Yakobo – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA YAKOBO

MAELEKEZO

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.

UTANGULIZI

Barua ya Yakobo kwenda kwa waamini wayahudi waliokuwa nje ya israeli, ni kitabu kinachoaminika kuwa ndio kitabu kikongwe zaidi katika vitabu vya Agano jipya. Kitabu hiki kiliandika katika kipindi cha miaka ya 45-58 BK, hivyo kalenda hii inakifanya kitabu hiki kuwa kitabu cha kwanza kuandikwa. Jumbe za kitabu hiki zina mfanano mkubwa na jumbe katika kitabu cha Mithali (Mithal 1-9) na jumbe za Bwana Yesu katika semina ya mlimani. Na ziadi ya hapo, maneno ya Kiyunani yaliyotumika katika barua hii yanamfanano mkubwa na maneno ya Yakobo katika hotuba yake katika kikao cha kwanza cha kanisa kule Jerusalem (Matendo 15:13-21).

MWANDISHI

Mwandishi wa kitabu hiki anajitambulisha kama Yakobo, mtumwa wa Mungu na Bwana Yesu kristo. Yeye ni mmoja kati ya ndugu wanne wa Bwana wetu Yesu (Galatia 1:19, Marko 6:3 na Mathayo 13:55) pamoja na kwamba hakuamua kutaja undugu wake na Bwana wake. Mmoja wa hao ndugu ni Yuda, mwandishi wa waraka wa Yuda (Yuda 1:1). Wakati wa huduma ya Yesu duniani akiwa katika mwili, Yakobo na ndugu zake wengine hawakumwamini yeye kama ndiye Kristo (Marko 3:21; Yohana 7:5). Hata hivyo, Yakobo alibadilika wakati Yesu alipomtokea baada ya kufufuka kwake, na tangu hapo akawa mwamini mwaminifu (1 Wakorintho 15:7). Yakobo alikuwepo pamoja na wanafunzi wengine katika siku ile ya Pentekoste (Matendo 1:14) na baadaye akawa mmoja wa viongozi wa kanisa la Yerusalemu (Matendo 12:17; 15:1-35). Alikuwa na nafasi muhimu katika kundi la wazee wa kanisa la Yerusalemu, ambapo inaonekana yeye alikuwa mwenyekiti wa kikao cha kwanza cha kanisa na ndiye aliyetangaza maamuzi ya kanisa kuhusu mataifa kushika sheria ya Musa (Matendo 15:13-29). Kwa sababu ya nafasi yake katika kanisa alijulikana kama mmoja wa “nguzo” za kanisa la Jerusalem (Wagalatia 2:9).

Katika Agano Jipya, kuna watu watatu maarufu wenye jina Yakobo: Yakobo, mwana wa Zebedayo (Mathayo 4:21), alikuwa mmoja wa mitume kumi na wawili na ndugu yake Yohana Mtume. Anajulikana kama Yakobo Mkubwa na alikuwa sehemu ya kundi la ndani la Yesu pamoja na Petro na Yohana (Marko 5:37); Yakobo, mwana wa Alfayo (Mathayo 10:3), alikuwa mwingine wa mitume kumi na wawili, wakati mwingine hujulikana kama Yakobo Mdogo ili kumtofautisha na Yakobo, mwana wa Zebedayo; na Yakobo, ndugu yake Yesu (Marko 6:3), pia anajulikana kama Yakobo Mwenye Haki, alikuwa kiongozi katika kanisa la Yerusalemu (Matendo 15:13), ambaye ndiye mwandishi wa waraka huu.

WAPOKEAJI WA AWALI WA UJUMBE

Kitabu cha Yakobo ni moja ya vitabu vya nyaraka (barua) ambavyo tunaona mwandishi anawataja walengwa wa awali wa ujumbe wake. Yakobo anaonesha wazi waliowaandikia kitabu hiki ni waamimi ambao walikuwa wametawanyika sehemu mbalimbali za ulimwengu ambao kwa sehemu kubwa walikuwa wahayudi, ndio maana anasema ujumbe wake ni “kwa kabila kumi na mbili waliotawanyika” (1:1). Ukiacha kauli hiyo ya mwandishi, kuna viashiria mbalimbali zinavyonyesha kwamba waandikiwa wa awali wa barua hii walikuwa ni wayahudi walioamini. Viashiria hivi ni kama vile: waandikiwa kukutana katika sinagogi (2:2), waandikiwa kuwa na imani thabiti katika umoja wa Mungu (2:19) na msisitizo wa mwandishi kuhusu sheria (2:8-13;4:11-12).

