UTANGULIZI.
Maandiko ya Msingi:
Mwanzo 1,2 na 3,
Warumi 5:12-21
Ufunuo 21:1-2.
Katika kujifunza jambo lolote duniani, ni vizuri kujifunza picha kubwa ya jambo kabla ya kujifunza taarifa za undani wa jambo husika. Hivyo, utangulizi huu una lengo la kukupa picha kubwa ya jambo hili linaloitwa Wokovu, na baada ya utangulizi huu, tutajifunza taarifa za undani za jambo hili.
Wokovu ni mpango wa Mungu wa kuurejesha uumbaji wake katika hali yake ya awali, ambayo Mungu alikuwa ameikusudia, hali ya kutokuwepo kwa dhambi na matokeo yake. Maneno haya yanamaanisha kwamba Mungu hapo awali aliumba vitu vyote vikiwa “vyema”. Hivi ndivyo kitabu cha Mwanzo kinavyotuambia, kwamba “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita. Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote.” (Mwanzo 1:31-2:1).
Lakini baada ya uumbaji huu, tatizo likatokea ambalo linaitwa “Dhambi” ambalo lilitekelezwa na mwanadamu. Dhambi ikazalisha matatizo mengine mengi mojawapo ni “Mauti”. Biblia inatufundisha kwamba “…kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;” (Warumi 5:12). Kwa hiyo, mauti ni matokeo ya dhambi ya Adamu ambayo ni hatma ya wanadamu wote. Mauti hapa ikiwa na maana zote mbili, yaani kutengwa na Mungu milele (mauti ya kiroho) pamoja na kutengana kati ya mwili na roho (mauti ya kimwili). Lakini pia Biblia inatufundisha kwamba kwa kutenda dhambi kwake Adamu kulisababisha wanadamu wote kuingia kwenye hali ya dhambi. Biblia inasema “Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi….” (Warumi 5:19). Na tena, dhambi ilisababisha mwanadamu awe mhukumiwa kama Biblia inavyosema kwamba “Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu…” (Warumi 5:18).
Mpaka hapa tunaona mwanadamu ana hali ya dhambi ndani yake (Warumi 5:19), ametengwa na Mungu milele na anatarajia kufa kimwili (Warumi 5:12), na amehukumiwa adhabu (Warumi 5:18).
Dhambi haikuishia kumhathiri mwanadamu tu, bali iliathiri uumbaji wote pia. Biblia inasema “Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa” (Warumi 8:20-22). Hivyo, uumbaji wote (viumbe vyote) uliathiriwa na dhambi, na hata sasa tunachokiona ni uumbaji ulioko chini ya utumwa wa uharibifu (yaani dhambi na matokeo yake).
Hivyo, Mungu kwa hekima yake akaandaa mpango wa kushughulikia (kutoa suluhisho) tatizo hili la dhambi na matokeo yake. Mpango huu, utekelezaji wake na utimilifu wake kwa pamoja ndio tunauita WOKOVU. Lengo la wokovu ni kuondoa dhambi na matokeo yake yote ili uumbaji uwe huru. Katika utekelezaji wa mpango huu, Mungu akaamua kumtuma mwanae duniani ili kushughulikia dhambi na matokeo yake. Huyu mwana akavaa mwili, akazaliwa kwa bikira Mariamu, akaishi maisha ya kumtii Mungu bila kufanya dhambi, akafa msalabani kuchukua hukumu iliyowapasa wanadamu, na akafufuka kama mtangulizi wa maisha ya baadaye. Huyu mwana anaitwa YESU KRISTO/MASIHI. Yesu alikuja kufanya yale Adamu alishindwa kufanya na yale aliyoyaharibu. Mwanadamu yeyote akimwamini YESU na kazi yake, anakuwa sehemu ya mpango huu wa wokovu, yaani anakuwa AMEOKOKA.
Kwa lugha nyingine, anayemwamini Yesu anafanywa mwenye haki kama Biblia inavyosema kwamba “Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki” (Warumi 5:19).
Anayemwamini Yesu anapatanishwa na Mungu kama Biblia inavyosema kwamba “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho” (2 Wakorintho 5:18-19).
Anayemwamini Yesu hahukumiwi tena kama Biblia inavyosema kwamba “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti” (Warumi 8:1-2). Yako mengi Yesu aliyoyafanya kwetu ambayo tutajifunza mbele, lakini jambo ambalo litawapata waliomwamini Yesu mpaka sasa ni kifo cha mwili (kutengana kati ya mwili na roho). Lakini Mungu kwa hekima yake ameweka suluhisho pia ambalo ni UFUFUO. Ufufuo utatokea pale Yesu atakaporudi mara ya pili, na wale ambao watakuwa hai wakati huo WATABADILISHA MIILI YAO na kuingia kwenye maisha mapya.
Kwa sasa bado tunaona dhambi na matokeo ya dhambi yakiwa kazini, lakini Yesu atarudi tena na kufanya mambo yote kuwa mapya, yaani ataumba dunia nyingine (Ufunuo 21 na 22), na ndani yake atauleta mji mpya kutoka mbinguni (Ufunuo 21:2) ambapo humo tutaingia tukiwa na miili mipya ya utukufu na hakutakuwa na dhambi wala matokeo ya dhambi humo. Na Mungu atafanya maskani yake pamoja na wanadamu na maisha haya yatakuwa ni KUTAWALA milele na milele. Hapo ndio mpango huu wa wokovu utakuwa umefika kilele chake.
Maswali.
1. Eleza kwa ufupi mpango wa Mungu wa wokovu.
2. Kwa nini dunia iko jinsi ilivyo leo? Kwa nini kuna magonjwa, uzee na kifo?
3. Nani ni kitivo cha Wokovu?
4. Mwanadamu anatakiwa afanye nini ili aokoke?
5. Hatma ya waliokoka ni nini?
A. HALI YA AWALI
1] Uumbaji Mwema wa Mungu.
Maandiko ya Msingi:
Mwanzo 1:1-2:24.
Biblia katika maandiko ya msingi hapo juu inatujulisha mwanzo wa kuwepo kwetu hapa duniani na mwanzo wa uumbaji wote. Biblia inaanza sura ya kwanza kwa kusema “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.” (Mwanzo 1:1) na pia inaanza sura ya pili kwa kusema “Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote.” Maneno haya yanatujulisha kwamba Mungu aliumba Mbingu (anga) na Nchi (ardhi) na vitu vyote vilivyomo ndani yake. Na kila kilichomo katika uumbaji, Mungu alikiona ya kuwa ni CHEMA baada ya kukiumba. Hii ndio maana Biblia inasema “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.” (Mwanzo 1:31).
