa haki kwa imani bila matendo ya sheria kama Ibrahimu (4:9-12). Wote ni warithi wa ahadi ya Ibrahimu, ndio maana Ibrahimu ni Baba yao wote (4:13-17).

Kwa sehemu kubwa sura ya 1-4 mtume Paulo yuko upande wa mataifa, akiwasahahihisha wayahudi (anasahihisha kujiona bora dhidi ya mataifa). Kwa sehemu ya pili, yaani sura ya 9-11, kwa sehemu kubwa mtume Paulo yuko upande wa wayahudi (taifa la Israeli) akiwasahihisha wamataifa. Mtume Paulo anasema, Mungu hajalitupa taifa lake Israeli alilolichagua pamoja na ukweli kwamba wengi wao hawajaamini. Anasema toka mwanzo sio kila myahudi wa asili katika mwili ilikuwa katika familia hii ya Mungu (9:1-33). Anasema kutokuamini kwa Israeli kumewapa wamataifa nafasi ya kuingizwa kwenye familia ya Mungu (11:11-16). Hivyo, mataifa wasijivune dhidi ya israeli, wao waendelee kuamini tu ili wasikatwe kama Israeli ilivyo sasa (11:19-22). Na mwisho anasema, pamoja na Israeli kama taifa kuwa nje ya familia ya Mungu kwa sasa, bado Mungu hajawatupa. Israeli wote wataokolewa pale tu muda wa mataifa kuingia katika familia utakapofika mwisho (11:25-27).

Kwa sababu ya theologia hiyo, Mtume Paulo anawaita waamini wayahudi na wamataifa kushirikiana na kukaribishana bila kuhukumiana au kudharauliana kutokana na tofauti zao za kiimani (14:1-15:13). Tofauti za kiimani Mtume Paulo anazozitaja ni mbili: Moja, ni kuhusu ulaji wa chakula na pili, ni kuhusu utunzaji wa siku. Wayahudi kwa sababu ya sheria wana masharti katika chakula na pia wana siku ambayo ni maalumu zaidi ya nyingine. Kwa upande wa pili, wamataifa hawana masharti yeyote katika chakula na siku zote wao ni sawa. Pamoja na tofauti hizo, Mtume Paulo anawaita waamini hawa washirikiane na kukaribishana katika Bwana.

Changamoto hii ya kimahusiano ilisababishwa na nini ?

Kama ilivyokuwa kawaida kwa makanisa mengi karne ya kwanza, wayahudi walikuwa wengi kuliko wa mataifa katika hatua za awali za ukuaji wa kanisa. Ndivyo, ulivyokuwa kwa kanisa la Rumi. Injili ilipofika Rumi waamini wayahudi ndio walikuwa wengi na hivyo kuwa na sauti kubwa katika kanisa kuliko wamataifa. Nafasi za kiuongozi katika makanisa mbalimbali katika mji wa Rumi zilikuwa kwa wayahudi. Na kwa sababu katika miaka ya awali ya karne ya kwanza ukristo ulianza kama dhehebu jipya ndani ya dini ya kiyahudi, dola ya Rumi haikuweza kutofautisha ukristo na uyahudi. Ukristo ulikuwa unampa Yesu nafasi ya umasihi (ukristo), kitu ambacho kilikuwa kinapingwa sana na wayahudi waliobaki katika imani yao ya kiyahudi. Kutokana na mabishano hayo ya kiimani katika mji wa Rumi, Kaisari Klaudio mnamo mwaka 49 BK aliwafukuza wayahudi wote katika mji wa Rumi (Matendo 18:2). Kuondoka kwa waamini wa kiyahudi kukaliacha kanisa kwa wamataifa. Kanisa sasa likawa na wamataifa watupu kwa muda wa miaka mitano. Baada ya kufa Kaisaria Klaudio, wayahudi wakaanza kurejea Rumi na hivyo kukuta mabadiliko makubwa katika kanisa. Hapo ndipo kukatokea mvutano kati ya wale waliorejea—Wayahudi ambao walikuwa wanafuata mila na desturi za Agano la Kale—na waamini wa Mataifa, wale walioachwa nyuma pamoja na waongofu wapya wa Mataifa waliopatikana wakati wa kutokuwepo kwa wayahudi. Mvutano huu ulikuwa ni wakutengana kabisa ndio maana Paulo anawasihi kukalibishana bila kuhukumiana wala kudharauliana.

Kwa ujumla, hizo sababu mbili ndio sababu kuu zilizomsukuma Mtume Paulo kuandika barua hii kwenda katika kanisa la Rumi.

