Wimbo Ulio Bora – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA KITABU CHA WIMBO ULIO BORA.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.

UTANGULIZI.

Kitabu cha Wimbo Ulio Bora ni cha kipekee sana kati ya vitabu vyote vya Biblia. Kwanza, kinapewa jina linalotukuza ushairi wake kuliko nyimbo nyingine zote, kwa kuitwa “Wimbo wa Nyimbo,” kama vile Mungu anavyoitwa Mungu wa miungu au Bwana wa mabwana. Lugha hii inaonyesha ubora wa wimbo huu kuliko nyimbo nyingine. Pili, kitabu hiki kinahusu mapenzi kati ya mwanamke na mwanaume bila kumzungumza kuhusu Mungu au imani katika yeye moja kwa moja. Tatu, ni kitabu ambacho mwanamke ndiye msemaji mkuu kuliko mwanaume, tena katika suala la mapenzi.

Kwa sababu ya upekee huu, maneno na ujumbe wa kitabu hiki kwa miaka mingi yametafsiriwa kwa kukwepa uhalisia wake. Pale ambapo mwanamke anaongea, Israeli au kanisa limewekwa kama msemaji. Pale mwanaume anapoongea, Mungu amewekwa kama msemaji. Hata hivyo, kitabu hiki kinazungumza moja kwa moja kuhusu mapenzi kati ya mwanamke na mwanaume. Pamoja na watu wengine kuuonea aibu ujumbe huu, bado ujumbe huu ni sehemu ya maandiko matakatifu kutoka kwa Mungu.

AINA YA UANDISHI/AINA YA KITABU.

Kama kichwa cha habari kinavyosema “Wimbo ulio bora”/”Wimbo wa nyimbo”, ujumbe wa kitabu hiki umeandikwa kwa njia ya wimbo (ushairi). Kwa kuwa ni ushairi kitabu hiki kina matumizi makubwa ya lugha ya picha kama ilivyo kawaida kwa ushairi wa kiebrania. Mfano wa lugha za picha zilizotumika katika ushairi huu ni pamoja na bustani (4:12), shamba (1:16) na maua ya yungi yungi/nyinyoro (2:1-2,16). Lugha hizi zote zinawakilisha mwili wa mwanamke hasa kusisitiza uzuri wake.

Sifa nyingine ya ushairi iliyopo katika ushairi huu ni usambamba. Usambamba ni sifa ya ushairi wa Kiebrania ambapo mstari wa pili au sehemu ya pili ya mstari hurudia au hupinga ujumbe wa mstari wa kwanza au sehemu ya kwanza ya mstari ili kusisitiza maana au kuboresha athari ya kifasihi. Mfano katika 2:1, sehemu ya pili ya mstari isemayo “Ni nyinyoro ya mabondeni” imerudia ujumbe wa sehemu ya kwanza ya mstari isemayo “Mimi ni ua la uwandani”. Usambamba hapa umesisitiza uzuri wa mwanamke. Katika aina zake, usambamba unaonekana katika maeneo mengi ya kitabu hiki. Maeneo hayo ni kama vile 2:1,16; 4:1; 6:4 na 8:6.

.

UJUMBE MKUU WA WIMBO HUU.

Lengo la kitabu hiki ni kutuonyesha namna gani mapenzi yalivyo kati ya mwanamke na mwanaume. Ujumbe wa uzuri, uhuru na nguvu ya mapenzi tunaupata kupitia kusikiliza jinsi mwanamke na mwanaume wanavyojieleza katika muktadha wa mapenzi. Mazungumzo yao yanaonyesha jinsi ambavyo upendo (mapenzi) ulivyo na nguvu kuliko kifo (8:6). Mazungumzo yao yanaonyesha jinsi mwanamke/mwanaume anavyofurahia uzuri wa mwenzake (4:1-8; 6:4-7; 7:2-8 na 5:10-16). Mazungumzo yao pia yanaonyesha jinsi wapenzi walivyo huru katika mapenzi yao: tofauti na kizazi cha leo kinachoonyesha kuzuiliwa kwa mwanamke katika mapenzi. Uhuru wa mwanamke kueleza hisia zake (1:2-7); Uhuru wa mwanamke kufanya jitihada “zinazoumiza” kwa ajili ya mapenzi (5:2-8) na uhuru wa kumwita mpenzi wake kwa ajili ya tendo la ndoa (4:16). Pamoja na uhuru huo, ushairi huu unatuonyesha kwamba mapenzi ni kati ya watu wawili tu; mwanamke mmoja na mwanaume mmoja (2:16 na 6:3). Wapenzi hao malengo yao ni mahusiano ya kudumu yenye kilele katika ndoa (4:8-15). Kwa sababu ya lengo hilo na kwa sababu ya nguvu ya mapenzi, ujumbe wa kitabu hiki unaonya kutokuyachochea mapenzi mpaka wakati wake utakapofika (2:7; 3:5; 8:4).