Jambo kubwa na la muhimu katika uumbaji ni kwamba, Mungu alimuumba mwanadamu katika siku ya sita kwa mfano wake na akampa agizo na mamlaka juu ya uumbaji wote, yaani mwanadamu akapewa KUTAWALA uumbaji. Biblia inasema “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo.” (Mwanzo 1:26-30).
Zaidi ya kupewa sura na mfano wa Mungu, kupewa kutawala kila kiumbe na kupewa agizo la kuzaa na kuongezeka, mwanadamu alikuwa na ushirika na Mungu ambao viumbe wengine hawakuwa navyo. Kutoka katika ushirika huu, Mungu alimwagiza mwanadamu asile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Katika Mwanzo 2:16-17 Biblia inatueleza kwamba “Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”
Hivyo, mwanadamu aliishi bila kujua jema wala baya. Maisha haya tunaweza kuyajua kwa sehemu kwa kujifunza kwenye maisha ya mtoto mdogo. Mtoto mdogo hufurahia maisha aliyonayo kwa sababu hajui jambo jema ni lipi na jambo baya ni lipi. Mtoto mdogo hana mawazo ya nitakula nini, nitalala wapi, kipi ni hatari, kipi ni salama na mengine mengi yanayofanana na hayo. Maisha haya ni mfano tu wa maisha ambayo Adamu na Eva, mkewe, waliishi bustanini. Na zaidi, hawakuhitaji kufanya ibada maalumu au kutoa sadaka ili kukubaliwa/kuzungumza na Mungu, maana Mungu mwenyewe alizungumza nao. Maisha haya yalikuwa ni MEMA kama Mungu alivyokuwa amekusudia.
Maswali.
1. Kujua kwamba Mungu aliumba vitu vyote kunatusaidia nini sisi leo?
2. Kujua maisha mazuri ya mwanadamu kabla ya ujuzi wa mema na mabaya yanatusaidia nini sisi leo?
3. Habari za uumbaji katika Mwanzo 1 na 2 kwa ujumla zinatufundisha nini sisi leo?
4. Nini ilikuwa kazi ya tunda ambalo Mungu alimwagiza Adamu asile?
2] Tatizo la dhambi.
Maandiko ya Msingi:
Mwanzo 3:1-6
Maisha mazuri ya mwanadamu tulivyojifunza mwanzo yaliingiliwa na dosari baada ya mwanadamu kutomwamini Mungu na kushawishiwa na ibilisi kujitafutia uhuru wake mwenyewe wa kujua mema na mabaya. Mungu kwa hekima zake alitaka mwanadamu asiupate uhuru huu. Tukio hili la dhambi tunaweza kujifunza katika Mwanzo 3:1-6 na matokeo yake katika Mwanzo 3:7-24. Baada ya hapa, Mwanzo 4 hadi 11 inaonyesha jinsi dhambi ilivyoendelea kuwatawala wanadamu. Katika Mwanzo 3:1-6 Biblia inasema “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.”
Mungu alisema matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya yasiliwe. Hivyo, Mungu hakuficha kazi ya matunda ya mti aliowakataza Adam na Eva wasile. Pia, Mungu hakuficha matokeo ya kula matunda hayo: matokeo yake yalikuwa ni kifo. Kama Biblia inavyosema kwamba “Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika” Mwanzo 1:16-17.
Shetani, katika ushawishi wake, alitumia kazi ya matunda ambayo Mungu aliiweka wazi kwa Adamu na Eva kuwa kigezo cha kumshawishi Eva kula tunda. Shetani anasema “kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya” Mwanzo 3:5. Lakini shetani alipindua matokeo Mungu aliyoyasema. Mungu alisema “kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika” Mwanzo 2:17na Shetani akamwambia Hawa “…. Hakika hamtakufa” Mwanzo 3:4.
Baada ya ushawishi huu Hawa “alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.” Mwanzo 3:6.
Hivyo kwa tukio hili mwanadamu alimkosea Mungu, alifanya kile Mungu alimwambia asifanye kwa kushawishiwa na shetani ambaye alipindua kweli ya Mungu iliyoeleza matokeo ya kula tunda.
Maswali.
1. Dhambi ya Adam na Eva ilikuwa ni ipi?
2. Je mbinu ya ushawishi iliyotumika na Shetani kwa Eva inatumika mpaka leo? Kama Jibu ni ndio toa mfano.
3. Ukimuacha shetani, Nini kilimshawishi Eva kula tunda la ujuzi wa mema na mabaya?
3] Matokeo ya Dhambi.
Maandiko ya Msingi:
Mwanzo 3:7-24
Warumi 5:12-21
Kwa kuwa Mungu alishasema kazi ya mti na matokeo yatakayotokea ni rahisi kujua nini kinafuata baada ya Adam na Eva kula tunda ambalo Mungu aliwaambia wasile.
Matokeo yake ni kama yafutayo:
1. Tunda likafanya kazi yake, Adamu na Eva wakafumbuliwa macho wakajua mema na mabaya. Jambo moja la haraka walilolijua ni kuwa “wako uchi”. Hii haina maana kwamba kwamba siku waliokuwa ndio walikuwa uchi, bali siku hii ndio walijua kuwa wako uchi. Jambo hili ni ishara ya moja kwa moja kwamba sasa mwanadamu alipata uwezo wa kujua mem ana mabaya.
Baada ya kujua wako uchi wakajisaidia kwa kutafuta kitu cha kuwasitiri bila mafanikio na hivyo wakaamua kujificha ili Mungu asiwaone wakiwa uchi. Hivi ndivyo Biblia inasema” Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo. Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone. Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? “ Mwanzo 3:7-11.
2. Laana ikaingia kwa Adamu na Eva mkewe.
Kwa sababu ya kutokutii, Mungu akamzidishia mwanamke uchungu wake katika uzazi, tamaa ya mwanamke ikiwa kwa mwanaume na hatimaye mwanamke akawekewa kutawaliwa na Mwanaume. Mwanzo tuliona Mungu aliwaambia mwanamke na mwanaume wote wawili WATAWALE uumbaji, lakini baada ya dhambi laana akija na hivyo Mwanamke akawekwa ili ATAWALIWE na Mwanaume. Hivi ndivyo Biblia inasema katika Mwanzo 3: 16 kwamba “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.”
Na kwa upande wa mwanaume, ardhi ikilaaniwa ili apate/atafute chakula kwa jasho. Laana juu ya ardhi haikumuathiri Mwanadamu tu bali na viumbe vingine vilivyo katika ardhi. Biblia inasema Mungu “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” Mwanzo 3:17-19.