MPANGILIO WA WARAKA

NambaMaandikoMaelezo
11:1-7Anuani ya waraka
21:8-15Shukrani na Maombi
31:16-17Sababu ya Kuhubiri Injili
41:18-4:25Kutoka kwenye dhambi mpaka kwenye haki
55:1-8:39Kutoka kwa Bwana dhambi kwenda kwa Bwana Haki
69-11Kwa nini Israeli hawajamwamini Mwokozi?
712:1-15:13Maisha mapya ndani ya Kristo
815:14-16:27Mwisho wa barua

MFULULIZO WA MAWAZO WA MWANDISHI

Waraka huu unaanza na anuani, na anuani hiyo ina utambulisho wa Mtume Paulo, mwandishi wa waraka huu. Utambulisho huu unaambatana na wito wake, wito wake ukiwa ni utume; na utume huu unahusu kuhubiri injili, injili ikiwa ni habari za mtoto wa Mungu aitwaye Yesu. Mwisho wa anuani hii, anawataja wapokeaji wa awali wa waraka huu (1:1-7).Baada ya anuani hiyo, Mtume Paulo anaingia kwenye shukrani na maombi. Katika shukrani, Mtume anamshukuru Mungu kwa sababu imani ya Warumi inayosikika kila mahali. Katika maombi, anatoa taarifa kwamba amekuwa akiwaombea Warumi mara kwa mara, na jambo moja kuu alilokuwa analiombea ni kufanikishwa na Mungu ili afike Rumi. Lengo la safari yake ni kufarijiana na kujengana katika imani na Warumi (1:8-12). Baada ya kutoa ripoti ya maombi yake, Mtume Paulo anawajulisha kwamba kushindwa kwake kufika Rumi hakukuwa kwa hiari, bali ni kwa sababu alizuiliwa. Pamoja na kuzuiliwa anaeleza kwamba ana deni la kuhubiri injili kwa kila aina ya watu, na kwa hiyo yuko tayari kuhubiri injili hata Rumi pia (1:13-15). Kwa nini yuko tayari kuhubiri injili Rumi? Kwa sababu haionei aibu injili[1]. Kwa nini haionei aibu injili? Kwa sababu injili ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza na kwa Myunani pia. Kwa nini injili ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye? Kwa sababu katika injili, haki ya Mungu imedhihirishwa. Haki ya Mungu ni kazi ya Mungu ya ukombozi inayowafanya watu kuwa wenye haki kwa imani, mwanzo hadi mwisho. Paulo anathibitisha hili kwa kunukuu Habakuki 2:4 (1:16-17).

Baada ya kusema kwamba katika Injili, haki ya Mungu imedhihirika na Injili ndiyo uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, Myahudi kwanza na kwa Myunani pia, Paulo sasa anaeleza kwa namna gani haki ya Mungu imedhihirika katika Injili. Kumbuka, haki ya Mungu ni kazi ya Mungu ya ukombozi inayowafanya watu kuwa wenye haki kwa njia ya imani. Paulo anafanya hivyo kwa kuanza kuonyesha tatizo (1:18-3:30) na mwisho anamalizia kwa kuonyesha suluhisho (3:21-4:25). Paulo anaanza kwa kuonyesha kwamba watu wote wa mataifa wako chini ya hukumu ya Mungu kwa sababu ya matendo yao maovu. Watu hawa wa mataifa hawana udhuru wa kusema kwamba hawakumjua Mungu, kwa sababu Mungu alijifunua kwao kupitia uumbaji wake (1:18-20). Walipouona ufunuo wa Mungu kupitia uumbaji, watu wa mataifa hawakumuabudu Mungu, bali walitengeneza sanamu za binadamu, wanyama na ndege ili waziabudu na kuzisujudia (1:21-25). Kwa sababu ya kumkataa Yeye, Mungu aliwaacha waendelee katika ibada zao za sanamu na katika dhambi za ushoga na usagaji (1:26-28). Na tena, Mungu aliwaacha waendelee katika kila aina ya uovu na dhambi (1:29-32).

Kwa kueleza maisha haya ya watu wa mataifa na jinsi wanavyostahili hukumu ya Mungu, Myahudi wa kawaida angemuunga mkono Paulo kwa kusema, ‘Ni kweli kabisa, hawa wa mataifa wanastahili hukumu ya Mungu kwa sababu ya dhambi zao.’ Kwa kulijua hilo, Paulo anamjibu Myahudi huyu kwa kumjulisha kwamba kuhukumu wengine hakukukwepi au hakukutoi katika hukumu ya kiungu kama unafanya yale yale wanayofanya mataifa (2:1-11). Paulo anaendelea kuongea na Wayahudi kwamba kuwa na sheria sio njia ya kukwepa hukumu ya Mungu, bali kutenda sawasawa na sheria (2:12-16). Pamoja na kupewa, kuipokea, na kuikubali sheria na kufanywa viongozi, waalimu, na mwanga kwa mataifa, ninyi Wayahudi mmefanya yale yale mnayowashutumu mataifa kufanya, ndiyo maana jina la Bwana limetukanwa, anasema Paulo (2:17-24). Ukiacha sheria, kitu kingine ambacho Wayahudi walijivunia ni tohara. Paulo pia anawaonyesha Wayahudi kwamba tohara inayofaa ni tohara ya moyoni, yaani tohara inayoambatana na kutii sheria, na sio tu tohara ya kimwili (2:25-29). Sasa kama myahudi anahukumiwa kama mmataifa, Je, kuwa myahudi kulikuwa na faida gani na kutahiriwa kulikuwa na faida gani? Hili ni swali ambalo Paulo anajua wayahudi watajiuliza. Paulo anajibu kwamba pamoja na wayahudi kuwa wadhambi kama wa mataifa bado wao wana faida kwa kuwa wao walikabidhiwa mausia (maneno) ya Mungu. Hata kama baadhi yao hawakuamini maneno hayo ya Mungu bado wana faida kwa sababu ya uaminifu wa Mungu kwa maneno yake. Lakini pia Paulo anasema, Mungu kuwa mwaminifu kwa taifa lake hakuwatoi watu wake katika hukumu (3:1-8).[2]