Pamoja na wayahudi hawa kuwa nje ya taifa lao, pia walikuwa katika umaskini na mateso makubwa mbalimbali (1:2). Matajiri waliwaonea kwa kutokuwalipa ujira wao (5:4-6), waliwapeleka mahakamani (2:6) na zaidi matajiri hawa walidharau imani yao (2:7). Hii haina maana kwamba waamini wote walikuwa maskini. Barua hii inaonyesha pia katikati ya waamini hawa kulikuwa na wafanya biashara matajiri (4:13-17).

UJUMBE MKUU WA WARAKA

Mwandishi anaandika waraka huu kwa dhumuni la kuwatia moyo waamini katika majaribu mbalimbali waliyokuwa wanapitia (1:2-4, 12-15; 5:7-11). Waamini hao walikuwa wanapitia changamoto mbalimbali kama vile kuonewa na matajiri (5:4-6), kupelekwa mahakamani (2:6) na kudharauliwa (2:7). Kutokana na mateso hayo Yakobo anawatia moyo waamini kwa kuwahimiza kustahimili yote.

Pamoja na kuwatia moyo waamini, Yakobo anawasisitiza waamini kuishi imani yao katika matendo (2:14-26). Mwandishi anasisitiza kwamba imani lazima izae matendo mema. Kwa kusisitiza hilo mwandishi anasema “imani, isipokuwa ina matendo, imekufa” (2:17, 26) na “imani pasipo matendo haizai” (2:20). Imani ya jinsi ya hiyo ambayo hata mashetani wanayo (2:19), Mwandishi anasema haiwezi kumfanya mwanadamu ahesabiwe kuwa ana haki (2:24) wala kumuokoa (2:14).

Jambo la tatu mwandishi analozungumza katika waraka huu ni kudhibiti kinywa katika kunena  (1:19-20, 26 na 3:1-12). Anasisitiza umuhimu wa waamini kuzungumza kwa hekima, kujua namna ya kuongea ipasavyo, na kutambua wakati wa kunyamaza. Haipendezi kwa waamini kuwa na tabia ya kuzungumza bila mipaka, akionya kwamba hii ni hatari kama njiti ndogo ya kiberiti inayoweza kuteketeza msitu mzima.

Na mwisho, mwandishi anakemea upendeleo wa matajiri dhidi ya maskini na kuwepo kwa matabaka ndani ya kanisa (1:9-11, 2:1-13). Kwa kufanya hivyo, mwandishi anatuonesha hali iliyokuwepo katika kanisa. Hivyo, mwandishi anapinga na kukemea vikali ubaguzi na matabaka, akiamuru kwamba visiwepo katikati ya waamini. Majivuno, kiburi, na kuhukumiana kati ya waamini ni mambo ambayo mwandishi ameyakemea pia (4:11-5:6).

MUUNDO NA MPANGILIO WA KITABU

Kitabu hiki kinaanza kama barua, kwa kuwa na anuani kama ilivyokuwa kawaida kwa barua za karne ya kwanza (1:1). Ukiacha anuani uandishi wa kitabu hiki uko katika mtindo wa HOTUBA. Mwandishi anaanza Hotuba yake katika sura ya kwanza kwa kutoa muhtasari wa kile ambacho ataenda kukiongelea katika hotuba yake nzima. Hivyo, katika sura ya kwanza Mwandishi anaongelea kwa ufupi jumbe zote alizoziongelea katika sura zinazofuata. Na sura ya mwisho anajitahidi kukazia mambo muhimu aliyokwisha kuyaongelea.