3. Kifo cha kimwili kikapata nafasi kwa mwanadamu. Kifo hiki kilipata nafasi kwa kuwa mwanadamu alitolewa kwenye bustani ambayo ilikuwa na mti wa uzima, ambao Mwanadamu kama angekula matunda hayo angeishi milele.
“Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.” Mwanzo 3:22-24
4. Mwanadamu akatolewa kwenye mahali ambako Mungu alipachagua kuwa ndio sehemu ya kukutana na Mwanadamu katika ushirika. Bustani ya Edeni ndio mahali Mungu alipachagua kuwa sehemu ya Adamu na Eva kuishi na hapo hapo ndio palikuwa mahali pa ushirika wao (Mungu na mwanadamu). Mungu alimtoa Adamu na Eva katika hiyo Bustani kama tulivyoona hapo juu (Mwanzo 3:22-24). Mungu kumfukuza Adamu na Eva kunaonyesha uhusiano wa Mungu na mwanadamu ukaathiriwa. Mungu akamtenga Mwanadamu mbali na yeye kwa sababu ya dhambi. Kitendo hiki cha mwanadamu kutengwa na Mungu ndio kifo kilichowekwa wazi na Mungu kwamba kitakuwa ndio matokeo ya kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya (Mwanzo 2:17).
5. Dhambi ikaingia ndani ya mwanadamu (Adam na Eva) na watoto waliozaliwa kwao nao wakaendelea kufanya dhambi.
WARUMI 5:12-21 inaeleza zaidi na kurudia yale yanayosemwa mwanzoni kuhusu dhambi ya Adamu na uhusiano wake kwa wanadamu wote, pamoja na suluhisho lililotolewa na Yesu na uhusiano wake na waamini (jambo ambalo tutalizungumzia vizuri mbele). Warumi 5:12-21 Paulo anafundisha kwamba “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi. Wala kadiri ya yule mtu mmoja aliyefanya dhambi si kadiri ya kile kipawa; kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo. Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima.Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi;ili kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu.”
Kutenda dhambi kwa Adamu na Eva kulisababisha kila mwanadamu anayezaliwa kuwa na ujuzi wa mema na mabaya, na kuingia chini ya utawala wa dhambi. Hii ilifanya kila mwanadamu kushiriki katika kutenda dhambi, na hivyo kifo kuwa ndio mshahara wa kutenda dhambi kwa wanadamu wote kama Mungu alivyosema. Na matokeo mengine yote ya dhambi yakawa ni sehemu ya maisha ya wanadamu wote.
Hivyo Mpaka sasa tumeona tatizo katika uumbaji mzuri wa Mungu ni DHAMBI na MATOKEO YA DHAMBI. Uumbaji wa Mungu ni MWEMA sana, lakini sasa umeingiliwa na DHAMBI na MATOKEO YAKE.
HIvyo Ukombozi/Wokovu utakuwa na lengo la kurejesha maisha kabla ya dhambi katika Uumbaji, yaani kuondoa DHAMBI na MATOKEO YAKE.
Maswali
1. Ni nini matokeo ya dhambi unayoyaona leo? (Matokeo matatu)
2. Kwa nini Adamu na Eva walijificha Mungu asiwaone?
3. Kwa nini tunakufa leo?
B. MAANA YA WOKOVU
Maandiko ya msingi:
2 Wakorintho 5:17-20
Waefeso 2:4-5
Wakolosai 3:12-14
Warumi 8:19-21
Yohana 11:25-26
Kwa mambo ambayo tumejifunza mpaka sasa (Kuhusu uumbaji mwema wa Mungu, tatizo la dhambi na matokeo yake) ni rahisi kujua nini kinatakiwa kurekebishwa. Hivyo, Wokovu kwa upana wake ni mpango wa Mungu wa kurejesha (Na zaidi kuboresha) uumbaji wake katika hali yake kwanza kabla ya kuingia kwa dhambi. Mpango huu sio tu mawazo ya Mungu ambayo hajayatekelezwa, bali ni mpango uliokatika utekelezaji sasa na utakamilika baada ya ujio wa Yesu mara ya pili.
Maeneo mahususi ya kurejeshwa ni kama ifuatavyo:
a. Uhusiano wa Mungu na Mwanadamu. Mwanadamu aliyefukuzwa na Mungu Bustanini akaribishwe tena. Mwanadamu aliyekufa apewe tena uhai (2 Wakorintho 5:17-20 na Waefeso 2:4-5).
b. Uhusiano wa mwanadamu na mwanadamu. Dhambi amemfanya mwanadamu afanye dhambi dhidi ya mwanadamu mwenzake, hivyo wokovu unatakiwa kurejesha uhusiano wa wanadamu (Wakolosai 3:12-14).
c. Uhusiano wa mwanadamu na uumbaji wote. Kwa sababu uumbaji uko kwenye matatizo kwa sababu ya mwanadamu, wokovu unahusisha laana kuondolewe kwenye uumbaji wote (Warumi 8:19-21).
d. Kupewa uwezo wa kuishi milele. Kwa sababu dhambi ilimfanya mwanadamu akose nafasi ya kuishi milele kimwili, wokovu unahusisha kurejesha nafasi hiyo (Yohana 11:25-26).
Katika kufanya Urejesho huu (Na zaidi uboreshaji), Mpango huu unatekelezwa kwa kusudi la kuondoa DHAMBI, MATOKEO YAKE na kumuondoa kabisa MSHAWISHI wa Mwanadamu.
Maswali
2. Je, wokovu unahusisha mwanadamu peke yake?
C: MPANGO WA MUNGU WA WOKOVU
Maandiko ya msingi:
Mwanzo 12:1-3
2 Samweli 7:12-16
Wafilipi 2:5-11
2 Petro 3:9-13
Baada ya dhambi kuingia na kuzalisha matokeo yake, uumbaji wote wa Mungu ulikuwa na dosari. Uumbaji sasa haukuwa kama Mungu alivyovema mwanzoni kwamba kila kitu ni chema. Hivyo, Mungu akaazimia kuurejesha uumbaji wote na kumrejesha mwanadamu kwenye hali yake ya awali. Jambo hili Mungu aliamua kwa hekima yake kulifanya kwa hatua.
- Mungu alianza na kuangamiza viumbe vyote juu ya nchi (Wanyama na wanadamu) na kubakiza viumbe vichache (Mwanzo 6 mpaka 10) ili kuukomboa uumbaji wake mbali na dhambi. Mungu alifanya jambo hili kupitia gharika.