Baada ya kuonyesha kwamba mataifa wako chini ya hukumu ya Mungu kwa sababu ya dhambi zao na hawana sababu ya kujitetea (1:18-32), na pia kwamba Wayahudi wako chini ya hukumu ya Mungu licha ya faida walizonazo (2:1-3:8), Mtume Paulo anahitimisha hoja yake kwamba wanadamu wote wako chini ya hukumu ya Mungu kwa sababu ya dhambi zao (3:9-20). Kwa kuwa wanadamu wote wako chini ya hukumu ya Mungu (tatizo), basi suluhisho la Mungu ni kazi yake ya ukombozi kupitia Yesu Kristo, inayowafanya wale wanaoamini kuhesabiwa haki (yaani kuhesabiwa kwamba hawana dhambi na hivyo hawako chini ya hukumu ya Mungu) bure (3:21-26). Msisitizo wa Paulo uko kwenye imani: imani inaondoa kujisifu kwa namna yoyote ile kwa wayahudi, inawapa mataifa nafasi, na inathibitisha sheria  (3:27-31).

Baada ya kusema kweli hio, Paulo anajua sasa anahitajika kuthibitisha anachofundisha kupitia maandiko. Paulo anakwenda katika maandiko katika kipindi ambacho hakukuwa na tofauti kati ya Wayahudi na Mataifa. Anarejea kwa mtu ambaye Wayahudi wanamheshimu kuliko wote katika maandiko. Kwa kunukuu Mwanzo 15:6, Paulo anathibitisha kwamba Ibrahimu mwenyewe alihesabiwa haki kwa imani, na si kwa matendo (4:1-5). Wanaohesabiwa haki kwa imani, Paulo anasema, wana heri kama Daudi anavyosema katika Zaburi 32:1-2 (4:6-8). Na kwa kuwa Ibrahimu alihesabiwa haki kabla ya kutahiriwa, ina maana alikuwa na haki kabla na baada ya kutahiriwa. Hivyo, Ibrahimu ni baba wa waamini wote, waliotahiriwa (Wayahudi) na wasiotahiriwa (Mataifa) (4:9-12). Tena, ahadi ya urithi wa ulimwengu aliyopewa Ibrahimu na uzao wake aliipokea kwa imani na si kwa sheria. Hivyo, wote wenye imani kama Ibrahimu ni warithi wa ile ahadi, si wale wa sheria tu (Wayahudi). Ndiyo maana Ibrahimu ni baba yetu sote, Wayahudi na Mataifa (4:13-17). Ibrahimu alikuwa na imani thabiti kwa sababu alijua kwa hakika Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi, licha ya uhalisia kwamba mwili wake haukuwa na uwezo tena wa kuzalisha na tumbo la Sara halikuwa na uwezo wa kubeba mimba. Kwa imani hiyo, Ibrahimu akahesabiwa haki (4:18-22). Habari hizi za imani ya Ibrahimu na kuhesabiwa kwake haki hazikuandikwa kwa ajili yake tu, bali kwa ajili yetu pia. Sisi ambao tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu; Yesu aliyetolewa kufa kwa ajili ya makosa yetu na kufufuliwa ili tuhesabiwe haki kwa imani kama Ibrahimu (4:23-25).