MAANDIKOMADAMUHTASARI
Yakobo 1:1Salamu na utambulisho 
Yakobo 1:3-27Muhtasari wa mada kuu anazokwenda kuzizungumzia, mfano;
Majaribu 1:2-4, 12-15,16-18
Hekima 1:5-8,
Matajiri na maskini 1:9-11
Ulimi 1:19-20, 26
Uaminifu wa kweli (utendeaji kazi wa neno) 1:21-27
Yakobo 2:1-13Masikini na matajiriYak 1:9-11
Yakobo 2:14-26Imani yenye MatendoYak 1:22-27
Yakobo 3:1-12UlimiYak 1:19-20, 26
Yakobo 3:13-18Hekima ya Mungu na hekima ya duniaYak 1:5-8
Yakobo 4:1-10TamaaYak 1:13-15
Yakobo 4:11-5:6Dhambi ya kuhukumu, kiburi, majivuno, na kujitapia mali kwa hilaYak 1:9-11, 20-21
Yakobo 5:7-20Hitimisho na kukazia mada kuu 
Majaribu 5:7-11,13
Kiapo 5:12
Maombi  5:13-18
Kuwarejesha waliorudi nyuma 5:19-20

Pamoja na kuwa na mpangilio huo, kitabu hiki kina ufanano mkubwa sana katika mtindo na mada zake na kitabu cha Mithali. Kama ambavyo kitabu cha Mithali kimejawa na hekima, ndivyo kitabu hiki kilivyojaa hekima. Kutokana na hilo, wengine wamekiita kitabu hiki “Mithali ya Agano Jipya.” Jedwali hapo chini linaonyesha ufanano wa mada kati ya kitabu hiki na kitabu cha mithali.

YAKOBOMADAMITHALI
Yakobo anasisitiza umuhimu wa hekima na anawahimiza waamini kutafuta hekima kutoka kwa Mungu (Yakobo 1:5, 3:13-18).HekimaMithali inasisitiza mara kwa mara thamani ya hekima na ufahamu (Mithali 1:2-6, 4:7).
Yakobo anazungumzia asili ya majaribu na jinsi yanavyopelekea dhambi (Yakobo 1:13-15).Majaribu na DhambiMithali inaonya dhidi ya vishawishi vya tabia ya dhambi na umuhimu wa kupinga majaribu (Mithali 1:10-19, Mithali 7).
Yakobo anazungumzia uwezo wa kuharibu wa ulimi na umuhimu wa kudhibiti maneno (Yakobo 3:1-12).ManenoMithali inatoa maarifa mengi juu ya matumizi ya maneno na athari za maneno (Mithali 10:19-21, Mithali 18:21).
Yakobo anaonya dhidi ya kiburi na anahimiza unyenyekevu mbele za Mungu (Yakobo 4:6-10).Unyenyekevu na KiburiMithali inaonya kuhusu hatari za kiburi na inasisitiza unyenyekevu (Mithali 3:34, Mithali 11:2).

Kwa upande mwingine pamoja na kitabu hiki kumtaja Yesu mara mbili tu, kimebeba mada zinazofanana sana na mafundisho na mahubiri yake. Mwandishi amefundisha mambo mengi sawa na yale Yesu alifundisha hasa Hotuba ya Yesu ya mlimani. Jedwali hapo chini linaonyesha mfanano wa mada kati ya jumbe za kitabu hiki na mafundisho ya Bwana Yesu.

YAKOBOSOMOYESU
1:2Kufurahi katika majaribuMathayo 5:10-12
1:5, 4:2-3,Ombeni nanyi mtapewaMathayo 7:7, Luka 11:9
5:1-6Onyo dhidi ya MatajiriLuka 6:24
1:22-25, 2:14-17Kuwa watendaji wa neno na si kuwa wasikiaji pekee.Mathayo 7:24-17, Luka 6:46-49, 11:28
5:12Kuhusu kuapaMathayo 5:33-37
4:11-12MsihukumuMathayo 7:1-2, Luka 6:37

MFULULIZO WA MAWAZO WA MWANDISHI

Kitabu hiki kinaanza na anuani ya barua kama ilivyokuwa kawaida ya barua za karne ya kwanza (1:1). Baada ya anuani hiyo, mwandishi anatoa muhtasari wa mada atakazozizungumzia katika waraka wake. Sura nzima ya kwanza ni muhtasari wa mada zitakazozungumziwa kuanzia sura ya pili hadi ya tano.