Baada ya kutoka katika safina Mungu akambariki Nuhu kama alivyowabariki Adamu na Eva. Pia akamwambia Nuhu akazae na kuongezeka na kutawala viumbe hai kama alivyowaambia Adam na Eva. Lakini kwa kuwa dhambi ilikuwa ndani ya mwanadamu, baada ya mwanadamu kutoka katika safina na kuzaliana dhambi ikaendelea (Mwanzo 11).
- Kwa kuwa dhambi na matokeo yake yaliendelea, Mungu akaanza tena mpango wake wa wokovu kwa kuanza na mtu mmoja. Mungu alianza na mtu aitwaye Abramu ili kupitia yeye mpango wake wa wokovu uwafikie wanadamu wote (Mwanzo 12).
Katika MWANZO 12:1-3 Biblia inatuambia kwamba “Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”
- Kupitia uzao wa Abramu Mungu anaanzisha taifa, taifa hili analiita Israeli. Mungu anafanya taifa hili, ili lifanyike kuwa mfano wa kuishi maisha ambayo Mungu aliyakusudia kabla ya kuingia kwa dhambi na matokeo yake. Hii ndio maana Mungu anawaambia Israeli wao ni ufalme wa kikuhani.
“Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.” Kutoka 19: 5-6
Mungu alitaka kupitia wao mataifa mengine (yaani wanadamu wengine) wajifunze kuishi anavyotaka yeye. Jambo hili liliwekwa wazi kwa Israeli wote kama Musa anavyowaambia:
“Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako;” Torati 4:5-9
- Kwa sababu ya uteule huu wa taifa la Israeli, Mungu akaweka uwepo wake katika Israel kwa njia ya Hema la kukutania (wakiwa njiani kutoka Misri) na Hekalu (wakiwa ndani ya taifa lao). Mungu alifanya hivi kama ambavyo aliwaweka Adam na Eva katika uwepo wake ndani ya bustani. Mungu akaweka na taratibu mbalimbali kwa ajili ya kushughulika na dhambi, kwa sababu bado dhambi ilikuwa ndani ya Mwandamu (Taratibu hizi ziko katika kitabu cha mambo ya walawi).
- Taifa la Israeli kwa kuwa nalo ni uzao wa Adam, nalo likafanya dhambi vile vile kama wanadamu wote. Hakukuwa na tofauti Mungu aliyokuwa ameikusudia. Kwa lugha nyingine, Israeli hawakufanya kazi waliyokusudiwa na Mungu. Mungu katika kuendeleza mpango wake wa wokovu, akatoa ahadi ya kumtuma MASIHI kufanya kile Israeli walishindwa kufanya na kile Adamu alichokiharibu. Masihi maana yake mpakwa mafuta ambaye atakuja kuwakomboa Israeli, watu waliochaguliwa na Mungu kuwa nuru kwa mataifa mengine. Masihi huyu Mungu aliahidi atakuwa ni kutoka katika ukoo wa Daudi (2 Samueli 7:12-16). Masihi huyu alipaswa kufa kwa ajili ya makos ana dhambi za wanadamu na baadaye kufufuka (Isaya 53:1-12). Hii ndio maana Yesu akiwa amefufuka akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kwamba haya yaliyotokea kwake sio bahati mbaya, bali ni utimilifu wa unabii uliokuwa unamhusu yeye. Hivi ndivyo Biblia inavyo shuhudia:
“Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki. Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa juu mbinguni. Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu”. Luka 24:45-53
- Pamoja na ukweli huo, kwamba Mungu anatoa ahadi ya kumtuma Masihi, kwa vinywa vya manabii wengine anatoa ahadi ya kuja yeye mwenyewe katika hekalu lake. Moja wa manabii wanaotabiri ujio wa Bwana yeye mwenyewe ni nabii Malaki.
Nabii Malaki anatabiri kwamba “Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.”
- Hivyo, ahadi ya mwisho ya Mungu kwa Israeli ni yeye mwenyewe kutembelea Hekalu lake. Lakini kabla ya Bwana kutembelea hekalu lake atatanguliwa na mjumbe wake. Na mjumbe huyu ni Eliya (Malaki 4:5). Na Upande wa pili wa ahadi hio ni ujio wa Masihi kwa ajili ya kazi ya ukombozi. Pande mbili za ahadi hii, zinatujulisha kwamba Mungu aliahidi kuja yeye mwenyewe kama mwanadamu katika cheo cha masihi/kristo. Hii ndio maana mtume Paulo kwa kujua hilo anasema:
“Kwa maana Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwawekea watu makosa yao, naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.” 2 Wakorintho 5:19
- Mpango wa Mungu wa wokovu unafika kwenye kitivo kwa yeye mwenyewe. Mungu kuamua kuvaa mwili na kuja kuishi dunaini na kulipa gharama ya ukombozi (Kufa msalabani na kufufuka siku ya tatu). Yohana anayaeleza haya katika mwanzo wa Injili yake kwamba:
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli” YOHANA 1:1-14
Mtume Paulo pia anaelezea kweli hii ya Mungu kuchukua mwili ili aje duniani kwa ajili ya kulipa ghalama ya ukombozi. Katika WAFILIPI 2:5-11 Paulo anasema “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
Kuja kwa Yesu (Mungu katika mwili wa kibinadamu) duniani ndiko kitivo cha mpango wa wokovu. Maisha yake na kazi yake vilikamilisha kazi ya Mungu ya ukombozi ambayo kwa muda mrefu ilitarajiwa kutimizwa. Hivyo, Yesu, kwa kufa kwake msalabani, alilipa gharama ya ukombozi wa uumbaji wote na sasa yuko mbinguni akisubiri wanadamu waingie katika mpango huu ili arudi kufanya mambo yote kuwa mapya. Yesu kurudi mara ya pili na kufanya mambo yote kuwa mapya ndio kilele cha mpango huu wa Mungu wa wokovu. Petro anatukumbusha hili akisema “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka?Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake ” 2 Petro 3:9-13
Maswali
1. Kwa nini Mungu alimchagua Ibrahimu katika mpango wake wa wokovu?
2. Kwa nini Mungu alilichagua taifa la Israeli katika mpango wake wa wokovu?
3. Elezea kwa ufupi mpango wa Mungu wa wokovu.
D. TUFANYE NINI ILI TUPATE KUOKOKA (WOKOVU)?
1. NIFANYE NINI ILI NIPATE KUOKOKA?
Maandiko ya Msingi:
Waefeso 2:8-10,
Marko 16:15-16
Yohana 3:16-21.