Baada ya Paulo kueleza kwa kirefu tatizo (yaani, kutenda dhambi kwa wote) na suluhisho la Mungu (kuhesabiwa haki bure kwa imani), sasa anaingia kueleza kile Mungu alichokifanya kwa katika picha kubwa. Kuanzia sura ya kwanza hadi ya nne (1:18-4:25), Paulo ameweka wazi tatizo la dhambi, ambapo dhambi ni matendo maovu wanayofanya wanadamu wote, Wayahudi na Wamataifa pia. Aidha, ameonyesha jinsi Mungu alivyowakomboa wanadamu kwa kuwahesabia haki bure wale wote wanaoamini kazi ya Yesu, yaani kifo na ufufuo wake. Kuanzia sura ya tano hadi ya nane (5-8), Paulo anaeleza jinsi Mungu alivyozishinda nguvu mbili kuu, Dhambi na Mauti, kupitia kifo na ufufuo wa Bwana Yesu Kristo na sio kupitia sheria. Katika sura hizi, dhambi si tu matendo wanayofanya Wanadamu, bali ni nguvu inayowaendesha wanadamu wote ambao wako nje ya Kristo. Kwa kuwa dhambi ni nguvu yenye mtoto aitwaye Mauti, Paulo anaeleza jinsi nguvu hiyo ilivyoharibiwa kupitia kifo na ufufuo wa Yesu Kristo. Kabla ya kuanza kueleza hayo kwa undani, Paulo anatoa muhtasari wa mafundisho aliyoyatoa hapo awali na kueleza matokeo yake. Muhtasari huu unaonyesha kuwa waamini tayari tumehesabiwa haki bure na Mungu, na matokeo yake ni kwamba tuna amani na Mungu na tuna uhakika wa kutokukumbwa na ghadhabu yake. (5:1-11).

Paulo anaanza kwa kutoa majibu ya swali, ilikuaje mpaka dhambi ikaingia ulimwenguni? Dhambi ilingia ulimweguni kupita Adamu, na matokeo yake ilikuwa ni mauti kuzaliwa. Na kwa kitendo cha Adamu cha kutotii, wanadamu wote walirithi hukumu. Hukumu hii ilipewa nguvu na sheria, kwa sababu sheria ndio iliyofanya watu wahesabiwe dhambi. Kinyume cha Adamu, kupitia Kristo, haki na uzima wa milele vinatolewa kwa wanadamu; kwa kitendo chake cha utii (kifo na ufufuo), wote wanaomwamini wanahesabiwa haki bure. Kuhesabiwa haki na kupata uzima ni matokeo ya neema ya Mungu. Kwa hiyo, kama vile dhambi ya Adamu ilivyoleta mauti kwa wote, utii wa Kristo unaleta uzima kwa wote wanaoamini (5:12-21).

Wakati tuko chini ya dhambi kwa sababu ya Adamu, Mungu alitupa kuhesabiwa haki kupitia Kristo bure. Je, tuendelee kuishi chini ya dhambi ili Mungu aonekane ana neema zaidi? Paulo anasema, “hilo haliwezekani.” Kwa nini hilo haliwezekani? Paulo anatoa sababu: Ni kwa sababu sisi tulioamini tulikufa katika ulimwengu ambao dhambi inatawala (ulimwengu wa Adamu) na tukafufukia katika ulimwengu ambao haki inatawala (ulimwengu wa Kristo). Tukio hili lilitokea wakati Yesu anakufa na kufufuka, na linaashiriwa sasa na ubatizo tunaoufanya (6:1-14).

Kama hatuko chini ya sheria, ambayo ndiyo ilisababisha dhambi kuhesabiwa, je, tuendelee kutenda dhambi kwa sababu kinachotuhesabia dhambi hakitutawali tena? Paulo anajibu tena, haiwezekani kuendelea kutenda dhambi baada ya neema. Hapa pia anatoa sababu: Sababu ni kwamba Mungu alishawatoa chini ya utawala wa dhambi na kuwapeleka katika utawala wa haki/utii. Dhambi ni bwana na utii/haki ni bwana, na haiwezekani kuwatumikia wote wawili kwa pamoja. (6:15-23).

Paulo, wakati anatoa sababu ya kwa nini haiwezekani kwa waamini kuendelea kuishi chini ya dhambi, alisema kwamba waamini wamekufa katika ulimwengu ambao dhambi inatawala (Ulimwengu wa Adamu) na wamefufuka katika ulimwengu ambao haki inatawala (Ulimwengu wa Kristo). Kufa katika ulimwengu ambao dhambi inatawala kuliwatoa pia waamini kutoka katika sheria. Sheria ndiyo iliyosababisha dhambi kuhesabiwa na kuwa kubwa (Warumi 5:13, 20). Hivyo, waamini walipokufa katika ulimwengu wa Adamu, walitolewa chini ya utawala wa dhambi na sheria—msaidizi aliyeipa dhambi nguvu. Kama ambavyo mwanamke anapofiwa na mume wake anakuwa huru kuolewa na mwingine, vivyo hivyo waamini walipokufa katika ulimwengu wa Adamu wakawa huru kuingia katika ulimwengu wa Kristo (7:1-4).