Mada ya kwanza katika muhtasari ni kuhusu majaribu. Waamini wanatakiwa kufurahia majaribu, kwa kuwa majaribu huzalisha saburi na hatimaye ukamilifu (1:2-4). Mada ya pili ni kuhusu hekima. Mtu akipungukiwa hekima, aombe kwa Mungu na aombe akiwa na imani pasipo shaka (1:5-8). Mada ya tatu ni kuhusu matajiri na maskini. Wote maskini na matajiri wanatakiwa kujitazama kama Mungu anavyowatazama kila mmoja wao (1:9-11).

Baada ya mada hizo, mwandishi anarudi tena kwenye mada ya majaribu. Mwamini anatakiwa kustahimili majaribu maana atapokea taji kutoka kwa Mungu. Pamoja na mwito huu, mwamini asidhani majaribu yanayomvuta kwenye dhambi yanatoka kwa Mungu (1:12-15). Mungu anatoa vitu vizuri tu, vinavyotusababisha tumfananie Mwana wake. Na kwa sababu hiyo shetani asiye akatudanganya vinginevyo (1:16-18). Mada ya nne katika muhtasari ni kuhusu kutawala kinywa (ulimi). Mwamini anatakiwa kuwa msikivu zaidi kuliko kuwa mzungumzaji (1:19-20). Na mada ya mwisho katika muhtasari ni kuhusu utendaji wa neno. Mwamini anatakiwa kuwa mtendaji wa Neno na si msikilizaji tu ambaye hatendi chochote (1:21-27).

Baada ya muhtasari huo, mwandishi anaingia kwenye ujumbe wake. Anaanza kwa kuzungumza kuhusu uhusiano kati ya matajiri na maskini. Mwandishi anawakataza waamini kuwapendelea matajiri na kuwadharau maskini, akitoa mfano wa namna upendeleo unavyoweza kufanyika. Pia, mwandishi anasema upendeleo ni dhambi mbele za Mungu na kwamba kuonyesha upendeleo ni kinyume na sheria ya Mungu (2:1-13). Baada ya hapo, mwandishi anaendelea na mada nyingine: Imani ya kweli huzalisha matendo. Kwa kutumia mfano, mwandishi anaonyesha kwamba imani isiyo na matendo haina matumizi (2:14-17). Kwa kutumia hoja kutoka kwa mpinzani wa kufikirika[1], mwandishi anasisitiza kwamba imani pasipo matendo haina matumizi yoyote. Zaidi, kwa kutumia mifano miwili kutoka katika maandiko, mwandishi anathibitisha kwamba imani inazalisha matendo (2:18-25). Mwisho, kwa kutumia ufananisho, mwandishi anahitimisha kwa kusema imani pasipo matendo haina uhai (2:26).

Baada ya mada hiyo, mwandishi sasa anahamia kwenye mwito wa kudhibiti ulimi (kinywa). Mwandishi anawaita waamini kudhibiti ulimi kwa kuwa kuna hukumu mbele yetu (3:1-2). Pia, mwandishi anatuita kuudhibiti ulimi kwa kuwa pamoja na udogo wake, ulimi una nguvu kubwa, kama lijamu kwa farasi na usukani kwa meli (3:3-5a). Nguvu hii kubwa ya ulimi inaweza kuwa na madhara makubwa, kama moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa (3:5b-8). Mwisho, mwandishi anatuita kudhibiti ulimi kwa kuwa haifai kutoa mchanganyiko wa mema na mabaya, au laana na baraka katika vinywa vyetu, kama ambavyo haiwezekani mti mmoja kuzalisha matunda mawili tofauti au chemchemi moja kutoa aina tofauti za maji (3:9-12).