Baada ya kuelezea mpango huu wa wokovu, swali la msingi ni, “Je, nifanye nini ili niwe sehemu ya mpango huu wa Mungu?” au kwa lugha iliyozoeleka, “Nifanye nini ili niweze kuokoka?” Swali hili, “Je, nifanye nini ili nipate kuokoka?” ni swali ambalo limeulizwa na wenzetu wengi kabla yetu. Majibu ya swali hili yamekuwa mengi kwa kuwa maandiko yanaonyesha watu walijibiwa kwa namna tofauti tofauti. Kwa mfano katika Marko 10:17-21 ilikuwa hivi “Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.”
Lakini kwa upande mwingine agizo la Bwana wetu Yesu Kristo linaloelezea namna ya kuokoka linasema kwamba “…Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Marko 16:15-16
Pia katika mahubiri ya kwanza ya Petro baada ya pentekosti majibu ya swali hili yalikuwa tofauti. Biblia inasema “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.” Matendo 2:37-40
Na tena Paulo katika barua yake kwa Warumi aliandika hivi “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu” Warumi 10:9-10. Pamoja na ukweli kwamba Paulo hakuwa anajibu swali letu moja kwa moja la “nifanye nini ili nipate kuokoka,” mafundisho yake ya mahali hapo yanatuonyesha nini kifanyike ili mtu apate wokovu.
Tukio lingine lilitokea katika mji wa filipi, swali liliulizwa na majibu yalitolewa na Paulo. Tukio hili lilikuwa kama ifuatavyo “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo. Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.”Matendo 16:25-34
Kutokana na maandiko kutuonyesha kwamba watu walijibiwa majibu tofauti tofauti au maelezo ya nini kifanyike ili mtu aokoke yapo kwa namna mbalimbali, swali la lazima linalokuja kichwani kwetu ni: Nifanye mambo mangapi na yapi ili niwe na uhakika kwamba nimeokoka??
Niamini, nikiri kwa kinywa, nibatizwe kwa maji, nitubu, niishike sheria na niuze mali zangu kwa maskini na kumfuata Yesu? Kwa maandiko machache niliyoorodhesha hapo juu, jumla ya mambo yanaweza kuwa matano au sita.
Swali lingine ni: Je, nikifanya mambo mengine na kukosa moja ninakuwa nimeokoka au bado? Mfano, nikiwa ninaamini, nimekiri kwa kinywa, nimebatizwa kwa maji, nimetubu, nimeshika sheria lakini sijauza mali zangu na kumfuata Yesu, ninakuwa bado sijaokoka? Au, ninaamini, nimekiri kwa kinywa, nimetubu na ninashika sheria ila sijabatizwa, ninakuwa nimeokoka au bado?
Swali la msingi la kutupa jibu letu la moja kwa moja ni hili: Je, ni jambo gani nisipofanya katika hayo ninakuwa sijaokoka??
Bwana wetu Yesu anatupa jibu la swali letu katika agizo lake kuu la kwenda kuhubiri injili. Biblia inasema “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Marko 16:15-16
Lakini pia Bwana Yesu anatujibu swali hili akiwa anamfundisha Nikodemo. Bwana Yesu anasema “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.” Yohana 3:16-21
Kutokana na maandiko hayo, mtu asipomwamini Yesu hata kama atafanya mambo mengine yote hawezi kupata wokovu. Hivyo, jambo kuu katika kupata wokovu ni IMANI KATIKA YESU. Mambo mengine huzaliwa baada ya imani (mfano, kubatizwa) au huendana na imani (mfano, kutubu) na mengine yanaweza yasifanyike kwa sababu mbalimbali na mtu huyu akawa ameokoka. Mfano, bubu anaweza asikiri lakini akiamini AMEOKOKA. Mwingine anaweza asibatizwe kwa kuwa ameamini akiwa kitandani hajiwezi; huyo pia kwa kuwa ameamini, amekwisha OKOKA.
Hii haina maana kwamba mambo haya (kama ubatizo) sio ya muhimu; mambo haya ni muhimu kwa kila anayeamini lakini yasipotendeka hayamfanyi mtu kuwa HAJAOKOKA. Lakini ikiwa kwa sababu yeyote mtu hamwamini YESU KRISTO, huyo kwake hakuna tumaini la wokovu.
Kujibu swali letu la “nifanye nini ili nipate kuokoka?” kwa msisitizo ni kwamba, mwanadamu anatakiwa kuamwamini Yesu kuwa ndiye mwokozi wake. Mambo mengine mbali na imani huambatana na Imani (mfano toba) na mengine huzaliwa baada ya imani (mfano kubatizwa).
Maelezo Kuhusu Toba au Kutubu.
Kutubu/Toba ni kugeuka kutoka kwenye mwelekeo wa mmoja na kugeukia mwelekeo mwingine. Hivyo, mtu anapomwamini Yesu anakuwa na toba moja kwa moja kwa kuwa mwanzo alikuwa anaamini vitu vingine (mwelekeo mmoja), lakini sasa anamwamini Yesu (mwelekeo mwingine). Hivyo, toba na imani havitengani; vinaenda pamoja.
Lakini pia, mitume wa Agano Jipya wametumia neno toba wakimaanisha “kugeuka kutoka kwenye maisha ya dhambi na kumgeukia Mungu (Imani).” Paulo anasema Bwana Yesu alimtuma akimwagiza akisema “uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi. Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni, bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao” Matendo 26:18-20. Hivyo toba na imani vinakwenda pamoja wala havitegani.
Lakini pia Biblia inafundisha kwamba toba huzaa mabadiliko (matunda) kama ambavyo imani huzaa mabadiliko. Pamoja na ukweli kwamba toba ni jambo la ndani ya moyo, matunda hutokea kwenye toba iliyo ya kweli. Yohana Mbatizaji, mhubiri wa toba kabla ya Yesu kuja, anafundisha hili sawa na Paulo anavyoeleza mbele ya Mfalme Agripa (Matendo 26:18-20). Yohana mbatizaji anasema “Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa. Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.” Luka 3:8-14
Mwisho kabisa, kujisikia huzuni sio toba bali huzuni huweza kuzalisha toba kama huzuni hii ni ya kimunngu. Maandiko yanasema “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.” 2 Wakorintho 7:10
Kwa hitimisho, Mtu anatakiwa kumwamini Bwana Yesu Kristo kwamba alikufa kwa ajili yake katika msalaba na alifufuka siku ya tatu ili kuokoka na imani hii huambatana na toba. Paulo katika Barua yake kwa Waefeso ametoa muhtasari (Summary) nzuri kuhusu jinsi wokovu unavyopatikana kwa mwanadamu. Mtume Paulo anasema “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.” Waefeso 2:8-10. Katika muhtasari ni vizuri kutoka ufafanuzi wa mambo matatu ambayo ni:
KWA MAANA MMEOKOLEWA KWA NEEMA.