Kwa sababu kuna aina mbili za maisha, Paulo anatoa muhtasari wa maisha ya kila ulimwengu. Kuna maisha ya zamani, yaliyojaa dhambi—iliyotiwa nguvu na sheria, ambayo mwisho wake ni mauti (7:5). Kwa upande mwingine, kuna maisha ya haki ndani ya Kristo yanayopewa nguvu na Roho (7:6). Mistari hii ni muhtasari; maelezo ya kina ya maisha ya zamani katika ulimwengu wa dhambi na sheria yanaelezwa na Paulo kwa kirefu katika Warumi 7:7-25. Maisha mapya ndani ya Kristo yanayopewa nguvu na Roho yanaelezwa na Paulo kwa kirefu katika Warumi 8:1-30.

Katika kuelezea maisha ya zamani, Paulo anaanza kwa kujibu swali: kama sheria ndiyo iliyotoa nguvu kwa dhambi hadi ikasababisha mauti, je, sheria ni dhambi? Jibu la msisitizo ni hapana. Pamoja na kwamba sheria iliipa dhambi nguvu, sheria ni takatifu, njema, na ya haki (7:7-13). Kwa nini basi, pamoja na sheria kuwa njema, ikaipa dhambi nguvu na kusababisha mauti? Paulo anajibu kwamba sheria ni ya rohoni, lakini mwanadamu asiyekombolewa yuko mwilini. Hivyo, kila wakati anakuwa katika vita vya daima kati ya “akili,” ambayo inakubaliana na sheria ya Mungu, na “mwili,” au “viungo,” ambavyo vinakubali sheria ya dhambi. Matokeo yake ni kwamba sheria ya Mungu, ambayo iliichochea dhambi, haina uwezo wa kuvunja nguvu ya dhambi ( 7:14-25). Ikiwa hali ilikuwa hivyo, je, jawabu la Mungu ni nini? Paulo anatoa muhtsari wa jibu katika Warumi 7:25a, lakini anatoa maelezo ya kina ya jawabu hilo la Mungu katika sura ya nane. Sura ya nane inaeleza maisha mapya ndani ya Kristo, kama ilivyoainishwa katika Warumi 7:6.

Kinyume na maisha ya zamani ya dhambi chini ya sheria, Mungu ametukomboa na kutuingiza kwenye maisha mapya ndani ya Kristo yanayopewa nguvu na Roho Mtakatifu. Roho anawaweka huru waamini, anawawezesha kutimiza maagizo yote ya sheria, anawapa uwezo wa kuishi maisha ya haki, na anahuisha miili yao. Kwa ujumla, asiyekuwa na Roho Mtakatifu si wa Kristo (8:1-11). Kwa sababu ya haya ambayo Roho anawafanyia waamini, waamini wote ni wadeni wa kuishi kwa kufuata maelekezo yake. Hata hivyo, wanaweza kuchagua kuasi na kuishi kwa kufuata mwili. Roho pia ndiye anayethibitisha kwamba sisi ni watoto wa Mungu, na kama ni watoto, basi ni warithi pamoja na Kristo (8:12-17). Pamoja na yote Mungu aliyoyafanya katika kazi yake ya ukombozi, bado uumbaji unakabiliwa na changamoto zilizosababishwa na dhambi. Uumbaji unaugua, na waamini walio na Roho pia wanaugua hata sasa. Lakini tunasubiri ukombozi wa uumbaji wote na ukombozi wa miili yetu kutokea. Matumaini haya tuliyonayo ndiyo kichocheo cha kuvumilia mateso ya sasa tunayoyapata, maana utukufu huo ujao ni mkuu, Mungu aliouandaa kwa wale aliowajua tangu asili (8:18-30). Kama Mungu amewatoa waamini kutoka ulimwengu wa dhambi, sheria, na hukumu kupitia kifo cha Mwanae Yesu Kristo, na tena akawapa Roho wake ili waishi maisha mapya kama watoto wake, na zaidi akawapa tumaini la kutukuzwa pamoja na uumbaji wote, ni nani atakuwa juu ya waamini? Ni nani atawashitaki au kuwahukumu? Na ni nani atakayewatenga na upendo huo wa Kristo? Jibu la msisitizo ni kwamba hakuna. Hakika, ushindi ni wa waamini (8:31-39).

Tangu mwanzo, Paulo ameonyesha kwamba wokovu ni kwa wote, Wayahudi na Mataifa, lakini Wayahudi wamepewa kipaumbele (1:16-17). Hata hivyo, kuwa Myahudi tu kuna faida katika mpango wa Mungu wa wokovu (3:1-2; 9:3-5). Kutokana na hilo, swali linajitokeza: imekuwaje Wayahudi wengi hawajaikubali Injili pamoja na faida walizonazo? Pili, Paulo alikuwa anafundisha kuhusu wokovu, ameeleza kuwa waamini wote (Wayahudi na Mataifa) ndio watoto wa Ibrahimu (4:1-25), watoto wa Mungu (8:14-17), na warithi wa ahadi za Mungu (4:16; 8:17). Swali linalofuata ni: je, fundisho hili linamaanisha kuwa nafasi ya uteule wa Israeli imechukuliwa na Kanisa? Je, Israeli haina tena nafasi yake ya uteule mbele za Mungu kama ilivyosisitizwa katika Agano la Kale? Tatu, kwa mujibu wa Neno lake, Mungu aliahidi wokovu kwa Israeli (kwa mfano, Isaya 59:20-21; Yeremia 31:31-34). Hata hivyo, uhalisia unaonyesha kuwa Israeli imekataa wokovu. Je, hili linamaanisha kuwa Mungu si mwaminifu kwa ahadi zake? Kwa maneno mengine, je, ahadi za Mungu zimeshindwa kutimia? Kwa muhtasari, katika sura ya 9 hadi 11, Paulo anajibu maswali haya: kwa nini Israeli imemkataa Kristo? Na kukataa kwao Kristo kuna maana gani katika kazi ya Mungu ya wokovu?