Katika kuzungumzia Hekima, Yakobo anaweka wazi kwamba mwenye hekima itokayo kwa Mungi ni yule mwenye mwenendo mzuri uliojaa amani na upole. Mwenye mwenendo wa uchungu, ugomvi, kujisifu na uongo huyo hana hekima ya Mungu bali anahekima ya dunia, tena hekima hiyo ni ya Shetani (3:13-18). Kwa kukosa hekima ya Mungu waandikiwa wa waraka huu walikuwa katika magomvi na mapigano. Kwa sababu hiyo, Mwandishi anawajulisha chanzo cha mapigano yao; Mapigano na magomvi yanatokana na tamaa mbaya ya vitu waliyonayo. Na vitu wanavyovitamani hawana ni kwa sababu hawaombi, na hata wakiomba hawapati kutoka kwa Mungu kwa sababu wanaomba kwa lengo baya (4:1-3). Kwa sababu ya kutokuwa waaminifu (kukosa hekima) mbele za Mungu, Mwandishi anawaita waamini hawa wazinzi (lugha ya picha ya kuonyesha kwamba wao sio waaminifu kwa Mungu). Anawajulisha kwamba urafiki na dunia ni sawa na uadui na Mungu. Pamoja na ukweli huo Yakobo anasema neema ya Mungu ipo na inatosha kwa wanyenyekevu (4:4-6). Kwa sababu neema ya Mungu ipo kwa wanyenyekevu, Yakobo anawaita waamini kuwa wanyenyekevu kwa kufanya mambo saba aliyoyataja (4:7-10). Mbali na mwito huo, Yakobo anawakataza waamini kusingiziana na kuhukumiana. Anawakataza waamini kufanya hivyo kwa kuwa hilo ni jukumu la Mungu na sio lao (4:11-12).

Baada ya hayo, Yakobo anawageukia matajiri. Kwanza anaanza na kukemea majivuno katika mipango yao. Anawaita katika unyenyekevu kwa kuwa wao ni kama mvuke, huonekana kwa kitambo kidogo na baadaye hupotea (4:13-17). Baada ya mwito huo, Yakobo anatangaza hukumu kwa matajiri wote ambao wametumia utajiri wao vibaya. Matajiri waliowadhulumu wafanyakazi wao mishahara, matajiri waliojifurahisha katika anasa na tamaa zao na wale waliowahukumu na kuwaua watu wasio na hatia (5:1-6).

Katika kuhitimisha ujumbe wake, Yakobo anazungumzia mambo manne. Moja, anawatia moyo waamini wanaopata majaribu mbalimbali. Anawahasa kuvumilia mateso yote (majaribu) bila kulalamika kwa kuwa Bwana Yesu yuko karibu kurudi ili kuwathibitisha wao. Zaidi, anawatia moyo kutazama mifano ya manabii wa kweli waliopata mateso lakini wakavumilia (5:7-11). Kumbuka mwito huu wa kuvumilia unakuja baada ya kutangazwa kwa hukumu juu ya matajiri waovu. Pili, Yakobo anawakataza waamini kuapa ili wasije wakaangukia hukumu[2] (5:12). Tatu, Yakobo anasisitiza waamini kuomba pale wanapokuwa katika hali mbalimbali mfano kupatwa na mbaya au kuumwa. Anasisitiza maombi kufanyika kwa imani na kwa bidii (5:13-18). Mwisho, Yakobo anafunga waraka wake kwa kuwatia moyo waamini wale wanaowarejesha waamini wengine wanaoingia kwenye maisha ya dhambi. Kitendo chao cha urejesho kina faida kubwa kwa mwamini husika na kwa jamii nzima ya waamini (5:19-20).

FOOTNOTES


[1] Mstari wa 18, una maneno ya mpinzani wa kufikirika anayesema kwamba “ Wewe unayo imani, nami ninayo matendo,” akijaribu kuonyesha kwamba imani na matendo vinaweza kutenganishwa. Lakini mwandishi anapinga na kumuonyesha kwamba imani siku zote katika historia imekuwa inaambatana na matendo, hivyo vitu hivi haviwezi kutengana (1:18b-25)

[2] Mstari huu unafuatisha kwa ukaribu zaidi mafundisho ya Bwana Yesu kutoka Mathayo 5:34-37.

Unakuja hivi karibuni….