MPANGILIO WA USHAIRI HUU.

NambaMaandikoMaelezo
11Kichwa cha habari
21:2-2:7Mwanzo wa mapenzi
32:8-3:5Kuwepo na kutokuwepo kwa mpenzi
43:6-5:1Bwana arusi na Bibi arusi
55:2-6:3Kutoweka kwa mpenzi
66:4-8:4Uzuri wa mwanamke na utayari wake
78:5-14Nguvu ya upendo

MFULULIZO WA MAWAZO KATIKA WIMBO HUU.

Kitabu hiki kinaanza na kichwa cha habari, kichwa kinachotambulisha aina ya kitabu hiki. Kitabu hiki ni wimbo ulio bora kuliko nyimbo zote unaomhusisha Suleimani[1] (1). Sehemu ya kwanza ya ushairi huu inaanza na maneno ya mwanamke anayemwita mwanaume katika mapenzi, mwanaume mwenye mvuto wa kuvutia wanawake wengi. Pamoja na mwanaume huyu kuvutia wanawake wengi, mwanamke mzungumzaji anasema yeye ni mzuri kuliko wanawake wengine, ingawa rangi yake imeathiriwa na jua kutokana na kazi alizokuwa akifanya alizopewa na kaka zake. Kwa kuwa mwanaume ni mchungaji, mwanamke anamwuliza ni wapi atakapolisha mifugo yake na ni wapi atakapopumzika ili aweze kumfuata bila kutangatanga. Mwanamke asipojua alipo ataishia kuzunguka kwa wachungaji wengine ambao wanaweza kumdhania kuwa ni kahaba. (1:2-7). Mwanaume anamwambia mwanamke afuate nyayo za kondoo ili aweze kumpata. Maelekezo hayo yananzisha mfululizo wa wapenzi hawa kumwagiana sifa. Mwanamke anaanza kumwagiwa sifa za uzuri wake na kujipamba kwake na mwanaume, huku akiahidiwa kufanyiziwa mikufu ya dhahabu yenye mapambo ya fedha (1:8-11). Baada ya sifa hizo, mwanamke pia anamwaga sifa za uzuri wa mwanaume kwa kutumia mifano miwili: mfuko wa manemane na kishada cha maua ya hina (1:12-14). Sifa hizo zote zinahusiana na harufu nzuri. Mwanaume anarudia tena kumwaga sifa za uzuri wa mwanamke kwa kueleza uzuri wa macho yake (1:15). Mwanamke anamaliza sehemu ya kwanza ya majibizano haya kwa kutaja uzuri wa mwanaume wake na kuelezea makazi yao (1:16-17). Sehemu ya pili ya majibizano ya kumwagiana sifa yanaanza na mwanamke kujisifu uzuri wake kwa kutumia lugha ya picha inayohusiana na maua (2:1). Mwanaume anakubaliana na sifa hizo zinazomfanya mwanamke wake awe bora katikati ya wanawake wengi (2:2). Vivyo hivyo, mwanamke anamtaja mwanaume wake kuwa bora kama mtofaa (mti wa apple) katikati ya miti mingine. Mwanamke anamalizia majibizano haya kwa kueleza uzoefu wake wa mapenzi na mwanaume huyu. Mwanaume humchukua na kumpeleka sehemu ya sherehe huku akimlinda kwa upendo. Uzoefu wa nguvu ya mapenzi kati yake na mwanaume huyu unamfanya mwanamke huyu kuwapa onyo mabinti kuhusu mapenzi; wasiyaamshe wala kuyachochea (2:3-7).