Paulo anaanza kutoa majibu kwa kueleza masikitiko yake makubwa juu ya Wayahudi kwa sababu wamemkataa Kristo, pamoja na kuwa na nafasi bora kuliko Mataifa katika mpango wa Mungu wa wokovu (9:1-5). Pamoja na Wayahudi wengi kumkataa Kristo, hiyo haina maana kwamba Neno la Mungu limeshindwa kutimia. Paulo anathibitisha hili kwa kuonyesha kwamba, tangu mwanzo, Waisraeli halisi hawakuwa ni wale waliozaliwa katika kizazi cha Ibrahimu bali ni wale ambao Mungu aliwatamkia Neno. Ibrahimu alikuwa na watoto wengi, lakini Isaka ndiye aliyetamkiwa Neno, na hivyo yeye ndiye Myahudi halisi. Vivyo hivyo, Yakobo ndiye aliyetamkiwa Neno, na sio Esau. Kwa ujumla, Paulo anasema tangu mwanzo, wokovu umekuwa ni kwa wale ambao Mungu amewachagua kwa mapenzi yake, na sio tu walio uzao wa Ibrahimu katika mwili. Kwa sasa, Wayahudi walioamini na Mataifa walioamini ndio ambao Mungu amewachagua kuwa sehemu ya watu wake aliowaokoa, na hivyo Neno lake halijashindwa kutimia (9:6-29).

Baada ya kuonyesha kwamba historia inathibitisha kuwepo kwa makundi mawili ndani ya Israeli tangu mwanzo — Israeli walio uzao wa Ibrahimu (Israeli kwa ujumla) na Israeli wa ahadi (wachache ndani ya Israeli) — Paulo sasa anaeleza kwanini Israeli, uzao wa Ibrahimu (taifa kwa ujumla), hawajapata wokovu, na badala yake, Mataifa wamepata. Paulo anasema kwamba Wayahudi wamekosa wokovu kwa sasa kwa sababu wameshindwa kutafuta haki ya Mungu kwa imani; badala yake, wamefanya bidii kutafuta haki ya Mungu kwa njia ya sheria. Hili limetokana na kutokutambua kwamba Kristo ndiye mwisho wa sheria. Kwa kuwa wokovu unapatikana kwa yeyote anayeamini, ndio sababu Mataifa wamepata wokovu kwa kuwa wameamini (9:30-10:14). Paulo anamalizia kwa kutoa ushahidi kwamba Israeli wamehubiriwa na wamesikia Neno la Kristo lakini hawajaamini. Hivyo, Mungu atawatia wivu Israeli kwa kuwachukua waamini wa Mataifa kuwa watu wake, ambao mwanzo hawakuwa watu wake (10:15-21).

Kwa kujibu swali, Je, Mungu amewatupa watu wake Israeli?, Paulo anarejea tena kwa alichokisema mwanzo, lakini sasa kwa kutumia mfano mwingine katika historia. Historia ya wakati wa Elia inaonyesha kuwa, ingawa taifa la Israeli lilimkataa Mungu na kuabudu sanamu, Mungu alijisazia watu elfu saba walioendelea kumwamini. Vivyo hivyo, Paulo anasema kuwa hata kwa sasa Mungu ana Wayahudi wanaoendelea kumwamini, yeye mwenyewe Paulo akiwa mmoja wao pamoja na kundi kubwa kutokuamini (11:1-5). Wayahudi hao wanaomwamini Mungu wamepewa nafasi hiyo kwa neema na si kwa matendo yao. Kwa upande mwingine, Wayahudi ambao hawajaamini Mungu amewapa roho ya usingizi, macho yasiyoona, na masikio yasiosikia (11:6-10).