Maana ya maneno haya ni kwamba, Mungu ameamua kutuokoa bila kuwa na sababu yoyote ya kumlazimisha kufanya hivyo. Kwa maneno mengine, ametupa wokovu kama zawadi tusiyostahili. Tulistahili jehanamu ya moto milele, lakini ametupa uzima wa milele. Ametupa nafasi katika mpango wake wa wokovu kwa mapenzi yake, sio kwa sababu tunasifa ya kuwa kwenye mpango huu mkuu. Jua kwamba Mungu angeweza kuangamiza uumbaji wote na kuumba tena viumbe vingine, au hata kuamua kutoumba kabisa. Lakini, akaamua kulipa gharama ili aokoe viumbe vyake, hasa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake.
KWA NJIA YA IMANI.
Zawadi hii tusiyostahili inatufikiaje? Inatufikia kwa njia ya imani—kwa kuamini. Kwa njia ya kummwamini Yesu tunapata zawadi hii. Mungu ameitoa kwa kila mwanadamu, lakini wale tu watakaoamini ndio wataipokea. Kwa sababu viumbe vingine havina utashi na uwezo wa kufanya maamuzi, ni mwanadamu pekee aliyepewa nafasi ya kuchagua kuwepo kwenye maisha yajayo ambayo Mungu ameyakusudia kuyafanya.
MATENDO MEMA.
Mambo mawili ya muhimu kujua kuhusu matendo mema kutoka katika muhtasari wa Mtume Paulo:
1. Hatujaokolewa kwa sababu ya matendo mema, hivyo hakuna wa kujisifu mbele za Mungu wala mbele za wanadamu.
2. Tumeokolewa ili tutende matendo mema maana hilo ni kusudi la Mungu tangu awali.
Kama tulivyojifunza kwamba, Mungu aliumba kila kitu na akaona kuwa kila kitu ni chema, lakini dhambi ndiyo ilileta uharibifu. Na ya kwamba lengo la Mungu la kumuokoa mwanadamu ni kumrejesha katika maisha kabla ya dhambi. Hivyo, baada ya kuokoka, matendo mema ni matokeo yanayotarajiwa. Hii ndio maana Yakobo anasema “Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.” Yakobo 2:17 na anatoa mfano ili tuelewe, akisema “Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa” Yakobo 2:26. Hivyo imani huzalisha matendo mema.
2. NINI MAANA YA KUMWAMINI YESU?
Maandiko ya Msingi:
1 Wakorintho 15:1-4
Kwa kuwa kuamini ndio njia ya kupokea wokovu na mtu asipoamini hana wokovu ni vizuri kuelezea nini maana ya “kumwamini Yesu”.
Kumwamini Yesu, ni kukubali moyoni na kuwa na uhakika moyoni ya kwamba Yesu ndiye Bwana na Mwokozi ambaye alikuja duniani akafa kwa ajili ya dhambi zako, akazikwa na siku ya tatu akafufuka. Na kwa yeye na kazi yake tunapata ukombozi. Jambo la msingi katika kumwamini Yesu ni kuamini kazi yake ya kifo msalabani kwa ajili ya dhambi zetu.
Kuna maelfu ya watu duniani na baadhi ya dini waamini kwamba ni kweli Yesu alizaliwa kwa bikira Mariam, aliishi duniani, alitumwa na Mungu, alifanya miujiza, alifundisha mafundisho mazuri, alikuwa masihi na wanaamini atarudi tena mara ya pili. Lakini Pamoja na hayo yote, hawaamini kama alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za ulimwengu. Namna hii ya imani haileti wokovu. Kutoa kifo cha Yesu msalabani kwa ajili ya dhambi na kufufuka kwake kunaondoa kabisa maana halisi ya imani ya Kibiblia inayoleta wokovu. Paulo anatuonyesha muktasari (Summary) wa injili aliyoihubiri na ambayo inaleta wokovu na kuwafanya watu wasimame katika wokovu. Paulo anasema “Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko;” 1 Wakorintho 15:1-4
Hivyo imani iokoayo ni imani inayohusisha kuamini kifo cha Yesu na kufufuka kwake. Imani kwa Yesu inayotoa kazi ya msalaba na kufufuka kwake sio imani inayompa mwanadamu nafasi katika mpango wa Mungu wa wokovu.
Maswali.
1. Mambo mangapi yanatakiwa yafanyike ili mtu apate kuokoka? Taja
2. Eleza nini maana ya “Kumwamini Yesu” kunakoleta wokovu.
3. Kuna uhusiano gani kati ya matendo mema na wokovu? 4. Mambo ya muhimu kuelezea unapohubiri injili ni yapi?
E. MUNGU ANAFANYA NINI TUNAPOOKOKA?
Maandiko ya Msingi:
Yohana 1:10-13,
2 Wakorintho 5:18-21
Waefeso 1:5, 13-14
Warumi 8:1-2, 14-16
Pale tu tunapomwamini Yesu, Mungu anatuunganisha na Yesu Kristo katika ulimwengu war oho. Hii ina maana Yesu kristo anaingia ndani yetu na sisi tunaingia ndani yake kwa Roho mtakatifu. Kwa Lugha nyingine Mungu anatuhamisha kutoka kwenye ukoo wa Adamu tunaingia kwenye ukoo wa Yesu. Ukoo wa Adamu ndio ukoo ulioathiriwa na dhambi na matokeo yake na ukoo wa Yesu ni ukoo usioathririwa na dhambi. Kwa tukio hili la kuhamishwa, tunatoka kwenye laana ya ukoo wa Adamu na tunaingia kwenye baraka ya ukoo wa Kristo. Tukio hili la muunganiko wetu na kristo linatupa mambo mengi ambayo Mungu anayafanya kwetu kwa njia ya Roho mtakatifu. Mambo ambayo Mungu hufanya kwetu ni mengi lakini machache ni kama yafuatayo: Mungu anatufanya watoto wake, Mungu anatuhesabu kuwa wenye haki mbele zake na anatupa Roho wake mtakatifu. Picha hapo chini inaonyesha kuhusu sisi kuungana na Kristo.