Sehemu ya pili ya ushairi huu inatangaza furaha ya mwanamke kuhusu ujio wa mpenzi wake. Mpenzi anakuja akirukaruka kuelekea kwake kama swala au paa na kusimama nje ya ukuta wake huku akichungulia kupitia madirisha (2:8-9). Mwanamke anatupa ripoti kwamba mwanaume akiwa dirishani alianza kumshawishi atoke nje aambatane naye. Mwanaume alimkumbusha kwamba kipindi cha mvua na baridi kimepita, kimekuja kipindi cha machipuo, kipindi kizuri kwao kuambatana (2:10-15). Mwanamke anathibitisha mapenzi yao na kwa kutumia lugha ya picha anaelezea jinsi mwanaume anavyohusiana na mwili wake mpaka asubuhi[2] (2:16-17). Pamoja na maelezo hayo, mwanamke anatueleza kwamba usiku mmoja alimtafuta mpendwa wa nafsi yake kitandani na mpaka mjini, lakini hakumpata. Mwanamke huyu alimtafuta kwa juhudi mpendwa wa nafsi yake, na hatimaye akampata, kisha akampeleka mpaka chumbani kwa mama yake kumficha. Kwa sababu ya nguvu ya mapenzi iliyoonekana wakati wa utengano kati ya mwanamke na mpendwa wake, mwanamke huyo anawaonya tena binti za Yerusalemu tena kwamba wasiyaamshe wala kuyachochea mapenzi mpaka yatakapoona vema yenyewe (3:1-5).

Sehemu ya tatu ya ushairi huu inaanza na maelezo ya usalama na ubora wa machela (kiti cha kifalme ambacho hutumiwa kuwabeba wafalme) ya Mfalme Suleimani akiwa katika msafara wake. Maelezo hayo yanaambatana na mwito wa binti za Sayuni kukusanyika ili wamtazame mfalme Suleimani akiwa amevaa taji yake (3:6-11). Baada ya maelezo hayo, Mwanaume anatoa sifa za uzuri wa mpenzi wake. Kwa kutumia lugha ya picha anaeleza uzuri wa macho yake, nywele , meno, midomo, kinywa, mashavu, shingo na maziwa yake mawili. Na katika maziwa mawili ya mpenzi wake, wanaume anasema hatatoka hata kama majira yatabadilika (4:1-7). Mwanaume, kwa kumtambulisha mpenzi wake kama “bibi arusi” anamuita atoke sehemu hatarishi na aje kwake.[3] Mwito huu ni kwa sababu mwanamke ameshikilia moyo wa mwanaume kwa mapenzi yake ya ajabu. Zaidi, Mwanaume anamuelezea mpenzi wake kama bustani iliyofungwa na chemchemi iliyotiwa muhuri. Bustani hii ina miti mingi yenye matunda mazuri na inachanua majani yenye harufu nzuri (4:8-15). Baada ya maneno hayo mazuri, mwanamke anaitikia kwa kukubali mwanaume iangie katika bustani hii ili ale matunda ya bustani hiyo (4:16). Mwisho, Mwanaume anatupa ripoti kwamba amekula matunda ya bustani yake, na anahimiza wapenzi kufanya hivyo (5:1).

Sehemu ya nne ya ushairi huu ina maelezo ya mwanamke kumkosa mpenzi wake akiwa kitandani usiku, kama ilivyokuwa katika sehemu ya pili ya ushairi huu (angalia 3:1-5). Mwanamke alimsikia mpenzi wake akibisha hodi, akiomba afunguliwe (5:2). Kama ilivyo katika michezo ya kimapenzi, mwanamke alimwambia mwanaume, atafunguaje wakati tayari amekwisha kulala? Hata hivyo, pamoja na maneno hayo, mwanamke alikwenda kufungua mlango kwa furaha na hisia kali za kimapenzi, lakini hakumkuta mpenzi wake kwa kuwa tayari alikuwa amekwisha ondoka. Mwanamke alifanya bidii ya kumtafuta, lakini akaishia kupigwa na walinzi wa mji. Hivyo, mwanamke anatoa wito kwa binti za Jerusalemu kwamba wakimuona mpenzi wake, wamjulishe kwamba yeye +anazimia kwa mapenzi. (5:3-8). Kutokana na mwito huo, Binti za Jerusalemu wanamuuliza mwanamke, mpenzi wake ana nini za zaidi kinachomfanya awasihi kwa uzito huo? (5:9). Mwanamke anajibu swali hilo kwa kuelezea uzuri wa mpenzi wake unaomfanya awe wa kipekee katikati ya maelfu ya wanaume. Kwa kutumia lugha ya kufananisha Mwanamke anaeleza uzuri wa ngozi, kichwa , nywele, macho, mashavu, midomo, mikono, mwili, miguu, sura na kinywa cha mpenzi wake (5:10-16). Baada ya majibu hayo mazuri, binti za Jerusalemu wanamuuliza tena mwanamke, mpenzi wake amekwenda wapi ili washirikiane naye kumtafuta? (6:1). Majibu ya mwanamke yanashangaza; Mwanamke anasema mpenzi wake yuko katika mwili wake, yaani mwili wa mwanamke[4]. Yuko kwa ajili ya kula na kuchuma nyinyoro/yungi yungi[5]. Muunganiko wao huu unathibitisha kwamba wao wanamilikiana (6:2-3).