Kutokana na yale Paulo amefundisha, inaweza kuonekana kana kwamba Mungu amewaacha kabisa taifa la Israeli na kuchagua wachache kati yao. Lakini Paulo anasema hapana, Mungu hajawaacha watu wake kabisa. Paulo anazungumza hapa na Wamataifa (mstari wa 13) na kuwaambia kwamba ugumu umewapata Israeli kwa muda tu, na kwa muda huo Wamataifa wamefikiwa na wokovu (11:11-15). Paulo anaendelea kuzungumza na Wamataifa, akiwaambia kwamba wasijisifu juu ya Wayahudi walio nje ya mpango wa Mungu kwa sasa. Wao ndio shina na sisi Wamataifa ni matawi yaliyopandikizwa, tena ni matawi mwitu. Wamataifa Paulo anasema tuogope na tuendelee kuamini; tusipoendelea kuamini Mungu hashindwi kutukata kama alivyowakata baadhi ya Israeli, ambao ni matawi ya asili (11:16-24).

Katika kuelekea kilele cha mafundisho yake, Paulo anawafunulia Wamataifa siri kwamba Israeli wote (bila makundi) wataokoka pale muda wa Wamataifa utakapokamilika. Hili litatokea kutimiza ahadi ya Mungu ya kuwaokoa Israeli (kama ilivyotabiriwa katika Isaya 59:20-21 na Yeremia 31:31-34). Hii ni pamoja na ukweli kwamba kwa sasa Israeli ni maadui wa Injili. Lakini kwa sababu ahadi za Mungu juu yao ni amina na kweli, Israeli wote wataokolewa wakati huo ukifika (11:25-32). Paulo anamalizia kwa kusifu hekima na maarifa ya Mungu yaliyoamua mambo kuwa vile yalivyo, kama alivyoyaelezea (11:33-36).

Baada ya kueleza kwa kirefu kuhusu Israeli, mwitikio wao kwa Injili na hatima yao, Paulo sasa anaingia kueleza namna gani waamini wanapaswa kuishi katika maisha yao mapya ndani ya Kristo. Sehemu hii iko katika makundi mawili: Kwanza, Paulo anaeleza kwa ujumla namna gani maisha mapya ndani ya Kristo yanapaswa kuwa, kama ambavyo anaeleza katika barua zake nyingine (12:1-13:14). Pili, anatoa maagizo maalum kwa Kanisa la Rumi kuhusu namna wanavyopaswa kuishi kwa mujibu wa kweli ya Injili. Mafundisho haya yanalenga kutatua tatizo la kimahusiano lililokuwepo kati ya waamini Wayahudi na Wamataifa (14:1-15:13).

Katika kufundisha kwa ujumla kuhusu namna gani maisha mapya ndani ya Kristo yanapaswa kuwa, Paulo anaanza na mwito wa kutoa miili yetu kuwa dhabihu (Mwito wa muelekeo). Anaunganisha na mwito wa katazo: tusiufuatishe namna ya dunia hii (12:1-2). Baada ya hapo, Paulo anatoa maelekezo kwa kila mwamini kukaa katika karama yake kama Mungu alivyompa. Anasisitiza kila mmoja kutumikia karama yake huku akiweka wazi kwamba tuko wengi na kila mmoja ana kazi yake kama viungo vilivyo vingi katika mwili (12:3-8). Paulo anaendelea mbele kwa kufundisha jinsi waamini wanavyopaswa kuishi huku wakiongozwa na upendo (12:9-21). Kabla ya kuendelea na kuhimiza waamini kuishi kwa upendo, Paulo anawahimiza waamini kutii mamlaka za kiserikali, kwa kuwa wao ni wajumbe wa Mungu wanaohimiza watu kutenda mema na sio mabaya (13:1-7). Baada ya hilo, Paulo anarudi tena kuhimiza waamini kuishi kwa upendo, akitukumbusha kwamba wakati wa kuokolewa kwetu kumekaribia zaidi kuliko tulivyoanza kuamini. Kwa maneno mengine, anahimiza upendo katika kipindi hiki cha mwisho, ambacho Bwana wetu Yesu yuko karibu kuja kututukuza. (13:8-14).

Kutokana na changamoto za kimahusiano zilizokuwa zikiendelea kati ya waamini wayahudi na wamataifa, Mtume Paulo anawaita kukaribishana bila kuhukumiana pamoja na tofauti zao za kiimani katika mambo kadhaa. Anaanza na kuwahimiza waamini walio “dhaifu katika imani” na “wenye nguvu” kukuribishana (kuwa na ushirika pamoja) badala ya kudharauliana au kuhukumiana, licha ya kuwa na mitazamo tofauti kuhusu masuala fulani katika imani. Mambo haya ni kama vile masharti katika vyakula na ufuatiliaji wa siku (14:1-13). Baada ya hapo, Paulo anawahimiza waamini “wenye nguvu” kuacha kutumia uhuru wao iwapo kwa kufanya hivyo wataweka kikwazo au mtego kwa waamini wenzao walio “dhaifu katika imani” (14:14-23). Kwa kutumia mfano wa Kristo jinsi ambavyo hakujipendeza yeye mwenye, Paulo anasisitiza waamini “wenye nguvu katika imani” kufanya jitihada katika kuwapendeza waamini wenzao ambao ni “dhaifu katika imani” (15:1-6). Katika muktadha huu, waamini “wadhaifu katika imani” ni waamini ambao kwa asilimia kubwa ni wayahudi, ambao walishika masharti ya torati kuhusu vyakula na kuhusu ufuatiliaji wa siku. Kwa upande mwingine, waamini “wenye nguvu katika imani” ni waamini ambao kwa asilimia kubwa ni wamataifa na wayahudi wachache, ambao hawakuwa na masharti yeyote kuhusu vyakula na kuhusu siku. Hivyo, Paulo anafikia kilele cha mwito wake kwa kuwasisitiza wote, wayahudi na wamataifa wakaribishane (wawe na ushirika) kama ambavyo Kristo amewakaribisha wao, ili Mungu atukuzwe. Yeye aliyefanya ukombozi huu wa wote kupitia kristo kama yanenavyo maandiko (15:7-13).