1. MUNGU ANATUFANYA WANAE
Biblia inaweka wazi kwamba tukimuamini Yesu, Mungu anatufanya sisi kuwa wanae. Kitendo hichi cha kufanyika watoto wa Mungu Biblia imekieleza kwa namna mbili tofauti, zote zikiwa zinatuelezea kuwa tumekuwa watoto wa Mungu.
Namna moja ni kwa njia ya kuzaliwa mara ya pili na namna nyingine ni kwa njia ya kuasiliwa na Mungu. Kuasiliwa ni kuchukuliwa kwenye familia ambayo haikuwa familia yetu kwa njia ya sheria (Kiingereza huitwa Adoption). Namna hii hutokea pale wazazi wanapomchukua mtoto asiye wao kibiologia na kumfanya wa kwao kwa njia ya sheria. Hivyo, sisi Biblia inaeleza kwamba hayo yote mawili yametokea kwetu kuonyesha kwamba sisi tulioamini tumekuwa watoto wa Mungu kweli kweli.
a. Tumezaliwa mara ya Pili.
Biblia inaweka wazi kwamba, Mungu anatuzaa sisi mara ya pili mara tu baada ya kumwamini Yesu. Na kwa kuzaliwa mara ya pili sisi tunafanyika kuwa watoto wake, kama ilivyo kwa binadamu akizaa mtoto huyo mtoto anakuwa wa kwake. Kweli hii ya Biblia inaelezwa katika maeneo mengi ya Biblia na sehemu chache ni kama zifuatazo:
“Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu”
Yohana 1:10-13
“Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. “1 Petro 1:3-4
b. Tumeasiliwa na Mungu.
Namna nyingine ambayo Biblia inaelezea kuhusu sisi kuwa watoto wa Mungu ni kwa kutumia wazo la kuasili. Hii ina maana kwamba, baada ya dhambi kuingia sisi wote tumekuwa katika ukoo wa Adamu, ukoo ulio chini ya dhambi. Lakini baada ya kuamini Mungu anatuchukua kutoka kwenye ukoo wa Adamu na kutuingiza kwenye ukoo wake kisheria na hivyo tunakuwa watoto wake.
Katika Waefeso 1:5 Biblia inasema “Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.” Neno lilotasfiriwa “tufanywe“ katika lugha yake ya asili lina maana ya kuasiliwa na Mungu. Kutoka katika muktadha wa maneno haya, tunajifunza kwamba kuasiliwa na Mungu ni moja ya baraka za rohoni Mungu alizotubarikia.
2. MUNGU ANATUHESABIA HAKI.
Kuwa Yesu hakutenda dhambi yeyote na sisi tumefanya au tunafanya dhambi. Tukimwamini Yesu, Mungu anatupa haki ya Kristo Yesu na dhambi zetu Yesu alikwisha kuzichukua na kufa kwa ajili ya hizo msalabani. Hivyo, mabadilishano yanatokea, Mungu anatupa haki ya kristo na kristo anachukua dhambi zetu. Mtume Paulo anaeleza vizuri kweli hii katika barua yake kwa Wakorintho.
Katika 2 Wakorintho 5:18-21 Mtume Paulo anasema “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.”
Kutokana na ukweli huu, sisi hatuna hatia mbele za Mungu na hakuna hukumu juu yetu kwa kuwa hukumu yetu tuliyostahili kristo alikwisha kuichukua. Ndio maana Mtume Paulo anasema “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” Warumi 8:1-2
3. MUNGU ANATUPA ROHO WAKE MTAKATIFU.
Pamoja na kwamba Biblia inatuambia tunaunganishwa na kristo kwa Roho (Mfano tunazaliwa na Roho ), Biblia pia inatuambia Mungu anatupa Roho wake kama mhuri wa kuonyesha ya kwamba sisi ni mali yake. Tunapoamini tu, Mungu anatutia mhuri wake ambao ni Roho mtakatifu na kupitia kupokea Roho mtakatifu tunapata uhakika kwamba sisi ni mali ya Mungu na pia ni watoto wa Mungu. Hivi ndivyo Mtume Paulo anaeleza kuhusu kweli hii, anasema;
“Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.” Waefeso 1:13-14
“Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” Warumi 8:14-16
Mungu kwa kufanya haya na mengine mengi tusiyoweza kuyaelezea kwa sababu ya nafasi, tunapata faida nyingi sana katika maisha yetu ya sasa na yale ya ulimwengu ujao. Kupitia mambo haya Mungu anayoyafanya baada ya kumwamini Yesu hatuwi tena sawa na watu walioko nje ya mpango huu wa wokovu.
Maswali.
1. Mambo gani matatu, Mungu anafanya kwetu pale tu tunapoamini?
2. Nini maana ya kuungana na kristo?
3. Ni kwa namna gani Mungu anatufanya sisi waamini kuwa watoto wake?
F. LENGO LA WOKOVU
Maandiko ya Msingi:
2 Petro 3:10-13,
1 Wathesalonike 4:1-7,
1 Wakorintho 15:51-54
Ufunuo 21 & 22
Kutoka kwenye maana ya wokovu ni rahisi kujua lengo la wokovu ni nini. Kama nilivyosema katika maana ya wokovu kwamba, Mungu alianzisha mpango huu kwa lengo la kuurejesha uumbaji wake katika hali ya kutokuwa na dhambi na matokeo yake. Katika kuelezea lengo la wokovu basi nitagawa eneo hili katika maeneo mawili; Lengo la wokovu kwa uumbaji wote na lengo la wokovu kwa kumlenga mwanadamu.
LENGO KWA UUMBAJI WOTE.
Je Mungu alikuwa anakusudia nini kufanya mpango huu wa wokovu? Au ni nini kilele cha mpango huu wa wokovu?
Lengo kubwa kama tulivyojifunza ni kuurejesha uumbaji wake wote katika hali ya kwanza na zaidi kuuboresha. Katika kutekeleza lengo hili, Mungu ameahidi kwamba atafanya kwa hatua mbili. Hatua ya kwanza Mungu atauharibu uumbaji wote (Mbingu na Nchi) tunaouona sasa. Mtume Petro analisema hili katika barua yake akisema “Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka?” 2 Petro 3:10-12
Na katika hatua ya pili, Mungu atafanya uumbaji mpya (Mbingu na nchi mpya). Mungu atafanya ardhi na anga jipya (Maneno mbingu na nchi yana maana ya anga na ardhi) kama alivyofanya katika uumbaji wa awali. Hivi ndivyo mtume Petro anaendelea kusema katika waraka wake kwamba “Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.” 2 Petro 3:13.