Sehemu ya tano ya ushairi inaanza na mwanaume kumwaga tena sifa za uzuri wa mpenzi wake. Mwanamke anasifiwa kwa kufananishwa na miji mizuri; macho yake, nywele, meno, na mashavu yanasifiwa kwa uzuri kwa kutumia lugha mbalimbali za mfananisho. Pamoja na kuwepo kwa wanawake wengi (malkia, masuria, na wanawali), mwanamke mpenzi wa mwanaume anaambiwa yeye tu ndiye wa kipekee. Uzuri wa mwanamke haufananishwi tu na vitu vilivyopo katika nchi bali pia na vile vilivyoko angani (6:4-10). Mwanaume tena anasema alikwenda bustanini (kumbuka bustani imetumika kama picha ya mwili wa mwanamke) ili kutazama uhai wa mimea, lakini ghafla akajikuta moyo wake umekamatwa (6:11-12). Baada ya hapo, tunasikia sauti ya marafiki wanawake wakimwita mwanamke arudi ili wamtazame (6:13a), na yeye anawahoji kwa nini wanataka kumtazama (6:13b). Mwanaume anajibu swali hilo kwa kutaja sifa za uzuri wa mpenzi wake. Hii ni kwa mara ya tatu katika ushairi huu. Mwanaume anamsifia mwanamke uzuri wa nyayo zake, mapaja, kitovu, tumbo, maziwa, shingo, macho, pua, kichwa, nywele, umbo, harufu ya pumzi, na kinywa chake. (7:1-9a). Kwa sababu mwanaume amemsifia mwanamke kwamba kinywa chake ni kama divai iliyo bora, mwanamke anaitikia kwa kusema kwamba, divai hiyo itiririke midomoni mwa mpenzi wake (7:9b). Mwanamke anaweka wazi kwamba mpenzi wake tamaa yake iko juu yake, hii ndio maana anamwita watoke waende nje ya mji. Nje ya mji kuna mazingira mazuri, utulivu na faragha na hivyo huko atampa mapenzi mazuri kwa kuwa amejiandaa (7:10-13). Pamoja na kumwita mpenzi wake sehemu ya faragha, mwanamke anatamani mwanaume angekuwa kaka yake ili awaze kumbusu hadharani bila kulaumiwa[6]. Na baada ya hilo, angempeleka nyumbani kwa mama yake ili kumnywesha divai yake huku mwanaume akimshika na kumkumbatia. Kwa sababu ya hisia kali na nguvu ya mapenzi, mwanamke anamalizia kwa kuwaonya tena binti za Jerusalemu kutokuyachochea mapenzi kabla ya wakati, lakini sasa kwa kutumia njia ya swali (8:1-4).