Baada ya mafundisho hayo, barua hii inafikia sehemu ya mwisho. Katika kufunga barua yake, Mtume Paulo anaanza na kuwaeleza Warumi kazi yake aliyopewa na kristo. Kazi ya kikuhani ya kuwatoa wamataifa kwenye maisha yao ya awali na kuwaleta katika utii wa imani, ili wakiisha kutakaswa na Roho wawe sadaka yenye kibali mbele za Mungu. Wito huu ndio uliomfanya Paulo aandike waraka huu kwao, pamoja na ukweli kwamba wao walikuwa na uelewa wa kiroho. Katika kueleza hayo, Paulo pia anataja maeneo ambayo ameyahudumia kwa injili (15:14-21). Kazi ya injili katika maeneo hayo ndiyo iliyomzuia kwenda Rumi hapo awali. Lakini sasa kwa kuwa kazi katika maeneo hayo imefika mwisho, Paulo yuko tayari kwenda kuhubiri Uhispania, na akiwa njiani atapitia Rumi. Kwa sasa, Paulo anawaambia Warumi kuwa anaenda Jerusalem kwanza kupeleka msaada wa kifedha kutoka kwa waamini wa Mataifa kwa kanisa la Kiyahudi (15:22-29). Aidha, kwa kuwa Paulo anafahamu kuwa kuna upinzani mkubwa kutoka kwa Wayahudi wasioamini, anaomba kanisa la Rumi limuombee ili asidhuriwe na Wayahudi hao na aweze kufika Rumi salama (15:30-33).

Baada ya hapo, Paulo anamtambulisha Fibi kwa kanisa na kulitaka kanisa kumhudumia vizuri. Fibi ndiye aliyepeleka barua hii Rumi kutoka Korintho. Fibi alikuwa ni mwanamke, mhudumu (shemasi) wa kanisa  la Kenkrea na mfadhili wa injili (16:1-2). Pamoja na kwamba Paulo hakuwahi kufika Rumi, kuna watu wengi anawafahamu walioko huko, hivyo anatoa salamu zake kwa waamini anaowafahamu katika makanisa mbalimbali huko Rumi (16:3-16). Kabla ya kuwasilisha salamu kutoka kwa waamini waliokuwa pamoja naye huko Korintho kwenda kwa kanisa la Rumi, Paulo anawaonya waamini wa kanisa hilo kujiepusha na waalimu wa uongo (16:17-20). Baada ya hayo, anawakilisha salamu za waamini waliokuwa pamoja naye kwenda kwa kanisa la Rumi (16:21-24). Anafunga barua hii kwa kumtukuza Mungu, ambaye anaweza kuwafanya Warumi kuwa imara sawa na injili aliyohubiri yeye (16:25-27).


FOOTNOTES

[1] Kwa nini Mtume Paulo anasema haionei aibu Injili? Kwa namna nyingine, kwa nini Mtume Paulo anahusisha Injili na aibu? Katika miji ya kimataifa/kipagani kama Rumi, Korintho, Efeso, na mingine, habari za wokovu kupitia kifo cha msalaba zilionekana kama jambo la kipuuzi, jambo ambalo watangazaji wa habari hizo walitakiwa kuona aibu (1 Wakorintho 1:18, 23). Hii ni kwa sababu, kabla ya Kristo, kuhubiri Injili ilikuwa ni kutangaza habari za ushindi wa vita vya Kaisari/mfalme fulani au habari za mfalme huyo kuingia katika madaraka yake.

[2] Aya ya 3:1-8 ni ngumu kuielewa kwa sababu ina maswali mengi na majibu mafupi. Kwa ujumla, Paulo anasema kwamba Wayahudi wana faida ukilinganisha na mataifa, lakini faida hizo haziwaondoi kwenye hukumu ya Mungu. Aidha, Paulo anachokizungumza hapa atakieleza kwa urefu zaidi katika sura ya tisa hadi ya kumi na moja.

Unakuja hivi karibuni…