Katika uumbaji huu mpya Mungu atakaoufanya, ndani yake ataweka mji mzuri ulioandaliwa na kupambwa kwa ajili ya kuwa makazi ya milele ya watu wake. Mji huu jina lake ni Jerusalem mpya. Haya ndiyo aliyoyaona Yohana katika maono yake akiwa kisiwani Patmo. Yohana anasema “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.” Ufunuo wa Yohana 21:1-2
Kama ambavyo ilikuwa hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na nchi na baadaye akatengeneza bustani kwa ajili ya mwanadamu kuishi, ndivyo itakavyokuwa hapo mbeleni. Mungu atafanya mbingu na nchi mpya na ndani yake ataweka mji mpya kwa ajili ya makazi ya wanadamu.
Mji huu hautakuwa na dhambi wala matokeo ya dhambi. Kutakuwa hakuna maumivu wala laana. Mungu atayafanya mambo yote kuwa mapya. Mji huo hahuitaji jua wala mwezi kama ilivyokuwa katika uumbaji wa kwanza, maana Mungu ndio mwangaza ndani ya mji huo. Ni mji wa kupendeza sana kwa kuwa umeandaliwa na Mungu mwenyewe. Habari hizi nzuri za uumbaji mpya na mji huu mzuri zinaelezwa na Biblia kwa kirefu katika Kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura ya ishirini na moja na ishirini na mbili.
LENGO KWA MWANADAMU.
Kwa kuwa mwanadamu ni sehemu ya uumbaji wa Mungu, na kwetu Mungu ametupa wokovu ili turudi kwenye hali yetu njema ya awali. Hali ya kutokuwa na dhambi au hali ya kutokuitumikia dhambi tena. Kwa mwanadamu lengo hili linaanza pale tu anapoamini na litakamilika katika ujio wa Yesu krito mara ya pili. Hivyo, tuna mambo mawili mbele yetu, moja ni jambo la hatua kwa hatua na jingine litatokea kufumba na kufumbua wakati wa kurudi Yesu kristo mara ya pili.
Jambo la hatua kwa hatua kutoka kwenye dhambi hutambulika kama UTAKASO katika Biblia. Jambo la Kufumba na kufumbua kutoka kabisa katika mwili wa dhambi na kuvaa wwili wa utukufu hutambulika kama KUTUKUZWA katika Biblia.
UTAKASO.
Kwa kuwa kristo Yesu ndiye mwanadamu pekee aliyeishi duniani bila kufanya dhambi, sisi mara tu baada ya kuamini Mungu anaanza kutubadilisha kila siku tutoke kwenye maisha ya dhambi na tufike kumfanania kristo Yesu. Hili ni jambo la siku hadi siku halitokei mara moja. Mungu hutubadilisha matendo yetu, mawazo yetu, nia zetu na kila kitu kilichondani yetu na sisi kazi yetu ni kutii na kukubali yale Mungu anayotuagiza kufanya au kutokuyafanya ili lengo lake litimie. Jambo hili linafundishwa na Biblia katika maeneo mengi na Paulo analisisitiza katika waraka wake kwa Wathesalonike, watu waliotoka kuamini hivi karibuni. Paulo anasisitiza kwa kusema; “Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu. Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu. Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili; kwa sababu Bwana ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama tulivyowaambia kwanza, tukashuhudia sana. Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso” 1 Wathesalonike 4:1-7
Mungu kupitia Roho wake hutumia neno lake kututakasa, ndio maana tunahitaji kujifunza neno lake na kulitii. Yesu aliyasema haya alipokuwa anatuombea kwa Baba, alisema “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.” Yohana 17:17-20
Neno la Mungu ndio linatutasa kwa msaada wa Roho mtakatifu. Hivyo ni muhimu kwa mwamini kujifunza neno la Mungu kwa kuwa ndio linaweza kututoa katika maisha ya dhambi. Kwa muda tunaoishi hapa duniani lengo la wokovu ni utakaso kwa kila anayeamini.
KUTUKUZWA.
Kutukuzwa ni jambo tunalolisubiri kutokea siku ambayo Bwana wetu Yesu tunayemwamini atakaporudi. Wakati ukifika, tutabadilishwa miili yetu ya sasa na kuwa na miili mipya ya utukufu. Miili ya utukufu ni miili isiyoweza kutenda dhambi kabisa. Miili isiyoweza kupatwa na matokeo yote ya dhambi kama vile kifo, uzee, maumivu wala magonjwa. Hii ndio miili tunayoisubiria Yesu Kristo atakaporudi.
Kwa wale ambao watakuwa wamekufa wakati wa kurudi kwa Bwana Yesu, Biblia inasema watafufuliwa na miili hii mipya. Waamini wale watakaokuwa hai wakati huo watabadilishwa kutoka kwenye miili ya asili kwenda kwenye miili ya utukufu kufumba na kufumbua. Paulo anaelezea jambo kwa kusema “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda” 1 Wakorintho 15:51-54. Miili hii mipya ya utukufu ni kama mwili ule alikuwa nao Yesu baada ya kufufuka kwake.
Hivyo, Kwa ujumla mango wa Mungu wa wokovu utafikia kilele pale ambapo waamini tutaishi katika mji mpya wa Jerusalem ndani ya mbingu na nchi mpya tukiwa na miili mipya kama tulivyojifunza hapo juu. Zaidi ya hapo tutaishi na Mungu milele na milele katika mji huo tukitawala uumbaji huu mpya. Kama mwanadamu alivyopewa kutawala uumbaji wa kwanza ndivyo hivyo hivyo waamini watapewa kutawala uumbaji huu mpya, wakiwa na makazi pamoja na Mungu milele na milele. Habari hii, ndio utimiligu wa lengo la mpango wa Mungu wa wokovu. Utimilifu huu kwa kuwa bado tunausibiri, unaitwa TUMAINI LETU na waandishi wa Biblia. Na ni kweli kwamba habari hii ndio tumaini letu sisi waamini.
Maswali
1. Eleza lengo kuu la wokovu kwa uumbaji wote na toa maandiko yanayounga mkono jibu lako.
2. Taja na ueleze hatua mbili ambazo Mungu atachukua ili kutekeleza lengo la wokovu kwa uumbaji wote.
3. Je, lengo la wokovu kwa mwanadamu lina hatua gani mbili kuu? Eleza kila hatua na toa maandiko yanayohusiana.
4. Kwa nini ni muhimu kwa mwamini kujifunza Neno la Mungu katika mchakato wa utakaso?
5. Eleza jinsi miili ya utukufu itakavyokuwa tofauti na miili yetu ya sasa.