Sehemu ya mwisho ya ushairi huu inaanza na swali kutoka kwa wanawake wakuiliza; Ni nani anayetoka nyikani akiwa amemwegemea mpenzi wake? (8:5a). Mwanamke bila kutoa majibu kwa wauliza swali, anatoa majibu kwa mwanaume wake kwamba, yeye ndiye aliyeamsha hisia zake katika mti wa mtofaa (mti wa apples). Zaidi, mwanamke anamsihi mwanaume kummiliki kikamilifu kwa sababu upendo (mapenzi) na wivu (hamu ya kuwa na mtu mmoja) vina nguvu kuliko kifo. Nguvu yake ni kama ya mwali wa moto. Upendo unadumu zaidi (hauwezi kuzamishwa) na thamani yake ni kubwa kuliko mali zote za nyumbani kwa mtu (8:5b-7). Kaka wa mwanamke wanaingilia mazungumzo kwa kuuliza; wafanye nini ili kumlinda mdogo wao wa kike ambaye hajakomaa (hajaota maziwa) hadi siku atakayoposwa? Wanajijibu wenyewe kwa kusema, kama mdogo wao ni kama ukuta (anajilinda/bikira) watamwekea ulinzi zaidi kwa kumjengea mnara wa madini ya fedha. Na kama mdogo wao ni kama mlango (yuko wazi kwa mapenzi), watamzuia kwa mbao za mierezi. (8:8-9)[7]. Mwanamke anawajibu kaka zake kwamba yeye amejilinda dhidi ya wanaume (ukuta) na amekomaa (maziwa yake kama minara), hivyo yuko tayari kwa ajili ya mahusiano na mwanaume wake. Kwa sababu ya ukomavu wake wa kijinsia na upekee wake mwanamke anasema analeta amani kwa mpenzi wake (8:10). Tofauti na Suleimani aliyekuwa na shamba la mizabibu ambalo hakuwezi kulitunza yeye mwenywe (ndio maana akakodisha kwa walinzi), mwanaume anasema shamba lake analitunza yeye mwenyewe na liko mbele yake. Mwanaume anasema mpenzi wake yuko mbele yake na anamtunza tofauti na Suleimani aliyeshindwa kutunza wake zake yeye mwenyewe kwa kuwa ni wengi  (8:11-12). Ushairi unafika mwisho kwa mwanaume na mwanamke kutaka kuungana tena. Mwanaume anamaliza mazungumzo yake kwa kuomba kuisikiliza sauti ya mpenzi wake, kama rafiki zake wa kike wanavyoisikia (8:13). Mwanamke anamaliza kwa kumtaka mpenzi wake aje kwake kwa haraka kama paa na ayala walivyo na wepesi (8:14).

FOOTNOTES


[1] Kichwa cha habari kwa kutafsiriwa kwa kiswahili kinapoteza msisitizo wa mpangilo wa maneno unaosisitiza ubora wa wimbo huu. Namna kitabu hiki kilitakiwa kuitwa kama lugha yetu ingeruhusu ni Wimbo wa Nyimbo, kama vile ilivyo Mfalme wa wafalme, Bwana wa Mabwana, Patakatifu pa patakatifu, Mtakatifu wa watakatifu au Mungu wa miungu. Mtindo huu wa maneno unasisitiza ubora wa kitu husika.

[2] Maneno anayosema mwanamke kwamba mpenzi wake hulisha kundi lake katika nyiroro/yinguyingu katika mstari wa 16 ni lugha ya picha inayoelezea kuhusiana kwao kimwili. Hii inaweza kuwa tendo la ndoa au mchezo wowote wa kimapenzi kati yao. Hii ni kwa sababu, mwanamke alishajitaja yeye kuwa ni nyiroro/yinguyingu (2:1).

[3] Maeneo ya Lebanoni, kilima cha mlima Amana, Seniri na Hermoni yanawakilisha sehemu ya mbali isiyofikiwa na mapango ya simba na milima ya chui inawakilisha hatari.

[4] Neno bustani katika ushairi huu limetumika kama picha ya kuwakilisha mwili wa mwanamke (Angalia, 4:12-15;16 na 5:1)

[5] Maua haya pia yametumika kuwakilisha mwili wa mwanamke (2:1-2,16;4:5) na mara moja kuwakilisha midomo ya mwanaume (5:13).

[6] Hii inaashiria kwamba wapenzi hawa walikuwa kwenye utamaduni ambao ndugu wanaweza kupigana busu hadharani lakini sio wapenzi.

[7] Kama ambavyo mdogo wao anavyowaelezea katika sura ya kwanza (1:6), kaka za binti huyu wanaonekana kuwa walinzi wa mdogo wao. Hii imekuwa kawaida katika utamaduni wa kiyahudi na hata leo katika jamii nyingi.

Unakuja hivi karibuni……